Nenda kwa yaliyomo

Urusi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mrusi)
Российская Федерация
Rossiyskaya Federatsiya

Shirikisho la Urusi
Bendera ya Russia Nembo ya Russia
Bendera Nembo
Kaulimbiu ya taifa: none
Wimbo wa taifa: Hymn of the Russian Federation
Lokeshen ya Russia
Mji mkuu Moscow
55°45′ N 37°37′ E
Mji mkubwa nchini Moscow
Lugha rasmi Kirusi
Serikali Jamhuri, Shirikisho
serikali ya kiraisi
Vladimir Putin
Mikhail Mishustin
Uhuru
{{{established_events}}}
{{{established_dates}}}
Eneo
 - Jumla
 - Maji (%)
 
17,075,400 km² (ya 1)
13
Idadi ya watu
 - 1-1-2021 kadirio
 - 2002 sensa
 - Msongamano wa watu
 
146,238,000 (ya 9)
145,164,000
8.3/km² (ya 217)
Fedha Rubl (RUB)
Saa za eneo
 - Kiangazi (DST)
(UTC+2 to +12)
(UTC+3 to +13)
Intaneti TLD .ru, (.su reserved)
Kodi ya simu +7

-

1 Rank based on Aprili 2006 IMF data



Urusi (kwa Kirusi: Россия, Rossiya) ni nchi ya Ulaya ya Mashariki na ya Asia.

Kwa eneo ni nchi kubwa kuliko zote duniani, ikiwa na km² 17,075,400.

Urusi imepakana na Norway, Ufini, Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Belarus, Ukraine, Georgia, Azerbaijan, Kazakhstan, China, Mongolia na Korea ya Kaskazini.

Iko karibu vilevile na maeneo ya Marekani (jimbo la Alaska liko ng'ambo ya mlango wa Bering) na Japani (kisiwa cha Hokkaido kiko ng'ambo ya mlango wa La Pérouse.

Kuna wakazi 146,238,000[1].

Mji mkuu ni Moscow.

Hadi mwaka 1991 Urusi ilikuwa kiini cha Umoja wa Kisovyeti na kuitwa Shirikisho la Jamhuri ya Kisovyiet ya Kijamii ya Kirusi.

Urusi ilikuwa udikteta chini ya chama cha kikomunisti. Tangu 1990 imekuwa demokrasia.

Muundo wa utawala ni shirikisho la jamhuri chini ya rais mtendaji.

Jiografia

Makala kuu: Jiografia ya Urusi

Eneo la Shirikisho la Kirusi linajumlisha sehemu kubwa ya kaskazini ya mabara ya Ulaya na Asia. Umbali kati ya upande wa magharibi na upande wa mashariki kabisa ni karibu kilomita 8,000.

Mkoa wa Kaliningrad haufuatani moja kwa moja na maeneo mengine ya Urusi: umetengwa nayo kijiografia na Lithuania.

Mara nyingi Urusi hutazamwa kama sehemu mbili: Urusi wa Ulaya hadi milima ya Ural na Siberia au Urusi wa Kiasia ambayo ni nchi pana kati ya Ural na Pasifiki.

Sehemu kubwa ya Urusi ni tambarare yenye vilima vidogo tu. Milima mirefu inapatikana kusini na mashariki mwa Siberia.

Bahari mpakani urusi - Bahari Nyeusi, Bahari ya Azov, Bahari Nyeupe, Bahari ya Barents, Bahari ya Kara, Bahari ya Laptev, Bahari ya Mashariki ya Siberia, Bahari ya Chukchi, Bahari ya Bering, Bahari ya Ohotsk na Bahari ya Japani.

Pwani na visiwa

Jumla Urusi ina pwani ndefu sana zenye urefu wa kilomita 37,000 kwenye Bahari Aktiki na Pasifiki, pia kwenye Bahari Baltiki, Bahari Nyeusi na Bahari ya Kaspi.[2]

Visiwa vikubwa vya Urusi ni Novaya Zemlya na Kisiwa cha Wrangel kwenye Bahari Aktiki na Sakhalin kwenye Pasifiki. Funguvisiwa muhimu ni Funguvisiwa ya Franz Josef, Severnaya Zemlya, Visiwa vya Siberia Mpya katika Bahari aktiki, halafu Kurili katika Pasifiki.

Kanda za uoto

Eneo kubwa la Urusi hugawiwa kwa macho ya ekolojia kwa kanda asilia tano:

Maeneo makubwa ni uwanda, hasa uwanda wa Ulaya ya Mashariki na uwanda wa Siberia ya Magharibi, halafu nyanda za chini za Siberia Kaskazini na Kolyma. Nyanda za juu za Siberia ya Kati na Lena halafu safu za milima kwenye kaskazini-mashariki na kwenye mpaka wa kusini.

