Nenda kwa yaliyomo

Ndugu Wadogo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Ordo Fratrum Minorum)
Mt. Fransisko na matukio ya maisha yake, mchoro wa karne ya 13.

Ndugu Wadogo ni jina la Wafransisko wa Utawa wa Kwanza. Hapa inaelezwa historia yao na jinsi walivyogawanyika katika mashirika mbalimbali.

Ndugu Wadogo kupambana hadi kutenganishwa (1226-1517)

[hariri | hariri chanzo]
"Uthibitisho wa Kanuni ya Kifransisko" kadiri ya Domenico Ghirlandaio (1449-1494), Cappella Sassetti, Florence, Italia.

Mwanzo wa mapambano (1226-1316)

[hariri | hariri chanzo]
Masalia ya Fransiko wa Asizi juu ya altare ya kanisa la chini ndani ya Basilika la Mt. Fransisko, Assisi.

Kifo cha Fransisko wa Asizi kiliwatia Ndugu Wadogo uchungu uliogeuka mapema kuwa mshangao wenye furaha nd. Elia Bombarone alipowaandikia juu ya ajabu la madonda matakatifu mwilini mwake lililobaki siri kwa wote, isipokuwa wachache.

Ajabu hilo lisingestahili kusisitizwa zaidi kama lisingekuwa na maana na matokeo makubwa kwa historia iliyofuata, hasa kwa sababu lilikuwa jipya: hivyo wengi waliona linamtambulisha mwanzilishi wao kama mtakatifu wa pekee aliyerudisha maisha ya Kiinjili ya Yesu ndani ya Kanisa; ilikuwa sawa na kusema hata shirika lake ni la pekee.

Kwanza alitafsiriwa kuwa Kristo wa pili, aliyelingana naye katika mengi, hivi kwamba hana mfano kati ya watakatifu na waanzilishi waliomtangulia.

Halafu alitafsiriwa kuwa malaika wa mhuri wa sita mwenye alama ya Mungu aliye hai (Ufu 7:2), yaani mtu aliyetabiriwa katika Biblia kuwa ataingiza historia ya wokovu katika hatua mpya. Tafsiri zote mbili zilitegemea madonda hayo kama alama ya pekee iliyomtambulisha pamoja na shirika lake.

Tukimchunguza kwa upana katika mazingira yake – ambayo upande mmoja alitokana nayo, na upande mwingine aliyaelekeza kwa nguvu njia mpya – tunaweza kuelewa sababu za msingi za mwangwi mkubwa aliousababisha kwa upya wa mtindo wa maisha yake, na kwa msimamo ambao aliutekeleza mpaka mwisho, akijua thamani na mvuto wa mfano alioutoa, lakini pia akitambua haja ya kundi lake dogo kugeuka shirika halisi la kitawa, lenye kanuni maalumu na miundo ya kufaa.

Ushahidi mkuu wa karama ya pekee ya Fransisko ni jinsi shirika lake lilivyoweza kustawi ajabu bila ya kutegemezwa na uongozi wa Kanisa Katoliki. Lakini uenezi huo wa kasi kwa wingi wa watu na kwa upana wa maeneo ulisababisha masuala mengi mazito kutokana na tofauti za hali na mazingira.

Alipokuwa bado hai, walio wengi kati ya wafuasi wake walimuona mara moja tu au hawakumfahamu kabisa. Hivyo hawakuweza kuelewa zaidi karama yake aliyoifuata kwa ari ambayo tangu aongoke ilikuwa imezidi tu.

Basi, kundi la Watumishi na wasomi wa utawa wake, likisaidiwa na viongozi wa juu wa Kanisa, lilimsonga ili alegeze masharti ya ufukara na kulinganisha zaidi shirika lake na yale ya zamani. Kwa karama yake ya pekee aliweza kukabili upinzani huo wote.

Juhudi yake ya mwisho ya kuzuia shirika lisipotoke ni wasia aliouandika ili kusisitiza msimamo wake, kudai kanuni yake isifafanuliwe, pamoja na kukataza wanashirika wasimuombe Papa hati yoyote.

Maelekezo aliyoyatoa humo ili kufafanua na kusisitiza utekelezaji bora wa kanuni yanaonyesha wazi alivyohisi hatari kubwa ya kuacha au walau kulegeza kipeo cha wongofu wake.

Lakini dalili mbalimbali zinaonyesha pia kwamba hakujidanganya kuhusu kesho. Kwa hisi yake ya hali halisi na ya mabadiliko yanayofuatana, pamoja na mang’amuzi ya maisha yake, alitaka hasa mfano wake na wa wenzake wa kwanza ubaki msingi imara wa kudumu, kama tukio la kukataa moja kwa moja mambo kadhaa ya zamani na la kuumua maisha ya kesho.

Kwa maana hiyo amebaki mhusika mkuu wa historia yote ya shirika: wingi wa vitabu vilivyoandikwa juu yake unatokana na haja ya ndugu zake wote kudumisha uhusiano naye ili kuathiriwa naye kwa namna moja au nyingine, kama ilivyojitokeza katika matawi mbalimbali.

Basi, ndani yake mwenyewe tunaona asili ya mvutano wa kudumu katika historia ya wafuasi wake na ya matawi yote yaliyojitokeza: kuwa na kielelezo kamili cha kufuatwa, lakini pia kukitekeleza kwa kuzingatia madai ya maisha, yaani kujitahidi mfululizo kulinganisha kipeo na hali halisi. Ndipo inapotokea katika historia yote ya Wafransisko ile hali ya kukosa utulivu, ile kani isiyo na mfano katika mashirika mengine yoyote, ambayo ni dalili ya uhai usiozimika.

Kwa sababu hizo ina umuhimu wa pekee karne ya kwanza ya Ndugu Wadogo, ambapo mfano wa mwanzilishi ulikuwa bado wa jirani na mchakato wa kuingia kikamilifu katika maisha ya Kanisa ulikuwa mgumu zaidi, kwa sababu muundo wake wenye miaka elfu na zaidi ulikabiliwa na magumu mengi ya ndani na ya nje.

Miaka michache baada ya kifo cha Fransisko, utawa wake ulijitokeza chachu bora ukapata sura maalumu katika mvutano wa kusisimua kati ya mapokeo, yaliyomzingatia zaidi mwanzilishi, na hali halisi za maisha zilizokuwa zinadai mabadiliko.

Miaka hiyo ilizidi kutokeza tofauti kati ya wale wachache walioshi karibu naye tangu mwanzo na kuambukizwa umotomoto wake, na wale wengi waliojiunga na shirika lililokwishafanikiwa.

Ilikuwa wazi kwamba, kwenye umati wa watawa, ni lazima kuzingatia sheria zaidi na zaidi; lakini wafanye nini ili wasiachane hivyo na nia ya mwanzilishi? Ndilo suala lililowachoma na kuwagombanisha.

Wanahistoria wa leo wanaweza kutambua kwa urahisi kuliko wao kwamba chemchemi ileile moja ilikuwa inabubujikia pande mbili ambazo kwa namna tofauti zikaja kuathiri kwa nguvu kubwa Kanisa la magharibi. Thamani yake inathibitishwa na wale wote waliochota kwa Fransisko na kwa wafuasi wake jambo hili au hili.

Miaka ya mwisho ya maisha yake, pamoja na kuzidi kuheshimiwa, alizidi pia kuonekana anazuia shirika lisifuate mkondo wa historia ndani ya Kanisa. Pamoja na kukiri utakatifu wake na wa karama yake asili, wengi waliona haja ya kuondoa kizuio hicho: ndiyo kazi aliyoikabili ndugu wa kwanza kuchaguliwa mwandamizi wa mwanzilishi baada ya kifo chake: nd. Yohane Parenti (1227-1232).

Uchaguzi wake unaonekana kuwa tokeo la tathmini makini juu ya mahitaji ya shirika: alikuwa mtu mkomavu (aliingia utawani pamoja na mwanae) ambaye alishiriki kwa jirani maisha asili ya Fransisko, lakini pia alipata mang’amuzi mengine kama Mtumishi wa Hispania. Hivyo aliweza kulinganisha mitazamo tofauti na kuchukua maamuzi ya kufaa akitegemea pia ujuzi wake wa sheria.

Tarehe 16 Julai 1228 alifurahia ibada ya fahari ya kumtangaza Fransisko kuwa mtakatifu, akimuachia nd. Elia kazi ngumu ya kumjengea kanisa ambalo lionyeshe alivyoheshimiwa na waamini wote.

Lakini ilimbidi pia kukabili masuala yote yaliyojitokeza shirikani kutoka nchi mbalimbali sana. Hasa lile la msingi lililozidi kusumbua ndugu wengi, kadiri walivyozidi kung’amua ugumu wa kutekeleza kanuni jinsi ilivyo bila ya kuifafanua kama ulivyodai wasia wa mwanzilishi.

Antoni wa Padua (1195 hivi - 1231) akimpakata Mtoto Yesu, mchoro wa Antonio de Pereda (1611 hivi - 1678)

Basi, yalizuka mabishano makali kati ya walioshikilia wasia huo na wale waliotaka shirika liweze kushindana na mashirika mengine. Yeye na Watumishi wengine kutoka kanda mbalimbali (mmojawao Antoni wa Padua) wakadhani utatuzi unaweza kutokea kwa Papa tu.

Akipokea ombi lao, Papa Gregori IX (1227-1241) alitoa tamko rasmi la kwanza juu ya kanuni (1230), akitumia mamlaka yake ya Kipapa na hasa ujuzi wake wa nia ya Fransisko (ndiye aliyemsaidia kutunga kanuni alipokuwa bado Kardinali, jina lake Ugolino).

Kuhusu wasia alitamka kuwa si sheria inayowabana Wafransisko wasiweze kufafanua kanuni yao wala kufafanuliwa na Kanisa, wala kuomba wala kupewa hati na fadhili za Papa. Sababu ya msingi ni kuwa Kanisa liko juu kuliko kanuni.

Kwa kukabili suala hilo kwa mtazamo wa sheria, alikata hamu ya mwanzilishi ya kuiona kanuni kama kituo cha kuanzia safari tu, si kituo cha mwisho. Kwa namna hiyo aliwaingiza zaidi Ndugu Wadogo ndani ya kawaida ya Kanisa.

Upande wa ufukara kwa jumla alitetea msimamo wa mwanzilishi (kwa jinsi alivyomheshimu hata akamtangaza mtakatifu karibu bila ya kesi), ila aliulegeza kiasi, kwa lengo la kufanikisha zaidi utume wa Ndugu Wadogo na hivyo kurekebisha Kanisa lililokuwa na hali mbaya kiroho.

Kwa ajili hiyo aliwapa pia hati na ruhusa nyingi za pekee dhidi ya mamlaka ya Maaskofu na maparoko. Hivyo njia ikawa wazi kuligeuza shirika la wadogo wanaohubiri toba kwa unyenyekevu chini ya padri yeyote, liwe shirika imara lililo chini ya Maaskofu kwa machache tu.

Mageuzi hayo, yaliyosababisha kwa muda mrefu upinzani mwingi wa Maaskofu na mapadri wanajimbo, yalichangiwa pia na ustawishaji wa elimu ndani ya shirika uliozidi kuwalinganisha Ndugu Wadogo na watawa wengine na kuongeza idadi ya mapadri kati yao.

Baada ya nd. Yohane Parenti alichaguliwa nd. Elia, ambaye awali aliteuliwa na Fransisko kuwa Mkuu wa utawa. Kwa wakati huo, jamaa ya kwanza ilipogeuka shirika halisi, alihitajika kiongozi mwenye msimamo na pengine ukali pia. Mt. Fransisko alijieleza kwamba hapendi kutesa, ingawa anaweza. Basi, akamuachia nd. Elia ambaye, mwanzilishi akiwa bado hai, alifuata maelekezo yake, ingawa alimueleza maoni yake pia kuhusu utungaji wa kanuni, hasa kwa lengo la kufanya iwezekane kwa kiongozi kudai utekelezaji wake.

Katikati ya vipindi viwili vya uongozi wake (1221-1227, halafu 1232-1239) alimjengea Mt. Fransisko kanisa zuri sana, halafu jirani nalo konventi kubwa mno, ili kushindana na abasia za Wabenedikto. Pia alionyesha ushindani fulani na nd. Yohane Parenti, hata akahamisha masalia yake bila ya kibali chake, akasababisha vurugu kutoka kwa Waasizi.

Ulijitokeza hivyo mvutano kati ya asili ya utawa huko Asizi na hali yake mpya ya kimataifa. Kwa kumchagua tena bradha huyo, shirika lililenga kuleta usuluhisho kati ya pande hizo mbili: si kurudia maisha ya awali, bali kuokoa usawa kati ya makleri na mabradha.

Nd. Elia alimgeuza mwanzilishi kuwa fahari ya shirika kuliko kielelezo cha kufuatwa. Mwenye vipawa na elimu, aliathiri sana viongozi wa dini (Gregori IX) na wa siasa (kaisari Federiko II), alistawisha misheni huko Mashariki na kukuza nyumba za masomo, lakini pia alidhulumu vikali watetezi wa kanuni.

Bila ya kuweza kutembelea kanda za shirika, alishika uongozi wote mikononi mwake, akichagua Watumishi na walinzi, akihamisha ndugu, akituma wawakilishi wake huko na huko wasimamie (pengine bila ya busara) kazi ya Watumishi, na akikataa kuwasikiliza na kuitisha mkutano mkuu.

Pamoja na hayo, fahari zake binafsi, ushuru aliowatoza mfululizo Watumishi (kwa ajili ya ujenzi n.k.), msisitizo wa kwamba kila ndugu ajishughulikie badala ya kusaidiwa na mabradha, vilisababisha hatimaye njama dhidi yake, hadi Gregori IX akaitisha na kuendesha mkutano mkuu ambao ulimuondoa madarakani na kutunga sheria za kupunguza mamlaka ya Mtumishi mkuu.

Badala yake alichaguliwa nd. Alberto wa Pisa (1239-1240), Mtumishi wa Uingereza, kanda ambayo kuliko zote ilikua mbali na Mt. Fransisko na kujali elimu. Ingawa alikufa baada ya miezi michache tu, uchaguzi wake ulionyesha kwamba maendeleo ya shirika, yaliyotakiwa na viongozi wa Kanisa na ndugu walio wengi, yataanza tena kusonga mbele moja kwa moja.

Kwamba maendeleo hayo yalikuwa kinyume cha nia asili ya mwanzilishi (walivyosisitiza wenzake na wengineo waliomfahamu vizuri) haikuwa kizuio kwa umati walioridhika kutekeleza amri za kanuni, kuwa mafukara kuliko watawa wengine na kuheshimiwa na waamini pia kwa niaba ya mzee wao aliyezidi kutazamwa mkuu ajabu.

Baada yake akachaguliwa nd. Aimoni wa Faversham (1240-1244), Mwingereza mwanateolojia aliyeongoza upinzani dhidi ya nd. Elia. Ndiye aliyelipatia shirika sura ya kudumu kufuatana na mfano wa Wadominiko upande wa muundo, utume, masomo na liturujia. Taratibu za maisha zikazidi kufuata mitindo ya kimonaki, pamoja na watawa kujitafutia visingizio vya kisheria wasibanwe nazo. Makao ya kifukara ya upwekeni yalizidi kuachwa ili wanashirika wahamie nyumba kubwa za mijini, zenye makanisa makubwa ambamo wafanye utume, wakiwanyang’anya maparoko waamini na sadaka zao.

Alikubaliwa na Gregori IX kwamba Watumishi wa kanda pia waweze kuruhusu ndugu wakahubiri. Kama alivyofanya mwenyewe huko Paris, Ndugu Wadogo wakazidi kushika nafasi kwenye vyuo vikuu na vinginevyo, na kuwa na uzito mkubwa ndani ya Kanisa, jambo lililowasogeza mbali na udogo uliowapasa.

Badala ya ndugu wote kuwa sawa, mabradha wakanyimwa kabisa nafasi za uongozi na kukubaliwa tu kutoa huduma ndogondogo za nyumbani (bustani n.k.), wakiwaachia raia huduma duni zaidi.

Kazi za mikono nje ya konventi zilikatazwa; badala yake ile ya kuombaomba ikaja kusifiwa na kushika nafasi ya kwanza upande wa uchumi. Zilipangwa pia njia za hakika za kupata mahitaji, hasa kwa nyumba za masomo.

Alipokufa, mvutano ndani ya shirika ulijitokeza kwa nguvu. Mtumishi mkuu aliyechaguliwa, nd. Kreshensi wa Iesi (1244-1247) akiona kwamba Fransisko alitazamwa bado na wote kuwa kielelezo cha wadogo, aliagiza mapema zikusanywe habari zote juu yake, halafu akamuagiza nd. Thoma wa Celano aandike upya maisha ya mwanzilishi.

Waliolilia hali ya awali (wenzi wa Mt. Fransisko na ndugu “wenye ari”) walipoona Mtumishi mkuu hakubaliani nao, walichagua wajumbe 72 wakajieleze kwa Papa Inosenti IV (1243-1254) ili aingilie kati. Lakini Kreshensi aliwasema kwa Papa na kumuomba awaadhibu; mwenyewe aliwatawanya wengine ili awavunje nguvu.

Papa, akiwa mwanasheria mwenye hakika kuhusu ukuu wa mamlaka yake, aliona kanuni ya Ndugu Wadogo, kama kanuni nyingine zote, ni sheria tu ambayo Papa anaweza kuifanyia lolote; vilevile aliona shirika lao kuwa kama mengine yote akalisukuma lizidi kutia maanani elimu. Hivyo alitoa (1245) tamko la pili juu ya kanuni ili kuilegeza: hasa alitamka kuwa vitu vyote ambavyo shirika linavyo, kama si vya wafadhili tena, basi ni vya Papa. Hivyo kwa kutofautisha kutumia vitu na kuvimiliki kisheria, Ndugu Wadogo waliweza kujidai mafukara ingawa wanatumia vingi, eti si vya kwao! Lakini wengi hawakuridhika na ujanja huo, usiolingana na roho ya Kiinjili ya Fransisko, wala na dhuluma za nd. Kreshensi dhidi ya ndugu wenye ari.

Basi, katika mkutano mkuu ulioagizwa na Papa walimuondoa madarakani wakamchagua Yohane wa Parma (1247-1257), mtu wa kufaa sana kwa elimu na utakatifu, aliyeongoza hasa kwa mfano wa maisha yake bora.

Kitu cha kwanza alifuta lawama na adhabu zote dhidi ya ndugu wenye ari. Halafu akatembelea kwa miguu kanda zote akiwa na kanzu moja tu tena kikuukuu na kuamsha nia ya kushika kanuni na wasia.

Ingawa aliwahi kufundisha katika vyuo vikuu vitatu, alikusudia hasa kurudisha shirika katika hali ya mwanzoni, kwa kukataa fadhili za Papa na kwa kuheshimu Maaskofu na mapadri. Hivyo mkutano mkuu (1254) ulisimamisha utumiaji wa fadhili kadhaa.

