Nenda kwa yaliyomo

Wachagga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyumba ya asili huko Marangu.

Wachagga[1] ni kabila la watu wenye asili ya Kibantu (lakini pia mchanganyiko wa damu, hasa ya Kikushi) wanaoishi kaskazini mwa Tanzania chini ya mlima Kilimanjaro, mkoani Kilimanjaro.

Wachagga ni kabila la tatu kwa ukubwa nchini Tanzania.[2] Takwimu za mwaka 2003 zinaonyesha kuwa idadi yao ni watu 2,000,000. Hata hivyo kabila hilo ni kama mchanganyiko wa makabila madogomadogo yenye lugha tofauti, jambo la pekee nchini Tanzania.

Shughuli kubwa ya Wachagga ni biashara, kilimo na kazi za ofisini.

Vikundi vya Wachagga

Wachagga wana historia ndefu ya asili yao na ya maingiliano yao na makabila mengine. Kabila la Kichagga ni mkusanyiko wa makabila madogomadogo (ya Kichagga) yaliyosambaa kijiografia kuzunguka mlima Kilimanjaro kuanzia mashariki (Tarakea, Rombo) hadi magharibi kwa Kilimanjaro (Siha, Machame).

Wachaga ni kama vile Wa-Vunjo ambao wanajumuisha watu wa Mwika, Mamba, Marangu, Kilema na Kirua ambayo ndiyo inajulikana na wengi kama Kirua Vunjo. Ukipenda unaweza kuwagawa watu hawa wa Vunjo kufuatana na vijiji hivyo. Wengine ni Wa-Old Moshi, Wa-Kibosho, Wa-Machame, Wa-Uru, na Wa-Siha.

Lugha ya Kichagga

Lugha ya Kichagga inabadilika kuanzia unapotoka Tarakea mpaka unapofika Siha magharibi mlima Kilimanjaro.

Kutokana na tofauti hizo Kichagga kimegawanyika katika Kirombo (ambacho nacho kinatofautiana kadiri unavyotoka eneo moja hadi jingine; mfano Kiseri, Kimashati, Kimkuu, Kimengwe, Kimahida), Kimachame, Kivunjo, Kimarangu, Kioldimoshi, Kingassa, Kiuru, Kikibosho, na Kisiha.

Lugha hizo zinakaribia kufanana kadiri makundi hayo yalivyopakana. Kwa mfano, Kivunjo kinafanana na Kioldimoshi. Vile vile Kisiha kinafanana sana na Kimachame ambacho pia kinafanana kidogo na Kikibosho.

Baadhi ya Wamachame walihamia sehemu za Meru, Arusha, na kuchanganyikana na Waarusha, hivyo lugha yao ikabadilika kidogo na kuwa Kimeru. Kwa sababu hiyo Wameru wanasikilizana sana na Wamachame ingawa lafudhi zao zinatofautiana kidogo.

Koo za Kichagga

Majina ya kiukoo ya Kichagga pia huashiria wanatoka sehemu gani ya Uchaga, japo si lazima kuwa hivyo: kwa mfano, familia maarufu za Kichagga nchini Tanzania ni kama ukoo wa akina Mushi au Moshi, Mmasy, Kimaro, Swai, Massawe, Lema, Urassa, Nkya, Ndosi, Meena n.k.

Akina Temu, Mlaki, Mlay, Lyimo, Moshiro, Mselle, Kamnde, Kileo, Tesha, Msaki, Assey, Kisaka, Mallya, Maembe, Shayo, Kessy, Ndanu, Macha, Mbishi, Moshi, Kombe, Njau, Mlingi, Chaky, Samky, Macha na Kilawe wanatoka Vunjo.

Majina mengine ya Old Moshi ni kama yafuatayo: Saria, Mmari, Macha, Machange, Mshiu, Kyara, Moshi, Massamu, Kimambo, Mboro, Mlngu, Saule, Tenga, Njau, Malisa, Maro, Maeda, Ringo,Olomi, Ngowi, Lyatuu na mengine mengi.

