Nenda kwa yaliyomo

Nairobi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mkoa wa Nairobi)






Nairobi

Bendera

Nembo
Nairobi is located in Kenya
Nairobi
Nairobi

Mji wa Nairobi (Kenya)

Majiranukta: 1°17′S 36°49′E / 1.283°S 36.817°E / -1.283; 36.817
Nchi Bendera ya Kenya Kenya
Kaunti Nairobi
Idadi ya wakazi (2019)
 - Wakazi kwa ujumla 4,397,073
Tovuti:  nairobi.go.ke
Sanamu ya Jomo Kenyatta.

Nairobi ni mji mkuu wa jamhuri ya Kenya na vilevile mojawapo ya kaunti za Kenya.

Kulingana na sensa ya mwaka 2019, Nairobi ina wakaaji 4,397,073 katika eneo la km2 696 (sq mi 269).

Pamoja na vitongoji vyake, Nairobi ni mji wa 12 kwa ukubwa barani Afrika.

Jina Nairobi limetokana na neno la Kimaasai, Enkarenairobi, linalomaanisha "mahali penye maji baridi."

Lugha zote za Kenya huzungumzwa Nairobi, lakini hasa ni Kiingereza na Kiswahili pamoja na Sheng.

Eneo la jiji la Nairobi

[hariri | hariri chanzo]
Kaunti ya Nairobi (nyekundu) ndani ya jiji la Nairobi (kijani).

Nairobi yenyewe iko ndani ya eneo la jiji la Nairobi (kwa Kiingereza: Greater Nairobi Metropolitan region) lililoundwa na kaunti 4 kati ya jumla ya 47 za Kenya.

Kaunti hizo ni:

Eneo Kaunti Eneo lake (km2) Idadi ya wakazi
Sensa 2009
Jiji/Mii/Manisipaa kwenye kaunti
Nairobi ya Kati Kaunti ya Nairobi 694.9 3,138,369 Nairobi
Eneo la Kaskazini Kaunti ya Kiambu 2,449.2 1,623,282 Kiambu, Thika, Limuru, Ruiru, Karuri, Kikuyu, Kahawa
Eneo la Kusini Kaunti ya Kajiado 21,292.7 687,312 Kajiado, Olkejuado, Bissil, Ngong, Kitengela, Kiserian, Ongata Rongai
Eneo la Mashariki Kaunti ya Machakos 5,952.9 1,098,584 Kangundo-Tala, Machakos, Athi River
Jumla Eneo la Jiji la Nairobi 30,389.7 6,547,547

Source: Kenya Census

Eneo hilo linazalisha asilimia 60 za pato la taifa.

Mazingira na hali ya hewa

[hariri | hariri chanzo]

Nairobi iko kilomita 150 upande wa kusini ya ikweta kwenye nyanda za juu za Kenya kando la mto Nairobi. Nairobi imeanzishwa mahali ambako nchi tambarare ya mto Athi inaanza kupanda juu hadi milima ya Ngong na vilima vingina vinyvyofanya ukuta wa mashariki wa Bonde la Ufa.

Kitovu cha Nairobi kiko zipatao m 1624 juu ya UB. Sehemu za mashariki za jiji ziko bado kwenye tambarare, na sehemu za magharibi ziko kwenye mtelemko unaopanda hadi mita 1800 kwenye mpaka wa jiji na mita 2000 juu ya UB kwenye nje ya jiji huko Limuru.

Hali ya hewa haina joto kali. Halijoto ya wastani ni 20,5°C mwezi wa Machi, na 16,8°C mwezi wa Julai. Wakati wa Juni na Julai usiku unaweza kuwa baridi halijoto ikishuka chini ya sentigredi 10.

Mvua nyingi hunyesha mwezi Machi (mm 199), kiangazi kina mm 14 tu wakati wa Julai.

Historia ya Nairobi

[hariri | hariri chanzo]

Chanzo kwenye kambi la reli

[hariri | hariri chanzo]

Nairobi ilianzishwa na Waingereza mwaka 1899 kama kambi ya kujenga Reli ya Uganda. Njia ya reli ilikuwa imefika kutoka Mombasa ikaonekana ya kwamba kuanzia hapa kasi ya ujenzi itachelewa kutokana na ugumo na eneo la Bonde la Ufa na mitelemko yake mikali. Mahali palikuwa karibu katikati ya Mombasa na Kampala, palikuwa na maji pakaonekana panafaa kwa kituo njiani. Hasahasa ilionekana tabianchi ya nyanda za juu ilifaa kiafya kwa Waingereza walioteswa na joto la pwani na kwenye nyanda za chini.

Kitangulizi cha Nairobi kilikuwa kituo kidogo kilichoanzishwa mwaka 1896 kando ya mto Nairobi na wakala Mwingereza wa reli kwa kusudi la kuajiri wafanyakazi wazalendo kwa ujenzi wa reli. Mwaka uliofuata 1897 wakaguzi walioandaa njia ya reli walipiga kambi karibu naye. [1].