Tabianchi na hali ya hewa

Sehemu kubwa za Urusi huwa na vipindi vya majira tofauti sana; joto kubwa inafuatana na baridi kali.

Tabianchi ya Urusi ni hasa ya kibara, kutokana na umbo la nchi na umbali wa sehemu nyingi na bahari. Maeneo mengi yana umbali wa kilomita 400 na zaidi kutoka ufukoni, na kitovu cha nchi kina umbali wa kilomita 3,840 kutoka bahari.

Zaidi ya hayo Urusi ina safu za milima mirefu hasa upande wa kusini na upande wa mashariki ambazo zinazuia kufika kwa urahisi kutoka Bahari Hindi na Pasifiki upepo wenye uwezo wa kupoza halijoto. Kinyume chake upepo kutoka Bahari Aktiki unaweza kuingia bila vizuizi vya aina hii na kuleta baridi kali.

Theluji hufunika uso wa ardhi kati ya siku 40 hadi 200 kwa mwaka katika Urusi ya magharibi, na siku 120 - 200 kila mwaka katika Siberia. Katika kaskazini karibu na Aktiki iko ardhi yenye hali ya jalidi ya kudumu kwa kina cha mita mia kadhaa. Halijoto ya wastani ya sehemu kubwa ya Siberia iko chini ya 0°C.

Sehemu kubwa za Urusi zina majira mawili tu ambayo ni majirajoto na majirabaridi yenye jalidi. Vipindi vya kati ni vifupi sana. Hii inaathiri pia njia za usafiri. Wakati wa majirabaridi, ambako maji yote kwenye mito na maziwa huwa yameganda, barabara zinafunguliwa juu ya barafu ya mito mikubwa au kupitia maziwa makubwa.

Kanda nyembamba la pwani kwenye Bahari Nyeusi huwa na tabianchi ya nusutropiki.

Wakati wa Januari halijoto ni −6°C huko Saint Petersburg, −27°C katika Siberia ya magharibi na −43°C huko Yakutsk katika Siberia ya Kati. Wakati wa majirajoto halijoto inapatikana kati ya wastani ya 4°C kwenye visiwa vya aktiki na wastani ya 20°C katika kusini.

Halijoto ya chini iliyopimwa ilikuwa −68°C huko Siberia ya kaskazini na +45°C kusini mwa nchi.

Ukali wa baridi una athari kubwa juu ya maisha yote, jinsi gani watu wanaweza kufanya kazi, na kama kilimo kinawezekana au la. Majengo yanapaswa kuwa na tabia za pekee hasa katika maeneo ya jalidi ya kudumu ambako ni lazima kuweka kila jengo juu ya nguzo zinazofikia kina cha jalidi kwa sababu uso wa ardhi unakuwa laini na matope wakati wa joto; mashine zinapaswa kutengenezwa kwa kutumia feleji inayovumilia tofauti kubwa za jalidi na joto.

Miezi ya jalidi ni pia kipindi cha giza, kwa hiyo kuna mahitaji ya pekee ya nishati na nguo.

Usimbishaji katika sehemu nyingi za Urusi si mkubwa kwa sababu maeneo mengi yako mbali na pwani, hivyo hayapokei hewa yenye unyevunyevu kutoka bahari.

Sehemu zinazopokea mvua nyingi ziko karibu na pwani, kama Sochi kwenye Bahari Nyeusi (mm 1500 kwa mwaka) na visiwa vya Kurili (mm 1000 - 1500, hasa theluji). Pwani ya Baltiki inapokea mm 600, Moscow mm 525 kwa mwaka. Maeneo yaliyo karibu na Kazakhstan hupokea mm 20 pekee kwa mwaka, na kwenye sehemu za pwani za Aktiki ni mm 15 pekee.

Mito na maziwa

Kwa jumla kuna mito elfu kadhaa. Mingi iko sehemu ya beseni ya utiririshaji ya Bahari Aktiki ambako kuna watu wachache. Kwa hiyo sehemu kubwa ya maji haina matumizi kwa manufaa ya binadamu. Kinyume chake maeneo ya Urusi ya kusini kwenye vipindi vya joto na wakazi wengi yanaona vipindi vya uhaba wa maji kama vile beseni za mto Don na mto Kuban.

Upande wa mashariki wa Ural kuna mito 40 yenye urefu unaozidi kilomita 1,000. Ni hasa mito 3 inayobeba maji ya Siberia kwenda Bahari Aktiki:

Mito hii mitatu humwaga kila sekunde 50,000 kwenye Bahari Aktiki.

