Njia ya reli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Ujenzi wa reli ya Uganda wakati wa ukoloni - misingi kuinuliwa penye hatari ya mafuriko

Njia ya reli ni barabara maalumu iliyojengwa kwa ajili ya matumizi ya treni.

Kwa kawaida njia hii hutengenezwa kwa kufunga pau mbili za feleji sambamba kwenye boriti za ubao, simiti au chuma zinazokaa juu ya msingi wa mawe ya kokoto.

Umbali kati ya reli mbili umesanifishwa katika kila nchi au angalau eneo la kampuni ya reli. Umbali huu unapaswa kulingana kikamilifu na upana wa magurudumu ya treni maana tofauti na magari barabarani treni hazilengwi na dereva bali na reli za njia zenyewe.

Muundo wa ujenzi wa njia ya reli
Ujenzi wa njia ya reli nchini Finlandi mnamo mwaka 1950

Muundo wa ujenzi[hariri | hariri chanzo]

Kazi ya kwanza ni kujenga msingi wa njia ya reli. Pale ambako ardhi si imara kanda la ardhi linapelekwa kwenye msingi. Juu yake kanda nyingine ya mchanga au kokoto ndogo inaweza kungezwa, kutegemeana na mazingira.

Juu ya hiyo panaweka kanda la mawe ya kokoto ambayo ni tako kwa boriti zinazobeba reli za garimoshi. Boriti hizi zinashika reli katika umbali unaotakiwa. Boriti zilikuwa zamani kwa kawaida za ubao mgumu, siku hizi pia mara nyingi za simiti, wakati mwingine pia za chuma.

Reli hushikwa kwa mabano yanayofungwa kwa parafujo ndefu katika boriti.

Uwezo wa njia ya reli kubeba treni nzito na pia treni za haraka unategemea uwezo wa msingi pamoja na uzito wa reli za garimoshi zenyewe.

Zamani ujenzi ulifanywa kwa mikono pekee lakini siku hizi kuna mashine za pekee (tazama filamu chini kabisa kwenye ukurasa inayoonyesha jinsi mashina inalaza boriti za simiti mfululizo nchini Ujerumani).

Kabla ya ujenzi wa njia kuna kazi ya kukagua eneo na kuchagua njia bora inayowezekana. Wakaguzi wanaangalia aina za udongo, mitelemko, hatari za mafuriko njiani na mengi mengine.

Reli za kutambuzwa[hariri | hariri chanzo]

Zamani vyuma vya reli za garimoshi vilifungwa kwa kuacha mapengo madogo kati yao. Hii ilikuwa muhimu kwa sababu chuma na feleji inapanuka kidogo wakati wa joto na kujikaza yaani kuwa fupi kidogo wakati wa baridi kali. Siku hizi vyuma hiyi vinashikwa pamoja kwa njia ya kufuma yaani tambuzo (kuyeyusha uso wa vyuma kwa joto kubwa na kuviunganisha hivyo). Mtutuko unaoweza kutokea ndani ya vyuma hubanwa kwa njia ya ujenzi imara zaidi. Kama ni lazima wajenzi wanaongeza sehemu za pekee za upanuzi.

Swichi[hariri | hariri chanzo]

Pale ambako njia za reli zinaungana au kuachana kuna swichi zinazowezesha treni kubadilisha njia. Swichi hizi kwenye njia zinazotumiwa na treni chache zinaweza kubadilishwa kwa mkono, na kwa kazi hii ni lazima kuwa na kituo au ofisi kwa wafanyakazi. Kwenye reli zilizoendelea swichi hizi hutawaliwa kwa mbali ama kupitia nyaya ndefu au siku hizi pia kwa njia ya elektroniki ilhali kila swichi ina injini ndogo ya umeme.

Penye usafiri mwingi njia za reli hujengwa kwa jozi yaani njia mbili kandokando ili treni mbili zinaweza kupitana bila matatizo, Pale ambako kua njia 1 tu ni lazima kupanga sehemu ambako treni 1 inaweza kusubiri hadi treni nyingine imepita.

Upana wa njia[hariri | hariri chanzo]

Upana kati ya reli mbili (ing. gauge) unatofautiana kati ya nchi na nchi. Kwa kawaida nchi jirani huwa na upana wa pamoja ili kurahisisha mwendo wa treni na mabehewa.

Upana sanifu wa kimataifa leo hii ni mita 1.435 (futi 4 inchi 8 1⁄2). Katika Afrika ya Mashariki reli za kwanza zilijengwa wakati wa ukoloni na Wajerumani pia Waingereza walijenga reli yenye upana wa mita 1 pekee kama vile Reli ya Tanganyika. Wakati ule hii ilitazamiwa kuwa inatosha kwa mahitaji ya usafiri tena ilipunguza gharama. Lakini siku hizi hairuhusu kutumia njia hizi kwa treni nzito wala treni za haraka. Kwa hiyo Kenya inapanga kubadilisha upana wa reli kwenda upana sanifu wa kimataifa.

Wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA nchini Tanzania upana wa mita 1.067 ulichaguliwa kwa sababu reli hii inaungana na reli ya Zambia huko New Kapiri Mposhi na reli zote za Kusini ya Afrika hutumia upana huu. Ndani ya Tanznia kuna matatizo ya kwamba mabehewa ya TAZARA na Tanzania Railway Corporation hayalingani yaani hayawezi kuingia kwenye njia za kampuni nyingine. Njia zote mbili za TAZARA na TRC zinakutana Daressalaam na pale Kidatu kuna kituuo cha kubadilishana kontena kati ya makampuni mawili.

Urusi na nchi zilizokuwa sehemu ya Umoja wa Kisovyeti huwa na upana wa mita 1.520 ambayo ni pana zaidi kuliko nchi nyingi za jirani. Kwa sababu ya uwingi wa usafiri wa reli ndani ya Urusi na nchi za Ulaya na China kuna vituo mbalimbali ambako sehemu ya chini za mabehewa zinabadilishwa kwa ajili ya upana husika wakati wa kuvuka mipaka.