Lakini, alivyosema Egidi wa Asizi (+1262), juhudi hizo nzuri zilikuwa zimechelewa zisiweze kurekebisha shirika lote. Wapinzani walimshtaki Yohane kwa Papa, akalazimika kujiuzulu. Mkutano mkuu ulitaka aendelee, lakini mwenyewe hakurudi nyuma. Hatimaye aliombwa amchague mwandamizi wake, naye akamtaja Bonaventura wa Bagnoregio akaenda kuishi upwekeni kwa miaka 30, akikataa mara mbili ukardinali.

Bonaventura wa Bagnoregio (1221 - 1274), mchoro wa Claude François, 1650-1660 hivi.

Bonaventura aliweza kuongoza muda mrefu (1257-1274) kuliko waliomtangulia. Kufuatana na tabia na malezi yake (alijiunga na shirika huko Paris), yeye alikubali hali ilivyo na kujitahidi kuepusha shirika na hatari za nje na za ndani alizoziona mapema.

Upande wa ndani, kielelezo cha Fransisko kilitakiwa kuzingatiwa na wote kwa umoja, bila ya kupishana kuhusu namna ya kukitazama. Kwa ajili hiyo Mt. Bonaventura alitunga kitabu rasmi cha maisha yake kilichopitishwa na mkutano mkuu hata ukaagiza maandishi yote yaliyotangulia yateketezwe. Ndivyo shirika lilivyopotewa kwa muda mrefu na habari nyingi muhimu juu ya mwanzilishi.

Kitabu alichokiandika, bila ya kusema uongo, kinasisitiza mang’amuzi yake bora ya kiroho kwa kuficha mambo fulanifulani kuhusu kipeo cha udogo. Kinaleta baadhi tu ya matendo na mafundisho ya Fransisko yaliyochaguliwa kwa makini ili kumchora kama mfano kamili wa Kristo msulubiwa, na hasa kama yule malaika wa mhuri wa sita mwenye alama (madonda matakatifu) ya Mungu aliye hai aliyetabiriwa na Ufu 7:2 kuwa ataleta Injili ya milele, yaani kanuni yake!

Ndugu Wadogo walimuona hivyo mwanzilishi wao wakajiona ndio shirika jipya ambalo lilete Kanisa la Kiroho lenye kufuata ufukara kadiri ya unabii na mafundisho yaliyolaaniwa ya abati Yohakimu wa Fiore (+1202).

Mt. Bonaventura aliheshimu ufukara kama sifa kuu na utukufu wa shirika, ingawa alifurahia baadhi ya mabadiliko yaliyotokea. Kwake elimu pamoja na utume ni sehemu ya lazima ya utendaji wa Kifransisko ndani ya Kanisa. Kwa ajili hiyo alikubali bila ya wasiwasi matamko ya Mapapa juu ya kanuni kama ufafanuzi rasmi wa wachungaji wakuu wa Kanisa na wa shirika pia, pamoja na ruhusa walilolipatia shirika, ingawa kwa udogo alipenda kupatana na Maaskofu na maparoko.

Alijipangia kulinganisha uaminifu kwa kanuni na mabadiliko ya shirika, akionyesha hayo hayaendi kinyume cha nia ya mwanzilishi. Ili athibitishe hayo ilimpasa kuziondolea lawama msingi wowote kwa kuadhibu vikali waliovunja kanuni.

Basi, chini ya uongozi wake shirika likatulia, kwa jinsi alivyoweza kulinganisha upendo kwa Fransisko na furaha kwa mabadiliko, hamu ya kuishi upwekeni na utetezi wa konventi za mijini.

Kwa nje shirika likazidi kuheshimiwa na kushika nafasi katika maisha ya Kanisa (utume mbalimbali, uchaguzi wa Papa, Mtaguso mkuu). Lakini mafanikio hayo yalizidisha kiburi cha wanashirika na upinzani wa Maaskofu na maparoko dhidi yao.

Alipokuwa bado Paris huo ulikuwa umeungwa mkono na chuo kikuu: hapo hazikupingwa tu ruhusa kadhaa walizopewa Ndugu Wadogo na Wadominiko, bali msingi wenyewe wa mtindo wa maisha yao. Baada ya yeye na Thoma wa Akwino kuutetea, Papa alilaani upinzani na kusifu sana mtindo huo wa Kiinjili. Mwalimu huyo kuchaguliwa kuwa Mtumishi mkuu kukawa ushindi mwingine mkubwa chuoni.

Katika miaka yake ya mwisho ilimbidi tena kutetea shirika lake kwa maandishi pia.

Bonaventura akafa akiwa Kardinali askofu, wakati wa Mtaguso II wa Lyon, ambao ulihatarisha mashirika ya Ombaomba, lakini hatimaye ulipitisha tu hati ya kuyafuta yote isipokuwa Wadominiko na Wafransisko, pamoja na Waaugustino na Wakarmeli. Hata hivyo iliwabidi hao wapatane na wanajimbo kwa kujinyima baadhi ya ruhusa walizopewa.

Mapapa waliofuata wakaendelea kuwarudishia au kuwanyang’anya tena, mpaka Mtaguso wa Vienne (1311-1312) ulipofaulu kuwatungia sheria ya kudumu: kwamba kuhusu maisha yao ya ndani na uongozi wawe chini ya Papa moja kwa moja, ila kuhusu utume nje ya makanisa yao wawe chini ya Maaskofu na maparoko.

Watumishi wakuu waliofuata hawakujaribu kuacha nyayo za Bonaventura; hata ushindani ulipozuka tena ndani ya shirika, hakuna aliyethubutu kukanusha ubora wa kazi yake.

Hata hivyo mambo yakawa magumu kiasi kwamba suala la ndugu “wa Kiroho” (yaani wenye nia ya kushika kanuni kadiri ya Roho Mtakatifu) likawa zito kwa Kanisa lote. Wakati wa Mtaguso II wa Lyon, baadhi ya ndugu walijiandaa kukataa maagizo waliyoambiwa watapewa kinyume cha haki. Upinzani wao ukalipuka hasa baada ya Papa Nikola III (1277-1280) kutoa hati nyingine juu ya kanuni (1279) ili kuwaondolea Ndugu Wadogo wasiwasi wowote kuhusu namna ya kuitekeleza, pamoja na kuwatetea dhidi ya maadui wa nje.

Hati hiyo inafuata kabisa msimamo wa Bonaventura kuhusu matumizi ya kifukara kweli: Ndugu Wadogo hawana haki ya kutumia vitu, ila wanaruhusiwa kuvitumia kadiri ya ufukara na uduni.

Ingawa hati hiyo ilitungwa kwa busara sana, baada ya kamati kabambe kuiandaa kwa miezi miwili, utekelezaji wake ukaja kusababisha mabishano makubwa kwa miaka mingi, kuanzia Ufaransa Kusini na Italia ya Kati.

Mwakilishi bora wa msimamo mkali ni nd. Petro wa Yohane Olivi (+1298), aliyeunganisha pande hizo mbili tofauti: wa kwanza ulitegemea ujuzi mkubwa ukaathiri zaidi Kanisa kwa ufundishaji, uchungaji na uanzishaji wa jumuia za waamini zilizowaunga mkono; wa pili ulitegemea zaidi kumbukumbu chungu za wenzi wa Mt. Fransisko na matabiri juu ya dhuluma utawani ukaishia kuathiri shirika (hata kwa utunzi wa vitabu muhimu, hasa cha Ubertino wa Casale +1329), lakini pia kufanya umisionari mkubwa hadi India na kuuchochea kama sehemu ya uaminifu wao kwa kanuni.

Mabishano yalichangiwa na Mtumishi mkuu kukosekana muda mrefu au kulemewa na majukumu mengine kutoka kwa Papa.

Viongozi waliofuatana katika ngazi mbalimbali, mara walijaribu kukomesha vikali msimamo mkali, mara waliuunga mkono. Mapapa kadhaa walitumia nguvu, isipokuwa Papa Selestini V (1294), aliyetazamwa kuwa “Papa wa kimalaika” atakayeanzisha Kanisa la Kiroho. Yeye aliwaruhusu waliotaka wajitenge na “jumuia” (walivyojiita umati wa ndugu waliopenda maendeleo) wakaishi upwekeni wakifuata kanuni na wasia bila ya kujali matamko ya Kanisa. Ilikuwa mara ya kwanza kwa shirika kugawanyika.

Alipojiuzulu, mwandamizi wake Papa Bonifasi VIII (1295-1303) alifuta mara maamuzi yake yote, na katika miezi michache iliyofuata aliwaagiza hao Waselestini warudi shirikani, akamuondoa madarakani Mtumishi mkuu aliyewatetea, akamweka mwingine kinyume chao, akawakatalia wasikate rufaa kwake dhidi ya dhuluma.

Viongozi wao, nd. Liberato wa Fossombrone (+1307) na nd. Anjelo Klareno (+1337), walikimbilia Ugiriki wasije wakafungwa tena (waliwahi kukaa gerezani zaidi ya miaka 10).

Jina la ndugu “wa Kiroho” likawa na maana mpya baadhi yao walipopinga uongozi wa Kanisa, wakitangaza ubatili wa kujiuzulu kwa Selestini V na wa kuchaguliwa Bonifasi VIII; halafu wakadai Mapapa waliotoa matamko juu ya kanuni kuwa wazushi.

Kinyume na mtangulizi wake, Papa Klemensi V (1305-1314) alipenda kusikiliza wote, halafu akatoa (1312) tamko jipya juu ya kanuni ili kuondoa wasiwasi hasa kwa kubainisha amri za kanuni na kiasi ambacho zinawabana Ndugu Wadogo. Ingawa hakukubali msimamo wa ndugu “wa Kiroho” kuhusu mamlaka ya Kanisa juu ya kanuni, aliwaweka chini ya ulinzi wake; viongozi waliowadhulumu waliondolewa, na makosa dhidi ya ufukara yalirekebishwa ili kukwepa farakano. Lakini ikawa bure.

Marekebisho na utengano (1316-1517)

[hariri | hariri chanzo]

Kiburi kilichowapata Ndugu Wadogo katika karne yao ya kwanza, kutokana na mafanikio yao na mashindano na Maaskofu, kikafikia upeo walipopingana na Papa pia, ambaye mamlaka yake ilikuwa imeanza kupunguza. Ndipo shirika lilipopitia hatari kubwa kuliko zote za historia yake.

Mara baada ya kuchaguliwa, Papa Yohane XXII (1316-1334), akisukumwa na Mtumishi mkuu nd. Mikaeli wa Cesena (1316-1328), alifululiza kutoa amri zilizolenga kukomesha ndugu “wa Kiroho”, mpaka 4 kati yao walichomwa moto sokoni. Hapo uasi wa wengi ukawa wazi usijali kutengwa na Kanisa wala kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Hasa Waklareno wakaendelea hivyo zaidi ya miaka mia mpaka Yohane wa Capestrano na Yakobo wa Marka walipowapatanisha na Kanisa (1430 hivi), hata wakarudi chini ya Mtumishi wa shirika lote (1473) wakiwa na Makamu maalumu wa kwao.

Mwaka 1323 Papa, akiendelea na vita vyake, alitoa hati ya kulaani dhana ya Ndugu Wadogo wote (iliyokubaliwa na mkutano mkuu 1322) kuwa Kristo na mitume hawakumiliki chochote wala binafsi wala kwa pamoja.

Badala ya kukubali tamko hilo, Mtumishi mkuu na wanashirika karibu wote walilikataa hata kumtangaza Yohane XXII kuwa mzushi. Mfalme mkuu wa Ujerumani, ili apate nguvu dhidi ya Papa, akawapokea Ndugu Wadogo chini ya ulinzi wake akafanya mmojawao atangazwe kinyume cha sheria kuwa ni Papa badala ya Yohane XXII (bado hai).

Baadaye kidogo uasi huo ukaisha, lakini matokeo ya kwazo kubwa hivi yalichangia sana kudidimia kwa shirika.

Matukio mengine ya nje yaliyochangia ni: vita vya miaka mia (1339-1453) katika sehemu kubwa ya Ulaya; tauni (1348-1350) iliyoua thuluthi mbili za wanashirika (matokeo yake waliobaki walikusanyika katika konventi kubwa zenye hali nzuri zaidi kiuchumi, walipunguza utume na kupokea miito bila ya kuichuja); farakano la Kanisa la Magharibi (1378-1418) lililoleta fujo na utovu wa nidhamu; hatimaye kufifia kwa tunu bora za karne za kati. Upande wa ufukara uamuzi wa Yohane XXII wa kulinganisha Ndugu Wadogo na mashirika mengine ulisababisha hao wasimamie mali na kutumia pesa (hata za binafsi) kinyume cha kanuni. Kilele cha fujo kikawa miaka ya farakano la Magharibi, ambapo kwa wakati mmoja kulikuwa na Watumishi wakuu wawili au watatu, kila mmojawao akimfuata Papa wa Roma, au yule wa Avinyoni au hatimaye yule wa Pisa. Hata hivyo baadhi yao waliongoza vizuri na kuchangia amani ya Kanisa hadi ulipopatikana umoja wake na wa shirika mwaka 1418.

Pamoja na matatizo hayo yote, kuanzia mwaka 1334 baadhi ya wanashirika Italia, halafu Hispania na Ufaransa, walijiombea ruhusa ya Mtumishi mkuu au ya Papa waweze kuishi kijumuia kadiri ya kanuni, bila ya kutumia fadhili za kuilegeza. Wakati huo marekebisho ya namna hiyo yalitokea hata katika mashirika mengine, ingawa kwa kiasi kidogo zaidi. Ni kwamba kati ya Wafransisko kuna utata wa kudumu kuhusu namna ya kulinganisha kipeo asili na maisha halisi, au sehemu mbalimbali za karama ileile: katika karne XIV-XV utata huo ulisababisha mapambano ya kishujaa. Walioanzisha urekebisho walikuwa watawa (wengi wao mabradha wasio na elimu) wasioridhika na hali ya shirika. Wakililia hali ya mwanzoni, walilaumu maisha ya wenzao na uongozi wa Watumishi. Hao waliitikia kwa ukali wakijisingizia wanapaswa kudumisha nidhamu na kutetea haki ya walio wengi ya kutumia ruhusa za Kanisa. Kwa kawaida waanzilishi wa marekebisho hawakuwa watakatifu, bali nia yao ilichanganyikana na upungufu wa unyenyekevu na utiifu. Wakidai haki ya kufuata kanuni “Kiroho” kadiri ya sura ya 10, walikimbilia ngazi za juu kwa msaada wa wanasiasa ambao – sawa na watu wa kawaida – kila mara walipendelea urekebisho. Kisha kukubaliwa, marekebisho yakavuta miito bora: k.mf. kati ya mwaka 1402 na 1416 walijiunga na Waoservanti Bernardino wa Siena, Yohane wa Capestrano, Alberto wa Sarteano na Yakobo wa Marka ambao wanaitwa “nguzo nne za Oservansya (= kushikakanuni)”. Marekebisho yote, pamoja na kusisitiza ufukara, yalijali sana kimya na sala ya moyo upwekeni. Kama tunda la maisha ya namna hiyo yalifanya pia kazi kubwa tena bora ya kuhubiri, na hivyo kurudisha ule uwiano aliokuwa nao mwanzilishi. Mwishowe haki ya kushika kanuni kiaminifu ikatambulikana na Kanisa.

Bernardino wa Siena (1380-1440), mchoro wa Jacopo Bellini (1400 hivi - 1470 hivi).

Mahali pa kwanza walipokusanyika ni makao ya upwekeni ya Brogliano karibu na Asizi. Aliyestawisha zaidi kwanzia mwaka 1368 ni Paolucho Trinci (+1390), bradha aliyefanywa mkurugenzi wa jumuia zilizofuata urekebisho Italia, akiwa na haki ya kupokea wanovisi na kuanzisha nyumba nyingine. Dhidi ya upinzani wa Watumishi, Mtaguso wa Konstans (1415) uliwaruhusu Waoservanti kuenea katika kanda zote za shirika, kupokea wanashirika wote watakaopenda kujiunga nao, tena kuwa na kiongozi maalumu, yaani Watunzaji wao wawe chini ya mmojawao kama makamu wa Mtumishi mkuu badala ya kubaki chini ya Watumishi wa kanda. Hata hivyo marekebisho mengine yaliyokwishaanza (Wavilyakresi, Wakoleta, Waamadei na Waklareno) hayakupenda kujiunga na Waoservanti. Wakonventuali walipinga vikali uamuzi wa Mtaguso, na juhudi za Mapapa hazikuweza kurudisha amani, kwa kuwa hao hawakukubali kurekebishwa, wala Waoservanti kukaa chini yao. Wakati majaribio mbalimbali yalipoendelea kushindikana, Oservansya ikaenea na kustawi, hadi Papa Eugenio IV (1431-1447) alipoiruhusu kujifanyia mikutano mikuu na ya kanda ili kujichagulia viongozi (1446). Ushindi mwingine ukawa tangazo la kuwa Bernardino wa Siena, Mkuu wake wa kwanza, ni mtakatifu (1450).

Papa Leo X (1513-1521) alifanya jaribio la mwisho alipoitisha mkutano mkuu wa wote pamoja (1517), wakiwa na viongozi wa marekebisho mengine. Wakonventuali wakakataa tena shirika lote lisifuate urekebisho wala kuongozwa na Mwoservanti. Basi, Papa akaamua kuwatenganisha moja kwa moja, na kupindua uhusiano kati yao: Waoservanti wawe na hadhi ya kuwa ndio shirika halisi (OFM), wakati waliotetea maisha yaliyofuatwa katika konventi kubwa wakakubaliwa kuendelea nayo kwa kutumia fadhili halali walizopewa, lakini kama tawi tu (OFMConv). Alimlazimisha Mtumishi mkuu wa Wakonventuali kujiuzulu na kukabidhi mhuri wa shirika kwa Waoservanti, ambao Mtumishi wao aitwe Mtumishi mkuu wa shirika lote, likiwa ni pamoja na marekebisho mengine. Wakonventuali wasishiriki tena uchaguzi wa Mtumishi mkuu, wala kiongozi wao asiitwe Mtumishi bali Mwalimu mkuu tu! Hata hivyo wasisumbuliwe kwa kutumia fadhili walizopewa na Kanisa. Waoservanti wabaki na nyumba zao, na Wakonventuali na nyumba zao, bila ya kuvuka toka upande mmoja kwenda upande mwingine.

Ingawa hakuna takwimu ya wanashirika kabla ya karne XVII, tunaweza kuwakadiria kutokana na idadi ya nyumba na ya wastani wa ndugu walioishi katika nyumba: mwaka 1226: ndugu 5000; mwaka 1300: ndugu 40000; mwaka 1400: ndugu 25000; mwaka 1517: ndugu 50000 na zaidi (elfu 20 au 25 Wakonventuali na 30 au 32 Waoservanti)

Maisha ndani ya shirika (1226-1517)

[hariri | hariri chanzo]

Kujua maisha ya ndani ya shirika lolote ni muhimu kuliko kujua matukio makuu ya miundo yake. Basi, tuone jamaa ya Ndugu Wadogo ilivyoendelea kwa ndani katika karne tatu za kwanza tulizokwishaziona.

Baada ya kifo cha mwanzilishi wanashirika walizidi kumiminika mijini, katika konventi kubwa zaidi na zaidi, na zenye sura ya kimonaki zaidi na zaidi (kanisa kubwa, ukumbi wa mikutano, ua, bustani na kuta za kandokando…). Kanuni iliendelea kuzingatiwa, lakini kwa mtazamo wa kisheria, kufuatana na matamko ya Mapapa juu yake. Ufukara mkuu ukaja kuwa sifa maalumu za kujitangazia shirika bora kuliko mengine, pamoja na kujipongeza kwa kuwa na mwanzilishi aliye Kristo wa pili, mtakatifu kuliko wengine (tazama ngao ya shirika ya karne XV yenye msalaba iliposulibiwa pamoja mikono ya Kristo na Fransisko). Lakini utekelezaji ukawa wa kinafiki sana, k.mf. tendo la ndugu kusafiri na boi ambaye amchukulie pesa asije akazigusa mwenyewe lilihukumiwa tayari na katiba ya Narbona (1260) iliyotungwa kama kinga ya kanuni, halafu ikarekebishwa mara nyingi ili kudhibiti makosa yaliyojitokeza pamoja na kudumisha usawa katika sura ya nje ya watawa na katika matumizi ya kila siku.

Kimya kilichosisitizwa na Fransisko kama sharti la sala, kikaja kuratibiwa kwa mfano wa monasteri: kwamba kimya kikuu kiwe cha kudumu katika kanisa, maktaba, vyumba vya kulala, ua na mezani wakati wa kula. Zaidi ya hicho, kitunzwe daima na popote kimya cha Kiinjili, yaani kukwepa maneno yoyote yasiyofaa (Mathayo 12:36). Katiba haikuzungumzia maburudisho, lakini sikukuu zilikuwa na nafasi za kufurahia udugu (vyakula na divai, nyimbo, maigizo na michezo), ingawa ilikatazwa mara nyingi ndugu wasipite kiasi. Hatujui vitendo vya toba vya kijumuia vilipoanza; lakini mwanzoni mwa karne XIV Ndugu Wadogo walikuwa wakijipiga mijeledi kila siku ya Kwaresima, halafu mara tatu kwa juma nyakati nyingine. Adhabu alizozitoa mwanzilishi zikaja kuongezwa chini ya Elia hata kuratibiwa na sheria. Mapema ulifuatwa mfano wa Wadominiko wa konventi zote kuwa na magereza, ila yajali utu. Wasiojirekebisha wafukuzwe shirikani.

Mpaka mwaka 1239 ndugu wakleri na mabradha waliishi kwa usawa alivyotaka Fransisko. Baadaye shirika likabadilika na kuwa la kikleri. Sababu ni mbalimbali: heshima kubwa ya mwanzilishi kwa mapadri, ongezeko la mapadri kwa idadi na ubora, chuki ya wengi kwa sera ya Elia aliyependelea mabradha wenzake katika uongozi. Miaka miwili tu baada ya kumuondosha, mabradha wakajikuta hawaruhusiwi tena kuwa na cheo chochote, halafu ikakatazwa wasipokewe tena shirikani, isipokuwa kwa sababu ya pekee. Pia mabradha walifungiwa kabisa mlango wa ukleri kwa kufafanua visivyo maneno ya kanuni yasemayo, “wasio na elimu wasijisumbue kusudi waipate”. Basi, baada ya katazo la kufanya kazi za mikono nje ya konventi kama zamani, sura ya bradha Mfransisko ikawa kwa karne nyingi ile ya mtu ambaye hana sauti wala kura, amekusudiwa kutoa huduma za konventini na kuombaomba, ambaye heshima yake kubwa ni kuwatumikia wanashirika mapadri. Hivyo miito ya namna hiyo haikutoka tena kwa watu wenye elimu wenye kulenga utakatifu wa Kifransisko, bali kwa watu wadogo, wasiojua kusoma, wasio na mbele wala nyuma, ambao wengi wao waliingia utawani kujitafutia tu maisha ya hakika. Hapo ilibidi wachujwe sana. Kwa njia hiyo sura ya ndani ya jamaa ilibadilika sana, kwa kuwa na matabaka yenye kazi tofauti, haki tofauti na malezi tofauti. Ila marekebisho yakajaribu kurudia hali ya mwanzoni.

Baadaye ikatokea migawanyiko mingine kati ya waliopewa na wasiopewa fadhili, yaani ruhusa za pekee. Kwanza zilitolewa kwa walimu na wanafunzi ili kustawisha masomo katika ngazi za juu, halafu katika ngazi ya kati na ya chini. Wakaja kuongezwa waliowahi kuwa na vyeo, wazee na hatimaye wahubiri. Malalamiko yakawa mengi, hasa walionyimwa walipokosa hata mahitaji yao, ingawa wagonjwa waliendelea kushughuliwa vizuri, na haki zao zilitetewa na sheria. Utaratibu wa kimonaki wa kuwapanga watawa kufuatana na muda wa kukaa utawani, uliokataliwa mwanzoni ukajipenyeza shirikani; hata katika hilo, na katika kuwapa viongozi heshima kubwa za nje, marekebisho yakarudia usahili wa mwanzoni.

Fransisko aliwazoesha wafuasi wake kuwa wazi kati yao, kuelezana habari za safari, kujishtaki kwa unyenyekevu na kuomba msamaha. Ndiyo asili ya “mkutano wa makosa” ambao uliagizwa na katiba (1260) mara moja kwa wiki, ukifuatwa na mkutano wa jumuia uliojadili masuala ya pamoja. Mpango wa mwanzilishi wa kuwatuma wafuasi wake ulimwenguni wawiliwawili uliendelea, ila kwa shabaha ya kulindana bila ya kuaminiana, badala ya kushuhudia umoja wa kidugu na kusaidiana. Malezi kwa jumla yalilenga zaidi maisha ya ndani kuliko kwenda ulimwenguni, jambo lililotarajiwa kuwa la nadra tu. Mipango ya kwanza kwa malezi iliratibiwa na katiba (1260). Walezi walisaidiwa na vitabu kadhaa, hasa “Kielelezo cha Nidhamu” cha Bernardo wa Besse (+1300 hivi) ambacho kinalenga nidhamu, adabu njema, usafi na taratibu za kimonaki kuliko mitindo ya Kifransisko. Baada ya kumaliza unovisi, watawa wapya waliendelea kulelewa walau miaka mitatu, ingawa kazi hiyo ilionekana mapema kuwa ngumu sana. Sehemu mbalimbali (hasa Wakonventuali) walianza kupokea watoto wadogo kama walivyofanya wamonaki.

Toka mwanzo kazi za Ndugu Wadogo zilikuwa tatu: sala, kazi za mikono na mahubiri; uvivu ulikuwa tishio kwa mwanzilishi na viongozi wengine. Bonaventura alipochaguliwa aliwaandikia mara wanashirika wote ili kuwaonyesha hatari hiyo kubwa, lakini alipinga kabisa watawa kufanya kazi za mikono zenye malipo. Badala yake walitafutiwa kazi nyingine mbalimbali: kusoma, kuimba Zaburi, kutoa huduma za nyumbani, kuombaomba n.k.

Mchango muhimu mmojawapo wa mashirika ya Ombaomba ni kujenga daraja kati ya liturujia ya monasteri na ya makanisa makuu na mahitaji ya kidini ya jamii yenye kubadilika. Ndugu Wadogo, wakitumia haki ya wakati huo ya kila shirika kujitengenezea liturujia yake, walistawisha kalenda na taratibu zao, pamoja na kufuata kimsingi zile za Roma. Walizifupisha kwa faida ya sala ya moyo, na kuzisogeza jirani na haja za mtu binafsi. Ingawa wapinzani walisema kufanya hivyo ni kuvuruga liturujia, Mapapa wakaja kueneza breviari ya Kifransisko katika Kanisa lote la Kilatini. Hata misale ya Kiroma iliyotumiwa na kurekebishwa na Ndugu Wadogo ikaja kuenea: taratibu nyingi za ibada, nyimbo na sikukuu mpya ziliingizwa nao kabla hazijakubaliwa kwa Kanisa lote. Kwa juhudi na mafanikio ya pekee zilistawishwa ibada kwa Ekaristi, jina la Yesu, kuzaliwa kwake na kuteseka (Njia ya Msalaba), Bikira Maria (Kukingiwa Dhambi ya Asili). Kwa ajili hiyo, nje ya ibada walitumia pia maigizo, wakisaidiwa na Utawa III. Baada ya jumuia zote kupata kanisa la kitawa ambapo iliwabidi waadhimishe Sala ya Kanisa, ibada zilizidi kuwa za fahari, hasa kwa lengo la kuwapa kazi ya kufanya ndugu wasiosoma wala kuhubiri. Kwa sababu hiyohiyo, juu ya Sala ya Kanisa vikaongezwa vipindi vingine kwa ajili ya wafu, kwa heshima ya Bikira Maria n.k. Hoja ya msingi ilikuwa kwamba walio wengi wasingefanya bidii katika sala ya binafsi. Kama kawaida, marekebisho yalirudia kusisitiza sala ya moyo na kusoma tu Zaburi, pamoja na kuadhimisha Misa pasipo fahari katika makanisa madogomadogo. Wasio mapadre walihudhuria Misa, ila ilikuwa kawaida kupokea Ekaristi kila baada ya wiki mbili. Kumbe maungamo yalikuwa mara mbili kwa juma.

Kati ya walimu wa kiroho Bonaventura alishika nafasi ya kwanza. Maandishi yake yote yalilenga maisha ya kiroho, na kuathiri sana shirika na Kanisa lote hadi leo; ndiyo sababu akatangazwa mwalimu wa Kanisa kwa jina la “mwalimu wa kiserafi”. Tukiacha waandishi wengine bora na kuzingatia waliofaulu kuyatekeleza kikamilifu maisha ya kiroho, tunakuta katika karne tatu za kwanza walifariki watakatifu 25 na wenye heri 61: ndio ushahidi bora wa jinsi kipeo cha Kifransisko kinavyofaa. Wa kwanza ni wafiadini wa Moroko (5 wa mwaka 1220, na 7 wa mwaka 1227). Kufuatana na mfano wao alijiunga na shirika Antoni wa Padua (+1231), “mwalimu wa Kiinjili” mwenye utakatifu usiosemeka kulingana na moyo wa mwanzilishi. Baada ya Bonaventura kuna askofu mwingine, Ludoviko wa Tolosa (+1297), aliyekufa kijana kama alivyotamani. Karne XIV, iliyojaa wamisionari na wafiadini, ina ndugu wanne kutoka nchi mbalimbali waliotangazwa watakatifu: Nikola Tavelic na wenzake waliouawa Yerusalemu (1391). Watakatifu wote sita wa karne XV ni Waoservanti ambao walipigania kanuni na kufanya utume mkubwa: Bernardino wa Siena (+1444), Yohane wa Capestrano (+1456) na Yakobo wa Marka (+1476) toka Italia, Petro Regalado (+1456) na Didakus wa Alkala (+1463) toka Hispania, halafu Yohane wa Dukla (+1484) toka Polandi.

Utume (1226-1517)

[hariri | hariri chanzo]

Tangu mashirika ya Wafransisko na Wadominiko yaanzishwe, Mapapa walitambua yanavyohitajika na kufaa kutegemezea Kanisa la Roma ambalo, baada ya kufikia kilele cha fahari na mamlaka wakati wa Papa Inosenti III (1198-1216), lilianza kukabiliana na upinzani mpya wa viongozi wa siasa. Ili waweze kuwatumia watawa hao bila ya pingamizi, Mapapa walijiwekea kuwasimamia wasikae chini ya Maaskofu, wakawapendelea katika tume nyingi. Hivyo toka mwanzo Ndugu Wadogo walifanya kazi katika ofisi za Papa na kupewa vyeo mbalimbali, kinyume cha matakwa ya Fransisko aliyetaka wabaki “wadogo”. Hasa baada ya Gregori IX, Mapapa waliona ustawi wa Kanisa unastahili uzingatiwe kuliko udogo wa Kifransisko. Ingawa shirika lilijitahidi kuzuia ongezeko la vyeo, katika karne XIII waliishi Maaskofu Wafransisko 250, katika karne XIV 746, katika karne XV 791, na miaka 17 ya kwanza ya karne XVI 70. Mabalozi wa Papa jumla walikuwa zaidi ya 300, Makardinali 29, na wawili wakawa Papa Nikolasi IV (1288-1292) na Papa Sixtus IV (1471-1484). Ndugu Wadogo walichangia sana Mitaguso mikuu yote ya karne hizo tatu: Lyons I (1245), Lyons II (1274), Vienne (1311-1312), Konstans (1414-1418), Firenze (1431-1445) na Laterano V (1512-1517). Vilevile ndugu wengine walitetea haki za Papa dhidi ya upinzani, na zaidi ya 200 walipokea hata kazi ya kuwahukumu wazushi, ingawa hiyo haikuwapendeza sana.

Kazi ya kawaida zaidi ilikuwa ile ya kuhubiri. Waliokubaliwa na Watumishi wakaja kuunda tabaka la juu kuliko mapadri wa kawaida (waliosoma Misa tu) na ya mabradha. Ilipobaki kazi ya wasomi tu, ikarudia mitindo ya vyuoni na kuachana na usahili wa mwanzo alioutumia na kuutaka mwanzilishi. Mhubiri mkuu wa kwanza ulikuwa Antoni ambaye kwa miaka 10 alichangamsha Italia na Ufaransa Kusini akishinda uzushi. Pamoja na kuhubiri, wengine wametuachia kwa maandishi hotuba zao, mifano mingi na maelekezo juu ya namna ya kuhubiri.

Karne XV ndiyo bora kwa mahubiri ya Kifransisko, ambapo “nguzo za Oservansya” walitoka upwekeni wakawashirikisha wote utajiri waliojipatia katika sala. Makanisa hayakutosha kukusanya wasikilizaji; wote waliguswa na wengi wakaongoka. Kutoka Italia wakahubiri nchi mbalimbali hadi Norwe. Tunda mojawapo la utume wa Yohane wa Capestrano ni ushindi wa Wakristo juu ya Waturuki waliotishia kuvamia Ulaya yote (1456). Huko Italia mahubiri hayo yalipinga mwelekeo mpya wa kuweka pembeni Ukristo katika maisha ya kila siku na kujali ustawi wa kidunia tu. Kitubio kilifuatana na mahubiri; hasa baada ya Mapapa kuruhusu watawa kutoa huduma hiyo, ikaja kuwa mojawapo ya kazi zao kuu.

Shirika likiwa na uhusiano wa pekee na watu wadogo toka mwanzo, daima ni jepesi kutambua hali na haja zao upande wa roho na wa mwili, na kuziitikia vizuri, hata kupitia Utawa III. Kipindi hicho watu walielekea sana kujiundia makundi kadiri ya fani zao n.k. Ndugu Wadogo waliwaelekeza kufanya hivyo bila ya kusahau dini, katika jina na taratibu walivyoyapatia. Walipatanisha mara nyigi wanasiasa wa miji au vyama tofauti, walisaidia maskini na wagonjwa (hata wenye ukoma na tauni), walianzisha hospitali, walilaumu hadharani dhuluma n.k. Kwa ajili hiyo, bila ya kujali upinzani wowote, walianzisha pia benki ambazo zikopeshe pesa kwa riba ndogo sana ili kukomesha waliodai riba pasipo kiasi (hasa Wayahudi).

Kabla hatujaeleza umisionari wa Ndugu Wadogo, tuangalie juhudi zao kwa ajili ya umoja kati ya Waortodoksi na Kanisa la Roma. Kabla Konstantinopoli haujatekwa na Waturuki (1453), udhaifu wa Wagiriki upande wa siasa na jeshi uliwaelekeza kutafuta msaada wa Wakristo wa Magharibi. Hivyo zilipatikana fursa nyingi za kukaribiana na kujaribu kuungana, ambazo Mapapa kila mara waliwatumia Wafransisko na Wadominiko. Kwa namna ya pekee Mtaguso II wa Lyons, kwa juhudi hasa za Bonaventura, ulifanikiwa kutangaza umoja, ingawa baadaye ukashindikana kwa sababu mbalimbali. Juhudi nyingine kulingana na mitazamo ya nyakati hizo zilifanywa na Ndugu Wadogo waliosambaa kotekote Mashariki na kutoa mifano bora ya maisha yao, pamoja na kutangaza kwa sauti na kwa maandishi ukweli wa Kanisa Katoliki ili kuwavuta Waortodoksi mmojammoja au makundimakundi kuingia katika ushirika kamili nalo. Sehemu fulanifulani matunda yaliridhisha, lakini wengine waliuawa, hasa baada ya Waturuki kuteka Ulaya Mashariki Kusini. Nje ya eneo hilo, utume huo ulifanyika pia Urusi, Georgia, Armenia, Irani, Lebanoni, Misri hata Ethiopia.

Kazi ngumu zaidi ilifanyika kwa wasio Wakristo. Karne XIII ilikuwa mwanzo wa umisionari wa aina mpya, ambao unaongozwa na Mapapa kwa kutumia mashirika ya Ombaomba (yaliyofaa sana kwa utayari wa kutumwa na kwa umoja wa miundo yake), unapata wamisionari mchanganyiko kutoka nchi yoyote, unaenea katika bara lote la Asia (ambalo linakuja kujulikana na Wazungu wakati huo) na hauna faida ya uchumi. Fransisko alichochea hayo kwa mifano na mafundisho yake ambayo alisisitiza kuwa wito huo ni wa Kimungu, kwa hiyo hautakiwi kuzuiwa. Kwa mang’amuzi yake alielekeza kutoa kwanza ushuhuda wa maisha ya Kikristo, halafu tu, kadiri ya mapenzi ya Mungu, kuhubiri wazi imani. Wafuasi wake hawakufuata daima maelekezo hayo, kwa maana wengi waliwachokoza Waislamu ili kuuawa.

Katika historia ya misheni za Kifransisko, tunaona kwanza uenezi mkubwa upande wa Mashariki, halafu karne nyingine ya kufifia, halafu katika karne XV msukumo mpya toka kwa Waoservanti, lakini kuelekea maeneo mapana ambayo yalivumbuliwa na Wazungu miaka ya mwisho ya karne hiyo na kuhitaji Injili. Kuanzia mwaka 1217 Wafransisko wametunza mahali patakatifu pa nchi ya Yesu, ingawa iliwabidi kuvumilia magumu mengi, dhuluma na vifodini; wengi walikufa pia kwa kuwashughulikia wenye tauni. Kuanzia mwaka 1219 wengine walitumwa Afrika Kaskazini, ambapo baadhi walifia dini. Shirika lilianza kupata Maaskofu kwa ajili ya Moroko, ingawa hawakuweza kukaa huko. Kumbe Tunisia na Libya waliruhusiwa kuwaongoa Waislamu wakachuma matunda kwa muda fulani, ingawa vipindi vingine waliweza tu kuwahudumia Wakristo wageni.

Ramani inayoonyesha kwa rangi ya buluu iliyokolea safari ya Yohane wa Pian del Carpine hadi Asia mashariki.

Mwaka 1241 Wamongolia, baada ya kujitwalia Asia karibu nzima, walivamia Ulaya na kufadhaisha Wakristo wote, kwa sababu hakuna aliyeamini uwezekano wa kuwashinda. Mapapa walijaribu kuwasimamisha kwa kutuma Wafransisko na Wadominiko (wa kwanza ni Yohane wa Pian del Carpine) waombe masharti ya amani. Ujumbe huo uliposhindikana, walianza kupenya kama wamisionari upande wa Ulaya Mashariki, wakasambaa kwa ruhusa ya watu hao wakatili sana katika utawala wao wote. Nikola IV alimtuma (1291) Yohane wa Montecorvino, mwanzilishi wa misheni za China na Askofu wa kwanza wa Beijing, mwenye majimbo sita chini yake katika ufalme mzima (hadi Urusi). Nyumba za kitawa katika eneo hilo lote likafikia kuzidi 50, baadhi zikiwa na ndugu wasiopungua 20. Papa Inosenti VI (1352-1362) aliomba mkutano mkuu wa mwaka 1353 uongeze wamisionari alivyotaka mfalme wa Mongolia, lakini itikio likawa hafifu, kwa kuwa tauni iliyoua wamisionari wengi, iliua pia watawa wengi Ulaya. Hivyo misheni zikaendelea kwa shida tu mpaka ikaja kufa China ilipojikomboa. Pia, Ndugu Wadogo waliongoa Walitwania, taifa la mwisho la Ulaya kuingia Ukristo (karne XIII na XIV).

Karne XV ilielekeza umisionari upande mwingine, na Waoservanti waliuchangamkia kuanzia visiwa vya Kanaria vilivyopokea Ukristo haraka kwa juhudi za ndugu waliofikia kuwa 200, mmojawao Didakus wa Alkala. Kutoka huko umisionari ulienea pwani za Afrika Magharibi. Mzunguko wa Afrika hadi Rasi ya Tumaini Jema (Bartolomeo Dias, 1488) na India (Vasko Da Gama, 1497-1498), na hasa uvumbuzi wa Amerika (Kristoforo Columbus, 1492) ulisisimua sana umisionari kwa maeneo, miundo na mbinu mpya. Wakati ambapo uenezi wa Waturuki Waislamu ulikuja kuzuia njia za Asia, na misheni zilizokuwa chini ya utawala wao zilidumaa, Ndugu Wadogo walistawisha upeo umisionari wao Amerika na Asia Mashariki kupitia baharini (wakati huo Asia Mashariki ilikuwa chini ya Askofu wa Funchal, katika kisiwa cha Afrika Magharibi!). Upande wa miundo wafalme wa Ureno na wa Hispania walipogawana ulimwengu kwa baraka ya Papa Alexander VI (1492-1503) walipewa pia usimamizi wa kazi zote za misheni, pamoja na haki ya kuchagua na kutuma wamisionari katika maeneo yao. Hivyo karne XVI idadi ya wamisionari OFM ilifikia 6,000, wengi wao wakitokea nchi hizo mbili, kwa sababu mataifa mengine waliweza wakabaguliwa na hata kurudishwa nyumbani.

Ndugu Wadogo 6 wa kwanza walifika Amerika (kisiwa cha Hispaniola, leo Dominikana/Haiti) mwaka 1493 na kuanza kuwahubiria wazalendo. Wengine wakafuata mapema na kuenea kadiri vilivyovumbuliwa visiwa vingine. Kufikia mwaka 1500 walikuwa wameshabatizwa wazalendo 3,000 Hispaniola na wengi zaidi Kuba. Mwaka 1504 yaliundwa majimbo matatu na mwaka 1505 kanda ya shirika. Mwaka 1511 alitawazwa Askofu wa kwanza wa Amerika visiwani (Dominikana) na mwaka 1513 wa bara (Panama), wote wawili wakiwa Wafransisko. Ila barani hatari zikawa nyingi. Waliohamia Brazili (1503) waliuawa baada ya miaka miwili, na wengi wa waliowafuata wakauawa pia. Hata hivyo Wafransisko wakaendelea na umisionari huko, wakiwa peke yao hadi 1549.

Vilevile Ndugu Wadogo ndio wamisionari wa kwanza kufika India kwa meli (1500, baada ya kupitia Brazili); wengine wakafuata. Mabanyani waliwaua 3, lakini wengine waliongoka jumla wakabatizwa pasipo mafundisho kutokana na uhaba wa wamisionari. Safarini, wengine walihubiri kisiwani Sokotra (karibu na Somalia) na kuongoa karibu wote, hata wakageuza msikiti kuwa kanisa la Bikira Maria; lakini Waarabu wakakiteka (1510) wakaharibu kila kitu.

Uenezaji wa Injili unatimia unapopenya utamaduni wa watu. Tuone basi Ufransisko ulivyoathiri Kanisa na jamii, kuanzia elimu, fasihi na sanaa.

Fransisko hakuwa msomi, tena alihisi uchu wa elimu unavyoweza kuzuia udogo na usawa wa wafuasi wake. Lakini, akitambua njia hiyo haiepukiki, alielekeza namna ya kuifuata bila ya kudhurika. Kwake Antoni wa Padua ndiye kielelezo, kwa jinsi alivyokuwa tayari kuweka pembeni usomi. Ndiyo sababu alimruhusu kuwafundisha ndugu teolojia huko Bologna mradi isizimishwe roho ya sala na ibada. Mwaka 1231 shirika lilikuwa na nyumba za masomo hata Paris na Oxford karibu na vyuo vikuu ili kuwaandaa walimu ambao wafundishe katika konventi muhimu zaidi za kila kanda. Ndipo walipojipatia sifa ya elimu na nafasi mpya za utume, ingawa Egidi na wengineo walizidi kulaumu Paris kwamba imeharibu shirika. Tangu karne XIV katika konventi karibu zote kulikuwa na vipindi vya lazima kwa wasio mabradha. Pia yalianzishwa masomo kwa waliotarajia kupata daraja takatifu. Mitindo ya kufundisha ilikuwa sawa na ile ya mashirika mengine na ya vyuo vikuu: vipindi asubuhi na jioni, mijadala, mahubiri ya walimu na ya wanafunzi vilevile.

Shirika halikuwa na mwalimu maalumu na mafundisho ya lazima, ila tabia na mazingira yake yote vilielekeza Ndugu Wadogo kuwaza namna fulani, yaani kusisitiza upendo kuliko ujuzi, na utashi kuliko akili; pia kumuona Mungu kama Wema kuliko kama Ukweli. Falsafa ya Wafransisko ilifuata ile ya Plato kumpitia Augustino (Antoni alitoka shirika lake). Kati ya walimu wa vyuo vikuu aliyeelekeza njia ni Aleksanda wa Hales (+1245), aliyemfundisha Bonaventura huko Paris. Kwa mtakatifu huyo, mwalimu ni Kristo tu, na elimu ni moja tu, ile inayotuunganisha naye, hasa Maandiko Matakatifu, ambayo peke yake yanawafaa Ndugu Wadogo. Baada yake teolojia ikabili mababu wa Kanisa na maandishi ya walimu wa teolojia. Wanafalsafa na waandishi wengine wasomwe tu kwa mpito kadiri wanavyosaidia kuelewa Biblia. Ndiyo njia ya kufikia elimu, lakini mtu akitaka hekima anapaswa kuwa na maisha matakatifu.

Oxford iliwatoa hasa: Roger Bacon (+1292), mtaalamu wa mambo mengi na mwanzilishi wa mtindo wa upimaji kama msingi wa sayansi; Yohane Duns Scoto (+1308), mwalimu mwenye uchambuzi mkali, anayesifiwa kwa kuonyesha Kristo kuwa kiini cha uumbaji, na kwa kutetea sifa ya Maria kukingiwa dhambi ya asili (Wafransisko wakaendelea kuitetea hadi ikatangazwa na Papa Pius IX, wa Utawa III, mwaka 1854, kuwa dogma); na Wiliamu wa Ockham (+1347) aliyepotosha falsafa akadai eti, akili haiwezi kujua yanayopita malimwengu: msimamo wake ukaenea sana, ukampa Martin Luther silaha dhidi ya imani katoliki, ukaathiri utamaduni wa Magharibi hadi leo.

Ufransisko uliathiri vilevile mwelekeo wote wa sanaa ya Magharibi. Ukiitikia vizuri matarajio yote ya kidini na ya kijamii ya kipindi cha mageuzi, ulieneza mtazamo mpya wa maisha unaojali mtu na viumbe vyote. Hivyo ulichangia sana upatikanaji wa mitindo mipya na njia mpya za kufurahia uzuri, ingawa bila ya kupotewa na imani. Fasihi ya Kifransisko inapenda kusimulia, tunavyoona katika maisha ya mwanzilishi yaliyoandikwa na wafuasi wake; uchoraji unaonyesha sura halisi ya kwake na ya wengineo; hata ujenzi unafuata njia mpya, hasa kufuatana na kielelezo cha kanisa la Fransisko huko Asizi. Hata katika ujenzi wa nyumba zao Ndugu Wadogo waliweza kuzingatia ufukara bila ya kupuuzia uzuri, kiasi kwamba upendevu wake unavutia wengi hadi leo.

Marekebisho kuendelea (1517-1762)

[hariri | hariri chanzo]

Matawi mapya kuchipuka

[hariri | hariri chanzo]

Utengano wa Waoservanti na Wakonventuali ulitatua tatizo moja, lakini haukufaulu kuunganisha makundi yaliyorekebishwa, ingawa Papa alikuwa ameagiza itungwe mara katiba moja kwa yote. Baadhi yalidumu kuwa na kanda zao, Waoservanti wa Italia wakaikataa katiba hiyo wakaendelea kuirekebisha mfululizo ile maalumu ya kwao, na kanda nyingine zilijitungia vilevile na kuzidisha tofauti shirikani. Kilichohatarisha zaidi umoja ni utaifa uliochochewa na serikali mbalimbali kwa faida ya siasa ya nchi zao dhidi ya nyingine. Wafalme waliingilia kwa njama na vitisho masuala ya mikutano mikuu, sawa na walivyoingilia uchaguzi wa Papa, lakini kila mara idadi iliwapa ushindi Wahispania, hata washindani wao (Wafaransa) wakagoma kuhudhuria mara kadhaa. Matatizo mengine yalihusu maisha yenyewe, hasa ufukara. Waliolazimika kujiunga na Waoservanti, na wale wasioacha kutumia fadhili walizokuwanazo wakiwa Wakonventuali, walikataa kurekebishwa. Kinyume chake, wengine hawakuridhika tena na namna OFM ilivyoshika kanuni, wakadai ruhusa ya kuishika kabisa. Ndivyo walivyofanya watawa wa mashirika mbalimbali, kwa kuwa haja ya urekebisho ilitambulikana na wote katika Kanisa la karne XV-XVI. Kwa namna ya pekee Ndugu Wadogo walichochewa kufanya hivyo na sura X ya kanuni pamoja na wasia. Ndiyo sababu Bonaventura aliona haja ya kuwepo makao ya upwekeni katika kila kanda ili kuwaachia uhuru wa kuishi hivyo wale wapendao. Kumbe Waoservanti wengi na baadhi ya viongozi wao hawakukubali kuwaachia wenye bidii uhuru huo, kwa sababu ingekuwa sawa na kukiri kwamba wamelegea. Hivyo wakawatenda ndugu hao kama Wakonventuali wa zamani walivyowatenda Waoservanti wa kwanza. Walioamini urekebisho unaweza kutoka kwa viongozi wakaja kujionea haiwezekani. Miundo iliyoanza kama urekebisho ikajikuta inajaribu kuzuia juhudi za waliopenda urekebisho, na viongozi wa shirika lililoanza kwa kushindana na viongozi wakawalaumu waliotaka kufanya vile wakisema eti, ni wakaidi tu! Kwa kukosa busara na wema walisababisha waliotaka urekebisho wakafuate njia zao ili kupata ruhusa walizozihitaji, kwa kumkimbilia Papa au viongozi wa serikali. Mara nyingine Wakonventuali walipokea makundi hayo chini ya ulinzi wao ili kuwakomoa Waoservanti waliokuwa wanawadharau wakijidai ndio wafuasi halisi wa Fransisko. Ndiyo asili ya matawi mapya, hasa lile la kujitegemea la Wakapuchini.

Mwaka 1525 Mateo wa Bascio alimkimbilia Papa Klementi VII (1523-1534) ili kuruhusiwa ashike kanuni, avae kanzu asili na kuhubiri huko na huko alivyotaka. Alipokubaliwa, walijiunga naye ndugu wawili, Ludoviko wa Fossombrone na Rafaeli wa Fossombrone. Mtumishi wa kanda aliwatafuta sana, lakini walilindwa vizuri na Katerina Cibo, ndugu wa Papa. Ili kukwepa dhuluma, wakajiunga na Wakonventuali, halafu wakapewa na Klementi VII haki ya kuwa na Mtumishi wao chini ya Mkuu wa Wakonventuali na ya kupokea wanovisi (1528). Mapema walianza kuitwa Wakapuchini kutokana na kofia yao kubwa. Upinzani wa Mkuu wa OFM dhidi yao haukufaulu; kinyume chake, kwa kuwa alitaka kuzuia hata makao ya upwekeni ndani ya shirika, ndugu wengi wenye bidii wakakata tamaa wakajiunga na Wakapuchini. Njama nyingine za kuwakomesha zikashindikana, hivi kwamba mwaka 1535 walikuwa tayari 700. Ndipo aliposhika uongozi wao Bernardino wa Asti aliyelipa shirika jipya sura ya kiroho ya kudumu, hasa kwa njia ya katiba iliyotungwa mwaka huo na kupitishwa mwaka uliofuata.

Feliche wa Cantalice akimfufua mtotoː mchoro wa Guercino.

Hatari nyingine zilitokea ndani ya shirika, kwa ukaidi wa Ludoviko, halafu kwa uzushi wa mwandamizi wa Bernardino. Hatimaye mambo yakatulia na tawi jipya likazidi kustawi kiroho na kitume, ingawa Papa Julius III (1550-1555) alikataza Waoservanti wasihamie tena kwa Wakapuchini. Hivyo hawa wakazidi kujisikia tofauti na Wafransisko wenzao. Mkutano mkuu wa mwaka 1552 ulionyesha kuwa juhudi kali za awali zimeanza kutulia na kujilinganisha na maisha: shirika lilipanga masomo na kuwa na watu maarufu upande wa elimu, utume na uongozi. Jambo muhimu zaidi, lilimzaa mtakatifu wa kwanza, bradha Felix wa Cantalice (+1587), kielelezo cha unyofu. Mtaguso wa Trento (1545-1563) ulisifu tawi hilo kama urekebisho wa kufaa na wenye uaminifu kwa wito wake hata kustahili kutazamwa na Kanisa kwa namna ya pekee. Shirika likazidi kukaza nidhamu ili kuzuia ulegevu, likaanza kuenea ng’ambo ya milima ya Italia Kaskazini (1573). Ulipozuka upinzani wa Wakonventuali, Kanisa lilikuwa limeshang’amua ubora wa Wakapuchini; basi, Papa Paulo V (1605-1621) alitamka kuwa ni Ndugu Wadogo halisi na wana wa Fransisko sawa na matawi mengine (1608), halafu akawaondoa chini ya Mkuu wa Wakonventuali na kuwapa Mtumishi wa kwao mwenye haki ya kuhesabiwa mwandamizi halali wa mwanzilishi (1619). Kwa wakati huo shirika limeshazaa tena Serafino wa Montegranaro (+1604), bradha asiye na vipawa vingi kiutu bali mwenye karama za ajabu, Yosefu wa Leonesa (+1612), padri Mkapuchini wa kwanza kutumwa kwa Waturuki Waislamu halafu mhubiri bora Italia, na Laurenti wa Brindisi (+1619), “mwalimu wa Kitume”, mtimilifu kuliko Wakapuchini wote kwa utakatifu, elimu na utume. Wakafuata Fidelis wa Sigmaringen (+1622), wa kwanza kutoka nje ya Italia, na wa kwanza kufia dini kati ya waliotumwa na Idara ya Papa kwa Uenezaji wa Imani, halafu Bernardo wa Corleone (+1667), mwongofu mwenye toba kali. Pia walipatikana wenye heri 6.

Kipindi hicho ndicho cha ukomavu wa shirika, mitazamo ya Kiitalia ilipopanuka kwa kuenea nje ya nchi na wanashirika waliposhika nafasi muhimu katika Kanisa. Baadaye hakuna matukio ya maana zaidi, isipokuwa mengine ya kufaa na mengine yasiyofaa ambayo yaliathiri shirika: idadi ya watawa na ya shughuli iliongezeka pamoja na sifa kutoka kwa viongozi wa Kanisa na serikali, lakini zilizuka vurugu pia kama ile ya utaifa (1636-1678). Papa Benedikto XIV (1740-1758) aliamua mhubiri wa Papa awe daima Mkapuchini, akasema, “Shirika la Wakapuchini linastahili yoyote yale, kwa kuwa ndilo kielelezo pekee cha ukamilifu wa Kiinjili kilichobaki hadi nyakati zetu”. Kweli urekebisho huo uliendelea kushika kikamilifu kanuni kwa muda mrefu kuliko mengine yote. Nyumba ziliendelea kujengwa ilivyoagizwa toka mwanzo, ndogo sana, nje ya miji na vijiji, zikielekeza ndugu kufuata ufukara na unyofu hata ulimwengu ulipokazania fahari. Watakatifu wa kipindi hicho ni bradha Krispino wa Viterbo (+1750), kielelezo cha furaha ya kiroho, Ignas wa Santhià (+1770), padri mwenye bidii kwa wagonjwa na wakosefu, Ignas wa Lakoni (+1781), bradha ombaomba aliyesaidia sana fukara, na Felix wa Nicosia (+1787), bradha mtiifu ajabu, mbali ya mwenye heri 1.

Kioo cha kanisa la Porto Alegre, Brazil, kinachomuonyesha Benedikto akimpakata Mtoto Yesu katika njozi.

Vilevile Italia, ndugu waliojikusanya katika makao ya upwekeni kuanzia mwaka 1535 (mkutano mkuu ulipowaruhusu ili kuzuia wengine wengi wasiwakimbilie Wakapuchini), kisha kuongezeka waliwekwa moja kwa moja chini ya Mtumishi mkuu tu (1579), wakapewa katiba maalumu (1595), ruhusa za pekee sana (1596), hatimaye Kiongozi mkuu na mkutano mkuu wa kwao. Hivyo mamlaka ya Mtumishi wa OFM kwao ikawa jina tu. Kati ya hao Wariformati katika kipindi hicho tunawakuta watakatifu mabradha watatu: Benedikto Mwafrika (+1589), mtoto wa watumwa huko Italia, Mnegro wa kwanza kutangazwa mtakatifu, Umile wa Bisignano (+1637), mnyenyekevu ajabu, na Karolo wa Sezze (+1670), aliyeandika vizuri sana kuhusu maisha ya kiroho; halafu mapadri Pasifiko wa San Severino (+1721), aliyezingatia sana maisha ya sala, na Leonardo wa Portomaurizio (+1751), tunda bora la Kirekebisho kilichoanzia mjini Roma karne XVII. Pia walipatikana wenye heri 4.

Huko Hispania, baadhi ya wafuasi wa urekebisho wa Pekupeku, baada ya kuunganishwa na Waoservanti (1517) walimkimbilia Mkuu wa Wakonventuali ili kukwepa vizuio vya OFM, na mmojawao, Petro wa Alcantara (+1562) akafanywa Mkurugenzi wao (1557). Alipokufa, Papa Pius IV (1560-1565) akawahamisha Waalkantara chini ya Waoservanti lakini bila ya kufuta kanda zao, katiba yao na mavazi yao maalumu. Papa Gregori XIII (1572-1585) akamkataza Mkuu wa OFM asiingilie masuala yao ya ndani (1578), na Papa Urban VIII (1623-1644) akawaruhusu wasifuate tena katiba ya shirika lote (1642). Jinsi sisitizo la sala na toba linavyozaa matunda imethibitishwa na umisionari wao (Amerika na Asia Mashariki) na hasa na watakatifu 9 wa urekebisho huo, wakiwa ni pamoja na Paskali Baylon (+1592), mwenye ibada ya pekee kwa Ekaristi, Petro Batista, Martino wa Kupaa na Fransisko Blanco, mapadri, halafu Fransisko wa mt. Mikaeli, Gonzalo Garcia na Filipo wa Yesu, mabradha, ambao wote walifia dini Japani (+1597), hatimaye Yohane Yosefu wa Msalaba (+1734), mpenda ufukara mkuu. Pia walipatikana wenye heri 22.

Huko Ufaransa makao ya upwekeni hayakustawi sana hadi mwisho wa karne XVI. Mwaka 1601 walioishi huko wakapewa na Kanisa Mkurugenzi mwenye mamlaka pana sana; hapo wakaenea haraka kwa msaada wa mfalme, hata kanda zote za Ujerumani na Uholanzi zikajirekebisha na kujiunga nao, wakaitwa Warekoleti. Mmojawao ni John Wall (+1679), aliyefia dini huko Uingereza.

Katika karne XVI-XVII karibu kila mkutano mkuu wa OFM ulizungumzia katiba na kupigania umoja, ambao haukuwa rahisi kutokana na mchanganyiko wa ndugu waliopenda fadhili za Wakonventuali na wengine waliotaka urekebisho. Katika hali hiyo Watumishi wakuu walijitahidi kuhuisha shirika lote, lakini wengi wao walitumwa na Mapapa kama mabalozi kwa wafalme na Maaskofu wa Ulaya, au walipewa uaskofu wa miji muhimu. Shirika halikupendezwa kwa sababu lilikuja kukosa uongozi imara: ndiyo maana mara kadhaa liliwadai kiapo cha kutokubali kazi hizo au walau cha kujiuzulu Utumishi. Watakatifu waliopatikana kipindi hicho ni: Salvatore wa Horta (+1567), bradha aliyefanya miujiza mingi ajabu (labda milioni moja), Nikolaus Pieck, Jeromu wa Weert, Teodoriko van der Eem, Nikasi wa Heeze, Wilehadi wa Denmaki, Godefrid wa Melveren, Antoni wa Weert, Antoni wa Hoornaert, Fransisko wa Roye, mapadri, halafu Petro wa Assche na Korneli wa Wijk-bij-Durstede (+1572), mabradha, ambao wote walifia dini Uholanzi, John Jones (+1588), aliyefia dini Uingereza, hatimaye Fransisko Solano (+1610), mmisionari bora Amerika Kusini aliyezunguka kotekote kwa miaka 14, akihubiri na kuimba. Wenye heri wa kipindi hicho ni 17.

Karne XVII ikawa ya utulivu na utendaji, lakini ongezeko kubwa mno la watawa lilisababisha matatizo makubwa na ulegevu hata katika marekebisho. Pamoja na utaifa kuzidi, matawi ya Italia yalishindana kwa maandishi makali ya kukwaza. Makwazo mengine yalitokana na desturi ya Watumishi kadhaa kutuma watawa wasiofaa kwenye kanda nyingine au kuwaacha nyumbani mwa marafiki au ndugu. Badala ya juhudi za watawa kwa ajili ya kanuni kama katika karne zilizopita, sanasana tunakuta viongozi wakijitahidi kuwalazimisha washike kanuni, lakini bidii za namna hiyo hazikuweza kufanikiwa kwa kuwa hazikutoka moyoni mwa watawa. Hatimaye mwaka 1676 mkutano mkuu ulikubali na kuagiza kila kanda ianzishe makao 3-4 ya upwekeni ambapo yafanyike malezi ya watakaji na wanovisi wote: baadaye katika mazingira hayo walistawi Thomas wa Cori (+1729), mhubiri maarufu na Teofilo wa Corte (+1740), mwanafunzi wake. Mtakatifu mwingine ni Junipero Serra (̟+1784), padri Mhispania aliyeinjilisha kwa mara ya kwanza Kalifornia (leo Marekani Magharibi). Lakini katika karne XVIII ilionekana wazi jinsi matazamio ya wengi yalivyolenga kupata kwa visingizio vyovyote fadhili na nafasi za kwanzakwanza. Kupitia mikutano mikuu upuuzi wa namna hiyo uliathiri sheria za shirika. Pia mabadiliko mengi mno ya katiba, badala ya kusaidia nidhamu, yalizidi kuipunguza kwa kusababisha ndugu wasiijali katiba isiyodumu.

Upande wa Wakonventuali, utengano na Waoservanti haukuwaondolea baadhi yao wasiwasi kuhusu utekelezaji wa kanuni, ingawa Mtaguso wa Trento ulitamka (1563) kwamba OFM na Wakapuchini tu hawaruhusiwi kuwa na mali hata kishirika, tofauti na Wakonventuali na mashirika mengine yote. Uhusiano na matawi yaliyokimbilia chini ya Mkuu wao ili kufuata urekebisho ulichochea hamu ya kuwaiga. Ndivyo walivyoanza Wakonventuali wa Urekebisho Hispania: uenezi wao ulichangia uamuzi wa Papa Pius V (1566-1572) wa kuunganisha na OFM Wakonventuali wote wa Hispania na Ureno (1566-1567). Juhudi za mikutano, za Watumishi wakuu na za watawa wenyewe zilileta nidhamu na ustawi, hasa mmojawao alipochaguliwa kuwa Papa Sixtus V (1585-1590) akaanza kuwasaidia kwa kila njia, kama vile kuunganisha chini ya Wakonventuali marekebisho madogo yaliyokuwa yameanza Italia (1562). Ila mwaka 1669 yakaja kutawanywa, baada ya kusumbuliwa sana na Wakonventuali wa kawaida na Wakapuchini (kuhusu sare zao zilizofanana). Kabla ya hapo mkutano mkuu ulitunga katiba mpya kabisa (1625) ili kuondoa misimamo tofauti kuhusu kanuni: katiba hiyo haikufuata matamko ya zamani ya Mapapa juu ya kanuni, bali ilipitisha moja kwa moja desturi za shirika zilivyokuwa. Baada ya kuthibitishwa na Urbani VIII, Wakonventuali wakaanza kuweka nadhiri zao kwa kutamka wazi kuwa watashika kanuni “kadiri ya katiba ya Urbani” tu.

Baada ya kujipatia hivyo msimamo wa kudumu, Wakonventuali wakazaa mwenye heri 1 na watakatifu 2 waliong’aa mmoja hasa upande wa sala, mwingine upande wa utume: Yosefu wa Copertino (+1663) na Fransisko Antonio Fasani (+1742), wote mapadri. Pia shirika liliendelea kusifiwa upande wa elimudini likaona mtawa wake mwingine kuwa Papa Klementi XIV (1769-1774) ambaye naye alilipendelea sana, k.mf. kwa kuwahamisha Waoservanti wote wa Ufaransa chini ya Wakonventuali. Kwa mara nyingine upendeleo huo ukazaa chuki ya wengine ilivyojitokeza kisha kufa kwake.

Takwimu ya jumla ya Utawa I ni kama ifuatavyo:

Mwaka 1575 hivi: (Waoservanti) 32,750; (Pekupeku) 1,700; (Wariformati) 500; (Warekoleti) 50 = OFM jumla 35,000; Wakonventuali 12,000; Wakapuchini 3,600 = Jumla kuu 50,600

Mwaka 1700 hivi: (Waoservanti) 36,400; (Pekupeku) 6,600; (Wariformati) 13,900; (Warekoleti) 9,200 = OFM jumla 66,100; Wakonventuali 15,200; Wakapuchini 27,300 = Jumla kuu 108,600

Mwaka 1762 hivi: (Waoservanti) 39,900; (Pekupeku) 7,000; (Wariformati) 19,000; (Warekoleti)11,000 = OFM jumla 76,900; Wakonventuali 21,000; Wakapuchini 34,000 = Jumla kuu 131,900.

Bila ya kujali tofauti kati ya tawi na tawi, karibu 60% walikuwa mapadri, ambao nusu ya idadi yao walikuwa wahubiri, nusu “mapadri wa Misa na sufuria” tu. Ongezeko lilipungua kwanza kutokana na Uprotestanti kuenea na kufuta kanda kadhaa Ulaya Kaskazini, na utawala wa Kiislamu kuenea Ulaya Mashariki Kusini, ingawa pande nyingine zilifidia. Karne yenye ongezeko la kasi zaidi ni ile ya XVII: ndio mwanzo wa wasiwasi na hofu kwa viongozi wa Kanisa na serikali, kwa kuwa mashirika mengine pia yalikua. Kuanzia mwaka 1634 Mapapa walichukua hatua kuzuia upokeaji wa wanovisi na kupunguza konventi (Italia zilifungwa 24.2%), hata kufikiria uwezekano wa kuwapeleka watawa vijana kupigana na Waturuki ili kuwapunguza! Lakini hatua hizo hazikufanikiwa. Kuhusu uenezi, wakati wa kufikia kilele cha idadi ya wanashirika mgawanyo ulikuwa ifuatavyo:

Italia na visiwa 52,400; Hispania na makoloni 26,100; Ufaransa 21,000; Ujerumani n.k. 20,300; Ureno na makoloni 4,000; Dola la Waturuki 2,800; Polandi na Urusi 3,000; Uingereza na Irelandi 1,750.

Maisha ndani ya shirika

[hariri | hariri chanzo]

Kadiri ya hati ya utengano (1517) Mkuu wa Waoservanti tu alikubaliwa kuitwa Mtumishi mkuu, wakati yule wa Wakonventuali alipewa jina la Mwalimu Mkuu; vilevile viongozi wa kanda. Lakini jina hilo jipya halikuja kutumika. Mkuu wa Wakapuchini aliitwa Makamu (wa Mkuu wa Wakonventuali aliyetakiwa kumthibitisha baada ya kuchaguliwa). Jina la “Mtumishi mkuu wa Shirika lote” lililotumiwa na Mkuu wa OFM lilichukiwa na kulalamikiwa na Wakonventuali na Wakapuchini, hadi Paulo V alipotamka kuwa hao wote ni wana halisi wa Fransisko, na Wakuu wao ni waandamizi wake halali (1619). Hata hivyo mabishano ya wazi yakaendelea kuhusu mlolongo wa uandamizi huo, mtindo asili wa kanzu na hasa kofia yake, mpaka Papa Alexander VIII (1689-1691) alipokataza maandishi yote juu ya hayo.

Kwanza Kardinali mlinzi alikuwa mmoja kwa wote, halafu Wakapuchini wakakubaliwa kuwa na mmoja wa kwao (1564), na vilevile Wakonventuali (1580). Mara kadhaa waliingilia mno masuala ya shirika hadi kulivuruga na kusababisha Mapapa walazimike kuwazuia. Mamlaka yao ilipungua ilipoanzishwa Idara ya Papa kwa Watawa (1586). Tofauti kati ya matawi kuhusu miundo ya ndani ziliendelea, hasa upande wa mikutano, lakini hazikupata kamwe kuwa kubwa mno, kwa sababu ya kanuni na mapokeo yao kuwa mamoja.

Haikuwa rahisi kwa viongozi kuhuisha kiroho umati mkubwa vile wa watawa, hasa tukizingatia jinsi Wafransisko wasivyopangika. Ili kuleta nidhamu zilitumika mbinu za kisheria: ziara za Mkuu zilizofanyika kwa ukali na adhabu hata ya kufungwa na kufukuzwa. Mbinu mpya (hasa kuanzia katikati ya karne XVII) ni mazoezi ya kiroho; pengine zilisambazwa pia barua za Mkuu.

Maisha ya kiroho yalistawi hasa Hispania katika karne XVI, Ufaransa katika karne XVII, na Italia katika karne XVI-XVIII. Katika hiyo karne ya dhahabu ya Hispania, Ndugu Wadogo walichanga na wananchi wenzao walioandika juu ya maisha ya kiroho: ufafanuzi kamili wa mang’amuzi ya ndani na teolojia ya kiroho pamoja na ugumu wa maisha, ingawa walifuata mapokeo ya shirika kwa kusisitiza zaidi uhuru wa roho, ubora wa upendo na usahili katika kumuelekea Mungu. Ndugu wa Italia walielekea zaidi utendaji hasa katika huruma, hivyo hawakulenga mirukoruko katika ibada. Hasa Wakapuchini walijitahidi toka mwanzo kuandika vitabu vyenye lengo la kujenga kiroho wasomaji na kuwaelekeza wote katika sala kama njia bora ya kurekebisha maisha. Ndugu wa Ufaransa walizingatia hasa matakwa ya Mungu kama muhtasari wa hatua tatu za maisha ya kiroho.

Katika karne hizo mtindo wa Baroko ulitawala sanaa na maisha ya jamii pia, ukijali sura kuliko undani, vitendo kuliko moyo: hivyo mapambo na madoido yakazidishwa sana. Hiyo ni sababu mojawapo ya marekebisho kusifiwa kadiri yalivyojitokeza katika miguu mitupu, nguo duni, majengo fukara na mwenendo adili. Mambo hayo yalipotokana na msimamo wa moyo yalijenga kweli, tofauti na yalipofanyika kwa nje tu.

Maisha katika marekebisho yalikuwa magumu, si ya kuvutia, ingawa riziki hazikukosekana kwa ukarimu wa walei. Kila mmojawapo mwanzoni ulilenga kuwa na ndugu wachache katika nyumba ili kurahisisha usahili, ufukara na udugu, lakini polepole idadi ikaongezeka kwa faida ya taratibu za kitawa na hasa fahari ya ibada. Mwaka 1680 kwa wastani kulikuwa na ndugu 17 kwa nyumba; mwaka 1762 walifikia 20. Pamoja na mapadri, mafrateri (kwa maana ya wenye kusomea upadri au walau walionyolewa tonsura) na mabradha kulikuwa na Watersyari wa kudumu katika jumuia. Mwanzoni mwa kila urekebisho mabradha walikuwa wengi, halafu wakazidi kupungua kutokana na kuchujwa sana; lakini pia kwa sababu wakazidi kukosa nafasi, wakipangwa hata baada ya wanovisi watakaosomea upadri! Mtaguso wa Trento uliwanyima haki ya kupiga na kupigwa kura, ila Pius V aliwarudishia Wakapuchini. Hivyo mabradha wengi walijitafutia ruhusa ya kuhamia kati ya mafrateri, kinyume cha sheria. Wasio mapadri walizidi kupokea Komunyo kuliko zamani. Shida kubwa ilikuwa bado namna ya kuwapa kazi mapadri wasio wahubiri, kwa kuwa hawakufanya utume wala kazi za mikono. Shughuli kuu ilikuwa Misa na Sala ya Kanisa iliyoadhimishwa usiku (lakini kwa Wakonventuali si mahali pote) na mchana kwa nyimbo (isipokuwa Wakapuchini na Wariformati walipendelea kuacha nafasi zaidi kwa sala ya moyo).

Haja ya kutafuta miito haikuwepo; kazi ilikuwa kuichuja tu kwa majaribu mengi. Hata desturi ya Wakonventuali ya kupokea watoto ikaja kwisha karne XVI. Ili mtu apokewe kama frateri alipaswa kuwa na elimu ya msingi na kujua Kilatini. Hayakufikiriwa makao ya malezi kwa watakaji. Kwa wanovisi Papa Klementi VIII (1592-1605) aliagiza (1596) zichaguliwe tu nyumba ambapo maisha ya kitawa yanashikwa kikamilifu; tena watengewe sehemu maalumu na kuwasiliana na mlezi wao na msaidizi wake tu, pamoja na kushiriki ratiba ya jumuia (sala, milo n.k.). Katika karne XVIII zikaanza kutokea nyumba za unovisi kwa mabradha tu, zilizozidisha utengano wa kitabaka ndani ya shirika. Kazi ya mwaka wa jaribio ilikuwa hasa kueleza kanuni na amri zake kadiri ya matamko ya Mapapa; mapokeo ya shirika; nidhamu; juhudi za kiroho; taratibu za ibada (pamoja na kuimba, kwa Wakonventuali na Waoservanti); Sala ya Kanisa; hasa utekelezaji wa sala na maadili. Walezi bora waliandika vizuri juu ya mang’amuzi yao. Baada ya nadhiri (ambazo zilikuwa za daima tu) watawa chipukizi walitakiwa kuendelea na malezi miaka mitatu katika nyumba ya kuaminika. Kulikuwa na maagizo kuhusu malezi ya kudumu pia (vipindi vya mara kwa mara kwa wote).

Mikutano mikuu ilishughulikia utume wa kuhubiri ikisisitiza ndugu waandaliwe na kuchujwa kwa makini, halafu wasiofaa wanyang’anywe ruhusa. Pia zilipangwa ngazi mbalimbali: kuanzia wahubiri wa konventi na wa kanisa lake hadi wahubiri wakuu wa mahali muhimu zaidi alipojiwekea Mtumishi mkuu (Italia palikuwa 30). Lakini mvuto wa elimu ulisababisha huduma za kiroho zisizingatiwe sana na ndugu wenye vipawa vingi zaidi. Basi, ili kuwavuta wakahubiri na kuungamisha Mkuu wa OFM alipewa haki ya kuwapa fadhili na vyeo, kama kawaida ya wakati huo.