Kati ya mito mingine mikubwa kuna:

Maziwa ya Urusi hushika takriban robo ya maji matamu yote duniani yasiyo barafu. [3]

Ziwa kubwa ni Ziwa Baikal ambayo ni ziwa yenye maji mengi duniani.[4] Maziwa mengine ni pamoja na Ladoga na Onega ambayo ni kati ya maziwa makubwa zaidi ya Ulaya.

Miji mikubwa

Majiji mawili makuu ni Moscow na Sankt Peterburg.

Kanisa Kuu la Vasili Blazeni na mnara wa Spasski wa Kremlin mjini Moscow

Moscow ni mji mkuu wa kale uliyorudishiwa nafasi yake baada ya mapinduzi ya kikomunisti ya mwaka 1918.

Sankt Peterburg ilikuwa mji mkuu kuanzia mwaka 1703 hadi 1918 kama makao makuu ya tsar au kaisari wa Urusi. Miaka 1924-1989 ikaitwa Leningrad kwa heshima ya Lenin, kiongozi wa mapinduzi.

Miji mingine mikubwa ni pamoja na:

Historia

Makala kuu: Historia ya Urusi

Historia ya Urusi kama nchi ya pekee ilianza polepole pale ambako makabila ya wasemaji wa Kislavoni cha Mashariki walipoanza kujenga maeneo yao kuanzia karne ya 8 BK.

Waskandinavia waliunda dola la kwanza katika eneo la Kiev, wakalitawala kama dola la Kislavoni. Wenyewe waliingia haraka katika lugha na utamaduni wa wenyeji, lakini waliacha jina lao kwa sababu "Rus" kiasili ilikuwa jina la Waskandinavia wale kutoka Uswidi ya leo.

Mwaka 988 Kiev ilipokea Ukristo wa Kiorthodoksi kutoka Bizanti. Tukio hilo liliathiri moja kwa moja utamaduni na historia yote iliyofuata.

Dola la Kiev liliporomoka kutokana na mashambulio ya Wamongolia baada ya Jingis Khan, na maeneo madogo zaidi yalijitokeza yaliyopaswa kukubali ubwana wa Wamongolia.

Upanuzi wa utemi wa Moscow

Kubwa kati ya maeneo yale madogo ulikuwa utemi wa Moscow. Watemi wa Moscow walichukua nafasi ya kwanza kuunganisha Waslavoni wa Mashariki dhidi ya Wamongolia na kupanua utawala wao.

Baada ya anguko la Konstantinopoli mwaka 1453 watawala wa Moscow walipokea cheo cha Kaisari wa Roma kilichoitwa "tsar" na kuwa cheo cha watawala wa Urusi hadi mwaka 1917.

Mpaka karne ya 18 eneo la Moscow lilikuwa tayari kubwa likabadilika kuwa Milki ya Kirusi iliyoendelea kupanuka katika Siberia na Asia ya Kati, ikawa kati ya milki kubwa kabisa za historia ikienea kutoka Poland upande wa magharibi hadi bahari ya Pasifiki upande wa mashariki.

Matengenezo ya kisiasa chini ya Petro I

Tsar Petro I (1689 - 1725) alitambua ya kwamba nchi yake ilikuwa nyuma upande wa teknolojia na elimu kulingana na mataifa ya Ulaya. Alianzisha mabadiliko mengi ya kuiga mfano wa Ulaya ya Magharibi akahamisha mji mkuu kutoka Moscow kwenda mji mpya aliounda sehemu ya magharibi ya milki yake akauita Sankt Peterburg.

Tangu wakati wa Petro I nchi ilishiriki katika siasa ya Ulaya pamoja na vita vingi vya huko.

Mwanzo wa karne ya 19 milki ikashambuliwa na Napoleon Bonaparte aliyeteka Moscow lakini Warusi walifaulu kuwafukuza maadui kwa msaada wa baridi iliyoua askari wengi wa Ufaransa.

Upanuzi katika Asia

Matsar wa Urusi waliendelea kutawala kwa kuwa na mamlaka zote bila kushirikisha wananchi jinsi ilivyokuwa kawaida katika sehemu nyingine za Ulaya. Miji iliona maendeleo ya viwanda na jamii ya kisasa, lakini sehemu kubwa ya wakulima waliendelea kukaa chini ya utawala wa makabaila.

Katika sehemu ya pili ya karne ya 19 Urusi ulipanua utawala wake juu ya maneo makubwa ya Asia ya Kati na milima Kaukasus ukashindana na Milki ya Osmani, Uajemi na athira ya Uingereza katika Asia.