Mji mkuu wa koloni

[hariri | hariri chanzo]

Njia ya reli ilifika kwenye kambi tarehe 30 Mei 1899. Hapo idadi ya wafanyakazi - hasa Wahindi - iliongezeka sana na kambi lilikuwa kubwa ya mahema na ghala za vifaa vya ujenzi. Mwezi wa Juni mizigo ya mabati ilifika kutoka Mombasa - tayari kwa reli - na majengo ya kudumu yalianza kutengenezwa katika mazingira ya eneo la kituo cha reli cha leo. Mwezi wa Agosti kamishna Mwingereza wa jimbo la Ukamba[2] aliamuliwa kuhamisha makao makuu yake Nairobi kutoka Machakos akajenga boma lake kwenye eneo la Moi Avenue, mbali na reli jinsi inavyoonekana hadi leo kwenye majengo ya polisi ya kihistoria yanayotazama Bustani ya Jivanji[3].

Barabara kuu ya kwanza ilikuwa "Station Road" [4] kandokando ya Mtaa wa Tom Mboya wa leo iliyoitwa Victoria Street ikawa mahali pa maduka na hoteli za kwanza zilizoendeshwa na Wazungu na baadaye pia na Wahindi kadhaa. Soko la Wahindi maskini likuwa kando. Kwenye sehemu kati ya mitaa ya Haile Selassie na Harambee kulikuwa na makazi ya kwanza ya wafanyakazi. Mwaka uleule wa 1899 ofisi kuu ya reli ikapelekwa huko kutoka Mombasa kwa shabaha ya kurahisisha mawasiliano.

Pale mwanzoni kulikuwa na wasiwasi kuhusu chaguo la mahali; baada ya mvua kali sehemu ya mahema na vibanda vilipatikana katikati ya ziwa la matope. Magonjwa yalisambaa na baada ya epidemia ya tauni soko la Wahindi Lilichomwa na kuhamishwa sehemu nyingine. Majaribio ya kukausha kinamasi yaliendelea kwa miaka kadhaa hadi kufaulu. Kutokana na usumbufu wa matope maafisa wa ngazi ya juu walijenga nyumba zao kwenye kilima cha karibu kilichojulikana kama Nairobi Hill.

Mwaka 1905 Waingereza walihamisha ofisi kuu ya serikali yao ya kikoloni kutoka Mombasa kwenda Nairobi, ambayo ikawa hivyo makao makuu ya Afrika ya Mashariki ya Kiingereza (British East Africa, baadaye Kenya Colony).

Uchumi wa mji ulitegemea pale mwanzoni hasahasa mahitaji ya utawala wa serikali na reli na utalii; matajiri wengi kutoka pande zote za dunia waliFIka kwa kusudi la kuwinda wanyama wakubwa [5] wakivutwa na wingi wa wanyama kwenye nyanda za juu na usafiri rahisi kwa reli. Baadaye ardhi katika mazingira ya mji ilitolewa kwa walowezi Wazungu na kilimo cha biashara kilianza kuchangia.

Kiasili Nairobi ilikuwa imepangwa kwa ajili ya Wazungu wa reli na serikali pamoja na Wahindi; Waafrika hawakupewa makazi isipokuwa mabweni ya wanfanyakazi wa reli na vibanda vya wafanyakazi wasaidizi kandokando ya nyumba za mabwana wao.

Lakini Waingereza waliajiri askari kutoka Sudan na Somalia katika jeshi na polisi, na hao walifuatwa na wafanyabiashara kutoka kwao. Wapagazi na askari kutoka sehemu mbalimbali za Afrika ya Mashariki walifika Nairobi kikazi na wengine waliamua kubaki. Mitaa ya vibanda iliota haraka nje ya mji wenyewe, mingine ilibomolewa haraka, mingine iliweza kubaki. Mnamo 1921 kulikuwa na Waafrika 12,000 waliokaa katika mitaa ya Waafrika iliyoitwa Mombasa, Masikini, Kaburini, Kariokor, Kibera, Pumwani na Pangani.

Tangu uhuru

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1963 ikawa mji mkuu wa nchi huru ya Kenya ikaendelea kukua haraka.

Nairobi ya leo

[hariri | hariri chanzo]
Nairobi leo: New Central Bank Tower (140 m), Teleposta Towers (120 m), Kenyatta International Conference Centre (105 m), NSSF Building (103 m), I&M Bank Tower (100 m), Government Office Conference Hall (98 m)[2].

Nairobi imeibuka kuwa mmojawapo kati ya miji mikubwa katika bara la Afrika. Mashirika mengi makubwa duniani yamefungua ofisi zao zinazoshuhudia eneo la Afrika ya Mashariki na Afrika ya Kati. Mojawapo ya mashirika haya ni ofisi za tawi la Umoja wa Mataifa (United Nations), UNEP. Kunazo pia ofisi za mabalozi wa nchi mbalimbali duniani.

