Agostino wa Hippo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Picha ya kale zaidi (karne ya 6) ya Agostino katika kanisa la Laterani, Roma (Italia).
Agostino wa Hippo akibatizwa na Ambrosi, mwaka 387.

Agostino wa Hippo (13 Novemba, 35428 Agosti, 430) alikuwa mwanatheolojia na kiongozi wa Kanisa katika Afrika ya Kaskazini wakati wa karne ya 5 BK.

Kutokana na maisha, mafundisho na maandiko yake bora amepewa cheo cha mtakatifu pia cha mwalimu wa kanisa. Hippo ni jina la kale la mji Annaba katika Algeria ya leo alipokuwa askofu.

Yaliyomo

[hariri] Maisha yake

Agostino alizaliwa mwaka 354 mjini Thagaste katika mkoa wa Numidia (leo: Algeria). Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Aurelius Augustinus. Wakati ule Ukristo ulikuwa tayari dini iliyokubaliwa katika Dola la Roma; dhuluma dhidi ya Wakristo yalikuwa yamekwisha mwaka 313.

Mama yake Agostino (Monika, anayeheshimiwa kama mtakatifu) alikuwa Mkristo, kumbe baba (Patrisi) alifuata dini ya jadi ya kuabudu miungu mingi kabla hajabatizwa mwishoni mwa maisha yake. Alipata elimu yake hata katika Chuo Kikuu cha Karthago (karibu na Tunis).

Katika sehemu za magharibi za Afrika ya Kaskazini wenyeji walikuwa Waberberi kama mama yake, lakini watu wa mjini, kama baba yake, na wenye mashamba makubwa walikuwa wa asili ya Ulaya wakitumia hasa lugha ya Kilatini. Kwa jumla sehemu hii ya Afrika ilikuwa karibu na utamaduni wa Ulaya ya Magharibi.

Agostino mwenyewe aliendelea kusoma Italia baada ya kumaliza masomo yake Karthago. Ndipo akakutana na watu, hasa Ambrosi askofu wa Milan, waliomvuta kuachana na dini ya Mani, aliyoifuata kwa karibu miaka 10, awe Mkristo Mkatoliki.

Baada ya kubatizwa na kunuia kuishi kitawa akarudi Afrika akapewa daraja ya upadri, halafu akachaguliwa kuwa askofu msaidizi wa mji wa Hippo huko Numidia mwaka 395 na mwaka uliofuata akawa askofu kamili.

Aliaga dunia Hippo mwaka 430 wakati washenzi Wagermaniki walioitwa Wavandali walipokaribia kuteka mji wake.

Mpaka kifo chake aliendelea kueleza na kutetea imani sahihi ya Kikristo kwa maandiko na vitabu vingi. Kwa njia hii amekuwa mwalimu muhimu sana katika Ukristo, hasa wa Magharibi (yaani Kanisa Katoliki na katika Uprotestanti uliotokea katika kanisa hilo. Kwa mfano Martin Luther alimtaja Agostino kuwa baba yake wa kiroho pamoja na Mt. Paulo).

Kaburi la Agostino katika basilika la San Pietro in Ciel d'Oro, Pavia (Italia).

[hariri] Kazi na mafundisho yake

Kazi kubwa ya Agostino si kuandika maelezo juu ya vitabu na maneno ya Biblia yenyewe alivyofanya Origene, bali hasa Biblia katika mazingira ya kiroho, kijamii na kisiasa ya wakati wake. Hapo aliuliza maswali na kutoa majibu yenye umuhimu mpaka leo.

Mafundisho yake yamesikika hasa juu ya suala la neema na dhambi halafu juu ya uhusiano wa Kanisa na serikali.

[hariri] Dhambi na neema

Katika mafundisho yake juu ya neema na dhambi ni Agostino aliyetoa mafundisho ya kwamba ubinadamu umerithi dhambi ya asili kutoka kwa Adamu. Uhuru umepotezwa na dhambi yake, na hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwa watu.

Alisisitiza kwamba si binadamu anayemtafuta Mungu, bali Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mwenye dhambi.

[hariri] Mji wa Mungu

Juu ya uhusiano kati ya serikali na kanisa aliandika kitabu "De civitate Dei" (kwa Kilatini: Mji wa Mungu. Badala ya "mji" tungeweza kutafsiri pia: "eneo au kikundi cha watu au utawala").

Alieleza kwamba iko "miji" miwili: mji wa Mungu (yaani Yerusalemu wa mbinguni, au kanisa) na mji wa dunia hii, yaani taratibu za kisiasa.

Katika "mji wa dunia hii" hali hubadilika. Hakuna taratibu za kudumu. Agostino alifahamu taratibu za Waroma wa kipagani walioangalia makaisari wao kuwa miungu, akafahamu habari za demokrasia ya Kigiriki ya kale. Akafahamu habari za mji mkubwa wa Roma ulioitwa "mji wa milele" lakini ulichomwa moto na maadui katika siku zake jinsi ilivyoanguka zamani miji ya Babeli na Yerusalemu.

