Waorthodoksi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Waorthodoksi ni Wakristo wanaofuata mapokeo ya Mitume wa Yesu jinsi yalivyostawi awali upande wa mashariki wa Dola la Roma na nje ya mipaka yake.

Jina hilo lina asili ya Kigiriki likitokana na maneno όρθος ("orthos", yaani "nyofu", "sahihi") na δόξα ("doksa", yaani "rai", "fundisho").

Jina hilo lilitungwa ili kutofautisha Wakristo waliofuata mafundisho rasmi ya imani yaliyotolewa na Mitaguso ya kiekumene dhidi ya uzushi.

Kwa namna ya pekee jina hilo lilitumika upande wa mashariki, hivi kwamba lilipotokea Farakano la Mashariki (hasa mwaka 1054), likabaki kama jina maalumu la makanisa yenye ushirika na Patriarki wa Konstantinopoli (leo Istanbul katika Uturuki).

Hivi karibuni hata makanisa mengine ya mashariki yamechagua kujiita hivyo, ingawa yanaendelea kukataa mitaguso mikuu iliyokubaliwa na Wakristo walio wengi.