Historia ya Kanisa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Historia ya Kanisa ni fani inayochunguza historia ya Ukristo na ya miundo yake mbalimbali tangu Kanisa lilipoanzishwa na Yesu Kristo katika karne ya 1 hadi leo.

Kwa kawaida historia hiyo hugawanywa katika hatua nne:

  1. kipindi cha Mitume wa Yesu na Mababu wa Kanisa (karne I-karne IX)
  2. Karne za kati (karne IX-karne XV)
  3. kipindi cha marekebisho (karne XVI-karne XVIII)
  4. kipindi cha sasa (karne XIX-karne XXI)

Pande mbili za Kanisa[hariri | hariri chanzo]

Kwa mtazamo wa imani, historia hiyo yote inaonyesha upande mmoja udhaifu na ukosefu wa Wakristo hata katika ngazi za juu, lakini pia uwezo wa neema ya Mwenyezi Mungu wa kuleta watakatifu wapya katika mazingira yoyote.

Ni kwamba kwa Wakristo, Kanisa ni kitu kizuri na muhimu sana. Ni bibiarusi wa Yesu, ni mwili wa Kristo, ni chombo cha Mungu cha kuunganisha waumini wake kwa Roho Mtakatifu. Limepewa na Mungu wito wa kuwaletea watu Neno lake. Hivyo linatangaza Habari Njema, ambayo ni faraja kwa watu wanaotaka kukata tamaa. Linaombea watu. Linasaidia wenye dhiki. Linatetea haki za binadamu. Ndiyo sababu ya kusema: Nasadiki Kanisa takatifu.

Lakini Kanisa lina upande mwingine. Kati ya habari za siku zetu tunaweza kusikia juu ya magomvi ndani ya madhehebu fulani. Viongozi wanaweza kushindana. Vikundi vinaweza kujitokeza na kujitenga na Kanisa. Mambo ya hela yanaweza kupata uzito kuliko mambo ya kiroho. Masharti ya ajabu yasiyo na msingi katika imani na mafundisho ya mitume, yanaweza kuzushwa ghafla na kutangazwa kuwa ya lazima mbele za Mungu.

Tukiingia katika historia ya Kanisa kwa undani tunapata habari nyingi za kusikitisha. Ni kwamba Wakristo ni binadamu. Waliopokea wokovu katika Kristo wako njiani kwenda mbinguni. Lakini bado ni wanadamu wenye dhambi na wenye kasoro. Kasoro hizo za kibinadamu zinaonekana katika historia ya Kanisa pia.

Mazingira ya Yesu na ya Wakristo wa kwanza[hariri | hariri chanzo]

Imani ya Wakristo ni juu ya Yesu kuwa Kristo, Mwana wa Mungu. Kwamba alikuja kwelikweli hapa duniani kuishi kama mtu kati ya watu. Alikuja miaka 2000 iliyopita katika nchi iliyoitwa majina mbalimbali katika historia yake ndefu, kama Kanaani, Israeli, Palestina au Uyahudi. Alizaliwa na mwanamke, aliishi na kufa kama sisi sote. Kwa maisha na kifo chake alidhihirisha upendo wa Mungu kwetu na kutualika tumrudishie.

Wanafunzi wengi, wa kiume na wa kike, walifuatana naye popote alipokwenda, na kuona aliyoyatenda na kusikia aliyoyasema. Kati yao Yesu alichagua wanaume 12 ambao aliwaita "mitume". Hakika alikuwa na maana kubwa kufanya hivyo. Ndio mbegu ya taifa kubwa la waamini wake wote linaloitwa Kanisa, yaani mkusanyiko. Ndio waliotekeleza maagizo yake, "Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyoamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dhahari." (Math 28:19-20) Hawakuwa watu mashuhuri kwa asili. Tena Biblia inatupa habari za aina hii: kwamba wale Mitume ni mifano ya Ukristo wetu katika nguvu au karama zao, lakini pia katika udhaifu wao.

Wayahudi[hariri | hariri chanzo]

Yesu na wanafunzi wake wa kwanza walitokana na Abrahamu na kuwa watoto wa Agano lililofanywa kati ya Mungu na taifa lake la Israeli zamani za Musa. Wakati wa Yesu Waisraeli hao waliitwa "Wayahudi". Walio wengi waliishi nje ya nchi ya Israeli, kutokana na ufukara wa nchi na vita vingi vya zamani vilivyosababisha wakimbizi kuhamia nchi zenye usalama zaidi. Jumuiya za Wayahudi zilipatikana katika miji yote mikubwa ya Afrika Kaskazini (hasa Misri na Libya), Ulaya Kusini na Asia Magharibi mpaka Uajemi. Kwa jumla watu wa huko walifuata dini zao za asili za kuabudu miungu mingi. Palikuwa na mchanganyiko wa imani mbalimbali. Wanajeshi Waroma waliokaa katika nchi nyingi walileta miungu yao na kuwajengea mahekalu pale walipokaa. Katika mazingira yao Wayahudi walikuwa watu pekee waliomshuhudia Mungu mmoja tu. Walikuwa tofauti na wengine kwani hawakushiriki katika ibada ya miungu ya serikali, tena walitunza utaratibu wa Sabato yaani kutofanya kazi siku ya saba. Kwa njia ya Wayahudi hao habari za Mungu mmoja zilikuwa zinasikika sehemu nyingi.

Kwa upande mmoja Wayahudi walitoka katika ukoo wa Abrahamu, hasa waliokaa nchini Israeli, lakini watu wengine, wenye asili ya mataifa tofauti, waliwahi kuvutiwa na imani ya Wayahudi hata wakachukua hatua ya kuongoka na kutahiriwa wakahesabiwa Wayahudi kamili.

Mitume wa Yesu walitumia usafiri uliopatikana wakati ule na kufikia nchi zilizojulikana katika mazingira yao lakini si mbali zaidi. Tena hapo awali kila walipokwenda walihubiri hasa katika jumuiya za Wayahudi na Kanisa lilionekana kama madhehebu ya Kiyahudi tu. Baada ya kuanza kupokea watu wengine pia bila kuwatahiri hali ilibadilika: Kanisa likawa taifa la Mungu kutoka kwa Wayahudi na kwa Mataifa.

Dola la Roma[hariri | hariri chanzo]

Dola la Roma lilikuwa na eneo kubwa sana katika nchi za mabara matatu kuzunguka Bahari ya Kati (Mediteranea). Mataifa mengi waliishi chini ya utawala wake. Utawala huo ulianza kabla ya Yesu kuzaliwa ukaendelea mpaka karne ya 5 baada ya Kristo. Hata mji wa Yerusalemu na nchi nzima ya Israeli vilikuwa chini ya Dola hilo. Vilikuwa na serikali yake ya Kiyahudi lakini pia na liwali au gavana wa Kiroma. Waroma hawakuwa na neno juu ya utamaduni na dini za nchi hizo ila walidai utiifu na kodi za mataifa na makabila yote yaliyokuwa chini yao. Walizima kwa ukali majaribio yote ya kupindua utawala wao. Wayahudi katika Israeli walijaribu mara mbili kuwafukuza Waroma nchini: miaka 66-73 na 135 BK Kila safari Waroma walilipiza kisasi, wakichoma moto miji na vijiji na kuwafanya wananchi kuwa watumwa au kuwaua kabisa.

Utawala wa Roma ulirahisisha biashara na uchumi pamoja na mawasiliano katika maeneo hayo yote. Waroma hawakuwa na mitambo ya injini lakini walikuwa wataalamu wa uhandisi. Walikuwa hodari sana kujenga barabara na nyumba za ghorofa. Majengo kadhaa waliyoyajenga husimama mpaka leo. Magofu ya miji yao yanaonekana kuanzia Misri na Algeria hadi Ujerumani na Asia. Wasanii wao walichonga sanamu za mawe za kudumu. Mkuu wa Dola aliitwa "Kaisari" na kukaa mjini Roma (Italia).

Watu wa Roma walifaulu kujenga dola hilo kubwa kwa karne nyingi. Kwa jumla walitawala kwa busara, hivyo wakafaulu kuendelea muda mrefu. Mwanzoni uraia ulikuwa kwa wakazi huru wa mji wa Roma tu, lakini polepole hata wakazi wa maeneo mengine chini ya Roma wakapewa haki za uraia.

Utawala wa Kiroma ulileta kipindi kirefu cha amani na cha maendeleo ya kiuchumi. Lakini maendeleo hayo yalijengwa juu ya utaratibu mkali wa unyonyaji wa nchi na mikoa ndani ya Dola. Kila sehemu wakazi walipaswa kulipa kodi. Kama kabila fulani lilijaribu kupinga utawala wa Roma wanajeshi wake wakafika haraka na kuzima ghasia. Kwa mfano Wayahudi walipojaribu kujipatia uhuru tena mnamo mwaka 70 BK mji wa Yerusalemu uliharibiwa kabisa na wakazi wote wakauzwa utumwani. Watoto wa watumwa walizaliwa watumwa. Njia nyingine ya kugeuzwa mtumwa ilikuwa kutolipa madeni. Mdaiwa aliweza kushtakiwa na akishindwa kulipa aliuzwa mwenyewe kama malipo ya madeni yake.

Idadi ya watumwa ilikuwa kubwa: katika mikoa kadhaa ya Dola la Roma watumwa walikuwa asilimia 20 za wakazi wote. Wengi wao walikuwa na maisha mabaya, lakini wengine waliweza kupata maendeleo na hata kupewa uhuru na mabwana wao.

Watumwa walifurahia sana kusikia mafundisho mapya ya Wakristo, kwamba kila mtu ni mtoto wa Mungu na anapendwa naye. Wakashangaa sana kusikia ya kwamba Yesu Kristo alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za watu wote, na Mungu hajali sifa au cheo cha mtu. Wakiingia katika ushirika wa Kikristo waliweza kushangaa wanavyoruhusiwa kukutana na watu huru na hata matajiri. Ibada za Kipagani zilitenga matabaka ya kijamii: haikuwa kawaida kwa tajiri kusali pamoja na watumishi wake.

Watumwa waliweza kusikia wakati wa ibada nyaraka za Mtume Paulo zinazokazia usawa kati ya Wakristo wote, akisititiza kwamba wote watazamane kama ndugu na viungo vya mwili mmoja. "Maana katika Roho mmoja tulibatizwa sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru" (1Kor 12:13).

Ndiyo sababu ujumbe wa Kristo ulienea hasa kati ya maskini na watumwa. Lakini hata watu wa matabaka ya juu walivutiwa na maneno ya Injili na mfano mzuri wa maisha ya Wakristo, uhodari wao katika mateso mbalimbali na utaratibu wao wa kusaidiana. Ilitokea pia kwamba, katika mwendo wa miaka, matatizo yalikua, vita vikaongezeka, uchumi na biashara vikashuka chini, thamani ya fedha ikapungua. Watu wengi wakaanza kukata tamaa au kutafuta faraja katika dini mbalimbali, Ukristo ukiwemo.

Afrika na sehemu nyingine za dunia[hariri | hariri chanzo]

Miaka 2000 iliyopita mawasiliano kati ya nchi na nchi hayakuwa rahisi. Hakukuwa na redio wala simu wala ndege wala magari. Usafiri ulikuwa kwa miguu au kwa kupanda wanyama (k.v. farasi, ngamia, punda), halafu kwa meli za tanga. Meli hizo ziliweza kufuata pwani tu, hazikuwa imara kutosha kuvuka bahari kubwa. Lakini hata kwa vyombo hivyo iliwezekana kufanya biashara kati ya Mediteranea na nchi za mbali kama Bara Hindi au Afrika Mashariki. Tunafahamu kitabu ambacho kiliandikwa mwaka 100 BK na kueleza usafiri wa baharini kutoka Misri hadi pwani ya Afrika Mashariki (iliyoitwa na Wagiriki "Azania"). Lakini watu waliojua habari hizo walikuwa wachache.

Mabara ya Amerika na Australia hayakujulikana na wataalamu wa Asia, Afrika na Ulaya. Watu wengi waliamini dunia kuwa tambarare yenye umbo la duara (kama sahani), ingawa wataalamu wa Misri walikwishagundua kwa njia ya vipimo kuwa dunia ina umbo la chungwa. Lakini si watu wengi walioamini au kujali elimu hiyo: ilikuwa nje ya upeo wao. Hali hiyo ilibadilika karne nyingi baadaye tu, wakati meli za kuvuka hata bahari kubwa zilipopatikana.

Wakati wa Yesu Afrika Kaskazini pia ilikuwa chini ya utawala wa Roma na wakazi wake hawakuwa [[Waarabu[[. Kiutamaduni kulikuwa na sehemu mbili: Wamisri upande wa Mashariki na Waberberi upande wa Magharibi. Nchi za Waberberi (Moroko, Algeria, Tunisia na Libya za leo) zilikuwa pia na miji mingi walipokaa wahamiaji kutoka Italia waliotumia lugha ya Kilatini. Mji mkuu wa sehemu ile ulikuwa Karthago (karibu na Tunisi ya leo). Mji mwingine unaotajwa katika Biblia ni Kurene (huko Libya). Misri ilikuwa kitovu cha utamaduni wa juu tangu karne nyingi. Mji mkuu wake ulikuwa Aleksandria. Eneo la utawala wa Roma lilifika mpakani mwa Sudan ya leo (eneo lililoitwa "Nubia").

Nchi za Afrika Kaskazini zilikuwa tajiri. Hali ya hewa ilikuwa afadhali kwa kilimo kuliko leo. Milima ya Atlas ilikuwa imejaa misitu. Katika Algeria na Tunisia ya leo ililimwa ngano kwa wingi na kuilisha Italia. Hata jina la "Afrika" lina asili yake katika kipindi cha Kiroma, lilipokuwa jina la mkoa mmoja uitwao leo Tunisia. Kutoka kule jina hilo lilitumika baadaye kwa sehemu nyingine za bara letu.

Nchi hizo hazikuwa na mawasiliano mengi na nchi za kusini kwa Sahara kwa sababu jangwa hilo lilikuwa kizuizi kikubwa kwa usafiri kati ya sehemu kubwa ya Afrika na nchi nyingine. Hivyo imani ya Kikristo ilifika haraka Kaskazini kwa Sahara isivuke jangwa hilo kubwa. Kumbe mawasiliano yalifanyika hasa kupitia Bahari ya Kati: ilikuwa rahisi kwa wafuasi wa Kristo kutumia mawasiliano hayo yaliyokuwepo tayari. Ni kweli kuwa watu kwa meli kutoka Mediteranea walifanya tayari biashara na pwani ya Afrika Mashariki, na tunaweza kuwaza wafanyabiashara Wakristo wakitembelea mapema sehemu zetu lakini hakuna kumbukumbu yoyote kwamba walihubiri n.k.

Watu wa Afrika Kaskazini walisafiri na kukaa katika miji ya Ulaya na Asia. Kutokana na hayo mawasiliano mazuri tunaona Waafrika mbalimbali katika taarifa za Agano Jipya, kwa mfano: - Yesu alipobeba msalaba wake kule Yerusalemu akaanguka chini. Askari wakamkamata mpitanjia jina lake ni Simoni wa Kurene. Jina linaonyesha kwamba alikuwa mgeni kutoka Libya (Lk 23:26). - wakati wa ushirika wa kwanza huko Yerusalemu Filipo alikutana na msafiri kutoka Kushi akambatiza. Kushi ni jina la kale la sehemu ya Sudan ya leo hata matoleo mengine ya Biblia hutafsiri: Mhabeshi au Mwethiopia (Mdo 8:26 n.k.). - katika mji mkubwa wa Antiokia (Asia Magharibi) kulikuwa na watu kutoka Afrika kati ya viongozi wa ushirika wa Kikristo. Mmojawao ni Lukio wa Kurene, mwingine ni "Simeoni aitwaye Nigeri" (Mdo 13). Neno "Nigeri" linatafsiriwa "Mweusi". Kumbe hata huyu anaonekana ametokea Afrika kutokana na rangi yake.

Haya yote si ajabu. Nchi za Misri mpaka Sudan na Afrika Kaskazini-Magharibi zilikuwa sehemu ya Dola la Roma wakati Ukristo ulipoanza kuenea.

Yesu mwenyewe alikaa miaka kadhaa Afrika katika utoto wake wakati wazee wake walipokimbilia pamoja naye Misri kwa sababu Mfalme Herode Mkuu alitaka kumwua. Mpaka leo Wakristo wa Misri wanatunza kumbukumbu ya uwepo wa Familia Takatifu katika nchi yao. Kuna makanisa mbalimbali mahali panapokumbukwa ya kwamba Yosefu, Maria na mtoto Yesu walipumzika.

Wakati wa Mitume[hariri | hariri chanzo]

Komunyo ya Mitume, kadiri ya Luca Signorelli, 1512.

Mwanzo wa Kanisa ni kule Yerusalemu, mji mkuu wa Wayahudi, ambako mnamo mwaka 30 BK Yesu wa Nazareti alikufa msalabani. Aliuawa na serikali ya kikoloni ya Kiroma. Liwali Mroma, kwa jina Pontio Pilato, alitoa dhidi yake hukumu ya mauti kwa ombi la viongozi wa Kiyahudi. Viongozi hao waliona kosa lake ni kwamba amejitangaza kwa uongo kuwa Masiya au Mwana wa Mungu. Lakini hilo halikuwa kosa machoni pa Waroma (ambao walikuwa Wapagani), hivyo wakatumia mashtaka yaliyoeleweka mbele za Pontio Pilato, la kwamba Yesu anataka kujipatia cheo cha Mfalme wa Wayahudi yaani kupindua utawala wa Kiroma. Biblia ya Kikristo inatuambia jinsi wafuasi wa Yesu walivyoanza kukata tamaa lakini baadaye wakakutana na Yesu aliyefufuka. Akaonana nao na kuwafundisha katika kipindi cha siku arobaini baada ya Pasaka na hatimaye akapaa mbinguni.

Kurasa 4 za Injili ya Luka zilizonakiliwa katika karne ya 3 katika nyasi zilizopondwa.

Kifo na ufufuko wa Yesu si mwisho wa ufunuo wa Mungu: ni lazima tupokee vilevile kama mpango wake yale yaliyojitokeza wakati wa Mitume wake. Miaka hiyo 70 hivi iliona Kanisa likizidi kusogea mbali na dini ya Kiyahudi na kuwa la kimataifa kweli pamoja na kupata muundo wa kudumu wa uongozi. Sambamba na hilo, makao yake makuu yalihamia Roma kutoka Yerusalemu uliokuja kuangamizwa tena mwaka 70. Ni wakati huohuo kwamba lilipata vitabu vitakatifu vya kwake vilivyokamilisha vile vya Agano la Kale. Kanisa linaheshimu kwa namna ya pekee, kama ushuhuda mkuu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu na kama moyo wa Maandiko matakatifu yote, Injili nne zilizoandikwa na Marko, Mathayo, Luka na Yohane kati ya mwaka 65 na 100 hivi. Mabadiliko hayo yaliyokusudiwa na Mungu hayakutokea bila ya matatizo, hasa kwa sababu yalikuwa magumu kueleweka kwa Wayahudi, ambao mwanzoni walikuwa wengi kati ya Wakristo, na hata kwa Mitume. Lakini Roho Mtakatifu aliwaongoza taratibu wakubali fumbo hilo lililofunuliwa hasa kwa Mtume Paulo. Suala gumu zaidi lilikuwa nafasi ya Torati katika Ukristo, hasa kwa waliojiunga nao moja kwa moja bila ya kutahiriwa kwanza ili wawe Wayahudi. Katika Agano Jipya inajitokeza misimamo 4 tofauti, na ni ajabu kwamba haikuvunja ushirika wa imani. 1. Wakristo wenye asili ya Kiyahudi, hasa ya Kifarisayo, walitaka watu wa mataifa watahiriwe kabla hawajabatizwa, halafu wafuate masharti yote ya Torati ili waweze kuokoka. 2. Wengine, kama Mtume Petro na Yakobo Mdogo, walitaka washike walau baadhi ya masharti hayo ili wasiwe chukizo kwa Wakristo wa Kiyahudi, hasa wakati wa kula pamoja ekaristi. 3. Paulo alikataa kupunguza uhuru wa Kiinjili kwa kudhani wokovu unategemea Torati kuliko msalaba wa Yesu; hata hivyo alisisitiza upendo kama tunu bora ya kuzingatiwa ili mtu asikwaze na kupoteza wengine dhaifu kama hao Wakristo wa Kifarisayo. 4. Hatimaye ulijitokeza msimamo mkali zaidi, wa kupuuzia kwa kiasi fulani Torati kama kitu kilichopitwa na wakati. Misimamo hiyo ya mwisho ulizidi kupata nguvu kadiri Wayahudi na Wakristo walivyozidi kutengana, lakini hata ule wa kwanza uliacha athari yake ya kudumu katika Kanisa hasa kupitia Injili ya Mathayo na Barua ya Yakobo.

Petro na wenzake[hariri | hariri chanzo]

Petro ni jina lenye maana ya "mwamba". Alipewa jina hilo na Yesu kwa sababu alitaka kumfanya msingi wa Kanisa lake. Alikutana naye akiwa mvuvi, akawa rafiki yake wa karibu sana. Yesu alipokamatwa Petro alitaka kutumia upanga wake ili amtetee. Lakini alipoulizwa baadaye kama yeye ni rafiki wa Yesu aliogopa akasema hamjui. Hata hivyo Yesu mfufuka alithibitisha uteuzi wake kwa kumkabidhi waumini wote, achunge kondoo na wanakondoo wake.

Katika ushirika wa Yerusalemu Petro alikuwa kiongozi mkuu. Alikuwa Mtume wa kwanza kumpokea katika Kanisa watu wasio Wayahudi bila kudai watahiriwe kwanza. Baada ya yeye kuhama Yerusalemu, Yakobo Mdogo ndiye aliyeongoza ushirika huo. Halafu Petro akawa katika mji mkubwa wa Antiokia lakini kadiri ya taarifa ya Luka alirudi kwa muda Yerusalemu aliposhauriana na Paulo na wengine juu ya namna ya kupokea Wapagani katika Ukristo (Mtaguso wa Yerusalemu wa mwaka 49). Baada ya kufanya utume Antiokia, aliweza kwa urahisi kutembelea mikoa ya Uturuki Kaskazini wa leo (Wakristo wa huko ndio aliowaandikia barua kwa msaada wa Sila) na Korintho, mji wa Ugiriki.

Kusulubiwa kwa Mtakatifu Petro, mchoro wa Filippino Lippi, 1481-1482 hivi, Firenze, Italia.

Kumbukumbu za kale zinasema alifika mpaka Roma alipouawa katika mateso ya kwanza ya Wakristo chini ya serikali kati ya miaka 64 na 68, wakiliachia Kanisa la mji huo usimamizi wa makanisa yote. Petro ni mfano mzuri wa nguvu na udhaifu katika maisha ya Kikristo. Alikuwa na moyo mkuu kumtetea Yesu kwa upanga asikamatwe - lakini hakuelewa kwamba njia ya Yesu si njia ya silaha. Alitaka kuwa karibu na Yesu - lakini kwa hofu akamkana. Alimwingiza katika Kanisa jemadari Mpagani - lakini baadaye akawaogopa waliodai Mpagani asijiunge na ushirika mpaka awe ametahiriwa na kuwa Myahudi kwanza. Mwishoni mwa maisha yake Petro akawa shahidi wa damu kwa Bwana wake akafa msalabani kama Yesu. Agano Jipya ina nyaraka mbili zilizoandikwa kwa jina lake.

Kanisa la Roma linamkumbuka kama mkuu wake wa kwanza. Baada yake, kila Askofu wa Roma huitwa "mwandamizi wa Petro" na “Papa” wa Kanisa Katoliki lote kwa sababu anashika nafasi yake na kuaminika kuwa wa kwanza kati ya maaskofu wote duniani.

Mitume wengine wa Yesu walikuwa Andrea, ndugu wa Petro, Yakobo na mdogo wake Yohane, washirika wao katika uvuvi, lakini pia Filipo, mwanakijiji mwenzao, na rafiki yake Nathanaeli Bartholomayo. Halafu kulikuwa na Mathayo mtozaushuru, Thoma, Simoni mwanaharakati, Yakobo Mdogo na Yuda wawili, yaani Tadayo na Iskarioti, maarufu kama msaliti wa Yesu. Wote walijitahidi kutekeleza agizo lake la kuinjilisha dunia yote, lakini kwa wengi wao hatuna habari za hakika walikwenda wapi.

Matendo ya Mitume[hariri | hariri chanzo]

Kati ya Wainjili, Luka hakuishia kuandika habari za Yesu tu, bali alizikamilisha kwa kuandika kitabu cha pili chenye historia ya mwanzo wa Kanisa. Kinajulikana kwa jina la Matendo ya Mitume, kwa kuwa kinawatokeza hasa watu wawili ambao Luka aliwafahamu, yaani Mtume Petro mpaka sura ya 12, halafu Mtume Paulo. Kwa namna ya pekee alikuwa mwanafunzi wa Paulo akamfuata mpaka kifo chake: hivyo si ajabu kwamba alipenda kushuhudia kazi zake na mateso yake kwa ajili ya Kristo na uenezi wa imani. Mpangilio wa kitabu hicho unaelezwa katika 1:8, yaani kuonyesha jinsi imani hiyo ilivyoshuhudiwa toka Yerusalemu hadi mwisho wa dunia upande wa magharibi. Ndiyo sababu kitabu kinaishia na habari za Paulo kufikia Roma na kuanza utume huko mwaka 61, ingawa kuandikwa kiliandikwa kama miaka 20 baadaye. Kuanzia Injili yake, Luka anaonekana alivyojitahidi kuzingatia ukweli wa historia, lakini pia jiografia: katika Injili mambo yote yanaelekea Yerusalemu, ambapo Yesu alikwenda kufa na kufufuka, na katika Matendo ya Mitume mambo yote yanaanzia Yerusalemu, ambapo Roho Mtakatifu aliwashukia. Tukipenda kujua historia ya wokovu ilivyoendelea baadaye, hatuna budi kufuata kitabu hicho tukilinganisha habari zake na zile tunazozipata hasa katika barua za mitume. Kwa namna ya pekee zile za Paulo tunaweza kuzipanga kwa faida katika mfululizo wa habari za maisha yake alizotuachia Luka, ingawa kuna utatanishi fulani.

Kanisa la Yerusalemu[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya kusimulia uenezi wa Ukristo, Luka aliandika habari za Kanisa mama, yaani lile la Yerusalemu. Katika msingi wake tunaona mitume wakiwa wanasali pamoja na mama wa Yesu na waamini wengine. Majina ya hao 11 yameorodheshwa tena, halafu pengo lililoachwa na msaliti Yuda Iskarioti likazibwa ili idadi muhimu ya 12 ikamilike tena. Aliyeamua ifanyike hivyo ni Petro akitumia tayari mamlaka aliyoachiwa na Yesu, na akiweka masharti kwa mapendekezo ya watu, hasa kwamba mteule awe shahidi wa utume na wa ufufuko wa Yesu (Mdo 1).

Pentekoste ya Mitume ilivyochorwa mnamo mwaka 586 katika Biblia ya Rabbula nchini Iraki.

Baada ya idadi hiyo kukamilika tena, Roho Mtakatifu akawashukia wote katika nafasi maalumu, yaani Pentekoste (neno hilo la Kigiriki, maana yake ni "hamsini", kwa kuwa sikukuu hiyo inatimiza Pasaka siku 50 baada yake). Kwa kuwa siku hiyo ni ya hija, mji wa Yerusalemu ulikuwa umejaa wageni waliofika kutoka sehemu nyingi za dunia kushiriki sikukuu za Kiyahudi, wakiwemo Wayahudi na watu waliovutiwa na dini yao. Siku hiyo wanafunzi wa Yesu walimpokea Roho Mtakatifu; safari hiyo alijitokeza kama upepo wa nguvu kubwa ajabu uliojaza nyumba nzima (yaani Kanisa lote) na kama ndimi za moto zilizowashukia mojamoja kila mwamini aliyekuwemo (kwa kuwa karama zake ni mbalimbali). Hapo hao waoga, waliokuwa wamejifungia ndani kwa usalama, wakatoka nje ya mkutano wao wakaanza kumshuhudia Bwana wao kwa kuhubiria umati wa watu waliokusanyika kwa kufuata upepo huo. Walikuwepo watu kutoka Asia, Ulaya na Afrika Kaskazini, lakini kila mmoja aliwaelewa mitume kwa lugha yake mwenyewe. Hivyo umoja wa binadamu uliovunjika Babeli katika kujenga mnara wa kiburi ukapatikana tena Yerusalemu kwa nguvu ya Yule aliye upendo wa Mungu. Toka mwanzo Kanisa si la kabila la Yuda tu au la lugha ya Kiaramu tu, bali la mataifa yote na la lugha zote. Aliyesimama kwa niaba yake lote atoe hotuba ya kwanza na kufafanua matukio hayo pamoja na kumshuhudia Kristo mfufuka ni Petro. Maneno yake yaliwachoma moyo wasikilizaji hata wakamuuliza wafanye nini. Jibu likawa watubu na kubatizwa ili wapate msamaha na Roho Mtakatifu. Watu ambao waliamini wakabatizwa. hawakupungua elfu tatu: ndio mwanzo wa ushirika wa Kikristo. Ndiyo sababu Pentekoste ni sikukuu ya kuzaliwa kwa Kanisa.

Luka ametuachia picha ya Kanisa mama hasa katika mihtasari mitatu (Mdo 2:42-47; 4:32-35; 5:12-16) ambayo inachora maisha ya Wakristo wa kwanza kama kielelezo kwa wale wote watakaofuata.

