Askofu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Picha ya Timotheo, mmoja kati ya maaskofu wa kwanza, ilivyochorwa katika Nuremberg chronicles f 109v(1493).

Askofu ni mtu mwenye cheo cha juu katika Kanisa. Kwa kawaida huliongoza katika eneo la jimbo dayosisi akisimamia shirika au parokia nyingi.

Historia ya Cheo[hariri | hariri chanzo]

Episkopos katika Agano Jipya[hariri | hariri chanzo]

Neno letu "askofu" limetokana na Kiarabu أسقف "uskufu" ambalo ni umbo la Kiarabu la neno la Kigiriki επισκοπος "episkopos". Neno hilo katika mazingira ya Wakristo wa kwanza lilitumika kumtajia mwangalizi au msimamizi wa shughuli mbalimbali serikalini, katika shirika za wananchi au penye ujenzi.

Maandiko ya kwanza ya Agano Jipya yanayotumia neno hili ni nyaraka za Mtume Paulo, ambaye anataja kazi hii katika Fil. 1,1. Lakini hakuna "episkopos" katika 1Kor. 12,28 inayoorodhesha vyeo na kazi mbalimbali. Hii imechukuliwa na wataalamu wengi kama alama ya kwamba wakati huo kile cha "episkopos" hakikuwa bado cheo cha kawaida katika shirika zote.

1Tim. 3,1-7 na Tit. 1,7 zinataja "episkopos" lakini wengine hudhani ya kwamba nyaraka hizi zimeandikwa baada ya Paulo.

Katika Mdo. 20,28 wazee au viongozi wa ushirika wa Efeso waitwa "episkopoi" kwa jumla.

Haya yote yanachukuliwa wa wataalamu wengi ya kuwa wakati wa uandishi wa Agano Jipya cheo cha "askofu" hakikuwa bado cheo maalumu. Lakini katika shirika kadhaa alipatikana tayari kiongozi aliyekuwa na cheo cha juu kuliko wazee.

Episkopos kama cheo[hariri | hariri chanzo]

Neno episkopos linaonekana kama cheo katika maandishi ya mwisho wa karne I na mwanzo wa karne II kama vile waraka wa kwanza wa Klementi ambapo askofu aonekana kuwa kiongozi mkuu wa kanisa la mji fulani.

Katika upanuzi wa Ukristo madaraka ya askofu yalipanuka. Kadiri makanisa yalivyoenea hata nje ya miji na mashambani askofu akawa kiongozi wa eneo si wa mji tu.

Wakati ule ngazi za daraja zilionekana: Kanisa la mji au eneo likiongozwa na episkopos (askofu) anayeshauriana na "presbiteri" (kiasili: wazee; baadaye: makasisi) na kusaidiwa na mashemasi au madikoni.

Kanisa Katoliki na Waorthodoksi[hariri | hariri chanzo]

Wakatoliki na Waorthodoksi wana daraja takatifu ya Askofu, ambaye kwa kawaida ni mkuu wa kanisa katika ngazi ya dayosisi. Askofu ni baba wa makasisi (mapadri) na waumini katika eneo lake.

Maaskofu hukutana kwenye sinodi na kufanya maazimio kuhusu mambo ya kanisa lote.

Maaskofu wa nchi au eneo kubwa wako pamoja chini ya usimamizi wa Patriarki au wa Askofu mkuu.

Katika Kanisa Katoliki askofu wa Roma ni mkuu wa Maaskofu wote na wa Kanisa lote duniani akitajwa kwa jina la Papa.

Mafundisho ya mlolongo wa mitume[hariri | hariri chanzo]

Katika mapokeo hayo askofu hutazamwa kama mwandamizi wa Mitume wa Yesu. Katika mafundisho hayo Yesu Kristo mwenyewe aliwaweka mitume wake 12 kuwa viongozi wa kanisa lote na kuwapa madaraka. Madaraka hayo yalitolewa na mitume kwa kuwawekea mikono kichwani waandamizi wao waliopata hivyo kuwa maaskofu wa kwanza baada yao, nao wakafanya hivyo kwa waandamizi wao.

Kwa namna hiyo kuna mlolongo wa kuwekeana mikono kati ya wanaopokea nafasi ya uaskofu kuanzia mitume na kila kizazi cha maaskofu hadi leo. Hivyo maaskofu ni kiungo kati ya Yesu na waumini wa leo.

Askofu kati ya Waprotestanti[hariri | hariri chanzo]

Askofu Luwum wa Kanisa la Anglikana la Uganda aliyeuawa na Idi Amin.

Baadhi ya madhehebu ya Uprotestanti, hasa ya Anglikana, yana kiongozi anayeitwa askofu, lakini mamlaka yake ni tofauti na ile ya maaskofu wa Kikatoliki na wa Kiorthodoksi, kutokana na mtazamo tofauti sana kuhusu Kanisa na sakramenti. Kwa kawaida viongozi wa Kiprotestanti hawakuwekewa mikono katika mlolongo wa kimitume.