Mapinduzi za 1905 na 1917

Mwanzoni mwa karne ya 20 Urusi ukaonekana tena kuwa nyuma ya nchi za magharibi na sababu kuu ilikuwa nafasi kubwa ya serikali iliyojitahidi kusimamia mabadiliko yote katika jamii na kuzuia mabadiliko yaliyoonekana magumu machoni pa Tsar, pa makabaila na pa maaskofu wa Kanisa la Kiorthodoksi.

Mwaka 1904 upanuzi wa Urusi katika Asia uligongana na upanuzi wa Japan. Katika vita dhidi ya Japani Urusi ulishindwa na tukio hili lilisababisha mapinduzi ya Urusi ya 1905. Tsar Nikolas alipaswa kukubali uchaguzi wa bunge la duma kwa mara ya kwanza. Hata hivyo haki za duma zilikuwa chache na mabadiliko yalitokea polepole mno.

Urusi ulijiunga mwaka 1914 na vita kuu ya kwanza ya dunia ukisimama upande wa Uingereza na Ufaransa dhidi ya Ujerumani na Austria-Hungaria. Vita havikuenda vizuri, wananchi wakaona njaa na mapinduzi ya Februari 1917 yakamfukuza Tsar aliyejiuzulu.

Vita vikaendelea na Wajerumani walizidi kusogea mbele. Serikali mpya ya bunge ikapinduliwa katika mwezi wa Oktoba 1917 na mapinduzi ya Bolsheviki chini ya kiongozi wao Vladimir Ilyich Lenin.

Utawala wa kikomunisti na Umoja wa Kisovyeti

Huo ulikuwa mwanzo wa vita ya wenyewe kwa wenyewe. Wakomunisti chini ya Lenin walishinda na kugeuza Urusi kuwa Umoja wa Kisoveti tangu mwaka 1922, wakitawala kwa mfumo wa kiimla wa chama chao. Ili kurahisisha utawala wao Wakomunisti waliamua kutawala Urusi wa awali kwa muundo wa shirikisho, wakaunda jamhuri mbalimbali kufuatana na mataifa ndani ya eneo hilo kubwa.

Urusi lilikuwa sasa jina la jamhuri kubwa katika umoja huu nao ukaitwa Shirikisho la Jamhuri ya Kisovyiet ya Kijamii ya Kirusi.

Kikatiba jamhuri hizo zote zilikuwa nchi huru lakini hali halisi zilitawaliwa zote kutoka makao makuu ya chama cha kikomunisti huko Moscow. Katiba hiyo ilipata umuhimu tangu 1989, wakati wa mwisho wa utawala wa Wakomunisti ambako jamhuri zote zilitafuta uhuru wao zikaachana na Umoja.

Mji mkuu Sant Peterburg ulibadilishwa jina kuwa Leningrad na baadaye makao makuu ya nchi yakahamishwa tena kwenda Moscow.

Kiongozi aliyemfuata Lenin mwaka 1924 alikuwa Josef Stalin aliyeweza kugeuza utawala wa chama kuwa utawala wake mwenyewe akiongoza kwa jina la Katibu Mkuu wa chama cha kikomunisti.

Mwaka 1939, mwanzoni mwa vita kuu ya pili ya dunia Stalin alipatana na Ujerumani wa Adolf Hitler kugawa maeneo ya Poland na nchi za Baltiki kati yao lakini mwaka 1941 Hitler alishambulia pia Umoja wa Kisovyeti.

Warusi walipoteza askari milioni kadhaa, lakini waliweza kuwazuia Wajerumani wasiteke Moscow na Leningrad. Kwa msaada wa Marekani Warusi waliweza kurudisha jeshi la Ujerumani na kusogea magharibi. Umoja wa Kisovyeti ukawa kati ya nchi washindi wa vita kuu ya pili ya dunia.

Mashindano ya vita baridi dhidi ya Marekani

Tangu mwaka 1945 jeshi la Urusi lilikaa katika nchi zote za Ulaya ya Mashariki hadi katikati ya Ulaya. Katika nchi hizo zote serikali za kikomunisti zilianzishwa na kusimamiwa na ofisi kuu ya chama cha kikomunisti huko Moscow.

Urusi ulikuwa kiongozi wa nchi za kijamaa, ukishindana katika vita baridi dhidi ya nchi za magharibi zilizoongozwa na Marekani. Athira ya Umoja wa Kisovyeti ilipanuka hadi Afrika, Asia na Amerika ya Kati ambako nchi mbalimbali zilianza kuiga mtindo wa kikomunisti.

