Hatua ya utakaso

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Hatua ya utakaso ni ya kwanza kati ya tatu za safari ya maisha ya Kiroho kadiri ya waandishi wengi, hasa wa Kanisa Katoliki.

Hatua zinazofuata ni ile ya mwanga na ile ya muungano.

Kujitakasa[hariri | hariri chanzo]

Utakaso unaohitajika kuelekea muungano na Mwenyezi Mungu huanzia na hisi, hasa tamaa za mwili na hasira.

Kwanza tukumbuke ni wajibu kushika amri za Mungu, hasa ile kuu ya upendo, kwa kuepa kila dhambi ya mauti, halafu polepole hata zile nyepesi za makusudi. Ingawa hatuwezi kuepa mfululizo dhambi zote nyepesi – tusipojaliwa msaada wa pekee kama bikira Maria – tunaweza kuepa kila mojawapo. Tuzidi pia kuepa matendo mapungufu, ambayo ni mema kiasi tu. Tendo jema kiasi si baya, lakini linaonyesha hatuna bidii zinazotakiwa katika utumishi wa Mungu. Katika maadili hatupaswi kusimama katika ngazi ya chini, bali kulenga juu; hasa vipaji vya Roho Mtakatifu vinatufanya tujitahidi zaidi ili kuendelea kwa kasi. Lakini juhudi hizo pia zina ngazi nyingi, kadiri tunavyotaka kupanda mlima wa ukamilifu kwa njia rahisi ya mzunguko, au kwa njia ya mkato inayofika haraka na juu zaidi.

Halafu tukumbuke kuwa mizizi ya dhambi inaelekeza kutenda dhambi nyingine ambazo mara nyingi ni kubwa zaidi. Hatuwezi kamwe kumuomba mno Mungu atuangazie ubaya wa dhambi na kutupatia majuto kamili. Hayo na upendo wa kidugu ni dalili kuu za maendeleo ya kiroho.

Tukumbuke pia kuwa dhambi nyepesi, hasa ikirudiwarudiwa, inaelekeza kutenda ya mauti, kwa sababu anayetenda kwa urahisi dhambi nyepesi anapotewa na nia safi, hivyo nafasi ikipatikana anafikia kutenda ya mauti. Kwa hiyo dhambi nyepesi iko kwenye mteremko wa kutisha; ni kama ukuta unaotuzuia tusifikie muungano na Mungu. Vilevile matendo mapungufu, yaani uhaba wa juhudi, yanatuelekeza kutenda dhambi nyepesi; ingawa yanastahili, yanatuelekeza kuteremka, kwa maana hayapingani inavyotakiwa na maelekeo yanayoweza kutuangusha. “Mara nyingi subira bandia ni utovu tu wa juhudi katika njia ya maendeleo; hatua za baadhi ya watu ni za polepole kiasi kwamba huenda Mungu mwenyewe akahukumu wamekuwa na subira kubwa mno!” (Yohane wa Msalaba).

Kufisha tamaa za mwili[hariri | hariri chanzo]

Nje ya ndoa, kila nyege iliyokusudiwa ni dhambi ya mauti: haina udogo, kwa sababu inatuelekeza kukubali nyingine kubwa zaidi. Kwa kuingiza kidole mashineni, mkono mzima utashikwa nayo. Ni mzizi wa dhambi unaozaa kutozingatia mambo, ugeugeu, upofu wa roho, kujipendea hata kumdharau Mungu na kukata tamaa ya wokovu. Kuufisha ni kuhakikisha roho iwe huru katika maisha yake bora isilemewe na mwili. Kwa ajili hiyo Kanisa limeagiza siku za kufunga na kujinyima nyama. Kuna magumu mengine tunayoweza kuyakusudia badala ya starehe. Waanzilishi wa mashirika wamepanga magumu ya pekee, kama kukesha na kujipiga viboko, zoezi ambalo linakinga na makosa, linadumisha upendo kwa maisha magumu, linafidia mapungufu na kufungua wengine waliojifunga. Utawani taratibu za sala na sadaka ni kama ganda la mti ambalo ukiliondoa lote, utomvu hauwezi kupanda juu tena, hivyo mti unakauka. Tukilegeza taratibu hizo, tutalegeza roho pia zisiwe na nguvu za kupiga mbio katika njia ya ukamilifu.

Uzinifu unashindwa kwa kukimbia hatari kuliko kwa kuzikabili ambako kungetufanya tufikirie mno jambo la kuvutia. Tukwepe iwezekanavyo yanayochochea ashiki hata tusipoikusudia, hasa kama kuna hatari kubwa ya kuikubali. Kwa hiyo inafaa wengi waepe maandishi (k.mf. ya uganga) vinavyoweza vikawa vya hatari kwa udhaifu wao, hasa wakivisoma kwa udadisi, si kwa wajibu. Tuwe macho pia kuhusu mapendo yanayoweza kugeuka ya kihisi na kupoteza amani ya moyo wetu. “Mapendo ambayo asili yake ni hisi kuliko ibada yakikumbukwa hayaongezi kumbukumbu ya Mungu wala upendo wake, bali matokeo yake ni lawama ya dhamiri” (Yohane wa Msalaba). Tusizoeane mno na viumbe ili tufurahie urafiki na Bwana. Aina nyingine za urafiki ni tauni halisi: polepole zinapoteza juhudi za Kiroho, zinaharibu taratibu za jumuia, pengine zinazaa mafarakano makubwa, hata kuhatarisha wokovu wa milele. “Kateni, vunjeni, pasueni; haitoshi kufumua aina hizo za urafiki kichaa, mnapaswa kuzing’oa pasipo huruma; haitoshi kufungua vifungo, tunapaswa kuvivunja na kuvikata” (Fransisko wa Sales). Tunapaswa kufikiria mengine na kuzama katika wajibu. “Huwa tunaanza na upendo mwadilifu, lakini tusipoangalia utachanganyikana na mapendo ya juujuu, halafu ya kihisi, hatimaye ya kimwili” (Fransisko wa Sales). Katika urafiki wenye mchanganyiko huo, upande wa roho ukitawala, tunaweza kuendelea nao mradi tuzidi kuutakasa kwa kuchunguza hisi na moyo; lakini upande wa hisi ukitawala, ni lazima kuusimamisha kwa muda mrefu kwa kuacha fungamano lolote lisilo la lazima. Hapo ufishaji wa moyo unahitajika sawa na ule wa mwili na wa hisi.

Hatimaye katika sala tusijitafutie faraja za kihisi kwa ulafi wa roho. Ulafi wa kawaida unazaa utani wakati usiofaa, porojo, mazungumzo yasiyo na maana, upumbavu na uchafu; ulafi wa roho, ambao matokeo yake yanafanana na hayo, unapatikana mara nyingi kwa wanaoanza: “Wanatamani furaha ya roho kuliko usafi wake na ibada halisi” (Yohane wa Msalaba). Kumbe faraja ni za ziada: zinafaa mradi tusizame ndani yake; tukizipenda mno, Mungu atatuondolea ili atujaribu. “Inawezekanaje mtu asielewe kuwa matokeo ya komunyo katika hisi si muhimu hata kidogo? Mara nyingi Mungu mwenyewe anawanyima wanaokomunika furaha yoyote ya kihisi ili awalazimishe kumzingatia kwa macho ya imani” (Yohane wa Msalaba). Anayempenda Mungu si kwa ajili yake, bali kwa ajili ya faraja za kihisi ambazo anazipokea au kuzitarajia, hayuko sawa kwa kuwa anapindua utaratibu: kwanza anajipendea, halafu anampenda Mungu kama anavyoweza akapenda tunda. Anayatumia vibaya yaliyo matakatifu zaidi na kukaribisha vishawishi vya kila aina: furaha za kihisi zikikusudiwa zinachochea maono yaliyosinzia ndani mwetu na kutufanya tuteleze kwenye genge la tamaa.

Uzinifu wa roho ni ashiki zisizokusudiwa zinazowapata wanaoanza wakati wa sala ya moyo au wa kupokea sakramenti. Kwa kawaida zinatokana na furaha ya ndani inayofurika katika hisi zisizotawaliwa au kutakaswa vya kutosha. Pengine zinatokana na shetani anayetaka kuvuruga na kuhangaisha mtu aache sala. Pengine hofu yenyewe ya ashiki kurudia inaweza ikazisababisha, na walio wepesi kuguswa moyo wanazipata kutokana na maono mbalimbali. Hizo zote si dhambi kama utashi hauzikubali, bali unazipinga, tofauti na ashiki zinazochochewa ingawa bila makusudi mazima (k.mf. kwa ujirani mkubwa mno na mtu unaoathiri urafiki wa Kiroho).

Upotovu ulio mbaya zaidi ni ule ambao unaathiri na kughushi yaliyo bora, kama vile sala bandia na upendo bandia. Kwa hiyo tunaonywa, “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu” (1Yoh 4:1). Kusudi tusijidanganye tunahitaji unyenyekevu na usafi wa moyo. Mafundisho kuhusu ufishaji wa tamaa yanaweza kujumlishwa katika maneno haya: “Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu” (Math 5:8).

Kufisha hasira[hariri | hariri chanzo]

Ufishaji mwingine unaosisitizwa na Injili unahusu hasira, vurugu ya pili ya hisi zetu. Kufisha hasira kunatupatia upole: si ule wa kuzaliwa nayo, wala ule unaoruhusu lolote kwa kukosa msimamo, bali adili la upole ambalo ni nguvu kubwa ya kujitawala, kudumisha roho katika utulivu wa Mungu, na kuwatendea mema wanaotukasirikia. Ufishaji wa hasira ni wa lazima kadiri matokeo yake yalivyo mazito kwa kuwa inaweza kufikishia madhambi mengine, hata kulikufuru jina la Mungu. Kinyume chake, upole ndio ua linalotunza matunda ya upendo, kwa kuwa unafanya mashauri na hata maonyo yake yapokewe. Kumbe yakifanywa kwa ukali hayazai kitu.

Yohane wa Msalaba alitaja ari chungu kati ya kasoro za wanaoanza, kwa kuwa wanaponyimwa faraja, mara wanakosa uvumilivu. “Ladha ya mambo ya Kiroho ikija kukosekana, umbile lao linavurugika; wanashikwa na huzuni, wanatimiza wajibu pasipo adabu, wanakasirikia mambo madogo sana na pengine haiwezekani kuwavumilia… Wanafanana na mtoto mchanga asiyeridhika kwa kuwa muda wa kuachishwa ziwa umefika”. Pengine wanatumbukia uzembe. Mara nyingine “wanalaumu kasoro za wengine, wakisukumwa na ari isiyo na kiasi. Wanawasema na kusukumwa kuwaonya kwa ukali… kana kwamba wenyewe tu ni waadilifu… Baadhi, wakiona kasoro zao wenyewe, wanasahau unyenyekevu na kujikasirikia, na huo utovu wa subira unaonyesha wazi kwamba walidai kugeuka watakatifu kwa mkupuo mmoja… Kwa wengine, ambao wamezoea kupanga makuu na kuweka maazimio ya kishujaa, lakini kwa kweli wana kiburi kuliko unyenyekevu, uponyaji wa hasira na upatikanaji wa upole wa Kiroho hauwezi kufanyika nje ya usiku wa giza”.

Ni kwamba kujitakasa upande wa hisi kunatakiwa kufuta vurugu hizo mbili: tamaa na hasira. Lakini hakuwezi kuzifuta kabisa; unahitajika utakaso mkubwa zaidi: ule unaotokana na Mungu mwenyewe anapoacha hisi katika ukavu wa muda mrefu ambapo anatutia mwanga wa kipaji cha elimu, yaani elimu ya ubatili wa malimwengu yote iliyo neema ya Kiroho tu. Utakaso huo ni namna mojawapo ya msalaba unaoleta wokovu ambao tuubebe ili kufikia maisha ya Kiroho kweli, ambayo yanatawala hisi na kutuunganisha na Mungu.

Kujitakasa upande wa ubunifu na kumbukumbu[hariri | hariri chanzo]

Tuliyoyasema kuhusu kujitakasa upande wa hisi yameshatuonyesha kuwa ufishaji wa nje si ule muhimu zaidi, ingawa mtu akiupuzuia atapuuzia pia ule wa ndani na hatimaye atapotewa kabisa na roho ya kujikana. Hasa akikataa ufishaji kwa makusudi atatumbukia fikra za kidunia tu zilizo kinyume cha imani, inavyotokea mara nyingi. Tukitaka kujipatia yale yote yanayotupendeza, katika chakula na starehe, bila kuzingatia kiasi cha Kikristo, tunaacha kulenga ukamilifu na kukumbuka wajibu wetu. Lakini ufishaji wa nje wa mwili na hisi hauzai vya kutosha usipoendana na ule wa ndani wa ubunifu na kumbukumbu, pamoja na na wa akili na utashi, tutakaozungumzia baadaye.

1. Ubunifu ni uwezo wa kufaa kwa kuwa roho iliyounganika na mwili haiwazi pasipo taswira; ndiyo sababu Bwana alisema kwa mifano ili kuinua umati toka jambo la kihisi hadi wazo la Kiroho. Lakini ubunifu uongozwe na akili iliyoangazwa na imani, la sivyo unakuwa kama kichaa wa nyumbani, ukitusogeza mbali na mambo ya Mungu na kutuelekezea mambo ya bure ambayo hayajengi kitu, hayapo au yamekataza. Walau unatuhamishia ulimwengu wa ndoto za mchana, inapozaliwa miguso ya juujuu ambayo ni kinyume cha ibada halisi inayoelekea yasiyoonekana, bila kusimama katika picha za kihisi zinazoyamaanisha: kadiri tunavyokaribia muungano na Mungu hatutegemei picha.

Hasa wakati wa uchovu hatuwezi kuondoa upesi taswira za bure na za hatari, lakini kwa msaada wa neema tunaweza kuacha kuzizingatia kwa roho, halafu polepole kupunguza idadi yake na mvuto wake. Hata waliokamilika wanasumbuliwa na mitawanyiko kadhaa ya mawazo isiyo ya hiari na inayotokana pengine na shetani. Lakini mtu akiendelea anazidi kujikomboa kutoka mitawanyiko hiyo na hatimaye anamtazama Mungu karibu pasipo kuzingatia taswira zinazoendana na tendo hilo la imani lenye kupenya na kuonja. Ni kama tunapoandikia peni bila kuzingatia aina yake, au tunapoongea na mtu bila kuangalia mtindo na rangi ya mavazi yake. Polepole ubunifu unaacha kuvuruga kazi ya akili, na hatimaye unatumiwa nayo kufafanulia pengine maisha ya Kiroho kwa mifano mizuri ajabu. Mifano iwe na kiasi isije ikajivutia akili za watu, badala ya kuzivuta kwenye mawazo inayosaidia kuyaeleza. Mfano ni kwa ajili ya wazo tu, nalo ni kwa ajili ya kufafanua ukweli. Hapo akili inatumia mfano pasipo kuishia ndani yake, kama vile mwadilifu anavyovaa nguo bila kuzitia maanani.

Lakini ulinganifu huo wa vipawa mbalimbali haupatikani pasipo kuratibu ubunifu ili kurudia utaratibu wa uadilifu asili ambapo sehemu ya juu ya roho ikimtii Mungu ilikuwa inatawala ubunifu na maono. Kwa ajili hiyo, tuondoe mara taswira za hatari, masomo yasiyo na faida, na ndoto za mchana ambazo zinapoteza muda wa thamani na kutuingiza katika udanganyifu wa kila aina, ambapo adui atucheke ili kutuangamiza. Tunapaswa kuwajibika kila nukta, kufanya vema tunachokifanya, tukielekeza utekelezaji wa wajibu kwa Mungu ili tumpende kuliko yote. Hivyo polepole akili na utashi vitatawala; na ubunifu ukitawaliwa utaona katika uzuri wa liturujia lishe ya maisha ya ndani.

2. Tuseme sasa kuhusu ufishaji wa kumbukumbu, inayotukumbusha mara nyingi mambo ambayo ni afadhali kuyasahau. Kumbukumbu yetu inahitaji kutakaswa kwa sababu, baada ya dhambi asili na ya dhambi zetu binafsi, imejaa mambo yasiyo na maana na pengine ya hatari. Tunakumbuka hasa tulivyokosewa, maneno makali ambayo aliyeyasema pengine ameyajuta na kuyaombea msamaha. Hatukumbuki hivyo mema tuliyotendewa, na pengine neno kali linatusahaulisha fungu la misaada tuliyopatiwa miaka na miaka. Lakini kosa kuu la kumbukumbu yetu ni kumsahau Mungu. Mara nyingi, badala ya kukumbuka yaliyo muhimu zaidi, inasahau kitu kile ambacho pekee ni cha lazima. “Je, mwanamwali aweza kusahau mapambo yake, au bibi arusi mavazi yake? Lakini watu wangu wamenisahau mimi kwa muda wa siku zisizo na hesabu” (Yer 2:32). “Wakayasahau matendo yake kwa haraka… Wakamsahau Mungu, mwokozi wao, aliyetenda makuu katika Misri” (Zab 106:13,21). Biblia inasema kuwa hasa katika tabu tunapaswa kukumbuka rehema za Mungu na kuomba msaada wake. Tukimsahau na kupuuzia fadhili zake kuu (k.mf. umwilisho uliotukomboa) tunakosa shukrani na kupoteza muda huu unaotakiwa kulenga uzima wa milele.

