Ndoa (sakramenti)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Ndoa kati ya wabatizwa wawili inahesabiwa na Kanisa Katoliki na Waorthodoksi kama mojawapo kati ya sakramenti saba zilizowekwa na Yesu Kristo.

Pamoja na Daraja takatifu ni kati ya sakramenti mbili za kuhudumia ushirika.

Fumbo la ndoa[hariri | hariri chanzo]

Kadiri ya mpango wa Muumba, ndoa halisi ina sifa tatu: umoja, uimara na utayari wa kuzaa. “Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, ‘Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja?’ Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe” (Injili ya Mathayo 19:4-6). “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, ‘Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha’” (Mwanzo 1:28). Mitara, uzinifu, talaka, ushoga na kukataa uzazi ni kinyume cha mpango huo.

Muungano usiovunjika mpaka kufa kati ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja waliobatizwa, ambao unafanyika kwa makubaliano yao ya hiari ambayo yanathibitishwa na Mungu anayewatia neema zinazohitajika waweze kutimiza malengo ya ndoa, ni ishara ya muungano wa kiarusi wa Yesu na Kanisa.

Yesu aliweka sakramenti ya ndoa kwa sababu ya umuhimu wa familia kwa ustawi wa mume na mke, watoto, jamii na ufalme wa Mungu, na kwa sababu ya uzito wa majukumu yanayohusika. “Siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwepo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake” (Injili ya Yohane 2:1-2), akaleta divai bora ya ndoa sakramenti badala ya ndoa ya kimaumbile. Hivyo ametuandalia neema tuweze kushinda “ugumu wa mioyo” (Mathayo 19:8) unaohatarisha daima uzuri wa mpango wa Mungu kuhusu upendo mwaminifu katika ndoa. “Mungu aliona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana” (Mwanzo 1:31).

Adhimisho la sakramenti ya ndoa[hariri | hariri chanzo]

Sakramenti za Wakatoliki na Waorthodoksi

Harusi ni wito wa maana sana katika Kanisa Katoliki. Vijana huhimizwa waoane maana Kanisa na jamii vinahitaji kuwa na vizazi vya kesho. Bila ndoa, hamtakuwa na mustakabali wa Kanisa wala jamii.

Ndoa ya Wakristo ni sakramenti ya Yesu na Kanisa lake. “Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi arusi, mke wa Mwanakondoo” (Ufu 21:9). Wakiwa na ndoa halisi, mume na mke waliobatizwa ni ishara wazi ya hao wanaarusi wawili wasioonekana. “Kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake” (Ef 5:24-25). Ndiyo sababu Mkatoliki hawezi kufunga ndoa bila ya kuhusisha Kanisa na kufuata taratibu zake.

Kwa kawaida Wakatoliki wanaiadhimisha wakati wa Misa, karamu ya arusi ya Mwanakondoo na Kanisa, lakini wanakubali Padre huwaleta pamoja bwana na bibi wawe kitu kimoja kilichofunganishwa kwa mapenzi. Yeye hutaka mashahidi na watu wote wasikie wakati maharusi wanachukua amri za kupendana maisha yao yote. Nao hupeana pete na kushangiliwa na wote waliojumuika kwa Misa. Kunako misa wakati huu, padre Sakramenti ya harusi hupewa hawa wawili maana wamekuwa kitu kimoja.

Hata hivyo, katika mazingira ya pekee ndoa ya Kikatoliki huweza kufungwa na wanaarusi mbele ya mashahidi wawili hata bila ya kuwepo padri [1].

Kumbe Waorthodoksi wanahesabu baraka ya padri kuwa sehemu ya lazima ya sakramenti, ambayo wanaarusi wanapewa.

Kubariki ndoa kwa Waprotestanti[hariri | hariri chanzo]

Martin Luther aliona sakramenti sharti iwe alama iliyowekwa na Yesu Kristo mwenyewe, lakini ndoa ni sehemu ya utaratibu wa uumbaji uliotangulia kuja kwa Yesu.

Kwa sababu hiyohiyo Waprotestanti wengi hawakubali ndoa kuwa sakramenti na wanabariki tu ndoa iliyofungwa kufuatana na sheria za dola.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]


Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ndoa (sakramenti) kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. Prayer of the Faithful Catholic Wedding. Jalada kutoka ya awali juu ya 2017-09-24. Iliwekwa mnamo 2017-10-20.