Aliandika kwamba wote waliobatizwa siku ya Pentekoste "waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kindugu, kumega mkate na kusali".(Mdo 2:42). "Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawana pamoja".(Mdo 2:44) "Jumuiya yote ya waumini ilikuwa moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kukabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake". (Mdo 4:32-35). Ushirika wa Wakristo leo unaonekana tofauti katika mambo mbalimbali. Tusishangae: Yesu alitumia mfano wa mbegu ndogo inayotarajiwa kuwa mti mkubwa baadaye. Watu 120 wa kwanza wamekuwa leo 2,500,000,000! Picha aliyotuachia Luka si sheria ambayo ni lazima tuifuate, bali ni mfano bora tu kwetu, ambao tuzingatie kwamba kila mahali mazingira ni tofauti. Tangu miaka 2000 Wakristo wamepata kusikia tena na tena habari hizo wakapata mawazo mazuri jinsi gani ya kujenga jumuiya ya kindugu na ya kusaidiana katika mazingira yao hapa duniani. Mpaka leo tabia kadhaa zilizotajwa katika Biblia zinakubalika kuwa alama za Kanisa:

  • a. kujifunza toka kwa mitume wa Yesu
  • b. kuishi pamoja kindugu na kuwasaidia wanyonge
  • c. kumega mkate, yaani kushiriki sakramenti
  • d. kusali

Katika historia yote ya Kanisa wengi wakaja kujipima kwa kuangalia kielelezo hicho cha umoja katika roho na katika mali. Hata hivyo ushirika wa Wakristo leo unaonekana tofauti katika mambo mbalimbali. Tusishangae: kila mahali mazingira ni tofauti na idadi ya waamini imefikia mabilioni. Picha hiyo ya awali si sheria ambayo ni lazima tuiige, bali ni mfano bora tu. Kwa miaka 2000 Wakristo wamepata kusikia tena na tena habari hizo wakapata mawazo mazuri kuhusu jinsi ya kujenga jumuiya ya kidugu na ya kusaidiana katika mazingira mapya hapa duniani.

Hali ya kushirikiana mali zote haikuendelea kama utaratibu wa kawaida wa Wakristo wote. Lakini kutokana na mfano huo zimejitokeza jumuiya mbalimbali katika maisha ya Kanisa. Hasa watawa wengi wakaja kujaribu kutekeleza tena umoja huo mashirikani mwao na hivyo kuwachochea waamini wenzao wote. Umoja huo ndio sifa ya kwanza ya Kanisa na mpango wa Mungu kwa watu wote.

Aina mpya ya viongozi[hariri | hariri chanzo]

Mwanzoni umoja ulifanikiwa kwa namna ya pekee, ingawa hapo pia ulikuwa na kasoro tunavyosoma katika vitabu vyote vya Agano Jipya. Kutokana na malalamiko ndani ya jumuia, mitume waliamua kuwashirikisha kazi yao katika ngazi ya chini watu saba ambao walishughulikie hasa huduma za upendo, yaani kuwagawia wajane na wazee misaada: idadi hiyo katika Biblia inamaanisha mataifa, na kweli wote walikuwa na majina ya Kigiriki (Mdo 6:2-6). Tofauti za waamini hasa upande wa lugha na utamaduni zinadai daima ubunifu na nia njema zisije zikavuruga umoja. Shida iliyotokea hapo ni utangulizi wa habari nyingine kuhusu Wakristo wa Kiyahudi kuwabana wenzao wenye asili ya Kipagani.

Kila jumuiya ina mbinu zake za uongozi. Kama kundi ni kubwa, haiwezekani kufanya kila kitu pamoja. Watu wakiwa wengi ni lazima kugawana kazi na madaraka. Suala hilo limekuwa muhimu sana katika historia ya Ukristo. Njia mbalimbali za uongozi ambazo zilitafutwa na kujaribiwa zinaonyesha tofauti kubwa kati ya madhehebu mbalimbali. Vyeo maalumu vilivyopo katika Ukristo leo, vina asili katika ugawaji wa madaraka ulivyokuwa wakati wa mitume.

Mkuu wa jumuiya ya wanafunzi wa Yesu tangu mwanzo alikuwa yeye mwenyewe. Katika ushirika wa kwanza kule Yerusalemu Mitume, yaani marafiki wa Yesu wa karibu waliotumwa naye na kupewa kazi ya kueneza Habari Njema, ndio waliokuwa viongozi. Lakini baada ya muda mfupi kazi zikawa nyingi, hivyo wakaongeza hao "Wasaidizi saba". Katika nyaraka za Paulo (ambazo ni maandiko ya kwanza ya Agano Jipya) tunaona hali ya miaka 20-35 baadaye: yeye anataja mitume, manabii, walimu, wenye vipawa mbalimbali (1Kor 12:28 n.k.), au maaskofu na mashemasi, pia wazee. Kwa jumla hakuna picha kamili ya utaratibu mmoja uliokuwepo kila mahali. Kumbe mwishoni mwa karne ya kwanza cheo cha "Askofu" kiliimarika sana, lakini pia chini yake vyeo vya Kasisi na Shemasi vilikuwa kawaida. Mashemasi wa kike walikuwepo, lakini walitoweka baadaye, labda kutokana na utamaduni uliotoa kipaumbele kwa wanaume. Hivyo mapema ulipatikana muundo mmoja wa uongozi kila jimbo, yaani askofu mmoja akisaidiwa na mapadri na mashemasi, badala ya mitindo mbalimbali iliyojitokeza awali. Ni hasa Ignas wa Antiokia ambaye katika barua zake anathibitisha muundo huohuo kila mahali alipopitia kutoka Siria hadi Italia mwanzoni mwa karne ya 2.

Katika Mdo 6-8 hao viongozi 7 wapya wanajitokeza kama mashujaa katika utume, ambao mwisho wake kwa Stefano ulikuwa ni kifodini. Katika kusimulia tukio hilo la mwaka 36 hivi, Luka alisisitiza kuwa mashtaka ya Wayahudi dhidi ya Stefano ni yaleyale yaliyomhusu Yesu: yaani upinzani dhidi ya mwalimu unaendelea dhidi ya wanafunzi wake. Vilevile Stefano akakabili mateso kama alivyofanya Yesu akimkabidhi Bwana roho yake na kuwaombea watesi wake. Kabla ya hapo Wakristo walikuwa wamedhulumiwa katika nafasi mbalimbali, lakini dhuluma hiyo ya tatu ikawa kubwa zaidi na kusababisha wengi wakimbie Yerusalemu. Lakini kwa mpango wa Mungu mtawanyiko huo ulichangia kueneza Injili.

Rembrandt, Ubatizo wa towashi, (1626 hivi).

Kufuatana na mpangilio wa kitabu, Mdo 8 inaeleza jinsi Mungu alivyoongoza uenezi wa Kanisa kwa watu wasiokubaliwa na Israeli, yaani kwanza kwa Wasamaria waliokuwa maadui wakuu wa taifa teule, halafu towashi (yaani mwanamume mbovu) toka Ethiopia. Katika nafasi hizo zote mbili Luka alisisitiza furaha iliyotokea kama dalili ya wokovu. Juhudi za Filipo mwinjilisti zikaja kuthibitishwa na mitume kwa kuwawekea mikono Wakristo wapya wa Samaria. Wakati uleule likatukia jambo lingine, la ajabu kabisa, ambalo limesimuliwa na Luka mara tatu, yaani uongofu wa Saulo/Paulo aliyekuwa mtesi mkuu wa Stefano na Wakristo wengine. Ndiye aliyechaguliwa na Mungu awe mwenezi mkuu wa imani ya Kikristo, mtetezi mkuu wa uhuru wa Wakristo wa mataifa kuhusu sheria za Kiyahudi, tena mwandishi mkuu wa Agano Jipya, mwenye kufafanua mafumbo ya imani kwa undani kabisa. Mungu alimteua awe chombo chake kiteule ili kuleta jina lake kwa mataifa (Gal 1:13-24; Mdo 9:1-31; Mdo 22:17-21): katika historia yote ya Kanisa baada ya Pentekoste hadi leo hakuna tukio lingine muhimu zaidi.

Paulo alikuwa Myahudi Farisayo mzaliwa wa Tarso (mji wa Kilikia, leo nchini Uturuki). Alikaa Yerusalemu kwa masomo ya kidini lakini hakumfahamu Yesu. Aliporudi huko, baada ya yeye kuacha dunia, alihusika na kifodini cha Stefano (Mdo 6) akatumwa na Baraza Kuu la Taifa kutafuta na kukamata kama wazushi Wayahudi waliojiunga na Ukristo. Aliposafiri kwa ajili hiyo hadi Dameski (mji mkuu wa Siria), alitokewa na Yesu katika ono akaongoka kuwa Mkristo. Hivyo mtesaji wa Wakristo akawa mhubiri mkuu wa Injili. Hakuna mwingine kati ya mitume wote ambaye alisafiri, kuhubiri na kuanzisha jumuia kama Paulo. Katika safari kubwa tatu alizunguka Asia Magharibi na Ulaya Kusini, lakini pia alifundisha kwa njia ya barua (au nyaraka). Nyaraka zake mbalimbali zimehifadhiwa katika Agano Jipya. Humo Paulo anaonekana kuwa mtaalamu wa Sheria ya Kiyahudi ilivyo katika Agano la Kale, lakini alionyesha jinsi uhuru katika Kristo unavyopita masharti ya sheria za Musa akatetea kupokea Wapagani katika Kanisa bila kuwadai wafuate masharti hayo.

Mwishoni akakamatwa Yerusalemu akashtakiwa ya kuwa amehatarisha amani. Kama mzaliwa wa Tarso alikuwa na uraia wa Roma akadai haki yake ya kukata rufaa kule, mbele ya Kaisari. Akapelekwa Roma (Mdo. 28). Baada ya kesi yake kushindikana alipata nafasi ya kusafiri tena na kuhubiri Injili mpaka Hispania. Lakini kumbukumbu ya kale inatuambia kuwa aliuawa Roma baada ya Petro kwa kukatwa kichwa katika mateso ya kwanza ya Wakristo (64-68 BK).

Paulo ni mfano mzuri wa jinsi mtu aliyepinga Injili vikali alivyoongozwa kuihubiri. Imekadiriwa kwamba kwa muda wa miaka 13 alisafiri umbali wa kilometa 14,000 hivi bila kujali afya yake mbovu. Tukikumbuka ugumu wa safari wakati ule, tunaweza kuhisi alivyokuwa na juhudi. Nyaraka zake zinatuonyesha jinsi gani Mkristo anaweza kutumia akili yake pamoja na imani. Katika maandishi yake tunamuona kama mtu aliyesukumwa na upendo wa Kristo kati ya matatizo na mateso makubwa. Anatufundisha kutoangalia Ukristo kama sheria au amri tu (Fanya! Acha!) bali kama jibu la upendo la mtu aliyeelewa Mungu alivyotupenda kwanza.

Ukubwa na ubora wa mchango wa Paulo unaeleweka tukizingatia kwamba alifanya kazi na kuandika kabla ya vitabu vya Agano Jipya kupatikana. Ndiye aliyeanza kuliandika akipanua mawazo aliyoyapokea katika Kanisa kwa kuzingatia Agano la Kale na mang’amuzi yake mwenyewe. Hapo alifafanua vizuri ajabu maisha ya Kikristo kama neema ya kumshiriki Yesu kwa imani, sakramenti na juhudi za kushinda umimi hadi kugeuka sadaka hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu. wokovu huo, utakaokamilika katika ufufuko wa mwili, unapatikana katika Kanisa, ambalo Paulo alilitambulisha kama bibiarusi wa Kristo na mwili wake.

Lakini, kabla Luka hajasimulia umisionari wake, aliandika habari nyingine ya ajabu ambayo pia inapatikana mara tatu katika Matendo ya Mitume, yaani uongofu wa Kornelio na nyumba yake (Mdo 10). Wapagani hao walijaliwa Roho Mtakatifu kabla hawajabatizwa, wakimsikiliza tu mtume Petro. Hivyo Mungu alimuonyesha mkuu wa mitume nia yake kuhusu wokovu wa mataifa, naye Petro akalitangazia Kanisa kwamba Wapagani wasilazimishwe kufuata sheria za Kiyahudi. Uamuzi huo uliofuata hiyo Pentekoste ya mataifa ilimfungulia Paulo mlango wa umisionari wake unaotawala Mdo 13-28. Ingawa Wakristo wenye msimamo mkali wa Kiyahudi walikubali maneno ya Petro (Mdo 11:1-18), hawakuweza kumuunga mkono Paulo aliposisitiza kwamba wokovu unategemea imani kuliko utekelezaji wa sheria. Basi, mvutano juu ya suala hilo ukaendelea kuvuruga maisha ya Kanisa kwa miaka mingi ya mbele.

Ni baada tu ya Petro kufungua mlango kwamba Mdo 11:19-26 inasimulia jinsi waliotawanyika baada ya uuaji wa Stefano walivyoeneza Ukristo huko walikohamia nje ya nchi takatifu, wakiwahubiria kwanza Wayahudi wenzao, halafu Wapagani. Kitabu kizima kinafuata utaratibu huo: Paulo mwenyewe kila alipofika aliwaelekea Wapagani baada tu ya Wayahudi kukataa Injili.

Kati ya miji ambapo ilianzishwa jumuia ya waamini wengiwengi, muhimu zaidi ni Antiokia (mpakani kwa Sirya na Uturuki wa leo): huko wafuasi wa Yesu walikuwa mchanganyiko mkubwa wa Wayahudi na mataifa, hivyo wakapewa jina jipya maalumu la Kiyunani (Wakristo). Ndipo walipofanya kazi Barnaba aliyetumwa na mitume, Paulo aliyeitwa naye kumsaidia, pamoja na manabii na walimu wengine.

Wakati huohuo (mwaka 44 hivi) Herode Agripa alimuua Yakobo Mkubwa (mtume wa kwanza kumfia Yesu) akakusudia kumuua hata Petro, lakini huyo akahama Yerusalemu (Mdo 12:1-17) akafanya kazi huko na huko kabla hajahamia moja kwa moja Roma akiuletea mamlaka yake.

Safari za kimisionari za Paulo zilivyoanza (46-49)[hariri | hariri chanzo]

Kanisa changa na motomoto la Antiokia likawa kituo cha umisionari kuanzia mwaka 46; kwa mara nyingine Roho Mtakatifu ndiye aliyechochea juhudi za kitume na kuteua watu wa kutumwa, yaani Barnaba na Paulo (Mdo 13:1-3). Safari yao ya kwanza ilichukua miaka 3 katika kisiwa cha Kupro na mikoa ya kusini ya Uturuki wa leo (Mdo 13:16-51; 14:19-23). Ilikuwa kawaida yao kuanzisha Kanisa katika miji mikubwa ili toka huko ujumbe ufike hadi vijijini.

Mtaguso wa Yerusalemu (49)[hariri | hariri chanzo]

Yakobo Mdogo, kiongozi wa Wakristo wa Kiyahudi mjini Yerusalemu, aliyekubali Wakristo wa mataifa wasilazimishwe kushika Torati.

Waliporudi Antiokia walipaswa kupambana na Wakristo wa Kiyahudi kuhusu uwezekano wa mataifa kuokoka pasipo kutahiriwa. Hatimaye suala likapelekwa Yerusalemu kwa Kanisa mama. Baada ya majadiliano marefu Petro akatoa neno la mwisho kwamba Wapagani wanaomuamini Yesu wasitwishwe mzigo usiobebeka wa kufuata sheria za Kiyahudi (Mdo 15:1-12). Katika Gal 2:1-10 Paulo pia ametuachia kumbukumbu ya mtaguso huo akisisitiza kuwa mitume waliokuwepo (Yakobo Mdogo, Petro na Yohane) walitambua rasmi karama ya kimisionari ya kwake na ya Barnaba na uhalali wake, wakiwaomba tu wachangishe pesa kati ya Wakristo wa mbali kwa ajili ya wenzao wa Yerusalemu wwnye hali ngumu. Hiyo ilikuwa namna mpya ya kutekeleza upendo wa kidugu na kudumisha umoja wa Kanisa baada ya uenezi wake.

Masuala hayo yakadai uamuzi mwingine ili Wakristo wa Kiyahudi waweze kuendelea kushirikiana na wenzao wa mataifa pasipo kuogopa unajisi ambao ungewazuia wasifuate ibada zao. Gal 2:11-14 inaeleza shida iliyotokea Antiokia: ingawa Paulo alimheshimu sana Petro, alipoona hafuati kwa unyofu uamuzi wa mtaguso hakusita kumkosoa kidugu hadharani ili aliepushe Kanisa na upotovu kuhusu suala la wokovu. Basi, kadiri ya Mdo 15:13-35, Yakobo Mdogo aliyeachiwa uongozi wa Kanisa la Yerusalemu alichagua makatazo makuu manne kutoka Mambo ya Walawi akidai Wakristo wote wayashike kama mambo mazito kwa dhamiri ya Kiyahudi. Uamuzi huo uliarifiwa kwa Wakristo wa Antiokia na mikoa ya jirani kwa wajumbe na barua. Barua zikaendelea kuandikwa hata leo kwa lengo la kudumisha umoja na amani katika Kanisa, kwa kuwa ni kazi ngumu kuelewana kwa watu tofauti kama hao waliozoea kudharauliana kwa matusi kama “mbwa”.

Safari ya pili ya Mtume Paulo (50-52)[hariri | hariri chanzo]

Mtume Paulo akitoa Hotuba ya Areopago huko Athene, kadiri ya Raffaello Sanzio, 1515.

Mdo 15:36-39 inasimulia ugomvi kati ya Paulo na Barnaba walipotaka kufunga safari tena (mwaka uleule 49). Mungu hakuzuia ugomvi huo kusudi hao wawili waeneze zaidi neno lake wakienda sehemu tofauti. Barnaba na Marko walielekea Kupro, kumbe Paulo alimchukua Sila na kufunga safari iliyodumu miaka mitatu, akielekea kwanza jumuia zile za bara alizoziunda miaka iliyopita (Mdo 15:40-16:5).

Paulo ni maarufu kwa juhudi zake za kueneza Ukristo mahali pengi palipokuwa bado, lakini pia tunajua upendo wake kwa watu aliowatangazia habari njema, na bidii zake kwa makanisa aliyoanzisha: alikuwa akiwaombea usiku na mchana, akiwaka hamu ya kuwatembelea, akiwaandikia barua za kusisimua ili kuwatia moyo au kuwakosoa, kutatua matatizo yao na kujibu maswali mbalimbali. Pengine aliwatumia watu alioongozana nao: kati yao alimpendelea Timotheo akashirikiana naye mpaka kufa.

Kadiri ya Mdo 16:6-15, katika safari hiyohiyo kwenye mikoa mbalimbali ya Uturuki wa leo, huenda Luka pia akajiunga na msafara akifuatana na Paulo hadi kufa kwake. Yeye anatia maanani uongozi wa Mungu ambaye kwanza aliwazuia mara mbili wasielekee walikokusudia, halafu kwa njozi alionyesha ni mapenzi yake wavukie Ulaya katika Ugiriki wa leo.

Inavyojulikana, Wayunani walikuwa na hamu kubwa ya kupata maarifa kuliko wengine, halafu kubishana nao kwa ufasaha na kuwashinda. Katika mazingira hayo, falsafa na dini zilikuwa mada kuu na kuingiliana na hadithi za ajabuajabu kuhusu miungu, malaika na wengineo. Karibu barua zote za mitume zilikabili hatari hiyo, ambayo ikazidi kuwa kubwa na kuleta mafarakano katika Kanisa hasa katika karne II, ilipoitwa “Gnosis” (= ujuzi). Hasa Paulo alijitahidi kuishinda mapema iwezekanavyo.

Huko Ugiriki wakaanzisha Kanisa kwanza Filipi, halafu Thesalonike. Kutokana na dhuluma za Wayahudi, Paulo alilazimika kuondoka akafika Athene, mji mkuu wa falsafa, akajaribu kutangaza Injili kwa ufasaha wa maneno ili kuwavuta hao watu wa elimu; kumbe akashindwa kabisa (Mdo 17). Ndipo alipoelewa kuwa imani haitegemei akili na elimu, akaamua kuhubiri kwa unyofu tu mafumbo ya imani (1Kor 1:17-2:5).

Mdo 18:1-11 inasimulia mang’amuzi mengine aliyoyapata katika jiji la Korintho, lenye bandari mbili katika bahari tofauti zilizoleta urahisi wa kuvusha bidhaa toka moja hadi nyingine badala ya kuzisafirisha kwa meli kandokando ya rasi. Kutokana na umuhimu huo na wa kuwa makao makuu ya mkoa wa Akaya (Ugiriki kusini), pamoja na biashara kubwa, kulikuwa na mchanganyiko wa watu, wakiwemo watumwa na makahaba wengi. Huko alikaa mwaka mmoja na nusu kutokana na kufunuliwa na Yesu kwamba ana wateule wengi jijini. Kweli utume wa Paulo ukazaa sana, ingawa kabla hajafika walikuwepo tayari Wakristo kadhaa kama Akwila na Priska waliofukuzwa na kaisari Klaudio mwaka 49 watoke Roma pamoja na Wayahudi wote hasa kutokana na mabishano yao kuhusu Kristo.

Barua za Paulo na wengine[hariri | hariri chanzo]

Paulo Akiandika Nyaraka Zake, karne ya 17.

Akiwa Korintho, Paulo akawaandikia kwa furaha barua tuliyonayo mpaka leo ili kuwahimiza na kuwaelimisha zaidi: ndiyo andiko la kwanza la Agano Jipya kwa kuwa ni wa mwaka 51 hivi.

Kati ya vitabu 27 vya Agano Jipya, 21 vina mtindo wa barua au nyaraka. Hiyo ni tofauti kabisa na Agano la Kale, ambamo vitabu kadhaa vinazileta, lakini si kitabu kizima hata kimoja. Mtume Paulo ndiye aliyetumia zaidi mtindo huo ili afikie na ujumbe na mamlaka yake pale asipoweza kufikia kimwili. Barua 14 zinahusishwa na yeye kwa namna moja au nyingine, wakati nyingine 7 zinahusishwa na Yakobo Mdogo, Mtume Petro, Mtume Yohane na Yuda Tadei. Hii haina maana kwamba ziliandikwa zilivyo na Mitume hao. Kwanza, tokea awali watu waliweza kuandika barua kwa mkono wao, au kwa kumuongoza karani aandike maneno yao wenyewe, au kwa kumpa maelekezo ya jumla kuhusu namna ya kuandika kama si kumuachia aandike anavyoona inafaa. Zaidi ya hayo, wakati wa Mitume ilikuwa kawaida kuandika kwa kutumia jina la marehemu fulani maarufu kama kwa kumwezesha aendelee kutoa ujumbe aliokuwa anautoa maishani. Pengine aliyeandika hivyo alikuwa na uhusiano wa pekee na marehemu huyo kama mwanafunzi au mwandamizi wake.

Pengine maandishi hayo hayakuwa tu barua fupi za kuwasiliana kuhusu shida fulani, bali hati au insha ndefu kuhusu mada fulani: ndizo zinazostahili kuitwa nyaraka. Ingawa tofauti kati ya barua na waraka inaeleweka kinadharia, pengine ni vigumu kugawa vitabu hivyo vya Agano Jipya katika makundi mawili: kwa hakika Eb ni waraka na 3Yoh ni barua, lakini nyingine ziko katikati. 2Pet, ambayo inafikiriwa kuwa ya mwisho kuandikwa, inashuhudia kwamba tayari barua za Paulo zilikuwa zimekusanywa na kuheshimiwa kama Maandiko Matakatifu.

Apolo, mmisionari kutoka Afrika[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 52 Paulo aliondoka kwa hiari Korintho kuelekea Yerusalemu na Antiokia. Njiani alihubiri kidogo Efeso, makao makuu ya mkoa wa Asia Ndogo (Uturuki Magharibi wa leo), lakini hakukubali kubaki muda mrefu zaidi, ila aliwaacha huko Priska na mumewe akiahidi kurudi, Mungu akipenda (Mdo 18:18-22). Huo ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya mseja na watu wa ndoa katika utume.

Mdo 18:24-28 inasimulia kwamba, baada ya Paulo kuondoka, alifika Myahudi wa Aleksandria, jina lake Apolo. Kama vile wenzake wengi wa Misri alikuwa na elimu ya Kiyunani na ujuzi wa Biblia.

Tena alikuwa motomoto katika kufundisha habari za Yesu, ingawa hazijui sawasawa, hasa hana habari ya ubatizo wake mpya (kasoro hiyo ikaendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa sababu baadhi ya wanafunzi wa Yohane Mbatizaji hawakumuamini Yesu, hivyo wakaendeleza ujumbe wa mwalimu wao).

Priska na mumewe wakamuelimisha zaidi, halafu wakampa barua ya kumtambulisha kwa Wakristo wa Korintho alipokwenda kuhubiri. Wamisionari wa namna hiyo wakazidi kustawisha na kuvuruga makanisa walau mpaka mwisho wa wakati wa mitume.

Safari ya tatu ya Mtume Paulo (54-58)[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kukaa Antiokia mwaka mmoja na nusu Paulo akafunga tena safari akiyapitia makanisa ya Galatia na Frigia ili kuyathibitisha (Mdo 18:23). Hatimaye akafika Efeso ambapo akabaki tangu mwaka 54 hadi 57, akifundisha kila siku na kueneza sana Injili katika mkoa mzima (Mdo 19:1-10). Pamoja na hayo aliandika barua kadhaa, ambazo baadhi zimepotea, nyingine tunazo hadi leo (kwa Wagalatia, kwa Wafilipi, ile ya kwanza kwa Wakorintho, inawezekana Filemoni pia).

Luka hakusimulia mateso yote ya Paulo, kwa mfano alivyohukumiwa mwaka 56 hivi hukohuko Efeso (1Kor 15:32; 2Kor 1:8-9).

Kutoka Korintho habari za kusikitisha zilimfikia Paulo akiwa Efeso (pengine mwaka 57): katika Kanisa hilo ambalo alilianzisha na kulipenda sana kulikuwa na shaka kuhusu imani, mafarakano, upinzani wa Wakristo wa Kiyahudi dhidi yake, na makwazo.

Kilichohatarisha zaidi jumuia hiyo ni karama mbalimbali ambazo hao Wakristo wachanga walizijali mno na hatimaye wakajivunia kuwa nazo. Vilevile walivutiwa kumfuata mtu kama Apolo, mwenye ujuzi na ufasaha mkubwa, mambo yaliyopendwa sana na Wagiriki. Ilimbidi Paulo arekebishe hali hiyo ili kuokoa hasa umoja wa Kanisa na heshima kwa viongozi wake halali.

Basi mwaka mzima akawa na mahangaiko kwa Wakorintho akawaandikia walau barua nne au tano, ingawa sisi tunazo mbili tu; pengine sehemu za baadhi yake zimeshonwa ndani ya 2Kor.

Mdo 19:21-20:1 inasimulia alivyohama Efeso kutokana na matatizo kuzidi, akaelekea Makedonia na Ugiriki. Toka huko alipata nafasi ya kuhubiri huko Iliriko, yaani Albania ya leo kwenda kaskazini (Rom 15:19).

Ingawa Paulo alikaa Efeso miaka mitatu, moyo wake wa kimisionari haukutulia kwa sababu alikumbuka alivyotabiriwa atafanya kazi hata mbali zaidi. Ndiyo maana alitaka kwenda Ulaya magharibi, yaani Roma na halafu Hispania, nchi iliyohesabika kuwa mwisho wa dunia. Ila kabla ya kwenda huko alipanga kuleta mchango wa Wakristo wa mataifa kwa wenzao wa Yerusalemu.

Basi, mwishoni mwa miezi mitatu aliyokaa Korintho (Mdo 20:2-3) akijiandaa kupanda meli, yaani mwanzoni mwa mwaka 58, Paulo aliwaandikia Wakristo wa Roma ili kuandaa utume atakaoufanya katika jiji hilo. Huko Ukristo uliingia toka mwanzo kabisa, ukiletwa na baadhi ya Wayahudi wengi walioishi Roma ambao walibatizwa Yerusalemu kwenye Pentekoste ya mwaka 30.

Wayahudi wote walipofukuzwa na Kaisari Klaudio (49), Wakristo wa mataifa mengine wakabaki ndio wengi, nao wakaachana na masharti mbalimbali za Kiyahudi, kama yale kuhusu vyakula.

Muda mfupi baada ya Klaudio kufa (54), Wayahudi walianza kurudi, kumbe wakakuta mabadiliko hayo makubwa ndani ya Kanisa, nao wakajiona wamewekwa pembeni kidogo, kama si kudharauliwa na Wakristo wa mataifa.

Mtume Paulo akijua umuhimu wa Roma, mji mkuu wa ulimwengu wa zamani hizo, aliwaandikia Wakristo wa huko barua ndefu tena nzito kuliko zote. Alitaka kuwaeleza kwa maandishi ya mpango mafundisho yake kuhusu wokovu, kwa sababu walikuwa wamesikia habari tofautitofauti juu yake bila ya kukutana naye.

Ingawa haina mafundisho yote ya Paulo, barua hii imechangia teolojia ya Kikristo kwa kiasi kikubwa, hasa upande wa magharibi.

Kwa namna ya pekee inajibu kinaganaga maswali kuhusu wokovu: unapatikana kwa njia gani? Kwa nini Wayahudi wengi walishindwa kumuamini Yesu ili kuupata? Kwa nini mataifa yameupokea badala yao? Aliyepata wokovu anaishi vipi? Je, Wayahudi wametupwa moja kwa moja?

Pamoja na kuwaandaa hivyo wampokee vizuri, alichukua nafasi ya kuimarisha umoja wao ulioingia dosari. Hasa aliwaonya Wakristo wa mataifa wasidharau Wayahudi, kwa sababu hao bado ni wateule wa Mungu. Akigusa zaidi maisha ya Kanisa la Roma ya wakati huo, yaliyovurugwa na masuala madogomadogo kuhusu vyakula na sikukuu, Paulo alidai wenye nguvu watekeleze upendo kwa walio dhaifu zaidi, pamoja na busara, uelewa, mfano wa Yesu na uaminifu kwake. Maelekezo hayo yanaweza kusaidia daima kukabili mvutano wowote kati ya wenye mitazamo tofauti (finyu na mpana, au wa kizamani na wa kisasa zaidi). Lengo ni ule umoja uliofundishwa katika sura nane za kwanza.

Ukristo baada ya Paulo kufika Roma[hariri | hariri chanzo]

Kusulubiwa kwa Mt. Petro kadiri ya Caravaggio.