Kumsahau Mungu kunaifanya kumbukumbu yetu izamie nyakati hizi isione zinavyohusiana na umilele na fadhili na ahadi za Mungu: ione yote katika mfululizo wa mambo yapitayo, isione nukta ya sasa inavyohusiana na ile pekee isiyo na mwisho, yaani isione namna ya Kimungu ya kuishi nukta hii ili kustahili uzima wa milele. Kumsahau Mungu kunatuacha tuone mambo pasipo maana yake, kumbe kumtazama Mungu ni kuona toka juu mambo yapitayo yanavyohusiana naye asiyepita kamwe. Kuzamia muda ni kusahau maana yake, yaani unavyohusiana na uzima wa milele. “Katika mambo yako yote uukumbuke mwisho wako, hivyo hutakosa kamwe hata hatima” (YbS 7:36).

Adili gani linapaswa kuondoa kosa hilo kubwa? Yohane wa Msalaba alifundisha kuwa tumaini ni kubwa kadiri kumbukumbu isivyo na habari za malimwengu akajibu, “Kumbukumbu inayomsahau Mungu inatakiwa kuponywa na tumaini la heri ya milele, kama akili inavyotakiwa kutakaswa na ustawi wa imani, halafu utashi na ustawi wa upendo”. Kama vile mababu na manabii wa Agano la Kale walivyoishi kwa kumtazamia Masiya aliyeahidiwa, sisi tuishi kila siku zaidi kwa kutumainia heri ya milele.

Kitabu cha Kumfuasa Yesu Kristo kinasema mara nyingi kuhusu utakaso wa kumbukumbu unaoandaa kumtazama Mungu, kinapozungumzia kutafakari kifo (I,23), kukumbuka fadhili za Mungu (III,22), uhuru wa moyo unaopatikana kwa kusali kuliko kwa kusoma (III,26), kuvisahau viumbe ili kumuona Muumba wao (III,31), kukwepa mahangaiko katika shughuli (III,39) na elimudunia isivyo na faida (III,43): “Nahitaji kupaa juu ya viumbe vyote, kuacha kabisa nafsi yangu, kuangalia mambo ya Mungu na kufahamu kwamba wewe Muumba hufanani na chochote… Lo! Moyo wa binadamu mjinga kama nini! Unafikiria mambo ya sasa tu, hauangalii ya mbele. Basi, yafaa ujitengeneze kwa mambo yote sawa kama ungalikufa leo hii… Hizi ni siku za kufaa. Kwa nini huzitumii vizuri zaidi basi, upate kustahili neema ya kuishi milele?… Jifunze kufia dunia, upate kuwa hai pamoja na Yesu siku ile. Jifunze sasa kudharau yote, siku ile upate kufika huru kwa Kristo… Usifikiri kitu ila usalama wako; usisumbukie lolote, isipokuwa ya Mungu… Mwanangu, usishindwe na maneno mazuri ya watu hata yakiwa na utaalamu mkubwa. Ufalme wa Mungu haupo katika maneno, bali katika maadili. Sikiliza maneno yangu: huwasha moyo, huangaza akili, huleta majuto ya dhambi, hutuliza kwa namna nyingi... Ukiisha kusoma na kujua mengi, bado ni lazima urudie neno hili lililo msingi wa elimu: kwamba ndimi nimfundishaye binadamu; ndimi niwapaye wanafunzi wangu hekima kubwa kuliko ile wanayoweza kufundishwa na mwalimu yeyote… Chochote kisichokuwa Mungu si kitu; na sharti kihesabiwe vile”.

Mafundisho hayo yaliendelezwa na Yohane wa Msalaba kuhusu kutozingatia neema za pekee ambazo kwa namna fulani ni za nje; kuzikumbuka kwa kujipongeza kunazuia muungano na Mungu. Tumaini linatuinua tumpende kuliko ujuzi wa neema hizo: “Kusudi tuishi kwa tumaini safi kamili kwa Mungu, hatutakiwi kusimama kwenye fahamu, sura na taswira maalumu. Tulivyokwishaeleza, kila zinapojitokeza tumuelekezee mara Mungu roho tupu kuhusu hizo, kwa mruko wa mapenzi yenye hisani. Hatutakiwi kuyafikiria wala kuyazingatia isipokuwa kadiri kumbukumbu yake inavyohusiana na majukumu”. Ndio utakaso halisi wa kumbukumbu inayohangaikia mengi yasiyo na faida au ni ya hatari. Hivyo polepole roho itainuka kumfikiria Mungu na fadhili zake. Kumbe mara nyingi tunaingia kanisani ili kuomba neema inayohitajika haraka, tukisahau kumshukuru Mungu kwa fadhili kuu ya ekaristi inayodai asante ya pekee, kwa kuwa ndiyo ukumbusho wa ahadi za uzima wa milele.

Kujitakasa upande wa akili[hariri | hariri chanzo]

Vipawa vya juu vya binadamu, alivyonavyo sawa na malaika, ni akili na utashi. Hivyo pia vinahitaji kutakaswa na kuratibiwa, kwa kuwa vimevurugwa na dhambi asili na dhambi binafsi. Mtazamo wa kwanza wa akili ya mtoto aliyebatizwa ni mnyofu, na vilevile mtazamo wa mtu anayeanza kuitikia wito kwa bidii. Lakini baadaye mtazamo huo unapotewa na unyofu kutokana na wingi wa mambo anayoyazingatia kwa moyo usio safi. Hapo unahitajika utakaso mkali ili kurudia unyofu wa awali unaoshika mandhari nzima ya maisha usiishie madogomadogo. Wana heri wazee wale ambao, baada ya majaribu na mang’amuzi mengi wanafikia unyofu wa hali ya juu wa hekima halisi waliowahi kuuchungulia kwa mbali. Kwa maana hiyo imesemwa, “Maisha mazuri ni wazo la ujanani lililotekelezwa katika utu uzima”.

Haja ya utakaso huo kutokana na kasoro za akili[hariri | hariri chanzo]

Akili imejeruhiwa na dhambi asili; donda hilo linaitwa ujinga, maana badala ya kuelekea mara ukweli, na hasa ukweli mkuu, akili inapata shida kuufikia: inaelekea kuzamia malimwengu isiinukie sababu zake; inaelekea kudadisi mambo yapitayo, kumbe ina uvivu katika kutafuta lengo letu kuu na njia za kulifikia. Matokeo yake, inadanganyika kwa urahisi, inatiwa giza na mawazo yasiyo na msingi yanayotokana na maono yasiyoratibiwa, hata inaweza ikafikia upofu wa roho. Tofauti na walivyoweza kudhani Waprotestanti wa kwanza na Wajanseni, dhambi asili haikufanya akili isiweze kujua ukweli, bali kwa juhudi za kudumu, pasipo msaada wa ufunuo, inaweza ikajua kweli kadhaa za msingi, k.mf. uwepo wa Mungu. Lakini Mtaguso wa kwanza wa Vatikano ulivyofundisha, wanaoweza juhudi hizo ni wachache, nao pia wanahitaji muda mrefu wasifaulu kujikomboa kutoka udanganyifu wote. Kwa ufunuo wa Mungu ndipo kweli za kimaumbile kuhusu dini zinapoweza kujulikana na wote upesi, kwa hakika na pasipo mchanganyiko wa makosa. Baada ya ubatizo donda la ujinga linaelekea kuwa kovu, lakini linaanza kutona tena kwa dhambi binafsi, hasa udadisi na kiburi cha roho.

