Isa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Isa katika Uislamu)
Isa kwa Kiarabu

Isa ni umbo la jina Yesu katika Qurani na pia katika lugha mbalimbali zilizoathiriwa na Uislamu. Ukurasa huu unahusu imani ya Uislamu kumhusu Yesu kadiri ya Kurani.

Kitabu hicho kilichoandikwa miaka 600 hivi baada ya Kristo kina aya 93 zinazomhusu, lakini hakileti mfululizo wa habari za maisha yake wala za mafundisho yake maalumu.

Ingawa Waislamu wanakiri pia vitabu vitakatifu vya Torati, Zaburi na Injili, katika ibada wanatumia Kurani tu na kwa kawaida ndiyo chanzo chao cha habari juu ya watu na matukio ya kabla yake.

Kwao nabii Isa ni mtume anayeaminiwa kuwa mmojawapo wa mfululizo wa mitume na manabii watukufu 124,000 wa Mwenyezi Mungu walioletwa ulimwenguni kuwapasha wanadamu ujumbe wa umoja wake, ili wamuabudu Yeye peke yake akiwa ndiye Muumba na Mruzuku wao hapa duniani.

Mitume na Manabii hao wameletwa katika zama mbalimbali na kwa watu, kaumu na umma mbalimbali, na mfululizo huu ulianza na Adamu, baba wa wanadamu wote, hadi Mtume Muhammad akiwa ndiye wa mwisho.

Isa ni miongoni mwa mitume wakubwa ambao Mwenyezi Mungu amewasifu kwa subira yao na ustahimilivu wao mkubwa: Manabii Nuhu na Ibrahimu na Musa na Isa na Muhammad. Tena ni miongoni mwa Mitume waliopewa Kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kiitwacho Injili. "Masihi Isa bin Mariamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Neno lake tu alilompelekea Mariamu, na ni Roho iliyotoka kwake" (sura ya 4 aya 171). Wakristo wanamuita kwa kawaida Yesu Kristo.

Kuzaliwa kwake[hariri | hariri chanzo]

Nabii Isa alizaliwa na bibi Maryam kimuujiza, kwani alizaliwa bila ya baba kwa amri ya Mola wake ambaye alimtuma malaika Jibril kumtangazia kupata kwa mtoto mtukufu.

Baada ya kuzaliwa, Nabii Isa, alisema utotoni mwake akiwa bado mchanga, ukiwa ni muujiza mwingine kwa watu ili kuwaonyesha kuwa yeye si mtoto wa kawaida, na kuwa mama yake hana dhambi ya kuja kwake bila ya baba.

Huo ni mfano mmoja katika mifano minne ya uumbaji aliyotuonyesha Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu alimuumba Adamu bila ya baba wala mama, na akamuumba Hawa bila ya mama, na akamuumba Isa bila ya baba, na akaumba wanadamu wote waliobakia kutokana na baba na mama.

Habari za kuzaliwa kwake Nabii Isa zinapatikana katika Kurani, surat "Maryamu" (19) kuanzia aya 16 - 35.

Na mtaje Maryamu katika Kitabu, pale alipojitenga na jamaa zake mahali upande wa mashariki. Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea Roho wetu, akajifananisha kwake sawa na mtu.(Maryamu) akasema: Hakika mimi najikinga kwa Mwingi wa Rehema aniepushe nawe, ukiwa ni mcha Mungu. (Malaika) Akasema: Hakika mimi ni mwenye kutumwa na Mola wako ili nikubashirie tunu ya mwana aliyetakasika. Akasema: Nitampataje mwana hali mwanamume yeyote hajanigusa, wala mimi si kahaba? (Malaika) akasema: Ni kama hivyo! Mola wako Mlezi amesema: Haya ni mepesi kwangu! Na ili tumfanye kuwa ni Ishara kwa watu, na Rehema itokayo kwetu, na hilo ni jambo lililokwishaamuliwa. Basi akachukua mimba yake, na akaondoka nayo mpaka mahali pa mbali. Kisha uchungu ukampeleka kwenye shina la mtende; akasema: Laiti ningelikufa kabla ya haya, na nikawa niliye sahaulika kabisa! Pakatangazwa kutoka chini yake: Usihuzunike! Hakika Mola wako amejaalia chini yako kijito kidogo cha maji! Na litikise kwako hilo shina la mtende, utakuangushia tende nzuri zilizo mbivu. Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Na pindi ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu. Akenda naye (mwanawe) kwa jamaa zake amembeba. Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu! Ewe dada yake Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba.
Akawaashiria (mtoto). Wakasema: Vipi tumsemeze aliye bado mdogo yumo katika mlezi? (Mtoto) akasema: Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Amenipa Kitabu, na amenifanya Nabii. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai, Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu. Na amani iko juu yangu siku niliyo zaliwa, na siku nitakayo kufa, na siku nitakayo fufuliwa kuwa hai. Huyo ndiye Isa mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Subhanahu, Yeye ametakasika! Anapolihukumia jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa.