Lakini pamoja na "mji" huo upo "mji" wa pili ndio mji wa Mungu ambao ni mji wa upendo na undugu penye neema yake Mungu.

Miji yote miwili iko pamoja ingawa taratibu zao ni tofauti. Mkristo ni raia wa miji yote miwili. Huitwa kuwa mwaminifu pande zote mbili. Lakini ajue kwamba mji wa dunia hii hauna shabaha ya kudumu. Umeingiliwa na dhambi. Kumbe mji wa Mungu utadumu. Umepewa lengo la kudumu, unashiriki enzi ya Mungu.

Ndiyo sababu inafaa serikali isikie mawazo ya kanisa, kwani ni kwa njia ya kanisa kwamba Mungu ameamua kufunua mapenzi yake. Mkristo anaweza kushiriki katika taratibu za kisiasa akijua ya kwamba mawazo na mipango yote ya siasa havidumu. Utakaodumu ni utaratibu wa Mungu.

Ni kutokana na mafundisho haya ya Agostino kwamba Kanisa la Magharibi lilijifunza umuhimu wa kuwa na msimamo imara mbele ya serikali mbalimbali kama ulivyojitokeza katika historia ndefu ya kanisa, ingawa Agostino alijua jinsi Kaisari Theodosi alivyotubu kanisani baada ya askofu Ambrosi wa Milan kumtenga kwa sababu aliwatuza wanajeshi wa serikali yake walioua watu wengi ovyo walipogandamiza fujo lililotokea katika mji wa Thesalonike. Watu wengi pamoja na Askofu walisikitikia tendo hilo. Baadaye Theodosi alipotaka kuingia katika ibada, Askofu huyo alimtangaza ametengwa kwa sababu ya damu ya wananchi wa Thesalonike, hivyo hawezi kushiriki meza ya Bwana. Kaisari akakubali kosa mbele ya umati. Hata baadaye viongozi wa kanisa la magharibi wakafuata mara nyingi mfano wa Ambrosio na mafundisho ya Agostino.

[hariri] Urithi wake

Mafundisho ya Agostino yaliathiri mawazo na fikra za Wakristo kwa karne nyingi za baadaye.

Tunaweza kuona aina mbili za matokeo ya urithi huo.

Kwa upande mmoja kanisa lilijaribu kutawala jamii na serikali katika nchi za Ulaya. Lilidai sheria zote za serikali zifuate taratibu za kanisa. Viongozi wa serikali walitakiwa kusimikwa na kanisa. Hoja hili huitwa "Uklerikali" (clericalism).

Nguvu ya kisiasa ya kanisa ilifikia kilele chake mwanzoni mwa karne ya 13 wakati wa Papa Inosenti III, halafu ilizidi kupungua hadi kupingwa kabisa na mapinduzi mbalimbali ya Ulaya na Amerika (kuanzia mapinduzi ya Ufaransa 1789).

Siku hizi wazo hili halipo tena lakini zamani lilileta matatizo mengi, kama vile ugandamizaji wa madhehebu tofauti na ya mtawala na hata vita.

Mafundisho ya Agostino yaliingiza hoja la "vita halali" katika Ukristo uliowahi kukataa ukatili na vita kama dhambi dhidi ya Mungu. Agostino alieleza ya kwamba wakati mwingine vita ni halali, na kama ni halali ni wajibu wa Mkristo pia. Maelezo haya yalitumiwa baadaye na watawala na wanasiasa Wakristo kwa kuhalalisha vita vya kila aina.

Lakini sehemu nyingine ya urithi huo wa Agostino imebaki: kazi ya kanisa kuzitetea haki za kibinadamu, hata dhidi ya serikali inayoweza kugandamiza haki hizo. Kwa mfano ndiyo makanisa yaliyopinga sana siasa ya ubaguzi wa rangi Marekani na Afrika ya Kusini, hata dhidi ya serikali zilizoutetea. Vilevile ni makanisa yanayotetea haki za wakimbizi katika nchi nyingi hata kama serikali zimeshachoka mzigo wa kupokea wageni maskini kutoka nchi zingine.

