Mtume Mathayo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mtume Mathayo
Mitume wa Yesu

Mathayo ni jina la mmojawapo kati ya Mitume wa Yesu anayeheshimiwa kama mtakatifu na Wakristo wengi sana, hasa kutokana na Injili yenye jina lake. Maana yake ni Zawadi ya Mungu. Labda aliitwa pia Lawi.

Kabla hajaitwa na Yesu Kristo amfuate, Mathayo alikuwa mtozaushuru, na kwa sababu hiyo alitazamwa na Wayahudi msaliti wa taifa na mkosefu. Hata hivyo Yesu alipomkuta forodhani alimuambia, "Nifuate" (Injili ya Marko 2:14). Ndipo Mathayo akaacha vyote akaanza kuwa mwanafunzi wake. Katika nafasi hiyo alimuandalia karamu kubwa waliyoishiriki watozaushuru wengi, hata kusababisha lawama toka kwa Mafarisayo.

Kuna ushahidi wa zamani kwamba aliwahi kuandika misemo ya Yesu kwa lugha ya Kiaramu. Kitabu hicho kilipotea mapema, na ni vigumu kusema kina uhusiano gani na Injili ya Mathayo iliyoandikwa moja kwa moja kwa Kigiriki fasaha.

Baada ya ufufuko wa Yesu, inasemekana Mathayo alieneza habari njema Ethiopia, ingawa masalia yake yanaheshimiwa huko Salerno (Italia) tangu mwaka 954.

Anaheshimiwa kama msimamizi wa watu wa benki, forodha, watunzahesabu n.k.