Kusambaratika kwa Umoja kwa Kisovyeti

Utawala wa kikomunisti uliendelea hadi mwaka 1990. Mwishoni matatizo ya uchumi yalizidi kwa sababu mfumo wa uchumi ulioongozwa moja kwa moja na serikali kuu, pamoja na utaratibu wa kiimla uliozuia wananchi kupinga siasa ya viongozi na kuleta hoja tofauti, ulisababisha tena nchi kubaki nyuma.

Tangu mwaka 1990 jamhuri kadhaa za Umoja wa Kisovyeti ziliondoka katika umoja na kutangaza uhuru wao ilhali serikali ilishindwa nguvu ya kuwazuia. Mwaka 1991 jamhuri wanachama za mwisho Urusi, Belarus na Ukraine ziliamua kumaliza Umoja wa Kisovyeti.

Urusi mpya

Tangu mwaka 1991 Urusi ulipungukiwa na maeneo mengi yaliyotwaliwa katika karne ya 19 na ya 18, ukabaki peke yake ingawa bado ni dola kubwa kuliko yote duniani.

Marais wa Urusi baada ya 1991 walikuwa Boris Yeltsin na Vladimir Putin.

Dmitry Medvedev alichaguliwa kuwa rais wa Urusi mwaka 2008 na mtangulizi wake Vladimir Putin akawa waziri mkuu. Mwaka 2012 Putin aliruhusiwa tena kikatiba kugombea uraisi akachaguliwa na kurudishwa tena mwaka 2018.

Siasa

Utawala

Kreml wa Moskwa ni kitovu cha serikali na ikulu ya Rais wa Urusi.

Kulingana na katiba ya nchi, Urusi ni shirikisho na jamhuri ambako rais ni mkuu wa nchi [5]na waziri mkuu ni kiongozi wa serikali.

Shirikisho la Urusi linafuata muundo wa demokrasia yenye mfumo wa vyama vingi. Kuna serikali ya kiraisi yenye mikono mitatu:

Rais huchaguliwa kwa kura ya wananchi wote kwa kipindi cha miaka sita akiweza kurudishwa mara moja madarakani; anaweza kugombea tena baada ya kupumzika angalau kipindi kimoja. [6]

Baraza la mawaziri lina waziri mkuu na mawaziri wake wanaoteuliwa na rais kulingana na pendekezo ka waziri mkuu. Waziri mkuu anahitaji kukubaliwa na duma.

Vyama vya kisiasa muhimu ni Urusi wa Umoja, Chama cha Kikomunisti cha Urusi, Chama Huria cha Urusi na Urusi wa Haki.

Mfumo wa Shirikisho

Kuna Maeneo ya Shirikisho la Urusi 85.

Ramani ya Maeneo ya Shirikisho la Urusi
Ramani ya Maeneo ya Shirikisho la Urusi

Kulingana na katiba ya nchi kuna maeneo 85 yanayofanya shirikisho lake [7] pamoja na eneo la Krim na mji wa Sevastopol.[8]

Maeneo ya shirikisho yanawakilishwa sawa katika bunge na kila moja linapewa wawakilishi wawili. [9] Lakini hali halisi yana viwango tofauti vya madaraka ya kujitawala katika siasa ya ndani.

  • Jamhuri za shirikisho 22 ambazo kwa jina zinajitawala, zina katiba zao zikiwa na gavana na bunge wanaochaguliwa na wakazi wake moja kwa moja. Sheria ya Urusi inaamuru uchaguzi wa moja kwa moja wa wakuu wa jamhuri lakini hao hawaruhusiwi tena kutumia cheo cha "rais".[10] Jamhuri ina haki ya kujiamulia kuhusu lugha rasmi. Hadhi ya jamhuri ilianzishwa kutokana na kuwepo kwa kabila kubwa au taifa lenye utamaduni usio wa Kirusi. Hali halisi jamhuri nyingi zina wakazi wengi Warusi kutokana na historia ya uhamiaji zamani za Umoja wa Kisovyeti.
  • Mikoa ya Urusi 55, ila kuna majina mawili kwa mikoa hiyo. Mingi inaitwa oblast ambayo ni hali ya kawaida na 9 inaitwa krai kwa sababu za kihistoria; zote zina gavana na wabunge wanaochaguliwa na wakazi moja kwa moja.
  • Majiji ya Shirikisho 3 ambayo ni majiji yaliyopewa hadhi ya pekee kutokana na umuhimu wao wa kitaifa (Moscow, Sankt Petersburg na Sevastopol)
  • Maeneo huru 5 ambayo ni maeneo makubwa yenye watu wachache yaliyopewa hadhi ya pekee kwa sababu ni maeneo ya kidesturi ya wakazi asilia wasio Warusi; siku hizi kote Warusi wamekuwa wengi lakini hadhi ya eneo huru ni jaribio la kuonyesha heshima kwa utamaduni wa pekee wa wenyeji. "Uhuru" katika mengi ni kwa jina tu, unahusu zaidi utamaduni na kutunza lugha ya wenyeji asilia: mengi hutawaliwa na mkoa wa jirani. Maeneo manne huitwa "okrug huru" na moja "oblast huru" ambayo ni Oblast huru ya Kiyahudi)

Maeneo yote ya Shirikisho yamepangwa katika kanda 9. Kila moja huwa na Mkuu wa Kanda anayeteuliwa na rais na jukumu lake ni kusimamia na kuangalia kazi ya serikali za maeneo.

Watu, lugha, dini

Warusi asilia ni 81%, lakini kuna makabila mengine 160 katika shirikisho, ambayo yanatumia lugha 100 hivi[11] (angalia orodha ya lugha za Urusi).

Kufuatana na sensa ya mwaka 2002 kulikuwa na watu milioni 142.6 wasemaji wa Kirusi, wakifuatwa na wasemaji wa Kitatari milioni 5.3 na Kiukraina milioni 1.8.[12]

Lugha rasmi na ya kawaida ni Kirusi kwenye maeneo yote ya Shirikisho la Kirusi lakini katiba ya nchi inatoa kibali kwa Jamhuri za shirikisho kujiamulia lugha rasmi ya nyongeza kwa eneo lao pamoja na Kirusi.[13]. Kuna pia "maeneo huru" ya pekee yenye lugha zao pamoja na Kirusi.

Dini

Mchoro wa Ivan Eggink ukionyesha Vladimir Mkuu akisikiliza mapadri wa Kiorthodoksi, huku mjumbe wa Papa akinuna pembeni.
Ubatizo wa Vladimir, mchoro wa ukutani wa Viktor Vasnetsov

Warusi wengi kabisa walikuwa wafuasi wa Ukristo wa Kiorthodoksi hadi mapinduzi ya 1917/18. Katika mapokeo yao wenyewe ni Mtume Andrea aliyeleta mara ya kwanza imani hiyo hadi Urusi.[14].

Chanzo cha mapokeo hayo yalitokeo kwenye eneo la Ukraine ya leo ambako mnamo mwaka 988 mtemi wa Kiev Vladimir Mkuu alipokea ubatizo kutoka kwa mapadre wa Kanisa la Bizanti uliofuatwa na ubatizo wa familia na wananchi wa Kiev[15].

Kanisa la Kiorthodoksi liliendelea kuwa dini rasmi katika milki za Kirusi hadi mapinduzi ya 1917. Wakomunisti walioshika utawala mwaka ule walikataa dini zote [16] Urusi pamoja na Umoja wa Kisovyeti ilikuwa nchi ya kwanza iliyoamua kufuata uatheisti kama itikadi kuu[17] [18][19] Serikali ya kikomunisti ilinyang'anya mali na majengo ya Kanisa, magazeti yake yalishambulia mafundisho ya dini, uatheisti ukafundishwa shuleni na waumini wakahangaishwa.[20] Makanisa mengi yaligeuzwa kwa matumizi ya ghala, ukumbi wa michezo na kadhalika au kubomolewa.

Mapadre, maaskofu na maimamu mara nyingi walikamatwa, kutupwa gerezani au kutumwa kwenye makambi ya GULAG. Kati ya miaka 1922 hadi 1926 jumla ya maaskofu 28 na mapadre zaidi ya 1,200 waliuawa. Wengi sana zaidi walidhulumiwa.[21]

Dini za awali ziliendelea chini ya ukomunisti lakini kwa matatizo makubwa. Waumini waliweza kusali kwao nyumbani na katika makanisa na misikiti michache iliyobaki. Wakati wa Vita Kuu ya Pili mateso yalipungua kidogo kwa sababu Joseph Stalin alitaka kuwaunganisha wananchi wote chini ya uongozi wake katika juhudi za vita.

Baada ya ukomunisti kuanguka mnamo 1990 jumuiya za kidini zimepata uhai mpya. Wafuasi wa dini hawahesabiwi katika sensa, hivyo kuna makadirio tu. Mnamo Agosti 2012 kulikuwa na kadirio la asilimia 46.8 za Warusi kuwa Wakristo [22] na asilimia 25 waliamini uwepo wa Mungu lakini bila kufuata dini yoyote. Makadirio mengine yalitaja asilimia 76 za Warusi kuwa Wakristo [23] au asilimia 65 [24].

