Ukulu mtakatifu
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ukulu mtakatifu au Ukulu wa Kitume ni hasa kiti maalumu alichowekewa Papa katika Kanisa kuu la Roma, ambacho ni ishara ya mamlaka ambayo Wakatoliki wanasadiki anayo ya kufundisha, kutakasa na kuongoza Taifa la Mungu kokote duniani.
Yaliyomo |
[hariri] Katika imani ya Kikatoliki
Kwa msingi huo, unamwakilisha kama kiongozi wa Kanisa Katoliki na kuhusiana na dogma ya kwamba Papa ana karama ya kutodanganyika anapofundisha "rasmi" (kwa Kilatini "ex cathedra", yaani "kutoka ukulu") kama mkuu wa kundi la maaskofu.
[hariri] Katika liturujia
Sikukuu yake inaadhimisha kila mwaka tarehe 22 Februari kwa jina la Ukulu wa Mtume Petro, anayeaminiwa kuwa ndiye aliyewarithisha Mapapa mamlaka yake kama mkuu wa Mitume.
[hariri] Katika sheria za Kanisa
Kadiri ya Mkusanyo wa Sheria za Kanisa la Kilatini (kanuni 361), "Ukulu mtakatifu" ni jina rasmi linalotumika kuwamaanisha Papa na miundo yote inayomsaidia kuongoza Kanisa Katoliki duniani yakiwa na makao makuu mjini Roma.
[hariri] Ukulu usipokuwa na Papa
Wakati Kanisa linapobaki halina Papa (kutokana na kifo au kujiuzulu), uongozi unashikwa na Kundi la Makardinali ambalo pia lina wajibu na haki ya kumchagua mwandamizi wake.
[hariri] Katika mafungamano ya kimataifa
Ukulu mtakatifu una hadhi ya nafsi ya kisheria katika sheria za kimataifa kutokana na umbile lake, mapokeo ya historia na mahitaji ya utume wake.
Ukulu mtakatifu unawakilisha kwa pamoja Kanisa Katoliki na nchi huru ya Mji wa Vatikani (ambayo iko chini ya mamlaka yake) katika mafungamano ya kimataifa na nchi yoyote duniani na miundo ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa.
[hariri] Ukulu mtakatifu na Vatikani
Kisheria, Ukulu mtakatifu ni tofauti na Mji wa Vatikani ambayo ni nchi huru inayotawaliwa na Papa.
Eneo dogo la nchi hiyo (kilometa mraba 0.44) linadaiwa na kutosha ili kuhakikisha uhuru wa miundo ya Kanisa katika kutekeleza majukumu yake.
Mabalozi wanaowakilisha nchi nyingine wanatumwa kwa Ukulu mtakatifu, si kwa Vatikani.