Kalenda

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Kalenda ni utaratibu wa kupanga wakati. Hupatikana kama orodha ya vipindi vya wakati kama vile siku, juma, mwezi na mwaka. Kalenda mbalimbali zimejua pia vipindi vya miaka kadhaa.

Kalenda inayotumika zaidi leo kimataifa ni kalenda ya Gregori iliyo muhimu kwa uchumi na biashara. Kuna pia nchi zinazotumia hasa kalenda zao za kitaifa au kalenda mbalimbali sambamba.

Hasa maisha ya kidini hupangwa kufuatana na kalenda maalumu. Kihistoria palikuwako na kalenda nyingi.

Yaliyomo

Migawanyo asilia ya wakati[hariri]

Mchana na usiku[hariri]

Kwa watu wengu duniani mabadiliko wa mchana na usiku ni utaratibu wa kwanza unaogawa wakati. Mchana na usiku pamoja inahesabiwa kama siku moja. Lakini kuna njia tofauti jinsi gani kuanza hesabu hiyo: asubuhi (mwanzo wa mchana) au jioni (mwanzo wa usiku) zilikuwa njia za kawaida za kuhesabu siku mpya. Tangu kupatikana kwa saa zinaonyesha masaa hata gizani saa sita usiki (katikati ya usiku) imeangaliwa kuwa mwanzo wa siku mpya.

Awamu za mwezi[hariri]

Awamu za mwezi huonekana vizuri kwa kila mtu. Kwa sababu hii awamu hizi zilikuwa mbinu unaoeleweka rahisi kupanga siku kwa vipindi. Kipindi kutoka mwezi mpya hadi mwezi mpya ni kipimo kinachopatikana katika kila nchi.

Majira kama msingi wa hesabu ya mwaka[hariri]

Majira au badiliko la vipindi vinavyorudi vya joto na baridi au vya ukame na mvua zilikuwa utaratibu mwingine ulioonekana kwa watu. Ila tu hesabu hii ilitegemea na mazingira na hali ya hewa katika eneo fulani.

Hasa katika nchi ambako majira yanatofautiana vikali na kufuata utaratibu wa kurudia hata mimea na wanyama hufuata mwendo wa majira. Katika mazingira kama hii imewezekana kutofautisha matokeo katika maisha kufuatana na idadi ya vipindi vya baridi au vya joto au vya mvua vilivyopita tangu tokeo fulani.

Mabadiliko ya mimea hutegemea mwendo wa jua na idadi ya mwanga pamoja na joto linalopatikana katika sehemu mbalimbali za dunia. Katika nchi karibu na ikweta tofauti hizi mara nyingi si kali sana na majira hazionekani vizuri isipokuwa majira ya mvua na ukame. Katika nchi hizi kalenda za kale mara nyingi zilitegemea nyota hasa Zuhura (Ng'andu) na mahali angani inapoonekana asubuhi au jioni kwa wakati fulani.

Kilimo na mwanzo wa Kalenda[hariri]

Inaaminika ya kwamba tangu kuanza kilimo watu wameanza pia kushika kumbukumbu ya wakati. Katika nchi nyingi kupanda na kuvuna kunategemea mwendo wa majira yanayorudia. Kazi ya pamoja inahitaji mpangilio na lugha ya pamoja. Hapa ni mwanzo wa kalenda.

Kalenda za Kisasa[hariri]

Hata leo hii kuna kalenda mbalimbali zinazotumiwa duniani. Kalenda inayotumiwa zaidi kimataifa ni kalenda ya Gregori inayohesabu miaka tangu Kristo kuzaliwa. Kalenda hii imepokea muundo wake kutoka kalenda ya Roma ya Kale hasa miezi na idadi ya siku zao.

Kalenda nyingine inayotumiwa katika nchi kadhaa ni kalenda ya Kiislamu inayohesabu miaka tangu hijra ya Muhamad; kalenda hii hutumiwa na Wasilamu wote kwa kukadiria sikukuu zao hata wakitumia menginevyo kalenda ya Gregori.

Kalneda nyingine ni kalenda kama ile ya Kichina, ya Kihindi na kadhalika zinazotumiwa kwa makadirio ya sikukuu katika dini au utamaduni wao lakini kwa maisha ya kawaida watu wengi wanatumia kalenda ya Gregori.

Nchi kadhaa huwa pia na namna ya pekee za kalenda kwa mfano Ethiopia hufuata kalenda yake inayohesabu tangu kuzaliwa kwake Kristo lakini kwa tofauti ya hesabu ya miaka 7 na miezi 3; ina miezi 13. Kalenda ya Uajemi huhesabu miaka tangu hijra lakini tofauti na Waislamu wengi hutumia mwaka wa jua si mwaka wa mwezi kwa hiyo kuna tofauti ya takriban miaka 40 hivi.

Wiki[hariri]

Hesabu ya wiki haifuati kalenda ni kipindi cha siku 7 kinachorudia mfululizo bila kujali mwisho au mwanzo wa mwaka. Asili yake iko katika Mashariki ya Kati hasa Babeli ikasambazwa kupitia imani ya Uyahudi na Ukristo. Inaanza kwa siku ya Jumapili inayotazamiwa kidini kama siku ya kwanza ya uumbaji wa dunia na kwa wakristo pia siku ya ufufuo wa Yesu unaotazamiwa kama uumbaji wa pili. Kwa kusudi la kupanga maisha na hasa kazi wiki za mwaka zinahesabiwa kuanzia 1 - 52; hapo wiki ya kwanza na wiki ya mwisho kwa kawaida si kamili kwa sababu siku kadhaa zimo katika mwaka uliotangulia au kufuata. Tangu kuenea desturi ya wikendi yaani mapumziko ambako wengi hawafanyi kazi siku za Jumapili na Jumamosi kalenda nyingi huonyesha siku ya kwanza ya wiki ambayo ni Jumatatu kama chanzo cha wiki ya kazi.

Tazama pia[hariri]

  1. Kalenda ya Gregori
  2. Kalenda ya Juliasi
  3. Kalenda ya Kiislamu


Science-symbol-2.svg Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kalenda kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.