Nenda kwa yaliyomo

Afrika Kusini

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka South Africa)
Republic of South Africa
Afrika Kusini
Bendera ya Afrika Kusini Nembo ya Afrika Kusini
Bendera Nembo
Kaulimbiu ya taifa: /Xam: !ke e: ǀxarra ǁke
(Kiswahili: "Umoja katika utofauti" au kifasihi, "Umoja wa watu tofauti")
Wimbo wa taifa: National anthem of South Africa
Lokeshen ya Afrika Kusini
Mji mkuu Cape Town (Bunge)
Pretoria (Serikali)
Bloemfontein (Mahakama Kuu)
33°55′ S 18°25′ E
Mji mkubwa nchini Johannesburg
Lugha rasmi Kiafrikaans, Kiingereza, Kizulu, Kixhosa, Kiswati, Kindebele, Kisotho cha Kusini, Kisotho cha Kaskazini, Kitsonga, Kitswana, Kivenda
Serikali Jamhuri
Cyril Ramaphosa
Uhuru
Muungano wa Afrika Kusini
31 Mei 1910
Eneo
 - Jumla
 - Maji (%)
 
1,221,037 km² (ya 25)
kidogo sana
Idadi ya watu
 - Julai 2005 kadirio
 - 2014 sensa
 - Msongamano wa watu
 
47,432,000 [1] (ya 25)
54,002,000
42.4/km² (ya 169)
Fedha Rand (ZAR)
Saa za eneo
 - Kiangazi (DST)
(UTC+2)
not observed (UTC+2)
Intaneti TLD .za
Kodi ya simu +27

-

1.) angalia: Makadirio ya idadi ya watu ni pamoja na vifo kutokana na UKIMWI.


Afrika Kusini ni nchi kubwa ya Afrika ya Kusini yenye wakazi takriban milioni 54.

Imepakana na Namibia, Botswana, Zimbabwe, Msumbiji na Uswazi. Nchi nzima ya Lesotho iko ndani ya eneo la Afrika Kusini.

Mji mkubwa ni Johannesburg. Majukumu ya mji mkuu yamegawiwa kati ya miji mitatu: Cape Town ni makao ya Bunge, Pretoria ni makao ya Serikali na Bloemfontein ni makao ya Mahakama Kuu.

Jina

Nchi ina majina rasmi 11 kutokana na lugha rasmi 11, nazo ni: Kiafrikaans, Kiingereza, Kizulu, Kixhosa, Kiswati, Kindebele, Kisotho cha Kusini, Kisotho cha Kaskazini, Kitsonga, Kitswana na Kivenda.

Historia

Zamadamu waliishi katika eneo la Afrika Kusini tangu miaka milioni 3 iliyopita, inavyoshuhudiwa na akiolojia.

Binadamu wameishi huko kwa miaka 170,000 mfululizo. Wakazi wa muda mrefu zaidi ni Wakhoikhoi na Wasani, ambao wazagumzumza lugha ya jamii ya Khoi-San.

Katika karne ya 4 au ya 5 walifika Wabantu ambao waliwazidi nguvu hao wa kwanza.

Koloni la Waholanzi kwenye Rasi

Chanzo cha Afrika Kusini kama nchi ni Koloni la Rasi iliyoundwa na Waholanzi katika eneo la Cape Town kuanzia mwaka 1652. Huko kabila jipya la Makaburu lilijitokeza kati ya walowezi Wazungu kutoka Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani. Lugha yao ilikuwa Kiholanzi iliyoanza kuchukua maneno ya Kifaransa, Kiafrika na Kiingereza na kuendelea kuwa lugha ya pekee Kiafrikaans.

Karne za kwanza za koloni la Kiholanzi ziliona pia kufika kwa watumwa kutoka Indonesia walioletwa kama wafanyakazi wa Waholanzi na Makaburu. Hao Waindonesia walikuwa chanzo cha jumuiya ya Uislamu kwenye rasi.

Pia machotara walitokea kutokana na kuzaliana kati ya Makaburu na wanawake Waafrika na Waindonesia. Sehemu ya machotara hao wameingia katika jumuiya ya Makaburu na wengi wao wanapimwa kuwa na mababu Waafrika.

Katika miaka ya baadaye ubaguzi wa rangi uliongezeka na watoto machotara wa Wazungu na Waafrika mara nyingi hawakukubalika; walianza kuishi kama kundi la pekee kati ya Waafrika na Wazungu, nao ni chanzo cha hao walioitwa baadaye "Cape Coloreds".

Milki za Waafrika na Mfecane

Sehemu kubwa ya eneo kaskazini kwa rasi ilikaliwa na makabila ya Waafrika.

Mnamo mwaka 1800 falme na milki zilianza kutokea hapa. Mwanzo wa karne ya 19 ni hasa Wazulu chini ya Shaka Zulu walioanza kuenea na kuwashambulia majirani katika vita vya Mfecane. Vita hivyo vilileta uharibifu mkubwa lakini vilisababisha pia kutokea kwa milki za Wasotho na Watswana na wengine walioiga mitindo ya Wazulu na kujenga madola yenye uwezo wa kijeshi.

Kuingia kwa Uingereza na jamhuri za Makaburu

Mwaka 1814 Koloni la Rasi lilitwaliwa na Waingereza na kuwa sehemu ya Milki ya Uingereza.

Utawala wa Waingereza ulisababisha uhamisho wa nje wa sehemu ya Makaburu waliotokana na Wazungu kutoka Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani; Makaburu hao walihama kwenda kaskazini wakaanzisha jamhuri ndogo kati ya maeneo ya Waafrika ama kwa njia ya mapatano au kwa njia ya vita.

Kati ya miaka 1840 na 1850 Waingereza waliwafuata Makaburu kwa kueneza maeneo yao hadi mto Oranje; waliteka jamhuri ya Kikaburu ya Natalia na kuanzisha koloni jipya la Natal.

Jamhuri mbili za Makaburu ziliweza kustawi kwa miaka kadhaa ambazo zilikuwa jamhuri ya Dola Huru la Oranje upande wa kaskazini wa mto Oranje na jamhuri ya Transvaal (ilijiita pia Jamhuri ya Kiafrika ya Kusini) upande wa kaskazini wa mto Vaal.

Waafrika, Waingereza na Makaburu waligongana

Milki za Kiafrika zilitafuta njia zao kati ya himaya hizi za Wazungu ambao walikuwa na nguvu kutokana na silaha za kisasa. Wengine walitafuta uhusiano mzuri na Makaburu na kushikamana nao; wengine waliona Makaburu kama hatari wakatafuta uhusiano wa ulinzi na Waingereza.

Mikataba kati ya Waingereza na milki za Kiafrika iliunda nchi lindwa zinazoendelea hadi leo kama nchi huru kama vile Botswana (Bechuanaland), Lesotho (Basutoland) na Uswazi (Swaziland).

Katika miaka ya 1880 almasi na dhahabu zilipatikana kwa wingi katika jamhuri hizi na kusababisha kufika kwa wachimbamadini wengi, hasa Waingereza, waliotaka kutajirika; Makaburu walisita kuwapa haki za kiraia kwa sababu waliogopa wageni wengi. Tatizo hilo lilisababisha vita vya Makaburu dhidi ya Uingereza na jamhuri za Makaburu zilitwaliwa na jeshi la Kiingereza hadi mwaka 1902 zikawa makoloni.

Karne ya 20: Muungano wa Afrika Kusini

Jitihada za kupatanisha Wazungu wa Afrika Kusini (yaani Waingereza na Makaburu) zilisababisha kuundwa kwa Muungano wa Afrika Kusini kama nchi ya kujitawala ndani ya Milki ya Uingereza. Waafrika kwa jumla hawakuwa na haki za kiraia katika nchi hiyo isipokuwa katika Jimbo la Rasi kama walikuwa na elimu na mapato ya kulipa kodi za kutosha.

Siasa ya Apartheid tangu 1948

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia Chama cha National kilichofuata itikadi kali ilipata kura nyingi na kuchukua serikali ya Afrika Kusini. Hapo ilianzisha mfumo wa ubaguzi wa rangi kwa jina la apartheid.

Haki za wasio Wazungu zilipunguzwa zaidi. Maeneo ya Kiafrika yalitangazwa kuwa nchi za pekee chini ya usimamizi wa serikali ya Kizungu ya Afrika Kusini; kwa hiyo wananchi kutoka maeneo hayo hawakuwa tena na haki za kukata rufaa mbele ya mahakama; walipewa vibali vya muda tu kukaa kwenye miji. Waafrika walipaswa kutembea muda wote na pasipoti na vibali; ndoa na mapenzi kati ya watu wa rangi tofauti zilipigwa marufuku. Shule na makazi zilitenganishwa.

Siasa hiyo ilisababisha farakano kati ya nchi nyingi za dunia na Afrika Kusini. Upinzani kutoka Uingereza na Jumuiya ya Madola ulisababisha kuondoka kwa Afrika Kusini katika jumuiya hiyo na kutangazwa kwa Jamhuri ya Afrika Kusini.

Afrika Kusini mpya

Mwaka 1990 Apartheid ilikwisha na serikali ya National Party ilipaswa kuendesha uchaguzi huru kwa wananchi wote na kukabidhi madaraka kwa serikali ya ANC chini ya Nelson Mandela.

Utawala na muundo wa shirikisho

Afrika Kusini ni shirikisho. Katiba mpya ya mwaka 1997 iliendeleza muundo huu uliundwa kama "Umoja wa Afrika Kusini" baada ya vita ya makaburu dhidi Uingereza.

Afrika Kusini ya kale ilikuwa na majimbo manne: Rasi, Natal, Dola Huru la Mto Orange na Transvaal. Maeneno makubwa yaliyokaliwa na Waafrika yalibaki nje katika katiba ya Apartheid yakiitwa bantustans (au: homeland). Katiba mpya ilichora mipaka upya.

Majimbo ya Afrika Kusini

Ramani ya majimbo na wilaya za Afrika Kusini

Mji mkuu wa jimbo watajwa katika mabano.

 1. Rasi ya Magharibi (Western Cape)¹ (Cape Town) kifupi: WC
 2. Rasi ya Kaskazini (Northern Cape) (Kimberley) kifupi: NC
 3. Rasi ya Mashariki (Eastern Cape) (Bhisho) kifupi: EC
 4. KwaZulu-Natal (Pietermaritzburg²) kifupi: KZ, KZN or KN
 5. Dola Huru (Free State) (Bloemfontein) kifupi: FS
 6. Kaskazini-Magharibi (Mafikeng) kifupi: NW
 7. Gauteng (Johannesburg) kifupi: GT or GP
 8. Mpumalanga (Nelspruit) kifupi: MP
 9. Limpopo (Polokwane) kifupi: LP

Miji Mikubwa

Ramani ya Afrika Kusini

Hii ifuatayo ni miji/manispaa/majiji kumi yenye wakazi wengi zaidi nchini.

Na. Manispaa au Jiji Wakazi (2001) Wakazi (1996) Asilimia ya badiliko
1996-2001
1. Johannesburg, Gauteng 3,225,812 2,639,110 22.2%
2. Durban, KwaZulu-Natal 3,090,117 2,751,193 12.3%
3. Cape Town, Rasi ya Magharibi 2,893,251 2,563,612 12.9%
4. East Rand, Gauteng 2,480,282 2,026,807 22.4%
5. Pretoria, Gauteng 1,985,984 1,682,701 18.0%
6. Port Elizabeth, Rasi ya Mashariki 1,005,776 969,771 3.7%
7. East London, Rasi ya Mashariki 701,881 682,287 2.9%
8. Vereeniging, Gauteng 658,422 597,948 10.1%
9. Bloemfontein, Dola Huru 645,441 603,704 6.9%
10. Thohoyandou, Limpopo 584,469 537,454 8.7%

Watu

Afrika Kusini ina mchanganyiko mkubwa wa watu. Waafrika asili ni asilimia 80.7, Machotara ni 8.8%, Wazungu ni 7.9%, Waasia ni 2.6%.

Lugha mama zinazotunika zaidi ni: Kizulu (22.7%), Kixhosa (16%), Kiafrikaans (13.5) na Kiingereza (9.6%), lakini hiyo ya mwisho ndiyo inayotumika zaidi kati ya makabila mbalimbali na karibu nusu ya wananchi wanajua kuiongea.

Wengi (78.8%) ni Wakristo wa madhehebu mengi sana, hasa ya Uprotestanti; Wakatoliki ni 6.8%. Dini nyingine ni: Dini za jadi (4.4%), Uislamu (1.6%), Uhindu (1%) na Uyahudi (0.1%). Asilimia 12.3 ya watu hawana dini yoyote.

Afrika Kusini inaongoza duniani kwa wingi wa watu wenye VVU/UKIMWI: mwaka 2015 walikuwa milioni 7. Mwaka 2018 silimia 20.4 za watu wenye umri wa miaka 15-49 walikuwa na virusi hivyo. Mayatima kutokana na ugonjwa huo ni 1,200,000.

Uchumi

Kiuchumi Afrika Kusini ni nchi yenye pande mbili kabisa.

Sehemu ya uchumi ina hali ya kimaendeleo kabisa ikiwa na viwanda na huduma zinazolingana na hali ya juu kabisa duniani; hali ya maisha ya wananchi waliomo katika sekta hii inalingana na nchi kama Australia au Ulaya magharibi.

Kwa upande mwingine hali ya maisha ya sehemu kubwa ya wananchi ni umaskini kama katika sehemu nyingine za Afrika au Uhindi wa mashambani. Lakini kwa ujumla hali ya maisha iko juu kuliko nchi nyingi za Afrika.

Sekta muhimu za uchumi ni migodi ya kuchimba dhahabu au almasi, viwanda na huduma kama benki au bima.

Jeshi

Jeshi la Afrika Kusini ina silaha za kisasa kushinda nchi zote za majirani. Uchumi unawezesha nchi kutumia kiasi kikubwa kwa ajili ya jeshi kuliko nchi zote za Afrika kusini kwa Sahara.

Afrika Kusini iliwahi kuwa na silaha za nyuklia lakini ilizibomoa baada ya mwaka 1993.

Watu maarufu

Kati ya watu mashuhuri sana wa Afrika Kusini ni:

Tazama pia

Tanbihi

 1. The Constitution of the Republic of South Africa (PDF) (toleo la 2013 English version). Constitutional Court of South Africa. 2013.{{cite book}}: CS1 maint: url-status (link)

Marejeo

 • A History of South Africa, Third Edition. Leonard Thompson. Yale University Press. 1 March 2001. 384 pages. ISBN 0-300-08776-4.
 • Economic Analysis and Policy Formulation for Post-Apartheid South Africa: Mission Report, Aug. 1991. International Development Research Centre. IDRC Canada, 1991. vi, 46 p. Without ISBN
 • Emerging Johannesburg: Perspectives on the Postapartheid City. Richard Tomlinson, et al. 1 January 2003. 336 pages. ISBN 0-415-93559-8.
 • Making of Modern South Africa: Conquest, Segregation and Apartheid. Nigel Worden. 1 July 2000. 194 pages. ISBN 0-631-21661-8.
 • South Africa: A Narrative History. Frank Welsh. Kodansha America. 1 February 1999. 606 pages. ISBN 1-56836-258-7.
 • South Africa in Contemporary Times. Godfrey Mwakikagile. New Africa Press. February 2008. 260 pages. ISBN 978-0-9802587-3-8.
 • The Atlas of Changing South Africa. A. J. Christopher. 1 October 2000. 216 pages. ISBN 0-415-21178-6.
 • The Politics of the New South Africa. Heather Deegan. 28 December 2000. 256 pages. ISBN 0-582-38227-0.
 • Twentieth-Century South Africa. William Beinart. Oxford University Press 2001, 414 pages, ISBN 0-19-289318-1

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:


Nchi za Afrika Bara la Afrika
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika Kusini bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Afrika Kusini kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.