Bernardo wa Clairvaux

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Picha ya zamani ya Bernardo wa Clairvaux
Filippino Lippi, Bikira Maria kumtokea Mt. Bernardo wa Clairvaux

Bernardo wa Clairvaux (Fontaine-lès-Dijon, Ufaransa, 1090 - Ville-sous-la-Ferté, Ufaransa, 20 Agosti 1153) alikuwa abati na mwenezaji mkuu wa urekebisho wa Citeaux wa shirika la Benedikto wa Nursia.

Ndiye mtu muhimu zaidi wa karne ya 12 katika Kanisa Katoliki, ambalo linamheshimu kama mtakatifu (alitangazwa na Papa Alexander III mwaka 1174) na mwalimu wa Kanisa (alitangazwa na Papa Pius VIII mwaka 1830).

Ni msimamizi wa wakulima.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 20 Agosti.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Nyumba alimozaliwa Bernardo
Bernardo akihimiza kwenda vitani

Bernardo alikuwa mtoto wa tatu kati ya saba waliozaliwa na Teshelino na Aleta, wote wa koo bora za watawala wadogo wa Borgogne (Ufaransa).

Alisoma kwa Wakanoni wa Nôtre Dame de Saint-Vorles, karibu na Châtillon-sur-Seine.

Kisha kurudi katika ngome ya baba yake huko Fontaines, mwaka 1111 alitawa pamoja na ndugu zake 5 na jamaa na marafiki kadhaa katika nyumba ya Châtillon, mpaka mwaka uliofuata akajiunga pamoja na wenzake 30 na monasteri ya Cîteaux (karibu na Dijon), iliyoanzishwa miaka 15 ya nyuma na Roberto wa Molesmes. Kwa wakati huo ilikuwa chini ya Stefano Harding.

Mwaka 1115 alihamia pamoja na wamonaki wenzake 12 katika mkoa wa Champagne, walipozawadiwa shamba kubwa karibu na mto Aube, wakaliita Clairvaux, yaani bonde angavu.

Alifaulu kuunganisha sala na masomo na utendaji mkubwa.

Kwa muda mfupi Abasia ya Clairvaux ikawa kivutio kikubwa kwa miito ya utawa hata ikaweza kuanzia mwaka 1118 kutuma wamonaki kuanzisha sehemu nyingine kama vile huko Trois-Fontaines, Fontenay, Foigny, Autun, Laon; Bernardo alipokufa abasia za urekebisho wa Citeaux zilikuwa 343, ambazo 66 kati yake zilianzishwa au kurekebishwa naye, kutoka Hispania hadi Siria, kutoka Italia visiwani hadi Uswedi.

Mbali ya kuwa mahali pa kuishi kidini, zilikuwa pia vyuo vya kilimo na ufundi.

Maisha yake yote Bernardo akawa mtetezi shujaa wa imani sahihi na wa mamlaka ya Kanisa.

Alipatanisha Wakristo (na watawala wao) waliokuwa wanagombana. Vita vya msalaba vya mwaka 1147 vilifanikiwa kuungwa mkono na watu wa Ufaransa na Ujerumani kutokana na mahubiri yake.

Mwishoni mwa mwaka 1152 alikuwa ameishiwa nguvu, lakini alisafiri hadi Metz ili kutuliza fujo za mji huo.

Aliporudi Clairvaux, akafa tarehe 20 Agosti 1153.

Njia ya sala ya Bernardo[hariri | hariri chanzo]

Bernardo hakuelekea ujuzi unaotokana na mantiki, bali ule unaopatikana kwa kuzama katika mafumbo kwa sala ya kujaliwa. Kwake ndiyo njia pekee ya kumfahamu kweli Mungu na kufikia amani na heri ya kuwa naye.

Hivyo, akipinga teolojia ya shule iliyokuwa inaanzaanza, alishikilia mapokeo ya Biblia, ya mababu wa Kanisa, ya liturujia na ya umonaki.

Aliandika vitabu vingi vya ufafanuzi wa Biblia, ambamo unajitokeza upendo hai uliomuongoza maishani kama alivyoandika, “Upendo ndio nguvu kuu ya maisha ya kiroho”.


Sala yake[hariri | hariri chanzo]

Bwana, mema yangu ni kukaa katika tabu, mradi wewe uwe nami.

Ni bora kuliko kutawala pasipo wewe, kula karamuni pasipo wewe, kujitukuza pasipo wewe.

Bwana, mema yangu ni kukukumbatia wewe katika tabu, kuwa nawe katika tanuri, kuliko kubaki pasipo wewe, hata kama ingekuwa mbinguni.

Kwangu kuna nini zaidi mbinguni, nami natamani nini zaidi ya wewe duniani?

Moto unatakasa dhahabu na jaribio la tabu linatakasa waadilifu.

Humo, Bwana, u pamoja nao; humo unakaa kati ya wale waliokusanyika kwa jina lako, kama zamani na vijana watatu.

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

 • De consideratione libri quinque ad Eugenium III
 • De diligendo Deo
 • De gradibus humilitatis et superbiae
 • De Gratia et libero arbitrio
 • De laude novae militiae ad Milites Templi
 • De laudibus Virginis Matris
 • Contemplatio Passionis
 • Expositio in Canticum Canticorum
 • Meditatio super fletus Virginis
 • Sermones
 • Sermones de tempore
 • Sermones super Cantica Canticorum
 • Epistola ad Raymundum dominum Castri Ambuosii
 • Sermo de miseria humana
 • Tractatus de interiori domo seu de conscientia aedificanda
 • Varia et brevia documenta pie seu religiose vivendi
 • Visio contemplativa

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]