Teresa wa Yesu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Mt. Teresa alivyochorwa na Pieter Paul Rubens
Livio Mehus, Mtakatifu Petro wa Alkantara akimkomunisha mtakatifu Teresa wa Avila; picha ya mwaka (1683) inayotunzwa Prato (Italia)
Teresa nje ya nafsi yake alivyochorwa na Gianlorenzo Bernini katika basilika la Santa Maria della Vittoria, Roma.

Teresa wa Yesu (Avila, Hispania, 28 Machi 1515 - Alba de Tormes, Hispania, usiku wa kuamkia tarehe 15 Oktoba 1582) ni jina la kitawa la Teresa Sánchez de Cepeda Ávila y Ahumada, maarufu pia kwa jina la Teresa wa Avila.

Mwanamke halisi, bikira, utu wake ulikomaa: alikuwa na tabia ya kupendeza, uchangamfu na busara sana, uhodari na msimamo, uwezo wa kukubali hali iliyopo akipanga vizuri na kufanikisha mambo.

Ni kati ya watu muhimu zaidi katika ya historia ya Kanisa ya karne ya 16, katika historia ya utawa na katika teolojia ya Kiroho kutokana na urekebisho aliouanzisha katika shirika la Wakarmeli (wanawake na wanaume vilevile) na kutokana na maandishi yake juu ya maisha ya kiroho yanayomfanya mwalimu wa sala aliye bora kuliko wote.

Alitangazwa na Papa Paulo V kuwa mwenye heri tarehe 24 Aprili 1614, na Papa Gregori XV kuwa mtakatifu tarehe 12 Machi 1622, na hatimaye na Papa Paulo VI kuwa mwalimu wa Kanisa tarehe 4 Oktoba 1970.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Oktoba.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Tangu utotoni, akisaidiwa na mfano wa wazazi wake, alionekana kuelekea sana maisha ya sala hasa upwekeni.

Alipofikia umri wa miaka 13, alifiwa mama yake, akatumwa kusomea shule ya bweni ya masista Waaugustino hadi alipoweza kukabili kazi ya kutunza familia ya baba yake.

Mpenzi wa kusoma vitabu vya mababu wa Kanisa, hasa Augustino na Gregori Mkuu, alipata wito wake wa kitawa kwa kusoma vile vya Jeromu.

Mwaka 1536, akiwa amefikia hakika ya kuitwa utawani, alijiunga na monasteri ingawa kwanza baba yake hakukubali.

Alipojiunga na monasteri ya Wakarmeli wa mji wake, alikuta juhudi za masista wamonaki zilikuwa za kiasi.

Mwenyewe, kisha kuweka nadhiri zake, aliamua kulenga ukamilifu, lakini kwa kukosa busara katika juhudi zake aliugua sana, ikambidi baba ampeleke kwa matibabu kwenye mji wa jirani, na hatimaye amrudishe nyumbani ili kusubiri kifo. Monasterini waliandaa kaburi, ila baba alikataa asizikwe.

Kumbe, baada ya siku nne za kupotewa kabisa na ufahamu, alianza kupata nafuu hata akaweza kurudi utawani, ingawa kwa muda fulani alikuwa amepooza tu.

Hatimaye, alipopona kabisa, alisema ni kwa maombezi ya Mt. Yosefu, ambaye tangu hapo alimheshimu sana.

Baada ya muda wa ulegevu, alipopoteza muda mwingi sebuleni, bila kujali maonyo ya muungamishi wake, aliguswa sana na sanamu iliyomuonyesha Yesu katika uhalisia wa mateso yake.

Tangu hapo (1555), Teresa alishika maisha magumu kabisa, akijitahidi kujikusanya peke yake mbele ya Mungu.

Baadaye aliishi karibu miaka mitatu katika nyumba ya mwanamke mjane mwenye ibada sana aliyeongozwa na Wajesuiti.

Halafu mwaka 1560, pamoja na wenzake wachache, alitambua haja ya kutengeneza upya maisha ya Karmeli, na alijisikia kuitwa na Mungu kuongoza kundi lao, akaanza kazi yake kubwa ya urekebisho wa shirika kwa msaada wa Yohane wa Msalaba upande wa wanaume.

