Wokovu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Wokovu kwa jumla unamaanisha kuondolewa hali isiyopendeza.

Kwa namna ya pekee, katika Ukristo Historia ya Wokovu ni wazo la msingi: maana yake ni kwamba katika mfululizo wa matukio Mungu anawakomboa binadamu kutoka dhambi zao na kutoka matokeo yake katika maisha ya duniani na katika uzima wa milele.

Biblia ya Kikristo inatamka kuwa neema ya Mungu ndiyo inayookoa watu, kwa kuwa hao hawawezi kujikomboa peke yao, lakini wanapokea wokovu kama zawadi kwa njia ya imani.

"Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu" (Waefeso 2:8).

Wokovu katika Agano la Kale [hariri]

Katika Biblia "wokovu" linatafsiri maneno mbalimbali yanayohusu kuondolewa mabaya ya kimwili na ya kiroho vilevile. Daima Mungu ndiye asili yake. Ndiye anayeokoa kwenye vita (Kutoka 15:2), ajali (Zaburi 34:6), mikono ya adui (2 Samueli 3:10), uhamisho (Zaburi 106:47), kifo (Zaburi 6:4), dhambi (Ezekieli 36:29).

Kwanza Waisraeli walifikiria hasa wokovu wa kidunia kwa taifa lao, lakini polepole kwa kuzingatia uovu, walifikia hatua ya kuona wokovu upande wa maadili na kuhusu mataifa mengine pia (Isaya 49:5,6; 55:1-5).

Kadiri yao, wokovu unapatikana kwa njia ya uadilifu uliotazamwa kama utekelezaji kamili ya Torati.

Wokovu katika Agano Jipya [hariri]

Maneno ya Kigiriki yanayotumiwa na Agano Jipya kumaanisha "kuokoa" na "wokovu" ni: σώζω (sōzō) e σωτηρία (sōtēria). Maana yake asili ni kuopoa kwa nguvu kutoka hatari (k.mf. ya ugonjwa).

Kwa kawaida Yesu alionyesha wokovu kuwa ni ukombozi kutoka dhambi ambao uanze kung'amuliwa mapema, ingawa utakamilika ahera: "Mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka" (Mathayo 10:22; 24:13).

Hasa Mtume Paulo alisisitiza wokovu ni tunda la kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, aliyeleta baraka zote kumpitia Roho Mtakatifu, kama vile wongofu, kuzaliwa upya, utakaso, kufanywa mwana, utakatifu na utukufu.

Ndiyo utatuzi wa tatizo la dhambi uliotolewa na Mungu.

Siku ya mwisho matokeo ya wokovu yatahusu ulimwengu wote ambao utajumlishwa pamoja na historia yote katika Kristo, aliye Alfa na Omega (Warumi 8:21,22; Waefeso 1:10).

Wokovu katika teolojia ya Kikristo [hariri]

Kutokana na mwelekeo wa watu wa magharibi, suala la mashari ya wokovu limeshika nafasi kubwa katika teolojia kuanzia Agostino wa Hippo, wakati masuala ya kinadharia zaidi yakiwatawala Wakristo wa mashariki.

Ni suala hilo lililosababisha Matengenezo ya kiprotestanti katika karne ya 16 na linaendelea kujadiliwa sana katika nchi zilipokea Ukristo kutoka nchi za magharibi.