Udadisi ni kasoro inayotuelekeza kuwa na hamu ya harakaharaka ya kusoma na kuzingatia mambo yasiyo muhimu, tukipuuzia yale ya Mungu na ya wokovu wa milele. Udadisi huo unatokana na uzembe na kutupotezea muda mwingi. Watu kadhaa wenye elimu ndogo walioshiba kweli za Injili wanapima mambo vizuri. Kumbe wengine, badala ya kujipatia kwa ndani kweli kuu za Ukristo, wanapoteza muda mwingi kukusanya taarifa ambazo hazina faida au walau zinasaidia kidogo kupima mambo: kwa kulimbikiza taarifa bila mpango, badala ya kuunda roho yao, wanaizima kama kwa kuzidisha kuni motoni. Hapo hawaoni tena mwanga wa mawazo makuu ambayo peke yake yanaweza kupanga taarifa hizo na kuwainua kwa Mungu, asili na lengo la vyote. Thoma wa Akwino alifafanua hivi maneno, “Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga” (1Kor 8:1): “Hapa mtume hamkubali anayejua mengi, asipojua namna ya kujua. Namna ya kujua ni kujua utaratibu, juhudi na lengo vinavyompasa: kujua utaratibu ili kukipa kipaumbele kinachochangia zaidi wokovu; kujua juhudi ili kukitamani zaidi kile kinachozaa zaidi upendo; kujua lengo, yaani kwa kujijenga na kumjenga jirani, si kwa majivuno na udadisi”. Adili la kusoma linapinga upande mmoja udadisi wa bure, upande mwingine uvivu wa akili, limuongoze mtu kusoma yale anayotakiwa kuyasoma, kwa namna na kwa wakati wake, tena kwa lengo adilifu na lipitalo maumbile. Udadisi huo ni kinyume cha kuzama ndani ya Mungu, ambako yote yanapimwa kwa kumzingatia yeye. Unaweza kufikishia upumbavu wa roho uliozungumziwa na Mtume Paulo: “Hekima ya dunia hii ni upuzi mbele ya Mungu” (1Kor 3:19). Upumbavu huo ni dhambi, unapingana na kipaji cha hekima, na unatokana hasa na uzinifu. Hapo mtu anapima kijuujuu mambo yote, hata yale makuu, kwa kuyazingatia upande wa chini, k.mf. kufuatana na tamaa au kiburi chake.

Kiburi cha roho ni vurugu kubwa kuliko udadisi; kinafanya tuiamini akili yetu hata tusikubali mashauri, hasa ya wakubwa wetu, wala kujitafutia mwanga kwa kuzingatia kwa makini na unyofu maneno ya wanaotupinga. Hivyo tunakosa wazi busara, na matokeo yake tutalazimika kuyalipa kwa uchungu. Tunafikia kubishana kwa ukali, kushikilia mno msimamo wetu, kudhihaki na kukataa katakata ile yote isiyolingana nao. Tena tunaweza tukafikia kuwakatalia wengine uhuru wa maoni tunaodai kwa ajili yetu, kutokubali miongozo ya viongozi wa Kanisa, kupunguza na kupuuzia dogma tukijisingizia tunataka kuzifafanua vizuri kuliko zamani. Ni hatari kushikilia mno msimamo na kukataa mashauri ya maana: pengine tabia hiyo wanayo watu waliopotoka baada ya kushika maisha ya Kiroho; hapo wana ari chungu inayotaka kulazimisha wote wafuate maoni yao, kana kwamba wao tu wanaye Roho Mtakatifu. Wamejaa kiburi cha roho, wanakosa upendo kwa kisingizio cha kurekebisha yote kandokando yao; wanaweza wakawa maadui wa amani na kusababisha mafarakano makubwa.

Hatimaye kasoro hizo, hasa kiburi, zinaweza zikatufikishia upofu wa akili ambao ni kinyume cha kuzamia mambo ya Mungu. “Ole wenu viongozi vipofu… wanafiki, kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia” (Math 23:16,23-24). Kadiri ya nabii Isaya (taz. 6:9-10), Yesu na Mtume Paulo, upofu huo ni adhabu ya Mungu anayewanyima mwanga wasiotaka kuupokea.

Kuna wakosefu ambao kwa kurudiarudia makosa wamekuwa hawatambui tena matakwa ya Mungu ingawa yameonyeshwa wazi, wala hawatambui kuwa mabaya yanayowapata ni adhabu zake, kwa hiyo hawaongoki. Wanaeleza hayo na matatizo ya kimataifa kwa kutoa sababu za kibinadamu (k.mf. uchumi) wasitambue kuwa sababu kuu ni ya Kiroho, yaani kwamba wengi, badala ya kumfanya Mungu kuwa lengo kuu la maisha yao, wanalenga mali zinazofitinisha kwa sababu haziwezi kuwa zote za wote kwa wakati mmoja.

Upofu huo unamfanya mkosefu apende mali kuliko mema ya milele, asisikie sauti ya Mungu inayomuita. Upofu wa roho ni adhabu yake, lakini ni dhambi pia ambayo tunaacha kwa makusudi kuzingatia kweli za Kimungu tukipendelea tamaa au kiburi chetu. Sawa na upumbavu wa roho, unatuzuia tusione ujirani wa kifo na hukumu, unatuondolea uwezo wa kuona ndani na unatuacha katika hali ya kutoelewa mambo ya juu: k.mf. ukuu wa amri wa upendo, thamani ya damu ya Yesu iliyomwagwa kwa ajili yetu na ya misa inayohudhurisha sadaka ya msalabani. “Kama mwizi anapoiba pesa angepotewa na jicho, wote wangesema ameadhibiwa na Mungu. Kumbe wewe umepotewa na jicho la roho, lakini unadhani Mungu hajakuadhibu” (Augustino).

Tunashangaa kuona Wakristo wenye elimudunia kubwa kuhusu sanaa au sayansi ambao hawajui vya kutosha kweli za dini, tena wanazichanganya na makosa mengi na maoni yasiyo na msingi: kukosa uwiano wa elimudunia na elimudini kunawafanya wabilikimo upande wa roho. Wengine wanaojua zaidi mambo ya imani, historia na sheria za Kanisa, wanaonyesha elekeo ambalo linakwenda kinyume cha hekima na kuwafanya walione Kanisa kwa nje tu, kama mtu anayetazama vioo vya rangi upande wa nje wa jengo, badala ya kuviona upande wa ndani kwa msaada wa mwanga kutoka nje.

Upumbavu huo unatuzuia hasa tusipokee ujumbe wa Mungu akisema kupitia matukio makuu ya leo, tunapoona maelekeo mawili ya kimataifa kushindana moja kwa moja. Upande mmoja ufalme wa Kristo unataka kuvuta wote kwa Mungu aliye uzima wenyewe; upande mwingine elekeo la kuwavuta kwenye mali, anasa na kiburi, hivi kwamba mfano wa mwana mpotevu unatimia kwa mataifa mazima. “Mvutano huo unazidi kuwa mkali mpaka utakaposababisha kitambaa kuchanika... Siku moja ushujaa wa Kikristo utakuwa utatuzi pekee wa matatizo ya maisha. Hapo, kwa kuwa Mungu analinganisha neema zake na mahitaji, asimjaribu mtu kuliko uwezo wake, tutaona kwa hakika utakatifu kuchanua kwa wingi wakati utakaokuwa mbaya kuliko zote za historia ya binadamu” (Jacques Maritain). Juhudi kuu za uovu zitafanyika wakati wa ushindi wa mwisho wa Kristo. Katika mashindano hayo tukimbilie sala na sadaka hata kuliko masomo na utume.

Namna ya kujitakasa upande wa akili[hariri | hariri chanzo]

Ili turekebishe vurugu hiyo tuliyonayo wote, ingawa kwa kiasi tofauti, tunahitaji ustawi wa imani: “Imani ndiyo chanzo cha utakaso wa moyo ili kujikomboa kutoka udanganyifu, halafu imani iliyo hai kwa upendo inakamilisha utakaso huo” (Thoma wa Akwino). Ni lazima akili inayoongoza utashi itakaswe, mzizi wa utashi usiwe umepotoka na kuchanganyikana na udanganyifu. Utakaso huo unategemea imani, inayotufanya kwanza tushike kweli zilizofunuliwa (kwa sababu ya mamlaka ya Mungu aliyezifunua), halafu tuzingatie na kupima yote kadiri ya kweli hizo. Hiyo inamtokea hata mkosefu mwenye imani, lakini hasa mwadilifu kwa kuwa ana vipaji vya Roho Mtakatifu. Hatutakiwi kushikilia tu kweli za imani, bali kwa njia yake kupima yote ambayo tuyawaze, tuyaseme, tuyatende au tuyaepe maishani mwetu. Ndiyo kuamua kwa imani na si kwa fikra za kidunia.

