Nenda kwa yaliyomo

Bantustan

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ramani za Bantustan za Afrika Kusini

Bantustan ilikuwa jina la eneo maalumu katika Afrika Kusini wakati wa siasa ya Apartheid (ubaguzi wa rangi wa kisheria). Eneo hilo lilitenganishwa kwa ajili ya kabila fulani la Waafrika asili. Kimsingi ilikuwa kama rizavu katika makoloni ya Uingereza, lakini chini ya siasa ya Apartheid ilitangazwa kuwa nchi ya pekee.

Neno Bantustan[hariri | hariri chanzo]

Neno Bantustan liliundwa na maneno "Bantu" (la kutajia Waafrika Weusi) na "-stan" (linalomaanisha kwa Kiajemi nchi ya watu fulani kama vile Uzbekistan = nchi ya Wauzbeki).

Maneno mengine yaliyotumiwa kwa ajili hiyo yalikuwa "homeland" (kwa Kiingereza) na "tuisland" (kwa Kiafrikaans) yakiwa na maana ya "nchi ya nyumbani".

Bantustan kama nchi huru kwa jina[hariri | hariri chanzo]

Bantustan kumi zilitangazwa katika Afrika Kusini, na kumi tena nchini Namibia iliyotawaliwa na Afrika Kusini.

Bantustan kadhaa zilitangazwa kuwa nchi huru lakini hazikutambuliwa na umma wa kimataifa. Hizi zilikuwa:

Zingine zilipewa madaraka ya utawala wa ndani kama vile:

Katika Namibia bantustan zifuatazo zilipewa madaraka ya utawala wa ndani:

Shabaha za siasa za Bantustan[hariri | hariri chanzo]

Shabaha za kuundwa kwa maeneo haya zilielezwa waziwazi na chama cha NP. Waziri Connie Mulder alitangaza mwaka 1978: "Tutakapotimiza siasa yetu kuhusu watu weusi hatabaki mtu mmoja mweusi kama raia wa Afrika Kusini. Kila mtu mweusi atakuwa na uraia katika moja ya hizi nchi huru mpya kwa njia ya heshima. Bunge hili halitakuwa tena na wajibu wa kuangalia watu hawa kisiasa."

Maana ya siasa hii ilikuwa kuhakikisha Afrika Kusini itaendelea kama nchi ya watu weupe hasa Maafrikaaner. Apartheid ilitaka kuondoa tatizo la watu weusi kuwa wengi nchini kwa kuwaondoa katika nchi kwa kuwahamisha katika Bantustan zilizotangazwa kuwa nchi za pekee tofauti na Afrika Kusini.

Kiini cha siasa hii kilikuwa pia kwamba bantustan zote kwa pamoja zilipewa asilimia 13 tu ya eneo lote la Afrika Kusini, na asilimia zaidi ya 80 zilitakiwa kubaki kama Afrika Kusini ya watu weupe. Hii ilimaanisha pia kwamba raia wa bantustan hizo hawakupata kazi na ajira kwao, wakategemea kupata ajira katika Afrika Kusini - ila tu si kama wenyeji bali kama wageni walioweza kuondolewa na kushughulikiwa kama wageni yaani bila ya haki zozote hasa bila ya haki za kutafuta msaada wa mahakama. Kwa mfano, asilimia 65 za wafanyakazi wa Bophuthatswana walifanya kazi nje ya eneo lao.

Hali za Bantustan[hariri | hariri chanzo]

Maisha katika Bantustan yalikuwa ya umaskini kwa watu wengi. Maeneo yalikuwa madogo mno na hasa maeneo yenye rutuba yalibaki nje mkononi mwa wakulima makaburu. Siasa hii ya kuteua maeneo bila ya thamani tu kwa ajili ya Bantustan ilionekana pia kwenye ramani inayoonyesha Bophuthatswana na KwaZulu kama mkusanyo wa viraka, si kama eneo moja.

Hakuna Bantustan hata moja iliyoweza kujidumisha, bali zote zilitegemea misaada kutoka serikali ya Pretoria. Mwaka 1985 Transkei ilipokea 85% ya mapato yake kama ruzuku kutoka serikali ya Afrika Kusini.

Tatizo kubwa ya bantustan ilikuwa ufisadi wa viongozi na tabaka la juu. Watu wachache walitajirika wakaweza kujenga maisha bora lakini idadi kubwa waliishi kimaskini mno. Wakubwa waliendesha biashara kama vilabu ambako raia wa Afrika Kusini waliweza kufurahia mambo yaliyokataliwa kwao: michezo ya kamari, biashara ya ngono na umalaya.

Mwisho wa Bantustan 1994[hariri | hariri chanzo]

Mwisho wa Apartheid ulikuwa pia mwisho wa Bantustan zote zilizorudishwa ndani ya Afrika Kusini.

Serikali kadhaa zilijaribu kupinga harakati hizi lakini raia walisimama upande wa ANC.

Katika Bantustan ya Ciskei jeshi na polisi ya Afrika Kusini waliingilia kati mwaka 1994.


Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika Kusini bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Bantustan kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.