Hekalu la Yerusalemu
Hekalu la Yerusalemu lilikuwa kitovu cha ibada za Uyahudi wakati wa Israeli ya Kale.
Kwa jumla kulikuwa na majengo mawili yaliyofuatana kwenye mlima wa hekalu mjini Yerusalemu.
Imani ya Kiyahudi inategemea kujengwa kwa hekalu la tatu pamoja na kuja kwa Masiya wakati ujao.
Katika imani hiyo sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu ndani ya hekalu palikuwa mahali ambapo Mungu mwenyewe aligusa dunia.
Yaliyomo |
[hariri] Hekalu la kwanza
Hekalu la kwanza lilijengwa na mfalme Suleimani kuanzia mwaka 957 KK. Hekalu hilo lilichukua nafasi ya hema ya kukutania iliyotunza vifaa vya ibada za Kiyahudi tangu siku za kale (iliaminiwa tangu Musa).
Hekalu hilo lilikuwa mahali pa pekee palipotazamiwa kuwa sehemu halali kwa ibada za sadaka.
Hata hivyo kuna taarifa, hasa katika sehemu za zamani za Biblia, kuhusu ibada kwenye "mahali pa juu" (yaani juu ya milima) zilizolaumiwa kama ishara ya imani potofu baada ya urekebisho wa mfalme Yosia uliofanya hekalu la Yerusalemu pekee kuwa halali.
Hekalu hilo la Suleimani lilibomolewa mwaka 587 KK wakati Nebukadreza II wa Babeli alipovamia Yerusalemu na kuharibu mji mzima.
[hariri] Hekalu la Pili
Baada ya ushindi wa Waajemi juu ya Babeli (mwaka 539 KK) mfalme Koreshi aliwaruhusu Wayahudi kujenga upya hekalu.
Kitabu cha Ezra katika Biblia kinasimulia habari hizi.
Ujenzi ulifuata mpango wa hekalu la kwanza na ulifanyika mahali palepale Yerusalemu kwenye "mlima wa hekalu".
Katika hekalu hilo la pili sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu ilikaa bila ya kitu ndani yake, kwa sababu Sanduku la Agano lilipotea tangu kubomolewa kwa hekalu la kwanza.
Hekalu liliharamishwa na mfalme Antioko IV mwaka 169 KK alipoweka hapa sanamu ya mungu wa Kigiriki Zeus.
Hatua hiyo ilisababisha upinzani wa Wamakabayo waliorudisha ibada ya Kiyahudi hekaluni na hadi leo sherehe ya Hanuka inakumbusha kutakaswa kwa hekalu.
[hariri] Matengenezo chini ya Herode
Mnamo mwaka 21 KK mfalme Herode Mkuu aliamuru matengenezo ya hekalu.
Wataalamu wengi huona ya kwamba matengenezo yalifanana na ujenzi mpya wa hekalu lililopambwa na kuongezeka.
Kwa kawaida hekalu linalotajwa katika Agano Jipya ni hilo la Herode.
Mwaka 70 jeshi la Dola la Roma lilivamia Yerusalemu na kubomoa hekalu.
Kuta za msingi zilibaki na ukuta mkubwa wa magharibi unasimama hadi leo, ukijulikana kama Ukuta wa Maombolezo wa Wayahudi.
[hariri] Baada ya kuharibika kwa hekalu
Waroma walijenga hapohapo hekalu kubwa kwa mungu wao Jupiter lililobomolewa baada ya ushindi wa Ukristo katika Dola la Roma.
Mara mbili kulitokea majaribio ya kujenga tena hekalu la Kiyahudi: mara ya kwanza chini ya Kaisari Julian Apostata, na mara ya pili wakati wa uvamizi wa Uajemi kwenye vita dhidi ya Bizanti mnamo 614 lakini majaribio yote yalishindikana.
Waislamu walipovamia Yerusalemu walikuta mlima wa hekalu kama mahali pa maghofu tu wakajenga hapa msikiti.
Leo hii kuna majengo ya Kiislamu ya msikiti wa Al Aqsa pamoja na Kubba ya Mwamba.
Ukuta wa magharibi wa hekalu la Herode unaoitwa Ukuta wa Maombolezo ni patakatifu pa Wayahudi.