Imani ingawa giza inatuangaza. Ni giza kwa kuwa inatufanya tushike mafumbo tusiyoyaona; lakini mafumbo hayo, yanayohusu maisha ya ndani ya Mungu, yanatuangaza akili tuone wema wake kwetu. Mwanga huo wa safari ni chombo cha muungano na Mungu unaomtambulisha kwetu kwa hakika na kwa namna ipitayo maumbile. Mwanga huo ni wa juu kuliko hakika yoyote tunayoweza kuipata duniani. Yaliyo wazi kwa hisi zetu si ya Kiroho, kwa hiyo si Mungu; yaliyo wazi kwa akili yetu yanaweza kuwa mawazo ya kweli juu ya Mungu, lakini si juu ya maisha yake ya ndani yanayopita maumbile yoyote. Ili tuyaone tunahitaji kufa na kujaliwa heri ya mbinguni; lakini imani inatufikishia maisha hayo tangu sasa katika giza.

Mtu akipenda njozi kuliko imani ya kumiminiwa anadanganyika kwa kupenda yaliyo ya nje, yanayofikiwa na hisi, yaliyo taswira tu, kuliko ukweli wenyewe upitao maumbile. Hivyo hata kama njozi zake ni za kweli anasogea mbali na hali ya kumzamia Mungu. Imani ingawa giza inatuangaza, kama usiku unavyotuwezesha kuona nyota na ukuu wa anga. Ajabu! Katika giza lake tunaona mbali kuliko mchana, tunapozuiwa na mwanga wa jua! Vilevile hisi na akili zetu zinaona maumbile, kumbe imani inatufumbulia ukuu upitao maumbile tutakaouona wazi milele. “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Eb 11:1). “Mambo yale ambayo ukweli wake haujaonekana kwetu, imani inatupa undani wake, kwa kuwa yenyewe ndiyo undani wake” (Yohane Krisostomo). “Imani ni adili la akili, ambalo uzima wa milele unaanza ndani mwetu, ukifanya akili ikubali yasiyoonekana” (Thoma wa Akwino).

Basi, ili tuishi kwa imani, tuzingatie yote kwa mwanga huo: kwanza Mungu, halafu sisi wenyewe, wenzetu wote na matukio ya kupendeza au ya kusikitisha. Tusiyazingatie upande wa hisi au wa akili, bali upande wa imani kwa macho ya Mungu, kidogo anavyoyaona yeye. Hivyo ni wazi haja ya kuitakasa roho kutoka udadisi, tusipende kusoma yasiyo muhimu kuliko kutafakari Injili na yale yanayoweza kulisha roho. Badala ya kusoma mengi ili kujuajua yote na kuyazungumzia, tusome kwa unyenyekevu yaliyo bora ili kuyachimba na kuyatekeleza na kuwafaidisha wengine pia. “Wapo wanaotaka kujua ili wajue tu, na huo ni udadisi; wengine wanataka ili wajulikane, na hayo ni majivuno; wengine wanataka ili wauze ujuzi, na hiyo ni biashara haramu; wengine wanataka ili wajengeke, na hiyo ni busara; wengine wanataka ili wajenge wenzao, na huo ni upendo” (Bernardo). “Elimu ikiwa peke yake, pasipo upendo, inavimbisha kwa kiburi. Muunganishe elimu na upendo, hapo elimu itafaa” (Thoma wa Akwino).

Ni wazi pia haja ya kutopima mambo kwa haraka inayosababisha udanganyifu mwingi; zaidi haja ya kutoshikilia maoni yetu, bali kuyarekebisha kwa kusikiliza Kanisa, kiongozi wa Kiroho, na Roho Mtakatifu anayetaka kutulea kwa ndani. Hapo kuzingatia madogomadogo kusingetusahaulisha ujumla, inavyotokea mara nyingi, kama vile kuona mti kwa jirani mno kunavyotuzuia tusione msitu. Wanaokwazwa na mabaya yanayotokea, na kusema hayaeleweki, wanazingatia mno kwa uchungu madogomadogo ya tabu na kusahau ujumla wa mpango wa Mungu ambamo yote yanalenga faida ya wanaompenda. Kumbe mtazamo wa jumla ukiwa safi ni wa juu tayari. Hivyo mtoto akitazama nyota anahisi ukuu wa Mungu. Baadaye akichimba sayansi huenda akasahau mtazamo wa jumla, ambao akili inapaswa kuurudia ili kuona undani wake. Elimu kidogo inasogeza mbali na dini, kumbe elimu ya juu inarudisha kwake.

Kuna watu wawili walio sahili hasa: mtoto ambaye hajaanza kujua uovu, na mzee mtakatifu aliyeusahau kwa kuushinda mfululizo; kwa hiyo mzee anampenda mtoto na kupendwa naye. Upande wa sala, mtazamo wa kwanza ni ule wa mtoto mbele ya pango la Noeli; mtazamo wa dhati ni ule wa mwanasala mwishoni mwa maisha yake. Kwa mtawa, mtazamo wa kwanza ulio mnyofu na wenye kupenya ni ule alionao anapoitikia wito wa Mungu; mara nyingi mtazamo huo ni wa juu kuliko mambo mengi atakayoyazingatia baadaye. Heri watakaourudia, wakitazama kwa hekima undani wa maisha yao yote.

Vivyo hivyo, matokeo makuu yaliyokusudiwa na Mungu ili kuangaza na kuokoa wanyofu, kama yale ya Lurdi, yanawaelea kwa urahisi wenye moyo safi, wanaoona upesi asili yake ya Kimungu, maana na uzito wake. Tukiacha mtazamo huo na kuzingatia madogomadogo tunaweza tukashindwa kuelewa chochote. Hatimaye elimu ya juu ikiendana na unyenyekevu, inarudisha kwenye mtazamo wa kwanza na kuuthibitisha ili kutambua kazi ya Mungu na faida ya roho. Baada ya kusoma miaka mingi falsafa na teolojia, mtu anarudi kwa furaha kwenye imani nyofu ya Abrahamu, Isaka na Yakobo, kwenye maneno ya Zaburi na mifano ya Injili. Ndio utakaso unaoiandaa akili kuzama katika mafumbo. “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru” (Math 6:22).

Kujitakasa upande wa utashi[hariri | hariri chanzo]

Utashi ndio kipawa cha juu kinachotuelekeza kwenye mema yaliyojulikana na akili. Kwa kuwa unalenga mema yoyote, unaweza kuinuka umpende Mungu aliye wema mkuu. Kila kipawa cha binadamu kinaelekea jambo maalumu lililo jema kwake (k.mf. macho yanaelekea vinavyoonekana), lakini utashi unaelekea mema ya mtu mzima na kuelekeza vipawa vingine vyote vitekeleze kazi yake (k.mf. akili itafute ukweli): ndiyo sababu utashi ukiwa mwadilifu, basi mtu ni mwema. Kinyume chake, utashi usipokuwa mnyofu unavyotakiwa, usipoelekea yaliyo mema kweli kwa mtu mzima, huyo anaweza akawa mwanasayansi mzuri, lakini si mtu mwema: ana umimi, na maadili anayoonekana kuwa nayo yanatokana hasa na kiburi, hofu ya kusumbuliwa n.k. Hiari ya utashi inafanya yawe na stahili si matendo yake maalumu tu, bali pia yale ya vipawa vingine vyote. Kwa hiyo kuratibu utashi ni kuratibu mtu mzima. Basi, tuone kasoro na upotovu vilivyomo ndani mwake kutokana na dhambi asili na dhambi binafsi.

Kasoro kuu ya utashi: umimi[hariri | hariri chanzo]

Nguvu ya utashi kwa kutenda na kuongoza vipawa vingine inatokana na usikivu wake kwa Mungu, kwa kuwa ukilingana na matakwa yake, hapo nguvu ya Mungu inaufikia. Ndilo wazo kuu la suala zima. Tunaona maana yake yote tukikumbuka kuwa katika uadilifu asili, utashi ulipokuwa chini ya Mungu kwa upendo na utiifu, uliweza kuzuia vurugu zote za hisi: maono yalikuwa chini ya utashi uliohuishwa na upendo. Lakini baada ya dhambi asili tunazaliwa huku utashi wetu haumuelekei Mungu, nao ni dhaifu kwa kutekeleza wajibu wowote, hata wa kiutu tu. Tunazaliwa huku utashi wetu unaelekea kujipendea. Ndilo donda la uovu linalojitokeza katika umimi mkubwa unaochanganyikana na kila tendo letu na ambao tunapaswa kujihadhari nao. Kwa hiyo utashi, kisha kuwa dhaifu kwa kutomtii Mungu, hauna tena mamlaka kamili juu ya hisi, bali unaweza tu kuzibembeleza zikubali kuutii. Baada ya ubatizo uliotuzaa upya donda hilo linaelekea kupona sawa na mengine; lakini linaanza tena kutoneshwa na dhambi binafsi.