Paulo kupeleka mchango Yerusalemu (Mdo 20:16-21:36) ndio mwisho wa kipindi cha utume wake mkubwa zaidi. Sura tisa za mwisho za Matendo ya Mitume zinatusimulia kinaganaga habari zake kuanzia 58 hadi 63, ambapo karibu miaka yote alikaa kifungoni akisubiri kesi (Mdo 23:12-24; 24:22-25:22; 28:11-16,23-30). Bila ya shaka ilikuwa ya majaribu makubwa kwake, lakini ilimpa nafasi ya kutafakari mafumbo ya wokovu kwa undani zaidi tena, na ya kumshuhudia Kristo mbele ya wafalme (Agripa II na nyumba ya Kaisari) alivyotabiriwa. Kwa Luka ni muhimu sana kwamba Paulo alifika Roma na kuanza huko kazi yake ya utume, kiasi kwamba hakuendelea kuandika kilichofuata. Hasa kwamba mwaka 64 mfalme Nero alianza dhuluma za serikali dhidi ya Wakristo zilizoendelea mpaka 313, ingawa si mfululizo. Petro na Paulo waliuawa mjini Roma kati ya mwaka huo na mwaka 68, wakiliachia Kanisa la mji huo usimamizi wa makanisa yote. Kuhusu kipindi hicho tuna ushahidi wa vitabu mbalimbali vya Kipagani, vya Kiyahudi na vya Kikristo. Baadhi yake ni vile vya mwisho vya Agano Jipya ambavyo tunataka kuendelea kuvichambua. Waandishi wake pengine walitumia majina ya mitume ili kuyapa nguvu maandiko yao: inawezekana walikuwa warithi wa mamlaka yao na kuendeleza kazi zao. Mkazo wa vitabu hivyo unaelekea miundo ya Kanisa (uchungaji) kuliko umisionari (uvuvi). Wakati huohuo viliandikwa vitabu vingine pia, kama Didake, ambavyo viliheshimika na kutumika sana lakini hatimaye havikupokewa katika Biblia.

Katika hiyo miaka ya mwisho ya ufunuo, Wakristo wa mataifa wakazidi kuwapita wale wa Kiyahudi kwa idadi na kwa umuhimu. Nafasi ya Yerusalemu katika Kanisa ulizidi kupungua kutokana na hali ya nchi, yaani vurugu kati ya Wayahudi, Wayunani na serikali ya kikoloni. Mwaka 62 Yakobo, ndugu wa Bwana na kiongozi wa Kanisa la huko, aliuawa na Wayahudi. Tangu mwaka 66 hadi 73 hao walipigania uhuru wakashindwa; mwaka 70 Yerusalemu ulitekwa tena na Waroma na kuteketezwa pamoja na hekalu lake. Kuanzia hapo hadi leo dini ya Kiyahudi imebaki haina ukuhani wala sadaka; nguvu yake ni katika masinagogi inapofanyika ibada ya Neno la Mungu chini ya walimu wa sheria. Maangamizi hayo yalizidi kutenganisha Wakristo na Wayahudi, hasa kwa sababu Wakristo wa Yerusalemu walikimbilia ng’ambo ya Yordani badala ya kupigania uhuru, halafu wakarudi mjini mpaka vita vya pili vya Kiyahudi (132-135) ambapo Waroma wakabomoa tena Yerusalemu na kuwafukuza Wayahudi wote wasiweze hata kuingia wilayani na kuona kwa mbali mlima wake.

Injili Ndugu[hariri | hariri chanzo]

Tulivyoona, kwa muda wa miaka 30 na zaidi Wakristo walitangaza habari za Yesu hasa kwa midomo, halafu kwa barua na maandishi mengineyo. Lakini wakati huohuo (miaka ya 50?) baadhi yao walianza kukusanya kwa maandishi ushuhuda wa mitume na wengineo kuhusu mafundisho na maisha ya Yesu, kama vile mifano aliyoitoa, mabishano yake na Mafarisayo, na hasa mateso yake. Kati yao tunaambiwa Mathayo aliandika kwa Kiaramu, ingawa hatuna hata kipande cha kitabu chake na cha vinginevyo. Ila Wainjili wetu walivisoma na kuvitumia kwa kutunga vya kwao. Baada ya Injili zao nne kupatikana, Kanisa likaacha vitabu vya kwanzakwanza hata vikapotea.

Wataalamu wengi wanakubaliana kusema Marko ndiye aliyetangulia kuandika kitabu kamili juu ya maisha na mafundisho ya Yesu kuanzia utume wa Yohane Mbatizaji hadi ufufuko wake. Ndiye aliyekiita kitabu cha namna hiyo Injili, hata neno hilo, lililokuwa na maana ya ujumbe kuhusu Yesu, likaja kuwa na maana mpya ya kitabu cha habari za Yesu. Marko aliandika akiwa Roma mwaka 65 hivi, mara baada ya serikali kuanza kuwatesa Wakristo, na akiwa na nia ya kuwaimarisha katika dhuluma.

Baada ya Marko, watu wawili tena waliandika vitabu kama cha kwake, wakikitegemea kwa kiasi kikubwa na kukipanua kwa habari za utoto wa Yesu, mafundisho mengi zaidi n.k. Wataalamu wanaona Injili hizo za Mathayo na Luka ziliandikwa kati ya miaka 80 na 90, hata hatujui ipi imetangulia. Mazingira ni yaleyale ya Mashariki ya Kati, labda Antiokia, ila walengwa ni tofauti. Injili ya Mathayo iliandikwa kwa ajili ya Wakristo wa Kiyahudi wakati mabishano kati ya Kanisa na Israeli yalipozidi, na ina lengo la kuwaimarisha katika imani yao kuwa Yesu ndiye Masiya, ndiye Musa mpya. Kumbe Luka ambaye alikuwa Mpagani kwanza aliwaandikia hasa Wakristo wa mataifa akisisitiza upendo wa Yesu kwa wote, na kwa namna ya pekee kwa maskini, wakosefu na wengine waliodharauliwa.

Injili hizo tatu zinaitwa “ndugu” kwa jinsi zinavyofanana katika mpangilio, katika habari na pengine katika maneno yenyewe; kwa Kigiriki zinaitwa “sunoptiki”, yaani zinazotazamika kwa pamoja. Kama tulivyoeleza, Luka aliiongezea Injili yake kitabu cha pili, yaani Matendo ya Mitume, kama mwendelezo wake, kwa kuwa aliona kazi ya Kristo inakamilishwa na Roho Mtakatifu katika ile ya Kanisa.

Maandishi ya Yohane[hariri | hariri chanzo]

Kundi la mwisho la vitabu vya Agano Jipya linajulikana kwa jina la Yohane, kwa kuwa Injili ya nne, barua tatu na kitabu cha Ufunuo viliandikwa na mtume huyo na wanafunzi wake. Akiwa kijana kuliko mitume wenzake, Yohane alijaliwa kuishi miaka mingi na kuandika hadi miaka 70 hivi baada ya Yesu kwenda mbinguni. Miaka hiyo yote alizidi kutafakari na kuhubiri maneno na matendo ya Bwana akitambua mafumbo mengi yaliyofichika ndani yake. Pengine alirekebisharekebisha maandiko yake mpaka mwishoni, halafu akawaachia wanafunzi wake kuyakamilisha na kuyaeneza kati ya Wakristo wa mkoa wa Efeso ambapo Yohane aliongoza Kanisa miaka mingi.

Injili ya Yohane ni tofauti sana na zile ndugu kwa mtindo na kwa mpangilio, kwa mafundisho na kwa habari zenyewe. Labda Yohane alisoma walau mojawapo, asipende kurudia habari zilezile, bali kuzikamilisha na kuzisahihisha akiwa ni shahidi bora kati ya mitume wote. Hata hivyo hakutaka kuandika kitabu cha historia tu, bali habari njema hasa kwa kuchimba ishara alizozitenda Yesu zinazotufumbulia fumbo lake mwenyewe na sakramenti zake. Lengo ni kuwafanya wasomaji wamuamini kuwa ni Mwana wa Mungu na kwa kumuamini wapate uzima wa milele. Injili hiyo inatudai tukomae katika maisha ya sala na kutafakari, tukizidi kumuuliza Yesu, “Wewe ni nani?” Katika Injili hiyo atatupa jibu moja baada ya lingine. Kitabu kilikaribia kukamilika mwaka 90 hivi; toleo la mwisho na sura ya 21 ni kazi ya wanafunzi wa Yohane miaka kama 10 baadaye (Yoh. 20:30-31; 21:24-25).

Uteuzi na ukusanyaji wa maandiko ya Agano Jipya[hariri | hariri chanzo]

Kati ya mambo muhimu zaidi yaliyojitokeza wakati wa Mitume ni hayo maandishi mbalimbali ambayo yalianza kukusanywa wakati huo na katika karne zilizofuata baadhi yake yalikuja kuunda Agano Jipya kama sehemu ya pili ya Biblia. Kama tulivyoona, maandishi ya kwanza ni barua zilizoandikwa na Mtume Paulo na wengineo tangu mwaka 50 hivi. Tangu mwaka 65 hivi zilianza kupatikana Injili, ambazo ni vitabu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu. Luka mwinjili aliiongezea ile ya kwake kitabu cha pili (Matendo ya Mitume) kuhusu uenezi wa Kanisa kutoka Yerusalemu hadi Roma. Hatimaye kuna kitabu cha Ufunuo ambacho peke yake ni cha kinabii, kikitumia mtindo wa kiapokaliptiko.

Uandishi (na halafu uteuzi) wa vitabu hivyo 27 kati ya vingine vyote ni sehemu muhimu ya maendeleo ya Kanisa chini ya Roho Mtakatifu. Baada ya hapo vitabu viliendelea kuandikwa hasa kwa kutetea, kutangaza na kufafanua imani sahihi, lakini havikukusanywa katika Agano Jipya, kwa sababu wakati wa Mitume (na wa ufunuo) ulikuwa umekwisha tayari.

Uenezi na mwanzo wa mafarakano[hariri | hariri chanzo]

Mtume anayekumbukwa sana huko India ni Thoma. Kaburi lake huonyeshwa katika mji wa Chennai. Mpaka leo kusini-magharibi mwa Bara Hindi wako "Wakristo wa Thoma". Kwa muda mrefu walikosa mawasiliano na Wakristo wengine wa mbali, lakini siku hizi wanashiriki katika umoja wa Kanisa duniani.

Ingawa hatujui vizuri kama yeye aliweza kufika mbali hivyo, wala wenzake walikwenda wapi kutangaza imani, kwa hakika Ukristo wa kwanza ulienea haraka katika mabara matatu: Asia Magharibi, Afrika Kaskazini na Ulaya Kusini na Magharibi.

Dola la Roma lilipofikia kilele cha uenezi wake mwaka 117.

Siri mojawapo ya uenezi huo ni kuwepo kwa Dola la Roma. Serikali yake ilitawala nchi nyingi kuanzia kando ya jangwa la Sahara upande wa kusini mpaka Uholanzi na Uingereza wa leo upande wa kaskazini, halafu kutoka milima ya Mesopotamia (leo Iraq) upande wa mashariki mpaka Ureno wa leo upande wa magharibi. Jumla kulikuwa na wakazi waliokadiriwa kuwa milioni 55-60 hivi.

Uwepo wa dola hilo ulisaidia sana uenezaji wa Ukristo. Ingawa watawala wake walijaribu muda mrefu kupinga imani mpya, kuwepo kwa utaratibu mmoja katika eneo kubwa hivyo kulisaidia kazi ya mitume na wahubiri wa Injili. Sababu ni kwamba:

  • a. katika eneo kubwa hakuna mipaka inayoweza kuzuia usafiri na mawasiliano. Ukisafiri leo kutoka Moroko kuelekea Misri unavuka mipaka minne, unahitaji pasipoti na vibali vingi kila safari.
  • b. kulikuwa na usafiri. Merikebu zilizunguka pote katika Mediteranea zikibeba mizigo na watu. Waroma pia walikuwa hodari kujenga barabara kwenye nchi kavu. Walihitaji barabara hizo kwa matumizi ya kijeshi lakini zilisaidia pia mawasiliano mengine ya kiuchumi na usafiri.
  • c. Walitumia popote hela moja, wakawasiliana katika lugha zilezile za Kigiriki na Kilatini. Mashariki Kigiriki kilikuwa lugha ya elimu ya juu na ya biashara. Magharibi walitumia zaidi lugha ya Kilatini. Mpaka leo lugha hizo ni muhimu kama lugha za elimu. Kwa mfano maneno mengi ya sayansi (fizikia, kemia, biolojia, jiografia n.k.) yanayotumiwa katika lugha mbalimbali, asili ni ileile ya Kigiriki.

Karibu na mwaka 100 hivi, yalipoanza kutokea mafarakano kati ya Wakristo, na kila kundi kujiita “Kanisa”, lile lililodumisha umoja wa wengi likaitwa "katoliki" maana yake Kanisa lililo zima, tena moja kwa mataifa yote. Neno hilo tunalikuta kwa mara ya kwanza katika maandishi ya Ignasi wa Antiokia, askofu na mfiadini, ambaye anahesabika kati ya mababu wa Kanisa wa kwanza ambao wanaitwa Mababu wa Kitume kwa sababu “walikuwa wanasikia bado sauti ya Mitume masikioni mwao na kuona bado mfano wa Mitume machoni mwao”. Katika barua zake Ignasi anaonyesha heshima ya pekee kwa Kanisa la Roma akiandika kuwa "linasimamia upendo". Pamoja naye wale maarufu zaidi ni Papa Klementi I na Polikarpo wa Smirna.

Hadi karne ya 8 Mababu wa Kanisa wengine wengi walifuata na kufafanua imani na maadili pamoja na kuimarisha umoja wa Kanisa kwa maandishi yao bora ambayo tunapaswa kuyazingatia hata leo kwa kuwa ndani mwake tunakuja kujua mapokeo ya Mitume yasiyoandikwa katika Biblia.

Katika karne ya 2 na ya 3 walijitokeza waandishi wanaoitwa Watetezi wa Imani ya Kikristo. Wasomi hao walijitokeza kuandika vitabu ili kutetea Ukristo dhidi ya masingizio na chuki ya wengi; waliweka kweli za imani katika maneno yaliyoeleweka kwa wasio Wakristo. Waliweka wazi ulinganifu na tofauti kati ya fikra za Kikristo na zile za wananchi wengine, hasa wasomi wenzao. Walijibu mashtaka ya uongo yaliyotolewa na maadui wa Ukristo. Walieleza utakatifu wa maisha ya Kikristo. Pengine kabla ya kubatizwa waliwahi kuwa wanafalsafa, kama Yustino, kwa vyovyote walikuwa wasomi walioweza kupanga hoja hata kuzituma kwa Makaisari ili kuwahimiza wasiendelee kudhulumu Kanisa kwa kuwa maisha ya wafuasi wa Yesu hayaendi kinyume cha sheria za dola, hivyo dhuluma dhidi yao hazikubaliki.

Wakati huohuo Wakristo wengine waliandika vitabu vya kupinga uzushi wa aina mbalimbali ambao ulianza kujitokeza tayari katika karne ya 1 na ulienea hasa tangu karne ya 2. Kwa maana ya kidini, uzushi ni kosa lolote katika kuelewa na kueleza suala la imani au la maadili kwa kusisitiza mno upande mmoja na kupoteza uwiano wake na pande nyingine, na hivyo kupoteza ulinganifu wa kweli zote. Kati ya aina hizo za awali kulikuwa na Ujuzilio (Gnosis), Umontani na Umarsioni. Aliyezipinga vizuri ajabu alikuwa askofu Irenei wa Lyon sehemu za Ufaransa, lakini wengine pia sehemu mbalimbali. Kazi hiyo haikuwa nyepesi kwa kuwa wazushi walidhani wanasema ukweli na walitoa hoja zilizokuwa rahisi kueleweka na kukubalika kulingana na mazingira ya wakati ule. Baadhi walikuwa werevu na kupenda mabishano; waliweza kutumia maneno yasiyo wazi au wenye maana zaidi ya moja. Hata hivyo hao Mababu wa Kanisa waliweza kupambanua imani sahihi na kuthibitisha ukweli wake kwa kufuata mapokeo ya toka mwanzo na kuyapanga kwa ulinganifu wa dhati dhidi ya mawazo mapya yasiyopatana nayo. Ndio mwanzo wa teolojia kama fani maalumu. Tofauti zake, kama zile kati ya shule ya Aleksandria na shule ya Antiokia, ndizo chanzo cha mabishano yaliyochangia mafarakano makubwa yaliyotokea hasa katika karne ya 5, ingawa kuanzia mwaka 325 mitaguso mikuu ilikusanya maaskofu wengi kutoka sehemu mbalimbali ili kumaliza migogoro. Tofauti za lugha na utamaduni, pamoja na utaifa, zilichangia sana mafarakano.

Aina nyingine za maandishi ya wakati huo ni habari za historia ya Kanisa na hasa masimulizi ya vifodini vilivyotokana na dhuluma za serikali; vitabu hivyo vilichochea ushujaa wa Wakristo katika kukabiliana nazo kwa kuendeleza teolojia ya msalaba yenye msingi katika Biblia.

Dhuluma za muda mrefu katika Dola la Roma (64-313)[hariri | hariri chanzo]

Dola la Roma lilikuwa na eneo kubwa sana katika nchi zinazozunguka Mediteranea katika mabara matatu. Mataifa mengi waliishi chini ya utawala wake. Utawala huo ulianza kabla ya Yesu kuzaliwa ukaendelea mpaka karne ya 5 baada ya Kristo upande wa magharibi wa bahari ya Kati na hadi karne ya 15 upande wa mashariki.

Katika utamaduni wa Kibantu hakuna wazo la miungu mingi. Katika mapokeo hayo Mungu ni mmoja, ila kuwasiliana naye ni kwa njia ya mizimu hasa, si moja kwa moja. Kumbe katika sehemu nyingi za dunia utamaduni wa asili ulikuwa na imani ya miungu mingi. Dini hizo zilikuwa kawaida Afrika Kaskazini, Ulaya na sehemu nyingi za Asia kabla ya uenezaji wa Ukristo, hivyo ziliathiri mazingira ya taifa la Israeli hata wakati wa Yesu na wa Kanisa lake. Kati ya miungu mingi iliyoabudiwa kila mmoja aliaminika kuwa na idara yake alipotawala hasa, kama vile hali ya hewa, vita, kifo, uponyaji, mavuno, mifugo, biashara, uzazi n.k. Miungu iliyomaanisha nyota au sayari kama vile Jua, Mwezi na Zohali ilikuwa mapokeo ya Roma. Lugha ya Kiingereza inatunza mpaka leo kumbukumbu ya miungu mingi iliyoabudiwa katika utamaduni wa Ulaya wa Kale kabla ya kuingia kwa Ukristo, maana siku za juma zina majina ya miungu ambayo iliaminiwa kuzisimamia.

Kwa jumla serikali ya Roma iliwaachia watu uhuru waendelee na desturi au mila zao ila tu ilikuwa lazima walipe kodi na kukubali utawala mkuu. Watu wengi sana walikuwa na imani ya miungu mingi. Waliabudu mahekaluni mbele ya sanamu za miungu ile. Walikuwa na imani ya kwamba miungu ni mikubwa na yenye nguvu kuliko watu na inaishi milele. Hata hivyo waliamini miungu kuwa na tabia nyingi zinazofanana na zile za binadamu. Serikali iliona ni muhimu kuabudu miungu yote kwani ingekuwa hatari mungu fulani angesahauliwa hata kusababisha akasirike.

Matendo ya Mitume 17:16-23 inasimulia kwamba Paulo alishangaa kuona sanamu nyingi za miungu kule Athene. Kati ya sanamu hizo aliona madhahabu (altare) yaliyotengwa kwa ajili ya “Mungu asiyejulikana". Kumbe serikali ya Athene iliogopa kumsahau mungu yeyote ikatoa sadaka za tahadhari.

Kwa upande mwingine watu waliamini kwamba hata mtu anaweza kupanda ngazi na kuwa kama mungu akiwa na sifa za kutosha zinazokubalika mbele za miungu yote na hasa mungu mkuu. Ndiyo asili ya kumtangaza mtawala mkuu au Kaisari wa Roma kuwa na sifa za kimungu. Raia walitakiwa kushiriki ibada za kumtolea sadaka mbele ya sanamu zake. Kwa watu wengi waliozoea kuabudu miungu mingi haikuwa vigumu kumwingiza Kaisari kama mungu wa nyongeza katika mawazo yao: kwao ilikuwa kuongeza tu jina moja katika orodha ya miungu iliyoabudiwa. Lakini kwa Wakristo haikuwezekana kushiriki ibada hizo. Imani ya Kikristo hukataa kuwepo kwa miungu mingi, vilevile hukataza kuiabudu. Kwa hiyo walionekana kama maadui wa serikali. Walikamatwa na polisi na kupelekwa mahakamani waadhibiwe kama waasi watakaosababisha hasira ya miungu juu ya watu wote. Juu yao iliandikwa, “Mto Tiber ukifurika ama Naili unakosa maji, nchi ikifunikwa na giza au inatetemeka, tena njaa, vita au tauni vikitokea, mara moja sauti husikika: ‘Wakristo watupwe kwa samba! Wakristo wauawe’”.

Ukali wa mateso ulitegemea siasa ya wakuu wa mikoa ya Kiroma. Wakati mwingine waliweza kujipatia sifa wakitoa taarifa ya kwamba wamekamata Wakristo wengi na kuwahukumu. Wakati mwingine waliona afadhali kuwaacha na kutosababisha vurugu katika mkoa. Wakristo waliweza wakahumiwa bila kusikilizwa, lakini ikiwa baraza lilikaa, uamuzi ulijulikana toka mwanzo. Mara nyingi walipelekwa kwenye viwanja vya michezo kama kile cha Nero kilichokuwa palipo leo basilika la Mt. Petro katika mtaa wa Roma unaoitwa Vatikano. Huko waliachwa peke yao bila chochote kupambana na askari wenye silaha au wanyama wakali, huku watazamaji wakishangilia damu inapomwagika. Baadhi ya waandishi Wapagani walieleza juu ya wingi wa Wakristo waliouawa na juu ya ukatili uliotumika dhidi yao. Usiku mmoja Nero mwenyewe alizunguka karibu na ikulu huko mitaa ikiangazwa na watu waliopakwa mafuta na kuwashwa moto wawe kama mienge.

Maonyesho hayo yalikusudiwa kutisha watu waogope kuwa Wakristo. Lakini yakageuka kampeni kwa ajili ya Ukristo, kwa sababu watazamaji walianza kujiuliza: Je, watu hao wana kosa gani? Ni imani gani inayowapa nguvu ya kusimama mbele ya wanyama mwitu na kuuawa badala ya kutoa sadaka mbele ya sanamu? Kwa nini wale wanaokufa hivyo wanajulikana kuwa watu wasioiba wala kusema uongo lakini wengine wenye tabia mbaya hawana matatizo wakitoa sadaka tu mbele ya sanamu? Kumbe damu ya mashahidi ilikuwa mbegu ya kukua kwa Kanisa.

Ni kwamba nje ya suala la kidini Wakristo walikuwa raia wema, lakini waliweza kuchukiwa kwa sababu mbalimbali: walichanganywa na Wayahudi waliochukiwa tayari kwa jinsi walivyojibagua na kudharau wengine wote, waliwazibia riziki waliofaidika na sadaka za Kipagani, walitiwa shaka sana kwa kufanya ibada zao kwa siri n.k.

Dhuluma ya kwanza ilitokea mwaka 64 BK, ya mwisho mwaka 313 BK. Katika kipindi hicho kirefu, vilirudia tena na tena vipindi vya mateso vikifuatana na vipindi vya amani. Lakini miaka yote Ukristo ulikuwa dini haramu, hivyo kila mara mateso yaliweza kuanza upya. Katika hali hiyo Wakristo walijenga utaratibu mzuri wa kufundishana na kusaidiana katika matatizo. Halafu wakakazia sana mafundisho ili waumini wasimame imara katika matatizo na dhuluma. Kuanzia katikati ya karne ya 2 ulipangwa ukatekumeni mrefu kwa wanaoomba ubatizo ili wajue la kusadiki na la kufanya. Wakajitahidi kuonyesha kwa maisha na matendo yao kwamba Ukristo ni imani yenye amani na upendo isiyoharibu umma. Waliofanya dhambi kubwa walitengwa na jumuia hadi atakapofanya kitubio cha hadhara na hatimaye kupokewa tena na askofu. Wakaendelea kuombea serikali na watu wote, hasa wakati wa ibada ya ekaristi, ambayo ilitiwa maanani sana na kuzidi kupambwa kwa namna mbalimbali. Kwa ajili hiyo walikutana katika nyumba za watu binafsi, au kwenye "katakombu" yaani mahandaki chini ya ardhi walipotengeneza makaburi yao, yakiwemo ya watakatifu waliofia dini. Walipokutana huko kwa ajili ya ibada, waliimarisha imani yao na utayari wa kuifia kama hao.

Kati ya dhuluma nyingine ambazo zilifuata, kali zaidi ni ile ya kaisari Decius miaka 250-251, halafu ile ya Valeriani mwaka 257.

Lakini ni hasa Kaisari Dioklesyano aliyejaribu kwa nguvu zote kuharibu Kanisa na kufuta Ukristo katika mateso ya miaka 303-305. Maelfu waliuawa: walikatwa vichwa na maaskari, walipelekwa katika kiwanja cha michezo kwa wanyamapori, walichomwa moto n.k. Mateso yalikuwa makali hasa kule Misri. Katika miji mikubwa kama Aleksandria watu wengi walikuwa Wakristo. Machoni pa wakuu wa serikali hali hiyo ilikuwa uasi, wakaona lazima kuuzima. Lakini idadi ya Wakristo iliendelea kuongezeka kote katika Dola la Roma na waliokuwa tayari kufa ilizidi uwezo wa serikali wa kuwaua.

Hatimaye mwaka 313 ulileta ukombozi: Kaisari mpya, jina lake Konstantino Mkuu, alitangaza mwisho wa mateso: “Tunataka mtu yeyote anayetamani kufuata dini ya Kikristo aweze kufanya hivyo bila hofu yoyote ya kusumbuka kwa ajili hiyo. Wakristo wawe na uhuru tele kufuata dini yao”.

Urithi wa Misri kwa Kanisa zima: elimu na umonaki[hariri | hariri chanzo]

Ndani ya Biblia hatuna habari juu ya jumuia za kwanza zilizoundwa Misri. Lakini Wakristo wa kule wanamkumbuka Marko Mwinjili aliyefika Aleksandria na kuhubiri Habari Njema na kuanzisha Kanisa huko. Anakumbukwa kama Askofu wa kwanza wa Aleksandria. Ndiyo sababu mpaka leo Patriarki wa Aleksandria huitwa "Mwandamizi wa Marko". Huyo hakuwahi kuwa mwanafunzi wa Yesu, ila alifahamu vizuri Mitume wake na kusafiri na Petro, hivyo aliweza kuandika taarifa juu ya maisha na mafundisho yake. Alikuwa mwandishi wa kwanza wa Injili. Mathayo na Luka walitumia taarifa za Marko walipoandika Injili zao. Anasemekana alifia imani chini ya serikali ya Roma.

Misri ikawa kitovu muhimu cha Ukristo wa kale. Uhodari wa Wakristo wake ulishinda dhuluma za serikali. Katika mapambano hayo Wakristo Wamisri wakaunda silaha mbili ambazo zimekuwa muhimu katika Kanisa zima mpaka leo: 1. Elimu ya Kikristo; 2. Maisha ya kimonaki (utawa).

Elimu ya Kikristo: Chuo cha Aleksandria[hariri | hariri chanzo]

Jiji la Aleksandria lilikuwa na maktaba kubwa kuliko zote duniani. Wakati ule haikujulikana jinsi ya kupiga chapa vitabu. Kila kitabu kiliandikwa kwa mkono kikawa na bei kubwa sana. Kununua kitabu kulikuwa na gharama zinazofanana na ile ya kununua gari leo. Kwa hiyo elimu ilikuwa na thamani kubwa, na maktaba kubwa ilikuwa na thamani kupita kiasi. Wataalamu toka pande zote za dunia walifika Aleksandria, mji wa elimu, ili kusoma na kunakili vitabu. Si ajabu kwamba Agano la Kale lote lilitafsiriwa kwa mara ya kwanza katika lugha ya Kigiriki huko Aleksandria mwaka 150 hivi KK.

Hivyo Wakristo wa Aleksandria walijisikia hawana budi kujadiliana na watu wenye elimu. Wawe tayari kujibu maswali yao juu ya Injili hata kutetea imani kwenye ngazi inayolingana na elimu ya hali ya juu. Wakristo wenye elimu walijitolea kuelimisha Wakristo wenzao. Katika mafundisho hayo kilitokea chuo cha kwanza cha Kikristo. Masomo yake yalihusu imani na Biblia lakini pia elimu kwa jumla. Falsafa ilikuwa muhimu katika mawazo ya wataalamu hata katika mafundisho ya kidini ya Wapagani na Wayahudi. Basi, ilionekana afadhali mwalimu Mkristo ajue falsafa na awe na msimamo wake juu ya uhusiano kati ya falsafa na imani ya Kikristo.

Chuo cha Aleksandria kilipata sifa chini ya Panteno. Mnamo mwaka 200 BK huyo aliacha uongozi wa chuo akawa mmisionari Bara Hindi. Aliyemfuata alikuwa Klementi wa Aleksandria aliyefaulu sana kuvuta Wapagani wenye elimu kumpokea Kristo.

Mwanafunzi wake mashuhuri alikuwa Origene, ambaye baadaye akapewa uongozi wa chuo hicho. Alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka 25. Origene alikuwa mtaalamu wa pekee: ndiye wa kwanza kutumia njia ya kisayansi katika kuchunguza fasiri za Biblia. Pamoja na makarani wake akaandika maneno yote ya Kiebrania ya Biblia pamoja na fasiri zake katika nguzo sita kwenye ngozi kubwa. Njia hiyo ilisaidia kuona mara moja makosa au udhaifu katika fasiri hizo. Aliwafundisha vijana wengi kutumia akili yao katika kutafakari imani kwani akili ni kipawa cha Mungu.

