Utawa wa Tatu
Utawa wa Tatu ni muundo wa Wakristo wa madhehebu mbalimbali wanaotaka kuishi kitawa bila ya kujiunga moja kwa moja na shirika fulani, lakini wakifuata karama yake, kama unavyoeleza kwa Wakatoliki Mkusanyo wa Sheria za Kanisa la Kilatini, kanuni 303.
Utawa mkubwa zaidi ni ule wa Wafransisko, ambao unaitwa Utawa wa Tatu wa Mt. Fransisko na kugawanyika kati ya wale wanaoishi katika mazingira ya kawaida (Wasekulari) na wale walioanzisha mashirika yenye nadhiri (Waregulari).
Historia
[hariri | hariri chanzo]Tangu mwanzo Kanisa liliona kufanya dhambi na toba si jambo la binafsi tu, bali linaathiri wengine pia. Ndiyo sababu liliwadai waamini malipizi ili kuwapa msamaha wa Mungu, na waliopaswa kuyafanya waliandikishwa katika orodha rasmi ya Watubu (Ordo Poenitentium). Kitubio cha siri kiliposhika nafasi ya utaratibu huo, wengi walijiamulia kufanya malipizi ya hadhara hata kwa dhambi za wengine wakajulikana kama Watubu. Toba ni neno la msingi katika historia ya Kanisa. Maana yake asili ni kujitoa kabisa kwa Mungu na kuishi kadiri ya Injili, lakini Wakristo wa karne za kati waliona inadai sana huzuni na fidia kwa dhambi za binafsi na za ulimwengu. Mtubu, akiwa peke yake au pamoja na wengine, alitarajiwa kuacha kazi zilizotazamwa ni kinyume cha Injili (k.mf. biashara na uaskari), kujitenga na jamii ili kufungamana zaidi na Mungu kwa maisha ya sala na tafakuri, kuhiji, kufunga, kujinyima, kutoa sadaka na kujitesa kwa wokovu wake na wa wote. Wengi kati yao walikuwa wanawake, hasa wa koo bora, kama mama wa Klara wa Asizi.
Tapo la toba liliwahusu walei, ambao baadhi yao wakawa baadaye watawa na hata makleri, tunavyoona kati ya Wahumiliati waliostawi kidogo tu kabla ya Fransisko wa Asizi. Wakati huo walei walihesabiwa kama ngazi ya chini (ya tatu) baada ya makleri na watawa. Uenezi wa Watubu ukasababisha wapewe na sheria hadhi ya pekee, kwa kuwahesabu kama kundi maalumu kati ya walei na watawa, na kuwapa haki na fadhili kadhaa za watawa. Watubu walikuwa walei, lakini wa pekee kutokana na azimio lao (propositum) lililowadai zaidi katika mengi. Kwanza walikuwa wanashika usafi kamili, lakini kuanzia karne XII baadhi yao wenye ndoa waliahidi tu kujinyima ndoa ya pili (wakifiwa) na hata tendo la ndoa siku za kufunga chakula na za kupokea sakramenti.
Mambo ya namna hiyo yanasomwa katika maisha ya Fransisko, kwa jinsi alivyoathiriwa na roho hiyo. Ndiyo sababu alipozungumzia maisha yake mapya alitumia neno “toba”, na jina asili la kundi lake lilikuwa “Watubu wa Asizi”. Baadaye ukubwa wa karama yake ulimfanya ajitokeze kama kiongozi wa tapo hilo, kwa kuwa namna yake ya kuelewa Injili iliathiri Watubu wengi walioanza kumfuata. Thoma wa Celano aliandika (1229) kwamba, “kwa uvuvio wa Mungu, watu wengi, maarufu kwa wadogo, makleri kwa walei, walimkaribia mtakatifu Fransisko wakijitolea kuishi chini ya uongozi wake na ualimu wake. Hao wote aliwashirikisha maji tele ya neema za mbinguni ambayo yalibubujika toka rohoni mwake na kustawisha maua ya maadili katika shamba la mioyo yao. Wanaume kwa wanawake walifuata mifano yake, kanuni yake na mafundisho yake; hivyo tunapaswa kumtangaza kwa haki mtendaji asiye na kifani wa hali mpya ya Kanisa na wa ushindi wa majeshi matatu ya wateule. Aliwapa wote mwongozo wa maisha na kadiri ya hali ya kila mmoja alielekeza kwa unyofu njia ya wokovu”. Hayo yalianza kutokea muda mfupi baada ya kukubaliwa na Papa Inosenti III (1198-1216), alipohubiri huko na huko (1211).