Kasoro kuu ya utashi ni kujipendea kwa kusahau upendo unaotupasa kwa Mungu na kwa jirani: ndiyo asili ya dhambi zote. Matakwa yetu yasiyolingana na yale ya Mungu ni hatari kwa kuwa yanaweza kupotosha mambo yote: hata yaliyo bora yanakuwa mabaya yakitokana na matakwa yetu, kwa kuwa yanajifanya lengo badala ya Mungu. Bwana akiyaona katika mfungo, sadaka n.k. anavikataa kama vitendo vya dini vilivyofanywa ili kujionyesha. Matakwa yetu yanatokana na umimi, kansa ya utashi inayouharibu zaidi na zaidi. Utashi unahitaji kutakaswa na kuundwa Kikristo kwa njia ya ustawi wa upendo “unaounganisha binadamu na Mungu, ili mtu asiishi kwa ajili yake bali kwa ajili ya Mungu” (Thoma wa Akwino).

“Inafaa ujue sana kwamba kujipendea kuna hasara inayopita hasara zote za ulimwengu. Upendacho na kufurahiwa nacho, ndicho kinachokunasa. Upendo wako ukiwa safi na kunyoka sawa, ukiongoka vema, hutaweza kufungwa mapingu na kiumbe chochote. Basi, usitamani jambo liwezalo kukupinga na kupunguza uhuru wa moyo wako. Kwa nini hujiweki mikononi mwangu kwa moyo wako wote, wewe pamoja na yote uliyo nayo, na pupa zako zote? Ni ajabu kweli! Kwa nini kupata majonzi ya bure? Kwa nini kuhangaika kwa tabu isiyo na maana? Simama thabiti katika hali ninayotaka mimi, hutapata hasara. Ukizidi kutamani leo mambo haya na kesho mambo mengine, au ukitaka kwenda mara huku mara huku upendavyo mwenyewe, hutatulia kamwe; hutakosa tabu hata siku moja. Hii ni kwa sababu kila jambo lina shida yake; kila mahali pana mtu atakayekusumbua” (Kumfuasa Yesu Kristo III,27:1-2).

“Ubinadamu ni mwerevu, huvuta wengi katika mitego, huwanasa. Kila mtu anaelekea kujipendea… Hitilafu zetu hazitaki kukomeshwa, wala kuzuiwa, wala kushindwa, wala kuamriwa, wala kutii… Maelekeo yetu ni kujitafutia raha na kuona njia ya kujipatia faida kwa watu wengine… tunapenda sana kupokea sifa na heshima… tunaogopa kupata aibu na dharau… tunapenda uvivu na kupumzisha mwili… tunataka mambo ya ajabu yanayong’ara, hatutaki yale hafifu yasiyo na thamani… tunathamini sana malimwengu, tunafurahia faida ya kidunia, tunakasirikia hasara, tunashika hamaki tunapokosewa kidogo… Ubinadamu wetu hupenda mali, hutamani kupata, si kutoa. Kwa ubinadamu wetu tunapenda vitu viwe vyetu… Ubinadamu wetu huelekea viumbe na mwili na upuuzi na maongezi mengi… hujivunia cheo au asili maalumu, hubembeleza wakuu, husifu wenye mali, hukubali walio na tabia ileile… hulalamikia upesi masumbuko na ukosefu wa vitu… hutamani kutambua mambo ya siri na kusikia mapya. Hupenda kuonekana mbele za watu na kusikia matamu mengi nafsini mwake. Hupenda kujulikana na kutenda maajabu yanayovutia sifa za watu… Kadiri ubinadamu unavyovunjwa na kuzuiwa, neema huongezwa, na kwa msaada wa neema hiyo mtu hugeuka polepole kuwa mpya kwa mfano wa Mungu” (Kumfuasa Yesu Kristo III,54:1-8).

Kadiri ya Katerina wa Siena, kujipendea “kunatia giza na kupunguza upana wa mandhari ya akili, ambayo hatimaye inaona na kutambua tu kwa mwanga bandia wa jema danganyifu, wa aina ya furaha ambayo pendo linashikamana nayo… Kujipendea kumetia sumu katika ulimwengu na katika mwili wa fumbo wa Kanisa, na kulijaza bustani ya Bibi arusi magugu yanayonuka”. Kunatufanya tuwakosee haki Mungu, kwa kutompatia utukufu unaompasa, na majirani, kwa kutowapatia mema wanayoyahitaji. Hatimaye kujipendea, kwa kupindua utaratibu uliowekwa na Mungu katika utashi wetu, kunatufikishia kufadhaika, kukata tamaa, kugombana, kufarakana na kukosa amani, ambayo ni utulivu wa utaratibu, kwa hiyo unapatikana tu katika wale wanaompenda Mungu kuliko nafsi yao na kuliko yote.

Utakaso wa utashi kwa ustawi wa upendo wa Mungu[hariri | hariri chanzo]

Tutawezaje kuurudishia utashi, ambao umedhoofika na kulemaa kwa kiasi fulani, nguvu ya kushinda uzembe na kiburi, ambacho ni udhaifu uliofichika nyuma ya kinyago cha nguvu? Tukikumbuka uadilifu asili, tunapaswa kuutiisha zaidi na zaidi utashi wetu kwa ule wa Mungu: hapo atazidi kutujalia neema tuendelee katika njia ya ukamilifu. Tuuunde kwa njia ya ustawi wa maadili yanayotarajiwa kuwemo ndani yake: adili la haki linalompatia kila mmoja yale anayostahili; adili la ibada linalompatia Mungu heshima inayotupasa kwake; adili la toba linalofidia chukizo la dhambi; adili la utiifu kwa wakubwa; adili la ukweli na uaminifu; hasa adili la upendo kwa Mungu na kwa jirani.

Katika utekelezaji wa maadili yote, kuyatii matakwa ya Mungu kunadai tukatae matakwa yetu yasiyolingana nayo. Roho ya sadaka tu, kwa kufisha ndani mwetu umimi, inaweza kuhakikishia upendo wa Mungu ushike nafasi ya kwanza na kutupa amani. Amani ya ndani haipatikani pasipo roho ya sadaka, ambayo tuwe tayari kuacha yote ili kutimiza matakwa ya Mungu: “Ee Mungu, moyo wangu u thabiti” (Zab 108:1). Tuseme kila siku aliyoyasema Mtume Paulo alipoongoka, “Nifanye nini, Bwana?” (Mdo 22:10).

Kwa watu kadhaa utakaso huo ni mgumu zaidi kutokana na marudio ya makosa, tena kwa wote hauwezekani pasipo neema ya Mungu, kwa kuwa upendo wake tu unaweza kushinda na kufisha umimi. Upendo huo ukistawi, magumu yanakuwa rahisi: “Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi” (Math 11:30). Utawani kazi hiyo inarahisishwa na utiifu, unaonyosha na kuimarisha utashi kwa kuulinganisha zaidi na zaidi na matakwa ya Mungu yanayojulikana kwa njia ya katiba na maagizo ya wakubwa.

Ili tufaulu kutakasa na kuimarisha utashi, ni lazima tutende kadiri ya misimamo ya imani ya Kikristo, badala ya kufuata ugeugeu wa roho yetu inayobadilika kadiri ya hali na rai za umma. Kisha kutafakari mbele ya Mungu na kumuomba neema, tutende kwa uthabiti kadiri ya wajibu wetu na ya matakwa yake. Nguvu halisi ya utashi ni tulivu, kwa hiyo ni dumifu pia, haikati tamaa kwa kushindwa kwa muda wala kwa donda lolote. Kushindwa tunashindwa tu tukiacha mapambano, na anayemfanyia kazi Bwana, anamtegemea badala ya kujitegemea.

