Watubu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Watubu ni waamini hususan wa dini ya Ukristo walioshika rasmi maisha ya toba.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Mt. Corrado Confalonieri, mtubu maarufu, alivyochorwa na Giovanni Lanfranco mwaka 1618.

Tangu mwanzo Kanisa liliona kufanya dhambi na toba si jambo la binafsi tu, bali linaathiri wengine pia. Ndiyo sababu liliwadai waamini malipizi ili kuwapa msamaha wa Mungu, na waliopaswa kuyafanya waliandikishwa katika orodha rasmi ya Watubu (Ordo Poenitentium).

Kitubio cha siri kiliposhika nafasi ya utaratibu huo, wengi walijiamulia kufanya malipizi ya hadhara hata kwa dhambi za wengine wakajulikana kama Watubu.

Toba ni neno la msingi katika historia ya Kanisa. Maana yake asili ni kujitoa kabisa kwa Mungu na kuishi kadiri ya Injili, lakini Wakristo wa karne za kati waliona inadai sana huzuni na fidia kwa dhambi za binafsi na za ulimwengu. Mtubu, akiwa peke yake au pamoja na wengine, alitarajiwa kuacha kazi zilizotazamwa ni kinyume cha Injili (k.mf. biashara na uaskari), kujitenga na jamii ili kufungamana zaidi na Mungu kwa maisha ya sala na tafakuri, kuhiji, kufunga, kujinyima, kutoa sadaka na kujitesa kwa wokovu wake na wa wote. Wengi kati yao walikuwa wanawake, hasa wa koo bora, kama mama wa Klara wa Asizi.

Tapo la toba liliwahusu walei, ambao baadhi yao wakawa baadaye watawa na hata makleri, tunavyoona kati ya Wahumiliati waliostawi mwishoni mwa karne XII. Wakati huo walei walihesabiwa kama ngazi ya chini (ya tatu) baada ya makleri na watawa. Uenezi wa Watubu ukasababisha wapewe na sheria hadhi ya pekee, kwa kuwahesabu kama kundi maalumu kati ya walei na watawa, na kuwapa haki na fadhili kadhaa za watawa. Watubu walikuwa walei, lakini wa pekee kutokana na azimio lao (propositum) lililowadai zaidi katika mengi. Kwanza walikuwa wanashika usafi kamili, lakini kuanzia karne ya XII baadhi yao wenye ndoa waliahidi tu kujinyima ndoa ya pili (wakifiwa) na hata tendo la ndoa siku za kufunga chakula na za kupokea sakramenti.

Mambo ya namna hiyo yanasomwa katika maisha ya Fransisko wa Asizi, kwa jinsi alivyoathiriwa na roho hiyo. Ndiyo sababu alipozungumzia maisha yake mapya alitumia neno “toba”, na jina asili la kundi lake lilikuwa “Watubu wa Asizi”. Baadaye ukubwa wa karama yake ulimfanya ajitokeze kama kiongozi wa tapo hilo, kwa kuwa namna yake ya kuelewa Injili iliathiri Watubu wengi walioanza kumfuata. Thoma wa Celano aliandika (1229) kwamba, “kwa uvuvio wa Mungu, watu wengi, maarufu kwa wadogo, makleri kwa walei, walimkaribia mtakatifu Fransisko wakijitolea kuishi chini ya uongozi wake na ualimu wake. Hao wote aliwashirikisha maji tele ya neema za mbinguni ambayo yalibubujika toka rohoni mwake na kustawisha maua ya maadili katika shamba la mioyo yao. Wanaume kwa wanawake walifuata mifano yake, kanuni yake na mafundisho yake; hivyo tunapaswa kumtangaza kwa haki mtendaji asiye na kifani wa hali mpya ya Kanisa na wa ushindi wa majeshi matatu ya wateule. Aliwapa wote mwongozo wa maisha na kadiri ya hali ya kila mmoja alielekeza kwa unyofu njia ya wokovu”. Hayo yalianza kutokea muda mfupi baada ya kukubaliwa na Papa Inosenti III, alipohubiri huko na huko (1211).

Kesi ya pekee ni ile ya kijiji cha Greccio, aliposhangaa kuona kilivyojaa Watubu wengi kuliko wale wa miji mikubwa. “Mara nyingi, ndugu walipoimba Masifu ya Jioni, kama walivyofanya sehemu nyingine nyingi, watu wa kijiji hicho, wakubwa kwa wadogo, walitoka nje ya nyumba zao na kusimama barabarani na kuwaitikia ndugu kwa sauti kubwa, Asifiwe Bwana Mungu wetu!” (Simulizi la Perugia).

Tangu zamani baadhi ya walei walikusanyika kuishi kando ya monasteri ili kufaidika nazo kiroho na kiuchumi. Baadhi yao waliweza kujifunga kwa namna mbalimbali waishi kwa useja, au kwa uadilifu, au kwa utiifu au kwa kufuata kanuni maalumu. Ikawa vilevile kwa Wakanoni, aina mpya za watawa.