Urekebisho wa Wakapuchini ulipinga mitindo ya kuhubiri kwa kurudia unyofu wa Injili, kuhimiza ushuhuda wa maisha na kulenga wongofu wa wasikilizaji. Kwa karne moja na zaidi hao waliendelea kuwa wahubiri bora, kwa jinsi wanavyoelewa watu na kugusa sio akili tu, bali mioyo pia, ya wadogo na hata ya wasomi. Hayo yalikuwa matokeo ya maisha bora ya kiroho, lakini pia ya maandalizi ya mpango chini ya walimu wa hakika. Walipoanza (1650 hivi) kufuata mitindo ya Baroko, matunda yakapungua. Wahubiri waliongoza pia roho binafsi. Wafransiskani waliungamisha sana, kumbe Wakapuchini walisita kupokea kazi hiyo, isije ikavuruga maisha yao ya sala hasa. Walianza kuifanya nje ya Italia (katika mkoa wa Alsasya kati ya mwaka 1740 na 1747 waliungamisha mara 24 milioni!), lakini walitakiwa kuwa na sifa maalumu.

Kati ya mahubiri zilishika nafasi ya pekee wiki za uamsho, hasa kuanzia mwaka 1650 hivi. Waliokusudiwa kuziendesha walidaiwa maandalizi kamili. Baadhi zilifanywa na ndugu 30 hadi 60 kwa pamoja. Kulikuwa na mafundisho maalumu kwa makundi (watoto, vijana, akina baba, akina mama) na pengine mfungo wa siku nne kwa makundi ya pekee. Mbinu zilikuwa mbalimbali, lakini licha ya kufundisha imani na maadili Wakapuchini hawakukosa kuelekeza watu wote namna ya kufanya sala ya moyo. Wahispania walitumia sana maandamano ya toba, rozari za hadhara n.k. Waitalia walikuwa wakipanda msalaba karibu na mji au kijiji uwe kumbukumbu. Maarufu kuliko wote waliofanya kazi hiyo ni Leonardo wa Portomaurizio, aliyeendesha wiki hizo mara 343, akiongozana kwa kawaida na mapadri 4 na bradha 1. Baada ya wiki mbili za mahubiri kulikuwa na wiki moja ya maungamo. Katika miaka 44 aliokoa watu wengi ajabu, na kuinua hali ya roho ya mapadri wanajimbo na watawa katika Italia karibu nzima. Ndiye mwenezaji mkuu wa Njia ya Msalaba, ibada iliyoanza kustawi katika karne XV ikiwa na vituo 7 hadi 37, mpaka ile ya 14 ilipopewa rehema ya pekee (1686) na hivyo kuenea popote. Kumbe kiini cha wiki za uamsho za Wakapuchini kilikuwa ni kuabudu ekaristi kwa saa 40 mfululizo, ibada iliyoanza mwaka 1535 na kutoa nafasi ya kuhubiri kwa nguvu zaidi.

Mkingiwa Dhambi ya Asili alivyochorwa na Bartolomé Esteban Murillo, 1678, Museo del Prado, Hispania.

Ndugu Wadogo walieneza ibada nyingine pia, hata kabla Kanisa halijazikubali rasmi, kama vile kwa Moyo wa Yesu, kwa Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili (aliyetangazwa na mkutano mkuu wa mwaka 1645 kuwa msimamizi wa shirika) na ile ya kujifanya watumwa wake. Kuanzia karne XV Wakonventuali walieneza rozari ya furaha saba za Bikira Maria, na chama cha kamba ya Kifransisko (ambayo hata watakatifu 4 wasio wanashirika walipenda kuivaa kiunoni). Ndugu Wadogo waliendelea kushika nafasi muhimu katika Kanisa: 739 walikuwa Maaskofu (kati ya mwaka 1503 na 1710), 16 Makardinali (karne XVI-XVIII), na 2 wakafikia Upapa. Wengine pia waliathiri sana siasa, k.mf. katika vita vya madhehebu, katika kutetea haki za Kanisa dhidi ya serikali, na hasa kama mabalozi wa Mapapa na wa wafalme Wakatoliki.

Hasa Wakapuchini walijihusisha na aina mbalimbali za utume wa kijamii, wakidaiwa na katiba kujitosa hadi ushujaa. Kwa namna ya pekee walifanya hivyo yalipoenea maradhi ya kuambukiza, hasa tauni. Katika karne XVI-XVII kila mara walijihatarisha na kufa ili wahudumie kiroho na kimwili walioambukizwa. Ilivutia sana kuona wanajumuia wote kujitolea. Tunafahamu zaidi ya ndugu 2,000 waliokufa hivyo, lakini walikuwa walau mara mbili zaidi, bila ya kuhesabu ndugu wengi wa matawi mengine. Katika miji mingi walikabidhiwa uongozi wa hospitali nzima, hata nje ya nyakati za tauni. Zaidi ya hayo Wakapuchini hasa walihudumia kiroho wagonjwa na walio mahututi, walianzisha vyama vya kutolea huduma hizo, walichapisha vitabu juu yake, walipenya magereza ili kuhudumia wafungwa na waliohukumiwa kufa. Ufaransa walikuwa wazimamoto pia. Hata vita viliwapa nafasi za kujitoa kwa upendo kama mapadri wa wanajeshi, hasa katika kuzuia Waturuki Waislamu wasiteke Ulaya nzima kati ya mwaka 1571 na 1686. Wafalme pia waliwatafuta sana Wakapuchini kama wahudumu wa roho na wa mwili wa askari wao.

Ndugu Wadogo walipambana na mifumo mbalimbali iliyofuatana kuzuka karne hizo na kupotosha imani na maadili, hasa Uprotestanti. Dhidi ya Rinascimento iliyotaka kurudisha Ulaya kwenye mitazamo ya kipagani, marekebisho ya karne XVI yalihubiri toba na kushuhudia dharau ya anasa. Dhidi ya Ujanseni shirika lilitetea kwa mahubiri na maandishi kipeo cha Kiinjili na mapokeo ya ibada. Dhidi ya waasi wa dini walioshambulia misingi ya Ukristo, huko Ufaransa walianzisha hata gazeti la kutetea dini.

Ingawa uenezi wa Uprotestanti ulifunga konventi nyingi, hakuna hata moja iliyoasi jumla. Idadi ya Wafransisko waliouingia ni ndogo kulingana na ile ya walioupinga tangu ulipoanza, kabla wengi hawajatambua hatari. Kardinali wa Brandeburg aliwakataza (1519) wasiendelee kuhubiri dhidi ya Martin Luther, kumbe Mtumishi mkuu alipofika Ujerumani aliagiza maandishi yake yachomwe, wahubiri waandaliwe kumshambulia tena na wanashirika wote wasali na kujiandaa kufia imani (kama walivyofanya walau 500 katika miaka 1520-1620). Walutheri walitokeza chuki yao kwa kueneza kitabu cha dhihaka “Kurani ya Pekupeku”. Baadaye Ndugu Wadogo wakawa kati ya mashirika muhimu zaidi katika kurudisha Ukatoliki kwenye miji na vijiji. Wakapuchini walianza kupambana na Uprotestanti kwa mahubiri na katekesi huko Italia usije ukaipenya, wakawa wa kwanza kujitolea kutumwa na Idara ya Papa kwa Uenezaji wa Imani mara ilipoanzishwa (1622). Chini yake juhudi ziliongezeka na kupangwa vizuri zaidi. Chuo chake mjini Roma kilianzishwa (1627) hasa kwa juhudi na ukarimu wa Kardinali Mkapuchini. Idara ilikuwa ikituma wale wote waliopendekezwa na wakubwa wao wakiwa na sifa upande wa maadili na elimu. Katika karne XVII idadi kubwa ya waliotumwa ni Wakapuchini. Agizo la shirika lilikuwa kuwasiliana na Waprotestanti kwa kufuata mbinu za Fransisko wa Sales (+1622), yaani kwa upole, usikivu na ushuhuda wa maisha safi yenye kujitosa. Pia Wakapuchini walishirikisha waamini katika kazi hiyo ngumu, na kuandika vitabu vya mabishano. Huko Uingereza na Irelandi baada ya kufukuzwa wote, kwa karne tatu Wafransiskani wakaendelea kuingia ili kufanya utume kwa siri kutoka Ulaya Bara walipopokea na kulea miito ya visiwa hivyo.

Wakonventuali walifanya kazi hasa kati ya Waortodoksi, wakivuta baadhi yao upande wa Roma na kutunza makundi madogomadogo ya Wakatoliki waliosambaa Mashariki. Pia walizuia Uprotestanti usienee kati ya Waortodoksi, hasa kwa kufaulu kumuondosha Patriarki wa Kostantinopoli aliyetaka kuhalalisha ungamo la imani la Wakalvini. Idara ya Papa ilistawisha pia misheni za Waoservanti chini ya utawala wa Waturuki, ambapo wengi walifia dini. Vilevile Wakapuchini walienea sehemu hizo na Urusi. Katika karne XVI Wafransiskani walichuma tunda bora India Kusini walipoungana na Roma Askofu Msiro-Malabari na familia 30,000. Wariformati walifanya kazi miaka 160 Ethiopia wakamwaga damu yao kwa wingi wasikate tamaa.

Kuhusu uenezaji Injili kwa wasio Wakristo, karne XVI-XVII zilikuwa na miito mingi ya kimisionari, hata likatokea swali, “Je, Watumishi wanaweza kuzuia watawa wasiende kwenye nchi za misheni?”. Kumbe karne XVIII wito huo haukuvutia tena umati wa ndugu wasio na kazi, hata swali likawa tofauti kabisa, “Je, Watumishi wanaweza kuagiza watawa wao waende Amerika?”. Mkuu wa OFM alifikia hatua ya kutangaza atawatenga na Kanisa watakaozuia watawa wasifuate wito huo. Kwa kuwachagua na kuandaa vilikuwa muhimu vyuo vya kimisionari, hasa miito hiyo ilipopungua: pamoja na kuwakusanya, kazi yake ilikuwa kuwafundisha lugha na kuwalea kiroho na kichungaji. Mara kwa mara Wakapuchini walisita kukubali misheni za mbali kwa kuhofia mazingira yatafanya watawa washindwe kufuata maisha ya shirika yaliyopangwa mtindo mmoja; pia umbali utamzuia Mkuu asiwatembelee kama desturi: ndiyo sababu hawakuanzisha miundo ya kudumu huko.

Upande wa Asia, Waturuki Waosmani walipoteka Yerusalemu (1517) walifunga wamisionari wote kwa miaka mingi, wakaendeleza dhuluma za kila aina pamoja na kuchochea ushindani na Waortodoksi kuhusu kumiliki mahali patakatifu hata kusababisha wauane nao. Utaifa uliwavuruga vilevile. Wafransiskani walianzisha kanda huko India (1583) wakazidi kuenea Mashariki hadi Indonesia walipoanzisha kanda nyingine (1622). Misheni za Filipino ni sifa kubwa ya Pekupeku walioanzisha kanda huko (1586) na kulipatia Kanisa (kwa msaada hasa wa Wajesuiti) nchi kubwa pekee ya Kikatoliki katika Asia nzima. Toka huko wakaenea katika nchi zote za kandokando kuanzia China, walipoongoa mtu aliyekuja kuwa Askofu Mchina wa kwanza. Ila mabishano yao na Wajesuiti kuhusu mbinu za umisionari yalikwaza sana hata kudai Papa aingilie kati. Dhuluma zilipoanza (1723), thuluthi moja ya Wakatoliki 300,000 wa China walikuwa chini ya Ndugu Wadogo, ambao wakafichama na kuendelea na kazi yao, bila ya kujali jela na kifo, kama walivyofanya pia Vietinamu na Kampuchia. Hata Japani ulizuka ushindani na Wajesuiti, halafu dhuluma kali za serikali, lakini umisionari ukaendelea na kuongoa wengi zaidi. Baada ya Wafransisko 354 wa Utawa I na III kufia dini, waamini wakaendelea kwa siri bila ya mapadri: wamisionari wapya walipofika (1865) wakakuta Wakristo wenye majina ya Kifransisko! Upande wa Wakapuchini walianzisha misheni India (1632) ambapo walishindana na Wajesuiti kuhusu madhehebu ya Kimalabari hadi mwaka 1744. Sifa kubwa zaidi ilipata misheni ya Tibet (1707-1745) iliyoeneza Injili hadi Nepali, Butani na Bengala.

Tofauti na India, Afrika na Brazili (zilizokabidhiwa na Papa kwa Wareno), sehemu nyingi za Amerika zilikabidhiwa kwa Wahispania. Kanda OFM ya visiwani ilizidi kustawi hata watawa wake kufanya kazi ngumu Venezuela na Guyana (1540); baada ya majaribio kadhaa wakafaulu kupenya kati ya wazalendo wa Panama halafu kuenea Kolombia, ambapo hadi mwisho wa karne XVI walibatiza Wahindi Wekundu 200,000. Wakati huo barani kulikuwa na kanda yenye ndugu 145; miaka 100 baadaye walikuwa 338. Wafransiskani 2 walifika Mexico pamoja na wavamizi (1519), lakini kazi rasmi ilianza miaka 5 baadaye, walipotumwa Waguadalupe 12 walioandaliwa vizuri; hao wakatunga sarufi, kamusi na katekisimu kwa lugha ya Kiazteka na kuanzisha shule. Watu waliongoka kwa wingi mkubwa ajabu: 200,000 hadi mwaka 1529, 1,000,000 hadi 1531, 5,000,000 hadi 1536, 9,000,000 hadi 1540 (Wamersedari, halafu Wadominiko na Waagustino walisaidia pia). Ndugu Wadogo walienea Kusini (1525) hadi Gwatemala, Honduras na Nikaragua, na Kaskazini (1527) katika maeneo ambayo sasa ni Marekani Kusini. Kanda ya Mexico iliyoanzishwa mwaka 1535 ikazaa nyingine 7 hadi Marekani Kusini (1612). Pekupeku pia walianzisha kanda (1599). Mwisho wa karne XVII kulikuwa na Wafransiskani 2,400, wengi wao wakiwa wananchi. Wavamizi wa Peruu pia waliongozana na Wafransisko katika safari ya kwanza (1527), halafu wakaletwa “mitume 12” waliofanya kazi bora Meksiko (1531), wakifuatwa na wengine wengi kutoka Hispania hata ikaundwa kanda (1553) ambayo nyumba yake mojawapo ilifikia kuhudumia parokia 29 kati ya Wahindi Wekundu: Wafransisko 129 waliuawa nao. Mjini Lima ilianzishwa konventi kubwa ya malezi kwa wamisionari wa Amerika Kusini karibu nzima. Mapema waliingia Ekwador (1533) wakaunda kanda (1565), sawasawa na walivyofanya Chile, ingawa huko hawakuongezeka sana kwa sababu wengi waliuawa katika mapigano ya muda mrefu ya wenyeji dhidi ya wakoloni. Toka Peruu Ndugu Wadogo walifanya umisionari kati ya Wahindi Wekundu wa Bolivia pia hadi mwaka 1793. Walikuwa pia wa kwanza kufika Amerika Kusini Mashariki (Paragwai, Ajentina na Urugwai) ilipoanzishwa kanda (1612). Huko Brazili, kwa miaka 100 Pekupeku walianzisha kanda mbili (1657, 1675). Katika karne XVII waliingia pia Wakapuchini na Waoservanti kufanya kazi hasa kwa Wahindi Wekundu, halafu kwa Wanegro na Wazungu. Wafransiskani wengine walifanya kazi katika makoloni ya Waingereza Marekani Magharibi, ingawa mmojammoja tu, halafu Wakapuchini waliingia katika makoloni ya Wafaransa visiwani, Guyana na Marekani ya Kati (1722), wakafanya kazi miaka mingi Panama, Haiti, Trinidad n.k. Hata Kanada wamisionari wa kwanza walikuwa Ndugu Wadogo (Warekoleti kuanzia mwaka 1615, halafu Wakapuchini): misheni zao zilifungwa kila mara maeneo ya Wafaransa yalipotekwa na Waingereza.

Upande wa Afrika, misheni ya Moroko iliendelea hadi alipouawa Mfransiskani wa Italia (1532) ikafunguliwa tena na Wakapuchini (1624-1700), wakifuatwa na Pekupeku (kuanzia 1630). Huko Tunisia Wakapuchini walipojaribu mara ya pili walifaulu kufungua nyumba (1674). Huko Libya Wariformati (1630), halafu Wakapuchini waliendelea muda mrefu kwa matunda mengi. Huko Misri Wafransiskani waliendelea hadi karne XIX. Afrika Magharibi (Gine, Kepuvede, Siera Leoni) walifanya kazi zaidi Wakapuchini (kuanzia 1634), ingawa walifukuzwa mara kadhaa. Wafransiskani walianzisha misheni ya kudumu Kepuvede (1656), iliyoeneza kazi yake hadi Siera Leoni. Misheni bora ni ile ya Wakapuchini Kongo-Angola (1645-1835), ingawa kulikuwa na matatizo mengi (kwa miaka 100 walifia huko wamisionari 144). Aliyeianzisha alikubaliwa kufungua nyingine Nijeria (1651-1693). Wakapuchini walianzisha misheni nyingine ya kudumu katika kisiwa cha Saotome (1686) wakihudumia hata Wakristo wa pwani.

Mtaguso wa Trento ulikuwa fursa kwa kila shirika kutambulisha wasomi wake. Ndugu Wadogo waliuchangia sana kupitia Maaskofu na wanateolojia waliohudhuria: Wakonventuali 67, Waoservanti 57 na Wakapuchini 8. Idadi inaonyesha kuwa upande wa masomo, waliofanya juhudi zaidi ni Wakonventuali, kwa kuwa hawakupatwa kamwe na wasiwasi wa marekebisho yote kuhusu hatari zake. Labda ndiyo kazi kubwa zaidi waliyolifanyia Kanisa, hasa kama washauri wa Idara za Mapapa na kama waandishi wa vitabu. Hata Waoservanti, walipoondoa wasiwasi huo, wakaona masomo kuwa kazi ya lazima kwa shirika, wakaendelea sana katika elimu (karne XVI-XVII). Kati ya Wakapuchini elimu ilishirikishwa kibinafsi tu, wasianzishe nyumba za masomo mpaka Mtaguso huo ulipolazimisha kuyapanga. Hapo wakasisitiza ndugu wasisome kwa ajili ya elimu, bali kwa kujirekebisha na kurekebisha wengine. Kwa jumla Ndugu Wadogo, hasa Italia, walikwepa vyuo vikuu na digrii mpaka Sisto V, katika jitihada zake kwa ajili ya Wakonventuali wenzake, alipoanzisha (1587) Chuo cha mt. Bonaventura kama kiini cha shirika lao upande wa elimu. Mwalimu huyo na Yohane Duns Scoto ndio waliofuatwa zaidi na Ndugu Wadogo wa karne hizo, ingawa hakuna aliyetangazwa rasmi kuwa afuatwe na shirika katika falsafa na teolojia. Katika nusu ya kwanza ya karne XVII walimtetea sana Scoto dhidi ya mashambulizi ya Wadominiko (washabiki wa Thoma wa Akwino), hata baadhi wakajaribu kumfanya atangazwe hivyo ili shirika lijitukuze kwa wataalamu wake kama mengine yalivyofanya. Mabishano hayakusaidia kujua ukweli, bali yalijenga ukuta kati ya mashirika hayo mawili yenye udugu wa asili. Hatimaye mkutano mkuu ukahimiza (1651) uhusiano mzuri na Wadominiko katika elimudini, shetani asiachiwe nafasi ya kufitini. Wakonventuali na Waoservanti waliujali sana muziki pia, kinyume cha Wakapuchini na Wariformati.


Ndugu Wadogo katika ulimwengu wa kisasa (1762–2005)

[hariri | hariri chanzo]

Matatizo ya ndani na ya nje (1762–1869)

[hariri | hariri chanzo]

Ongezeko la watawa lilifikia kilele chake kati ya mwaka 1760 na 1770, likishinda vizuio vilivyowekwa na viongozi wa Kanisa. Kama kawaida, shaka zilizosababishwa na mageuzi ya harakaharaka katika jamii na uchumi zilichangia pia ongezeko la miito ya wasiwasi yenye kutafuta usalama konventini. Kadiri hiyohiyo ilionekana wazi kuwa wingi si hoja na kuwa umati wa watawa haukuhuishwa na vipeo halisi. Uvivu haukuepukika ukazaa ulegevu na maovu mengi. Ingawa watu wadogo waliendelea kuwaheshimu watawa, wasomi walizidi kuwaona vielelezo wa tunu zisizo na maana tena. Jamii ilipokuwa inaelekea kasi matazamio mapya hata upande wa dini, watawa walizidi kujitenga konventini wakijali desturi zao na elimu yao ya kidini bila ya mawasiliano na elimudunia. Kati yao wachache tu walijitahidi kulinganisha imani na sayansi.

Kwa muda mfupi mashirika, hasa ya Ombaomba, yalikuja kudharauliwa na wengi. Kufuatana na mawazo mapya kuhusu uchumi, serikali zilizidi kuyatazama kama mzigo au donda kwa jamii. Bahati mbaya, hali ya mashirika ilistahili lawama nyingi zilizotolewa. Sababu nyingine zilizoleta dhoruba juu ya watawa ni kwamba serikali zilitamani mali za mashirika yao, na maadui wa Kanisa waliwafanya shabaha ya kwanza, kwa kuwa kila mara ndio wanaohakikisha zaidi uimara wa ukatoliki chini ya Papa na dhidi ya utaifa (ambao wakati huo ulichochewa na serikali na kupendeza Maaskofu wengi). Ukweli wa dhati ni kwamba Mungu alitaka kutakasa watu aliowakusudia wawe moyo wa Kanisa.

Katika barua rasmi za miaka hiyo, Watumishi wakuu waliweka wazi matatizo yaliyokuwepo (utaifa, ugomvi, uchu wa vyeo, wivu, malezi ya kulipua, kujiingiza katika masuala ya siasa, utovu wa unyofu na unyenyekevu, utovu wa usafi na nidhamu) pamoja na utabiri wa dhoruba ijayo. Ugumu wa hali unaonekana pia katika miundo mikuu ya utawa kwenda kinyume cha kawaida: OFM toka 1791 karibu mfululizo iliongozwa na Watumishi wakuu Pekupeku na Mriformati badala ya Waoservanti (waliokuwa na msimamo laini); vilevile Wakapuchini toka 1754 hadi 1789 waliongozwa karibu mfululizo na wasio Waitalia (tofauti na wanashirika wenzao, watawa wa nchi hiyo walikuwa wakiridhika zaidi na hali ya shirika na kupinga urekebisho). Pia mikutano mikuu haikufanyika muda mrefu: katika OFM tangu 1768 hadi 1856; kwa Wakonventuali tangu 1789 hadi 1847. Iliwabidi Mapapa wateue Watumishi wakuu.

Utatuzi ulijaribu kuelekea pande mbili: urekebisho wa hiari (kwa watawa wenyewe kujituma, hasa kwa kuanzisha makao ya upwekeni) na wa lazima (kwa viongozi kuimarisha nidhamu). Upande wa urekebisho wa hiari, kwa Waoservanti makao ya upwekeni yalikuwepo rasmi na kuhitaji kuhuishwa tu; kumbe matawi mengine hayakuwanayo. Watumishi wakuu wa Wakapuchini walijitahidi kuyaanzisha Italia na Hispania (huko kwa jina la “vyuo vya kimisionari”, yaani vituo vya sala na malezi ambapo watawa wajiandae kuhubiri) lakini walipingwa sana hata na washauri wao waliodai eti, shirika linafuata kwa umoja katiba yake, hivyo kukubali urekebisho ni kukiri limelegea; tena eti, anayetaka ukamilifu anaweza kuupata popote pale shirikani, hakuna haja ya kujitafutia mazingira ya pekee. Zilipokosekana juhudi za kutoka rohoni ililibidi shirika, hasa katika ngazi ya kanda, lidai vitendo vya nje vilivyopangwa kikamilifu katika vitabu vya taratibu na desturi vilivyoandikwa hasa wakati huo. Hivyo uaminifu ulidhaniwa kuishia katika utekelezaji wa vipengele vingi hivyo, ambavyo tena viliachwa iwezekanavyo vishikwe na vijana na mabradha, huku wengine wakijitafutia fadhili ili kuviepa.

Serikali zilianza kuchukua hatua kali, zikidai haki ya kujihusisha na maisha yote ya Kanisa. Kisha kuwafukuza Wajesuiti kutoka nchi mbalimbali (1759-1768) zilimlazimisha Papa Klementi XIV (1769-1774) kulifuta kabisa shirika lao (1773) lililokuwa kizuio kikubwa kwa serikali kutawala Kanisa mahalia (Maaskofu walikuwa wakiridhika au kunyamaza badala ya kutetea mamlaka ya Papa juu ya majimbo yote duniani). Kuhusu mashirika mengine serikali (kuanzia Ufaransa, 1765) zilitumia mbinu ya kuanzisha “kamati ya urekebisho” chini ya Maaskofu, zikificha hivyo malengo halisi. Hizo kamati zilitunga sheria za kunyongea mashirika: kupunguza au kufunga konventi zote za sehemu fulani au za aina fulani, kukataza kuombaomba, kupandisha umri wa kuingia unovisi, kupanga idadi yao, na hasa kuzuia mahudhurio katika mikutano mikuu kwa kudai mikutano ya kitaifa tu, vilevile katiba ya kitaifa badala ya ile ya shirika lote, uongozi wa kitaifa usio chini ya ule wa shirika lote, kukataza kukata rufaa kwa Papa n.k. Tukiondoa Dola la Kipapa, nchi zote za Ulaya zilipanga kunyonga mashirika. Kwa miaka 13 Ndugu Wadogo wa Ufaransa walipungua 3,756; kwa miaka 9 Hispania walipungua 5,582; kwa miaka 28 Polandi watawa walipungua asilimia 67! Chini ya siasa hiyo mashirika yalielekea kwisha bila ya sifa.

Kumbe mapinduzi ya Kifaransa yalipoanza kutumia nguvu zaidi na kuamua kufuta mashirika yote (1790) watawa wengi walipata taji la kifodini. Kisha kutupwa nje ya konventi, walipaswa kuchagua kati ya kula kiapo haramu cha kutii serikali badala ya Papa, au kuhama nchi au kukatwa kichwa. Wengi walikubali kwa furaha mwaliko wa kuacha utawa na kupewa pensheni; lakini wengiwengi pia walikwenda kuishi kitawa hasa Amerika, au walitoa uhai wao ili kutetea haki za Kanisa: kati ya wafiadini hao Wafransisko ni zaidi ya 250. Jeshi la Ufaransa llilipovamia karibu Ulaya nzima, sheria za namna hiyo zilienezwa Ubelgiji (1796), Italia Kaskazini-Magharibi (1802), Ujerumani Magharibi (1803), Italia Kusini (1809), Hispania (1810). Hata nchi nyingine za Ulaya ya kati zilifuta mashirika au kuyabana zaidi. Katika kipindi hicho waliishi watakatifu Egidi Maria wa mt. Yosefu (+1812), Pekupeku ombaomba, na Yohane wa Triora, Mwoservanti aliyefia dini China (+1816), na Waoservanti 8 waliofia dini huko Syria (+1860): mapadri Manuel Ruiz, Karmelo Bolta, Engelbati Kolland, Nikanori Ascanio, Petro Nolasko Soler, Nikola Maria Alberca na mabradha Fransisko Pinazo na Yohane Yakobo Fernandez. Akaja kufuata Mkapuchini Fransisko Maria wa Camporosso (+1866), bradha ombaomba mwenye upendo mkuu. Pia kuna wenye heri 17.

Wafaransa waliposhindwa, mkutano wa amani wa Vienna (1815) uliamua kurudisha iwezekanavyo hali iliyokuwepo Ulaya kabla ya mapinduzi. Hata mashirika wakajaribu kufanya hivyo, lakini haikuwa rahisi. Mawazo ya mapinduzi yalikuwa yameenea, yakidai uhuru na maendeleo. Watawa waliozoea kwa miaka kadhaa kuishi mmojammoja ulimwenguni, walipolazimishwa na Kanisa kurudi konventini hawakukubali tena nidhamu ya nadhiri. Pia ilikuwa vigumu kwao kuishi pamoja kutokana na misimamo yao tofauti kuhusu mapinduzi. Wasiwasi kuhusu kesho ukaendelea pia kwa sababu serikali mpya zilikuwa na siasa ileile ya kabla ya mapinduzi, hivyo mashirika yakaanza tena kufutwa: Urusi, ukiwa na Polandi chini yake (1831 hadi 1864), Ureno (1832-1890), Hispania (1836-1880), Italia Kaskazini Magharibi (kuanzia 1855), Italia nzima (kuanzia 1866), Ujerumani (1871-1875), Ufaransa (1880 kwa muda mfupi, tena kuanzia 1903). Wakati huo makoloni ya Amerika ya Kilatini yalijipatia uhuru (1820-1824): watawa wananchi walisimama wote upande wa mapinduzi, kumbe wamisionari (hasa Wahispania) waliyapinga wakateswa hadi kuuawa. Baada ya ushindi jamhuri mpya pia zilianza kudhulumu mashirika hata karibu kuyakomesha (k.mf. Brazili konventi zote ziliagizwa kufungwa mwaka 1822, Mexico mashirika yote yalifutwa mwaka 1855). Hivyo kila yalipotaka kuinuka, mashirika yalikumbwa na matatizo mapya. Hatimaye yalijikuta mali zake zimepungua sana, na wanashirika vilevile, lakini waliobaki wametakaswa kiasi kikubwa.

Kwa jumla, si wengi sana waliofurahia hatua za serikali kuwaondoa utawani, ingawa katika nchi nyingi walipewa pensheni. Kati yao mapadri walifanya kazi ya kichungaji jimboni, na baadhi wakawa Maaskofu; mabradha walitoa huduma katika sakristia au hospitali, ila wengine walirudi kwa ndugu zao. Idara ya Papa kwa Watawa ilitoa miongozo kuhusu hali yao na uhusiano na shirika, ikiwahimiza daima waishi kijumuia kadiri iwezekanavyo. Ndizo juhudi za Watumishi wakuu pia, ingawa waliona ugumu wa kuzitekeleza. Mang’amuzi ya maisha ya nje, yasiyo na hakika kiuchumi, yaliwasaidia watawa kuelewa watu wa kawaida, ambao si wakulima hasa kama zamani, bali umati wa wafanyakazi wenye kudhulumiwa na ubepari katika nchi za viwanda. Wakiishi ulimwenguni hasa Ndugu Wadogo waliacha usomi wao na tabia nyingine za tabaka la juu walizokuwanazo, wakajenga uhusiano mpya na watu na kuwajibika kuwasaidia hata kijamii. Miaka ya kukaa nje ya konventi ndiyo miaka ambapo mashirika mengi ya huduma yalianzishwa na watawa hao.

Ukarabati (1869-1962)

[hariri | hariri chanzo]

Maisha ya kitawa yalipoanza kuruhusiwa tena, waliojitahidi kufufua mashirika yao hawakufikiria kutekeleza karama asili katika mazingira mapya, bali kukarabati tu kilichobaki cha karne iliyopita. Waliridhika kujiona wanashangiliwa bado na watu wema wengi, bila ya kujali jamii inavyozidi kusogea mbali na tunu zao. Hivyo katika malezi wakasisitiza mambo yaleyale ya zamani hasa katika nchi (k.mf. Italia) ambapo miaka ya utawa kuzuiwa haikuwa mingi. Ndugu Wadogo waliweza kupata kwa urahisi miito ya kibradha, ila si ya kipadri, kwa kuwa wengi hawakuwa na elimu au ilikuwa tofauti na ile iliyodaiwa na Kanisa. Tena, waliokuwa wamesoma waliona wazi mbele yao njia za kufanikiwa ulimwenguni, na hawakuweza kufuata mitindo ya malezi ya kitawa iliyokuwa ileile ya zamani, yenye kusawazisha mno watu wenye vipawa tofauti. Basi, miito ikatafutwa kati ya watoto wa familia bora za wakulima wasioweza kuwasomesha: kwao ilikuwa heshima kuwa na mtoto padri mtawa. Ndivyo zilivyoanza (1869) seminari za kiserafi ambazo, baada ya kupingwa na watawa wazee, zikaja kuenea haraka na kuhimizwa rasmi katika matawi yote. Hapo muundo mzima wa malezi ukaja kubadilika, kwa kupatikana madarasa ya vijana wa kuongozana kuanzia umri wa miaka 11-12 hadi upadri, wakipata malezi yote utawani na hivyo kufyonza desturi, misimamo, mitazamo na matarajio ya shirika. Hawakukosekana watawa maarufu waliopinga malezi ambayo pengine haikuwa na maana tena wala ukweli na unyofu wa Kifransisko, ikitaka kusawazisha wote katika mitindo ya nje, na kugeuza vijana kuwa wanasesere wanaotenda lolote kwa kuongozwa. Hata hivyo seminari hizo ndogo zikawa mbinu kuu kwa karibu miaka mia.

Jubilei ya miaka 700 tangu azaliwe Fransisko (1882) iliadhimishwa kwa unyonge, lakini Papa Leo XIII (1878-1903) alitoa hati iliyohimiza kufufua miundo ya Kifransisko, hasa Utawa III, dhidi ya ubinafsi unaotawala dunia. Miaka miwili baadaye Wakapuchini wakaadhimisha mkutano mkuu muhimu sana, uliochukua hatua mbalimbali na kumchagua Mtumishi mkuu bora aliyeongoza miaka 24 kwa mafanikio makubwa katika yote, k.mf. wanashirika wakiongezeka kutoka 7,896 hadi 10,083. Mwaka 1889 Wafransiskani pia, baada ya kuongozwa miaka 20 na Mriformati bora, wakafaulu kufanya mkutano mkuu uliotunga katiba kwa shirika lote, jambo lililokusudiwa bure tangu mwaka 1517; hata hivyo Wariformati walidai ruhusa ya kufuata pia sheria zao maalumu. Mwaka 1895 Leo XIII aliupendekezea mkutano mkuu muungano wa matawi OFM uwe agenda kuu, na Kardinali akaeleza namna ya kuyaunganisha. Waoservanti wote wakakubali, Warekoleti vilevile kwa sharti la kutunza ufukara kwa uangalifu, kumbe Wariformati na Pekupeku walio wengi wakakataa; jumla ya kura ikawa 77 ndiyo na 31 hapana. Basi kamati ikaandaa katiba mpya iliyothibitishwa mwaka 1897, halafu Leo XIII akatangaza rasmi muungano kamili wa matawi yote chini ya Mtumishi mkuu tu, ambao uonekane wazi hata kwa nje (kanzu ya mtindo mmoja badala ya ainaaina na rangi ya kahawia badala ya zile tofauti za awali: nyeusi, ya kijivu, ya zambarau na ya baharia). Akaagiza kanda zisizokubali wasiweze kupokea wanovisi tena, na watawa binafsi wasiokubali wapangiwe nyumba maalumu ambapo wakae wao tu, bila ya kuchanganyikana na walioungana. Hata hivyo muungano haukufanikiwa vizuri; Wahispania walikubali katiba lakini wakaendelea kujiongoza kitaifa hadi 1932; hasa majaribio ya kuunganisha katika kanda moja Wafransiskani wa matawi mbalimbali yalisababisha ushindani mwingi hadi juzijuzi. Hatimaye Wakonventuali pia walianza tena kufanya mikutano mikuu (1891); mwaka 1904 wakamchagua Mtumishi mkuu kutoka kanda ya Marekani, iliyoanzishwa 1872: hatua hiyo ilionyesha wazi mwelekeo mpya wa kimataifa.

Jubilei ya miaka 700 tangu shirika lianze (1909), iliadhimishwa kwa fahari zaidi, kutokana na hali ya kutumainisha ya matawi yote. Ila lilizuka suala la uhalisi wa shina na uongozi kuhusiana na Fransisko. Hapo Papa Pius X (1903-1914) akatamka kwamba, “Watumishi wakuu wa familia tatu za Kifransisko wako sawa kwa heshima na mamlaka walizonazo, nao watazamwe sawia kama makamu na waandamizi halisi wa Fransisko, kila mmoja katika familia yake... Mashirika matatu ya familia ya Ndugu Wadogo ni kama matawi matatu ya mti uleule, ambao mzizi na shina lake ni Fransisko, na viungo vyake ni Ndugu Wadogo kwa haki kamili na sawia”.

Vita vikuu vya kwanza (1914-1918) na Mkusanyo wa Sheria za Kanisa (1917) havikuleta mabadiliko makubwa utawani. Jubilei ya kifo cha mwanzilishi (1926) ilichochea Wafransisko wote; hali ilikuwa tofauti na karne iliyopita, kwa sababu ya kujitolea sana hata kijamii, jambo lililowafanya waheshimiwe upya na Waprotestanti na waasi wa dini pia. Hata hivyo katika nchi chache dhuluma zikawajia tena: kwanza Mexico (1926-1932), halafu Hispania (1936-1939), walipouawa Ndugu Wadogo 320 na Wafransisko wengine 88. Baadaye vikazuka vita vikuu vya pili (1939-1945) vilivyoharibu sana hasa Ulaya ya Kati na kanda zake.

