Watiriko

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Watiriko ni kabila dogo lililo kusini mwa wilaya ya Mpwapwa, mkoa wa Dodoma ulio katikati ya nchi ya Tanzania, hasa Kibakwe, Chamtumile, Ikuyu, Wotta na maeneo ya karibu na hayo.

Kabila hilo lina asili ya mchanganyiko wa Wahehe na Wagogo. Maneno yao ni mchanganyiko wa maneno ya makabila hayo mawili, isipokuwa mila na desturi zao zimeelemea sana kwa Wagogo, mfano: wanatahiri watoto Mwanaume. Michezo yao ya kiutamaduni na nyimbo zao ni za Kigogo zaidi, japo pia wana baadhi ya nyimbo za kitamaduni zenye asili ya Kihehe kama "kiduo".

Historia[hariri | hariri chanzo]

Inasemekana wahamizi wa zama za vita vya kikabila kabla ya vita kuu ya kwanza, walitokea upande wa kusini wa Tanganyika, hasa mkoa wa Iringa, wakaja mpaka mto Ruaha, wakavuka mto hadi Mpwapwa kusini ya sasa, wakachagua kuishi huko.

Kusudi wapate kukubalika katika jamii ya nchi hii mpya (ambapo ilikuwa ni himaya ya Wagogo, ijapo walikuta sehemu ile haikuwa na wakazi) iliwalazimu kuiga mila na desturi za wenyeji wa karibu na eneo lile, mfano: kutoga masikio, kutoa meno mawili ya chini, kufanya tohara kwa wanaume na watoto wa kike. Kwa njia hiyo walikubalika katika jamii ile na waliweza kuwa watawala (au watemi).

Waliweza kuoa wenyeji wa pale, na matokeo yake ikapatikana lugha iliyokuwa mchanganyiko wa Kigogo na Kihehe; hadi leo lugha hiyo wanaiita Kitiriko.

Kabila hili linatawaliwa na koo chache zenye nguvu kama vile Mduwile ambao chimbuko lao ni maeneo ya bondeni katika kijiji cha Lwihomelo ambapo kuna eneo lijulikanalo kama Pitiliko. Koo nyingine ni kama Chugulu, Semwali na Kinoga ambao asili yao ni mlima Semi karibu na Kibakwe.

Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Watiriko kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.