Mavazi
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mavazi huvaliwa na watu kwa kusudi la kufunika mwili au sehemu zake. Mavazi huwa na kusudi mbalimbali:
- hukinga mwili dhidi ya baridi au jua kali pamoja na athira nyingine za mazingira zinazoweza kuathiri vibaya mwili uchi.
- huwasilisha ujumbe kwa watu wengine kwa kuonyesha mtu fulani ni sehemu ya kundi (k.m. jeshi, kanisa, mavazi ya kikabila) au tabaka (nguo ghali za mtajiri) au anapendelea jambo (nembo kwenye nguo).
Kimsingi nguo zinalingana na hali ya hewa na mazingira. Penye joto mavazi huwa nyepesi na penye baridi huwa nzito zaidi. Kila utamaduni umebuni aina yake ya mavazi. Historia inaonyesha pia ya kwamba tangu kale tamaduni mbalimbali zimepokea mavazi kutoka nje na kubadilisha mitindo yao. Hata kama katika majira ya utandawazi watu wanavaa nguo zilezile bado wanaweza kuzitumia tofauti.
Kuna mavazi ya aina nyingi kwa mfano ya kitambaa, nguo, sufi, ngozi au plastiki.
Vilevile mavazi hutofautishwa kama ni ya wanaume, wanawake au watoto, kama ni mavazi ya kikazi au ya nyumbani au ya sikukuu.
Tofauti nyingine kama ni mavazi ya chini au ya juu, au kama ni mavazi ya sehemu mbalimbali za mwili kama vile suruali, mashati, koti au viatu.
Utengenezaji na biashara ya mavazi ni sehemu muhimu ya biashara na kuna kazi nyingi zinazotegemea mavazi.
| Makala hiyo kuhusu "Mavazi" bado ni mbegu. Unaweza kusaidia kuikuza kwa kubofya kitufe kilichoandikwa "hariri". Ikiwepo makala kuhusu Mavazi kwa lugha nyingine, unaweza kuitafsiri kwa Kiswahili. |