Roberto Bellarmino

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Roberto Francesco Romolo Bellarmino (Montepulciano, wilaya ya Siena, nchini Italia, 4 Oktoba 1542 - Roma, Italia, 17 Septemba 1621) alikuwa mtawa wa Shirika la Yesu, halafu padri, askofu na kardinali wa Kanisa Katoliki anayeshika nafasi muhimu katika historia ya karne ya 16 na 17.

Alitangazwa na Papa Pius XI kuwa mwenye heri tarehe 13 Mei 1923, mtakatifu tarehe 29 Juni 1930 na mwalimu wa Kanisa tarehe 17 Septemba 1931.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 17 Septemba[1].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Dottrina cristiana breve, 1752

Utoto na ujana[hariri | hariri chanzo]

Roberto alizaliwa Montepulciano, wilaya ya Siena, Italia, tarehe 4 Oktoba 1542, katika familia kubwa, akiwa mtoto wa kiume wa tatu kati ya watano; wazazi wake walikuwa na asili ya kisharifu, lakini hali ya uchumi ilikuwa tofauti. Baba yake, Vincenzo Bellarmino, alikuwa jaji, na mama yake, Cinzia Cervini, alikuwa dada wa Papa Marcello II.

Tangu utotoni alikuwa na afya mbovu na mwelekeo mkubwa kwa mambo ya dini kama mama yake. Baada ya kupata malezi nyumbani, alitumwa Padova kwa masomo.

Alipofikia umri wa miaka 18, akifuata wito wake wa upadri, na kuvutiwa na mfano wa Ignas wa Loyola, aliamua kujiunga na Shirika la Yesu alilolianzisha, na tarehe 21 Septemba 1560 aliweka nadhiri zake za kwanza.

Badala ya kujivunia undugu wake na Papa, alidumu kuwa na unyenyekevu na bidii.

Alisomea Roma tangu mwaka 1560 hadi 1563, halafu alianza kufundisha Firenze na Mondovì, katika shule za shirika lake.

Mwaka 1567 alianza kusoma kwa mpango teolojia huko Padova, lakini kutokana na sifa yake kama mhubiri, mwaka 1569 mkuu wa shirika, Fransisko Borja, alimtuma Louvain (leo katika Ubelgiji), kwenye chuo kikuu maarufu cha mji huo. Ndipo alifahamu kwa karibu Uprotestanti na kuanza kujitokeza hasa katika mabishano na Walutheri na Wakalvini.

Ufundishaji[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kupewa upadrisho huko Gand tarehe 25 Machi 1570, alibaki Louvain miaka sita kama mwalimu wa teolojia na mhubiri, akizidi kupata wanafunzi na wasikilizaji kutoka kila upande.

Mwaka 1576 Papa Gregori XIII alimuita Roma afundishe hoja dhidi ya uzushi, kama alivyofanya hadi mwaka 1586, Akiandika vitini ambavyo baadaye vikaunda kitabu “Controversiae” (“Mabishano”), ambacho kilisifiwa mara kwa utajiri, uwazi na msingi wa kihistoria katika kutoa msimamo wa Kikatoliki juu ya Ufunuo, Kanisa, sakramenti na neema. Humo alisisitiza muundo wa Kanisa, kama ilivyohitajiwa na hali tete ya imani wakati huo, asisahau roho yake inayohuisha kwa ndani muundo huo. Pia alikwepa kushambulia Waprotestanti, akikazia kutetea mafundisho ya Kanisa kwa hoja za akili na za mapokeo.

Mtaguso wa Trento ulikuwa umemalizika tangu miaka, na Kanisa Katoliki lilikuwa bado na haja ya kujiimarisha kielimu na kiroho. Kazi ya Roberto iliingia moja kwa moja katika juhudi hizo za Urekebisho wa Kikatoliki.

Kuanzia mwaka 1588, akiwa kiongozi wa kiroho wa Wajesuiti wanafunzi wa Collegio Romano, alishirikiana na Papa Sixtus V, ingawa huyo hakumpenda sana yeye wala shirika lake. Kati ya vijana aliowalea huko, maarufu zaidi ni Alois Gonzaga, ambaye alifariki mwaka 1591 kutokana na tauni aliyoambukizwa na mtu aliyemuokota barabarani.

Baada ya kushughulikia kesi ya kumtangaza mwenye heri, aliomba azikwe karibu naye, kama ilivyotokea baadaye.

Tangu mwaka 1592 hadi 1594 alikuwa gombera wa seminari hiyo, halafu mwaka 1595 akawa mkuu wa shirika katika kanda ya Napoli.

Ukardinali[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1597 Papa Klementi VIII alimrudisha Roma kama mshauri wake katika masuala ya teolojia n.k.

Miaka ya 1597-1598 alitunga katekisimu kubwa na ndogo, ambazo ziliathiriwa na mazingira ya mabishano kati ya madhehebu ya Kikristo, na kuenea sana hadi mwisho wa karne XIX. Mchango wake huo katika malezi ya vizazi vipya vya Kikatoliki ulimstahilia sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Tarehe 3 Machi 1599 Papa alimteua kuwa kardinali akieleza kwamba, "Kanisa la Mungu halina mwingine sawa naye katika elimu". Bellarmino alijaribu kwa kila njia kumfanya Papa abadili uamuzi, lakini mwishoni alilazimika kukubali. Pamoja na hayo, hakuacha maisha yake magumu, na mapato ya cheo hicho aliyaelekeza karibu yote kwa maskini.