Lakini mabaya zaidi yakafuata Ulaya Mashariki ukiwa chini ya Ukomunisti ambao, pamoja na kueneza mafundisho ya wakanadini na kupotosha maadili, pengine ulifuta mashirika yote, pengine uliyawekea vizuio vingi. Kumbe Magharibi tunu nyingi zikaja kufifia kadiri uchumi ulivyostawi na kuleta anasa. Watawa wote na Kanisa zima wakajiuliza upya kuhusu maana ya uwepo wao katika ulimwengu wa kisasa. Majibu yakawa tofauti, na vizazi vikabishana: katika hali hiyo Papa Yohane XXIII (1958-1963) aliitisha Mtaguso II wa Vatikani (1962-1965).

Padri kijana Pio wa Pietrelcina alipolazimishwa kupigwa picha ikionyesha madonda matakatifu ya Yesu mikononi.

Ingawa kesi za kutangazia watakatifu zinachukua kwa kawaida miaka mingi, baadhi ya ndugu wa kipindi hicho wameshafikia hatua hiyo. Kuna Wafransiskani wanane waliofia dini China (1900): Maaskofu Gregori Grassi, Francesco Fogolla na Antonino Fantosati, halafu mapadri Elia Facchini, Teodoriko Balat, Giuseppe Maria Gambero na Cesidio Giacomantonio, hatimaye bradha Andrea Bauer. Wakapuchini wako watatu: bradha Konrado wa Parzham (+1894), bawabu; halafu mapadri Leopoldo Mandich (+1942) na Pio wa Pietrelcina (+1968), mashujaa wa kitubio. Mkonventuali ni mmoja, Maksimiliani Maria Kolbe (+1941), shahidi wa upendo katika makambi ya maangamizi ya Wanazi. Wenye heri wako 50, wengi wao wakiwa wafiadini.

Changamoto ya Mtaguso II wa Vatikani (1962-2005)

[hariri | hariri chanzo]

Mtaguso huo ulisisitiza kweli za kudumu na kuelekeza namna ya kukabili kichungaji ulimwengu wa kisasa. Kwa ajili hiyo watawa pia walidaiwa kujirekebisha upya, hasa kiroho. Ndugu Wadogo, sawa na watawa wote, walipaswa kurekebisha katiba zao pia kwa kutoa wote maoni yao, kufanya mikutano mikuu na majaribio mbalimbali. Kazi hiyo ilichukua miaka mingi kuliko ilivyotarajiwa, kwa kufikiria upya vipengele vyote vya maisha ya Kifransisko. Kwa mara ya kwanza mabadiliko ya katiba yaliwekwa mikononi mwa wanashirika, kwa kujali wingi si ubora wao, basi, iliwezekana kufuta harakaharaka mambo yaliyowashinda wengi, bila ya kujali kama yanafaa bado au la. Halafu wasiwasi uliokuwepo kabla ya Mtaguso ulilipuka na kusababisha wengi wapotewe na dira hata katika imani na maadili. Matokeo yake wengi waliacha utawa na upadri. Wengine walibaki pasipo msimamo, kwa kuona mengi ya zamani yamebadilishwa na mapya ni ya muda (yamekubaliwa kwa majaribio). Ratiba ya sala ilipunguzwa sana, kama si kuachwa kabisa. Utafiti uliofanywa na uongozi wa Wakapuchini ulionyesha kwamba wanashirika walio wengi wasingeshauri kijana kujiunga nao. Ndiyo sababu, pamoja na miito kujitokeza kwa nadra Ulaya, idadi ya Ndugu Wadogo ikapungua haraka tangu mwaka 1963 (OFM) na 1964 (OFMCap); kumbe Wakonventuali walipungua haraka kati ya 1968 na 1975, halafu wakaanza kuongezeka polepole sana.

Wengine wasioridhika na mabadiliko hayo, baada ya kunyimwa na Watumishi wao uhuru waliotaka kwa kufuata maisha ya kijumuia ya Kifransisko zaidi, wakaamua kuanzisha matawi mapya. Wakapuchini kadhaa (wakifuatwa na Wafransiskani pia) wakaanzisha Ndugu Wadogo Wapya huko Italia (1972) na Ndugu Wadogo Wamisionari huko Brazili (1973). Akielewa nia yao njema katika hali ya fujo iliyotanda, Papa Paulo VI (1963-1978) aliwakubalia wabaki na nadhiri zao kuu baada ya kuacha shirika walipoziweka. Wakapuchini wengine wa Italia walianzisha Ndugu wa Mt. Fransisko (1983), na wa Marekani Wafransisko wa Upyaisho (1987). Hatimaye Wakonventuali kadhaa wa Italia na Filipino wakaanzisha Wafransisko wa Imakulata (1990) kwa ruhusa ya pekee ya Papa Yohane Paulo II (1978-2005) aliyewafanya mapema kuwa shirika la Kipapa. Huko na huko kuna makundi mengine madogo, na akina dada wanaoyafuata kwa kushika vilevile kanuni ya Utawa I. Juhudi za kuyaunganisha zimeshindikana kwa kuwa yana sura tofauti. Kwa jumla mashirika hayo hayakuongezeka sana. Hata hivyo uwepo wake umekuwa changamoto kwa matawi makubwa ambayo yakaanza kujirudi kidogo, baada ya kupungukiwa na wengi wasiokuwa na msimamo pamoja na kutambua matokeo ya majaribio yaliyofanywa; shida ni kwamba kujirekebisha baada ya kulegea sana si rahisi, hasa kama kazi hiyo inahusu idadi kubwa ya watu.

Polepole karama ya mwanzilishi na ya kila tawi ikaja kuzingatiwa tena kwa furaha, badala ya kujali masuala ya miundo tu. Mambo mengi yaliyosahauliwa kwa karne kadhaa yakaja kuonekana muhimu hasa leo, kama vile roho ya kanuni (udugu na udogo) kuliko mtazamo wa kisheria uliotawala matamko ya Mapapa wa zamani; au usawa wa watawa wote bila ya tabaka; au uwajibikaji wa kila mmoja katika uendeshaji wa jumuia, kanda na shirika; au umuhimu wa mikutano, kuanzia ngazi ya nyumba (ambapo ulikuwa umebaki kwa Wakonventuali tu). Wakati huohuo mabishano kati ya matawi yakapungua sana kwa njia ya ushirikiano wa kidugu mkubwa zaidi na zaidi katika ngazi zote. Hatimaye katiba zikaja kuthibitishwa na Kanisa kulingana na toleo la pili la Mkusanyo wa Sheria zake kwa Walatini (1983). Utulivu upande huo umeleta msimamo mkubwa zaidi kwa viongozi na kwa wanashirika jumla: kinadharia njia imeeleweka; sasa kazi ni kuifuata hadi mwisho.

Baada ya Ukomunisti kuanguka (1989) matawi yote yamejitahidi kujiimarisha Ulaya Mashariki walipopata tena nafasi ya kuhubiri na kupokea miito, ambayo huko ni mingi. Mungu anazidi kuongoza historia.

Utume (1762-2005)

[hariri | hariri chanzo]

Kati ya 1762 na 1889 dhuluma zilifyeka idadi ya Wafransisko kwa asilimia 82.1 na kufuta kabisa kanda nyingi (Ufaransa zote 32!) na kuziacha nyingine hoi. Hata hivyo, kanda chache zilistawi, kwa kuwa mawazo ya uhuru kwa wananchi yalikomesha dhuluma za kidini pale zilipokuwepo toka muda mrefu sana, hasa Irelandi na Uingereza. Kwa namna ya pekee mashirika yakaja kustawi Amerika Kaskazini walipohamia watawa wengi.

Baada ya dhuluma hizo kwisha, kadiri Ndugu Wadogo walivyorudi kupenya maisha halisi ya Kanisa na ya jamii, walielewa ni tofauti sana na yalivyokuwa kabla ya dhoruba. Iliwabidi kutumia ubunifu wa Kifransisko kuitikia mahitaji mapya ya watu kwa utendaji usiozimika, ingawa ukatokea mgongano kati ya taratibu za maisha ya kijumuia na madai ya utume huo.

Mahubiri yaliendelea kuwa njia kuu ya utume, sio tu katika wiki za uamsho, maandalizi ya sherehe na mafungo, bali pia kwa njia ya vyombo vya upashanaji habari: baada ya magazeti (la kwanza lilianzishwa na Wakapuchini wa Ufaransa mwaka 1861; kufikia mwaka 1919 yalikuwa 164 tayari, halafu yakazidi tena), Ndugu Wadogo walifanya kazi katika redio na televisheni au kuzimiliki wenyewe. Katika nusu ya kwanza ya karne XX utume wa maungamo ulishika nafasi kubwa hata kwa Wakapuchini, ambao toka mwanzo hadi mwaka 1847 walikuwa wakizuiwa na katiba wasifanye kazi hiyo.

Nusu ya pili ya karne XIX na nusu ya kwanza ya karne XX juhudi za Ndugu Wadogo zilizaa vyama vingi vya kitume. Kati ya vile vilivyoenea zaidi tukumbuke kile cha Mashujaa wa Imakulata (1917) cha Maximiliani Maria Kolbe, na kile cha Makundi ya Sala cha Pio wa Pietrelcina. Baadaye Ndugu Wadogo wengi wakaja kupendelea matapo mapya ya kiroho, yaliyoanzishwa na walei, wakajihusisha nayo kuliko walivyojihusisha na shirika lao, hata kusababisha swali: je, kwao ni muhimu zaidi kuwa wanashirika au kufuata tapo fulani?

Utume wa kijamii ulipata sura nyingi kulingana na mahitaji ya watu wadogo: huduma za huruma, mshikamano wa kutumia kiasi (katika kunywa), upatikanaji wa kazi na vitendeakazi, vyuo kwa mabubu-viziwi, benki, utume kwa wazururaji, kwa watu wa kuhamahama, na kwa wahamiaji wa nchi zilizoendelea, huduma hospitalini n.k.

Baada ya vita vikuu vya pili, na hasa mara baada ya Mtaguso, karama maalumu iliposahauliwa ili kujali zaidi upadri wa mtawa, mashirika yalikimbilia utume wa mapadri wanajimbo kwa kupokea parokia nyingi. Kumbe yalipokumbuka tena karama ya kitawa yakaona ugumu wa kupunguza utume wa aina hiyo (kurudisha parokia kwa jimbo lililopungukiwa mapadri). Hivyo, pamoja na uhaba wa miito yakajikuta yanalemewa yasiweze kutua mzigo waliojitwisha. Upande wa umisionari, katika karne XIX ukoloni wa Wazungu, waliokuja kutawala maeneo makubwa duniani kote, ulifungua njia na milango kwa uenezaji wa imani. Kanisa lilichangamkia tena kazi hiyo kuanzia Ufaransa, na kufanya mipango mingi ya ushirikiano na wamisionari, hata kuanzisha miundo ya kimataifa ambayo yakaja kuwekwa moja kwa moja chini ya Papa, na vilevile mashirika mbalimbali ya kimisionari tu. Ndugu Wadogo walipoanza kuinuka baada ya dhoruba wakakuta juhudi hizo zimeshaenea hata zikaja kufikia kilele chake kati ya vita vikuu. Basi matawi yote matatu yakajitosa katika kazi hiyo, tena kwa upana na mpango kuliko zamani. Kufikia mwaka 1934 Wafransiskani walishika nafasi ya kwanza kati ya mashirika yote kwa wingi wa wamisionari (3,600). Pigo kubwa lililowapata ni kufukuzwa wageni wote 550 waliokuwepo China katika majimbo 29 ya kwao (1949). Wakapuchini wamisionari waliokuwa 377 mwaka 1890, wakaongezeka hadi kuwa 1,562 mwaka 1975, wengi wao Afrika, India na Indonesia.

Hivyo kanda za Amerika ya Kilatini zikastawi (ndugu 1,600 wa mwaka 1905 wakawa 4,700 mwaka 1975); zikaanzishwa nyinginyingi Asia, na chache Afrika na Australia. Basi, kama inavyotokea kwa Kanisa lote, asilimia ya Wazungu shirikani inazidi kupungua, kumbe ndugu wa kontinenti nyingine wanaongezeka. Kwa mfano, kati ya Wakapuchini mwaka 1997 asilimia 15 walikuwa Amerika ya Kilatini, 14 Asia-Australia na 10 Afrika.

Takwimu ni kama ifuatavyo:

Mwaka 1762 hivi: (Waoservanti) 39,900; (Pekupeku) 7,000; (Wariformati) 19,000; (Warekoleti) 11,000 = OFM jumla 76,900; Wakonventuali 21,000; Wakapuchini 34,000 = Jumla kuu 131,900.

Mwaka 1889 hivi: (Waoservanti) 6,200; (Pekupeku) 900; (Wariformati) 5,700; (Warekoleti) 1,600 = OFM jumla 14,400; Wakonventuali 1,500; Wakapuchini 7,600 = Jumla kuu 23,500.

Mwaka 1964 hivi: OFM 27,100; Wakonventuali 4,800; Wakapuchini 11,229 = Jumla kuu 43,129.

Mwaka 2005: OFM 15,794; Wakonventuali 4,595; Wakapuchini 11,229; Wafransisko wa Imakulata 282 = Jumla kuu 31,900.

Upande wa elimu, kulingana na sheria za Kanisa, mipango ya masomo imebadilika, miaka ya falsafa na teolojia kwa ajili ya upadri imeongezeka, mbali ya seminari ndogo kuna vituo vingi wanaposoma pamoja watawa wa mashirika mbalimbali na pengine waseminari wa majimbo, kila tawi limeunda kituo kikuu cha malezi ya juu huko Roma, ambapo kuna vyuo vikuu vya Wakonventuali (Seraphicum) na OFM (Antonianum), na digrii kati ya wanashirika zimeenea.

  • The Poor and the Perfect: The Rise of Learning in the Franciscan Order, 1209–1310 by Neslihan Senocak. (Cornell University Press; 2012) 280 pages; shows how Franciscans shifted away from an early emphasis on poverty and humility and instead emphasized educational roles
  • A History of the Franciscan Order: From Its Origins to the Year 1517 by John Richard Humpidge Moorman, Franciscan Institute Publications, 1988. ISBN 978-0-8199-0921-3
  • Origins of the Franciscan Order by Cajetan Esser, Franciscan Institute Publications, 1970. ISBN 978-0-8199-0408-9
  • The Leonine Union of the Order of Friars Minor by Maurice Carmody, Franciscan Institute Publications, 1994. ISBN 978-1-57659-084-3
  • Friars Minor in China: 1294 – 1944, by Arnulf Camps and Pat McCloskey, Franciscan Institute Publications, 1996. ISBN 978-1-57659-002-7
  • In the Name of St. Francis: A History of the Friars Minor and Franciscanism until the Early Sixteenth Century, by Grado Giovanni Merlo, translated by Robert J. Karris and Raphael Bonanno, Franciscan Institute Publications, 2009. ISBN 978-1-57659-155-0
  • The History of Franciscan Theology, by Kenan Osborne, Franciscan Institute Publications, 1994. ISBN 978-1-57659-032-4
  • Friars Minor in Ireland from Their Arrival to 1400, by Francis Cotter, Franciscan Institute Publications, 1994. ISBN 978-1-57659-083-6
  • The Franciscan Spirituals and the Capuchin Reform, by Thaddeus MacVicar, Franciscan Institute Publications, 1986. ISBN 978-1-57659-086-7
  • Medieval Franciscan Houses, by John R. H. Moorman, Franciscan Institute Publications, 1983. ISBN 978-1-57659-079-9
  • A Poor Man's Legacy: An Anthology of Franciscan Poverty, by Cyprian Lynch, Franciscan Institute Publications, 1989. ISBN 978-1-57659-069-0
  • The Franciscan Concept of Mission in the High Middle Ages, by E. Randolph Daniel, Franciscan Institute Publications, 1992. ISBN 0-8131-1315-6
  • Peace and Good in America, A History of the Holy Name Province, Order of the Friars Minor, 1850s to the Present, by Joseph M. White, Franciscan Institute Publications, 2004. ISBN 978-1-57659-196-3
  • The Birth of a Movement, by David Flood and Thaddee Matura, Franciscan Institute Publications, 1975. ISBN 978-0-8199-0567-3
  • A History of the Franciscan Order: From Its Origins to the Year 1517 by John R. H. Moorman, Oxford University Press, Oxford, (1968) ISBN 0-19-826425-9; reprint: Franciscan Herald Press, Chicago, IL (1988) ISBN 0-8199-0921-1
  • Franciscan Philosophy at Oxford in the Thirteenth Century by D.E. Sharp, Oxford University Press, London (1930); (a more recent ed.: ISBN 0-576-99216-X)
  • Medieval Monasticism: Forms of Religious Life in Western Europe in the Middle Ages (3rd Edition) by C.H. Lawrence, ISBN 0-582-40427-4
  • The Spiritual Franciscans: From Protest to Persecution in the Century After Saint Francis by David Burr. ISBN 0-271-02128-4
  • Francis and Clare: The Complete Works By Ignatius C. Brady, Regis J. Armstrong, Paulist Press, Mahwah, New Jersey, (1982) ISBN 0-8091-2446-7
  • The Fraternal Economy: A Pastoral Psychology of Franciscan Economics By David B. Couturier, Cloverdale Books, South Bend (2007) ISBN 978-1-929569-23-6
  • Francis of Assisi: Early Documents 3 Volumes. Edited by Regis J. Armstrong, OFM Cap., J.A. Wayne Hellmann, OFM Conv., and William J. Short, OFM. New York: New City Press. Copyright 1999, Franciscan Institute of Saint Bonaventure University, Saint Bonaventure, NY. ISBN 978-1-56548-110-7.
  • "The Franciscan Story" by Maurice Carmody, Athena Press Publishing Co. UK (2008). ISBN 1-84748-141-8 ; ISBN 978-1-84748-141-2
  • "Santo António de Lisboa - Da Ciência da Escritura ao Livro da Natureza", Maria Cândida Monteiro Pacheco, Imprensa Nacional casa da Moeda,Lisboa, (1997), ISBN 972-27-0855-4
  • "O Simbolismo da Natureza em Santo António de Lisboa", José Acácio Aguiar e Castro,Universidade Católica Portugesa- Fundação Engº António de Almeida, Porto, 1997, ISBN UCP 972-9290.13-X /FEAA 972-8386-03-6

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Orodha ya Watakatifu Wafransisko

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:

Tovuti rasmi

[hariri | hariri chanzo]

Utawa wa Kwanza

[hariri | hariri chanzo]

Utawa wa Tatu

[hariri | hariri chanzo]

Wafransisko wa Kilutheri

[hariri | hariri chanzo]

Wafransisko wa Anglikana

[hariri | hariri chanzo]

Wafransisko wasio na madhehebu

[hariri | hariri chanzo]

Marejeo ya kitaalamu zaidi

[hariri | hariri chanzo]