Cape Town

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sehemu ya Mji wa Cape Town







Jiji la Cape Town

Nembo
Jiji la Cape Town is located in Afrika Kusini
Jiji la Cape Town
Jiji la Cape Town

Mahali pa mji wa Cape Town katika Afrika Kusini

Majiranukta: 33°55′48″S 18°27′36″E / 33.93000°S 18.46000°E / -33.93000; 18.46000
Nchi Afrika Kusini
Majimbo Rasi Magharibi
Tovuti:  www.capetown.gov.za
Cape Town inavyoonekana kutoka Mlima wa Meza (nyuma baharini Robben Island alipofungwa Nelson Mandela)
Mlima wa Meza ni ishara ya mji

Cape Town (yaani "Mji wa rasi", kwa Kiafrikaans: Kaapstad; kwa Kixhosa: iKapa) ni mji mkubwa wa tatu wa Afrika Kusini na mmoja kati ya miji mikuu mitatu ya nchi ikiwa ni makao ya Bunge. Pia ni mji mkuu wa jimbo la Rasi Magharibi (Western Cape / Wes-Kaap). Ni sehemu ya Jiji la Cape Town. Eneo lake ni km² 1,644 lenye wakazi 2,375,910 (mwaka 2005).

Jina la mji limetokana na Rasi ya Tumaini Jema iliyoko karibu na mji upande wa kusini.

Jiografia[hariri | hariri chanzo]

Cape Town ni mji ambako bahari ya Hindi hukutana na Bahari ya Atlantiki. Uko kwenye latitudo ya 33.55° S (sawa na Sydney na Buenos Aires) na longitudo ya 18.25° E.

Ishara ya mji ni Mlima wa Meza unaotazama hori ya Cape Town ukitenganisha kitovu cha mji na makazi ya Cape Flats. Kitovu cha mji kiko kati ya mlima na bahari, sehemu yenye umbo kama la bakuli. Upande wa kusini iko rasi yenyewe, kama ulimi wa nchi wenye milimamilima kwa urefu wa kilomita 40.

Ng'ambo ya mlima kuna tambarare ya Cape Flats na hapo ni sehemu maskini zaidi za mji zenye wakazi wengi.

Cape Town ina uwanja wa ndege wa kimataifa mkubwa wa pili nchini. Ni mji wa Afrika Kusini unaotembelewa na watalii kushinda miji mingine yote. Wengi wanaona iko kati ya miji inayopendeza hasa kote duniani.

Kisiwa cha Robben Island kilikuwa mahali pa gereza alikofungwa Nelson Mandela; leo ni makumbusho yanayotembelewa na maelfu wa watalii kila mwaka.

Cape Town ni mji pekee Afrika ya Kusini wenye muingiliano mkubwa wa watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, hivyo kuufanya mji wenye mchanganyiko wa tamaduni nyingi kuliko yote Afrika Kusini.

Ukipita mitaa ya Wynberg utakutana na watu wengi wanaoongea lugha ya Kiswahili kutoka Tanzania, Kenya, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kiswahili ndiyo lugha kubwa ya kigeni ya Kiafrika inayozungumzwa sana Cape Town.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Ni mji wa kwanza ulioanzishwa katika eneo la Afrika Kusini hivyo huitwa mara nyingi "Mji Mama" wa nchi. Kihistoria mji ulianzishwa kama kituo cha mapumziko kwenye njia ya safari za meli kati ya Uholanzi na makoloni yake huko Asia, hasa Indonesia ya leo.

Kutoka zamani za historia ya awali kuna ushuhuda wa kiakiolojia wa kuwepo kwa watu waliopamba mapango ya makazi kwenye zama za mawe.

Taarifa za kihistoria zinaanza baada ya Vasco da Gama kugundua njia ya kupita Afrika upande wa kusini kutoka Atlantiki kwenda Bahari Hindi mwaka 1497.

Katika karne iliyofuata mabaharia Wareno, Wafaransa, Wadenmark, Waholanzi na Waingereza walipumzika katika hori ya Table Bay wakisafiri kati ya Ulaya na Asia. Walikuta huko Khoikhoi waliovua samaki, kuwinda sili, kukusanya konokono za baharini na kufuga ng'ombe[1]. Walitafuta vyakula hasa nyama kutoka wenyeji hao wakibadilishana nao chuma, shaba au tumbaku.

Kampuni ya Kiholanzi ya India ya Mashariki iliamua kuanzisha hapa kituo kwa jahazi zilizopita kwenye rasi katika safari ndefu. Kampuni hiyo ilimtuma Jan van Riebeeck kusudi aanzishe kijiji ambako vyakula vitalimwa kwa ajili ya mabaharia njiani.

Walowezi Waholanzi pamoja na Wajerumani na Wafaransa walifuata. Mwanzoni ilikuwa vigumu kupata walowezi na Waholanzi waliona wenyeji Khoikhoi wakikataa kuwafanyia kazi. Hivyo waliamua kuleta watumwa kutoka visiwa vya Indonesia na Madagaska. Ndio mwanzo wa jumuiya muhimu ya Waislamu wa Cape Town.[2][3]

Van Riebeeck na magavana waliomfuata walipeleka mimea mingi, hasa mazao kutoka Ulaya na Asia kwa eneo la rasi. Mimea hii ya nje ilibadilisha uoto asilia hadi leo. Kati ya mimea hii kuna mizabibu, nafaka, karanga, viazi na miti ya matunda kama mitofaa au milimau.[4]

Table Bay na meli za Dutch East India Company, 1683 hivi.
Cape Town ilivyoweza kuonekana mwaka 1800.

Utawala wa Waholanzi ulidumu miaka 150. Mnamo 1795, wakati wa vita zilizofuata mapinduzi ya Ufaransa, jeshi la Kifaransa liliingia Uholanzi. Jamhuri mpya ya Kiholanzi ilifuata siasa ya Ufaransa na baadaye ya mtawala wake Napoleon Bonaparte.

Hapo Uingereza, adui wa mapinduzi, ilichukua hatua za kutwaa maeneo ya ng'ambo yaliyokuwa chini ya Ufaransa. Hivyo jeshi la Uingereza lilivamia Cape Town. Tangu mwaka 1814 rasi ilikuwa koloni la Uingereza. Mji wa Cape Town ulikuwa mji mkuu wa Koloni ya Rasi.

Tangu mwaka 1853 Cape Town ilikuwa pia mahali pa bunge la kwanza wakati koloni la Rasi ilipewa haki ya kujitawala. Kila mwanamume, bila ubaguzi wa rangi, mwenye mali ya thamani ya pauni 25 aliweza kupiga kura. Baadaye sharti la elimu ya msingi liliongezwa.

Katika karne ya 20 haki hiyo ilifutwa kwa Waafrika wakati wa kuanzishwa kwa siasa ya Apartheid.[5][6]

Cape Town ulikuwa mji mkubwa wa Afrika Kusini hadi kupatikana kwa dhahabu katika eneo la Johannesburg kuanzia 1887.

Mwaka 1910 Muungano wa Afrika Kusini ulianzishwa baada ya ushindi wa Uingereza juu ya jamhuri za Makaburu. Hapo Cape Town ilikuwa mji mkuu wa bunge la Muungano.

Baada ya ushindi wa Chama cha NP, siasa ya apartheid ilianzishwa pia katika jimbo la Rasi na Cape Town. Serikali mpya ililenga hasa kuunda mitaa ndani ya mji iliyotenganishwa kufuatana na rangi na mbari za watu. Hivyo kama eneo lilitangazwa "nyeupe" Waafrika, Wamalay na Wahindi walipaswa kuondoka, nyumba zao zikabomolewa.

Mfano mashuhuri wa siasa hii ulikuwa historia ya District Six. Mwaka 1965 ilitangazwa eneo kwa watu weupe tu nyumba zote zikabomolewa na watu 60,000 walifukuzwa. [7]

Gereza la Robben Island ambalo lipo kwenye kisiwa baharini kilomita kadhaa nje ya Cape Town ilikuwa mashuhuri kwa sababu viongozi wengi wa mapambano ya kupinga ubaguzi wa rangi walifungwa hapa, pamoja na Nelson Mandela.

Tangu 1994 mji huu ulipambana na matatizo ya madawa ya kulevya na jinai. Wakati huohuo utalii umepanuka sana na Cape Town ikawa inatembelewa na wageni wengi kutoka pande zote za dunia.

Wakazi[hariri | hariri chanzo]

Msongamano wa watu mjini Cape Town
     <1 /km²      1–3 /km²      3–10 /km²      10–30 /km²      30–100 /km²      100–300 /km²      300–1000 /km²      1000–3000 /km²      >3000 /km²
Ugawaji wa lugha za kwanza mjini Cape Town (2011)      Kiafrikaans     Kiingereza     Kixhosa     Eneo la mchanganyiko

Kufuatana na sensa ya mwaka 2011 jiji lote lina wakazi 3,740,026. Tangu sensa ya 2001 idadi hii imekua asilimia 2.6 kila mwaka. [8]

Uhusiano wa jinsia ni 69 maana yake kuna wanawake wengi kidogo kuliko wanaume. Asilimia 42.4 ya wakazi wanajiita "Coloured" (yaani mchanganyiko au chotara), asilimia 38.6 Waafrika weusi, asilimia 15.7 "White South African" na 1.4% kuwa "Indian South African".[8]:56–59

Mwaka 1944 ni asilimia 47 waliohesabiwa kuwa watu weupe na 46 kuwa "Coloured", chini ya 6% Waafrika Weusi na 1% Waasia.[9]

Wakiulizwa kuhusu lugha ya kwanza 35.7% walisema Kiafrikaans, 29.8% Kixhosa na 28.4% Kiingereza.

24.8% za wakazi wote ni watoto chini ya umri wa miaka 15 ilhali 5.5% ni wazee wenye miaka 65 au zaidi.[8]:64

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Emile Boonzaier, The Cape Herders: A History of the Khoikhoi of Southern Africa uk. 54; Publisher: Ohio University Press January 1, 1997; ISBN-10: 0821411748; ISBN-13: 978-0821411742, imeangaliwa 30.11.2016 kupitia google books
  2. Cape-Slavery-Heritage " Coloured People of the Western Cape have the most Diverse Ancestry in the World :: iBlog. Cape-slavery-heritage.iblog.co.za (1 May 2009). Iliwekwa mnamo 17 March 2011.[dead link]
  3. Slavery and early colonisation , South African History Online. Sahistory.org.za (22 September 1927). Iliwekwa mnamo 17 March 2011.
  4. Pooley, S. ‘Jan van Riebeeck as Pioneering Explorer and Conservator of Natural Resources at the Cape of Good Hope (1652–62),’ Environment and History 15 (2009): 3–33. doi:10.3197/096734009X404644
  5. Bell, Charles. A painting of the arrival of Jan van Riebeeck in Table Bay. Jalada kutoka ya awali juu ya 2011-12-30. Iliwekwa mnamo 11 April 2011.
  6. McCracken, J.L. (1967). The Cape Parliament, 1854-1910. Clarendon Press, Oxford, 1967. 
  7. Recalling District Six. SouthAfrica.info (19 August 2003).
  8. 8.0 8.1 8.2 Census 2011 Municipal report: Western Cape. Statistics South Africa. 2012. ISBN 978-0-621-41459-2. Retrieved 30 November 2016. [dead link]
  9. Rebekah Lee (2009). "African women and apartheid: migration and settlement in urban South Africa". I.B. Tauris. p.205. ISBN 1-84511-819-7

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Government
Habari
Mengine
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika Kusini bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Cape Town kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.