Kimsingi, utashi imara ni ule usiojengeka juu ya kiburi, bali juu ya Mungu na neema yake inayotupasa kuiomba kila siku kwa tumaini nyenyekevu. Tukidumu kuomba hivyo neema za lazima kwa utakatifu na wokovu, hakika tutajaliwa tulivyoahidiwa, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa” (Math 7:7). Sala ndiyo nguvu yetu katika udhaifu: “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” (Fil 4:13). Ndivyo anavyopaswa kusema hasa anayefia dini. Hapo utashi una nguvu ya Kimungu: “Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana” (Zab 18:1). Kwa neema utashi wa mtu unashiriki uweza usio na mipaka wa Mungu na unajikomboa kutoka umimi, kutoka mvuto wa yale yote ambayo yanausogeza mbali na Mungu na kuuzuia usiwe mali yake tu. Kujikana na roho ya sadaka ndiyo njia pekee ya kuungana naye kwa upendo wake kushinda umimi. Anayejichukia kitakatifu hivyo anaokoka milele na kupata tangu hapa duniani amani na muungano na Mungu ambavyo ni mwonjo halisi wa uzima wa milele. Ndiyo malezi halisi ya utashi.

Kutoambatana na lolote[hariri | hariri chanzo]

Yohane wa Msalaba ameacha mafundisho bora kuhusu kukataa kikamilifu matakwa yetu, akielekeza njia ya mkato ya kufikia ukamilifu, na akionyesha ugumu wa njia nyembamba unavyofikishia utamu wa muungano na Mungu. Tukikumbuka ukuu wa lengo, hatutadhani anatudai mno. Aliyepania kupanda mlima mrefu, hasimami akipata shida; anajua zinahitajika juhudi, kwa hiyo anajikaza na kusonga mbele moja kwa moja. Ndivyo anavyopaswa kufanya aliyepania kufikia kilele cha ukamilifu. Hapa tunafupisha mafundisho hayo kuhusu kutoambatana na yale yote yasiyo Mungu wala matakwa yake.

Tusiambatane na mema ya nje, mali na heshima: “mali izidipo msiiangalie sana moyoni” (Zab 62:10). Tusiambatane na mema ya mwili, uzuri na afya: ni upotovu kuthamini kuliko muungano na Mungu hayo yatakayopita kama maua. Kumbe tunajali afya kuliko tunavyodhani; kuondolewa moja kwa moja ni sadaka kubwa kwetu, lakini ni sadaka tunayoweza kudaiwa. Tusijipongeze kwa maadili tuliyonayo: ni majivuno na pengine dharau kwa jirani. Tuthamini maadili si kama mali yetu, bali kadiri yanavyofikisha kwa Mungu. Tukipata faraja katika sala tusiambatane nazo, la sivyo tutafuata kiburi cha roho na kuzigeuza kizuio badala ya msaada kwa kumuendea Mungu; tutasimama kwa umimi katika kiumbe na kuigeuza njia kuwa lengo. Si kila kinachong’aa ni dhahabu, hivyo tunapaswa kuwa macho. “Utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa” (Math 6:33), yaani yale yote yanayofaa kwa roho na kwa mwili, hata matatizo ambayo yanatuondolea udanganyifu na kuturudisha kwenye njia yenyewe. Hatimaye, tukijaliwa neema za pekee tusiambatane nazo, kwa kuwa, “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao” (1Kor 13:1). “Msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni” (Lk 10:20).

Kuhusu kipaji cha kuhubiri, Yohane wa Msalaba aliandika, “Sikanushi kuwa mtindo wa hali ya juu, ujuzi mkubwa wa mafundisho, lugha bora na vitendo vya kupendeza vinaweza kuwa na matokeo makubwa, mradi vyote vihuishwe na roho ya ibada sana, la sivyo itabaki nini? Hisi zimeridhika, na akili vilevile, lakini utashi haujapenywa na moto wala utomvu. Badala ya kuwa tayari kwa lolote, unajikuta mwoga na dhaifu kama kwanza, ingawa yamesemwa mambo mazuri ajabu, tena kwa ufasaha kamili… Maneno hayo yote mazuri yanayeyuka na kusahaulika kwa sababu hakuna lililowasha utashi”. Ni lazima mhubiri atakase nia yake ili Neno la Mungu lizae matunda ya kudumu milele; aishi kwa sadaka na kujikana ili upendo wa Mungu na wa jirani uhakikishiwe nafasi ya kwanza ndani yake.

Tunda la utakaso huo wa utashi ni amani, ambayo si furaha daima, ila inaelekea zaidi na zaidi kuwa ya dhati na ya juu, na kuenea hata kwa watu wasiotulia ikiwafanya wamjue na kumpenda Mungu.

Kiutekelezaji, kila mmoja ajiulize: je, roho ya kujikana inastawi au kufifia ndani mwangu? Ikiwa majikanio ya nje yamekwisha, maana yake hata ya ndani yametoweka, hatulengi tena ukamilifu, tumekuwa chumvi isiyo na ladha. Tumuombe Bwana atujulishe tunavyozuia kazi yake ndani yetu, pengine bila kujitambua; halafu atupe nguvu ya kuondoa vizuio hivyo, na tukiwa walegevu katika kuviondoa, aviondoe mwenyewe. Hapo tutapokea misalaba mingi, lakini yenyewe itatubeba kuliko sisi tunavyoibeba, kama vile ndege anavyoinuliwa na mabawa kuliko kuyainua. Ndiyo njia halisi ya kuingia ufalme wa Mungu.

Kupona kiburi[hariri | hariri chanzo]

Ili tukamilishe tuliyoyasema juu ya kujitakasa, tunapaswa kuzungumzia uponyaji wa maradhi mawili ya roho yanayotuua kwa hakika, yaani kiburi na uzembe.

Dawa kuu ya kiburi ni kutambua kimatendo ukuu wa Mungu, asili ya mema yote ya kimaumbile na yapitayo maumbile: “Maana ni nani anayekupambanua na mwingine? Nawe una nini usichokipokea? Lakini iwapo ulipokea, wajisifia nini kana kwamba hukupokea?” (1Kor 4:7). “Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lolote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu watoka kwa Mungu” (2Kor 3:5). “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Fil 2:13). Mema si mali yetu, bali yanakusudiwa kumtukuza Mungu, asili yake.

Dawa ya kiburi ni kujikumbusha kwamba sisi si kitu, tumeumbwa kwa upendo wa bure wa Mungu anayetudumisha kwa hiari, la sivyo tungerudia utovu wa vyote. Tukiwa na neema, ni kwa sababu tu Yesu ametukomboa kwa damu yake.

Dawa ya kiburi ni pia kujikumbusha kwamba ndani mwetu tuna hali duni kuliko ile ya kutokuwepo, yaani vurugu ya dhambi na matokeo yake. Tukiwa wakosefu, tunastahili dharau na aibu yoyote; ndivyo watakatifu walivyoona, vizuri kuliko sisi.

Hatimaye, tunawezaje kujikuza kwa stahili zetu kana kwamba zingetokana nasi tu? Pasipo neema inayotia utakatifu na neema za msaada tusingeweza kutenda lolote la kustahili. “Mungu akituza stahili zetu anatuza zawadi zake” (Augustino).

Hakika hiyo isibaki nadharia tu, bali iongoze matendo yetu. “Anayejijua vema anajidharau asipendezwe na sifa za watu… Ukitaka kujua kitu kinachofaa kufunzwa vema, usipende kujulikana, ila uvumilie dharau… Hata ungemuona mtu kutenda dhambi kwa wazi, au kufanya makosa makubwa, si lazima ujione mwema kumshinda yeye; kwa sababu hujui utasimama wima siku ngapi. Sisi sote tu dhaifu; lakini wewe sema hakuna mtu dhaifu kuliko ulivyo… Usione haya kuwatumikia watu wote kwa ajili ya Yesu Kristo, ukaonekane maskini hapa duniani… usitegemee elimu yako… ila uitumainie neema ya Mungu, mwenye kusaidia wadogo na kushusha wenye kiburi… Usijione mwema kushinda wengine; kwa kuwa labda Mungu anayejua binadamu kwa ndani kabisa, atakuona wewe mwovu kuliko wao… mara nyingi hapendezwi na mambo yanayopendeza binadamu… Mtu mnyenyekevu ana raha siku zote, bali moyo wa mtu wa majivuno una wivu na hasira nyingi… Mungu humtunza mnyenyekevu, humuokoa, humpenda, humtuliza. Mungu humuelekea mnyenyekevu, humpa neema nyingi… Mtu mnyenyekevu hufumbuliwa na Mungu mambo yaliyositirika, huvutwa naye, hualikwa naye” (Kumfuasa Yesu Kristo I,2:1-4; I,7:1-3; II,2:2).

