Benedikto Mwafrika

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kioo cha kanisa la Porto Alegre, Brazil, kinachomuonyesha Benedikto akimpakata Mtoto Yesu katika njozi.

Benedikto Mwafrika (San Fratello, wilaya ya Messina, mkoa wa Sisilia, Italia, takriban 1524 - Palermo, 4 Aprili 1589) alikuwa bradha Mfransisko maarufu kwa unyenyekevu na imani katika maongozi ya Mungu.

Kutokana na sifa yake, mwaka 1652 aliteuliwa na Bunge la Palermo kuwa mmojawapo kati ya wasimamizi wa jiji hilo. Tarehe 15 Mei mwaka 1743 Papa Benedikto XIV alimtangaza mwenye heri, halafu Papa Pius VII alimtangaza mtakatifu tarehe 24 Mei 1807, akiwa Mnegro wa kwanza kutangazwa na Kanisa Katoliki kuwa hivyo.

Anaheshimiwa kama msimamizi wa Waafrika, hasa Amerika Kusini.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Benedikto Manasseri alizaliwa na Kristoforo na Diana, watumwa walioletwa Sicilia kutoka Afrika (labda Ethiopia). Kwa kibali cha bwana wao Manasseri, mtoto huyo wa kwanza alizaliwa huru, tofauti na mdogo wake Marko na mabinti wawili waliofuata, Baldassara na Fradella.

Tangu utotoni alijitokeza kwa hamu ya kukaa upwekeni na kufanya malipizi hata wakaanza kumuita mtakatifu, ingawa wenzake walimdhulumu kwa hilo.

Alipofikia umri wa miaka 18 aliacha familia yake akaanza kujitegemea na kusaidia fukara.

Alipofikia umri wa miaka 21 alijiunga na wakaapweke wa Mtakatifu Dominiko, karibu na kijiji alichozaliwa, lakini baada ya muda si mrefu ilimbidi ahame (pamoja na mwanzilishi wao, Girolamo Lanza) kutokana na wingi wa watu waliomkimbilia ili awaombee miujiza.

Hapa walipohamia Platanella, halafu Mancusa, waamini waliendelea kumtafuta. Hivyo wakafichama juu ya mlima Pellegrino, karibu na Palermo. Kwa miezi 20 alikwenda kukaa patakatifu pa Bikira Maria wa Dayna, karibu na Marineo, halafu akarudi mlimani.

Girolamo Lanza alipofariki, Benedikto alichaguliwa na wananajumia kuwa mkubwa wao ingawa hakuwa na elimu yoyote.

Mwaka 1562 Papa Pius IV alifuta jumuia hiyo akadai watawa wake wajiunge na konventi nyingine. Benedikto alihamia kwa Wafransisko Ndugu Wadogo Wareformati kwenye ile ya Mtakatifu Anna huko Giuliana, alipobaki miaka 4, halafu kwenye ile ya Bikira Maria wa Yesu huko Palermo alipobaki hadi kufa.

Kwanza alifanya kazi kama mpishi, halafu akachaguliwa kuwa mkubwa wa konventi (1578), na baadaye tena akasaidia malezi ya wanovisi kabla hajarudia kazi ya upishi.

Miujiza aliyowapatia watu ilimvutia heshima ya matabaka yote, hata viongozi wa Kanisa na naibu wa mfalme walikuwa wakimuomba shauri kwa maamuzi muhimu.

Mwezi Februari mwaka 1589 alipatwa na ugonjwa uliosababisha kifo chake tarehe 4 Aprili.

Masalia yake yanatunzwa na kuheshimiwa katika kanisa la konventi alipofariki.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Attwater, Donald and Catherine Rachel John. The Penguin Dictionary of Saints. 3rd edition. New York: Penguin Books, 1993. ISBN 0-140-51312-4.

St Benedict the Moor Church in Dayton, Oh, On 2 Februari 2003, the parish community of St. James/Resurrection broke ground on eleven acres of property at the corner of Liscum Drive and McLin Parkway (State Route 35). Under the tenacious leadership of Father Francis Tandoh, C.S.Sp., a Holy Ghost priest from Ghana, St. Benedict the Moor will celebrate the “homecoming” of a faith journey that started many years ago on 14 Mei 2005.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.