Mpeketoni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Mpeketoni
Nchi Kenya
Kaunti Lamu
Idadi ya wakazi
 - Wakazi kwa ujumla 25 000
Barabara ya Mpeketoni

Mpeketoni ni mji wa Kenya katika kaunti ya Lamu[1].

Si mji wa kale bali ulianzishwa katika miaka ya 1960 kama mradi wa kujenga makazi ya watu na rais wa jamhuri, Jomo Kenyatta.

Kwa asili eneo lilikaliwa na Wabajuni lakini wakati wa uhuru, na baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wakenya wengi walirudi kutoka Tanzania hasa Wakikuyu, walio sehemu kubwa ya wakazi wa leo, pamoja na Waluo na Wakamba.

Mashamba yaliyoanzishwa na walowezi hao yanaendelea hadi leo. Kilimo ni hasa ya mahindi, pamba, muhogo, korosho, maembe, tikiti maji na ndizi.

Kabla ya ukoloni wa Kiingereza eneo lilikuwa chini ya usultani wa Zanzibar. Wafanyabiashara ya watumwa walitumia njia ya pwani kupeleka watumwa hadi Lamu. Hadi sasa mwembe mkubwa unakumbusha mahali ambako misafara ya watumwa ilipumzika na wafungwa walikula maembe na kuacha mbegu.

Karibu na Mpeketoni kuna ziwa Kenyatta.

Vijiji ndani ya tarafa ni pamoja na Kiongwe, Baharini, Mkunumbi, Bomani, Uziwa, Mapenya, Lakeside, Kibaoni.

Mashambulizi ya al-Shabaab 2014[hariri | hariri chanzo]

Tarehe 16 Juni 2014 mji huo ulishambulia na kikosi cha al-Shabaab kutoka Somalia walioua watu 48. Mnamo saa 3 jioni waliingia katika mji kwa kutumia magari 3 wakati wakazi wengi walikuwa wakiangalia mechi ya Kombe la Dunia la FIFA. Washabaab walitangulia kushambulia kituo cha polisi lakini walishindwa kuingia kutokana na upinzani wa maafisa. Waliendelea kushambulia hoteli, mabaa, benki na ofisi za serikali ilhali walifyatulia risasi hovyo wananchi waliowaona pamoja na watoto wadogo na wakinamama. [2]

Baada ya saa sita usiku waliondoka tena lakini njiani waliua wananchi wengine, kwa mfano watu sita huko Kibaoni.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

  • www.wimvandenburg.nl. shirika la Kiholanzi linalotoa misaada kwa miradi katika Mpeketoni