Sabato

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Meza ya chakula cha kuanzisha Sabato ya Kiyahudi; mlo huanza kwa kubariki divai na mkate.

Sabato (kwa Kiebrania: שבת, shabbāt, yaani pumziko kwa Kiswahili) ni siku ya pumziko ya kila juma katika Uyahudi kwa ujumla na hasa katika nchi ya Israeli.

Desturi hiyo imesababisha simulizi la kitabu cha Mwanzo (1:1-2:4a) katika Biblia ya Kiebrania kuhusu jinsi Mwenyezi Mungu alivyomaliza kuumba mbingu na nchi kwa siku sita akaona vema kupumzika siku ya saba.

Wayahudi tangu kale wameona fahari kufuata mfano wa Mungu wakipumzika siku ya saba. Sabato husheherekewa kila Jumamosi kuanzia saa za jioni kwenye Ijumaa hadi jioni ya Jumamosi.

Kati yao, wale wanaofuata dini huanza kwa sala ya jioni kwenye sinagogi halafu kwa chakula cha pekee nyumbani.

Amri ya Sabato katika Biblia

Msingi wa utaratibu wa sabato katika Biblia uko hasa katika kitabu cha Kutoka sura ya 20:8-11 zinapoorodheshwa Amri Kumi alizopewa Musa juu ya Mlima Sinai:

Ikumbuke siku ya sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya sabato akaitakasa.

Amri hii ilichukuliwa kama amri ya kutofanya kazi yoyote bali kupumzika kabisa.

Sifa ya pekee ya amri hiyo ni sharti la kuwapa hata wafanyakazi na watumwa nafasi ya kupumzika, hasa inavyotajwa katika Kumbukumbu la Torati 5:12-15 ambamo sababu inayotajwa si uumbaji bali ukombozi ambao Mungu kwa njia ya Musa aliwatoa Waisraeli utumwani Misri. Hivyo amri hiyo inatazamwa kama sheria ya kwanza ya kutetea haki za wafanyakazi.

Kadiri ya Kutoka 31:13-17 adhimisho la Sabato lilitolewa na Mungu kwa Waisraeli kama ishara ya agano la kudumu kati yake na wao.

Mapokeo ya Talmudi

Tangu kale wataalamu Wayahudi wamejadili swali hili: je kazi ipi iko chini ya masharti ya amri ya Sabato. Majadiliano hayo yanaonekana hata katika maandiko ya Agano Jipya, kwa mfano pale ambapo Yesu aligongana na Mafarisayo kuhusu suala la uponyaji siku ya Sabato (Mk 3 na penginepo).

Wataalamu Wayahudi walijadiliana hadi kuorodhesha katika Talmudi aina 39 za shughuli ambazo ni marufuku siku ya Sabato. Kwa mfano ni marufuku kuwasha moto, kuandika, kutekeleza kazi yoyote kwa chombo, kununua au kuuza kitu, kugusa hela. Wayahudi Waorthodoksi hutunza masharti hayo hadi leo.

Wataalamu wameendelea kuangalia mapokeo ya Talmudi katika mazingira ya kisasa. Sharti la kutowasha moto limeendelezwa kwa kutowasha taa za umeme na hata kutobonyeza swichi yoyote siku ya Sabato. Lakini inaruhusiwa kutumia mitambo inayofuata saa au programu na kuwasha taa au mashine bila mtu kuigusa. Vilevile Wayahudi hao hawaendeshi gari kwa sababu kuwasha injini ni sawa na kuwasha moto.

Wayahudi huria hawachukui amri hiyo vikali vile. Kwa mfano Myahudi huria asingeandika chochote kinachohusika na kazi yake lakini hana shida kuandika barua isiyo ya kikazi. Atajaribu kuepukana na tendo la kununua kitu dukani lakini kama kuna haja atafanya hivyo.

Wayahudi wote wanafundisha ya kwamba sheria zote za Sabato zinaweza kuvunjwa kama uhai wa binadamu uko hatarini.

Wakristo na Sabato

Katika Ukristo adhimisho la Sabato limehamishiwa siku ya Jumapili, isipokuwa kati ya madhehebu madogo kama Waadventista Wasabato.

Chanzo cha badiliko hilo kinaonekana katika taarifa ya Matendo ya Mitume 20:7 inayoonyesha ya kwamba wakati wa Mtume Paulo Wakristo walikuwa wakikutana siku ya kwanza ya juma, yaani Jumapili. Sababu yake ilikuwa kukumbuka ufufuko wa Yesu aliyetoka kaburini siku hiyo ya kwanza. Tena aliendelea kuwatokea (Yoh 20:26-29) na kuwateremshia Roho Mtakatifu (Mdo 2:1-12) siku ya Jumapili. Vilevile Paulo aliwaandikia wanafunzi wake wa Wakorintho wakusanye mchango kwa ajili ya Wakristo fukara wa Yerusalemu kila Jumapili (1Kor 16:2); agizo hilo linafikiriwa kuwa limetokana na desturi ya kufanya ibada siku hiyo, si siku ya saba.

Agano Jipya halielezi badiliko hili lilitokeaje, lakini linahusianishwa na matukio mawili ya Kanisa katika karne ya 1:

  1. polepole Wakristo wa mataifa waliwapita wale wa Kiyahudi kwa idadi na bidii, nao kwa kuzingatia uamuzi wa mtaguso wa Yerusalemu (49) hawakujiona tena kupaswa mambo mengi ya Agano la Kale (Mdo 15:23-29);
  2. amani kati ya Wakristo na Wayahudi ilizidi kupungua, na baada ya maangamizi ya Hekalu la Yerusalemu (70 BK) hao wa mwisho waliwakataza hao wa kwanza wasiendelee kushiriki ibada zao sinagogini, hasa siku ya Sabato, hivyo hata Wakristo wa Kiyahudi wakajikuta katika hali tofauti na awali.

Barua kwa Wakolosai 2:16 inawahimiza Wakristo wa mji huo wasijisikie kubanwa na masharti ya Kiyahudi wala wasikubali kusumbuliwa na mtu yeyote kuhusu Sabato na siku nyingine za kalenda ya Kiyahudi.

Sababu kuu ya kiteolojia inayotajwa tangu mwanzo wa karne ya 2 (baada ya kipindi cha Biblia ya Kikristo kutungwa) ni kwamba ufufuko wa Yesu Kristo ulikuwa mwanzo wa uumbaji mpya na hivyo katika kipindi cha Agano Jipya ile sikukuu ya agano la kwanza haisimami tena. Kwa sababu hiyo Dominika kama Siku ya Bwana inaitwa siku ya nane, ambapo kwa kumfufua Yesu, Mungu alianza juma jipya la uumbaji mtukufu zaidi.

Siku za juma (wiki)
Jumapili - Jumatatu - Jumanne - Jumatano - Alhamisi - Ijumaa - Jumamosi
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.