Kavishe, Mrosso, Bongole, Mariki, Moshi, Tarimo, Laswai, Mallya, Mrema, Mkenda, Mushi, Massawe, Silayo, Lyaruu, Makyao, Mowo, Lamtey, Tairo, Masue, Maleto, Mramba, Kauki, Kiwango na Kyauke wanatoka Rombo.

Mchaki, Masawe, Sawe, Usiri, Shayo, Kiwelu, Makundi, Urasa, Mtui, Moshi, Meela, Minja, Njau, Saria, Mtei wanatoka Marangu na Kilema.

Rite, Makule, Minja, Mashayo, Chao, Shao, Makawia, Ndesano, Kimario, Tilla, Mariale, Tarimo, Mafole, Kituo, Mrosso, Lyakundia, Kessy, Mmbando, Matemba, Ndenshau, Morio, Akaro, Matowo, Towo, Mkony, Temba, Foya, Munishi, Kilawe, na kadhalika hutoka Kibosho.

Ukoo wa akina Teri wako Mamba, Chami, Chuwa, Kiria Owoya na wachache Sango, Old Moshi na wengine walihamia Maji ya Chai, Mkoa wa Arusha.

[3]

Utawala wa jadi wa Wachagga

Watawala wa Kichagga waliitwa "Mangi". Akina mangi walihodhi mashamba, ng'ombe na waliheshimiwa kama viongozi wa jadi. Walikuwa na nguvu za kisiasa na utajiri. Baadhi ya Ma-mangi mashuhuri katika historia ni kama Mangi Shangali (wa ukoo wa Mushi) kutoka Machame, Mangi Rindi aliyeingia mikataba na wakoloni (Wajerumani), Mangi Sina wa Kibosho na Mangi Horombo wa Keni - waliojulikana kwa uhodari wao wa vita katika kupigana na Wamachame na kupora ng'ombe na mazao yao, na Mangi Marealle wa Marangu na Vunjo. Mangi Meli alikuwa mangi wa Waoldmoshi ambaye alipigana na Wajerumani na aliishia kukatwa kichwa; mpaka sasa fuvu lake lipo Ujerumani, alizikwa kiwiliwili tu baada ya kunyongwa; mti aliyonyongewa upo mpaka sasa sehemu ya Oldmoshi bomani karibu na Kolila Sekondari. Alinyongwa kwa sababu alikataa kuwa kibaraka wa kutumika na Wajerumani.

Wakoloni walipokuja Kilimanjaro waliingia mikataba na viongozi hao wa kikabila ili kuweza kuweka misingi yao ya kikoloni. Pia ndugu na watoto wa Ma-mangi walikuwa wa kwanza kupata elimu ya kikoloni, kwa hiyo waliweza kushirikishwa katika serikali za kwanza. Hao pia wanaaminika walikuwa kama mabepari wa kwanza wa kijadi, maana walifanyiwa kazi na watu wengine wakati wao wamekaa kuhesabu mali zao. Hii ni desturi ya watawala, hasa wafalme kote ulimwenguni.

Elimu kati ya Wachagga

Wachagga wanajulikana kwa uwezo wao mkubwa katika uwanja wa elimu, hususani katika masomo ya sayansi na hisabati. Moshi ni maeneo ya mwanzo ambayo wamisionari wa Ukristo walijenga makanisa na shule.

Sababu hii imefanya Wachagga kuwa kabila namba moja lenye watu wengi zaidi walio na elimu ya kisasa (elimu ya juu) na mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kwa idadi ya shule za sekondari nchini Tanzania. Kulingana na takwimu za elimu mkoa huo una shule za sekondari zaidi ya 320. Pia mkoa una shule za msingi zipatazo 950. Idadi hii ya shule ni kubwa zaidi ya idadi ya shule katika mikoa mingine Tanzania.

Shule nyingi za sekondari ziko katika mkoa huu kwa sababu zifuatazo:

  1. Hali ya hewa na vivutio vya kitalii katika mkoa huu viliwavutia zaidi walowezi na wakoloni na kuweka makazi yao hapo. Hivyo wamisionari walijenga shule za kwanza wakifuatiliwa na serikali za wakoloni
  2. Serikali ya Tanzania ilirithi shule zilizojengwa na wakoloni
  3. Wachagga waliobahatika kupata fedha binafsi baadaye waliwekeza kwenye ujenzi wa shule binafsi kama kitega-uchumi, wakati wakazi wa mikoa mingine kadhaa walisubiri serikali iwajengee shule.
  4. Ukichanganya sababu 1, 2 & 3 utagundua shule katika mkoa Kilimanjaro zimezidi sana idadi ya shule katika mikoa mingine yote.

Ni vema pia kusema kuwa shule hizo huvutia wanafunzi kutoka Tanzania nzima, haziwasomeshi Wachagga tu.

Ardhi

Ingawa ardhi ni msingi wa maendeleo kwa watu wote, kwa Wachagga, ardhi ni mali sana kwa sababu kilimo chao ni cha mazao ya kudumu kama kahawa na ndizi hukaa shambani kwa muda wa miaka mingi.

Mojawapo ya urithi wapewayo watoto ni "kihamba". Hii ni sehemu ya ardhi ambayo mtoto anategemewa atajenga na kuanzisha familia yake. Bahati mbaya watoto wa kike walikuwa hawapewi kipaumbele katika ugawanaji wa vihamba. Uhaba wa ardhi huko Uchaga ulipelekea Wachagga wengi kuhamia mikoa mingine. Hivi leo utakuta Wachagga wakiishi Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya n.k. wakiwa wamepanda migomba yao na kuendesha biashara za maduka ya vyakula, pamoja na biashara nyingine.

Ukienda kwenye mikoa hiyo utakuta wamejenga jamii zao na vyama vyao vya kusaidiana wakati wa sherehe au matatizo. Aidha hata pombe ya mbege utaweza kuikuta kwenye makusanyiko ya Wachagga katika mikoa mbalimbali.

Kilimo na chakula

Chakula cha Wachagga.

Wachagga hulima mazao ya chakula kama vile mahindi, maharagwe, viazi, ndizi, ulezi na mboga mbalimbali. Pia mazao ya biashara kama vile kahawa, nyanya na vitunguu.

Ndizi za Wachagga na upishi wa samaki

Ingawa Wachagga wa leo wanakula vyakula mbalimbali kama vile ugali, wali na viazi, chakula kikuu cha Wachagga ni ndizi.

Kuna ndizi za aina mbalimbali na kwa matumizi tofauti. Mfano ndizi sukari ni fupi na huachwa hadi ziive na huliwa mbivu kama tunda.

Ndizi mshale hukatwa zikiwa mbichi na kupikiwa vyakula mbalimbali pamoja na nyama ya ng'ombe, kondoo au mbuzi. Mara nyingine hupikwa na maharage, choroko, kunde au hata maziwa ya mtindi. Vyakula vya ndizi huja kwa ladha tofauti kama vile ndizi nyama, mtori, machalari, kiburu na kadhalika.

Aina nyingine ni ndizi ng'ombe ambazo huachwa ziive halafu humenywa na kutumiwa kutengenezea kinywaji maarufu kiitwacho mbege. Mbege hutengenezwa kwa kutumia ndizi mbivu, maji, na ulezi.

Aina nyingine ni ndizi mzuzu. Hizi zikikomaa huachwa zianze kuiva kidogo halafu huchomwa na kuliwa kama kitafunwa pamoja na chai au kinywaji kingine. Ukipita mitaa ya Dar es Salaam utaona ndizi mzuzu zikichomwa sambamba na muhogo au kuku vumbi au kiti moto.

Wachagga na muhogo

Inasemekana kuwa "Mchagga halisi hali muhogo - akila muhogo atakufa". Usemi huu umetokana na historia ya mababu kuwa Wachagga waliopanda mihogo Kilimanjaro enzi za kale walikufa baada ya kuila. Historia hiyo yaweza kuwa ya ukweli kwa sababu aina nyingi za mihogo zinajenga sumu ya sianidi ndani yake; watu waliozoea kutumia mihogo huwa na njia za kuondoa sumu kwa kuiloweka mihogo katika maji kwa muda. Lakini kama Wachagga wale wa zamani, hasa wa Machame, walifanya jaribio bila kujua mbinu ya kuondoa sumu, ajali iliweza kutokea. Cha kushangaza ni kwamba hukohuko Kilimanjaro, majirani na watani wa Wachagga, yaani Wapare, walikuwa wameshazoea mihogo na ilikuja kuwa moja ya chakula chao kikuu.

Ulaji kiti-moto

Pamoja na kilimo cha mazao, Wachagga hupendelea sana kufuga nguruwe kwa ajili ya biashara kwani nyama ya nguruwe hupendwa sana na watu na huuzwa sana kwenye baa na hoteli mbalimbali mijini hasa katika jiji la Dar es Salaam. Tabia ya kula nyama ya nguruwe ijulikanayo leo kwa jina la "kiti moto" ni moja ya mambo yaliyoenezwa na Wachagga. Ulaji wa "kiti moto" haukuwapendeza baadhi ya wenyeji wa Pwani na Dar es Salaam ambapo Wachagga walihamia, kwani wengi wao ni Waislamu, kwa hiyo nguruwe kwao ni haramu. Wakazi wa Dar es Salaam watokao makabila mengine na wasio Waislamu kwao kula nguruwe ilikuwa "ruksa".

Maoni juu ya Wachagga

Kipato cha Wachagga ni kikubwa kulingana na cha makabila mengine.

Wanawake wa Kichagga (hasa kutoka Machame) hujulikana kama wafanyakazi hodari. Huchangia sana katika mapato ya nyumbani na chakula. Mama wa Kichagga anaweza kushinda shambani kutwa na hana desturi ya kubeba watoto mgongoni kwenda nao shambani, hivyo wanakuwa nyumbani na mayaya au peke yao. Mfano ulio dhahiri ni nyakati za asubuhi na mapema kwenye vyombo vya usafiri karibu robo tatu ya abiria ni wanawake wakienda katika shuguli za biashara na kilimo na vivyo hivyo nyakati za jioni wakirudi majumbani. Hao ni nje ya wale wanaotumia usafiri wa miguu ambao ni wengi zaidi.

Ingawa wanaume wa Kichagga hupendelea kufanya kazi mbali na kwao, wake zao hukaa nyumbani (Kilimanjaro) kufuga ng'ombe na kufanya kazi za shambani. Kwa sasa kutokana na ugonjwa wa ukimwi tabia hii imepungua miongoni mwao.

Pia baadhi ya kina mama wa Kichaga wanawajali waume zao zaidi kwani nyama nzuri ni ya baba. Ili kuepuka gharama baba ataandaliwa chakula kizuri, tofauti na chakula walichoandaliwa watoto, japo ni chakula kilekile.

Pia Wachagga wamekuwa na desturi ya kuwaenzi wazee wao waliotangulia mbele za haki kwa kuwatambikia kwa pombe na nyama za mbuzi pale tu wanaporudi nyumbani mwezi Desemba. Hilo limekuwa suala la kawaida sana. Wengi wao huwa wanarudi na magari, ndiyo sababu utaona ya kwamba kila mwaka ufikapo mwezi Desemba foleni za magari zimekuwa zikiongezeka katika mji wa Moshi kutokana na Wachagga kurudi nyumbani msimu wa sikukuu. Wengi wao wamekuwa wakitoka sehemu mbalimbali za nchi na hata nje ya nchi.

Wachagga wengi hupenda kurudi nyumbani kipindi cha Krismasi, ikiwa ni kuwatembelea wazazi wao, rafiki, au ndugu. Pia imekuwa kama desturi wanaukoo kukaa pamoja na kujadiliana mambo jinsi yalivyokwenda katika kipindi kizima cha mwaka na wakati mwingine inakuwa sehemu ya kwenda kuwatambulisha watoto kwa bibi na babu zao, hasa wale waliozaliwa mijini. Ni kipindi chenye shangwe na furaha sana: hakuna kaya utakayokuta haina furaha kwa sababu hata kama huna sherehe kuna mialiko mbalimbali ambao haihitaji kadi au michango.

Ingawa wengi hudhani kwamba Wachagga wamepokea sana dini (imani) ya Ukristo kwa kuwa wengi wao ni Wakristo na hiki huwa kipindi cha likizo kwao, inaaminika pia kuwa kurudi kwao wakati wa Krismasi ni pamoja na kutembelea ndugu zao na kujumuika pamoja katika kuumaliza mwaka baada ya kazi nyingi za kutafuta pesa mwaka mzima.

Sababu kuu za Wachaga wengi kwenda kwao mwisho wa mwaka

  1. Kupumzika, hii ni baada ya kufanya kazi kwa mwaka mzima bila kwenda, biashara asubuhi, jioni mahesabu, kwao Desemba ni mwezi wa kutulia tu na familia ndugu na jamaa
  2. Kuchinja mbuzi, hapa kuna za matambiko na za kula na kufurahia tu. Matambiko hayo ni kushukuru wazee wao waliokufa mapema kwa baraka walizopata kwa kipindi chote cha mwaka mzima
  3. Sherehe mbalimbali: sherehe za wafu, maadhimisho ya ndoa mbalimbali, Krismasi, Ubatizo, Kipaimara, Komunyo, kutoa watoto jandoni na Mwaka mpya wenyewe. Kila inayoitwa sherehe hufanyika kipindi hiki, kuanzia tarehe 25 Desemba kufika tarehe 1 Januari ni shughuli tu, kula kunywa kusaza.
  4. Utambulisho mbalimbali kwa wazee, jamaa wa nyumbani kama vile mke, mchumba, mume, gari jipya, nyumba mpya, watoto n.k.
  5. Kukutana na watu mbalimbali ambao hamuonani baada ya kipindi hicho kama, marafiki, majirani, ndugu na jamaa. Hii ni kwa wale wanaofanya kazi mikoa tofauti (huyu Morogoro yule Mwanza mwingine katoka Dar es Salaam)
  6. Utekelezaji wa miradi mbalimbali hapo nyumbani kama ujenzi au ukarabati wa nyumba, njia pana za magari na kukagua mashamba n.k.

Si wote wanakwenda kwa sababu hizo zote bali lazima sababu mojawapo ihusike.

Kutokana na sababu hizo wanaokwenda ni watu wote wa dini zote. Ukienda tofauti na kipindi hiki huwezi kukuta watu wengi sana. Kwanza baada ya kipindi hicho kupita kila mtu anashughulika na mambo yake (kutafuta pesa).

Kama umekwenda na huna chochote, utakumbana na ubaguzi na manyanyaso makubwa.[4]

Tanbihi

  1. The term "Dschagga" appears to have been first used to refer to a location rather than a group of people. Johannes Rebmann refers to "the inhabitants of the Dschagga" while describing the Taita and Kamba peoples on his first trip to the mountain. It appears that "Dschagga" was the general name given to the entire mountainous region by distant residents who had cause to describe it, and that when the European traveler arrived there, his Swahili guide used "Dischagga" to describe other portions to him in general rather than giving him specific names. For instance, Rebmann on his second and third journeys from Kilema to Machame speaks of "going to Dschagga" from Kilema. The word was anglicized to "Jagga" by 1860 and to "Chagga" by 1871. Because it used to be thought of by Swahillis as a perilous area to visit, Charles New chose the latter spelling and identified it as a Swahili name that meant "to stray" or "to get lost." This was beacuase of the dense forest around the mountain that confused visitors when they entered.
  2. Levinson, David (5 Julai 1998). Ethnic Groups Worldwide: A Ready Reference Handbook. Oryx Press. ISBN 9781573560191 – kutoka Google Books.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. MAJINA YA KOO ZA KICHAGA KWA UJUMLA 1.Mushi au Moshi 2.Kimaro 3.Swai 4.Massawe 5.Lema 6.Urassa 7.Nkya 8.Ndoshi 9.Meena 10.Meela 11.Temu 12.Mlaki 13.Mlay 14.Lyimo 15.Moshiro 13.Matiri 16.Mselle 17.Kamnde 18.Kileo 19.Kishimbo 20.Tesha 21.Msaki 22.Assey 23.Kyara 24.Kessy 25.Ndanu 26.Macha 27.Mbishi 28.Mbasha 29.Kombe 30.Njau 32.Mmari 33.Mshiu 34.Massamu 35.Kimambo 36.Mboro 37.Mlingu 38.Tenga 39.Mtenga 40.Malisa 41.Maro 42.Muro 43.Maeda 44.Ngowi 45.Lyatuu 45.Salema 46.Lyakurwa 47.Lyaruwa 48.Lyaruu 49.Lyakunda 50.Kawiche 51.Kavishe 52.Kawau 53.Tarimo 54.Lasway 55.Lamtey 56.Mtey au Mtei 57.Mallya 58.Mrema 59.Mremi 60.Mkenda 61.Silayo 62.Makyao 63.Mowo 64.Tairo 65.Mramba 66.Kauki 67.Sawe 68.Usiri 69.Shayo 70.Kiwelu 71.Makundi 72.Mtui 73.Minja 74.Rite 75.Ramale 76.Makule 77.Massae 78.Mashayo 79.Chao 80.Shao 80.Chonjo 81.Makawia 82.Massenge 83.Kimario 84.Tilla 84.Mariale 85.Mafole 86.Kituo 87.Kitomari 88.Mrosso 89.Mbando 90.Matemba 91.Munuo 92.Mono 93.Monyo 94.Akaro 95.Kanje 96.Uisso 97.Woisso au Wisso 98.Oisso 98.Mwanga 99.Matowo 100.Towo 101.Mkonyi 102.Temba 103.Foya 104.Munishi 105.Kilawe 106.Teri 107.Chami 108.Chuwa 109.Kiria 110.Owoya 111.Mongi 112.Shirima 113.Mosha 114.Mboya 115.Mbowe 116.Mbuya 117.Mateo 118.Saleko 119.Mrina 120.Lyamuya 121.Mshanga 122.Mamuya 123.Assenga 124.Nyaki 125.Urio 126.Mero 127.Marandu 128.Riwa 129.Mariki 130.Ulomi au Olomi 131.Ngowo 132.Manyanga 133.Mariwa 134.Saritta 135.Kowero 136.Makoi 137.Lekule 138.Kaale 140.Mbatia 141.Kyisima 142.Matei 143.Materu 144.Ngomuo 145.Mengi 145.Kamasho 146.Mkaro 147.Kiwoli 148.Msaki 145.Kihundwa 146.Natai 147.Mambo 148.Nyange 149.Kissaka 150.Massao 151.Hamaro 152.Mng’anya 153.Mangale 154.Njuu 155.Mambali 156.Kilenga 157.Saria 158.Olotu 159.Senguo 160.Mosile 160.Mandari 161.Kwayu 162.Kinyaha 163.Kisanga 164.Mringo 165.Mawala 166.Mghase 167.Mwase 168.Mangia 169.Silemu 170.Mlang’a 171.Masue 172.Mangesho 173.Kinyaiya 174.Ngoli 175.Nkini 176.Rimoi 177.Teti 178.Machangu 179.Mossile 180.Marua 181.Mria 183.Komu 182.Kinyaha 182.Mghase 183.Mwase 184.Mangia 185.Kitali 186.Kweka 187.Kilawe 188.Matesha 189.Matowo 190.Manjuu 200.Mashayo 201.Mashao 202.Machao 204.Mosha 203.Ikamba 204.Hamaro 205.Mleo 206.Rimoy 207.Pacho 208.Tilya 209.Meena 210.Meela 211.Kway 212.Keenja 213.Kimei 214.Maleo 215.Salema 216.Malekia 217.Matemba 218.Matesha 219.Mamasawe 220.Mashirima 221.Maswai 222.Makavishe 223.Makawiche 224.Makanje 225.masaritta 226.Makimario 227.Masalema 228.Masilayo 229.Mamrema 230.Maramale 231.Masilemu 232.Machao 233.Mashao 234.Makimambo 235.Meli 236.Matiri 237.Matari 238.Mashayo 239.Mamroso 240.Malyimo 241.Matesha 242.Makawishe 243.Mamongi 244.Mamoshii 245.Makimambo 246.Makimaro 247.Mameela 248.Mameena 249.Malema 250.Mamengi 251.Masalema 252.Masilemu 253.Makiwoli 252.Maolotu 253.Maurassa 254.Mankya 255.Mandanu 256.Mamramba 257.Matairo 258.Mamonyo 259.Mandanu 260.Makituo 261.Makimambo 262.Makiwoli 263.Mangesho 264.Mamonyo 265.Maoisso 266.makinyaiya 267.Makitali 268.Mamangia 269.Mamlay 270.Matemu 271.Makishimbo 272.Mamatiri 273.Mambasha 274.Maurio 275.Mamtenga 274.Mamalisa 275.Matenga 276.Makamnde 277.Mamsele 278.Manjau 279.Mamsaki 280.Makileo 281.Mafoya 282.Mamunishi 283.Mamkenda 284.Mamacha 285.Mambishi 286.Mandoshi 287.Mamoshiro 288.Makombe 289.Mammari 289.Manjuu 290.Mamosile 291.Miku 292.Kishimbo 293.Kilawe 294.Shangali 295.Kitefure 296.Shiletikwa 297.Mramu 298.Kishewo 299.Mrang'u 300.Kireti 301.Kereti 302.Kimati 303.Shikonyi 304.Komu 305.Mafole 306.Konyanga 307.Mamboro 308.Horombo 309.Sekei 310.Ndeuka 311.Lesuo 312.Kway 313.Shio 314.Ngowi 315.Makupa 314.Matiro 315.Mangalu 316.Katembo 317.Mahoo 318.Mola 319.Chaki 320.Masecha 321.Mchau
  4. "Hizi ndizo Shughuli zinazowapeleka wachagga Kilimanjaro kila mwaka".

Marejeo

  • Ehret, Christopher (2002). The Civilizations of Africa. University of Virginia Press. ISBN 0-8139-2085-X.
  • Gray, R (1975). The Cambridge History of Africa. Cambridge University Press. ISBN 0-521-20413-5.
  • Fasi, M El (1992). Africa from the Seventh to the Eleventh Century. University of California Press. ISBN 0-520-06698-7.
  • Johnson, H.H (1886). "Copyright: Tubner & Co". Journal of the Royal Anthropological Institute of Great Britain and Ireland. XV: 12–14.
  • Yakan, Mohamad A (1999). Almanac of African Peoples & Nations. Transaction Publishers. ISBN 1-56000-433-9.
  • P. H. Gulliver (1969). Tradition and Transition in East Africa: Studies of the Tribal Element in the Modern Era. University of California Berkeley.

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wachagga kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.