Mabati

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Paa ya mabati
Kanisa la mabati mjini London
Ndege ya Ju52 ilifunikwa kwa mabati

Mabati ni vipande bapa za chuma vilivyofunikwa na ganda nyembamba la zinki. Vinatumiwa kwa ujenzi hasa kwa kufunika paa lakini pia kwa shughuli nyingine kama kujenga kuta za majengo au kwa ajili ya magari. Zinki inazuia kutu isiharibu chuma.

Umbo la kawaida[hariri | hariri chanzo]

Kuna aina mbalimbali za mabati. Umbo linalotumiwa mara nyingi ni bapa ikiwa na mabonde umbo la viwimbi. Umbo hili linafanya bati kuwa imara zaidi haikunjiki kirahisi kwenye mwelekeo wa mabonde yake lakini bado inaweza kuviringishwa.

Faida za ujenzi kwa mabati[hariri | hariri chanzo]

Mabati ni nyepesi na hubebwa kirahisi. Katika ujenzi faida yake ni gharama dogo kwa sababu mabati yanafungwa juu ya maunzi ya ubao au feleji. Maunzi yanaweza kujengwa mepesi pia kwa sababu hayana kazi ya kubeba mambo mazito. Pia si gharama kubwa kupeleka vifaa hivi vyepesi hadi mahali pa kujenga. Wafanyakazi wachache wanaweza kufunga mabati juu ya maunzi ya ndani. Yote hupunguza gharama za ujenzi.

Hutumiwa kwa ajili ya majengo mbalimbali kama vile kuta na paa za

  • karahana na viwanda
  • zizi la wanyama au ghala za vyakula
  • gereji ya magari
  • tangi za maji
  • nyumba rahisi za kuishi watu hasa katika mitaa ya vibanda

Hasara[hariri | hariri chanzo]

Hayapendezi kwa ujenzi wa nyumba za watu lakini kutokana na gharama ndogo watu maskini wanayatumia mara nyingi. Hasara ya nyumba hizi ni ukosefu wa kinga dhidi ya joto na baridi kwa sababu metali ya mabati inapitisha joto na baridi haraka.

Si kifaa cha kudumu sana. Hali halisi zinki juu ya mabati hayawezi kuzuia chuma kushikwa na kutu. Hatari ni hasa mvua asidi au chumvi hewani kaika maeneo karibu na bahari na katika mazingira haya kutu inaonekana baada ya miaka michache. Mabati yanaweza kukingwa zaidi kwa kuyapakia rangi.

Aina nyingine za vifaa vinavyoitwa mabati[hariri | hariri chanzo]

Umbo tofauti ni ile ya trapezi pachasawa ambayo ni imara zaidi.

Bapa kama mabati hutengenezwa pia kwa kutumia feleji au alumini; zinaweza kufunikwa kwa ganda la rangi au plastiki badala ya zinki au juu ya zinki. Kama bapa za plastiki zinapewa umbo la viwimbi wakati mwingine zinaitwa pia "mabati" na kutumiwa vile.

Umbo la bapa ya viwimbi hutengenezwa pia kwa saruji ya kuimarisha kwa kuiga mfano wa mabati.