Nenda kwa yaliyomo

Peter I wa Urusi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Tsar Peter I wa Urusi

Peter I wa Urusi (au Petro Mkuu) alikuwa Tsar yaani Kaisari wa Urusi. Jina lake la Kirusi lilikuwa Пётр Алексеевич Романов, Pyotr Alekseyevitch Romanov. Alizaliwa tarehe 9 Juni 1672 na kufariki tarehe 8 Februari 1725. Ndiye mtawala aliyeingiza Urusi, iliyokuwa na historia ya Kiasia zaidi, katika siasa na utamaduni wa Ulaya.

Petro Mkuu alianza utawala wake mwaka 1689 akiwa na umri wa miaka 17. Mwanzoni alilenga kuimarisha jeshi la Urusi na hasa wanamaji. Akiona ya kwamba mafundi wote wa kujenga meli walitoka Ulaya, hasa Uholanzi, alifunga safari akakaa Uholanzi na kuwa mfanyakazi wa kujenga jahazi kwa miezi minne.

Aliporudi kutoka safari hii alikuwa na wazo la kwamba nchi yake Urusi ilikuwa nyuma sana kulingana na nchi za Ulaya, hivyo alianza mipango mingi ya kuleta maendeleo Urusi. Aliamuru waungwana wote kwenye jumba la kifalme kukata ndevu zao na kuvaa nguo za Kizungu. Alialika mafundi na wataalamu wengi kutoka Ulaya.

Hasa alianza kujenga mji mkuu mpya kwenye mwambao wa Baltiki, yaani katika pembe la magharibi kabisa la milki yake. Mji huo uliitwa Sankt Peterburg ukachukua nafasi ya Moskva kuanzia mwaka 1712 hadi 1918.

Katika vita mbalimbali alivunja nguvu ya Uswidi na kutwaa majimbo mapya ya Estonia na Latvia.

Alibadilisha pia mfumo wa utawala wa Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi. Aliondoa cheo cha Patriarka (Askofu Mkuu Kabisa) na badala yake aliunda ofisi ya Sinodi Kuu iliyokuwa mkono wa serikali yake.

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Peter I wa Urusi kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.