Lugha ya ishara

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ishara ya lugha nyingi inayomaanisha "mkalimani".
Preservation of the Sign Language (1913)

Lugha za ishara (pia lugha za alama) ni lugha zinazohusisha miendo ya mikono, uso, kichwa, mabega na pia sehemu nzima ya juu ya mwili badala ya kuhusisha sauti. Lazima lugha za aina hiyo zionekane kwa sababu hazisikiki. Lugha hizo zinatumiwa hasa na watu viziwi, lakini vilevile wanaosikia wanaweza kujifunza hizo.

Lugha za alama ni lugha za asili na za kawaida zenye cheo cha kiisimu sawa na lugha za sauti. Hizo si mifumo tu ya kuleta msaada kwenye mawasiliano.

Duniani kuna mamia mengi ya lugha za alama. Idadi sahihi haijulikani. Lugha hizo vilevile si nakala tu za lugha ya sauti inayozungumzwa kwenye eneo hilohilo. Kwa sababu ya mwanzo wake na maendeleo yake visivyotegemea lugha za sauti, zina sarufi zake zenyewe zinazotofautiana na zile za lugha nyingine (za sauti) zinazozungumzwa na walio wengi. Kwa mfano, katika Kiitalia (lugha ya sauti) kitenzi kikuu kipo kwa kawaida baada ya kiima na kabla ya yambwa. Katika Lugha ya Alama ya Italia, ambayo inazungumzwa nchini humohumo, kitenzi kikuu kipo kwa kawaida mwishoni mwa sentensi.

Vilevile lugha za alama zinaweza kutumia mielekeo na mahali pa ishara ili zifikishe taarifa muhimu kama vile kuhusu kiima na yambwa. Kwa mfano, katika lugha nyingi za ishara, alama inayomaanisha "kuuliza" inabadilika ikitegemea ni nani anayemuuliza nani: "ninakuuliza" inafikishwa kwa mwendo mmoja tu wa mbele kutoka mahali panapowakilisha "mimi" kuelekea panapowakilisha "wewe", ilhali alama inayomaanisha "unaniuliza" ina mwendo wa kinyume ulioelekea "mimi". Pia inawezekana kufikisha taarifa nyingine wakati huohuo, kama vile kwa ishara maalumu ya uso inayoweza kubadili ishara inayomaanisha "kuendesha gari" ikamaanishe "kuendesha gari kwa purukushani".

Zinazuka bila kupangwa wakati wowote watu wengi viziwi (hasa watoto) wanapokusanyika na kutumia muda mwingi wao kwa wao wakijaribujaribu kuwasiliana. Kwa kawaida, viziwi wasiojua lugha ya ishara (k.m. kwa sababu ya kukua kwenye familia ambapo wengine hawaijui) wamezoea kutumia ishara wanazozibuni ili wawasiliane na wengine. Ishara hizo zinazobuniwa zinajaribiwa kufahamika waziwazi kadiri iwezekanavyo. Viziwi hao wengi wanapokusanyika, baada ya muda wanaanza kutumia ishara zilezile. Hivi msamiati unajengwa. Kwa matumizi mengi inazuka pia sarufi. k.m. ambapo shule mpya ya viziwi inafunguliwa).

Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Lugha ya ishara kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.