Utatu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Jina hilo la kiteolojia linatumika kufafanulia imani ya Wakristo wengi kwamba Mungu pekee, sahili kabisa, ni Nafsi tatu zisizotenganika kamwe: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kwa agizo la Yesu watakaomuamini wanatakiwa kubatizwa kwa jina la hao watatu (Mathayo 28:19).

Umoja wa Nafsi hizo unatokana na asili yake pekee, yaani Baba ambaye ndani mwake anamzaa milele Mwana kama mwanga toka kwa mwanga, kama Neno au Wazo lake (Hekima), tena anamvuvia Roho Mtakatifu kama Upendo ambao unamuunganisha na Mwana na kukamilisha umoja wao.

Kimsingi ni kwamba Mungu pekee anajifahamu na kwa kujifahamu anajipenda.

Imani hiyo ilizidi kufafanuliwa hasa katika karne IV, mitaguso mikuu ya kwanza ilipochukua msimamo dhidi ya wazushi waliokanusha umungu wa Yesu na wa Roho Mtakatifu. Ilipata muundo wa kudumu katika Kanuni ya Imani ya Nisea-Kostantinopoli inayotumika hadi leo katika madhehebu mengi.