Aimoni wa Faversham
Aimoni wa Faversham alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na mkuu wa utawa wa Ndugu Wadogo (1240-1244), kutoka Uingereza.
Alipojiunga na shirika hilo mwaka 1225 alikuwa tayari padri (mwanajimbo) na mwalimu wa teolojia huko Paris (Ufaransa), .
Kisha kufundisha tena katika vyuo mbalimbali, alifanywa balozi wa Papa kwa kaisari wa Dola la mashariki Yohane III wa Nisea mwaka 1233.
Aliongoza upinzani dhidi ya Elia Bombarone na baada ya kifo cha Alberto wa Pisa akachaguliwa kuwa mkuu wa shirika lote.
Ndiye aliyelipatia sura ya kudumu kufuatana na mfano wa Wadominiko upande wa muundo, utume, masomo na liturujia. Taratibu za maisha zikazidi kufuata mitindo ya kimonaki, pamoja na watawa kujitafutia visingizio vya kisheria wasibanwe nazo.
Chini yake makao ya kifukara ya upwekeni yalizidi kuachwa ili wanashirika wahamie nyumba kubwa za mijini, zenye makanisa makubwa ambamo wafanye utume, wakiwanyang’anya maparoko waamini na sadaka zao.
Alikubaliwa na Papa Gregori IX kwamba Watumishi wa kanda pia waweze kuruhusu ndugu wakahubiri. Kama alivyofanya mwenyewe huko Paris, Ndugu Wadogo wakazidi kushika nafasi kwenye vyuo vikuu na vinginevyo, na kuwa na uzito mkubwa ndani ya Kanisa, jambo lililowasogeza mbali na udogo uliowapasa.
Badala ya ndugu wote kuwa sawa, mabradha wakanyimwa kabisa nafasi za uongozi na kukubaliwa tu kutoa huduma ndogondogo za nyumbani (bustani n.k.), wakiwaachia raia huduma duni zaidi.
Kazi za mikono nje ya konventi zilikatazwa; badala yake ile ya kuombaomba ikaja kusifiwa na kushika nafasi ya kwanza upande wa uchumi. Zilipangwa pia njia za hakika za kupata mahitaji, hasa kwa nyumba za masomo.
Akiwa mku wa shirika alitoa ufafanuzi wa kanuni ('Expositio regulae) wa walimu wa Paris na breviari ya Wafransisko.
Alipokufa, mvutano ndani ya shirika ulijitokeza kwa nguvu.