Kwa njia hiyo Chuo cha Aleksandria kimekuwa mwanzo wa elimu ya juu katika Ukristo. Mpaka leo ni kawaida kwamba mtumishi wa Kanisa awe na elimu. Wachungaji, mapadri na watawa wanasomeshwa katika vyuo mbalimbali hadi ngazi ya chuo kikuu. Ukristo umekuwa imani ya wasomi. Asili ya jambo hilo ni katika juhudi za Wakristo wa Misri.

Katika mji mkuu wa Afrika Kaskazini-Magharibi, Karthago, hakikuanzishwa chuo kama kile cha Aleksandria, lakini walitokea walimu maarufu kama padri Tertuliani na askofu Sipriani walioanzisha teolojia kwa lugha ya Kilatini. Ni kwamba wakati ule kulikuwa na tofauti kubwa kati ya utamaduni wa Misri na ule wa Afrika Kaskazini-Magharibi. Misri ulikuwapo mchanganyiko wa utamaduni wa Kikopti (yaani kiasili cha Misri) pamoja na wa Kigiriki. Katika sehemu za magharibi za Afrika Kaskazini watu wa asili ni Waberberi, lakini watu wa mjini na wenye mashamba makubwa walikuwa wa asili ya Ulaya wakatumia hasa Kilatini iliyokuwa lugha muhimu ya kimataifa pamoja na Kigiriki. Kwa jumla sehemu hiyo ya Afrika ilikuwa karibu na utamaduni wa Ulaya ya Magharibi, lakini Misri ilikuwa karibu na utamaduni wa Asia ya Magharibi na Ulaya ya Mashariki.

Umonaki - maisha ya pekee[hariri | hariri chanzo]

Watawa ni Wakristo walioamua kuishi kwa njia ya pekee. Mara nyingi tumezoea kuwaona katika Kanisa Katoliki. Lakini wako vilevile kati ya Waanglikana na Walutheri, ingawa si wengi. Ulaya wako hata masista Wamoravian na Wabaptisti. Mtawa amepokea katika maisha yake ushauri wa mtume Paulo (ambaye hakuoa): «Nawaambia wale wasiooa bado, Ni heri wakae kama nilivyo» 1Kor 7:8. Yesu mwenyewe aliwahi kueleza ya kwamba watakuwepo wale watakaochagua maisha ya pekee bila familia na uzazi kwa ajili ya Ufalme wa Mungu (Mt 19:12: "Wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni»).

Kwa jumla watawa ni kundi muhimu linalosaidia sana kazi ya kiroho katika Ukristo. Wako huru kuliko wengine kujitolea katika huduma za Kanisa, kwani hawalazimiki kufikiria maendeleo ya watoto wao. Watawa wanaweza kuishi peke yao lakini mara nyingi wanajiunga na shirika au jumuiya na kuweka nadhiri za useja mtakatifu, ufukara na utiifu.

Asili ya jumuiya hizo iko Misri. Katika karne ya 3 mateso yalizidi chini ya serikali ya Waroma Wapagani. Wakristo wengine walijificha jangwani wakiogopa kulazimishwa kutoa sadaka kwa sanamu. Wengine waliona jinsi familia yao ilivyouawa katika dhuluma za kidini. Wengine karibu walikata tamaa wakiona Wakristo wengine walivyokana imani kwa kuogopa mateso. Kumbe wengine hawakuona raha tena katika maisha ya kawaida, wakajitenga na dunia wakaenda porini kuishi kwa kufunga, kusoma Biblia na kusali.

Watawa hao waliitwa kwa jina la Kigiriki "wamonaki" (monos= moja; monakos= anayekaa peke yake). Walikaa jangwani katika maeneo yaliyokuwa mbali na miji na vitovu vya utawala wa Kiroma. Lakini waliheshimiwa sana na wananchi wa kawaida. Watu wakazoea kuwaendea kuomba ushauri wao katika mambo ya kiroho au maisha kwa ujumla, kuombewa katika magonjwa n.k. Wengine walipokea zawadi za wanavijiji wakaelekea maisha ya kuombaomba.

Antoni abati anaitwa baba wa umonaki kwa jinsi alivyovuta wengi kwenye mtindo huo mpya wa maisha ya kiroho katika Ukristo.

Wamonaki wa kwanza walikaa kila mmoja peke yake bila kushirikiana. Antoni wa Misri alikuwa mmojawao, naye akaona umuhimu wa kuweka utaratibu fulani kati ya wamonaki wenzake.

Mwanafunzi wake Pakomi aliendeleza mkazo wake akawaunganisha wamonaki mahali pamoja akawapa utaratibu wa kazi na sala. Katika utaratibu huo kila mmonaki (pia masista katika mashirika yao) hutoa ahadi au nadhiri tatu: 1. Useja mtakatifu: atachagua maisha bila ndoa; badala yake kujiunga na shirika la wenzake kama familia ya kiroho. 2. Ufukara: ataacha mali yake ya binafsi na hatatafuta tena utajiri wa kidunia. 3. Utii: atamtii mkuu wa shirika hilo aliyechaguliwa kati yao (huitwa "Abba/Abati") na kutii taratibu za ushirika wake.

Utaratibu huo wa umonaki ulienea haraka: watawa wakaanza kukaa na kufanya kazi pamoja ili kujipatia mahitaji yao wenyewe. Baadaye vituo vya wamonaki vilikuwa vitovu vya elimu ambapo sehemu ya wamonaki walisoma, kuandika (au kunakili) vitabu, kuanzisha shule n.k.

Leo hii mashirika ya watawa ni maelfu. Kwa kawaida kila shirika lina mkazo wake wa pekee, kama vile maisha ya kimya katika sala au huduma za upendo: hospitali, nyumba za mayatima, ufundishaji, uinjilishaji, misheni, au n.k. Hivyo mtawa anaweza kuwa na maisha ya kutotoka katika nyumba ya shirika lake au anaweza kuishi kati ya Wakristo na wasio Wakristo akiwatolea huduma zake.

Wamisri wamisionari katika mabara matatu[hariri | hariri chanzo]

Panteno wa Chuo cha Aleksandria alikwenda India kuhubiri Injili. Wamisionari wa Kanisa la Misri walianzisha Kanisa katika Sudan, Sudan Kusini,Ethiopia na Eritrea za leo.

Hata sehemu mbalimbali za Ulaya zinakumbuka wamisionari kutoka Afrika waliohubiri huko Injili wakati wa Dola la Roma. Askari Wamisri katika jeshi la Roma walikaa miaka mingi Uswisi na kwingineko. Kati yao kulikuwa na Wakristo waliohubiri huko Injili kwa mara ya kwanza.

Huko Ireland Wamisri waliunda monasteri mnamo mwaka 500 na kufundisha Injili. Waireland wanafunzi wa Waafrika hao ndio wainjilisti wa Ujerumani na Uholanzi baadaye.

Ukristo katika Afrika Kaskazini Magharibi[hariri | hariri chanzo]

Hakuna habari kuhusu mwanzo wa Kanisa Afrika Kaskazini-Magharibi, ila katika karne ya 2 (labda 130 hivi) lilikuwepo tayari katika mji mkubwa wa Karthago likaanza kutoa wafiadini wake katika kumshuhudia Yesu.

Wakristo wengi Waafrika walionyesha uhodari wa kutokana imani yao na wa kufa kama mashahidi wa Yesu. Mfano huo ulisababisha Wapagani wengi kuwa Wakristo. Lakini si wote walisimama imara mbele ya vitisho. Wengi wakatoa sadaka mbele ya sanamu wakatubu baadaye na kuomba wasamehewe udhaifu huo. Wengine waliwahonga maafisa wa serikali wakanunua vyeti vilivyothibitisha ya kwamba walitoa sadaka zile ingawa haikuwa kweli. Mbinu moja ya dhuluma ilikuwa kukusanya Maandiko matakatifu yote na kuyachoma moto. Katika miaka hiyo migumu walitokea hata maaskofu kadhaa na wachungaji walioona heri kuwakabidhi askari Maandiko matakatifu kuliko kuuawa.

Baada ya mateso hayo kwisha na uhuru kupatikana Wakristo walioasi au kukana imani walirudi. Hata wachungaji na maaskofu waliowahi kuwa dhaifu walipokewa tena baada ya kutubu. Lakini Wakristo wa Karthago walio wengi walikataa kuwakubali tena. Walitaka kuongozwa na wale tu waliosimama imara (au labda: waliokuwa na bahati ya kutokamatwa). Jambo hili lilisababisha ndani ya Kanisa farakano lililoitwa kwa jina la askofu Donato Mkuu. Huyo alisititiza kwamba aliyeasi hawezi kutoa sakramenti za kweli. Maana yake akibatiza, kusikia kitubio au kutoa ekaristi si sakramenti. Kumbe Kanisa Katoliki lilitetea fundisho la kuwa kila Mkristo anaweza kuteleza katika dhambi lakini toba inaponya makosa yote. Wafuasi wa Donato walijitenga wakijiona ndio Kanisa la kweli lenye waumini na viongozi walio safi. Wakijivuna kuwa Wakristo bora kuliko wengine, walifikia kuwa na maaskofu 200. Wakristo wengi, hasa wa asili ya Kiberberi vijijini, walifuata mafundisho ya Donato. Waberberi waliojisikia kunyonywa na serikali ya Kiroma waliona Wadonato kama chombo cha upinzani. Hivyo matatizo ya kisiasa na ya kikabila yalichangia. Upande wao, viongozi wa Kanisa Katoliki walikosa mara nyingi upendo wakati wa kuwashughulikia. Farakano hilo lililodumu hadi karne ya 5 lilikuwa jeraha kubwa katika Ukristo wa Afrika Kaskazini.

Uhuru wa dini katika dola na matokeo yake[hariri | hariri chanzo]

Mozaiki ya Konstantino pamoja na bombwe la majengo ya Konstantinopoli.

Mateso ya Wakristo yaliendelea lakini idadi yao iliendelea kuongezeka kote katika Dola la Roma. Mwaka 312 Konstantino alipigania Ukaisari (cheo cha mtawala mkuu) akishindana na mgombea mwingine. Inasemekana siku moja alimuomba Mungu wa Wakristo akaona msalaba mkubwa uking’aa angani akasikia sauti iliyosema: "Kwa ishara hii utashinda". Hapo aliwaruhusu wanajeshi wake waliokuwa Wakristo kusali akamshinda mpinzani katika vita. Mwaka 313 Kaisari Konstantino akatangaza sheria iliyoruhusu Wakristo kuabudu kwa uhuru. Ukristo ukawa dini halali katika Dola la Roma.

Kipindi kipya kikaanza katika historia ya Ukristo. Kwa wengi hali hiyo ilikuwa ajabu la Mungu mwenyewe aliyemaliza matatizo yao, jinsi Biblia ilivyosema katika kitabu cha Ufunuo. Wakristo wakazidi kujenga na kupamba makanisa kila mahali. Vilevile ibada zilizidi kupangwa kwa utaratibu mzuri wa matini na vitendo. Maaskofu waliweza kukutana bila matatizo. Mikutano ya maaskofu (mitaguso ya ngazi mbalimbali) iliamua juu ya masuala na matatizo yaliyojitokeza. Tangu mwanzo wa karne ya 1 kila mji ulikuwa na askofu wake. Baada ya muda maaskofu wa eneo au mkoa mmoja walikuwa chini ya Askofu Mkuu. Maaskofu wa Roma (Ulaya na Afrika Kaskazini-Magharibi), Aleksandria (Afrika Kaskazini-Mashariki), na Antiokia (Asia) waliheshimika kuliko maaskofu wengine wote wakaitwa “Papa" na "Patriarki". Cheo cha Patriarki kilipatikana pia kwa Askofu wa Konstantinopoli baada ya makaisari wa Roma kuhamia kule na kwa askofu wa Yerusalemu.

Lakini mwisho wa dhuluma za serikali haukuwa mwisho wa matatizo yote: badala ya hatari za nje, sasa zilijitokeza zaidi hatari za ndani, hasa mafundisho ya kizushi yaliyogawanya waumini.

Mwaka 325 mkutano mkuu wa kwanza ulifanyika kule Nisea (Asia Ndogo). Wakristo wa nchi mbalimbali walikuwa wanatofautiana katika maelezo yao juu ya Umungu na utu wa Kristo. Kama ni mtu, je aliumbwa kama wanadamu wote? Lakini akiitwa Mungu ndiye Muumba mwenyewe. Kama yeye ni Mungu, aliwezaje kuteseka msalabani? Au ni Mungu aliyejificha tu katika umbo la mwili, kumbe hakuteswa kweli, ilikuwa kama igizo tu?

Maaskofu wa Kanisa zima walikutana kule Nikea wakapatana juu ya mafundisho ya "Kanuni ya Imani ya Nisea" yanayosema "Twamwamini Bwana mmoja, Yesu Kristo, mwana pekee wa Mungu, mwana wa azali wa Baba, yu Mungu kutoka kwa Mungu, yu nuru kutoka kwa nuru, yu Mungu kweli kutoka kwa Mungu kweli, Mwana wa azali, asiyeumbwa; aliyeshuka kutoka mbinguni kwa ajili yetu wanadamu na kwa wokovu wetu; akatwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu katika Bikira Maria, akawa mwanadamu; akasulibiwa kwa ajili yetu zamani za Pontio Pilato; aliteswa, akazikwa, siku ya tatu akafufuka kama yanenavyo maandiko matakatifu; akapaa mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Baba; kutoka huko atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu walio hai na wafu; na ufalme wake hauna mwisho." Maneno hayo hutumika mpaka leo katika ibada za kikristo (pamoja na "Kanuni ya Imani ya Mitume").

Baada ya Konstantino Kanisa lilikua sana. Watu wengi walijiunga na Ukristo. Zamani ilikuwa hatari kuwa Mkristo, kumbe sasa imekuwa faida, hata watu wenye imani haba waliosita zamani wakajiunga na Kanisa. Makaisari wenyewe walikuwa Wakristo, isipokuwa Juliani Mwasi (361-363) aliyejaribu kurudisha Upagani kwa kuwadhulumu tena.

Mwaka 380 mambo yaligeuka kinyume cha hali ya awali: serikali ya Kaisari Theodosi I ilitangaza Ukristo wa Kikatoliki kuwa dini rasmi ya dola. Kanisa lilipewa hela na serikali. Kaisari mpya aliwekwa wakfu katika ibada kanisani. Kabla yake Armenia ilikuwa nchi ya kwanza kupokea Ukristo kama dini ya taifa (301). Ushindi huo ulifanya wengi watamani vyeo ndani ya Kanisa, kwa kuwa viliendana sasa na heshima na mali: hivyo ubora ulipungua.

Mwishoni serikali ilianza kufunga na kubomoa mahekalu ya Wapagani. Asiyekuwa Mkristo alianza kupata matatizo. Ilitokea mara kadhaa ya kwamba walimu wapagani walipigwa na kuuawa na umati wa Wakristo.

Katika miji mbalimbali watu walianza kuwatesa hata kuwaua Wayahudi wakiwashutumu kwamba ndio waliomwua Yesu. Sisi tunaweza kushangaa jinsi hali hiyo ilivyoweza kutokea. Yesu mwenyewe alikuwa Myahudi na mpaka msalabani alifuata taratibu za taifa la Israeli. Mtume Paulo alifundisha ya kwamba Wayahudi hawawezi kupoteza ahadi na agano la Mungu kwao hata wakimkataa Yesu Kristo.

Bila shaka Yesu hakutaka watu walazimishwe kujiunga na Kanisa lake. Lakini katika mawazo na uzoefu wa Waroma dini na serikali zilikuwa kitu kimoja. Ikiwa sasa Kaisari, wakubwa wa serikali na watu wengi ni Wakristo walihisi ni kawaida kwa wote kufuata dini hiyo. Kumbe Kanisa lilianza kutumiwa na wanasiasa kwa malengo yao ya kidunia.

Atanasi na wengineo[hariri | hariri chanzo]

Aleksandria ndiko ulikotokea uzushi mkuu wa historia yote ya Kanisa: mwaka 321 hivi padri mzee Ario alikanusha umungu wa Yesu. Mafundisho yake yalienea kote mashariki na kuungwa mkono na watawala kwa nguvu za dola, hivi kwamba hata maaskofu wengi wa huko waliyakubali kwa namna moja au nyingine.. Lakini ni Kanisa la Misri lililompinga kwa uimara wa pekee, bila kujali dhuluma.

Picha takatifu ya Atanasi wa Aleksandria, Askofu mkuu (Patriarki) wa Aleksandria na mtetezi mkuu wa umungu wa Yesu Kristo.

Kati ya wote, alijitokeza Atanasi wa Aleksandria anayeitwa Mkuu (Aleksandria, Misri, 295 hivi - Aleksandria, 2 Mei 373), Patriarki wa Kanisa Katoliki la madhehebu ya Misri kati ya mitaguso mikuu miwili ya kwanza: Nisea I (325) na Konstantinopoli I (381).

Maisha yote ya Atanasi yalihusika na juhudi kubwa za Kanisa kwa ajili ya kufafanua na kutetea imani sahihi juu ya Yesu na juu ya Utatu hata akaitwa mapema “nguzo ya Kanisa” (Gregori wa Nazianzo).

Pamoja na kupatwa na vurugu nyingi maishani (hasa kufukuzwa mara tano kutoka mji wake), Atanasi aliandika sana: hotuba na barua, lakini pia vitabu juu ya imani, historia, ufafanuzi wa Biblia, pamoja na maisha ya Kiroho. Kitabu chake maarufu kimojawapo kinahusu umwilisho wa Neno; humo aliandika kuwa Neno wa Mungu “alifanyika mtu ili sisi tuweze kufanywa Mungu”.

Mbali ya Atanasi, katika karne ya 4 na ya 5 Kanisa la Mashariki lilizaa mababu wengine bora: Basili Mkuu (Kaisarea wa Kapadokia, leo Kayseri, nchini Uturuki, takriban 329 – Kaisarea wa Kapadokia, 1 Januari 379, Gregori wa Nazianzo (Arianzo, leo Güzelyurt nchini Uturuki, 329 - Arianzo, 25 Januari 390) na Yohane Krisostomo (Antiokia wa Siria, leo Antakya, nchini Uturuki, 347 hivi - Comana Pontica, Uturuki, 14 Septemba 407). Wote walikuwa maaskofu na wote walipitia kwanza umonaki. Ndio waliofafanua kwa dhati zaidi mafumbo ya Ukristo, kuanzia lile la Utatu mtakatifu, na ndio waliobaki kielelezo kwa liturujia na uchungaji bora.

Kitabu cha Atanasi ambacho kilienea na kuathiri zaidi maisha ya Kanisa labda ni "Maisha ya Antoni" ambacho kilieneza umonaki haraka mashariki na vilevile magharibi.

Tangu karne IV umonaki ulijitokeza magharibi pia: huko Italia, Ufaransa na Hispania kulikuwa na monasteri za kike na za kiume zilizosimamiwa na maaskofu watakatifu. Kati yao wa kwanza kupitia umonaki ni Martino wa Tours (316-397).

Hasa maandishi ya Yohane Kasiano (360-435) yalieneza hekima ya wamonaki wengi wa mashariki alioongea nao.

Augustino wa Hippo (354-430), babu wa Kanisa muhimu kuliko wote, baada ya kuongoka na kutembelea baadhi ya monasteri, alirudi Afrika Kaskazini aanzishe maisha ya pamoja. Kwanza aliishi na walei wenzake, halafu akiwa askofu aliishi na mapadri wake, akawashirikisha utajiri wake wa akili na roho ili wafanye vizuri utume. Katika kanuni yake, iliyotumika kwa wanawake pia, umoja uliwekwa kuwa lengo lenyewe la utawa, si jambo lake mojawapo tu. Hata yeye aliathiri sana maisha ya kitawa ya magharibi kote.

Benedikto wa Nursia (480-547) ndiye aliyeunda umonaki wa magharibi kwa namna ya kudumu hasa kwa njia ya kanuni aliyoitunga polepole, kutokana na mang’amuzi yake, Kanuni ya Mwalimu asiyejulikana na mafundisho ya Bazili na mababu wengine wa jangwani.

Kanuni yake iliunganisha vizuri maelekeo mawili ya umonaki wa zamani: kumtafuta Mungu kwa juhudi upwekeni na kuishi kwa umoja. Sifa yake nyingine ni mchanganuo mzuri wa sala na kazi mbalimbali ambazo ziliokoa elimu ya zamani na kufufua uchumi wa Ulaya Magharibi baada ya makabila ya Kijerumani kuvuruga kote. Yeye alidumisha ubaba wa Kiroho katika jumuia nzima: ndiyo maana abati ana nafasi ya pekee na ya kudumu kwa wamonaki, ambao aliwafafanua kuwa watu “wanaoishi katika monasteri na kutii kanuni moja na abati mmoja”. Kwake monasteri ni shule ya utumishi wa Bwana, ambapo abati ndiye mwalimu, na kanuni ndiyo kitabu. Kinyume cha watawa wazururaji wa zamani hizo za misusuko, Benedikto alidai udumifu katika monasteri.

Kutokana na kila monasteri kujitegemea, Wabenedikto wakapata sura tofautitofauti bila ya kuachana na kanuni. Ushirikiano kati ya monasteri mbalimbali unategemea asili yake na mitindo yake.

Kati ya aina nyingine za umonaki wa magharibi inakumbukwa hasa ile ya Wakristo wa Kiselti (Ulaya visiwani). Hao hawakuwa na majimbo bali walimtegemea askofu-abati wa monasteri ya jirani na kufuata desturi za kimonaki, hasa maisha magumu ya malipizi na maungamo ya mara kwa mara. Kutoka huko wamonaki wengi walihamia Ulaya bara kama wasafiri wa Kristo na wamisionari wakieneza desturi hizo. Kati yao anasifiwa hasa Kolumbani (540-615).

Hatimaye wakaja kukubali kanuni ya Benedikto pamoja na desturi za Kanisa la Roma.

Wamonaki wengine pia walichangia sana uenezaji wa Ukristo Ulaya, k.mf. Augustino wa Canterbury (+605), aliyetumwa Uingereza na Papa Gregori I (540-604), mmonaki wa kwanza kufikia Upapa, halafu Bonifas (672-754), mtume wa Ujerumani na mfiadini.

Augustino na wengineo[hariri | hariri chanzo]

Augustino wa Hippo akibatizwa na askofu Ambrosi, mwaka 387.

Augustino (Thagaste, leo Souk Ahras nchini Algeria, 13 Novemba 354Hippo, leo Annaba, Algeria, 28 Agosti, 430) alikuwa mtawa, mwanateolojia, padri na hatimaye askofu mkuu wa Hippo.

Ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki katika Afrika Kaskazini mwanzoni mwa karne ya 5. Augustino alizaliwa wakati ambapo Ukristo umekuwa tayari dini iliyokubaliwa katika Dola la Roma. Mateso ya Wakristo yalikuwa yamekwisha. Mama yake alikuwa Mkristo, baba Mpagani. Augustino alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Karthago, akaendelea kusoma Italia. Ndipo alipokutana na watu waliomvuta kuwa Mkristo, akabatizwa akarudi Afrika akapewa upadrisho akachaguliwa kuwa askofu wa mji wa Hippo mwaka 395. Mpaka kifo chake aliendelea kueleza na kutetea imani kwa maandishi na vitabu vingi. Kwa njia hiyo amekuwa mwalimu muhimu sana katika Ukristo wa Magharibi (yaani Kanisa Katoliki na madhehebu yaliyotokana nalo).


Katika historia yote Augustino ni kati ya watu wenye akili kubwa zaidi, iliyopenya masuala yoyote, pamoja na ubunifu wa ajabu na moyo mpana. Aliunda upya teolojia ya mapokeo akiitia chapa yake mwenyewe.

Kati ya mababu wa Kanisa, ndiye aliyetuachia maandishi mengi zaidi, kuanzia yale maarufu sana yanayoitwa "Maungamo", kwa kuwa humo miaka 397-400 aliungama sifa za Mungu na ukosefu wake mwenyewe kwa kusimulia alivyoishi hadi miaka ya kwanza baada ya kuongoka.

Kila wakati ulifurahia zaidi kitu fulani katika Augustino. Siku hizi anapendwa hasa kwa unyofu wake katika kujichunguza na kutoa siri zake, akikiri makosa yake na kuyageuza yawe sifa kwa Mungu.

Uzingatifu wake wa fumbo la nafsi yake ambamo fumbo la Mungu limefichama, ni mzuri ajabu kiasi cha kubaki hata leo kilele cha kujitafiti kiroho. Aliandika: “Usiende nje, rudi ndani mwako; ukweli unakaa katika utu wa ndani; na ukiona umbile lako ni geugeu, panda juu yako. Lakini kumbuka, unapopanda juu yako, unapanda juu ya roho inayofikiri. Basi, ufikie pale mwanga wa akili unapowaka”. Tena: “Naona ni lazima wanadamu warudishiwe tumaini la kupata ukweli”.

Posidi, mtu wa kwanza kuandika habari za maisha ya Augustino (kwa Kilatini, “Vita Augustini”), alisema “waamini wanamkuta daima hai” katika vitabu vyake. Kweli havionyeshi imepita miaka 1600 tangu viandikwe: humo anaonekana kama rafiki yetu wa wakati huu anayesema nasi kwa imani isiyozeeka.

Augustino mwenyewe aliviorodhesha 1,030, ambavyo si vyote.

Kazi yake kubwa haikuwa kuandika maelezo juu ya vitabu na maneno ya Biblia yenyewe alivyofanya Origene, bali kuingiza Biblia katika mazingira ya kiroho, ya kijamii na ya kisiasa ya wakati wake. Hapo, akitegemea mamlaka ya imani inayodhihirishwa na Biblia, maandiko ya Kimungu yasiyoweza kukosea yakisomwa katika mapokeo ya Kanisa lililoorodhesha vitabu vinavyoiunda, aliuliza maswali na kutoa majibu yaliyo muhimu mpaka leo.

Akilinganisha imani na akili, Augustino alichunguza hasa fumbo la Mungu (Ukweli mkuu na upendo wa milele, unaohitajiwa na roho ili kupata amani) na la binadamu (ambaye ni sura na mfano wa Mungu). Huyo katika roho yake isiyokufa, bado ana uwezo wa kuinuka hadi kwa Mungu, ingawa uwezo huo umeharibiwa na dhambi na unahitaji kabisa kurekebishwa na neema.

Teolojia yake kuhusu Utatu inaendeleza ile ya mapokeo na kuathiri Kanisa lote la Magharibi. Augustino anaweka wazi kuwa Nafsi tatu ni sawa lakini hazichanganyikani; tena anajaribu kuufafanua Utatu kwa kutumia saikolojia (mfano wa kumbukumbu, akili na utashi). Kitabu muhimu zaidi kuhusu Utatu (kwa Kilatini kinaitwa “De Trinitate”) alikiandika miaka 399-420. Kilichukua muda mrefu kwa kuwa alisimamisha uandishi wake miaka minane “kwa sababu ni kigumu mno na nadhani wachache tu wanaweza kukielewa; basi kuna haraka zaidi ya kuwa na vitabu vingine tunavyotumaini vitafaidisha wengi”.

Hivyo alielekeza nguvu zake kutunga vitabu vya katekesi kwa wasio na elimu (hasa “De Catechizandis Rudibus”). Akijibu hoja za Wadonati, ambao walitaka Kanisa la Kiafrika na kuchukia mambo ya Kilatini, alikubali kurahisisha lugha hata kufanya makosa ya kisarufi kusudi wamuelewe zaidi akifafanua umoja wa Kanisa ulivyo muhimu kwa mahusiano na Mungu na kwa amani duniani.

Papa Gregori I, aliyeitwa Mkuu kutokana na umuhimu wake katika historia ya Kanisa.

Hasa hotuba zake, zilizoandikwa na wengine wakati alipokuwa anazitoa kwa watu akiongea nao kirahisi, zimechangia kueneza ujumbe wake. Tunazo bado karibu 600, lakini zilikuwa zaidi ya 3,000.

Pia alifafanua upya imani kuhusu umwilisho wa Mwana wa Mungu, akiwahi kutumia misamiati iliyokuja kupitishwa na Mtaguso wa Kalsedonia (451): uwepo wa hali mbili (ya Kimungu na ya kibinadamu) katika nafsi moja. Lengo la umwilisho lilikuwa wokovu wa watu, hivyo hakuna anayeweza kuokoka bila Kristo aliyejitoa sadaka kwa Baba, “akitakasa, akifuta na kutangua makosa yote ya binadamu, akiwakomboa kutoka mamlaka ya shetani”. Mafundisho yake yamesikika hasa juu ya swali la neema na dhambi halafu juu ya uhusiano wa Kanisa na serikali.

Katika mafundisho yake juu ya neema na dhambi ni Augustino aliyetoa fundisho la kwamba ubinadamu umo katika dhambi ya asili tangu Adamu. Uhuru wa kibinadamu umepotea katika dhambi ya Adamu, hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwetu. Alisisitiza kwamba si mwanadamu anayemkuta Mungu lakini Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mwenye dhambi.

Juu ya uhusiano kati ya serikali na Kanisa aliandika kitabu "De Civitate Dei" (Mji wa Mungu). Badala ya "mji" tungeweza kutafsiri pia: "eneo au kikundi cha watu au utawala". Alieleza kwamba iko "miji" miwili: mji wa Mungu (yaani Yerusalemu wa mbinguni, au Kanisa) na mji wa dunia hii, yaani taratibu za kisiasa. Katika "mji wa dunia hii" hali hubadilika. Hakuna taratibu za kudumu. Augustino alifahamu habari za taratibu za Waroma wa kipagani walioangalia makaisari wao kuwa miungu, akafahamu habari za demokrasia ya Ugiriki wa kale. Akafahamu habari za mji mkubwa wa Roma ulioitwa "mji wa milele" lakini ulichomwa moto na maadui katika siku zake sawasawa jinsi ilivyoanguka zamani miji ya Babiloni au Yerusalemu. Lakini pamoja na "mji" huo upo "mji" wa pili, ndio mji wa Mungu, ambao ni mji wa upendo na udugu penye neema yake Mungu. Miji yote miwili iko pamoja ingawa taratibu zao ni tofauti. Mkristo ni raia ya miji yote miwili. Huitwa kuwa mwaminifu katika pande zote mbili. Lakini ajue ya kwamba mji wa dunia hii hauna shabaha ya kudumu. Umeingiliwa na dhambi. Lakini mji wa Mungu utadumu. Umepewa lengo la kudumu, unashirikiana katika enzi ya Mungu. Ndiyo sababu inafaa serikali isikie wazo la Kanisa kwani ni kwa njia ya Kanisa kwamba Mungu ameamua kufunua mapenzi yake. Mkristo anaweza kushiriki katika taratibu za kisiasa akijua ya kwamba mawazo na mipango yote ya siasa havidumu. Utakaodumu ni utaratibu wa Mungu tu.

Kutokana na mafundisho hayo ya Augustino Kanisa la Magharibi lilijifunza kuwa na msimamo wake mbele ya serikali mbalimbali zilizojitokeza katika historia yake ndefu. Augustino alipokuwa kijana alishuhudia jinsi Mkuu wa Dola Kaisari Theodosi alivyolazimika kutubu kanisani baada ya Askofu Ambrosi wa Milano kumtenga kwa sababu ya kumpandisha cheo Mkuu wa wanajeshi wake walioua ovyo watu wengi sana walipogandamiza fujo lililotokea katika mji wa Thesalonike. Watu wengi walisikitikia tendo hilo. Hivyo Theodosi alipotaka kuingia katika ibada Askofu alimtangaza hawezi kushiriki meza ya Bwana kwa sababu ya damu ya wananchi wa Thesalonike. Basi, Kaisari akakiri kosa mbele ya umati akatubu. Hata baadaye viongozi wa Kanisa la magharibi wakafuata mara nyingi mfano huo wa Ambrosi na mafundisho ya Augustino.

Tunaweza kuona matokeo mawili ya urithi huo: kwa upande mmoja Kanisa lilijaribu kutawala juu ya jamii na serikali katika nchi za Ulaya. Lilidai sheria zote za serikali zifuate taratibu za Kanisa. Viongozi wa serikali walitakiwa kusimikwa na Kanisa. Hoja hiyo huitwa "Uklerikali". Nguvu ya kisiasa ya Kanisa lilipingwa na kupinduliwa katika mageuzi na mapinduzi mbalimbali ya Ulaya na Amerika (kuanzia mapinduzi ya Ufaransa 1789, katika mapinduzi ya Amerika Kusini karne ya 19 hadi mapigano mengi katika nchi kama Hispania na Austria wakati wa karne ya 20). Siku hizi wazo hili halipo tena lakini zamani lilileta matatizo mengi, kama vile ugandamizaji wa madhehebu mengine na hata vita.

Lakini sehemu nyingine ya urithi huo imebaki: kazi ya Kanisa ya kuzitetea haki za kibinadamu, hata dhidi ya serikali inayoweza kugandamiza haki hizo. Kwa mfano makanisa ndiyo yaliyopinga sana siasa ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na zamani zaidi Marekani, hata dhidi ya serikali iliyotetea utaratibu huo. Vilevile ni makanisa yanayotetea haki za wakimbizi katika nchi nyingi hata kama serikali zimeshachoka na mzigo wa kupokea wahamiaji maskini kutoka nchi nyingine.

Mwishoni tusifiche sehemu ya urithi wa Augustino iliyo na ugumu zaidi mpaka leo. Katika mikoa ya Afrika Kaskazini walikuwepo Wakristo wengi waliojitenga na Kanisa kubwa na kuanzisha madhehebu ya Wadonato. Augustino alijadiliana nao miaka mingi akijaribu kuwavuta warudi tena.

Mwaka 411 BK serikali ya Kiroma ilitafuta shauri la Augustino katika suala la Wadonato kwa kuwa ilitaka kuwe na umoja wa kidini kati ya wananchi. Tena wapinzani wa utawala wa Roma huko Afrika Kaskazini walikuwa wamejiunga na Kanisa la Wadonato. Basi Augustino aliona kwamba Wadonato wameshika mafundisho ya uongo, akaogopa wataongoza waumini wao jehanamu. Akaona Kanisa lisiache wafundishe uongo, bali litumie nguvu ya serikali kuwalazimisha kurudi katika Kanisa kubwa. Mwenyewe hakukubali adhabu ya kifo kwa "wazushi" hao, lakini serikali ilichukua kibali chake cha kuingilia kati kama msingi wa kuwatesa vikali na kuwaua wengi. Wadonato walipoteswa hivyo na serikali, Augustino akanyamaza, hakupinga.

Mateso hayo ya Wakristo Wadonato chini ya serikali ya Kikristo mbele ya macho ya Kanisa Katoliki yaliendelea muda mrefu yakawa mwanzo wa mwisho wa Ukristo Afrika Kaskazini-Magharibi. Tatizo halikuishia Afrika Kaskazini. Augustino katika kitabu chake kimojawapo alitetea siasa ya ugandamizaji wa wazushi bila kuruhusu wauawe. Katika karne zilizofuata maandiko hayo yaliongoza sera ya Kanisa la magharibi dhidi ya wazushi kote Ulaya. Kanisa lilikubali wazo la kwamba wazushi wanapaswa kugandamizwa. Basi kwa karne kadhaa Kanisa la magharibi likaendelea kuwagandamiza na kuwatesa Wakristo wasiokubali mafundisho yake au uongozi wake. Watu walifungwa gerezani, wakateswa hata kuchomwa moto, yote hayo kwa idhini ya Kanisa. Hata madhehebu ya Kiprotestanti kama Walutheri, Waanglikana na Wareformati yalitenda hivyo baada ya kuwa dini rasmi ya serikali katika maeneo yao. Bila shaka Augustino hakutegemea matokeo hayo lakini hata habari hizi za kuhuzunisha ni sehemu ya urithi wa mtu huyo ambaye kwa mengine tunamkumbuka kama mwalimu mkubwa wa Ukristo mzima.

Mbali ya Augustino, Kanisa la Magharibi katika karne ya 4 hadi ya 6 lilizaa mababu wa Kanisa wengine walioathiri moja kwa moja imani, maadili, liturujia na uchungaji: kwanza askofu Ambrosi (Trier, leo nchini Ujerumani, 340 hivi - Milano, Italia, 4 Aprili 397), ambaye ndiye aliyembatiza Augustino, halafu padri Jeromu (Strido, leo nchini Korasya 347 - Bethlehemu, Israeli, 420) na Papa Gregori I (Roma, Italia, 540 hivi – Roma, 12 Machi 604).

Tukiacha hao viongozi bora, na kuangalia maisha ya waumini wa kawaida, tunapaswa kusema kuwa wengi hawakuridhika tena kupokea Ekaristi Jumapili tu; walianza kuheshimu si wafiadini tu, bali watakatifu wengine pia kama hao tuliowataja, na masalia yao; kwa namna ya pekee heshima ilizidi kutolewa kwa Bikira Maria na kwa Msalaba wa Mwanae. Kwa ajili hiyo walioweza kufunga safari ya hija walikwenda mahali patakatifu walipoishi Yesu na hao watakatifu wake.

Mafarakano ya kudumu ya mataifa mazima[hariri | hariri chanzo]

Katika karne ya 4 Dola la Roma lilianza kupata matatizo. Hali ya hewa ilibadilika: watu wakakosa chakula cha kutosha. Hiyo ilisababisha kipindi kirefu cha vita na vurugu. Makabila kutoka Ulaya kaskazini yalianza kuhamia kusini wakiwasukuma majirani wao kuhamahama vilevile. Matembezi hayo yalifika kwenye mipaka ya Dola la Roma. Waroma walishindwa kuwazuia kutokana na uzazi wao kupungua na polepole mataifa yale yasiyostaarabika yakaingia katika eneo la dola na kutwaa mikoa mbalimbali. Waroma wakatumia hela nyingi sana kwa ajili ya jeshi lao lakini bila kufanikiwa.

Mwaka 395 Kaisari akagawa dola la Roma katika sehemu mbili, yaani Magharibi (makao makuu Roma) na Mashariki (makao makuu Bizanti). Mpaka wa katikati ulifuata tofauti ya utamaduni kati ya maeneo yaliyotumia zaidi lugha ya Kigiriki na maeneo yaliyotumia zaidi Kilatini. Ugawaji huo ulikuwa na kusudi la kurahisisha utawala na utetezi. Lakini mwaka 410 makabila yasiyostaarabika yaliteka na kuharibu mji wa Roma. Mwaka 476 Kaisari wa mwisho wa Magharibi aliuawa.

Ubatizo wa Chlodwig, mfalme wa Wafaranki, uliingiza kabila hilo kubwa katika Kanisa Katoliki. Tukio lilivyochongwa katika pembe ya ndovu (karne ya 9).

Makabila ya Kijerumaniki yalichukua utawala katika sehemu zote za Ulaya mpaka Afrika Kaskazini. Dola la Roma la Magharibi likagawanywa katika nchi nyingi ndogondogo. Kila sehemu makabila toka Kaskazini yalitawala kama tabaka dogo la juu wakiwategemea wenyeji kuendelea kuzalisha mali na wenyewe kupokea kodi zao. Lakini utaratibu, mawasiliano na usalama viliharibika kabisa. Uchumi na utamaduni vilirudi nyuma. Umoja wa kisiasa uliharibika, badala yake yalitokea maeneo mengi madogo ya kikabila. Ulaya Magharibi ilibaki na chombo kimoja tu chenye umoja uliovuka mipaka: Kanisa Katoliki chini ya uongozi wa Askofu wa Roma. Ndiye aliyetunza urithi wa jina kubwa la Roma akiheshimiwa pia kama mwandamizi wa Mtume Petro. Kwa sababu elimu ilishuka chini popote Ulaya Magharibi, ni ndani ya Kanisa tu kwamba mapadri na wamonaki wakaendelea kusoma na kutunza elimu ya kale. Watu kutoka Ulaya kaskazini hawakuwa wasomi. Hivyo watawala wao walitegemea watu wa Kanisa wakitaka kuandika au kusomewa barua au mikataba. Polepole watawala wapya pamoja na makabila yao wakapokea Ukristo. Walifundishwa kwamba mfalme hupewa madaraka yake na Mungu, hivi anapaswa kufuata shauri la Kanisa ambalo linatangaza mapenzi ya Mungu. Kutokana na hali hiyo ya kiutamaduni na ya kiroho Kanisa lilikuwa na athari kubwa sana.

Papa kama mchungaji mkuu alilazimika kuwajibika ili kuokoa jahazi. Ndivyo walivyofanya hasa Papa Leo I na Papa Gregori I. Wafaranki, kabila kubwa la Kigermanik waliwahi kujiunga na Kanisa Katoliki wakawa msaada mkubwa kwa Mapapa. Isipokuwa, kwa kuwaachia watawale Italia ya Kati, walisababisha Papa aanze kuwa kama mfalme wa dunia hii, jambo lililoathiri sana majukumu yake ya kiroho hadi mwaka 1870.

Kwa juhudi za wamonaki Wabenedikto na wengineo, ustaarabu wa kale uliokolewa katika vitabu vyake na uinjilishaji uliendelea katika Ulaya ya Kati. Ni kwamba watu kutoka Ulaya kaskazini hawakuwa wasomi. Hivyo watawala wao walitegemea watu wa Kanisa wakitaka kuandika au kusomewa barua au mikataba. Polepole watawala wapya pamoja na makabila yao wakapokea Ukristo wa Kikatoliki. Walifundishwa kwamba mfalme hupewa madaraka yake na Mungu, hivi anapaswa kufuata shauri la Kanisa ambalo linatangaza mapenzi ya Mungu. Kutokana na hali hiyo ya kiutamaduni na ya kiroho Kanisa lilikuwa na athari kubwa sana.

Utamaduni na utaratibu wa kale, pamoja na taratibu za siasa na uchumi, viliendelea katika sehemu ya mashariki ya dola. Watawala wa Bizanti wakaendelea kutumia cheo cha Kaisari wa Roma. Wengine wao walijaribu kutawala tena eneo lote la zamani hata upande wa magharibi lakini ilishindikana. Kanisa huko liliendelea kuwa dini rasmi. Kwa sababu serikali ilikuwa yenye nguvu zaidi, Kanisa lilikuwa chini yake. Kaisari alikuwa mlezi mkuu wa Kanisa. Ndiye aliyemthibitisha Askofu Mkuu wa Konstantinopoli na maaskofu wa dayosisi.

Kwa sababu ya matatizo ya ndani ya dola la Roma la Mashariki mafarakano yalitokea katika nchi za Misri na Siria zilizokuwa chini ya Kaisari wa Bizanti. Katika nchi hizo, baada ya mtaguso wa Kalsedonia (451), sehemu kubwa ya Wakristo walijitenga na kuendelea kama Kanisa la kitaifa. Kanisa la Misri lilifuatwa na Kanisa la Nubia na la Ethiopia. Kwa namna hiyo makanisa hayo ya kale ya Afrika yameendelea hadi leo kwa namna ya pekee. Ilitokea vilevile kwa Kanisa la Siria, la Armenia n.k. Hawakuwa tena waamini binafsi walioshika msimamo tofauti na ule rasmi, bali Wakristo karibu wote wa nchi fulani chini ya maaskofu wao waliojitenga na umoja wa Kanisa.

Kanisa la Mashariki kwa Dola la Roma lilipofikia kilele cha uenezi wake.

Kabla ya hapo, kufuatana na mtaguso wa Efeso (431), Wakristo wa nje ya Dola la Roma upande wa mashariki (Mesopotamia, Uajemi n.k.) walikuwa wameshajitenga na kuendeleza maisha ya Kikristo chini ya dhuluma za Dola la Uajemi, huku wakieneza habari njema mbali zaidi na zaidi, hadi China na Indonesia.

Kumbe Kanisa Katoliki liliendelea tofautitofauti katika sehemu hizo za mashariki na magharibi za Dola la Roma. Wakristo wa Magharibi (nchi za Ulaya magharibi pamoja na Afrika kaskazini) wakafuata uongozi wa Papa yaani Askofu wa Roma. Kanisani walitumia lugha ya Kilatini. Wakristo wa Mashariki wakafuata maaskofu wao waliokuwa chini ya serikali ya Kaisari wa Bizanti. Kama lugha walitumia Kigiriki.

Pamoja na magomvi katika uenezaji wa Ukristo kwenye maeneo ya Ulaya yaliyokuwa bado ya Kipagani (hasa kati ya Waslavi), tofauti hizo zilisababisha desturi na mawazo yaliyozidi kutofautiana. Ziliweka msingi wa kutokea kwa madhehebu mawili makubwa yanayoendelea mpaka leo yaani Kanisa Katoliki la Kiroma (magharibi) na Kanisa la Kiorthodoksi (mashariki).

Ethiopia na Nubia[hariri | hariri chanzo]

Frumensi, mmisionari wa ufalme wa Aksum (Ethiopia na Eritrea ya leo).

Jangwa kubwa la Sahara lilifanya mawasiliano yote kati ya Afrika Kaskazini na sehemu nyingine za bara kuwa magumu. Lakini tangu zamani mto Nile ulisaidia biashara na athari za kiutamaduni na za kisiasa kuvuka kanda la jangwa. Hivyo upo uhusiano wa pekee kati ya Misri na eneo linaloitwa leo "Sudan". Zamani nchi hiyo kusini kwa Misri iliitwa kwa jumla "Nubia"; sehemu moja ilijulikana kwa miaka mingi kwa jina la Kushi". Mdo 8 inaonyesha kwamba safari kati ya Kushi (Sudan) na Misri mpaka Yerusalemu zilikuwa kawaida. Njiani Filipo alimbatiza "towashi wa Kushi" yaani afisa wa serikali ya malkia Kandake wa Kushi katika mji mkuu wa Meroe (si Ethiopia ya leo). Lakini hatuna habari zaidi kama huyo afisa alihubiri Injili kwake nyumbani.

Kuanzia karne ya 3 athari za Ukristo katika Nubia zinajulikana. Wamonaki Wamisri walihubiri Injili huko. Kuanzia mwaka 600 wakazi wengi wa Kushi walikuwa Wakristo. Makanisa mengi, tena makubwa, yalijengwa na kupambwa katika miji mikubwa kama Dongola na Soba. Kwa miaka elfu moja utamaduni wa Kikristo uliendelea. Kutoka Dongola wamisionari walifika kusini mwa Sahara mpaka eneo la Tibesti (yaani Chad ya leo) ambapo maghofu yanaonyesha alama za Ukristo kule.

Kusini-Mashariki kwa Kushi tunakuta eneo kubwa lenye milima mirefu iliyosimama kama mnara katika tambarare ya nchi jirani. Ni nyanda za juu za Ethiopia au Uhabeshi. Mnamo mwaka 300 BK kulikuwa na ufalme katika eneo la Aksum (Ethiopia ya leo). Wakati Kaisari Konstantino alipotawala Roma, meli moja iliyokuwa safarini kutoka Shamu kwenda Bara Hindi iliharibika kwenye pwani ya Ethiopia. Vijana wawili waliokolewa wakapelekwa kwa mfalme kule Aksum. Mmojawao kwa jina Frumensi alipata haraka sifa za kuwa na elimu na hekima. Akapanda ngazi kuwa mshauri wa mfalme na mwalimu wa mwana wa mfalme aliyeitwa Ezana. Frumensi alipanda mbegu za imani moyoni mwa kijana huyo. Baada ya kuwa mfalme, Ezana akaendelea kumtumia Frumensi kama mshauri wake. Siku moja Frumensi aliomba ruhusa ya mfalme aende nyumbani kuangalia kama wazazi wake bado wanaishi. Mfalme akamruhusu akamwomba atafute kule walimu wanaoweza kufundisha elimu aliyokuwa nayo Frumensi pamoja na imani ya Kikristo. Frumensi akamwendea Askofu Mkuu wa Misri naye alimweka wakfu kuwa askofu wa Waethiopia. Mfalme Ezana akabatizwa akifuatwa na watu wengi wa makao makuu. Kwa muda mfupi dini hiyo mpya ilienea katika ufalme wote.

Baadaye walifika huko wamonaki kutoka Misri na Shamu. Ndio walioanza kufundisha na kubatiza Wahabeshi wengi. Ndio mwanzo wa taifa la Kikristo la Ethiopia. Wahabeshi wametunza urithi wao wa Kikristo mpaka leo. Ukristo wao unafuata mapokeo ya Kiorthodoksi ya Mashariki yalivyo Misri: mpaka karne ya 20 walipokea Maaskofu wao wote kutoka Kanisa la Kikopti la Misri.

Uenezi wa Uislamu ulivyorudisha nyuma Ukristo na umisionari wake[hariri | hariri chanzo]

Uenezi wa Uislamu hadi mwaka 661.

Katika karne za kwanza baada ya Kristo Afrika Kaskazini ilipata kuwa ya Kikristo, lakini baadaye yalitokea mageuzi makubwa sana katika historia ya Afrika: uenezi wa Uislamu.

Mnamo mwaka 610 sehemu kubwa ya Afrika Kaskazini iliunganika tena chini ya Dola la Roma Mashariki lililotawaliwa kutoka mji wa Bizanti. Lakini utawala huo ulikuwa hafifu kulingana na ule wa Roma ya kale. Wenyeji wa Misri na mkoa wa "Afrika" (= Tunisia ya leo) waliupinga. Wakristo wengi katika nchi hizo walikataa usimamizi wa Askofu Mkuu wa Bizanti wakiwafuata viongozi wao wa kitaifa. Viongozi wa Kanisa la Kikopti (Misri) waliteswa na serikali ya Bizanti. Dola la Roma Mashariki lilimaliza nguvu zake vitani dhidi ya majirani yao wa Uajemi na makabila yasiyostaarabika kutoka kaskazini.

Hali hii ilibadilika ghafla mwaka 640. Habari za imani mpya zilisikika kutoka eneo la Maka na Madina huko Uarabuni. Muhammad aliunganisha makabila yote ya Waarabu kwa jina la Mungu mmoja, (kwa Kiarabu: Allah).

Mwaka 622 Mwarabu huyo alikimbia mji wa Maka akaelekea mji wa Jathrib (leo Madina) akiongozana na marafiki wachache. Wakazi wa Maka walikuwa wamemkasirikia Muhamad. Kwa miaka 12 aliwahubiria ufunuo aliodai ameupokea kutoka kwa malaika wa Mungu. Alipinga desturi na maadili ya watu wa mji wake. Akatangaza "Uislamu" yaani imani katika Mungu mmoja aliyetoa amri zake kwa wanadamu. Kumbe viongozi wa Maka waliona anaharibu dini ya jadi ya kuabudu sanamu za miungu. Makabila ya Waarabu walikuwa wakija kila mwaka kuabudu sanamu za Maka katika jengo la Kaaba. Wakati wa ziara hizo biashara ya Maka ilistawi sana. Muhammad alionekana kuwazibia viongozi hao riziki wakakasirika wakajaribu kumwua lakini akakimbia.

Madina alipokewa vizuri, na wenyeji wakamwamini. Habari zake zikaenea haraka pande zote za Uarabuni. Makabila mbalimbali ya Waarabu walimwunga mkono. Akawa kiongozi wao kidini, kijeshi na kisiasa. Mwaka 630 akawashinda watu wa Maka kivita lakini alionyesha busara kwa kuwahurumia mradi wajiunge na Uislamu.

Alipofariki mwaka 632 karibu Waarabu wote waliungana chini ya bendera ya Uislamu wakashambulia maeneo jirani ya Waroma wa Bizanti na ya Waajemi. Miaka mia moja baada ya kifo cha Muhamad sehemu kubwa ya dunia kati ya Moroko na Bonde la Indus (leo Pakistan) ilikuwa chini ya Uislamu.

Uenezi huo ulikuwa wa haraka sana. Mwaka 636 Waarabu wakawashinda Waroma wa Bizanti kule Shamu wakateka Dameski na Yerusalemu. Mwaka uleule wakawashinda Waajemi kule Mesopotamia (Iraq). Mwaka 639 wakaingia Misri na kuteka Aleksandria miaka mitatu baadaye. Mwaka 642 waliteka sehemu kubwa ya Uajemi wenyewe. Miaka 670/696 waliteka mkoa wa Afrika ya Kiroma pamoja na Karthago. Mwaka 711 wakavuka mlangobahari na kuingia Hispania (Ulaya Kusini). Walifika mpaka Ufaransa wakarudishwa na wenyeji mwaka 732 lakini walitawala sehemu za Hispania kwa karne saba zilizofuata. Mwaka 718 walikuwa wameshindwa pia kuteka Konstantinopoli yenyewe iliyoendelea kutawala Asia Ndogo. Badala yake wakaenea pia Asia ya Kati wakasimama ana kwa ana mbele ya wanajeshi wa Wahindi na mwaka 751 walipigana na jeshi la China.

Ushindi wa Wafaranki juu ya Waislamu huko Tours (732) ulizuia uenezi wa dini hiyo Ulaya Magharibi.

Wakristo kugeuka Waislamu[hariri | hariri chanzo]

Dunia nzima ilishangaa kusikia habari ya kwamba Waarabu kutoka jangwani walifaulu kuwashinda wanajeshi hodari wa Kiroma na wa Kiajemi. Lakini Waarabu walikutana na maadui waliokosa nguvu: katika miaka iliyotangulia dola hizo mbili kubwa ziliwahi kupigana vita virefu na vikali. Wananchi wote na wanajeshi wao walichoka. Uchumi ulidhoofika baada ya miaka 20 ya vita. Tena wenyeji wa Misri na Siria walisikitikia utawala wa Kaisari wa Bizanti. Walidai tangu muda mrefu uhuru wa kitaifa lakini wakagandamizwa.

Uislamu ulienea haraka sana kwa nguvu ya kijeshi katika nchi hizo zilizokuwa na Wakristo wengi. Mwanzoni walikuja Waarabu kadhaa tu: walichukua madaraka ya serikali kuu na kujenga makambi ya kijeshi katika kila nchi. Vijana wa Kiarabu walifuata baba zao wakiitikia wito wa dini uliokuja pamoja na nafasi ya kupata maisha nafuu. Mbali ya nguzo tano za Uislamu, walifundishwa kwamba ikiwa watakufa katika vita vitakatifu watapokewa na Mungu kama mashahidi wa imani na kuingia Paradiso moja kwa moja. Lakini wasipokufa vitani watakuwa matajiri wakitawala nchi mpya na kupokea kodi za wenyeji wasio Waislamu. Imani ya aina hii iliwapa nguvu kweli na iliendelea kuvuta Waarabu wengi kutoka kwao kuhamia Afrika Kaskazini na Asia ya Kati.

Kwa kawaida Wakristo hawakulazimishwa kuacha imani yao. Viongozi wa Waarabu washindi walifanya mikataba na maaskofu wa Kikristo katika maeneo waliyoyateka. Wakristo waliahidiwa ulinzi wa makanisa yao wakiambiwa wanaweza kuendelea na mila na desturi walivyozoea. Lakini hawakuwa na haki zote za uraia. Wasio Waislamu walijiona wanabaguliwa mbele ya Waislamu. Walitozwa kodi kubwa ya pekee. Mahakamani hawakuweza kushuhudia dhidi ya Mwislamu, walilazimishwa kuvaa nguo za pekee tofauti na Waislamu, walikataliwa kupanda farasi, kujenga makanisa mapya, au kutumia kengele makanisani. Waislamu walipata kipaumbele katika mambo yote. Hivyo polepole wenyeji walianza kutumia lugha ya Kiarabu pamoja na kujiunga na Uislamu. Bila shaka wazazi wengine walitumaini kuwasaidia watoto wao wapate maendeleo maishani wakifuata dini ya watawala.

Masharti ya kujiunga na Uislamu ni rahisi. Hakuna mafundisho magumu, mwanzoni inatosha kutamka "shahada" ya Kiislamu ambayo ni fupi sana: As-haddu inna la ilaha ila allah, wa Muhamad rasul ullah. (Nakiri ya kwamba Mungu ndiye mmoja tu, na Mohamad ni mtume wa Mungu). Lakini baadaye haiwezekani kurudi katika Ukristo maana sheria ya Kiislamu inaruhusu Mkristo kugeuka Mwislamu lakini inakataza kwa adhabu ya kifo Mwislamu asitoke katika imani hiyo na kufuata dini nyingine.

Sababu kubwa ya udhaifu wa Wakristo hao ilikuwa mafarakano kati yao, na hasa majaribio ya serikali ya Bizanti kuwalazimisha wote kufuata uongozi wake, wakiitumia na kuitawala dini kama nguzo ya siasa yake. Lakini mambo ya imani hayafai kulazimishwa. Hivyo katika nchi kama Misri Wakristo waliotaka uhuru wa kisiasa walilazimishwa kuwa chini ya Askofu wa Bizanti, wakajisikia wanagandamizwa kidini pia, si kisiasa tu. Baadhi yao waliwapokea Waislamu kwa matumaini ya kuwa watamaliza utawala wa kidikteta wa Bizanti. Jeshi la Bizanti lilishindwa kwa kukosa msaada wa wazawa. Kiongozi Mwislamu aliahidi madhehebu yote yataheshimiwa. Alifanya mkataba na Wakristo waendelee na ibada zao na desturi zao. Ahadi hiyo ilitimizwa kwa namna tofauti. Baada ya muda Wamisri walijikuta wamekuwa watu wa ngazi ya chini. Mabwana wapya walianza kubadilisha utamaduni wa nchi. Aliyejiunga na Uislamu na kujifunza Kiarabu alikubaliwa lakini Wakristo wenyeji waliotunza urithi wao walibaguliwa. Majaribio yote ya kupigania uhuru yaligandamizwa vikali.

Baadaye Waislamu waliteka sehemu iliyobaki ya Afrika Kaskazini kama Tunisia na Algeria. Huko Ukristo ulikuwa dhaifu kutokana na mafarakano mengi ya miaka ya nyuma na dhuluma za kidini. Nguvu zake za ndani zilivunjika wakati wa mateso makali ya Wadonato kwa mikono ya Wakatoliki, yakifuatwa na mateso makali ya Wakatoliki kwa mikono ya Wakristo Waario. Baada ya karne za kulaumiana na kuuana kati ya Wakristo, wengine walikuwa na wasiwasi juu ya ukweli wa mafundisho ya Kanisa. Si ajabu kwamba huko Ukristo ulipotea baada ya karne chache za utawala wa Kiislamu. Pamoja na matatizo yaliyowapata Wakristo chini ya utawala huo, kwa muda mfupi wenyeji wengi wa sehemu hizo walisilimu. Tena katika nchi za jirani (Italia na Hispania) vita vikali vilipigwa kati ya Waarabu walioshambulia na Wakristo waliojitetea; labda hali hiyo iliongeza moyo wa Waislamu kutovumilia uwepo wa Wakristo. Kanisa la Afrika Kaskazini-Magharibi lilikoma baada ya karne chache, tofauti na Misri ambako Wakristo walishika imani yao katika karne zote ingawa kwa matatizo makubwa chini ya serikali ya Kiislamu.

Mara kwa mara upande wa watawala na wakubwa yalijitokeza matendo mabaya, kama makanisa kubomolewa au kugeuzwa misikiti, n.k. Kwa mfano msikiti mkuu wa Dameski (Siria) ulikuwa zamani Kanisa la Mt. Yohane Mbatizaji. Mwanzoni Waarabu waliahidi kuliheshimu, lakini mtawala aliyefuata alitaka jengo kubwa lililopatikana mjini kwa ajili ya ibada yake. Ndivyo ilivyotokea Waturuki walipoteka Konstantinopoli: Kanisa Kuu la Hagia Sofia (Hekima Mtakatifu) liligeuka msikiti.

Vipindi vya kulazimisha vilitokea tena na tena, hasa baada ya mataifa mapya kuwa Waislamu. Waarabu wenyewe walionyesha ustahimilivu zaidi kwa wenye imani nyingine (Wakristo, Wayahudi n.k.). Lakini Waturuki, Waajemi na Wamongolia baada ya kuwa Waislamu walikuwa wakali. Hasa vipindi vya vita vya msalaba kati ya Wakristo kutoka Ulaya na Waturuki viliongeza uchungu kwa Wakristo waliokuwa chini ya utawala wa Kiarabu. Katika vipindi hivyo Wakristo chini ya Waislamu waliweza kuangaliwa kama wasaliti na kuteswa, makanisa yao kubomolewa n.k.