Mageuzi ya jamii yalipozidi kuvuta watu mijini ili wafanye kazi tofauti na kilimo, walei wengi waliona mashirika ya Ombaomba yanalingana zaidi na mahitaji yao ya kiroho, wakayafuata kama Watubu. Bila ya kuacha kazi zao mpya wala ndoa wakaanza kuvaa nguo ya kitawa ya shirika husika (walau joho), nyeusi kwa Wadominiko, ya kijivu kwa Wafransisko. Hata kabla Fransisko hajafa, walikuwepo Watubu, hasa wanawake, walioamua kuishi pamoja ili kushika vizuri zaidi azimio lao; k.mf. mwaka 1213 kulikuwa na jumuia ya kike huko Padua.

Fransisko, akiwajibika kwa watu hao, aliwaandikia aina ya kanuni katika Barua kwa Waamini (1215), alimojumlisha mahubiri yake kwa waliotamani kushika toba nyumbani kwao. Katika toleo la pili la barua hiyo (1221) akaongeza mawaidha na miongozo akitanguliza dibaji iliyo nzito kiteolojia na kiroho.

Chini ya Papa Inosenti III, na zaidi chini ya Papa Honori III, hasa kwa juhudi za Kardinali Ugolino, Kanisa lilikusudia kulipa tapo la toba umoja na muundo fulani, pamoja na kulikinga dhidi ya uzushi. Hivyo lilitunga kanuni maalumu (1221) kwa kuchota mengi katika Azimio la Wahumiliati lililokubaliwa mwaka 1201. Kanuni hiyo mpya iliitwa Kumbukumbu ya Azimio (Memoriale Propositi) ikarekebishwa 1228. Hiyo ni sheria hasa yenye namba 39. Ya kwanza inahusu uduni wa mavazi; halafu kuna katazo la kuhudhuria karamu, tamasha na michezo; agizo la kufunga chakula mara moja au mbili kwa wiki; la kusali Masifu kama makleri au Baba Yetu kadhaa; la kupokea ekaristi Noeli, Pasaka na Pentekoste; la kulipa zaka; la kutotumia silaha na kutokula kiapo kwa kawaida; la kufanya familia nzima iishi Kikristo; la kukutana mara moja kwa mwezi kwa Misa, mafundisho na mchango kwa ndugu na wengineo wenye shida; la mtumishi kutembelea ndugu wagonjwa kila wiki; la kushiriki mazishi ya ndugu na kuwaombea; la kuandika wasia mapema ili kuzuia ugomvi; la kupatana kidugu; la kuungama kila mwezi. Kati ya masharti ya kumpokea ndugu mpya, lipo la kutokuwa na madeni, uadui na uzushi; pia mwanamke awe na ruhusa ya mume. Baada ya mwaka wa jaribio, anayefaa aweke ahadi kwa maisha yote asiweze kuacha jamaa tena isipokuwa kwa kuingia shirikani. Pia kuna taratibu za kusamehe na za kufukuza ndugu. Hatimaye kuna maelezo ya kuwa kuvunja kanuni si dhambi, ingawa kunastahili adhabu. Kwa jumla hakuna mambo ya pekee ya Kifransisko.

Ugolino, kisha kuchaguliwa awe Papa Gregori IX, aliwaandikia Maaskofu wa Italia (1227) juu ya aina mbili za Watubu: wale wa kawaida walioishi nyumbani kwao, na wale walioishi upwekeni kwa mfano wa watawa halisi: ndio msingi wa tofauti iliyoratibiwa baadaye. Mwenyewe aliandika pia (1238) kwamba Fransisko alianzisha aina tatu za utawa: “ule wa Ndugu Wadogo, ule wa Akina Dada wa Ugo na ule wa Watubu”.

Papa Nikolasi IV, Mfransisko, alitoa (1289) kanuni mpya kwa Watubu wote, wa kiume na wa kike, wa wakati huo na wa wakati ujao, akiwaweka chini ya Ndugu Wadogo kama “wakaguzi na washauri” wao, kwa kumuona Fransisko kama “mwanzilishi wa Utawa wa Toba” (tamko ambalo si sahihi kihistoria). Kanuni hiyo haikubadili sana sheria za Memoriale, ila ilizipanga vizuri zaidi kulingana na zile za kitawa. Ina sura 20 zenye jumla ya namba 60, ambamo 1-13 zinahusu mapokezi na ustawi; 14-42 namna ya kuishi; 42-60 maisha ya kidugu na uongozi.

Kanuni hiyo iliweza kuchangia ustawi wa Watubu, lakini ilipingwa mapema na mashirika mengine yenye watu wa namna hiyo (k.mf. mwaka 1285 Wadominiko walikuwa wameamua kushughulikia Watubu waliofuata karama yao, hivyo wakaendelea mpaka walipokubaliwa kanuni maalumu mwaka 1405, baada ya mfumo wao kumzaa Katerina wa Siena). Shida nyingine iliyojitokeza ni kwamba kanuni ya Nikola IV haikuzungumzia walioishi kijumuia: hiyo ilizidi kuwaletea matatizo mpaka walipopewa kanuni tofauti (1521).

Christianity Symbol.png Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Watubu kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.