Mwaka 1562, baada ya kushinda shida mbalimbali, alianzisha monasteri ya kwanza ya urekebisho mjini Avila chini ya usimamizi wa Mt. Yosefu.

Ingawa alipaswa kusafiri na kushughulika sana ili kuanzisha monasteri mpya huko na huko, pamoja na kukabiliana na matatizo mengi makubwa, Teresa alifikia vilele vya maisha ya sala na kujaliwa neema nyingi za pekee.

Hiyo inashuhudiwa na maandishi yake, yaliyokusudiwa kufundisha hasa masista wenzake, na ambayo ni kati ya vitabu bora vya Kanisa Katoliki:

Humo inaonekana wazi kwamba juhudi za Kikristo ni hasa kupokea na kuitikia kazi ambayo Roho Mtakatifu anaifanya ndani ya mtu kuanzia ubatizo ili kumlinganisha na Yesu.

Mafundisho yake hayakutokana na vitabu alivyosoma, bali na mang’amuzi yake binafsi pamoja na uchunguzi wa yale ya wengine. Ndiyo maana si ya nadharia tu, bali hasa yanafafanua kinachotokea, yakiingia mpaka ndani ya nafsi.

Kati ya semi zake maarufu zaidi, kuna maneno haya: “Usivurugwe na lolote, usitishwe na lolote. Yote yanapita, Mungu habadiliki. Subira inapata yote. Aliye na Mungu hakosi lolote. Mungu tu anatosha”. (Shairi, 9)

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

 • Maisha yake mwenyewe (Autobiografia), yaliyoandikwa baada ya mwaka 1567 chini ya padri Pedro Ibáñez, muungamishi wake;
 • Safari ya ukamilifu (Camino de perfecciòn), iliyoandikwa vilevile baada ya mwaka 1567 chini ya muungamishi wake;
 • Jumba la ndani, Makao (Castillo interior, Las Moradas), kitabu chake bora, kilichoandikwa mwaka 1577, ambamo anafananisha mtu wa sala na jumba lenye vyumba 7 vinavyofikiwa kimoja baada ya kingine kadiri ya maendeleo ya kiroho;
 • Ripoti, nyongeza ya kitabu cha maisha yake kwa mtindo wa barua juu ya mang'amuzi yake ya ndani na ya nje;
 • Mawazo ya upendo
 • Mishangao
 • Barua (342 nzima na sehemu 87 za nyingine).

Kulinganisha maandishi yake na yale ya Yohane wa Msalaba[hariri | hariri chanzo]

Tangu tusome mara ya kwanza maandishi ya Teresa wa Yesu na Yohane wa Msalaba, ni rahisi tutambue tofauti ambazo zimesisitizwa mara nyingi. Zinatokana na tofauti za mitazamo yao.

Teresa alitegemea mang’amuzi yake binafsi, akidokeza neema za pekee alizojaliwa (njozi n.k.) asiwe makini kuzitofautisha na mambo yaliyo ya lazima katika “makao saba” ya jumba la Kiroho. Hivyo alitia maanani kuliko wengine matukio ya kihisi, ya nje na ya ziada yanayoweza yakaendana na sala ya kumiminiwa; vilevile alisisitiza kuzingatia ubinadamu wa Yesu.

Yohane pia alisema kwa mang’amuzi yake binafsi na ya watu aliowaongoza, lakini hakuyataja, akijitahidi kuyachimba kiteolojia, jambo ambalo ni muhimu ili kutofautisha yaliyo ya kawaida na yaliyo ya ziada. Alieleza sababu za hali mbalimbali za sala kwa mafundisho juu ya maadili ya Kimungu na ya vipaji vya Roho Mtakatifu vinavyoendana nayo.

Kwa mtazamo huo alizingatia yaliyo ya lazima katika safari ya kuelekea utakatifu, hasa matakaso ya Kimungu yanayohitajika kwa usafi kamili wa upendo. Hivyo hakuelekea kujali neema za pekee zinazoendana pengine na sala ya kumiminiwa, wala hakusisitiza kuzingatia ubinadamu wa Yesu, akilenga moja kwa moja shabaha kuu ya sala, yaani Mungu aliyemo mwetu, tunayemfikia katika giza la imani kwa njia ya ujuzi ambao anatumiminia na unafanana na mang’amuzi.