Pamoja na Wakristo wengi kugeuka Waislamu, umisionari kwa mataifa mengine ya Afrika na Asia ulizuiwa na dola la Kiislamu lililozunguka karibu pande zote nchi za Kikristo.

Athari nyingine ya Uislamu katika historia ya Kanisa, hasa la Mashariki, ilikuwa dharau kwa sanamu na picha takatifu zilizokuwa zimeenea tangu karne za kwanza BK. Ni kwamba, kisha kupigwa vitani na Waislamu mara kadhaa, kwenye miaka ya 720 Kaisari Leo III wa Konstantinopoli alizikataza hizo na masalia ya watakatifu akaagiza zilizokuwepo ziteketezwe kwa sababu eti, ni sawa na kuabudu miungu. Lengo lake lilikuwa kupunguza uadui wa Waislamu dhidi ya Wakristo na Dola la Roma. Lakini waamini wengi wa dola lake walipinga uamuzi huo, wakiungwa mkono na Papa Gregori III. Hatimaye Mtaguso wa pili wa Nisea (787) ulitetea na kupitisha uhalali wa picha hizo katika Ukristo.

Kanisa lilivyoendelea hasa Ulaya[hariri | hariri chanzo]

Tangu kuja kwa Uislamu uenezaji wa Injili katika Afrika ulikwama na kurudi nyuma. Kusini kwa Sahara ilifika kupitia Nubia lakini baada ya Nubia kuwa ndani ya eneo la Kiislamu athari hii haikuendelea. Kumbe uenezi wa Ukristo katika kipindi kile ulipatikana Ulaya na Asia.

Kule Ulaya makabila mengi yaliendelea kupokea Ukristo. Wakati mwingine watu walivutwa na mahubiri kuacha Upagani na kubatizwa. Mara nyingi waliona ya kwamba miungu ya kikabila haina msaada tena katika mazingira iliyobadilika. Waliweza kuvutwa na mfano bora wa wamonaki walioishi kati yao, au kushangazwa na elimu au maendeleo yao. Wakati mwingine wafalme waliamua kuwa Wakristo kwa sababu za kiroho au za kisiasa wakabatizwa pamoja na kabila au taifa zima. Katika mawazo ya Wazungu wa kale dini haikuwa jambo la mtu binafsi bali jambo la kijamii. Wakati mwingine washindi wa vita waliamua kuwabatiza maadui ili kujenga uhusiano wa kiroho nao. Ndiyo sababu ya ubatizo wa mabavu ulioweza kutokea katika nchi kadhaa.

Karolo Mkuu na Papa Adrian I. Karolo alitawazwa na Papa Leo III kuwa Kaisari wa magharibi (800). Ushirikiano kati ya Mapapa na Makaisari wa Dola Takatifu la Kiroma (leo Ujerumani na nchi za kandokando) ulikuwa na mafanikio kadhaa na matatizo mengi zaidi na zaidi.

Mfano mmojawapo ni ubatizo wa Wasaksoni, kabila kubwa katika eneo la Ujerumani kaskazini. Baadhi ya mababu wao walivuka bahari na kuteka Uingereza pamoja na Waangli. Wakati ule Wajerumani wengi walikuwa Wakristo lakini Wasaksoni waliendelea kutetea Upagani wao.

Mfalme wa eneo la Ufaransa na Ujerumani Magharibi aliyeitwa Karolo Mkuu alipigana nao mara kwa mara. Mwishowe aliona wakibaki Wapagani hatawashinda. Mwaka 800 B.K. aliwapa chaguo: upanga au ubatizo. Mwanzoni walikataa akawaua machifu 4000 wa Wasaksoni katika siku moja. Waliobaki wakabatizwa wakawaamuru wenzao kubatizwa vilevile. Hivyo eneo kubwa lilipokea Ukristo, lakini si kwa sababu ya imani, ila kwa kulazimishwa.

Si ajabu ya kwamba kwa muda mrefu Ukristo wa Ulaya katika nchi mbalimbali ulikuwa wa juujuu tu, ukaonyesha dalili za mchanganyiko wa Injili na desturi za kale za Upagani. Kumbe Ukristo ulikwenda njia ndefu sana tangu zamani za mashahidi wa Aleksandria na Karthago waliokufa badala ya kukana Ukristo wao mpaka wale Wakristo wapya wa Kisaksoni walioona heri wabatizwe kuliko kufa.

Maeneo mapya ya Ukristo yalifuata desturi za kule walikotokea wahubiri wao. Ndivyo makabila ya Ulaya kaskazini walivyojiunga na Kanisa Katoliki la Kilatini. Kumbe makabila ya Mashariki wakawa Waorthodoksi wakipokea ubatizo kutoka kwa wajumbe wa Askofu wa Bizanti. Mpaka leo Ulaya mataifa ya Warusi, Waukraina, Waromania, Wabulgaria na Waserbia (pamoja na Wagiriki wenyewe) ni Waorthodoksi. (Afrika ni hasa nchi za Misri, Ethiopia na Eritrea zinazofuata mapokeo ya Kiorthodoksi ya Kikopti). Mnamo mwaka 1000 karibu maeneo yote ya Ulaya yalikuwa na Wakristo, ingawa mara nyingi kwa jina tu.

Baada ya mafarakano ya muda (hasa la miaka 863-867 kuhusu upatriarki wa Fosyo), mwaka 1054 wajumbe wa Askofu wa Roma walimtembelea Askofu Mkuu wa Konstantinopoli, Mikaeli Cerularius, ambaye alikuwa amejidai kuwa sawa na Papa na kulaumu desturi mbalimbali za Roma. Walianza kupingana naye vikali kuhusu desturi zao tofauti na mwishoni wakalaaniana bila kuzingatia umoja wao katika imani na sakramenti. Tangu mwaka ule farakano kati ya Ukristo wa Magharibi na Waorthodoksi limedumu hadi leo, kwa kuwa majaribio mbalimbali ya kurudiana yalishindikana. Ilichukua miaka mingi kufuta laana hizo. Mwaka 1967 Papa Paulo VI wa Roma alikutana na Patriarki Athenagoras wa Konstantinopoli (leo: Istanbul) wakapatana tena na kusameheana makosa ya zamani, ingawa umoja kamili haujapatikana. Uelewano umeanza kujengwa pia kati ya makanisa yaliyofarakana zamani kuliko Konstantinopoli kama vile Waashuru, Wakopti na Wasiria.

Kule Asia Ukristo wa Kiorthodoksi uliendelea vizuri katika nchi nyingi. Tangu mwanzo mpaka leo lipo Kanisa la India Kusini (jimbo la Kerala). Wamisionari wa Kanisa la Mesopotamia na Uajemi walihubiri kote Asia ya Kati hadi Uchina na Indonesia. Lakini maendeleo hayo yalirudishwa nyuma na mashindano kati ya Ukristo na Uislamu. Kiasili Uislamu ulikuwa na uvumilivu kwa dini za Wakristo na Wayahudi. Katika maeneo ya Waarabu kama Misri au Siria Kanisa liliendelea kupata ustahimilivu: liliweza kuendelea na ibada ya Kikristo ingawa kwa matatizo.

Lakini huko Asia makabila na mataifa mapya walipokea Uislamu, mara nyingi kwa njia ya vita. Makabila hayo ya Waturuki na Wamongolia yalifuata imani ya Kiislamu kwa ukali kuliko Waarabu wenyewe. Walilazimisha wote waliokuwa na imani tofauti (Wakristo, Wabuddha au wafuasi wa dini za jadi) wawe Waislamu. Mtawala Mwislamu wa Wamongolia, Tamerlano, aliua Wakristo lukuki na kubomoa makanisa elfu kadhaa alipofanya vita vyake Asia ya Kati. Katika vita hivyo Ukristo wa Asia ya Kati uliharibika kabisa. Maeneo makubwa yalichomwa moto, watu walilazimishwa kwa upanga kuwa Waislamu au kuuawa. Mnamo mwaka 1400 Ukristo wa Asia ulibaki katika Mashariki ya Kati tu (Asia ya Magharibi) pamoja na India Kusini. Kumbe uzito wa Ulaya uliongezeka katika Kanisa kwani ni huko tu lilipoweza kuendelea bila maadui wa nje.

Mwaka 1200 kwa jumla Ulaya ilikuwa bara la Kikristo. Popote Kanisa lilikuwa chini ya ulinzi wa serikali. Watu wote walipaswa kuonekana Wakristo. Watu pekee wenye tofauti walikuwa Wayahudi, lakini waliruhusiwa kuishi katika nchi kadhaa tu; katika nchi nyingine walifukuzwa. Kanisa Katoliki (au: la Kiorthodoksi katika Mashariki) lilikuwa dini rasmi. Katika mila na desturi za Ulaya zilizotangulia kuja kwa Ukristo umoja huo wa dini na kabila ulikuwa kawaida.

Kwa upande mmoja Ukristo ulikuwa na nguvu sana Ulaya wakati ule. Lakini kwa ndani ulikuwa na udhaifu wa aina mbalimbali. Wataalamu wengine wa historia ya Ulaya huita kipindi hicho "Karne za Kati" au hata "Nyakati za Giza". Maana yake ni kipindi kati ya kuanguka kwa utamaduni na uchumi wa hali ya juu uliokuwapo wakati wa Dola la Roma na kipindi cha kuanzia mwaka 1500 ambacho uchumi na elimu vilianza kusonga mbele tena. Kumbe tutajaribu kuangalia pande zote mbili, yaani mafanikio na matatizo.

Kuingiliana kwa dini na siasa[hariri | hariri chanzo]

Katika nchi nyingi tumezoea kwamba serikali haina dini maalumu. Kila mwananchi ni huru kuchagua imani yake. Kumbe wazo hilo si la kawaida popote duniani. Mpaka leo tunasikia habari za nchi zinazotoa kipaumbele kwa dini au madhehebu fulani upande wa serikali. Taratibu hizo ni mabaki ya zile zilizokuwa kawaida katika sehemu nyingi za dunia. Zamani katika nchi nyingi ilikuwa kawaida kuangalia mambo ya dini na mambo ya dola pamoja. Agano Jipya halina amri yoyote juu ya kuunda "serikali za Kikristo". Kinyume chake Wakristo walifundishwa na mtume Paulo kuiombea serikali ya Kipagani ya Kaisari wa Roma. Lakini baada ya viongozi wa mataifa kuwa Wakristo waliona lazima kulitumia Kanisa kama chombo kinachoongeza umoja na nguvu ya nchi.

Katika Ulaya ya Karne za Kati Kanisa na serikali vilikwenda pamoja. Katika sehemu za Waorthodoksi Kanisa lilikuwa chini ya wafalme waliokubaliwa kuwa walezi wake wakuu. Ulaya magharibi kwenye Wakatoliki wengi Kanisa lilikuwa huru zaidi. Lakini hata huko mambo yaliingiliana. Utaratibu wa utawala wakati ule ulikuwa wa kikabaila yaani machifu na watu wa familia za wakubwa walitawala maeneo chini ya serikali kuu ya mfalme.

  • a. Wafalme na hata watawala wadogo walipewa madaraka yao kwa ibada maalumu kanisani.
  • b. Watawala waligandamiza wapinzani wa Kanisa kwani waliona wangeleta vurugu hata kisiasa.
  • c. Watawala walikabidhi madaraka mengi kwa maaskofu. Askofu aliweza kuunganisha uongozi wa Kanisa na mamlaka ya kiserikali katika eneo lake. Viongozi wa Kanisa waliaminika kuliko machifu wa kawaida. Machifu wakikabidhiwa madaraka fulani kwa muda walijaribu mara nyingi kuyashika kama mali yao. Wakatafuta kuongeza mali yao kuwa urithi wa familia. Faida ya kutumia watu wa Kanisa ilikuwa kwamba mapadri na hasa maaskofu hawaoi wala hawana hamu ya kutafuta urithi kwa ajili ya watoto wao.
  • d. Maaskofu (na viongozi wengine wa Kanisa) walichaguliwa mara nyingi kutokana na sifa zao za kisiasa kuliko uwezo wa kuongoza kiroho. Kwa sababu cheo cha askofu kiliambatana na mapato makubwa, ni familia za machifu zilizopeleka wanao katika nafasi hizo. Kwa njia hiyo matabaka ya kijamii yalionekana vilevile ndani ya Kanisa: viongozi wake walitoka katika familia za wakubwa, nafasi za chini walipewa watumishi kutoka familia za kawaida.

Marekebisho ya karne IX-XII[hariri | hariri chanzo]

Ni kawaida ya binadamu kuanzisha kazi kwa nguvu halafu kuchoka, kuanza safari kwa kasi halafu kupunguza mwendo. Vilevile jumuia zina vipindi vya bidii na vya ulegevu.

Kanisa lenyewe, ingawa ni takatifu, linaathiriwa na ukosefu wa wanae. Ila Roho Mtakatifu haliachi bila ya msaada wa watu motomoto ili kulirekebisha.

Utawa unahusika kabisa na utakatifu wa Kanisa: ukistawi mmoja, unastawi wa pili pia. Hasa katika karne IX hadi XII Kanisa la magharibi lilitambua wazi haja ya urekebisho katika umonaki na katika maisha yake yote.

Kati ya matukio muhimu yaliyoandaa ukombozi wa Kanisa kutoka mikono ya wanasiasa kuna uundaji wa monasteri ya Cluny (leo nchini Ufaransa) mwaka 910 ikiwa chini ya Mtume Petro (yaani chini ya Papa tu), si chini ya mtawala wa dunia hii. Monasteri hiyo ilizaa nyingine nyingi kote Ulaya ambazo kwa kutoingiliwa waliweza kuongozwa na watu wa kiroho waliochaguliwa na wamonaki wenyewe kwa malengo ya imani.

Kati ya matawi mapya ya Kibenedikto yaliyotokana na juhudi hizo, mbali ya lile la Cluny (ambalo lilikazia liturujia kuliko kazi za mikono), lile la Camaldoli (lililofufua ukaapweke) na lile la Citeaux (ambalo lilirudia maisha magumu katika ufukara na kazi).

Kaisari Henri IV akiomba msamaha wa Papa Gregori VII huko Canossa (1077) katika mchoro wa Carlo Emanuelle.

Wamonaki wa matawi hayo wakaja kushika nafasi muhimu katika kurekebisha Kanisa na kukomboa Upapa pia katika kuingiliwa na wanasiasa, hasa Petro Damiani (1007-1072), aliyesababisha sheria ya kwamba Mapapa wachaguliwe na makardinali tu, Papa Gregori VII (1028-1085), aliyeshindana na Kaisari akitumia mamlaka ya kiroho, na Bernardo wa Clairvaux (1090-1153), aliyethubutu kuwakosoa Papa na maaskofu uso kwa uso.

Wakati huohuo Bruno (1035-1101) alianzisha aina mpya ya ukaapweke iliyodumu kuwa na juhudi hadi leo (Wakartusi).

Wakati huohuo tena, ili kuboresha maisha ya mapadri wanajimbo, toka zamani ulisisitizwa uundaji wa jumuia kati yao, ambamo wasali na kufanya utume kwa pamoja.

Hasa kuanzia karne XI wengi walifanya hivyo kwenye makanisa makubwa kama mtindo mpya wa kitawa unaosisitiza liturujia ya fahari pamoja na uchungaji.

Inavyoweza kueleweka, hao walifuata kanuni ya Augustino na kuitwa Wakanoni. Maarufu zaidi katika yao ni Norbert (1082-1134), mwanzilishi wa Wapremontree.

Utajiri wa Kanisa[hariri | hariri chanzo]

Kanisa lilikuwa tajiri sana. Makanisa yalijengwa na wakubwa waliotoa baadaye shamba fulani kuwa mradi wa kanisa lile. Ilikuwa kawaida kwa kanisa kumiliki mashamba yenye nia mbalimbali: moja kugharimia matengenezo ya jengo, lingine kumtunza mchungaji au paroko, lingine kumlipa msaidizi wake n.k. Kanisa kubwa lenye watumishi wengi lilikuwa na mapato makubwa. Watu wa vijiji kadhaa walitakiwa kuchanga sehemu ya mavuno yao na kulifanyia kanisa kazi siku mbili kwa juma kama kodi kwa ajili ya gharama za jengo, mapadri kadhaa au askofu.

Mara nyingi zawadi hizo za mashamba au vijiji zilitolewa kama sadaka, ama kama alama ya toba ama kama shukrani. Sadaka za makabaila ziliongeza utajiri wa Kanisa.

Familia za makabaila zilichagua nafasi za uaskofu kwa watoto wao. Mwana wa chifu aliyepokewa katika upadri alizuiliwa kuunda familia na kurithi cheo cha baba, lakini alipanda ngazi ndani ya Kanisa, kupata cheo cha heshima katika jamii na kuwa na mapato makubwa yaliyomwezesha kuishi maisha mazuri na tajiri kama familia yake.

Wakati wa njaa maskini waliweza kupata misaada kanisani, hasa katika nyumba za watawa. Wamonaki waliweza kuwasaidia maskini hata kwa kuuza hazina ya kanisa hata mapambo ya dhahabu yaliyopatikana wakati wa utajiri. Lakini mara nyingi maaskofu walijisikia kuwa wakubwa na wengi wao hawakujali matatizo ya wadogo.

Uhaba wa elimu[hariri | hariri chanzo]

Karne za Kati kule Ulaya zilikuwa kipindi pasipo elimu kwa watu wengi. Kwa jumla utamaduni wa juu wa Kiroma ulikuwa umeanguka chini. Karibu watu wote hawakujua kusoma wala kuandika. Katika nchi nyingi ni watawa tu waliosoma. Tatizo mojawapo lilikuwa uhaba wa vitabu. Mashine za kupiga chapa vitabu hazikujulikana. Maana yake kila kitabu kiliandikwa kwa mkono. Nakala ya Biblia ilihitaji kuandikwa na mtu kwa muda wa mwaka au zaidi. Hivyo vitabu vilikuwa ghali sana. Mtu wa kawaida alishindwa kununua kitabu, hata kama angeweza kusoma. Matokeo yake ni kwamba Wakristo wengi sana hawakuwahi kusoma Biblia.

Zaidi ya hayo Kanisa Katoliki lilitumia popote Biblia katika lugha moja tu, yaani Kilatini, ambacho kilikuwa pia lugha ya ibada zote kwa ajili ya nyimbo, masomo na sala. Kutumia lugha moja popote kulisaidia sana kutunza umoja wa Kanisa. Lakini watu wa kawaida hawakuelewa Kilatini, hata mapadri wengi hawakukielewa vizuri. Kidogo ingekuwa kama kusoma Biblia na kuhubiri katika makanisa ya Afrika kwa Kiingereza au Kifaransa tu.

Hali hii ilisababisha elimu ya Kikristo kuwa chini kati ya waamini wa kawaida. Hivyo walimuona Mungu kama Bwana Mkuu ambaye walipaswa hasa kumtii na kumtumikia kwa hofu, na walijali sana mambo ya pembeni kama vile masalia ya watakatifu. Watu wengi waliona muhimu sana kuhiji kwenye "mahali patakatifu" wakiamini ya kwamba safari za aina hii zinaleta sifa mbele za Mungu. Ilikuwa vema kusafiri ili kusali kwenye kaburi la mtakatifu (k.mf. shahidi aliyekufa kwa ajili ya imani yake zamani), lakini mifano mbalimbali inaonyesha jinsi gani imani ya asili ya ushirikina ilikuwa bado na nguvu baada ya Ukristo kuenea.

Pamoja na hayo, maadhimisho ya sakramenti yalibadilika na pengine kuachwa na waumini wengi, kiasi kwamba Mtaguso IV wa Laterano (1215) uliona haja ya kuwalazimisha wote kupokea kitubio na ekaristi walau mara moja kwa mwaka.

Vita vya msalaba[hariri | hariri chanzo]

Mtawa Petro mkaapweke akihubiri vita vya msalaba mbele ya makabaila wa Ufaransa.

Wakristo waliohiji Yerusalemu kutoka Ulaya walishambuliwa njiani mara kwa mara. Naye Kaisari wa Bizanti aliomba msaada wa Wakristo wa magharibi dhidi ya mashambulio ya Waturuki Waislamu.

Kuanzia mwaka 1095 Wakristo Wakatoliki wa Ulaya walijaribu kuwaondoa Waislamu katika nchi za Mashariki ya Kati. Papa aliwaita mataifa ya Kikatoliki ya Ulaya kuikomboa nchi takatifu. Tangu mwaka 1096 hadi mwaka 1270 kampeni za kijeshi zilianzishwa Ulaya kuelekea Yerusalemu.

Kampeni hizo huitwa "Vita vya msalaba" kwani wanajeshi walipokea kanisani alama ya msalaba wa kitambaa waliobandika juu ya nguo zao. Walifundishwa kuwa vita hivyo ni vitakatifu: atakayekufa atafika mbinguni kwa hakika. Wataalamu wanahisi kama hapo athari za mafundisho ya Kiislamu juu ya "jihadi" zimeingia katika Ukristo.

Mwaka 1099 jeshi la Ulaya lilifika mbele ya kuta za Yerusalemu. Baada ya mapigano mafupi jeshi la msalaba liliwashinda wateteaji Waislamu. Katika hasira ya mapigano waliua ovyo wakazi wengi sana, wazee na watoto, wakiwemo Waislamu, Wakristo na Wayahudi. Mkabaila Mfaransa alipokea cheo cha "Mfalme wa Yerusalemu".

Lakini miaka 100 baadaye Sultani Salah-ed-Din wa Misri aliwafukuza wanamsalaba tena kutoka Yerusalemu. Miaka 40 baadaye alirudisha mji huo kwa hiari baada ya kupatana na Mfalme Mjerumani.

Lakini muda wote huo Wazungu walitawala sehemu ya Palestina na Siria tu. Waislamu waliwaona kama maadui. Hata Wakristo wenyeji (Waorthodoksi) hawakuwakubali kuwa wakombozi kwani walijaribu kuwaunganisha Wakristo wote chini ya Kanisa Katoliki.

Safari moja iliyoondoka Ulaya mwaka 1204 ili kuikomboa Yerusalemu, kumbe ilifika mpaka Bizanti tu ambako wanajeshi wa msalaba waliteka mji, kupora utajiri na kumfukuza Kaisari wa Bizanti. Miaka 100 baadaye Kaisari alirudi na kuunda upya Ufalme wa Roma ya Mashariki.

Mwaka 1291 jeshi la Kiislamu liliwafukuza kabisa wanajeshi wa msalaba katika nchi takatifu wasirudi tena. Lakini kabla ya kuondoka waliwahi kuvunja nguvu ya Bizanti kiasi cha kutosha. Kumbe Ulaya Magharibi iliharibu ulinzi wa dola la mashariki dhidi ya Waturuki waliofaulu baadaye kuingia Ulaya.

Badala ya kufukuzwa, jeshi la Waturuki lilianza kuishambulia Ulaya Kusini-Mashariki. Mwaka 1453 ulianguka mji wa Bizanti, na mwaka 1529 Waturuki walifika mpaka Vienna, mji mkuu wa Mfalme wa Ujerumani. Hapo walirudishwa nyuma, lakini nchi nyingi za Ulaya Kusini-Mashariki pamoja na Wakristo wao walikaa chini ya Waturuki kwa karne tatu zijazo.

Katika karne XII, ambapo baadhi ya Wakristo walipiga vita vya msalaba kuikomboa nchi takatifu, na baadhi walitekwa na Waislamu kuwa watumwa, zilianzishwa aina mpya za watawa ambao washike maisha ya Kiroho pamoja na upanga ili kusindikiza, kukaribisha, kulinda na kutibu waliohiji Yerusalemu, au wajitolee kukomboa watumwa hata kwa kubadilishana nao.

Mt. Yohane wa Matha

Baadhi ya mashirika hayo yanadumu mpaka leo, lakini yamebadili sana malengo na mbinu. Kati ya waanzilishi wakumbukwe Yohane wa Matha (1154-1213) na Petro Nolasco (1180-1249).

ingawa Wafransisko walikabidhiwa patakatifu kadhaa na kuyatunza hadi leo. Wakristo wengi walionyesha imani na uhodari katika mapigano, lakini kulikuwa na ukatili na maonevu mengi pia, vilivyofanywa hasa na wale waliokwenda vitani kwa malengo ya kidunia tu. Vita hivyo vilidhoofisha Wakristo wa Mashariki waliozoea kuishi chini ya Waarabu Waislamu. Kipindi cha vita vya kidini kilisababisha mateso mengi kwa Wakristo Waorthodoksi chini ya Waislamu. Walilipa madeni yaliyoachwa nyuma na ndugu zao kutoka Ulaya Magharibi.

Katika uhusiano mgumu kati ya dini hizo mbili kule Ulaya na Mashariki ya Kati, Waislamu wanastahili pia sifa. Ahadi nyingi walizozifanya zilivunjika, lakini mahali pengi Wakristo walipewa nafasi za kuendelea kuishi kati ya Waislamu hata kama ilikuwa kwa ubaguzi na mateso.

Maisha haya yalikuwa mara nyingi magumu, lakini mahali pengi waliweza kubaki. Waliruhusiwa kuendelea na ibada zao (lakini waliweza kukataliwa kujenga makanisa au hata kutengeneza makanisa ya kale isipokuwa kwa kulipa tena kodi za nyongeza).

Katika mambo ya ndoa au urithi wa mali walikuwa chini ya makanisa yao. Viongozi wa makanisa yao waliwajibika mbele ya serikali ya Kiislamu juu ya ushirikiano mwema. Kwa namna hiyo jumuiya za makanisa kama vile la Kigiriki, la Kikopti, la Kisiria, la Kiarmenia n.k. zilihifadhiwa mpaka leo katika nchi za Kiarabu, isipokuwa idadi ya waumini wao iliendelea kupungua. Sababu kuu ni kwamba kama Mkristo amekuwa Mwislamu hakuweza kurudi tena. Sheria ya Kiislamu inamruhusu Mkristo kugeukia Uislamu, lakini mtu aliyekuwa Mwislamu anastahili adhabu ya kifo akigeukia Ukristo au dini nyingine. Pamoja na hayo Wakristo walianza kuhamia nchi ambako watakuwa raia huru bila kasoro.

Kumbe historia inaonyesha kwamba giza lipo hata upande wa Wakristo. Wakati ule Wakristo wengi walikosa vilevile ustahimilivu kwa watu wenye imani tofauti. Hakuna Mwislamu aliyeweza kubaki katika nchi za Hispania na Ureno baada ya kuvunjwa wa utawala wa Kiarabu.

Inatosha kulinganisha hali ya Waislamu kule Hispania. Sehemu kubwa ya Hispania ilikuwa miaka mamia chini ya utawala wa Waarabu Waislamu. Katika vita vingi mfululizo Wahispania waliteka nchi yao tena. Mwaka 1492 mfalme wa mwisho Mwislamu alishindwa. Waislamu wakaishi chini ya utawala wa Wahispania Wakatoliki. Lakini miaka michache baadaye Waislamu wote walilazimishwa wapokee ubatizo, wengine waliuawa au kufukuzwa.

Bila shaka hayo ni matokeo ya hali ya vita kati ya Waislamu na Wakristo. Wahispania walionyesha tabia zinazofanana na zile za Wamongolia Waislamu walioharibu makanisa yote ya Asia ya Kati.

Lakini ipo mifano mingine: Wakristo wote walifyekwa Uarabuni kwenyewe kumbe Waislamu waliweza kubaki chini ya Waaustria Wakristo waliotawala nchi za Ulaya Kusini-Mashariki. Kweli kati ya dini hizo mbili hakuna anayeweza kujisifu tu juu ya historia ya dini yake bila kukiri makosa na kasoro pia.

Ugandamizaji wa wazushi[hariri | hariri chanzo]

Papa Inosenti III ndiye aliyefikisha Upapa hadi kilele cha mamlaka zote Ulaya.

Serikali ziliona ni lazima kutetea umoja wa Kanisa. Hivyo viongozi wa Kanisa walishawishika kutumia nguvu ya serikali kuhakikisha uongozi wao ufuatwe. Ikiwa walijitokeza Wakristo waliodai mabadiliko au kupinga uongozi wa Kanisa, serikali iliingilia kati na kuwagandamiza kama "wazushi". Ilikuwa hasa utajiri wa Kanisa na wa maaskofu wengi uliosababisha ugomvi.

Katika karne ya 13 Ufaransa alijitokeza mfanyabiashara Petro Waldo aliyesikia wito wa Kristo katika maisha yake. Aliwapa maskini mali yake yote akaanza maisha ya kuhubiri akijaribu kumwiga Bwana Yesu.

Akafundisha ya kwamba Mkristo wa kweli anapaswa kumfuata Yesu hata katika maisha ya umaskini. Akauliza: mbona Kristo alikuwa maskini, lakini maaskofu wa leo ni matajiri? Wafuasi wake kwanza waliruhusiwa, halafu wakaanza kukutana nje ya makanisa. Kanisa liliwatangaza kuwa wazushi wakatafutwa na kukamatwa na serikali. Wengine wakafungwa gerezani, wengine wakauawa.

Baadaye ilikuwa kawaida kuweka "wazushi" mbele ya mahakama za pekee na hata kuwachoma moto. Papa Inosenti III akaunda idara ya pekee "Baraza la Ulinzi wa Imani". Ofisi hiyo ilikuwa na kazi ya kuwatafuta "wazushi" na kuwahoji juu ya imani zao. Wakionekana kuwa na makosa wasitake kutubu walikabidhiwa mikononi mwa serikali iliyotoa adhabu ya kifo. Hata hivyo mawazo yao yaliendelea kuzunguka kati ya watu wa kawaida. Wawaldo walihubiri kwa siri katika nchi nyingi.

Fransisko na tapo la mafukara[hariri | hariri chanzo]

Mchoro wa zamani wa Fransisko wa Asizi unaoaminiwa kufanana naye kuliko yote.

Kama kawaida bidii kwa urekebisho wa Kanisa zilifanikiwa kiasi tu: hasa walei hawakuridhika na wengine walianza kukata tamaa juu ya hali ya Kanisa.

Pia hija na vita vya msalaba vilifanya wengi wajionee nchi ya Yesu na hivyo kuvutiwa upya na maisha yake. Ndiyo sababu walistawisha mifumo mbalimbali ya Kiinjili na kulenga maisha ya Kanisa la mwanzoni.