Nairobi, kama miji mingi mikubwa, ina matatizo mengi yanayotokea kwa sababu ya ukubwa wake. Watamaduni walioupanga mji wa Nairobi hawakutegemea kuwa utatanuka hivyo. Wataalamu wengi wametoa maonyo mengi kuhusu ukubwa wa mji huu na uwezo wake wa kuwahudumia wakazi wote ambao wanazidi kuongezeka kila mwaka.

Nairobi imewavutia wakazi wengi, wote wakiwa na hamu ya kujitafutia riziki yao. Ijapokuwa wapo wanaofanikiwa, wengi wao hujipata wameangulia patupu wakaachwa bila pesa au hali ya kujikimu. Jambo hili limepelekea kuwepo kwa wakazi wa maeneo yasiyotengwa wananchi, maarufu kama 'slums' kwa Kimombo. Eneo kubwa zaidi jijini Nairobi ni Kibera. Eneo hili lina ukubwa wa kilomita 2 kwa 2 na wakazi takribani milioni moja. Eneo hili halina mipango yoyote ya kuruhusu binadamu kuishi lakini umaskini umewavutia wengi kuishi kule.

Kunayo pia matatizo ya ujambazi na utekaji nyara wa magari. Matatizo haya yamesababisha watu wengi kutoupendelea mji wa Nairobi.

        Mwaka         Wakazi
1906 11.500
1911 14.000
1921 24.300
1926 29.900
1929 32.900
1931 47.800
1939 61.300
1944 108.900
1948 119.000
1955 186.000
        Mwaka         Wakazi
1957 221.700
1960 251.000
1962 266.800
1965 380.000
1969 509.300
1979 827.775
1989 1.324.570
1995 1.810.000
1999 2.143.254
2005 2.750.561
2009 3.138.369
Picha ya Nairobi kutoka Westlands

Maeneo bunge

[hariri | hariri chanzo]
Kenyatta International Convention Centre na Times Tower.

Kaunti ya Nairobi imegawanywa katika maeneo bunge 17 na kata 85,[6].

Maeneo bunge Kata
Westlands Kitisuru · Parklands/Highridge · Karura · Kangemi · Mountain View
Dagoretti North Kilimani · Kawangware · Gatina · Kileleshwa · Kabiro
Dagoretti South Mutu-ini · Ngand'o · Riruta · Uthiru/Ruthimitu · Waithaka
Langata Karen · Nairobi West · Ngumo · South C · Nyayo Highrise · Otiende  · Sunvalley I/II · St.Mary's Hospital· Royal Park
Kibra Laini Saba · Lindi · Makina · Woodley/Kenyatta Golf Course · Sarang'ombe
Roysambu Roysambu · Garden Estate · Muthaiga · Ridgeways · Githurai · Kahawa West · Zimmermann · Kahawa
Kasarani Clay City · Mwiki · Kasarani · Njiru · Ruai
Ruaraka Babadogo · Utalii · Mathare North · Lucky Summer · Korogocho
Embakasi South Imara Daima · Kwa Njenga · Kwa Reuben · Pipeline · Kware
Embakasi North Kariobangi Kaskazini · Dandora Area I · Dandora Area II · Dandora Area III · Dandora Area IV
Embakasi Central Kayole North · Kayole North Central · Kayole South · Komarock · Matopeni/Spring Valley
Embakasi East Upper Savanna · Lower Savanna · Embakasi · Utawala · Mihang'o
Embakasi West Umoja I · Umoja II · Mowlem · Kariobangi Kusini
Makadara Maringo/Hamza · Viwandani · Harambee · Makongeni · Mbotela · Bahati
Kamukunji Pumwani · Eastleigh North · Eastleigh South · Airbase · California
Starehe Nairobi Central · Ngara · Pangani · Ziwani/Kariokor · Landimawe · Nairobi South
Mathare Hospital · Mabatini · Huruma · Ngei · Mlango Kubwa · Kiamaiko

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. Christine Stephanie Nicholls, Red Strangers, uk. 37 f.
  2. Ukamba ilikuwa moja kati ya majimbo 4 ya Afrika ya Mashariki ya Kiingereza (iliyokuwa koloni la Kenya tangu mwaka 1920) na makao makuu yalikuwepo Machakos
  3. Kituo cha polisi (Nairobi Central Police Station) iko mahali pa boma lile la kwanza
  4. ikaitwa baadaye Government Road, leo hii ni Moi Avenue
  5. Kama wale maarufu "Big Five" yaani tembo, simba, nyati, kifaru na chui
  6. [1] Archived 19 Machi 2013 at the Wayback Machine

Kujisomea

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: