Krim

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Krim katika Ukraine
Mahali pa Krim (kijani cheusi) katika Ukraine (kijani cheupe) na Ulaya

Krim (Rus. Крым Krym; Ukr. Крим Krim; Kitartari Qırım; ing. Crimea) ni rasi kwenye upande wa kaskazini ya Bahari Nyeusi yenye eneo la 26.100 km². Kisiasa ni jimbo la kujitawala ndani ya nchi ya Ukraine na jina rasmi ni "Jamhuri ya kujitawala ya Krim". Tangu mwaka 2014 ilivamiwa na kutekwa na jeshi la Urusi. Zaidi ya nusu ya wakazi 1.994.300 (mwaka 2005) ni Warusi (58,5 %), takriban robo Waukraine (24,4 %) halafu kuna pia Tartari 243.400 (12,1 %).

Historia[hariri | hariri chanzo]

Rasi hii ina historia ndefu iliyoona mabadiliko mengi kiasi ya kwamba haiwezekani ni nani wanaoweza kuitwa "wakazi asilia" wa nchi hii.

Katika historia inayojulikana Krim ilitawaliwa na Waskithi, Wagiriki wa Kale, Roma ya Kale, Wagothi, Bizanti, Wahunni, Wakhazari, Wamongolia, Waitalia kutoka Venezia na Genua, Watartari, Waosmani, Urusi na tangu 1991 nchi huru ya Ukraine.

Kwa muda mrefu lugha ya mawasiliano ilikuwa Kigiriki hadi kuingia kwa Watartari Waislamu mnamo karne ya 15 walioleta lugha yao ya Kiturki.

Tangu 1783 Krim ilikuwa sehemu ya Milki ya Urusi na Warusi walileta walowezi wengi kutoka kwao. Sehemu ya Watartari walihamia Uturuki. Chini ya utawala wa Kirusi muundo wa wakazi ulibadilika hadi Warusi walikuwa kundi kubwa.

1853 hadi 1856 rasi iliathiriwa vibaya na vita ya Krim ambako jeshi la Waturuki Waosmani pamoja na Uingereza na Ufaransa lilishambulia ngome ya Kirusi ya Sevastopol.

Baada ya kuporomoka kwa Milki ya Urusi mwaka 1917 Watartari walitangaza jamhuri la kujitegemea kwa muda mfupi. Tangu 1918 Krim ilirudishwa Urusi kwa nguvu ya kijeshi na kuwa sehemu ya Shirikisho la Jamhuri ya Kisovyiet ya Kijamii ya Kirusi ndani ya Umoja wa Kisovyeti. Hapa Krim ilikuwa eneo la kujitawala chini ya Urusi. Mwaka 1944, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia Watartari wote walifukuzwa katika Krim kwa amri ya Stalin na kupelekwa sehemu za Asia ya Kati hasa Uzbekistan.

Mwaka 1954 serikali ya Umoja wa Kisovyieti iliamua kuhamisha eneo lote la Krim kutoka jamhuri ya Urusi kwenda Jamhuri ya Kisovyeti ya Kijamii ya Kiukraine. Kuanzia miaka ya 1980 Watartari walianza kurudi Krim kutoka sehemu za Asia ya Kati. Leo hii wako tena na lugha yao inakubalika kama lugha rasmi kimkoa pamoja na Kirusi.

Wakati Umoja wa Kisovyeti iliporomoka mwaka 1991 na Ukraine kuwa nchi huru rasi ya Krim ilikuwa ndani ya Ukraine kwa hali ya "Jamhuri ya kujitawala ya Krim".Baada ya mapindizi ya Ukraine ya mwaka 2014 sehemu ya wakazi wa Krim walikataa mwelekeo mpya wa serikali ya Kiev. Rais wa Urusi Vladimir Putin alitumia nafasi hii kutuma wanajeshi wa Kirusi wasiovaa sare rasmi ndani ya Krim na baada ya kura ya maoni wananchi wengi walipigania kura kujiunga na Urusi. Mwezi wa Machi Urusi ilitangaya eneo la Krim kuwa sehemu ya Shirikisho la Urusi.