Dhidi ya mwenendo wa mapadri na wamonaki, walisisitiza ufukara na unyofu hata wengi walifikia hatua ya kuliasi Kanisa. Ulikuwa wakati wa utajiri kuzidi hata kufanya watu kadhaa waukinai.

Katika matatizo hayo Mungu aliita watu wairudishe upya roho ya Injili. Hivyo katika karne XIII yalianzishwa mashirika mbalimbali (hasa Wafransisko na Wadominiko, lakini pia Waaugustino, Wakarmeli na Watumishi wa Maria) yaliyoitwa ya ombaomba kwa jinsi yalivyokaza ufukara.

Fransisko wa Asizi alizaliwa katika familia tajiri akawa kijana aliyependa sana muziki na sherehe. Vitani alifungwa mwaka mmoja akaanza kumtafuta Mungu.

Siku moja aliposali akasikia sauti, "nenda ukatengeneze Kanisa langu linalotaka kubomoka". Basi, akachukua pesa akaanza kutengeneza kanisa dogo lililokuwa bovu sana. Baba yake akakasirika akiona kijana anapoteza mali ya familia. Fransisko akakutana na baba mbele ya Askofu uwanjani akavua nguo zake na kumrudishia baba pamoja na pesa zakeː "Kuanzia sasa nitasema tu, Baba yetu uliye mbinguni".

Fransisko akaishi maisha kama mtawa akimwomba Mungu amwonyeshe njia. Siku moja kanisani alisikia somo la Mathayo 10:7-20, akajua: Hiyo ndiyo njia yangu! Alielewa maana yake "ukatengeneze Kanisa langu": kwamba si jengo lile dogo alipoanzia, lakini Kanisa la Kristo lililobomolewa kwa sababu ya ujumbe wa Injili kusahauliwa.

Alianza maisha ya ufukara akijaribu kuiga mfano wa Yesu. Akazunguka akivaa kanzu ya gunia na kuhubiri upendo wa Mungu. Vijana wengine wakamfuata wakaunda utaratibu wa maisha ya pamoja.

Fransisko akaona ya kwamba nyumba za wamonaki zilikuwa tajiri sana (mmonaki mwenyewe hakuwa na mali, lakini jumuiya yake iliweza kuwa tajiri). Kwa wafuasi wake alikataza jumuiya zisiwe na mali.

Fransisko alipendwa sana kwani alionyesha imani na furaha katika Kristo na upendo kwa watu wote. Mwenyewe alisafiri mpaka Afrika akahubiri mbele ya Sultani wa Misri. Ingawa wakati ule vita vilikuwa vinaendelea kati ya jeshi la Kikatoliki la Ulaya na Waislamu, Sultani alimpokea kwa heshima, akamsikiliza na kumruhusu kurudi kwake.

Fransisko aliamini ya kwamba majaribio yote ya kuwashinda Waislamu kwa silaha ni ya bure. Kwa Mkristo hakuna njia nyingine kuliko mfano wa Bwana Yesu, yaani upendo na unyenyekevu.

Mfumo wa Wafransisko ulienea haraka sana. Ndugu hao walitembea popote wamevaa usiku na mchana kanzu ileile na kupewa chakula kutoka kwa Wakristo wa kawaida. Tofauti na wamonaki, wakaishi kati ya watu wakihubiri na kufundisha. Walikuwa mfano wa kumtegemea Mungu kabisa katika umaskini kwani hawakuwa na mali wala mapato kuliko sadaka za hiari kutoka kwa Wakristo.

Katika maisha hayo walifanana na vikundi kama Wawaldo lakini wakawafundisha Wakristo kufuata uongozi wa Kanisa na maaskofu. Hivyo Wafransisko walikuwa silaha muhimu ya Kanisa Katoliki dhidi ya waliopinga utajiri wake. Mahali pengi Wakristo wa kawaida wakajiunga na jumuiya za kiroho zilizokuwa chini ya ulezi wa Wafransisko.

Dominiko wa Guzmán, mwanzilishi wa Shirika la Ndugu Wahubiri.

Muda uleule Mhispania kwa jina Dominiko Guzman (1170-1221) aliunda shirika la watawa. Kusudi lake lilikuwa kuhubiri. Akiwa padri aliguswa na uenezi wa uzushi akajitahidi kutatua tatizo hilo. Ili akubaliwe na watu wote kama mhubiri halisi wa Injili alishika ufukara wa Yesu na mitume wake: kwenda wawiliwawili, kwa miguu, bila ya kuchukua chochote kwa safari. Hivyo aliliandalia Kanisa kundi la watu wanaofanya kazi ya kuhubiri, ambayo awali ilikuwa maalumu ya maaskofu. Kwa lengo hilo utawa wake ulipunguza miundo ya kimonaki na urefu wa liturujia ili kuacha nafasi ya kusoma na kusali zaidi mmojammoja: hivyo ndugu wahubiri watajipatia ukweli ambao wawashirikishe wengine kwa kuhubiri na kufundisha. Ndio utume unaolingana zaidi na maisha ya sala na kusoma.

Wafransisko na Wadominiko walinyosha kiasi kasoro za kukosa mahubiri katika Misa ya kawaida. Walifanya kazi muhimu sana ya kuwafundisha watu wadogo waliokuwa maskini na bila elimu wala uwezo wa kusoma. Baadaye Wadominiko waliogopwa pia kwa kazi ya kutafuta na kushtaki walioitwa "wazushi".

Watawa wa kike hawakuweza kufuata mtindo uleule: waliishi kimonaki lakini kwa kuzingatia ufukara na udugu wa Kifransisko na kwa kuombea utume wa hao ndugu wadogo. Klara wa Asizi (1193-1253), “mche mdogo” wa Fransisko, ndiye mwanamke wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa. Tapo hilo ni maarufu kwa marekebisho yaliyofuatana hadi leo kuhusu ufukara.

Giovanni di Paolo, "Mt. Katerina wa Siena", 1475 hivi. Fogg Art Museum, Cambridge, Uingereza.

Tangu karne XII wanawake wengine pia walichangia sana ustawi wa utawa, wa maisha ya Kiroho na wa Kanisa kwa jumla hata kwa maandishi yao. Kati yao Katerina wa Siena (1347-1380), wa utawa wa tatu wa Mt. Dominiko, ametangazwa kuwa mwalimu wa Kanisa.

Kuanzia karne XIII zilijitokeza pia jumuia nyingine ambazo pengine zinahusiana na mashirika ya kitawa (yaani za Utawa wa Tatu), lakini hazina nadhiri au si za hadhara. Kwa kuenea, zikaja kuwa na muundo kama wa mashirika (1401), ingawa kwa kawaida ya kwao yalikuwa na jumuia za kiume na za kike ndani yake.

Baada ya upinzani mwingi, wanawake wakaja kukubaliwa wafanye utume na kuanzisha mashirika yasiyobanwa na ugo. Kwa namna ya pekee Anjela Merici (1474-1540) alitaka wafuasi wake waishi na kutumikia kati ya watu; baada ya karne nne shirika lake likakubaliwa kutambulika kuwa la kilimwengu.

Upande wa wanaume Filipo Neri (1515-1595) ndiye maarufu zaidi kati ya walioanzisha jumuia ambapo watu wanaishi pamoja ili kujipatia malezi na kufanya utume fulani, lakini bila ya kuwekwa wakfu.

Farakano la Magharibi[hariri | hariri chanzo]

Wengi wanaona karne ya 13 kuwa kilele cha matunda wa Kanisa Katoliki katika kulea upya Ulaya magharibi kwa kuzaa hasa mashirika ya ombaomba ya Fransisko wa Asizi na Dominiko Guzman, mitindo mipya ya sanaa, pamoja na vyuo vikuu walipostawi walimu wa Kanisa kama Thoma wa Akwino na Bonaventura.

Lakini utaifa, uliotokea Ulaya magharibi kuanzia ufalme wa Ufaransa katika karne ya 14, ulivuruga umoja wa Kanisa na matatizo yalionekana mpaka ngazi ya Upapa. Mara nyingi Papa mpya (Askofu wa Roma) alichaguliwa kufuatana na ukoo au sifa za kisiasa tu. Cheo cha Papa kiliingizwa katika siasa kubwa kati ya wafalme wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa.

Mwaka 1300 Papa Bonifas VIII alidai kuwa na madaraka juu ya wafalme wote. Mfalme wa Ufaransa alikasirika akataka kulipiza kisasi.

Migongano hii ilisababisha tatizo la Mapapa kwenda kukaa miaka 68 (1309-1377) huko Avinyon (leo nchini Ufaransa) badala ya kuongoza mjini Roma. Aliyefaulu kumrudisha Papa katika jimbo lake hilo ni Katerina wa Siena, bikira mwenye karama ya unabii.

Lakini baada ya muda mfupi makardinali waliofanya uchaguzi wa Papa mpya walisababisha farakano ndani ya Kanisa lililoendelea kwa muda wa karibu miaka 40 (1378-1417). Katika hilo Farakano la Kanisa la Magharibi, baadhi ya maaskofu na waamini wengine walimfuata Papa wa Roma na baadhi Antipapa wa Avignon wakidhani ndiye Papa wa kweli.

Hali ilizidi kuwa mbaya: mwaka 1409 walikuwepo watu watatu waliojiita "Papa" na kukubaliwa na sehemu ya maaskofu. Maaskofu na Wakristo walichoka sana farakano hilo. Mwaka 1417 Mtaguso mkuu wa Konstanz (Ujerumani) ulifaulu kuwaondoa wote watatu na kumchagua Papa mpya, Martin V.

Farakano la magharibi liliisha kwa Mtaguso wa Konstanz. Viongozi mbalimbali wakajitahidi kufuta maovu ndani ya Kanisa lakini hawakufaulu sana. Walikuwepo watu wakubwa wengi mno waliofaidika na hali halisi.

Nyumba za wamonaki zilienea sana, pia kwa sababu ilikuwa kawaida kupeleka utawani watoto wasioweza kurithi.

Cheo cha uaskofu kilikuwa nafasi iliyotafutwa sana na familia za makabaila kwa ajili ya wanao wasioweza kurithi cheo cha baba. Uaskofu ulipatikana mara nyingi kwa njia ya kuwahonga wenye haki ya kumchagua au kumthibitisha askofu. Viongozi wa Kanisa katika eneo fulani walipokea hela kabla ya kumchagua askofu mpya. Papa wa Roma alidai hela kabla ya kumthibitisha askofu yeyote aliyechaguliwa. Mfalme alidai hela kabla ya kumkabidhi askofu madaraka ya kiserikali katika eneo lake.

Lakini malipo hayo yote yalifidiwa tena na watu wa kawaida, wakulima na wafanyabiashara wa eneo hilo waliopaswa kumlipa askofu kodi zao kila mwaka.

Maaskofu wengine walianguka kabisa wakitumia hela zao katika vita dhidi ya majirani wao, kwa ujenzi wa maboma na makanisa uliopita uwezo wao, au kwa maisha ya ulevi na uasherati. Askofu alikataliwa kuoa lakini wengi walikuwa na wapenzi wao na kuwajengea nyumba kubwa pamoja na watoto wao.

Wakristo wengi wakasikitika juu ya hali hii. Mapapa mbalimbali walijaribu kusimamisha maovu hayo lakini bila mafanikio makubwa.

Yohane Hus na Umoja wa Ndugu[hariri | hariri chanzo]

Padri Yohane Hus alikuwa mwalimu wa teolojia kwenye Chuo Kikuu. Mwaka 1412 alihubiri kwa nguvu sana kule Praha (leo mji mkuu wa Ucheki), akafundisha ya kwamba mamlaka kuu Kanisani ni katika Biblia si katika maamuzi ya maaskofu au Papa.

Maaskofu wakamtangaza kuwa mzushi. Alishtakiwa mbele ya mfalme lakini wengi walimfuata. Akahifadhiwa na kufichwa na kabaila katika boma lake.

Miaka 1414-1418 kulikuwa na Mtaguso mkuu wa Kanisa Katoliki kule Konstanz, Ujerumani. Hus akaitwa kujitetea mbele ya mkutano huo, akaahidiwa ulinzi wa mfalme, yaani kwamba ataweza kurudi tena hata akionekana kuwa mzushi. Lakini kinyume cha ahadi alikamatwa akahukumiwa kuwa mwasi na mzushi, akachomwa moto akiwa hai.

Wafuasi wake katika mikoa ya Bohemia na Moravia (leo Ucheki) wakasikitika mno. Wengine wakachukua silaha wakataka kutenga nchi yao kutoka uongozi wa Kanisa.

Vita vya miaka mingi vilianza kati ya Wahus na askari wa mfalme na maaskofu. Alama ya Wahus ilikuwa kikombe cha Ekaristi kwani Hus alifundisha ya kwamba Wakristo wote wanapaswa kupokea kikombe kanisani (katika karne XII Kanisa Katoliki lilianza desturi ya kutoa kikombe kwa mapadri tu).

Mwishoni Ukristo wa Bohemia na Moravia uligawanyika. Wahus wakali waliojaribu kuunda utaratibu wa kisiasa juu ya mahubiri ya Yesu na kuwalazimisha wote kuufuata kwa silaha wakashindwa. Wengine wakafuata Wahus wasio wakali waliopatana na wakubwa wa nchi. Wengine wakabaki ndani ya Kanisa Katoliki, wakaruhusiwa kuwa na ibada ya Misa (chakula cha Bwana) wakipokea sakramenti katika maumbo ya mkate na divai.

Mwaka 1457 kikundi kidogo cha wafuasi wa Hus waliochoka uuaji na vita vya kidini walianzisha jumuiya ya Kikristo iliyoitwa "Umoja wa Ndugu", wakajaribu kuishi kama ndugu wakikaa pamoja, kufanya kazi na kusali pamoja. Mwanzoni hawakupokea matajiri waliotaka kujiunga nao.

Mbinu hii ilifanana na watawa aina ya Wafransisko lakini walikuwa jumuiya ya watu wenye ndoa na watoto. Waliona muhimu wasiwe na taratibu za utawala katika Kanisa, lakini viongozi wawe kama ndugu na watumishi wa wengine. Hawakutaka kumlazimisha yeyote katika mambo ya imani kama ilivyokuwa katika maeneo ya Wakatoliki na ya Wahus wengine.

Mwanzoni walihudumiwa kiroho na mapadri wa Kanisa Katoliki, lakini mwaka 1467 waliamua kuchagua watumishi wao wenyewe, wakiwemo mpaka leo mashemasi, makasisi na maaskofu. Umoja huo ulienea Bohemia na Moravia ukawa chanzo cha madhehebu ambayo yalistawi upya kuanzia mwaka 1722 na yanaitwa ya "Wamoravia" (leo wengi wao wanaishi nchini Tanzania).

Mwisho wa Karne za Kati[hariri | hariri chanzo]

Karne za 15 na 16 zilikuwa muhimu katika historia ya Ukristo.

Huko Asia ya Kati jeshi la Wamongolia Waislamu chini ya kiongozi Timur liliteka na kuharibu nchi nyingi. Makanisa yalichomwa moto popote Asia ya Kati na Uajemi mpaka Palestina. (Wakaharibu vilevile nyumba za dini nyingine kama Wabuddha au Wahindu).

Mwaka 1453 mji mkubwa wa Bizanti ukatekwa na jeshi la Waturuki Waislamu. Ulikuwa mwisho wa Dola la Roma lilivyoendelea katika eneo la mashariki. Tangu muda ule Wakristo wote wa Mashariki ya Kati wameishi chini ya Waislamu.

Waturuki wakaendelea kuingia Ulaya ya Kusini-Mashariki. Kwa muda wakatawala eneo la nchi za Ugiriki, Bulgaria, Romania, Masedonia, Serbia, Albania, Montenegro na Hungaria za leo. Ukristo wa Kiorthodoksi ulibaki huru katika nchi za Urusi na Ethiopia tu.

Lakini Hispania wafalme Wakatoliki walifaulu kuwafukuza Waarabu kutoka rasi ile. Tangu mwaka 711 hadi 1491 sehemu za Hispania na Ureno zilikuwa chini ya Waarabu Waislamu. Baadhi ya wenyeji walisilimu.

Kumbe 1491 mji wa mwisho uliotawaliwa na Waarabu ulitekwa, na mfalme wake akakimbilia Moroko. Wakristo wa nchi hizo walichukua nafasi ya kulipiza kisasi kwa mateso yote ya nyuma. Waislamu waliobaki walilazimishwa kubatizwa, wengine waliuawa.

Ingawa uhusiano kati ya mataifa ya Waislamu na ya Wakristo ulikuwa mgumu yaliendelea kufanya biashara. Kwa jumla Waarabu walikuwa na ujuzi zaidi katika mambo ya elimu na ufundi. Vilevile walifaulu sana katika biashara. Ni Waarabu walionunua bidhaa kule India na kuzipeleka mpaka Italia.

Wazungu walisikitikia sana bei kubwa ya bidhaa hizo na hasa faida kubwa ya wafanyabiashara Waislamu lakini wakazinunua kwani wenyewe walishindwa kuzitengeneza.

Katika kipindi kilekile mawazo mapya yalienea duniani. Anguko la Bizanti mwaka 1453 lilisababisha wasomi wengi wa mashariki kukimbilia Ulaya Magharibi wakileta vitabu vyao. Wataalamu walianza kusoma tena vitabu vya Wagiriki na Waroma wa kale. Elimu ilisonga mbele. Hasa mijini shule ziliundwa.

Mjerumani kwa jina Gutenberg alitengeneza mashine ya kwanza ya kupiga chapa vitabu. Hivyo vitabu vilianza kupatikana kwa urahisi. Habari zikazunguka haraka kati ya nchi na nchi, hali isiyojulikana karne nyingi tangu anguko la Dola la Roma.

Yakaanza kusambaa tena mafundisho ya kale kuwa dunia si tambarare lakini mviringo kama chungwa. Alijitokeza nahodha Mwitalia kwa jina Kristoforo Kolombo aliyetaka kujaribisha mafundisho hayo. Ikiwa dunia kweli ina umbo la chungwa inawezekana kuelekea magharibi kutoka Hispania na kufika mashariki katika Bara Hindi. Kwa njia hiyo inawezekana kufanya biashara moja kwa moja na nchi tajiri za mashariki bila kuwapa faida wafanyabiashara Waarabu. Mfalme wa Hispania akampa Kolombo fedha za kuandaa meli tatu.

Mwaka 1492 Kolombo akaondoka Hispania akakuta bara jipya magharibi lililoitwa baadaye Amerika. (Mwenyewe alifikiri amefika Bara Hindi, hivyo akawaita wenyeji "Wahindi" na visiwa alipofika mwanzoni mpaka leo huitwa "West Indies" = India Magharibi).

Wahispania walipora utajiri wa mataifa ya Amerika yaliyokosa silaha za kushindana nao. Utajiri huo mpya ulisaidia maendeleo ya Ulaya kupiku yale ya mataifa ya Waislamu na ya Asia.

Urekebisho wa Kikatoliki na Matengenezo ya Kiprotestanti[hariri | hariri chanzo]

Martin Luther mwenye umri wa miaka 46.

Umoja halisi wa Kanisa unaweza kupatikana tu katika ukweli wa Injili ya Yesu Kristo. Ni habari mbaya kwamba katika karne ya 16 kuupigania ukweli huo kulivunja umoja wa Ukristo wa magharibi. Haiwezekani kushangilia mafarakano ya wafuasi wa Yesu.

Yale ya karne hiyo yalitokana na kuelewa tofauti kweli za imani ya Kikristo na yalikuwa na ukali kwa sababu pande zote zilisadiki kwamba kushikilia kwa usahihi ufunuo wa Mungu ni suala la wokovu wa milele. Kwa mfano, Martin Luther aliandika, «Sikubali mafundisho yangu yahukumiwe na yeyote, hata kama ni malaika. Asiyekubali mafundisho yangu hawezi kufikia wokovu».[1]

Pamoja na hayo, mambo mengi yalichangia farakano, si teolojia tu, bali siasa, uchumi, jamii na utamaduni. Wakati huo mara nyingi hoja za imani na malengo ya kisiasa vilichanganyikana: wanasiasa wengi walitumia hoja hizo ili kufikia malengo ya kiutawala, na vilevile wanateolojia walitumia siasa kutetea mafundisho yao ili kuvuta watu. Ndiyo sababu Luther alichorwa kama shujaa wa taifa la Ujerumani.

Mara nyingi pande zote zilipotosha maana ya wapinzani na kuwachora vibaya wakivunja amri ya nane inayokataza uongo dhidi ya jirani. Hata waliojitahidi kusema ukweli tu juu ya wengine kwa kawaida hawakujitahidi vya kutosha kuelewa msimamo wao na kuona kwamba pengine si mbaya zaidi. Kila mmoja alitaka ushindi akachangia ugomvi uliorithishwa kwa vizazi vilivyofuata.

Hivyo, kilichosababisha zaidi farakano si masuala ya imani yaliyojadiliwa na Waprotestanti, bali lawama zao dhidi ya hali mbaya ya Kanisa la wakati huo iliyokuwa inakera wengi na kuwaelekeza kuunga mkono urekebisho.

Hapo kale neno hilo (kwa Kilatini reformatio) lilihusu badiliko la hali mbaya iliyopo ili kurudia hali nzuri zaidi ya awali. Katika Karne za Kati lilitumika mara nyingi kwa marekebisho ya umonaki.

Katika karne ya 15 haja ya urekebisho ilionekana wazi si tu kwa mashirika ya kitawa bali kwa Kanisa lote. Hasa Mtaguso wa Konstanz (1414-1418) ulidai kabisa ufanyike «katika kichwa na katika viungo». Lakini kwa jumla mitaguso yote ya Karne za Kati na mikutano mingi ya Bunge la Dola la Ujerumani ililenga urekebisho wa Kanisa.

Kwa kweli Karne za Kati zilikuwa na mchanganyiko wa mambo yaliyopingana: ibada za nje tu na za dhati kabisa; teolojia iliyoelekeza kutenda kwa msingi wa nipe nikupe na hakika ya kwamba binadamu anategemea kabisa neema ya Mungu; kutojali wajibu hata upande wa viongozi wa Kanisa na marekebisho safi ya mashirika ya kitawa.

Karne XV ilikuwa kipindi cha umotomoto wa pekee katika Kanisa, ambapo walei wengi zaidi na zaidi walipata elimu nzuri, hivyo walitamani hotuba bora na mafundisho ya kuwasaidia kuishi Kikristo zaidi. Luther aliitikia haja hizo zilizomgusa sana kama mtu wa wakati wake.

Mwenyewe alitumia kwa nadra neno urekebisho, lakini likaja kuwa jina la kawaida la matukio yale mengi ya miaka 1517 - 1555, yaani kuanzia uenezi wa hoja 95 za Martin Luther hadi amani ya Augsburg. Kati yake mabishano ya Kikanisa yaliyosababishwa na teolojia ya Luther, yalichanganyikana mapema na siasa, uchumi na utamaduni, kutokana na hali halisi ya wakati huo, mbali kuliko mwenyewe alivyofikiri.

Viongozi Wakatoliki, yaani Papa na Mfalme mkuu wa Ujerumani, waliona kwa masikitiko kutokea kwa mafarakano lakini mawazo yao yalitekwa na shughuli nyingi za siasa na vita hata wakatumia nguvu zao kushindana kati yao.

Mwanzoni walimwona Luther kuwa padri mdogo tu apaswaye kurudishwa kwenye njia iliyo halali. Papa Leo X hakuona umuhimu mkubwa katika habari zake: mwaka 1521 akamtenga Luther katika Kanisa, halafu akapokea habari za Bunge la Ujerumani lililomhukumu Luther kuwa mzushi na adui wa taifa.

Miaka 1522/1523 akafuata Papa Adriano VI: akiona uenezaji wa haraka wa mafundisho ya Luther kila mahali akakiri Kanisa lilikuwa na makosa. Lakini uongozi wake ulidumu muda mfupi mno.

Papa Klementi VII aliyefuata hakuwa na mawazo ya kiroho, akashughulikia zaidi siasa akipigana vita na Mfalme juu ya kutawala mikoa mbalimbali ya Italia.

Mwaka 1527 jeshi la Mfalme liliteka Roma, Papa akakimbia. Walipatana mwaka 1529 lakini mwaka uleule Waturuki Waislamu walifika mbele ya mji mkuu wa mfalme, Vienna. Kwa shida tu jeshi la Wakristo liliwashinda.

Mfalme Karolo V wa Ujerumani alikuwa pia Mfalme wa Hispania. Mwaka 1521 jeshi la Wahispania liliteka Meksiko, baadaye Peru katika Amerika Kusini. Dhahabu na fedha za huko zilianza kuletwa Hispania. Mfalme hakuwa na muda wala nguvu kushindana na sehemu kubwa ya makabaila wa Ujerumani waliomuunga mkono Luther.

Kivulini mwa matokeo hayo mafundisho ya Waprotestanti yalienea haraka pande nyingi za Ulaya. Kuanzia mwaka 1530 ilikuwa wazi kwamba farakano limetokea, likitenga na Papa sehemu kubwa ya Ulaya Kaskazini pamoja na matengenezo yenyewe kuvunjikavunjika katika madhehebu mbalimbali.

Sasa sauti ya wale waliodai urekebisho ndani ya Kanisa Katoliki ilisikika zaidi. Papa Paulo III akachukua hatua mbili: kwanza aliandaa mtaguso wa maaskofu wote halafu aliimarisha Baraza la Ulinzi wa Imani. Ofisi hiyo ilikuwa na kazi ya kufuatilia habari zote za upinzani dhidi ya Kanisa Katoliki na kuomba serikali zilizokuwa mikononi mwa Wakatoliki kugandamiza wote waliotaka kufuata mafundisho ya Luther na wenzake.

Baraza hilo lilikuwa na nguvu sana: kwa jumla lilifaulu kufuta vikundi vyote vya Wainjili katika nchi kama Italia, Ureno na Hispania. Lakini ugandamizaji huo uliongeza uchungu kati ya madhehebu ukasababisha ugandamizaji wa Wakatoliki katika maeneo ya Walutheri na ya Wareformati.

Chombo kingine kilikuwa "Orodha ya vitabu vilivyopigwa marufuku" kwa kila Mkatoliki asivisome, navyo havikuruhusiwa katika nchi katoliki. Orodha hiyo ilifutwa rasmi na Papa Paulo VI mwaka 1965.

Ignas wa Loyola, mwanzilishi wa Shirika la Yesu, alivyochorwa na Peter Paul Rubens.

Chombo kingine muhimu zaidi cha urekebisho wa Kikatoliki kilikuwa Shirika la Yesu, jumuia ya mapadri iliyoongozwa na "Jenerali" wake akitumia nidhamu ya kijeshi.

Mwanzilishi wake ni Ignas wa Loyola, Mhispania ambaye alikuwa mwanajeshi. Mwaka 1521 alijeruhiwa vibaya vitani. Alipokaa hospitalini muda mrefu akasikia wito wa Mungu uliobadilisha maisha yake.

Kisha kuacha jeshi, akamtolea Bikira Maria upanga wake akawa "Mwanajeshi wa Kiroho". Alifuata kwa juhudi zote maisha ya kiroho na kutunga Mazoezi ya Kiroho ili kuongoza watu wamfuate Yesu Kristo.

Mwaka 1534, Ignas alikusanya vijana sita wakaweka nadhiri za ufukara, useja mtakatifu na utiifu, halafu ile ya kumtii daima Papa.

Kisha kusoma teolojia akapadrishwa. Akakusanya kikundi cha marafiki akiwaongoza kujenga maisha ya kiroho kwa njia ya mazoezi ya pekee. Wote walifuata utaratibu uleule. Kila mwaka walikutana kwa kipindi cha sala, kutafakari na kusoma kilichofuata hatua au mbinu maalumu. Wengi walianza kumfuata na chama chake kikakubaliwa na Papa mwaka 1540.

Shabaha kuu ilikuwa kutetea Kanisa chini ya Papa.

Kila mwanachama alitakiwa kuwa na elimu ya juu. Hivyo Kanisa Katoliki liliimarika katika teolojia, jambo lililowahi kukazwa zaidi na Waprotestanti.

Mapadri Wajesuiti walifanya hasa kazi ya ualimu wakiunda shule na kufundisha vijana elimu pamoja na upendo kwa Kanisa Katoliki.

Mkazo mwingine ulikuwa kufufua utaratibu wa maungamo. Popote Ulaya Wajesuiti walikuwa washauri hasa wa watawala Wakatoliki. Waliposikiliza ungamo la dhambi zao walipata nafasi nzuri ya kuwapa mawazo na kusababisha hatua za serikali dhidi ya Waprotestanti.

Hivyo kwa athari ya Wajesuiti polepole Uprotestanti ulirudi nyuma katika nchi za Ulaya ambako wakazi wengi walikuwa wameanza kufuata mafundisho ya Martin Luther na Calvin lakini watawala walikuwa bado Wakatoliki.

Mbali nao, mashirika mengine yalifanya kazi kubwa ya kuzuia uenezi wa Uprotestanti, kuanzia Wafransisko waliowahi kutambua hatari kabla ya viongozi wa Kanisa. Baadaye ulikuwa hasa urekebisho wa Wakapuchini uliorudisha wengi katika Kanisa Katoliki kwa upole, usikivu na ushuhuda wa maisha safi yenye kujitosa.