Upande wa Wakristo, wengi wanakadiriwa kuwa Waorthodoksi (kati ya hao wengi hawashiriki kwenye ibada za mara kwa mara) na wachache ni Wakatoliki na Waprotestanti.[25]

Hekalu la dini zote mjini Kazan, Tatarstan

Uislamu ni dini yenye wafuasi wengi baada ya Kanisa la Kiorthodoksi.[26] Ni dini kuu kati ya watu wengi wa Kaukazi kama vile Wachecheni, Waingushi na Wacherkesi, pia kati ya wasemaji wengi wa Lugha za Kiturki kama vile Watatari na Wabashkiri. Kwa jumla kuna kadirio la kuwepo kwa Waislamu milioni 9.4 ambao ni sawa na asilimia 6.5% ya wananchi wote. Walio wengi ni Wasunni, pamoja na wafuasi wachache wa Shia na Ahmadiya. Sehemu kubwa wanajihesabu kuwa Waislamu bila madhehebu.[27] [22][28]

Katika maeneo matatu kuna wafuasi wa Ubuddha ambayo ni Buryatia, Tuva na Kalmykia.

Dini za jadi hufuatwa bado katika sehemu za Siberia na Mashariki ya Mbali kama vile Yakutia na Chukotka.

Kwa jumla Waslavi mara nyingi ni Wakristo wa Kiorthodoksi, wasemaji wa lugha za Kiturki ni zaidi Waislamu, na wenye lugha za Kimongolia mara nyingi hufuata Ubuddha.[29]

Kuhusu watu wasio na dini kuna makadirio kuwa kati ya 16% na 48% ya wananchi wote.[30]

Idadi ya watu wanaojihesabu kuwa Waatheisti ni asilimia 7 na idadi yao imeendelea kupungua. [31]