Ujumbe wake[hariri | hariri chanzo]

Nabii Isa aliletwa kwa wanadamu kufikisha ujumbe kwao wa kuwafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja, hana mwenzake, na kuwa Yeye pekee ndiye mwenye kustahili kuabudiwa kwa haki. Ujumbe huu ndio ujumbe uleule uliotumwa kwa Mitume na Manabii wote kwa wanadamu ili kuwaongoza, naye alikuja kutilia mkazo na kusisitiza jambo hili na kuzipa nguvu tume za Mitume na Manabii waliopita.

Kadiri ya sura ya 3 aya ya 50 alisema ni "msadikishaji wa yale yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na ili niwahalalishieni baadhi ya yale mliyoharimishiwa, na nimewajieni na Ishara kutoka kwa Mola wenu, kwa hiyo mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii".

Alitabiri kuwa baada yake atakuja Mmoja ambaye atawafundisha wanadamu ukweli wote na kuwaongoza kwenye haki na kuwaeleza kila wanalolihitaji katika maisha yao. Ujumbe wake ulikuwa ni wa mwisho kabla ya ule wa Mtume Muhammad ambao ndio wa mwisho kabisa kwa wanadamu wote.

Kitabu cha Nabii Isa[hariri | hariri chanzo]

Mwenyezi Mungu ameleta Mitume na Manabii wengi ulimwenguni, lakini alichagua baadhi yao na kuwateremshia vitabu vya uongozi na sharia na hekima kwa wafuasi wao. Katika vitabu vilivyoteremshwa kwa Manabii mbalimbali ni Taurati kwa Nabii Musa, Zaburi kwa Nabii Daudi, Injili kwa Nabii Isa, na Qurani kwa Nabii Muhammad. Kitabu cha Nabii Isa kiliteremshiwa Wayahudi ambao ndio walengwa wake wa kwanza wa Nabii Isa, kama ilivyothibitishwa na Qurani wakati aliposema:

Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria Mtume atakayekuja baada yangu jina lake ni Ahmad! Lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio wazi!

Miujiza ya Nabii Isa[hariri | hariri chanzo]

Nabii Isa alipewa na Mwenyezi Mungu miujiza mbalimbali kumsaidia katika kazi yake ya kutangaza dini ya Mwenyezi Mungu, kwani ilikuwa kawaida kwa Mtume au Nabii kuonyesha miujiza kwa watu au kaumu yake ili awathibitishie kuwa yeye kweli ni mjumbe aliyeletwa na Mola wa ulimwengu huu. Mitume waliotangulia kabla ya Nabii Isa, kama Nuhu na Ibrahim na Musa na wengineo wote walikuja na miujiza mbalimbali.

Baadhi ya miujiza ya Nabii Isa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ni kuumba ndege kutokana na udongo, kuponyesha vipofu wakaweza kuona, na kuwaondoshea ukoma wale wenye ukoma, na kuhuisha mtu aliyekufa, na kuwateremshia wafuasi wake chakula kutoka mbinguni ili iwe ni dalili kwao wote.

Imani ya Kikristo kuhusu Isa[hariri | hariri chanzo]

Muhammad alikuta Wakristo au Manasara wakiwa wamehitilifiana katika imani yao kuhusu Nabii Isa, kwani wote walimkiri kuwa Mwana wa Mungu, lakini kwa wengi hii ilikuwa na maana kuwa yeye ni Mungu aliyejifanya mtu, isipokuwa wachache walitafsiri tofauti.

Makundi ya namna hiyo yalitengana baada ya Nabii Isa kuondoka ulimwenguni na kuwaachia wafuasi wake waendeleze kazi yake ya kutangaza dini ya Mwenyezi Mungu. Wafuasi waliokuja baada ya wale kumi na mbili waliokuwa pamoja naye, walitoa fikra na mawazo yao kuhusu Isa, hivyo baada ya muda waligawanyika makundi mbalimbali.

Kurudi kwa Nabii Isa[hariri | hariri chanzo]

Waislamu pamoja na Wakristo wanaamini kuwa Isa atarudi tena ulimwenguni kukamilisha kazi yake aliyoiacha baada ya kupaa kwenda kwa Mola wake, na haya yanaelezwa katika vitabu vya dini vya Kiislamu na vya Kikristo, lakini wanahitilifiana kuhusu namna na njia aliyoondokea ulimwenguni.

Waislamu wanasema kuwa Isa alichukuliwa na Mola wake na kupandishwa kwake mbinguni baada ya Wayahudi kutaka kumuua, na kwa hivyo hawakuweza kumuua wala kumsulubu. Wakristo kwa upande mwingine, wanaamini kuwa aliwahi kusulubiwa na kuzikwa kisha akafufuka siku ya tatu. Muhimu hapa ni kujua kuwa atarudi tena duniani kukamilisha kazi aliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Hivyo ni kweli kwamba imani kwa nabii Isa na kwa Yesu Kristo ni tofauti sana katika Ukristo na Uislamu.

Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.