Nenda kwa yaliyomo

Bikira Maria

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Bibi Maryam)
Ukuu wa Bikira Maria unamtegemea Mwanae, Yesu.
Stabat Mater, yaani picha ya Bikira Maria chini ya msalaba wa Yesu, kadiri ya Gentile wa Fabriano, 1410-1412 hivi.
Mfululizo wa kurasa juu ya Yesu
Yesu
Yesu Kristo na Ukristo

Umwilisho  • Utoto wa Yesu  • Ubatizo
Arusi ya Kana • Utume wa Yesu • Mifano ya Yesu  • Miujiza ya Yesu
Kugeuka sura • Karamu ya mwisho • Msalaba wa Yesu  • Maneno saba
Kifo cha Yesu  • Ufufuko wa Yesu
Kupaa mbinguni  • Ujio wa pili
Injili  • Majina ya Yesu katika Agano Jipya  • Yesu kadiri ya historia  • Tarehe za maisha ya Yesu • Kristolojia

Mazingira ya Yesu

Wayahudi • Kiaramu • Bikira Maria • Yosefu (mume wa Maria) • Familia takatifu • Ukoo wa Yesu • Ndugu wa Yesu • Yohane Mbatizaji

Mitazamo juu ya Yesu

Mitazamo katika Agano Jipya · Mitazamo ya Kikristo • Mitazamo ya Kiyahudi • Mitazamo ya Kiislamu • Yesu katika sanaa

Maria alikuwa mwanamke Myahudi aliyeishi kati ya karne ya 1 KK na karne ya 1 BK. Mke wa Yosefu, alimzaa Yesu Kristo.

Kwa sababu hiyo na kwa utakatifu wake anapewa heshima ya pekee katika madhehebu mengi ya Ukristo, lakini pia katika Uislamu.

Jina asili kwa Kiaramu ni מרים, Maryām lenye maana ya "Bibi"; watafsiri wa kwanza wa Biblia ya Kiebrania wanaojulikana kama Septuaginta (LXX) waliliacha kama lilivyo wakiandika kwa Kigiriki Μαρίαμ, Mariam, au walilifupisha wakiandika Μαρία, Maria.

Katika Kurani jina hilo kwa Kiarabu ni مريم, Maryam.

Jina hilo limeenea sana duniani kote, hasa kwa heshima ya mama wa Yesu.

Mwenyewe anatajwa kwa kawaida kwa kutanguliza sifa yake mojawapo, hasa Bikira.

Mapokeo ya karne ya 2 (Injili ya Yakobo) kuhusu Bikira Maria yanasema alikuwa binti pekee wa Yohakimu na Ana. Lakini habari muhimu zaidi ni zile zinazopatikana katika Biblia ya Kikristo.

Bikira Maria katika Biblia

[hariri | hariri chanzo]

Biblia inashuhudia kuwa umuhimu wa watu unatofautiana

[hariri | hariri chanzo]

Maandiko matakatifu yanawasifu watu mbalimbali kutokana na jinsi walivyomuamini Mungu na kutenda makuu kwa ajili ya taifa lake.

Abrahamu alimuamini Mungu akawa tayari kumtolea sadaka mwanae Isaka, tukio lililomfanya apate baraka ya pekee ya kuwa baba wa waamini (Mwa 22:15-18).

Yosefu, mwana mpenzi wa Yakobo-Israeli, alikuwa mwaminifu hata akaliokoa taifa lisiangamie kwa njaa (Mwa 50:20).

Musa ndiye mkombozi wa taifa la Mungu katika Agano la Kale: aliongoza Israeli kutoka utumwani Misri akalipatia sheria kutoka kwa Mungu katika mlima Sinai. Maandiko ya Agano la Kale yanakiri, “Wala hajainuka kiongozi kama alivyokuwa Musa” (Kumb 34:10-12).

Waliofuata ni Yoshua, Debora, Gideoni, Ruthu, Samweli, wafalme Daudi na Solomoni, manabii Eliya, Isaya, Yeremia, Ezekieli na wengineo.

Mwishoni Yesu Kristo akamsifu Yohane Mbatizaji akisema, “Ni mkuu kati ya uzao wa wanawake” (Lk 7:24-28).

Elizabeti, mama wa Yohane, alijiona hastahili kutembelewa na Bikira Maria, Mama wa Yesu, akamuita, “Mama wa Bwana wangu” (Lk 1:43).

Bikira Maria si mtu wa ziada katika mpango wa Mungu bali ni mshiriki mkuu wa ukombozi wa binadamu. Maria amechangia wokovu kwa kukubali mpango wote wa Mungu aliyetaka amzae Mwanae, amlee na kumfuata kiaminifu hadi msalabani, aliposhiriki kumtoa kama sadaka ya kutuokoa. Msimamo wake ulikuwa mmoja tu: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema” (Lk 1:38).

Tukichunguza nafasi yake katika fumbo hilo, tunaweza kukiri pamoja naye kuwa ni Mwenyezi Mungu aliyemtendea makuu (Lk 1:49), kwa kuwa, “Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu” (Yoh 3:27).

Yale yote ambayo Wakristo wengi wanayasadiki kuhusu Bikira Maria, hakujipatia bali alijaliwa na Mwenyezi Mungu huku akiitikia kwa hiari fumbo la mpango wake.

Utabiri kuhusu Bikira Maria

[hariri | hariri chanzo]

Biblia inatupatia utabiri uliotolewa na Mungu mwanzoni mwa historia kuhusu mwanamke atakayemshinda nyoka wa kale (Shetani): “Nitaweka uadui kati yako na huyu mwanamke, kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa chako” (Mwa 3:15). Juu ya [[Eva wa kale, ambaye alidanganywa na kuangushwa na Shetani atende dhambi, imesemwa: “Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa, kwa kuwa ndiye aliye Mama wa walio hai” (Mwa 3:20). Hata hivyo Adamu na Eva wa kale wametuletea kifo (Rom 5:12). Mababu wa Kanisa wanamtazama Bikira Maria kama Eva mpya aliyemshinda Ibilisi na kuwa mama wa wote walio hai. Yesu, aliye Adamu mpya, alipokuwa anakamilisha sadaka ya ukombozi pale msalabani alimfanya Mama yake awe Mama wa waliokombolewa kwa kumkabidhi mwanafunzi, tena yule aliyempenda zaidi. “Penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Kleopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, “Mama, tazama, mwanao”. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama, mama yako”. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake. (Yoh 19:26-27).

Utabiri mwingine ulisema, “Tazama Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamuita jina lake Emanueli, yaani Mungu pamoja nasi” (Isa 7:14). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:34-35, “Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu akakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli. Kwa sababu hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu”. “Imba, ee binti Sion, piga kelele, ee Israeli, furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti Yerusalemu. Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana yu katikati yako” (Sef 3:14-15). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:28: “Malaika akaingia nyumbani mwake akamwambia, ‘Furahi Maria, umejaliwa neema kubwa, Bwana yu pamoja nawe’”. “Umebarikiwa wewe katika kila hema la Yuda na katika kila taifa, nao wanaposikia jina lako watafadhaika. Imani yako haitatoka mioyoni mwa watu wanaoukumbuka uweza wa Mungu milele” (Yudithi 14:7; 15:9). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:42, “Akapaza sauti kwa nguvu akasema, ‘Umebarikiwa wewe kuliko wanawake wote, na yeye utakayemzaa amebarikiwa’”.

Bikira Maria ni fumbo la ajabu alilolifanya Mungu katika mpango wa wokovu kwa ajili yake na kwa ajili yetu. Jamaa yake Elizabeti alimpongeza tena akiongozwa na Roho Mtakatifu, “Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale uliyoambiwa na Bwana” (Lk 1:45).

Hivyo manabii mbalimbali kwa mwanga wa Roho Mtakatifu walimuagua Maria kwa heshima. Mambo yaliyotabiriwa katika Agano la Kale yalitimia katika Agano Jipya: ukombozi ulianza Bikira Maria alipokubali kwa imani fumbo la umwilisho wa Mwana wa Mungu. Bikira Maria hakuwa “chombo” tu kilichotumika bila ya kuelewa, bali alikuwa mshiriki huru wa kazi ya ukombozi ya Mwanae, kwa kuwa alipopashwa habari na malaika alikubali kwa hiari mpango wa Mungu akisema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyonena” (Lk 1:38).

Bikira Maria katika maisha ya Yesu

[hariri | hariri chanzo]

Yesu, kama mtu yeyote mcha Mungu, aliwaheshimu na kuwatii wazee wake: “Basi, akarudi pamoja nao Nazareti, akawa anawatii” (Lk 2:51).

Ishara ya kwanza kwenye maisha ya hadhara ya Yesu iliongozwa na Bikira Maria katika arusi ya Kana ya Galilaya, akisukumwa na huruma kwa wenye shida: kwa ombi lake Yesu aligeuza maji kuwa divai, na wanafunzi wake wakamwamini. Yohane alisimulia hivi, “Siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, ‘Hawana divai’. Yesu akamwambia, ‘Mama tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia’. Mamaye akawaambia watumishi, ‘Lo lote atakalowaambia, fanyeni’. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, ‘Jalizeni mabalasi maji’. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, ‘Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza’. Wakapelekea. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maj), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, ‘Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa’. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini. (Yoh 2:1-12).

Bikira Maria anasifiwa kwanza kwa imani yake kuu kabisa, kuliko kwa kumchukua Yesu tumboni tu. Yesu alitaka kuwainua wasikilizaji wake wafuate mambo ya roho kuliko ya mwili. “Basi, mtu mmoja akamwambia, ‘Mama yako na ndugu zako wako nje, wataka kusema nawe’. Lakini Yesu akamjibu huyo mtu aliyemwambia hivyo, ‘Mama yangu ni nani, na ndugu zangu ni akina nani?’ Kisha akanyosha mkono wake juu ya wanafunzi wake akasema, ‘Hawa ndio Mama yangu na ndugu zangu, maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye kaka yangu na dada yangu na mama yangu’” (Math 12:46-50). Vilevile, wakati wa utume wake, alimsikia “mwanamke mmoja katika lile kundi la watu akisema, ‘Hongera kwa mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha’. Yesu akamjibu, ‘Barabara, lakini heri yake zaidi yule anayelisikia Neno la Mungu na kulishika’” (Mk 11:27-28).

Bikira Maria alivyoshiriki Mateso ya Yesu

[hariri | hariri chanzo]

Katika kumfuata Mwanae Bikira Maria alitabiriwa wazi na mzee Simeoni uchungu kama upanga utakaopenya moyo wake, “Tazama huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe uchungu ulio kama upanga utauchoma moyo wako” (Lk 2:34-35).

Bikira Maria alishiriki kwanza mateso ya ukimbizi huko Misri kwa lengo la kumficha Mwanae asiuawe na Herode Mkuu, “Hivyo Yosefu aliamka akamchukua mtoto pamoja na Mama yake akaondoka usiku akaenda Misri akakaa huko mpaka Herode alipokufa” (Math 2:14-15).

Bikira Maria alishuhudia hatua kwa hatua kuteswa kwa Yesu; wanafunzi walipokimbia au kumtazama kwa mbali, yeye alikuwa karibu akaona vema kila teso lililompata Mwanae. Kutokana na fungamano la upendo wa ajabu lililokuwepo kati ya Yesu na Mamaye, alipoyashuhudia yote aliteseka sana katika moyo wake safi, kiasi kwamba Bernardo wa Klervoo akasema, “Msalaba wa Yesu uliwasulubisha wote wawili, Yesu mwilini na Mama yake moyoni”. Uaguzi wa mzee Simeoni ulitimia hivyo.

Kadiri ya mtume Paulo kuteseka ni kutimiliza yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya Kanisa, “Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo” (Kol 1:24). “... maana tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake” (Rom 8:17b).

Pale msalabani Bikira Maria, kwa njia ya mtume Yohane alifanywa Mama wa wote wanaompenda Mwanae; kisha kumzaa pasipo uchungu Bwana wa uzima, pale alituzaa sisi kwa uchungu wa kutisha uliotokana na kumuona Mwanae akifa msalabani. Hata hivyo Bikira Maria aliendelea kumuamini Mwanae aliyeonekana ameshindwa.

Bikira Maria baada ya kifo cha Yesu

[hariri | hariri chanzo]

Bikira Maria alikuwepo hapo mwanzo wa Kanisa, akilivutia zaidi Roho Mtakatifu kwa sala yake. “Hao wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria Mama yake Yesu na ndugu zake” (Mdo 1:14).

Yesu alisema, “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili, lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote” (Yoh 16:12-13). Kwa msaada wa Roho Mtakatifu heshima kwa Bikira Maria ilienea katika Kanisa lote tangu zamani kabisa kadiri ya utabiri wake kuwa ataheshimiwa na vizazi vyote, “Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mdogo, hivyo tangu sasa vizazi vyote wataniita mwenye heri” (Lk 1:48).

Dogma za Kanisa Katoliki kuhusu Bikira Maria

[hariri | hariri chanzo]

Kuna mafundisho makuu manne kumhusu Bikira Maria ambayo ni lazima kila Mkatoliki ayasadiki kutokana na ufunuo wa Mungu:

  1. B. Maria mkingiwa dhambi ya asili
  2. B. Maria Mama wa Mungu
  3. B. Maria Bikira daima
  4. B. Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho

Mkingiwa Dhambi ya Asili

[hariri | hariri chanzo]

Malaika alimsalimia Maria “umejaa neema” (Lk 1:28) maana ndiye tunda bora la ukombozi ulioletwa na Yesu. Ni imani ya Wakatoliki kwamba kwa stahili za Mwanae alikingiwa asirithi kwa wazazi dhambi ya asili na madonda yanayotokana nayo, wala asitende dhambi maisha yake yote. Kwa maneno mengine, Bikira Maria tangu atungwe mimba Mungu alimkinga na kila doa la dhambi kwa kutazamia stahili za Yesu Kristo aliye Mkombozi wa binadamu wote. Maria ndiye aliyekombolewa kwa namna bora kushinda viungo vyote vya Kanisa. Maisha yake yote hakutenda dhambi hata moja. Mapokeo ya mashariki yanamuita “A Panagia” = “Mtakatifu tu”. Dogma hiyo ilitangazwa na papa Pius IX mwaka 1854, halafu mwaka 1858 Bikira Maria alijitambulisha kama Mkingiwa kwa Bernadeta Soubirous huko Lurdi (Ufaransa) kadiri ya njozi zilizokubaliwa na Kanisa hilo. Tena waumini wake wanaelekezwa kuamini kwamba mwaka 1917 huko Fatima (Ureno) aliwafunulia Lusia, Fransisko na Yasinta Marto moyo wake safi usio na doa.

Mama wa Mungu

[hariri | hariri chanzo]

Injili ya Yohane inaanza kwa kishindo, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” (Yoh 1:1). Huyo Mungu Mwana alitwaa ubinadamu katika Bikira Maria akazaliwa mtoto, jina lake Yesu, maana yake Mungu Mwokozi. Huyo ni binadamu kama sisi katika yote isipokuwa dhambi. Ubinadamu wa Yesu unategemea Nafsi yake ya Kimungu: akisema, ‘Mimi’, ni kwa Nafsi yake hiyo. Ndiyo maana aliwaambia Wayahudi, “Kweli nawaambia, kabla Abrahamu hajazaliwa, nalikuwepo” (Yoh 8:50). “Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai” (Yoh 5:26).

Mtume Paulo akaeleza, “Wakati maalumu ulipotimia Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4). Bikira Maria ni Mama wa Mungu kwanzia wakati huo: tangu Bikira Maria alipojaliwa kumchukua mimba, kumzaa, kumnyonyesha na kumlea mtu ambaye kwa asili ni Mungu. Cheo hicho kimemuinua juu kuliko hata malaika. “Malaika alimwambia, ‘Hicho kitakachozaliwa kitaitwa Kitakatifu, Mwana wa Mungu’” (Lk 1:35).

Dogma ilitangazwa mwaka 431 kwenye Mtaguso wa Efeso uliomuita “Mzazi wa Mungu”, ukisema Maria anastahili kuitwa hivyo kwa sababu Mwana wa milele wa Mungu, ambaye ni Mungu sawa na Baba, alifanyika mtu toka kwake. Akiwa mja mzito alishangiliwa: “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” (Lk 1:42-43). Ungamo hilo la Elizabeti likakamilishwa na Mtume Thoma aliyemuambia Yesu mfufuka: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yoh 20:28).

Bikira na Mama

[hariri | hariri chanzo]

Wakristo na Waislamu wote wanakiri kuwa Yesu alitungwa bila ya mchango wa mwanamume. La ajabu zaidi katika imani hiyo ni kwamba hata uzazi wenyewe haukuondoa ubikira wake, bali uliutakasa: ni Bikira daima. Ingawa akili inasita, ni lazima kukiri na malaika, “Hakuna lisilowezekana kwa Mungu” (Lk 1:38). Yosefu, ingawa kisheria alikuwa mume wake, hakutenda naye tendo la ndoa.

Ni imani ya Wakatoliki na Waorthodoksi kuwa Mama wa Yesu anastahili kuitwa “Bikira daima” kwa sababu alimchukua mimba akiwa bikira, akamzaa bila ya kupotewa na ubikira, akabaki bikira hadi mwisho wa maisha yake. Hamu yake ya kuwa bikira hata kisha kuchumbiwa inajitokeza katika jibu alilompa malaika aliyemtabiria mimba: “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?” (Lk 1:35). Ni kielelezo cha Wakristo ambao Mtume Paulo aliwaandikia: “Nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi” (2Kor 11:2), “mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine” (1Kor 7:35).

Wanaosemwa katika Injili “ndugu zake Yesu” si watoto wa Bikira Maria, bali ndugu wa ukoo waliokuwa jirani sana na familia hiyo takatifu. Kama Bikira Maria angekuwa na watoto wengine, Yesu angekuwa amefanya kosa la kuwanyang’anya Mama yao na kumfanya awe Mama wa mtume Yohane alipomkabidhi msalabani, “‘Mwana, tazama Mama yako’. Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake” (Yoh 19:27).

Katika Agano Jipya yupo Yakobo anayeitwa na mtume Paulo “ndugu yake Bwana” (Gal 1:19): Yakobo huyo alikuwa maarufu katika Kanisa la Yerusalemu (Mdo 12:7; 15:13-21; 21:18-20; Gal 2:9). Yakobo huyo si mtume Yakobo kaka yake Yohane (Lk 6:12-16), bali ni Yakobo ndugu yake Yose na mama yao kwenye Injili anaitwa “Maria mwingine”, si Maria Mama wa Yesu. “Walikuwepo pia wanawake waliotazama kwa mbali. Miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose” (Mk 15:40). Maria lilikuwa jina la kawaida kwa Wayahudi: akina Maria wakiwa wengi hivyo, tujue kuwatofautisha kwenye Injili, ambazo zinamtaja Bikira Maria kama “Mama wa Yesu”.

Kupalizwa Mbinguni mwili na roho

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya maisha haya ya duniani Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho, ishara ya mwanamke mshindi. “Ishara kubwa ikaonekana mbinguni, ambapo mwanamke aliyevikwa jua, pia na mwezi chini ya miguu yake, na taji la nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake” (Ufu 12:1). Maneno ya shangilio lake yametimia: Mungu “amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza” (Lk 1:52).

Imani hiyo ya mapokeo ya kale, yanavyoshuhudiwa na Mababu wa Kanisa, ilitangazwa rasmi na Papa Pius XII kwa niaba ya maaskofu wote mwaka 1950.

Heshima za Liturujia ya Kiroma kwa Maria

[hariri | hariri chanzo]

Katika liturujia ya Roma, mbali ya kumtaja Mama Bikira Maria katika kila Misa wakati wa sala ya ekaristi, kuna maadhimisho kwa heshima yake. Hapa yamepangwa kulingana na kiwango cha heshima hiyo:

  • 8 Desemba – Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
  • 1 Januari – Bikira Maria Mama wa Mungu
  • 25 Machi – Bikira Maria Kupashwa Habari
  • 15 Agosti – Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni

Tena kila Jumamosi isiyo na adhimisho maalumu, Kanisa huadhimisha kumbukumbu ya hiari ya Mama wa Mungu.

Pia zipo heshima za binafsi kwa Bikira Maria: mashariki zinatumika tenzi na nyimbo mbalimbali, k.mf. Akatistos inayomuita “daraja linalounganisha dunia na mbingu”, “ngazi aliyoiona Yakobo” “kina kisichochunguzika kwa macho ya malaika” (Mwa 28:12); magharibi anaheshimiwa kwa rozari.

Wakristo wanaomheshimu Bikira Maria hawamuabudu hata kidogo, lakini wanamtolea heshima ya juu kuliko watakatifu wengine. Tofauti ni kwamba Mungu tu anastahili kuabudiwa (kwa Kigiriki, ‘latria’) watakatifu wanapewa heshima (‘dulia’) na Bikira Maria heshima zaidi (‘yuper-dulia’). Kanisa Katoliki linakiri neema zote za Mungu zinampitia Maria.

Bikira Maria kati ya Waorthodoksi

[hariri | hariri chanzo]
Panagia kutoka Yaroslavl, karne ya 13.

Kwa kiasi kikubwa imani ya Waorthodoksi kuhusu Maria inalingana na ile ya Wakatoliki, ingawa hawakubali jinsi baadhi ya dogma hizo zilivyotangazwa na pengine hata jinsi zinavyofafanuliwa.

Bikira Maria katika Uprotestanti

[hariri | hariri chanzo]

Martin Luther alipoanza Matengenezo ya Kiprotestanti aliandika kwa heshima juu ya Bikira Maria, lakini kadiri mabishano yalivyozidi kati ya madhehebu ya Kikristo, Waprotestanti walizidi kupinga mafundisho ya Kanisa Katoliki juu ya Mama wa Yesu. Siku hizi baadhi yake, hasa Waanglikana na Wamethodisti wanamrudishia Maria nafasi yake kama kielelezo cha imani na cha kupokea neema ya Mungu.

Bikira Mariamu katika Uislamu

[hariri | hariri chanzo]

Kurani inamtaja mwanamke mmoja tu, tena mara 34: ni Mariamu, mama wa nabii Isa. Akichanganywa na dada wa Haruni na Musa, aliyekuwa na jina hilohilo, anatajwa kama binti Imrani. Pia habari nyingine kadhaa zinapishana na zile za Injili.

Hata hivyo anapewa heshima ya pekee, kama inavyoonekana katika sura ya 3:43: “Na kumbukeni malaika waliposema, ‘Ewe Mariamu, kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuchagua na kukutakasa na kukutukuza kuliko wanawake wa walimwengu”. Tena katika aya 3:46: “Na kumbukeni waliposema malaika: ‘Ewe Mariamu, bila shaka Mwenyezi Mungu anakupa habari njema za Neno litokalo kwake, jina lake Masihi Isa mwana wa Mariamu, mwenye heshima katika dunia na ahera, na yu miongoni mwa waliokaribishwa’”.

Aliambiwa amefanywa “ishara” pamoja na mwanae, ingawa haisemwi ni ishara ya nini. Sura ya 19, yenye jina lake, inaeleza kwamba Malaika Jibrili (Gabrieli) akimpasha habari ya mimba alisema, ‘Hakika mimi ni mjumbe wa Mola wako ili nikupe mwana mtakatifu’. Akasema, ‘Ninawezaje kupata mtoto hali hajanigusa mwanamume yeyote, wala mimi si mwasherati?’ Akasema, ‘Ni kama hivyo; Mola wako amesema: Haya ni rahisi kwangu, na ili tukufanya ishara kwa mwanadamu na rehema itokayo kwetu, na ni jambo lililokwisha hukumiwa’ ” (19:19-21). “Na mwanamke yule aliyejilinda tupu yake na tukampulizia roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe ishara kwa walimwengu” (21:91).

Pamoja na kusifiwa kwa usafi wake, anaongezewa sifa za imani na unyenyekevu: “Na Mariamu binti Imrani aliyejilinda uchi wake, na tukampulizia humo Roho yetu na kayasadikisha maneno ya Mola wake, na vitabu vyake; na alikuwa miongoni mwa wanyenyekevu” (66:12).

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. http://www.guardian.co.uk/media/2007/aug/18/religion.news featured in ITV documentary
  2. "The Muslim Jesus, ITV─Unreality Primetime". Primetime.unrealitytv.co.uk. 2007-08-18. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-10-16. Iliwekwa mnamo 2010-03-02.

Marejeo mengine

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]