Kama kardinali aliongoza idara mbalimbali za Papa na, baada ya kupewa uaskofu tarehe 21 Aprili 1602, akawa Askofu mkuu wa jimbo la Capua (1602-1605), alipojitokeza kwa bidii yake ya kuhubiri katika kanisa kuu, kwa kutembelea parokia kila wiki, kwa sinodi 3 za jimbo alizoendesha na kwa kuanzisha mtaguso wa kanda.

Alikuwa anajua kujilinganisha na watu wa kawaida, nao walifurahia usahili wa mtu msomi kiasi hicho.

Baada ya kushiriki uchaguzi wa Papa Leo XI na wa Papa Paulo V, aliitwa tena Roma kushughulikia idara mbalimbali, lakini pia alitumwa kama balozi huko Venezia na Uingereza akatetee haki za Kanisa.

Mzigo wa majukumu na ubovu wa mazingira havikumsahaulisha juhudi kwa ajili ya utakatifu aliodaiwa na hadhi yake kama mtawa na askofu, akimlenga Yesu ili kumjua, kumpenda na kumuiga kwa dhati. Kwake ilikuwa furaha kubwa kujikusanya kwa utulivu na unyofu asali na kumzingatia Mungu.

Miaka ya mwisho alitunga vitabu mbalimbali kuhusu maisha ya Kiroho alipokusanya matunda ya mazoezi yake ya kiroho ya kila mwaka, kama vile “Akili Kupanda kwa Mungu”, “Ufundi wa Kufa Vema” na “Mlio wa Njiwa”. Humo inajitokeza hisia yake kubwa ya wema usio na mipaka wa Mungu, ambaye alijisikia mwanae mpendwa.

“Ee roho, mfano wako ni Mungu, uzuri usio na mipaka, mwanga usio na kivuli, uangavu unaopita ule wa mwezi na jua… Yeyote anayempata Mungu, amepata yote, yeyote anayemkosa Mungu amekosa yote”.

Katika kuhimiza kwa nguvu urekebisho wa Kanisa, kuanzia wakleri hadi walei, alielekeza kwanza wongofu wa moyo kadiri ya mafundisho ya Biblia na ya watakatifu.

Alifariki Roma tarehe 17 Septemba 1621.

Sala yake[hariri | hariri chanzo]

Kaburi la Roberto Bellarmino ndani ya Kanisa la Mt. Ignas wa Loyola kwenye Campo Marzio huko Roma

Wewe, Bwana, u mwema, umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili, kwa watu wote wakuitao; nani hatakutumikia kwa moyo wote baada ya kuanza kuonja walau kidogo utamu wa mamlaka yako ya Kibaba?

Unawaagiza nini watumishi wako, Bwana?

Unasema, Jitieni nira yangu. Na nira yako ikoje?

Unasema, Nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.

Nani hatabeba kwa moyo radhi kabisa nira isiyobana bali inapendeza, na mzigo usiolemea, bali unainua?

Kwa hiyo umeongeza kwa haki, Nanyi mtapata raha nafsini mwenu.

Na ikoje nira yako hiyo ambayo haichoshi, bali inapumzisha?

Kwa hakika ndiyo amri ya kwanza tena kuu, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote.

Nini ni rahisi, nono na tamu kuliko kupenda wema, uzuri na upendo?

Na hayo yote ndiwe wewe, Bwana Mungu wangu.

Nawe unafikia hatua ya kuahidi tuzo kwa wale wanaoshika sheria zako, ingawa tayari zenyewe ni za thamani kuliko dhahabu nyingi, na tamu kuliko sega la asali?

Ndiyo, unaahidi kweli tuzo, tena tuzo kubwa mno.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

Opera Omnia zilizokusudiwa kukusanya maandishi yake yote zilitolewa Cologne (1617), Venezia (1721), Napoli (1856), Paris (1870).

Kati ya yale muhimu zaidi kuna haya yafuatayo: Mabishano:

  • Disputationes de Controversiis Christianae Fidei adversus hujus temporis hereticos
  • De Exemptione clericorum na De Indulgentiis et Jubilaeo, ambayo yaliingizwa baadaye katika De Controversiis
  • De Transitu Romani Imperii a Graecis ad Francos
  • Responsio ad praecipua capita Apologiae [...] pro successione Henrici Navarreni
  • Judicium de Libro quem Lutherani vocant Concordiae
  • Responsio Matthaei Torti ad librum inscriptum Triplici nodo triplex cuneus
  • Apologia Bellarmini pro responsi one sub ad librum Jacobi Magnae Britanniae Regis
  • Tractatus de potestate Summi Pontificis in rebus temporalibus, adversus Gulielmum Barclay

Katekesi na maisha ya kiroho:

  • Dottrina Cristiana Breve
  • Dichiarazione Più Copiosa Della Dottrina Cristiana
  • Dichiarazione del simbolo
  • Admonitio ad Episcopum Theanensem nepotem suum quae sint necessaria episcopo
  • Exhortationes Domesticae
  • Conciones habitae Lovanii
  • De Ascensione mentis in Deum
  • De Aeterna felicitate sanctorum
  • De gemitu columbae
  • De septem verbis Christi
  • De arte bene moriendi

Ufafanuzi wa Biblia na mengineyo:

  • De Scriptoribus ecclesiasticis
  • De Editione Latinae Vulgatae, quo sensu a Concilio Tridentino definitum sit ut ea pro authenticae habeatur
  • In omnes Psalmos dilucida expositio

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]