Utoto wa Yesu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mozaiki ya Bikira Maria Eleusa, Athens, Ugiriki.
Mfululizo wa kurasa juu ya Yesu
Jesus
Yesu Kristo na Ukristo

Umwilisho  • Utoto wa Yesu  • Ubatizo
Arusi ya Kana • Utume wa Yesu • Mifano ya Yesu  • Miujiza ya Yesu
Kugeuka sura • Karamu ya mwisho • Msalaba wa Yesu  • Maneno saba
Kifo cha Yesu  • Ufufuko wa Yesu
Kupaa mbinguni  • Ujio wa pili
Injili  • Majina ya Yesu katika Agano Jipya  • Yesu kadiri ya historia  • Tarehe za maisha ya Yesu • Kristolojia

Mazingira ya Yesu

Wayahudi • Kiaramu • Bikira Maria • Yosefu (mume wa Maria) • Familia takatifu • Ukoo wa Yesu • Ndugu wa Yesu • Yohane Mbatizaji

Mitazamo juu ya Yesu

Mitazamo katika Agano Jipya · Mitazamo ya Kikristo • Mitazamo ya Kiyahudi • Mitazamo ya Kiislamu • Yesu katika sanaa

Utoto wa Yesu unamaanisha maisha ya Yesu tangu azaliwe hadi alipokuwa na umri wa miaka 12, kwa sababu Wayahudi walihesabu miaka 13 kuwa mwanzo wa wajibu wa kushika Torati yote.

Katika Agano Jipya[hariri | hariri chanzo]

Injili nne zilizomo katika Agano Jipya zina habari chache juu yake katika miaka hiyo. Sanasana ni zile za Mathayo na Luka ambazo kila mojawapo ina sura mbili za kwanza kuhusu Yesu kuzaliwa na kuanza kukua:

Ni katika tukio hilo la mwisho kwamba alijitokeza kama mwenye hekima ya pekee akijiona Mwana wa Mungu, si wa Yosefu hasa.

Katika Injili ya Mathayo[hariri | hariri chanzo]

1:18 Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 19 Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. 20 Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. 22 Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema,

23 Tazama, bikira atachukua mimba,

Naye atazaa mwana;

Nao watamwita jina lake Imanueli;

Yaani, Mungu pamoja nasi.

24 Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe; 25 asimjue kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU.

2:1 Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2 Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. 3 Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. 4 Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? 5 Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii,

6 Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,

Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda;

Kwa kuwa kwako atatoka mtawala

Atakayewachunga watu wangu Israeli.

7 Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota. 8 Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie. 9 Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. 10 Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. 11 Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. 12 Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.

13 Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. 14 Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; 15 akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema,

Kutoka Misri nalimwita mwanangu.

16 Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi. 17 Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema,

18 Sauti ilisikiwa Rama,

Kilio, na maombolezo mengi,

Raheli akiwalilia watoto wake,

Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako.

19 Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, 20 akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. 21 Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli. 22 Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya, 23 akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo.

Katika Injili ya Luka[hariri | hariri chanzo]

2:1 Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. 2 Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. 3 Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. 4 Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; 5 ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. 6 Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, 7 akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.

8 Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. 9 Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. 10 Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; 11 maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. 12 Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe. 13 Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema,

14 Atukuzwe Mungu juu mbinguni,

Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.

15 Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. 16 Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. 17 Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. 18 Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. 19 Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. 20 Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.

21 Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.

22 Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, 23 (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), 24 wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. 25 Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. 26 Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. 27 Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, 28 yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,

29 Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako,

Kwa amani, kama ulivyosema;

30 Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,

31 Uliouweka tayari machoni pa watu wote;

32 Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa,

Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.

33 Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. 34 Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. 35 Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.

36 Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. 37 Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. 38 Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.

39 Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti. 40 Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

41 Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. 42 Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; 43 na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. 44 Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; 45 na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. 46 Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. 48 Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. 49 Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? 50 Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. 51 Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.

52 Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Katika vitabu vya baadaye[hariri | hariri chanzo]

Kumbe vitabu vingine vilivyoandikwa baadaye, kuanzia karne ya 2, kama vile Injili ya Yakobo, vinasimulia mengi, ila hayana hakika au hayaaminiki kabisa. Inaonekana lengo la habari hizi mpya lilikuwa kumuonyesha mtoto Yesu akifanya miujiza kuanzia umri mdogo.

Kati yake labda maarufu zaidi ni ile ya kwamba alifinyanga vindege kwa udongo na hatimaye kufanya viruke alipoulizwa kwa nini anafanya kazi ya namna hiyo siku ya Sabato.[1]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Roten, J. and Janssen, T., "Jesus as a Child". Jalada kutoka ya awali juu ya 2014-05-13. Iliwekwa mnamo 2014-07-27.
Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Utoto wa Yesu kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.