Miaka 1545-1563 maaskofu wa Kanisa Katoliki walikutana Trento, Italia kaskazini, wakajadiliana juu ya mafundisho na hali ya Kanisa, wakachukua hatua za kuondoa matatizo na kuimarisha imani. Maazimio yake makuu yalibaki muhimu mpaka karne ya 20:

  • a) Msingi wa imani ni Biblia pamoja na mapokeo ya Kanisa.
  • b) Sakramenti ziko saba.
  • c) Juu ya kuhesabiwa haki (jinsi ya kupata wokovu) ni kwamba mwanadamu hahesabiwi haki kwa sababu ya matendo yake mema bali kwa neema ya Mungu, lakini lazima mwanadamu ashiriki katika kupokea na kutumia neema hiyo.
  • d) Kanisa peke yake lina mamlaka ya kueleza maana ya Biblia; Mkristo asijisomee bila mwongozo wa Kanisa; toleo pekee la Biblia linalofaa ni lile linalotolewa na Kanisa Katoliki katika lugha ya Kilatini (lililoitwa "Vulgata" - pamoja na vitabu vya "Deuterokanoni" vilivyotengwa na Luther).
  • e) Kufuta maovu katika Kanisa: kampeni za kuuza vyeti vya rehema, malipo ya maaskofu kwa Papa ili awathibitishie cheo, askofu kuwa na majimbo zaidi ya moja (walivyofanya zamani kwa sababu ya mapato).
  • f) Mapadri wawe na elimu, wote wapitie masomo ya seminari, kila mmoja afuate utaratibu wa kusoma Biblia kila siku, mahubiri yawepo katika kila Misa ya Jumapili.
  • g) Itungwe Katekisimu ya kwanza ya Kanisa Katoliki, pamoja na vitabu vipya vya liturujia.

Kwa jumla Mtaguso wa Trento ulishindwa kuwavuta Wainjili warudi, lakini uliendeleza urekebisho wa Kanisa Katoliki. Katika nchi zilizobaki chini ya Roma Kanisa lilipata nguvu tena kwa kuimarisha mafundisho ya kale pamoja na kuondoa kasoro mbalimbali. Hata hivyo haikuwezekana kufuta farakano lililotokea tayari.

Vita kati ya madhehebu ya Kikristo[hariri | hariri chanzo]

Karolo V vitani alivyochorwa na Tiziano (1548) ili kuadhimisha ushindi wake katika mapigano ya Mühlberg.

Karolo V, Kaisari wa Dola Takatifu la Kiroma, aliendesha Vita vya Schmalkald (1546-1547) dhidi ya maeneo ya Walutheri yaliyokuwa ndani ya dola hilo kubwa la Ujerumani.

Lengo lake lilikuwa kuwalazimisha watawala wadogo waliowaunga mkono Walutheri wafute matengenezo yote.

Mwanzoni alishinda (20 Julai 1547); kwenye Bunge la Augsburg (1547-1548) alidai Walutheri wakubali kuwa chini ya maaskofu na Papa wa Kanisa Katoliki. Ingawa aliruhusu ndoa ya mapadri na kupokea ekaristi kwa maumbo yote mawili (mkate na divai), maitikio hayakuwa mazuri hata kidogo: kukawa na vurugu kubwa.

Mwaka 1552, baada ya njama ya watawala hao dhidi ya Karolo V, vilianza tena vita ambavyo vilimlazimisha kukimbia Austria. Hatimaye watawala Walutheri walipatana na mwanae, mfalme Ferdinand III. Hivyo jaribio la kufuta Ulutheri kijeshi lilishindikana kabisa.

Vita vilimalizika mwaka 1555 kwa amani ya Augsburg. Mapatano hayo yalilenga kuwezesha wananchi wenye imani tofauti waishi katika taifa lilelile. Watawala walipewa haki ya kuwachagulia madhehebu ya dini raia wao. Wasiokubali kufuata imani ya mtawala, walipewa tu haki ya kuhamia eneo lingine ambapo mtawala wake alikuwa na imani yao.

Hivyo katika Dola la Kijerumani yalikubalika rasmi maeneo yaliyoshikilia Ungamo la Augsburg na yale yaliyobaki katika Kanisa Katoliki, lakini si wenye imani tofauti na hizo mbili, kama vile Wareformati na Waanabaptisti.

Amani ya Augsburg kwanza ilifaulu kuleta mahusiano imara upande wa siasa, lakini baadaye haikuweza kuzuia mlipuko wa vita vikali vya karne XVII: vita vya miaka 30 (1618-1648).

Madola ya Ujerumani yalipigana kati yao, na nchi za nje zilishiriki zikiwemo Hispania, Ufaransa, Uswidi, Uholanzi na Denmark, lakini mapigano yake yalitokea hasa katika Ujerumani kwenye eneo la Dola Takatifu la Kiroma.

Ni kwamba uhusiano kati ya madhehebu ya Kikristo ulikuwa mbaya kwa muda mrefu. Karibu katika kila nchi Wakristo walilazimishwa kufuata madhehebu rasmi, ama Ukatoliki ama Ulutheri. Ikiwa mtawala fulani aliona vema kukubali mawazo ya Luther mapadri wote walipewa chaguo la kufuata Ulutheri au kuhama nchi. Vilevile baada ya kifo chake ikiwa mtawala aliyefuata alikuwa na msimamo tofauti, mapadri wakarudi na wachungaji wa Kiinjili wakafukuzwa.

Raia hawakuulizwa wenyewe wanasadiki nini, isipokuwa katika miji iliyojitawala na kuwa na utaratibu wa kidemokrasia. Lakini hata mijini huko haikuwa kawaida kuruhusu madhehebu mawili mahali pamoja.

Mafundisho ambayo kwetu leo yanaonekana kuwa na tofauti ndogo yaliweza kumfikisha mtu gerezani au hata kifoni.

Uhusiano mbaya ulikuwepo vilevile kati ya wafuasi wa Luther na Wareformati. Katekisimu zao zilitumika kama bendera. Walishutumiana kuwa wazushi wasioelewa vizuri kiini cha imani.

Kilichofuata ni kipindi cha vita vya kidini kule Ulaya. Kilele kilikuwa Vita vya Miaka 30 ambavyo vilianza kule Bohemia na Moravia kwa sababu watawala wadogo waliokuwa karibu na Umoja wa Ndugu walijaribu kumpindua Mfalme Mkatoliki.

Vita hivyo vilianza kama mapigano ya kidini kati ya madhehebu tofauti ya dola moja la Ujerumani, lakini viliendelea kuwa vita vya Ulaya nzima ambako nchi ya Wakatoliki kama Ufaransa ilishikamana na Uswidi ya Kiprotestanti dhidi ya Kaisari Mkatoliki.

Vita hivyo vilileta uharibifu mkubwa mno katika Ujerumani. Kuna makadirio ya kwamba karibu theluthi moja ya wakazi wote walikufa kutokana na mauaji, njaa na magonjwa. Katika maeneo ya Ujerumani ya Kusini zaidi ya nusu ya watu walipotea.

Wanajeshi walikuwa askari wa kukodiwa ambao mara nyingi hawakulipwa bali walipewa uhuru wa kutwaa kwa mabavu chochote walichotaka.

Uchovu ulileta majadiliano juu ya amani. Mwaka 1648 wawakilishi wa wafalme walipatana katika amani ya Westfalia kuhusu kanuni za amani.

  • Madhehebu matatu yaliyokubaliwa Ulaya ni Wakatoliki, Walutheri na Wareformed; mengine (kama Waanabaptisti na Umoja wa Ndugu) yaliangaliwa kuwa ya kizushi popote.
  • Kila mtawala aliamua kwa dola lake ni yapi kati ya madhehebu matatu halali yatafuatwa lakini raia walikuwa na haki ya kutoka katika nchi kama mtawala alikataa dini yao. Sheria ilikuwa: "Cuius regio, eius religio" (mwenye nchi ni mwenye kuamua dini)
  • Katika maeneo kadhaa Wakristo wa madhehebu tofauti walipewa ustahimilivu, lakini katika maeneo mengine walipaswa kuhamia nchi ya madhehebu yao au kufuata madhehebu rasmi ya nchi.
  • Ikiwa mtawala atabadili madhehebu baadaye wananchi wataruhusiwa kuendelea walivyozoea.
  • Uholanzi na Uswisi zilitoka katika Dola Takatifu la Kiroma kama nchi huru za pekee.
  • Mfalme wa Uswidi alitwaa maeneo makubwa katika Ujerumani ya Kaskazini

Kumbe mapatano hayo yaliunda ramani ya kimadhehebu kule Ulaya yenye maeneo ya Wakatoliki, Walutheri au Wareformati watupu. Jumuiya ndogo ziliendelea kugandamizwa wakapata ustahimilivu mahali pachache. Hivyo wafuasi wa madhehebu madogo walilazimika kuficha imani yao au kuhamahama katika Ulaya.

Wakati ule nafasi mpya ilitokea: Mfalme wa Uingereza alikuwa na makoloni Marekani lakini alikosa watu. Akatafuta walowezi kwa ajili ya makoloni yake akiwaahidia wote kwamba watapata shamba pamoja na uhuru wa dini. Hivyo watu kutoka nchi nyingi za Ulaya walianza kuhamia Marekani, hasa wale waliokosa uhuru huo. Mpaka leo nchi mbalimbali za Ulaya zinafuata hasa madhehebu moja, na Marekani ina madhehebu makubwa ambayo hayana wafuasi wengi Ulaya, k.mf. Wabatisti.

Umisionari kupamba tena[hariri | hariri chanzo]

Fransisko Saveri akimuongoa Paravas huko Goa, India, katika picha ya karne ya 19.

Wakati wa matengenezo na mafarakano ulikuwa pia kipindi kilicholeta habari za nchi mpya kwa watu wa Ulaya. Mataifa ya Wahispania na Wareno yalijenga aina mpya za meli zilizoweza kusafiri kote duniani hata kuvuka bahari kubwa.

Wafanyabiashara na wanajeshi wao walizunguka pande zote za dunia wakiambatana na mapadri wao. Hao walikutana na wenyeji wengi wa nchi mbalimbali wasio Wakristo, au walikuwa Wakristo lakini si washiriki wa Kanisa Katoliki (kama Waethiopia au Wahindi wa Kusini).

Wakaanza kuwaeleza imani, wakahubiri mbele ya Mfalme wa China, mbele ya Negus Negesti wa Ethiopia na mbele ya watawala wa Amerika Kusini.

Tatizo la misheni hizo lilikuwa kwamba liliambatana na uenezaji wa kijeshi wa Hispania na Ureno. Hasa Amerika wamisionari walijikuta kati ya mahitaji ya walowezi, waliotaka kuhudumiwa kiroho, na mahitaji ya wazalendo, waliogandamizwa vibaya na walowezi walewale.

Serikali ya kikoloni ilikuwa vilevile serikali ya mfalme Mkatoliki. Haikuwa rahisi kwa wamisionari kutofautisha kati ya pande hizo mbili. Mara nyingi Kanisa lilibariki tu utawala wa kikoloni uliogandamiza wenyeji.

Lakini mara kwa mara walijitokeza Wakristo wengine waliopinga unyama na kuleta taarifa za kweli kule Ulaya. Mmojawao alikuwa Askofu Bartolomeo Las Casas aliyewashtaki walowezi Wahispania kwa sababu waliua wenyeji wengi wakiwalazimisha kufanya kazi zao migodini na mashambani bila kujali afya zao. Akafaulu kuleta sheria zilizolinda Waamerika na kupunguza ukali dhidi ya watumwa, lakini walowezi walijaribu kumwua.

Zaidi tena Wajesuiti walijaribu kuwalinda Waindio wa Paraguay wakiwakusanya katika vijiji vya ujamaa vilivyojitegemea kiuchumi na hata kisiasa. Lakini walishtakiwa na walowezi majirani waliotaka kuwinda watumwa, ati wanadhoofisha utawala wa kikoloni. Mwishoni Wajesuiti walifukuzwa na serikali, na vijiji vya Wakristo wenyeji waliharibiwa na wawindaji wa watumwa.

Kule Asia mapadri wa Shirika la Yesu walifaulu kupanda mbegu ya Injili mpaka Japani na China. Walijitahidi kupatanisha Injili na utamaduni wa nchi hizo ambao ni tofauti na desturi za Ulaya. Lakini uongozi wa Kanisa kule Roma uliwakataza wasitumie mbinu hizo. Hivyo Wakristo wa Japan walionekana kufuata dini ya kigeni. Kwa sababu hiyo waligandamizwa, ila wachache walishika imani yao kwa siri mpaka kutokea kwa uhuru wa dini katika karne ya 19.

Kati ya wote anakumbukwa hasa Fransisko Saveri (Francisco de Jasso y Azpilicueta) (Javier, Navarra, leo nchini Hispania, 7 Aprili 1506 - kisiwa cha Shangchuan, China, 3 Desemba 1552), padri wa Shirika la Yesu, ambalo alichangia kulianzisha pamoja na Ignas wa Loyola.

Baadaye alitangaza Injili katika nchi nyingi za Ulaya, Afrika na Asia hata akawa kati ya wamisionari maarufu zaidi ya historia ya Kanisa.

Kati ya miaka 1500 na 1850 wamisionari Wakatoliki walihubiri kwenye pwani ya Afrika, hata Afrika Mashariki. Walifuata uenezi wa Wareno waliojaribu kutawala pwani hiyo kama vituo vya biashara kati ya Ulaya na Bara Hindi. Ustawi wa pekee ulipatikana katika ufalme wa Kongo (kusini kwa mto huo) ambapo Wakristo walifikia kuwa 50% za wakazi wote, na kati yao alipatikana askofu Mwafrika wa kwanza kutoka Kusini kwa Sahara, Dom Enrique.

Kutoka kwa makao yao ya Sofala na Msumbiji walijaribu pia kutawala biashara ya dhahabu iliyochimbwa katika eneo la Mwene Mtapa (Zimbabwe).

Kati ya matunda bora ya uinjilishaji huo wanakumbukwa "Mashahidi wa Mombasa" waliomfia Yesu mwaka 1631.

Mizizi ya Kanisa Afrika ilikauka tena mnamo karne za 16-18 kwa sababu ya kuingiliana kwa hotuba ya Injili na siasa ya ukoloni. Udhaifu wa kibinadamu uliongezea ugumu wa mazingira na hali ya hewa kwa ajili ya wamisionari kutoka Ulaya.

Upietisti[hariri | hariri chanzo]

Philipp Jakob Spener (16351705) anaitwa pengine "Baba wa Upietisti".

Upietisti (kwa Kiingereza Pietism, kutoka neno la Kilatini pietas, yaani heshima kwa Mungu, kwa wazazi, kwa ndugu na kwa nchi asili) ulikuwa tapo lenye athari kubwa kati ya Walutheri, lakini pia kwa madhehebu mengine ya Uprotestanti, na hata kwa Wakatoliki huko Ulaya na Amerika Kaskazini[2] tangu mwishoni mwa karne ya 17.

Uliunganisha mikazo ya Kilutheri kuhusu mafundisho ya Biblia ya Kikristo na mikazo ya Kikalvini kuhusu maadili imara.

Asili yake ni Ujerumani ya leo na kazi ya Philipp Jakob Spener, mwanateolojia Mlutheri aliyesisitiza mabadiliko ya Mkristo kwa aina ya kuzaliwa upya. Ingawa yeye hakudai wafuasi wake wajitenge na Wakristo wenzao, mahimizo yake yalielekea huko.

Upietisti ulienea kwanza Uswisi na nchi nyingine za lugha ya Kijerumani barani Ulaya, halafu Skandinavia na Baltiki (ulipoathiri zaidi tena utamaduni wa Kikristo kupitia watu kama Hans Nielsen Hauge huko Norway, Carl Olof Rosenius huko Sweden, Katarina Asplund huko Finland na Barbara von Krüdener katika nchi za Baltiki), na hatimaye Ulaya nzima.

Kutoka huko ulipelekwa Amerika Kaskazini, hasa kwa njia ya wahamiaji kutoka Ujerumani na Skandinavia, ukaathiri Waprotestanti wenye asili tofauti ukachangia katika karne ya 18 mwanzo wa Ukristo wa Kiinjilisti, ambao leo una waumini milioni mia tatu.

Tapo la Upietisti ndani ya Ulutheri lilifikia kilele chake katikati ya karne ya 18, lilififia kati karne ya 19 na kutoweka Amerika mwishoni mwa karne ya 20.

Hata hivyo, baadhi ya misimamo yake iliathiri Uprotestanti kwa jumla, ikimchochea kasisi Mwanglikana John Wesley kuanzisha tapo la Wamethodisti, na vilevile Alexander Mack kuanzisha tapo la Schwarzenau Brethren kati ya Waanabaptisti.

Huko Marekani, Upietisti ulitawala pia kati ya Quakers, Wakalvini, Wabaptisti, Waanglikana n.k.

Umisionari wa Kiprotestanti[hariri | hariri chanzo]

Tumeshaona kwamba tangu mwaka 1500 wamisionari Wakatoliki walienda sehemu mbalimbali za dunia. Katika karne ya 17 Waprotestanti walienea nje ya Ulaya, lakini bila kumtangaza Kristo kwa wenyeji, kwa mfano katika makoloni ya Marekani mashariki ya leo. Kumbe katika 18 walianza kuiga mifano ya wamisionari Wakatoliki.

Uenezaji wa Ukristo wa Kiprotestanti ulianzishwa na Wakristo kutoka nchi za Ulaya zilizoendelea kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Mapinduzi ya viwandani yaliongeza sana uwezo wa kiuchumi wa mataifa hayo.

Biashara ya kimataifa ilianza kuunganisha nchi za mbali sana. Vyombo vya usafiri kama vile meli, reli na baadaye hata ndege vilifikisha watu na bidhaa kila sehemu za dunia. Watu walianza kupata habari za nchi zisizojulikana kwao mpaka wakati ule.

Wakristo wa nchi za Ulaya walitumia mawasiliano hayo. Labda tunaweza kulinganisha hali hiyo na sera za mitume ambao walitumia njia zilizofunguliwa na biashara ya Kiroma katika karne za kwanza. Wengine waliona uwezo wao kama wito wa Mungu kwa Wakristo wa Ulaya katika karne ile hasa.

Mahali pengi Ulaya Wakristo hawakuridhika tena na hali ya Kanisa. Ukristo ulikwisha kuwa sehemu ya utamaduni na jambo la kawaida. Bila kutafakari sana, mtoto alibatizwa, akafundishwa na kupewa Kipaimara, akafunga ndoa kanisani, akawabatiza watoto wake halafu akazikwa kwa ibada.

Kanisa lilikuwa kama idara ya serikali iliyosaidia taifa kuweka utaratibu wa kidini kwa manufaa ya maadili ya umma. Serikali zilihimiza watu washiriki na kuhudhuria ibada. Wasipofika kanisani waliweza kutozwa faini.

Lakini mazingira na hali ya maisha vilibadilika. Watu walianza kuhamia mijini, jumuiya za vijiji zilianza kulegea na kuvunjika.

Mahali pengi watumishi wa makanisa hawakujua kujibu maswali mapya ila tu kukumbusha mazoea ya kale na mila nzuri za zamani.

Ndiyo asili ya matapo ya uamsho yaliyotokea kwa nguvu sana. Wasioridhika na hali hiyo walikutana nje ya makanisa. Katika maeneo ya Kiprotestanti hali ilitegemea. Penye uongozi wenye busara walipewa nafasi zao shirikani. Watu waliguswa upya na neno la Mungu na Roho wake, walitafuta njia mpya za kuishi na kuonyesha imani yao. Hivyo vilijitokeza vyama vya kusaidia wagonjwa, wajane, mayatima na maskini.

Penye uongozi mkali uliokataa njia na mbinu mpya Wakristo walikutana na kusali katika nyumba za watu. Wengine walianzisha jumuiya na madhehebu ya pekee. Lakini sehemu kubwa ya Wakristo wa uamsho walielewa kazi yao ya kutengeneza upya makanisa yao badala ya kuunda vikanisa vipya.

Katika maeneo ya Wakatoliki matapo yaliyofanana na uamsho yalisababisha mara nyingi kutokea kwa shirika jipya la watawa au la walei. Muundo wa Kanisa Katoliki unasaidia kuwapa watu wenye wito au vipawa vya pekee nafasi zao katika mashirika hayo.

Kanisa la Anglikana liliunda kamati ya kupeleka Injili katika nchi za ng'ambo lakini ilishughulikia hasa Waingereza waliohamia makoloni. Polepole wazalendo wachache walianza kuwaendea pia, jambo lililokuwa gumu kutokana na hali ya ukoloni wenyewe.

Kanisa la kwanza la Kiprotestanti lililotuma wamisionari hasa kwa watu wasiomjua Kristo lilikuwa ni la Ndugu wa Herrnhut (Wamoravia).

Katika kijiji hicho kidogo cha Ujerumani waliishi wakimbizi kutoka Moravia waliopewa ustahimilivu kuanzisha upya ushirika wa Umoja wa Ndugu kufuatana na urithi wao kutoka Ucheki. Walikuwa watu wa kawaida kama wakulima na mafundi.

Siku moja katika mwaka 1732 walikutana na mgeni, kwa jina Antoni, mtumishi wa Mdenmark aliyemtembelea Mkuu wa Herrnhut, Ludwig von Zinzendorf. Antoni alikuwa mtumwa mwenye asili ya Afrika aliyenunuliwa na bwana wake katika Visiwa vya Karibi. Baadaye akapewa uhuru wake akasafiri pamoja na bwana wake hadi Denmark.

Kwa Antoni Ndugu wa Herrnhut wakasikia kwa mara ya kwanza habari za hali mbaya ya watumwa Waafrika kule Karibi, na jinsi walivyozuiwa kusikia neno la Mungu pamoja na mateso yao mengine. Usiku ule ndugu wawili wakasali pamoja na asubuhi yake wakamwendea Mkuu wa Herrnhut wakamwomba ruhusa ya kusafiri hadi Karibi ili wawahubirie wale watumwa. Katika sala hiyo ya maseremala wawili ilianza kazi ya misheni ya Umoja wa Ndugu (Wamoravia).

Baadaye Ndugu Wamoravia waliendelea kuhubiri kule Greenland, Urusi, Nikaragua, Afrika Kusini na kati ya Waindio wa Amerika. Mawasiliano mapya yakaleta habari hiyo katika kila pembe ya dunia zisizosikika zamani kwa watu wengi.

Wamoravia walihubiri mahali pengi Ulaya kati ya Wakristo wa madhehebu yote bila kuwashawishi wajiunge nao lakini walieneza sana habari za misheni.

Wakiitikia mfano wa Ndugu wa Herrnhut Wakristo kutoka vikundi mbalimbali vya uamsho walianza kuelewa wajibu wao wa kueneza Injili kote duniani.

David Livingstone (1813-1873) kutoka Uskoti ni kati ya wamisionari bora wa Afrika.

Mnamo mwaka 1800 Wakristo Waingereza waliunda vyama mbalimbali vya misheni, kama Wabatisti mwaka 1792, Chama cha Misheni cha London mwaka 1795 na Chama cha Misheni cha Kanisa (la Kianglikana = Church Missionary Society/CMS) mwaka 1799. Waprotestanti wa nchi nyingine za Ulaya walifuata.

Mara nyingi wakati ule si viongozi wa madhehebu ya Kiprotestanti (isipokuwa kwa kiasi Waanglikana) walioendesha kazi ya misheni, kwa kuwa walijali maeneo yao tu wakikosa mtazamo wa dunia nzima kama wenzao Wakatoliki.

Kumbe walikuwa walei na wachungaji wa kawaida waliounda vyama vya misheni, kuiombea kazi hiyo, kutafuta habari za nchi nyingine na kuchanga pesa wakiandaa vijana watakaokuwa tayari kuacha ndugu zao wakielekea nchi za mbali zisizojulikana nao.

Kanisa Katoliki na la Kiorthodoksi katika karne ya 18[hariri | hariri chanzo]

Wakati Ukristo ulipozidi kuenea na kuchangamka katika bara lote la Amerika, huko Ulaya Kanisa Katoliki lilipitia kipindi cha udhaifu, hasa kutokana na mashambulizi ya falsafa ya Mwangaza dhidi yake.

Falsafa hiyo ilienea katika matabaka ya juu ya nchi nyingi na kufuatwa na serikali zake, ambazo zilianza kulibana kwa njia nyingi, hasa kwa kuzuia mashirika ya kitawa.

Mambo yalizidi kuwa magumu Mapinduzi ya Ufaransa yalipopiga vita dini, kuanzia Ukatoliki. Akili ilisimikwa kama mungu mpya. Kalenda mpya ilitengenezwa ili kufuta wiki na Jumapili pamoja na sikukuu za Kikristo. Monasteri zote zilibomolewa, wengi waliuawa au kufukuzwa nchini kwa sababu ya imani yao. Mali za Kanisa zilitaifishwa na mapadri walidaiwa kula kiapo cha kufuata serikali badala ya Papa. Mnamo 1799 Papa Pius VI alitekwa hadi Ufaransa na hatimaye kufa kifungoni.

Kiongozi wa Ufaransa, Napoleon Bonaparte, alizidi kueneza misimamo mipya katika sehemu kubwa ya Ulaya aliyoiteka.

Hata Waorthodoksi walipata shida za namna hiyo hasa Urusi, ambapo mwaka 1721 Kaisari Petro I alifuta Upatriarki nchini na kuweka Kanisa moja kwa moja chini ya serikali.

Ukristo katika karne ya 19[hariri | hariri chanzo]

Pius IX, Papa aliyeongoza Kanisa kwa muda mrefu kuliko wote (1846-1878).

Baada ya Ufaransa wa Napoleon kushindwa (1815), nchi za Ulaya zilikubaliana kurudisha hali ilivyokuwa kabla ya mapinduzi, lakini haikuwa rahisi. Umati wa watu ulizidi kusogea mbali na dini.

Baada ya mateso yao, Papa na Kanisa Katoliki walipewa tena heshima, lakini siasa iliendelea kuwa dhidi yao.

Kilele chake ni Kulturkampf (kwa Kijerumani: vita vya utamaduni) iliyotangazwa na Chansela Bismarck ili kuzuia umoja wa Wakatoliki wa Ujerumani na Papa. Majimbo na parokia nyingi vilibaki bila mchungaji, mapadri wengi walifungwa n.k.

Kabla ya hapo, Papa Pius IX alikutanisha maaskofu mjini Roma kwa Mtaguso wa kwanza wa Vatikano (1869-1870) uliotangaza dogma ya karama ya Papa kutokosea anapotoa mafundisho ya moja kwa moja "ex cathedra".

Mtaguso ulikatishwa na jeshi la Italia lililovamia Roma na kuuteka moja kwa moja, likikomesha Dola la Papa (1870). Tukio hilo lilimkomboa Papa kutoka majukumu ya kisiasa na kumwezesha kuimarisha mamlaka yake ya kiroho duniani kote dhidi ya utaifa uliotesa Kanisa kwa karne kadhaa.

Karne ya 19 iliona pia Wakatoliki kuchangamkia tena umisionari, kuanzia Wafaransa.

Jambo lingine la pekee katika Kanisa Katoliki la karne hiyo ni uundaji wa mashirika ya kitawa ya kike na ya kiume zaidi ya 2000 yaliyolenga huduma maalumu, k.mf. kuhubiri vijijini, kulea vijana, kufundisha mafukara, kuuguza wagonjwa, kuanzisha misheni, kushughulikia upashanaji habari. Mara nyingi mashirika hayo yanafanana ingawa yalianzishwa wakati na mahali tofauti, kwa kawaida chini ya askofu wa jimbo, baada ya mashirika ya zamani kuzuiwa na serikali.

Kati ya waanzilishi muhimu zaidi wakumbukwe Karolo Yosefu Mazenod (1782-1861), Vinsenti Pallotti (1795-1850), Antoni Maria Claret (1807-1870), Yohane Bosco (1815-1888), Daniele Comboni (1831-1881), Arnold Janssen (1837-1909). Kati ya wanawake, Yoana Antida Thouret (1765-1826), Magdalena wa Canossa (1774-1835), Visensya Gerosa (1784-1847) pamoja na Bartolomea Capitanio (1807-1833), Fransiska Saveri Cabrini (1850-1917).

Uprotestanti uliendelea kufaidika na uamsho, ingawa huko Marekani walifikia hatua ya kuanzisha madhehebu mengi ya aina mpya, yaliyojaribu kuanza kila kitu upya kwa msingi wa Biblia, yakidharau historia yote ya Kanisa kama upotoshaji wa imani.

Miaka ya mwisho ya karne ya 19 iliona ustawi wa elimu ya Biblia iliyoongozwa na mawazo mapya kabisa yaliyoyumbisha imani ya wengi kwa kukanusha mambo yapitayo maumbile (teolojia ya Usasa).

Karne ya 20[hariri | hariri chanzo]

Papa Yohane Paulo II (1978-2005) anahesabiwa na wanahistoria kadhaa kama mtu aliyeathiri ulimwengu kuliko watu wote wa karne ya 20, hasa kwa kusambaratisha Ukomunisti na kumaliza vita baridi.

Wakati Ulaya ulipozidi kuachana na dini, Ukristo ulienea kwa kasi ya ajabu katika bara la Afrika, na kwa kiasi tofauti katika maeneo mengine yasiyokuwa na mapokeo hayo.

Mang'amuzi ya kimisionari yalifanya Wakristo watambue upya haja ya umoja kati yao. Walianza Waprotestanti (Kongamano la Edinburgh, 1910), halafu Waorthodoksi na Wakatoliki.

Masomo ya liturujia na uchungaji pamoja na uchunguzi wa maandishi ya mababu wa Kanisa vilileta pumzi mpya katika madhehebu mbalimbali.

Mtaguso wa pili wa Vatikano (1962-1965) ulioitishwa na Papa Yohane XXIII ulielekeza Kanisa Katoliki kukabili vema ulimwengu wa kisasa badala ya kuulaumu tu.

Lakini karne ya 20 inakumbukwa hasa kwa dhuluma za kidini zisizowahi kutokea: hasa Ukomunisti, ulioteka Urusi ukaenea polepole hadi kutawala theluthi moja ya binadamu wote, ulipiga vita dini kwa namna zote na kuua mamilioni ya waamini, hasa Waorthodoksi.

Hatimaye, chini ya Papa Yohane Paulo II, wa kwanza kutoka mataifa ya Kislavi, Wapolandi walifaulu kuangusha serikali ya Kikomunisti, wakifuata na wenzao wa nchi zote za Ulaya Mashariki.

Baada ya hapo, Ukristo uliamka upya katika nchi hizo.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Martin Luther, Weim., X, P. Il, 107, 8-11
  2. In places, such as parts of England and America, where Pietism was frequently juxtaposed with Roman Catholicism, Catholics also became naturally influenced by Pietism, helping to foster a stronger tradition of congregational hymn-singing, including among Pietists who converted to Catholicism and brought their pietistic inclination with them, such as Frederick William Faber.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]