Dola la Roma

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Dola la Roma mnamo mwaka 117
Upanuzi wa eneo la Roma kuanzia 510 KK hadi 480 BK;
nyekundu = Jamhuri ya Roma 510KK-40KK
dhambarau= Dola la Roma 20BK-360BK
Buluu = Dola la Roma la Magharibi 405AD-480AD
Njano = Dola la Roma la Mashariki (Bizanti) 405AD-480AD

Dola la Roma lilikuwa milki kubwa katika nchi zinazopakana na bahari ya Mediteranea. Lilianza kwenye mji mkuu wa Roma na rasi ya Italia ikaendelea kuunganisha makabila na mataifa ya nchi nyingi kwenye mabara matatu ya Ulaya, Afrika na Asia.

Watawala wa Dola wakaitwa makaisari na Kaisari wa kwanza alikuwa Augusto.

Nchi nyingi za sasa ziliwahi kuwa sehemu ya Dola la Roma kama vile Uingereza, Ufaransa, Hispania, Italia, Ugiriki, na nchi za Balkani upande wa Ulaya, Moroko, Algeria, Tunisia, Libia na Misri upande wa Afrika, na Uturuki, Syria, Lebanon, Palestina, Jordan na hata Irak upande wa Asia.

Lugha ya Dola la Roma ilikuwa Kilatini, ila katika sehemu za mashariki pamoja na Kigiriki cha Kale.

Sehemu ya magharibi ya Dola la Roma iliishia mwaka 476 baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Kaisari wa mwisho Romulus Augustulus aliyefukuzwa na jemadari wa Kigermanik wa jeshi la Roma.

Upande wa mashariki Dola la Roma likaendelea hadi 1453 kwa majina kama "Roma ya Mashariki" au Bizanti.

Dola-mji[hariri | hariri chanzo]

Chanzo cha dola la Roma kilikuwa dola-mji mjini Roma penyewe. Mji uliundwa katika karne ya 9 KK hivi kwenye vilima kando ya mto Tiber katikati ya rasi ya Italia. Waroma wenyewe walipenda kutaja mwaka 753 KK waliotumia kama chanzo cha kalenda yao "ab urbe condita" (tangu kuundwa kwa Roma). Lakini akiolojia imeonyesha dalili za makazi ya mapema zaidi katika eneo la mji.

Mji ulitawaliwa awali na wafalme. Mwaka 509 KK mfalme wa mwisho alifukuzwa na kipindi cha jamhuri ya Roma kilianza. Mji wa Roma ulieneza athira yake kwa njia ya mapatano au vita na miji na makabila jirani.

Upanuzi katika Italia[hariri | hariri chanzo]

Dola la Roma lilianza kupanuka katika Italia. Mwaka 396 KK mji jirani wa Veio ulitwaliwa na kuharibiwa. Katika karne ya 4 KK vilitokea vita kati ya Roma na majirani na eneo lote la Lazio likatawaliwa na Roma.

Roma ilianzishwa utaratibu wa ushirikiano na majirani. Mara chache tu wapinzani walimalizwa kabisa kama Veio. Mara nyingi walilazimishwa kutia sahihi mikataba ya ushirikiano walimopaswa kuwasaidia Waroma kwa wanajeshi na kutokuwa na uhusiano wowote na makabila ya nje. Makabila na miji iliyoshirikiana vizuri na Roma walipewa uraia wa Roma sawa na wenyeji wa mji wenyewe.

Katika karne ya 3 KK Waroma waliendelea kutwaa sehemu kubwa ya rasi ya Italia. Katika vita dhidi ya Pyrrho wa Epirus (kati ya Albania na Ugiriki) miaka ya 280 KK - 275 KK Roma ilishinda mara ya kwanza dhidi ya jeshi lililotoka nje ya Italia. Vita hii ilisababisha ubwana wa Roma juu ya miji ya Kigiriki katika kusini ya Italia ilipaswa kukubali ubwana wa Roma tangu 275 KK pia makabila ya milimani.

Eneo la Karthago mnamo 264 kabla ya vita za Kipuni

Vita za Wapuni na kipaumbele katika Mediteranea ya magharibi[hariri | hariri chanzo]

Ushindi huu ulisababisha ugomvi na Karthago iliyotawala pwani za Mediteranea pamoja na kisiwa cha Sisilia. Hali ya vita ilianza tangu mwaka 264 kk kati ya Roma na Karthago au "Wapuni" jinsi walivyoitwa na Waroma. Vita hii ya kwanza ilikwisha 241 KK na Karthago ilipaswa kuwaachia Waroma Sisilia yote. Katika vita hii Waroma waliendelea kushinda baharini pia siyo kwenye nchi kavu tu.

Vita ya pili dhidi ya Wapuni (218 to 201 KK) ilianzishwa na Karthago. Jemadari Hanibal alitaka kulipiza kisasi akavuka milima ya Alpi kwa tembo zake za kivita. Alishinda mara kadhaa jeshi za Waroma lakini Waitalia wengine walisimama imara upande wa Roma. MwiShowe Roma ilishinda mara ya pili na Karthago ilipaswa kuwaachia Waroma pwani yote ya kaskazini-magharibi ya Mediteranea pamoja na Gallia (Ufaransa) ya kusini, Hispania na visiwa vya Mediteranea. Karthago ilibaki upande wa Afrika tu.

Mabaki ya himaya ya Karthago pamoja na mji yalimalizwa na Roma katika vita ya tatu dhidi ya Wapuni kati ya 149 KK hadi 146 KK. Karthago iliharibiwa kabisa na wakazi wote wasiouawa kuuzwa kama watumwa.

Upanuzi katika Ugiriki[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa vita ya pili ya Wapuni mfalme Filipo V wa Makedonia aliwahi kuwasaidia Karthago. Roma ilitumia nafasi ya ushindi kupinga upanuzi wa Makedonia katika Ugiriki kwa kusaidia madola madogo za Ugiriki ya kusini dhidi Filipo V. Vita hizi kati ya Roma na Makedonia zilikuwa na shabaha za kuzuia kipaumbele cha ufalme wowote wa Ugiriki. Roma likabaki katika siasa ya Ugiriki zaidi kama mtazamaji.

Mwaka 192 mfalme Antioki III wa milki ya Waseleuko aliingia kijeshi katika Ugiriki. Roma ikajibu kwa kutuma legioni zake na kuanzisha mfululizo wa vita zilizoendelea hadi mwaka 146. Waseleuko walipaswa kujiondoa katika Ugiriki kabisa. Uwezo wa Makedonia ikapunguzwa na sehemu kubwa ya Ugiriki kuwa majimbo ya Kiroma ya Achaea, Epirus na Makedonia.

Jaribio la mwisho la Wagiriki kutetea mabaki ya uhuru wao yalisababisha uangamizi wa mji wa Korintho mwaka 146 pamoja na uharibifu wa Karthago.

Kuingia Asia[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 133 mfalme wa Pergamon katika Asia Ndogo (Uturuki wa leo) aliyeogopa fitina kati ya warithi wake aliamua kukabidhi milki yake kwa jamhuri ya Roma baada ya kifo chake. Milki hii ikawa jimbo la Kiroma la Asia lililoonekana kuwa jimbo tajiri kabisa. Tukio hili likawa mlango wa Roma kupanua zaidi katika masjhariki ya Mediteranea.

Jimbo jipya la Asia likavuta wanasisasa Waroma wenye hamu ya kujitajirisha likawa kitovu cha ufisadi katika milki ya Roma.

(kuendelea)

WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Hourglass.svg Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Dola la Roma kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.