Nenda kwa yaliyomo

Vasco da Gama

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Vasko Da Gama)
Vasco da Gama

Vasco da Gama (1460 au 1469- 24 Desemba 1524) alikuwa baharia na mpelelezi kutoka Ureno.

Alikuwa Mzungu wa kwanza aliyefika Uhindi kwa kuzunguka Rasi ya Tumaini Jema kusini mwa Afrika.

Upande wa dini, alikuwa Mkristo wa Kanisa Katoliki, tena mwanachama wa Utawa wa Tatu wa Mt. Fransisko.

Utangulizi

Vasco alikamilisha mradi uliofuatwa nchini Ureno tangu siku za mfalme Henrique baharia baada ya mwaka 1400. Henrique alianza kutuma jahazi zilizopeleleza pwani ya Afrika na kuelekea kusini zaidi na zaidi.

Vasco alitanguliwa na mpelelezi Mreno Bartolomeo Dias aliyewahi kuzunguka Rasi ya Tumaini Njema hadi mto wa samaki mwaka 1488 akitambua ya kwamba njia ya kuendelea mpaka Uhindi ilikuwa wazi mbele yake. Diaz alirudi wakati ule kwa sababu mabaharia wake walikuwa wagonjwa, hivyo hawakuwa tayari kuendelea tena.

Safari ya Vasco da Gama

Safari ya kwanza ya Uhindi

Da Gama aliondoka kwa amri ya mfalme wa Ureno tarehe 8 Julai 1497 kwa jahazi nne na watu 170. Wakati wa Krismasi walikuwa wakizunguka rasi hiyo tayari na kupita kwenye pwani ya mashariki ya Afrika Kusini wakaiita pwani hii "Natal" kutokana na sikukuu ya Krismasi.

Bandari za Afrika ya Mashariki

Mwezi wa Januari walifika Kisiwa cha Msumbiji (kwa Kireno: Ilha de Moçambique) walipokutana mara ya kwanza na Waislamu waliosema lugha ya Kiarabu. Wakaelekea Kenya wakafika kwanza Mombasa wasipopokewa vema wakaendelea hadi Malindi. Huko walijenga uhusiano mwema na sultani wa mji wakaona Wahindi wa kwanza.

Kufika Uhindi

Walifaulu kumuajiri nahodha aliyewaongoza kuvukia Bahari Hindi hadi kufika Calicut, Uhindi, tarehe 20 Mei 1498. Wareno walipeleleza pwani na kununua bidhaa mbalimbali.

Kurudi Ureno

Tarehe 29 Agosti 1498 da Gama aliondoka tena lakini aliacha Wareno wachache nyuma kwa amri ya kuanzisha kituo cha biashara.

Safari ya kurudi ilikuwa ngumu ikachukua muda mrefu kutokana na mwelekeo wa upepo. Nusu ya watu wake walikufa baharini kabla hawajafika Malindi. Jahazi mbili zilifaulu kurudi hadi Ureno zilipofika mnamo Julai na Agosti 1499.

Safari ya pili na ya tatu

Mfalme wa Ureno alituma wapelelezi na maafisa wengine Uhindi walioanzisha koloni na vituo vya Kireno.

Vasco da Gama alirudi Uhindi mara mbili. Safari iliyofuata ilifanywa mwaka 1502 na safari ya tatu mwaka 1524. Baada ya kufika Uhindi mara ya tatu aliambukizwa malaria akaaga dunia huko Cochin tarehe 24 Desemba 1524.

Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Vasco da Gama kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.