Historia ya Nairobi
Historia ya Nairobi, mji mkuu wa Kenya ni kama ifuatavyo.
Chanzo kwenye kambi la reli
[hariri | hariri chanzo]Nairobi ilianzishwa na Waingereza mwaka 1899 kama kambi ya kujenga Reli ya Uganda. Njia ya reli ilikuwa imefika kutoka Mombasa ikaonekana ya kwamba kuanzia hapa kasi ya ujenzi itachelewa kutokana na ugumo na eneo la Bonde la Ufa na mitelemko yake mikali. Mahali palikuwa karibu katikati ya Mombasa na Kampala, palikuwa na maji pakaonekana panafaa kwa kituo njiani. Hasahasa ilionekana tabianchi ya nyanda za juu ilifaa kiafya kwa Waingereza walioteswa na joto la pwani na kwenye nyanda za chini.
Kitangulizi cha Nairobi kilikuwa kituo kidogo kilichoanzishwa mwaka 1896 kando ya mto Nairobi na wakala Mwingereza wa reli kwa kusudi la kuajiri wafanyakazi wazalendo kwa ujenzi wa reli. Mwaka uliofuata 1897 wakaguzi walioandaa njia ya reli walipiga kambi karibu naye. [1].
Mji mkuu wa koloni
[hariri | hariri chanzo]Njia ya reli ilifika kwenye kambi tarehe 30 Mei 1899. Hapo idadi ya wafanyakazi - hasa Wahindi - iliongezeka sana na kambi lilikuwa kubwa ya mahema na ghala za vifaa vya ujenzi. Mwezi wa Juni mizigo ya mabati ilifika kutoka Mombasa - tayari kwa reli - na majengo ya kudumu yalianza kutengenezwa katika mazingira ya eneo la kituo cha reli cha leo. Mwezi wa Agosti kamishna Mwingereza wa jimbo la Ukamba[2] aliamuliwa kuhamisha makao makuu yake Nairobi kutoka Machakos akajenga boma lake kwenye eneo la Moi Avenue, mbali na reli jinsi inavyoonekana hadi leo kwenye majengo ya polisi ya kihistoria yanayotazama Bustani ya Jivanji[3].
Barabara kuu ya kwanza ilikuwa "Station Road" [4] kandokando ya Mtaa wa Tom Mboya wa leo iliyoitwa Victoria Street ikawa mahali pa maduka na hoteli za kwanza zilizoendeshwa na Wazungu na baadaye pia na Wahindi kadhaa. Soko la Wahindi maskini likuwa kando. Kwenye sehemu kati ya mitaa ya Haile Selassie na Harambee kulikuwa na makazi ya kwanza ya wafanyakazi. Mwaka uleule wa 1899 ofisi kuu ya reli ikapelekwa huko kutoka Mombasa kwa shabaha ya kurahisisha mawasiliano.
Mwanzoni kulikuwa na wasiwasi kuhusu chaguo la mahali; baada ya mvua kali sehemu ya mahema na vibanda vilipatikana katikati ya ziwa la matope. Magonjwa yalisambaa na baada ya epidemia ya tauni soko la Wahindi Lilichomwa na kuhamishwa sehemu nyingine. Majaribio ya kukausha kinamasi yaliendelea kwa miaka kadhaa hadi kufaulu. Kutokana na usumbufu wa matope maafisa wa ngazi ya juu walijenga nyumba zao kwenye kilima cha karibu kilichojulikana kama Nairobi Hill.
Mwaka 1905 Waingereza walihamisha ofisi kuu ya serikali yao ya kikoloni kutoka Mombasa kwenda Nairobi, ambayo ikawa hivyo makao makuu ya Afrika ya Mashariki ya Kiingereza (British East Africa, baadaye Kenya Colony).
Uchumi wa mji ulitegemea pale mwanzoni hasahasa mahitaji ya utawala wa serikali na reli na utalii; matajiri wengi kutoka pande zote za dunia waliFIka kwa kusudi la kuwinda wanyama wakubwa [5] wakivutwa na wingi wa wanyama kwenye nyanda za juu na usafiri rahisi kwa reli. Baadaye ardhi katika mazingira ya mji ilitolewa kwa walowezi Wazungu na kilimo cha biashara kilianza kuchangia.
Kiasili Nairobi ilikuwa imepangwa kwa ajili ya Wazungu wa reli na serikali pamoja na Wahindi; Waafrika hawakupewa makazi isipokuwa mabweni ya wanfanyakazi wa reli na vibanda vya wafanyakazi wasaidizi kandokando ya nyumba za mabwana wao.
Lakini Waingereza waliajiri askari kutoka Sudan na Somalia katika jeshi na polisi, na hao walifuatwa na wafanyabiashara kutoka kwao. Wapagazi na askari kutoka sehemu mbalimbali za Afrika ya Mashariki walifika Nairobi kikazi na wengine waliamua kubaki. Mitaa ya vibanda iliota haraka nje ya mji wenyewe, mingine ilibomolewa haraka, mingine iliweza kubaki. Mnamo 1921 kulikuwa na Waafrika 12,000 waliokaa katika mitaa ya Waafrika iliyoitwa Mombasa, Masikini, Kaburini, Kariokor, Kibera, Pumwani na Pangani.
Tangu uhuru
[hariri | hariri chanzo]Mwaka 1963 ikawa mji mkuu wa nchi huru ya Kenya ikaendelea kukua haraka hadi leo ambapo ni kama ya majiji makubwa zaidi duniani.
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Christine Stephanie Nicholls, Red Strangers, uk. 37 f.
- ↑ Ukamba ilikuwa moja kati ya majimbo 4 ya Afrika ya Mashariki ya Kiingereza (iliyokuwa koloni la Kenya tangu mwaka 1920) na makao makuu yalikuwepo Machakos
- ↑ Kituo cha polisi (Nairobi Central Police Station) iko mahali pa boma lile la kwanza
- ↑ ikaitwa baadaye Government Road, leo hii ni Moi Avenue
- ↑ Kama wale maarufu "Big Five" yaani tembo, simba, nyati, kifaru na chui
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Nairobi kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |