Kanisa Katoliki
Jina hilo linatumika hasa kumaanisha Kanisa la Kikristo linalokubali mamlaka ya kiroho ya Papa wa Roma kama mkuu wa Maaskofu juu yake lote.
Kanisa hilo linaamini kuwa ndani yake linadumu moja kwa moja Kanisa pekee lililoanzishwa na Yesu Kristo ambalo wanaunganishwa nalo wote wanaobatizwa katika madhehebu yoyote.
Tofauti kati yao ni kwamba baadhi (Wakatoliki) wana ushirika kamili nalo, wakati wengine (hasa Waorthodoksi na Waprotestanti) wana ushirika nalo kwa viwango mbalimbali, kadiri wanavyokubali mafundisho, sakramenti na uongozi wake.
Neno "katoliki" linatokana na kivumishi cha Kigiriki καθολικός (katholikòs), lenye maana ya «kamili, kadiri ya utimilifu». Tunalikuta kwa mara ya kwanza katika maandishi ya Ignas wa Antiokia kwa Wakristo wa Smirna mwanzoni mwa karne II: «Alipo Yesu Kristo ndipo lilipo Kanisa Katoliki» (Ad Smyrnaeos, 8).
Kati ya madhehebu ya Kikristo, Kanisa Katoliki linakusanya waamini 1,166,000,000, yaani nusu ya wafuasi wote wa Yesu, na 17.4 % ya binadamu wote, likiwa na asilimia kubwa ya waamini kati ya wananchi wa Amerika na Ulaya.
Kanisa Katoliki linaishi katika majimbo 2,945, ambayo kwa kawaida yanaongozwa na Maaskofu (kwa jumla wako 5,002) wakisaidiwa na mapadri (409,166) na mashemasi; kati ya hayo, mengi yanafuata utaratibu wa Kanisa la Kilatini, ila kuna mengine yanayofuata taratibu za makanisa katoliki ya mashariki.
Majimbo yanagawanyika katika parokia zinazoongozwa na padri anayeitwa paroko.
Kati ya waamini wana nafasi ya pekee wamonaki na watawa wengine ambao wanaishi kwa mitindo iliyostawi katika historia ya Kanisa ili kumfuata Yesu kwa karibu zaidi katika useja mtakatifu, ufukara na utiifu.
| Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kanisa Katoliki kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |