Apartheid

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Tangazo la Apartheid mjini Durban mwaka 1989: Bahari hii inaogelesha watu weupe tu!

Apartheid ni neno la Kiafrikaans linalomaanisha "kuwa pekee" au "utengano". Kwa kawaida hutaja siasa ya ubaguzi wa rangi wa kisheria nchini Afrika Kusini kati ya 1948 hadi 1994.

Siasa hii ilikuwa na utaratibu wa sheria nyingi zilizolenga kutenganisha watu wa rangi au mbari mbalimbali. Kusidi lake lilikuwa kimsingi kutunza kipaumbele ya makaburu na kuhakikisha Waafrika Weusi wasianze kushindana nao kwenye soko la kazi na nafasi za kijamii.

Utaratibu wa Apartheid[hariri | hariri chanzo]

Vikundi vya kimbari[hariri | hariri chanzo]

Sheria za Apartheid ziligawa wakazi wa Afrika Kusini katika vikundi vifuatavyo:

  • Watu weupe
  • Watu weusi
  • Chotara wa asili ya mchanganyiko
  • Baadaye kundi la nne lilitengwa ni Waasia.

Kila mtu alitakiwa kujiandikisha.

Kutenganisha mbari[hariri | hariri chanzo]

Katika ngazi za kwanza watu wa rangi mbalimbali zilikataliwa kuoana au kuwa na uhusiano wa kimapenzi. Baadaye walitenganishwa kijiografia. Maeneo yalitangazwa kuwa eneo la watu weupe pekee au la wasio weupe. Waafrika waliruhusiwa kuingia au kukaa katika maeneo "meupe" kwa kibali maalum tu, kwa mfano kama walikuwa na ajira hapa.

Tangazo la vyoo vya pekee kwa ajili ya watu weupe na wengine

Huduma za pekee[hariri | hariri chanzo]

Hatua ya ziada ilikuwa sheria juu utengano wa huduma (Separate Amenities Act of 1953) iliyoweka masharitiy kwa ajili ya uwanja za michezo, mabasi, mahospitali, shule, vyuo vikuu, nafasi za kupumzika na hata vyoo vya pekee kwa ajili ya watu weupe na wasio weupe.

Kwa kawaida huduma kwa ajili ya watu wasio weupe zilipewa pesa kidogo kulliko vifaa kwa ajili ya weupe zikawa za sifa hafifu.

Kuondoa haki za kisiasa[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya 1948 chotara na Waafrika kadhaa wenye elimu walikuwa na haki ya kupiga kura katika jimbo la Rasi. Haki hizi zilifutwa. Chotara na Waasia walipewa bunge za pekee bila mamlaka ya maana. Waafrika weusi waliambiwa kupiga kura kwao katika maeneo ya kikabila.

Kuondoa uraia[hariri | hariri chanzo]

Hasa Waafrika weusi waliondolewa uraia wa Afrika kusini kwa kuunda bantustan au "homelands". Bantustan hizi zilikuwa maeneo ya kikabila yaliobaki chini ya machifu. Bantustan hizi zilitangazwa kuwa mataifa ya pekee na kila mwafrika mweusi alitangazwa kuwa raia wa bantustan fulani. Azimio hili lililenga kuondoa maswali yote kuhusu haki za waafrika za kushiriki katika siasa ya Afrika Kusini penyewe.

Kijana wa Soweto abeba maiti ya mtoto Hector Pieterson aliyepigwa risasi na polisi mwaka 1976

Upinzani[hariri | hariri chanzo]

Sheria hizi zilikuwa na upinzani nyingi nchini na kimataifa. Awali serikali ya 1948 ilipita kwa kura chache tu kushinda wapinzani wake. Lakini Chama cha NP kilifaulu kuunganisha sehemu kubwa ya Makaburu waliokuwa kundi kubwa kati ya raia weupe wa Afrika Kusini. Utawala wa NP uliendelea hadi 1994.

Upinzani kwa upande wa watu weupe ilitokea hasa kati ya wasemaji wa Kiingereza na wengine. Upande wa Waafrika chama cha ANC kilikuwa mbele hadi ilipopigwa marufuku.

Wapinzani kama ANC na wengine walijaribu kuendesha vita ya msituni dhidi ya serikali ya Pretoria lakini kwa jumla hawakufaulu kijeshi. Lakini upinzani usiokuwa wa kijeshi ulitokea kama mwendo wa watoto wa shule tangu mwaka 1976 Soweto. Maandamano ya wanafunzi yalikandamizwa vikali na polisi. Baada ya watoto kuuawa maandamano yaliendelea kupanua yakafaulu kurudisha swali la Apartheid kwenye ajenda ya kimataifa. Mwishowe zilikuwa matatizo ya kiuchumi (kuporomoka kwa bei ya dhahabu), gharama kubwa ya ukandamizaji wa upinzani shindikizo la kimataifa na mwishowe mageuzi makubwa baada ya anguko la Ukomunisti zilizolazimihsa viongozi wa Afrika Kusini kukubali mabadiliko.

Rais Frederik Willem de Klerk alikuwa na busara ya kuanzisha mazungumzo na kiongozi wa ANC Nelson Mandela aliyekaa gerezani kisiwa cha Robben. Baada ya kuachishwa kwa Mandela kutoka gereza sheria za Apartheid zikafutwa haraka. Uchaguzi huru wa kwanza kwa ajili ya raia wote ulimaliza Apartheid kama utaratibu wa kisheria.