Kwa kufanya hivyo amekamilisha maandishi ya Teresa na kutusaidia tuyaelewe.

Hata hivyo, chini ya tofauti hizo kuna msingi mmoja, kwa kuwa Teresa alijua vya kutosha mang’amuzi ya wafuasi wake aweze kuelewa na kueleza nini inatokea kwa kawaida kwa watu wanaopitia hayo makao saba. Tukitumia maelekezo aliyoyatoa huko na huko tunaweza kubainisha zaidi yaliyo ya lazima na yaliyo ya ziada.

Kimsingi watakatifu hao walielewa vilevile sala ya kumiminiwa, muungano na Mungu unaotokana nayo, na matakaso ya Kimungu yanayohitajika ili kuufikia ule kamili.

Ikifaa kuonyesha tofauti zao, inafaa zaidi kuonyesha wanavyolingana na kutambua teolojia inavyoweza kusaidia katika masuala hayo magumu.

Sala zake[hariri | hariri chanzo]

Bwana wangu, je, hukuweza kujumlisha yote katika neno moja na kusema, “Baba, utupe yote tunayoyahitaji”?

Kwa yule anayejua yote vizuri kabisa, inaonekana haihitajiki zaidi.

Lo, hekima ya milele! Kwako na kwa Baba yako hiyo ingetosha, na kweli ndivyo ulivyosali katika bustani la Getsemane: ulionyesha matakwa na hofu yako, lakini ukajiachilia kwa matakwa yake.

Hata hivyo kwa kuwa unajua hatuko tayari kama wewe, Bwana wangu, kutii matakwa ya Baba yako, ilikubidi ubainishe vizuri maombi, tuweze kuona kama tunayoyaomba yanatufaa, na tujizuie kuomba tukiona haitufai.

Kwa sababu ndivyo tulivyo kwamba, tusipopewa tunayotamani, kwa hiari yetu tunayakataa tunayopewa na Bwana, hata yakiwa mambo bora.

Kwa kuwa hatujioni matajiri mpaka tushike fedha mikononi.


Bwana wangu, kwa hakika saa niliyoitamani sana hatimaye imefika.

Kwa hakika wakati wa sisi kuonana umefika.

Bwana na mwokozi wangu, kwa hakika huu ni wakati wa mimi kuchukuliwa kutoka uhamisho huu niwe nawe milele.

Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.

Usinitenge na uso wako, wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Ee Mungu, uniumbie moyo safi.

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

 • Teresa of Avila, "The Book of Her Life" (Translated, with Notes, by Kieran Kavanaugh, OCD and Otilio Rodriguez, OCD. Introduction by Jodi Bilinkoff). Indianapolis/Cambridge: Hackett Publishing Company, 2008. ISBN 978-0-87220-907-7
 • "The Delighted Angel" drama about Teresa of Ávila and Rabija al-Adavija by Dževad Karahasan, Vienna-Salzburg-Klagenfurt, ARBOS 1995.
 • "The Interior Castle (Edited by E. Allison Peers)," Doubleday, 1972. ISBN 978-0-385-03643-6
 • "The Way of Perfection (Translated and Edited by E. Allison Peers)," Doubleday, 1991. ISBN 978-0-385-06539-9
 • "The Life of Teresa of Jesus: The Autobiography of Teresa of Avila (Translated by E. Allison Peers)," Doubleday, 1991. ISBN 978-0-385-01109-9
 • "Teresa of Avila: An Extraordinary Life", Shirley du Boulay, Bluebridge, 1995 ISBN 978-0-9742405-2-7
 • "Teresa: Outstanding Christian Thinkers," Rowan Williams, Continuum, 1991. ISBN 0-8264-5081-4
 • "The Eagle and the Dove" Saint Teresa of Avila and Saint Thérèse of Lisieux. by Vita Sackville-West. First published in 1943 by Michael Joseph LTD, 26 Bloomsbury Street, London, W.C.1

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]