Tanbihi

  1. https://www.breitbart.com/national-security/2021/01/29/russias-population-drops-to-15-year-low/?inf_contact_key=e71d9f39f2e179dc29c4bc51137e481109c74070ac2bf3cfa7869e3cfd4ff832
  2. The World Factbook. "CIA". Central Intelligence Agency. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-07-03. Iliwekwa mnamo 26 Desemba 2007.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. Library of Congress. "Topography and drainage". Iliwekwa mnamo 26 Desemba 2007.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. "Lake Baikal—A Touchstone for Global Change and Rift Studies". United States Geological Survey. Iliwekwa mnamo 26 Desemba 2007.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  5. "The Constitution of the Russian Federation". (Article 80, §1). Iliwekwa mnamo 27 Desemba 2007.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  6. "The Constitution of the Russian Federation". (Article 81, §3). Iliwekwa mnamo 27 Desemba 2007.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  7. "The Constitution of the Russian Federation". pravo.gov.ru (kwa Russian). 11 Aprili 2014. ku. 19, 21.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link) CS1 maint: unrecognized language (link)
  8. "Treaty Between the Russian Federation and the Republic of Crimea on Ascension to the Russian Federation of the Republic of Crimea and on Establishment of New Subjects Within the Russian Federation" (kwa Kirusi). Kremlin.ru. 18 Machi 2014. Iliwekwa mnamo 10 Aprili 2014.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  9. "The Constitution of the Russian Federation". (Article 95, §2). Iliwekwa mnamo 27 Desemba 2007.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  10. "Federal Law of 28.12.2010 No. 406-FZ". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-01-16. Iliwekwa mnamo 2016-04-05.
  11. "Russia". Encyclopædia Britannica. Iliwekwa mnamo 31 Januari 2008.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  12. "Russian Census of 2002". 4.3. Population by nationalities and knowledge of Russian; 4.4. Spreading of knowledge of languages (except Russian). Rosstat. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2011-07-19. Iliwekwa mnamo 16 Januari 2008.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  13. "The Constitution of the Russian Federation". (Article 68, §2). Iliwekwa mnamo 27 Desemba 2007.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  14. Microsoft Encarta Online Encyclopedia 2007. "Russia". Russia. Archived from the original on 2008-01-09. https://web.archive.org/web/20080109010927/http://encarta.msn.com/encyclopedia_761569000_6/Russia.html. Retrieved 2007-12-27. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2008-01-09. Iliwekwa mnamo 2016-04-17.
  15. Oleg Rapov, Russkaya tserkov v IX–pervoy treti XII veka (The Russian Church from the 9th to the First 3rd of the 12th Century). Moscow, 1988.
  16. Arto Luukkanen (1994), The Party of Unbelief, Helsinki: Studia Historica 48, ISBN 951-710-008-6, OCLC 832629341
  17. Kowalewski, David (Oktoba 1980). "Protest for Religious Rights in the USSR: Characteristics and Consequences". Russian Review. 39 (4): 426–441. doi:10.2307/128810. JSTOR 128810 – kutoka JSTOR. {{cite journal}}: Unknown parameter |registration= ignored (|url-access= suggested) (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  18. Ramet, Sabrina Petra. (Ed) (1993). Religious Policy in the Soviet Union. Cambridge University Press. ku. 4.
  19. Anderson, John (1994). Religion, State and Politics in the Soviet Union and Successor States. Cambridge, England: Cambridge University Press. ku. 3. ISBN 0-521-46784-5.
  20. "Anti-religious Campaigns". Loc.gov. Iliwekwa mnamo 2011-09-19.
  21. Country Studies: Russia-The Russian Orthodox Church U.S. Library of Congress, Accessed 2008-04-03
  22. 22.0 22.1 Arena – Atlas of Religions and Nationalities in Russia. Sreda.org
  23. "Nakala iliyohifadhiwa" Пресс выпуски - В России 74% православных и 7% мусульман€ [Press releases - In Russia 74% are Orthodox and 7% are Muslims]. levada.ru (kwa Kirusi). 17 Desemba 2012. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2012-12-31. Iliwekwa mnamo 29 Aprili 2015. {{cite web}}: C1 control character in |script-title= at position 60 (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  24. Ценности: религиозность [Values: Religious]. fom.ru (kwa Kirusi). 14 Juni 2013. Iliwekwa mnamo 29 Aprili 2015.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  25. Сведения о религиозных организациях, зарегистрированных в Российской Федерации по данным Федеральной регистрационной службы [Data about religious organizations registered in Russian Federation according to Federal Migration Service records] (kwa Russian). 19 Desemba 2006. Iliwekwa mnamo 27 Desemba 2007.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link) CS1 maint: unrecognized language (link)
  26. "Russian Federation". Europe: Belarus, Russian Federation and Ukraine. World and Its Peoples. Marshall Cavendish. 2010. uk. 1387. ISBN 978-0-7614-7900-0. Iliwekwa mnamo 29 Aprili 2015.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  27. Ingvar Svanberg; David Westerlund (6 Desemba 2012). Islam Outside the Arab World. Routledge. uk. 418. ISBN 978-1-136-11330-7. Iliwekwa mnamo 29 Aprili 2015.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  28. 2012 Survey Maps Ilihifadhiwa 20 Machi 2017 kwenye Wayback Machine.. "Ogonek", No. 34 (5243), 27 August 2012. Retrieved 24 September 2012.
  29. Richard Hellie. "Russia". Encyclopedia Britannica. Iliwekwa mnamo 29 Aprili 2015.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  30. Zuckerman, P. (2005). "Atheism: Contemporary Rates and Patterns". Katika Michael Martin (mhr.). The Cambridge Companion to Atheism. Cambridge University Press.
  31. Социологи вновь посчитали верующих россиян [Sociologists have counted Russian believers anew] (kwa Russian). Sova Center. 15 Januari 2013. Iliwekwa mnamo 29 Aprili 2013.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link) CS1 maint: unrecognized language (link)

Viungo vya nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Serikali
Vingine
Makala hii kuhusu maeneo ya Urusi bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Urusi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Nchi na maeneo ya Asia

Afghanistan | Armenia2 | Azerbaijan | Bahrain | Bangladesh | Bhutan | Brunei | China | Falme za Kiarabu | Georgia2 | Hong Kong3 | Indonesia | Iraq | Israel | Jamhuri ya China (Taiwan) | Japani | Kamboja | Kazakhstan | Kirgizia | Korea Kaskazini | Korea Kusini | Kupro2 | Kuwait | Laos | Lebanoni | Macau3 | Malaysia | Maldivi | Mongolia | Myanmar | Nepal | Omani | Pakistan | Palestina | Qatar | Saudia | Singapuri | Sri Lanka | Syria | Tajikistan | Timor ya Mashariki | Turkmenistan | Uajemi | Ufilipino | Uhindi | Urusi1 | Uthai | Uturuki1 | Uzbekistan | Vietnam | Yemen | Yordani

1. Nchi ina maeneo katika Asia na Ulaya. 2. Nchi iko Asia lakini inahesabiwa pia kati ya nchi za Ulaya kwa sababu za historia au utamaduni. 3. Eneo la pekee la China.