Konstantino Mkuu
Kutoka Wikipedia
Konstantino Mkuu (jina kamili: Flavius Valerius Constantinus ; 27 Februari 272 – 22 Mei 337) alikuwa Kaisari wa Dola la Roma tangu mwaka 306 akitawala peke yake tangu 324. Anakumbukwa kama mtawala aliyefaulu kumaliza kipindi cha vita ya wenyewe kwa wenyewe na kukubali Ukristo kama dini huru katika dola. Alihamisha mji mkuu kutoka Roma kwenda Bizanti iliyoitwa baadaye Konstantinopoli.
Baba yake Constantius alikuwa mmojawapo wa makaisari wanne walioshirikiana pamoja katika utawala wa dola. Baada ya kifo cha baba jeshi lake likamtangaza Konstantino kuwa Kaisari pia lakini bila mawasiliano na wengine. Hata hivyo alikubaliwa kama Kaisari mdogo akihusika na majimbo ya Gallia na Britania.
Mwaka 311/312 fitina kati ya makaisari yalikuwa vita na Konstantino alilenga kupanusha himaya yake. Mpinzani wake alikuwa hasa Maxentius aliyekaa Italia. Konstantino aliweza kumshinda kwenye mapigano kwa daraja la Milvio karibu na Roma. Hapa alikuwa na ndoto alipoona msalaba wa Kristo katika jua akasikia sauti "Utashinda chini ya alama hii!". Baadaye vikosi vya Konstatino vilikuwa na bendera iliyoonyesha herufi za chi-rho ambazo zilimaanisha jina la "Kristo".
Ushindi huu ulimfanya Konstantino mkuu wa nusu ya magharibi ya Dola la Roma.
[hariri] Uhuru kwa Wakristo
313 alikutana na Licinius Kaisari wa mashariki ya dola. Pamoja makaisari wawili walipatana tamko la Milano lililotangaza mwisho wa mateso dhii ya Wakristo: "Baada ya kukutana hapa Milano sisi Kaisari Konstantino na Kaisari Licinius tumeamua kuwapa Wakristo pamoja na watu wote uhuru wa kuchagua dini yao ili Mungu wa mbinguni atupe fadhili zake."
Hadi mwaka 311 Wakristo waliteswa vikali kwa amri ya Kaisari Diokletiano. Konstatino alibadilisha siasa hii baada ya ushindi na kukubali Ukristo mara ya kwanza kama dini iliyokubaliwa rasmi akafaulu pia kupata kibali cha Kaisari mwenzake. Hakufanya Ukristo kuwa dini rasmi na yeye mwenyewe hakupokea ubatizo hadi kuwa mzee akabatizwa muda kidogo kabla ya kifo chake. Hakuna uhakika kuhusu sababu zake lakini inajulikana ya kwamba mama yake Helena alikuwa Mkristo lakini hakuna uhakika alikuwa na arhira gani katika ulezi wa mwanawe.
[hariri] Mtawala wa pekee
Tangu mwaka 316 Konstatino alianza kugongana na kaisari mwenzake wa mashariki Licentius baada ya huyu alionekana kusaidia mipango ya uasi dhidi ya Konstantino. 324 alimshinda na kumkamata akawa mtawala wa pekee.
Hapa aliamua mara moja kuhamisha mji mkuu kutoka Roma kwenda Bizanti. Alitumia pesa nyingi kwa ujenzi na kuiweka wakfu rasmi mwaka 330.
Aliratibu upya utawala wa dola akaweka misingi iliyoweza kudumu kwa miaka mingi hata baada yake. Hata hivyio alipaswa kutetea mipaka ya dola dhidi ya Wagermanik pia dhidi ya Waajemi.
[hariri] Konstantino na Kanisa
Konstantino alionekana mapema kama msaidizi wa Wakristo. Machoni pa Wakristo mageuko yale yalikuwa kama miujiza ya Mungu. Tangu Kaisari Nero (mnamo mwaka 60) mateso ya Wakristo yalikuwa yamerudia tena na tena. Sasa yalikwisha na Wakristo walipewa nafasi ya kusikilizwa na Kaisari mwenyewe.
Mwaka 321 Kaisari alitangaza jumapili kama "siku ya jua" kuwa sikukuu na ofisi za serikali zilipumzika.
Mwaka 325 alialika maaskofu wa kanisa la kikristoo kwa mtaguso wa Nikea. Mtaguso huu ulikuwa mkutano wa maaskofu wa kikristo kutoka pande mbalimbali za dola la Roma. Mkutano uliamua kuhusu maswali mablimbali ukakubali ungamo la Imani ya Nikea inyaoendelea kutumiwa kanisani hadi leo. Kwenye mkutano Konstantio alivutwa pia ndani ya fitina kati ya Wakristo hasa kuhusu Arius na mafundisho yake. Hapa Kaisari alishawishwa kuingilia kati kwa kumkataa mara Arius asiendelea kufundisha mara kumkataa mpinzani wake askofu Athanasius na kuwaamuru waondoke katika mji mkuu.
Kanisa la Kiorthodoksi lilimtangaza Konstantino kuwa mtakatifu.