Kesi ya pekee ni ile ya kijiji cha Greccio, aliposhangaa kuona kilivyojaa Watubu wengi kuliko wale wa miji mikubwa. “Mara nyingi, ndugu walipoimba Masifu ya Jioni, kama walivyofanya sehemu nyingine nyingi, watu wa kijiji hicho, wakubwa kwa wadogo, walitoka nje ya nyumba zao na kusimama barabarani na kuwaitikia ndugu kwa sauti kubwa, Asifiwe Bwana Mungu wetu!” (Simulizi la Perugia). Tangu zamani baadhi ya walei walikusanyika kuishi kando ya monasteri ili kufaidika nazo kiroho na kiuchumi. Baadhi yao waliweza kujifunga kwa namna mbalimbali waishi kwa useja, au kwa uadilifu, au kwa utiifu au kwa kufuata kanuni maalumu. Ikawa vilevile kwa Wakanoni, aina mpya za watawa. Mageuzi ya jamii yalipozidi kuvuta watu mijini ili wafanye kazi tofauti na kilimo, walei wengi waliona Mashirika ya Ombaomba yanalingana zaidi na mahitaji yao ya kiroho, wakayafuata kama Watubu. Bila ya kuacha kazi zao mpya wala ndoa wakaanza kuvaa nguo ya kitawa ya shirika husika (walau joho), nyeusi kwa Wadominiko, ya kijivu kwa Wafransisko. Hata kabla Fransisko hajafa, walikuwepo Watubu, hasa wanawake, walioamua kuishi pamoja ili kushika vizuri zaidi azimio lao; k.mf. mwaka 1213 kulikuwa na jumuia ya kike huko Padua.
Fransisko, akiwajibika kwa watu hao, aliwaandikia aina ya kanuni katika Barua kwa Waamini (1215), alimojumlisha mahubiri yake kwa waliotamani kushika toba nyumbani kwao. Katika toleo la pili la barua hiyo (1221) akaongeza mawaidha na miongozo akitanguliza dibaji iliyo nzito kiteolojia na kiroho.
Chini ya Inosenti III, na zaidi chini ya Papa Honori III (1216-1227), hasa kwa juhudi za Kardinali Ugolino, Kanisa lilikusudia kulipa tapo la toba umoja na muundo fulani, pamoja na kulikinga dhidi ya uzushi. Hivyo lilitunga kanuni maalumu (1221) kwa kuchota mengi katika Azimio la Wahumiliati lililokubaliwa mwaka 1201. Kanuni hiyo mpya iliitwa Kumbukumbu ya Azimio (Memoriale Propositi) ikarekebishwa 1228. Hiyo ni sheria hasa yenye namba 39. Ya kwanza inahusu uduni wa mavazi; halafu kuna katazo la kuhudhuria karamu, tamasha na michezo; agizo la kufunga chakula mara moja au mbili kwa wiki; la kusali Masifu kama makleri au Baba Yetu kadhaa; la kupokea ekaristi kwenye Noeli, Pasaka na Pentekoste; la kulipa zaka; la kutotumia silaha na kutokula kiapo kwa kawaida; la kufanya familia nzima iishi Kikristo; la kukutana mara moja kwa mwezi kwa Misa, mafundisho na mchango kwa ndugu na wengineo wenye shida; la mtumishi kutembelea ndugu wagonjwa kila wiki; la kushiriki mazishi ya ndugu na kuwaombea; la kuandika wasia mapema ili kuzuia ugomvi; la kupatana kidugu; la kuungama kila mwezi. Kati ya masharti ya kumpokea ndugu mpya, lipo la kutokuwa na madeni, uadui na uzushi; pia mwanamke awe na ruhusa ya mume. Baada ya mwaka wa jaribio, anayefaa aweke ahadi kwa maisha yote asiweze kuacha jamaa tena isipokuwa kwa kuingia shirikani. Pia kuna taratibu za kusamehe na za kufukuza ndugu. Hatimaye kuna maelezo ya kuwa kuvunja kanuni si dhambi, ingawa kunastahili adhabu. Kwa jumla hakuna mambo ya pekee ya Kifransisko.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Catholic Encyclopedia: Third Orders & Tertiaries
- National Fraternity of the Secular Franciscan Order in the U.S.A.
- Third Order of St. Dominic Archived 11 Februari 2011 at the Wayback Machine.
- Third Order Secular of the Most Holy Trinity Archived 27 Julai 2011 at the Wayback Machine.
- Secular Order of the Servants of Mary Archived 15 Novemba 2010 at the Wayback Machine. (Secular Servites)
- international Augustinian Order's website Archived 26 Septemba 2011 at the Wayback Machine.
- site of Secular Augustinians in Canada Archived 29 Mei 2011 at the Wayback Machine.
- Secular Augustinian Recollects Archived 19 Julai 2011 at the Wayback Machine.
- Secular Trinitarian Way -Third Order of the Holy Trinity Archived 5 Juni 2010 at the Wayback Machine.