[hariri] Maandishi yake makuu

[hariri] Maandishi kuhusu maisha yake

  • Confessiones (Maungamo) 397-398 - anamoeleza maisha yake pamoja na njia yake ya imani. Ni kitabu ambacho baada ya Biblia kilisomwa zaidi katika Karne za Kati
  • Retractationes (Masahihisho) 426-428 - anamopitia maandiko yake ya awali akitaja mifano jinsi alivyobadilisha mawazo na hoja zake

[hariri] Maandishi juu ya falsafa na teolojia

  • De Musica (kuhusu muziki)
  • De civitate Dei (Mji wa Mungu) 413 - 426
  • De Trinitate (Kuhusu Utatu) 400-416 - andiko lake kubwa lenye vitabu 15
  • De doctrina christiana (kuhusu mafundisho ya kikristo) 397-426
  • De libero arbitrio (kuhusu nia huru)
  • De beata vita (kuhusu maisha mema) -- kuhusu raha na kumjua Mungu
  • De magistro (juuy a mwalimu) -- mafundisho kuhusu umuhimu wa lugha
  • De vera religione (kuhusu dini ya kweli) -- kuhusu imani ya kikristo
  • Soliloquia (mazungumzo na nafsi) -- kuhusu uwezo wa akili ya kujijua
  • De immortalitate animae(kuhusu roho isiyokufa)

[hariri] Marejeo kwa Kiswahili

  • MT. AUGUSTINO, Kanuni– tafsiri ya Mapadri Waaugustino – ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Peramiho 1992 – ISBN 9976-67-059-1
  • M. CULLEN, O.S.A., Maungamo ya Mtakatifu Augustino kwa Muhtasari – tafsiri ya E. Msigala, O.S.A. - ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Ndanda – ISBN 9976-63-643-1
  • M. CULLEN, O.S.A., Mtakatifu Monika: Mlinzi wa Akina Mama Wakristu – tafsiri ya E. Msigala, O.S.A. - ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Ndanda 2002 – ISBN 9976-63-641-5

[hariri] Vyanzo vingine

g Saint Augustine, pages 30, 144; City of God 51, 52, 53 and The Confessions 50, 51, 52
  • Nelson, John Charles (1973). "Platonism in the Renaissance", Dictionary of the History of Ideas 3. New York: Scribner, 510–15 (vol. 3). ISBN 0684132931. “(...) Saint Augustine asserted that Neo-Platonism possessed all spiritual truths except that of the Incarnation. (...) 
  • Brown, Peter (1967). Augustine of Hippo. Berkeley: University of California Press. ISBN 0-520-00186-9. 
  • Matthews, Gareth B. (2005). Augustine. Blackwell. ISBN 0-631-23348-2. 
  • O'donnell, James (2005). Augustine: A New Biography. New York: ECCO. ISBN 0060535377. 
  • Ruickbie, Leo (2004). Witchcraft out of the Shadows. London: Robert Hale, 57–8. ISBN 0709075677. 
  • Tanquerey, Adolphe (2001). The Spiritual Life: A Treatise on Ascetical and Mystical Theology. Rockford, IL: Tan Books & Publishers, 37). ISBN 0895556596. 
  • von Heyking, John (2001). Augustine and Politics as Longing in the World. Columbia: University of Missouri Press. ISBN 0826213499. 
  • Lubin, Augustino (1659). Orbis Augustinianus sive conventuum ordinis eremitarum Sancti Augustini - chorographica et topographica descriptio. 
  • Pollman, Karla (2007). Saint Augustine the Algerian. Göttingen: Edition Ruprecht. ISBN 3897442094. 
  • Règle de St. Augustin pour les religieuses de son ordre; et Constitutions de la Congrégation des Religieuses du Verbe-Incarné et du Saint-Sacrament (Lyon: Chez Pierre Guillimin, 1662), pp. 28–29. Cf. later edition published at Lyon (Chez Briday, Libraire,1962), pp. 22–24. English edition, (New York: Schwartz, Kirwin, and Fauss, 1893), pp. 33–35.
  • Zumkeller O.S.A., Adolar (1986). Augustine's Ideal of the Religious Life. New York: Fordham University Press. ISBN 0823211053. 
  • Zumkeller O.S.A., Adolar (1987). Augustine's Rule. Villanova: Augustinian Press. ISBN 0941491064. 
  • Pottier, René (2006). Saint Augustin le Berbère (in French). Fernand Lanore. ISBN 2851572822. 
  • Fitzgerald, Allan D., O.S.A., General Editor (1999). Augustine through the Ages: An Encyclopedia. Grand Rapids: William B. Eerdmans Publishing Co.. ISBN 0-8028-3843-X. 
  • Plumer, Eric Antone, (2003). Augustine's Commentary on Galatians. Oxford University Press. ISBN 0-199-24439-1. 
  • Weiskotten, Herbert T. (2008). The Life of Saint Augustine: A Translation of the Sancti Augustini Vita by Possidius, Bishop of Calama. Merchantville, NJ: Evolution Publishing. ISBN 1-889-75890-6. 
  • Pagels, Elaine Adam, Eve, and the Serpent: Sex and Politics in Early Christianity Vintage Books (Sep 19 1989) ISBN 0679722327

[hariri] Viungo vya nje

Vifaa binafsi
Maeneo ya wiki

Vibadala
Vitendo
Urambazaji
Vifaa
Lugha zingine