Ili tufikie unyenyekevu huo tunahitaji utakaso wa ndani. Ule tunaojipatia hautoshi, mpaka tutakaswe na mwanga wa vipaji vya Roho Mtakatifu unaotuondolea kitambaa cha kiburi tuone vizuri undani wetu wa udhaifu na unyonge, pamoja na faida ya aibu na matatizo, hata tuseme, “Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, nipate kujifunza amri zako” (Zab 119:71). “Inatufaa kuvumilia upinzani, watu wakitudhania vibaya hata tunapotaka kutenda mema. Mambo hayo yanasaidia unyenyekevu na kutukinga na majivuno” (Kumfuasa Yesu Kristo I,12:1). Katika matatizo ndipo tunapoweza kujifahamu na kujua tunavyohitaji msaada wa Mungu.

Baada ya kutakaswa hivyo, kiburi na matokeo yake vitajitokeza kidogo zaidi na zaidi. Badala ya kuwaonea kijicho wenye sifa kubwa kuliko sisi, tutajiambia kuwa mkono unatakiwa kufurahi kwamba jicho linaona na hivyo kuufaidisha mkono pia. “Kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho” (1Kor 12:26). Basi, katika mwili wa fumbo wa Kanisa, tunapaswa kufurahia kitakatifu sifa njema za jirani; hata tusipokuwa nazo, tunafaidika nazo. Tena tunapaswa kufurahia yale yote yanayoweza kuchangia utukufu wa Mungu na wokovu wa watu. Hapo tunarudishiwa unyofu wa kupenya mambo, ambao polepole unatuingiza katika uzima wa ndani wa Mungu.

Kupona uzembe[hariri | hariri chanzo]

Kati ya mizizi ya dhambi, mmojawapo unapingana moja kwa moja na upendo wa Mungu na furaha inayotokana na bidii ya kumtumikia: kilema hicho kinaitwa uzembe. Ni lazima tukizungumzie ili kukamilisha yale tuliyoyasema kuhusu kujitakasa upande wa utashi.

“Tunapaswa daima kukimbia dhambi, lakini kuhusu kishawishi kinachoelekeza kwake, pengine ni vema kukikimbia, pengine ni afadhali kupambana nacho. Tunapaswa kukikimbia ikiwa kukizingatia kunazidisha hatari; ndivyo tunavyopaswa kukimbia kishawishi cha uzinifu… Kinyume chake tupambane nacho ikiwa kulizingatia jambo linalokisababisha kunaondoa hatari inayotokana na kuliona kijuujuu tu. Ndivyo ilivyo kuhusu uzembe, kwa sababu kadiri tunavyofikiria mema ya Kiroho tunapendezwa nayo, na ukinaifu unaotokana na kuyajua kijuujuu tu unakuja kutoweka” (Thoma wa Akwino).

Basi, tushinde uzembe kwa upendo wa Mungu, kwa utayari wa utashi kumtumikia hata hisi zikiwa kavu. Tuzingatie mema ya milele tuliyoahidiwa. Ili tupate roho hiyo ya imani pamoja na juhudi kubwa ya upendo kwa Mungu, tujifunge kutoa kila siku sadaka fulani katika yale yanayotushinda zaidi (k.mf. kuamka saa iliyopangwa au kujiweka tayari kutumikia wote). Hatua ya kwanza ndiyo ngumu. Baada ya kujitahidi wiki moja, jambo limeshakuwa rahisi zaidi.

Dawa mojawapo ni unyofu wa dhati kuhusu nafsi yetu na kwa muungamishi, utafiti makini wa dhamiri kila siku, utekelezaji wa mfululizo wa wajibu wetu, uaminifu katika sala na katika kumtolea Mungu matendo yote. Maadamu hatuna mengi yanayostahili, tumtolee mara nyingi damu azizi ya Yesu na sadaka inayodumu katika moyo wake wa Kimungu.

Hasa sadaka fulani kila siku itafaa kuyarudishia maisha ya Kiroho nguvu na ubora: polepole juhudi halisi itarudi hata pasipo umotomoto wa hisi, ambao tukubali kupungukiwa nao kama malipizi ya makosa yaliyopita. Ni vema pia kupanga matumizi ya kidini ya saa za siku (kwa kuadhimisha vipindi vya liturujia au Rozari n.k.) na ya siku za wiki (kufuatana na mafumbo ya imani yaliyo kanuni ya maisha yetu). Hivyo, badala ya kupoteza muda unaokimbia, tutarudi kufaidika nao na kujipatia uzima wa milele. Polepole tutaona tena furaha ya Kiroho aliyozungumzia Mtume Paulo, “Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu” (Fil 4:4-7).

Uchelewaji na sababu zake[hariri | hariri chanzo]

Unahitajika uongofu wa pili ili, kwa bidii kubwa walau kiasi, tuvuke kutoka hatua ya utakaso ya wanaoanza kuingia ile ya mwanga ya wanaoendelea. Lakini wengine hawavuki kamwe: ni wachelewaji, ni kama watoto wenye matatizo wasiovuka vizuri ubalehe, na hivyo, bila kubaki watoto, hawafikii kamwe ukomavu wa mtu mzima. Inasikitisha kuwa pengine wachelewaji hao, wasiopangika kati ya wanaoanza wala kati ya wanaoendelea, ni idadi kubwa. Wengi wao waliwahi kumtumikia Mungu kwa uaminifu; kumbe sasa karibu hawajali kitu. Kwa hakika wametumia vibaya neema zake, la sivyo angeendeleza kazi aliyoianza ndani mwao, kwa sababu hawanyimi msaada wanaofanya wanavyoweza. Hapa chini zitatajwa sababu za uvuguvugu huo.

Uzembe katika mambo madogo[hariri | hariri chanzo]

Uzembe huo unaonekana mwepesi, kumbe unaweza ukawa na matokeo mazito. Kama vile matone ya maji yanavyochimba polepole mwamba, na kama vile matone ya mvua yanavyoleta uhai katika ardhi kavu, ndivyo matendo mema yakirudiwarudiwa yanavyozaa zoea jema (adili la kujipatia) na kulidumisha na kulistawisha; yakitokana na adili la Kimungu, yanapata listawi. Toka alfajiri hadi usiku maadili yanaunda stahili zetu. Katika utumishi wa Mungu mambo yanayoonekana madogo ni makubwa kwa kuwa yanahusiana naye. Tunatakiwa kuyatenda kwa imani, tumaini na upendo, maadili yapitayo maumbile. Tukifanya hivyo, tunamkumbuka daima Mungu na kuishi kwa ajili yake, kwa kuongozwa na Roho wake, badala ya kuishi kibinadamu, kufuatana na umimi. Polepole ndani mwetu ari kwa utukufu wa Mungu na kwa wokovu wa watu inakua.

Kuzembea mambo madogo ya utumishi huo kunasababisha mapema uzembe katika yale makubwa na kumfanya padri au mtawa, k.mf. asali Sala ya Kanisa pasipo roho ya ibada, asijiandae vya kutosha kwa misa, aiadhimishe kwa kulipua au kuihudhuria pasipo uangalifu unaotakiwa. Hatimaye katika mteremko huo anakuwa tu afisa wa dini, akishughulikia mambo matakatifu kwa uzembe, na kuzingatia yale yanayompatia sifa kama mwalimu, mwandishi, mhubiri au mtendaji. Polepole umuhimu wa maisha unahama kutoka sadaka ya misa kwenda utendaji wa binafsi anapotafuta mambo yake badala ya lengo halisi lipitalo maumbile, hata akasahau wokovu wa watu na yale unayoyadai. Usahaulifu huo unasababisha asizae kitu. Kwa kawaida anayepuuzia madogo atafikia hatua ya kupuuzia makubwa pia: hapo hataweza kukabili magumu anayoweza kudaiwa.

Kukataa sadaka zinazodaiwa[hariri | hariri chanzo]

Sababu ya pili ya uvuguvugu ni kumnyima Bwana sadaka anazoziomba. Wengi wanajisikia kuitwa waishi kikamilifu zaidi, kwa kulenga sala hasa na kutekeleza unyenyekevu ambao usipokuwepo hapana maadili halisi. Lakini wanakataa ama moja kwa moja ama kwa kujisingizia. Hawataki kusikiliza maneno yanayokaririwa katika mwaliko, “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake: Msifanye migumu mioyo yenu” (Zab 95:7-8). Mara kadhaa wanaoshughulikia kitu kinachowatambulisha wanajisemea, “Kwa kweli, jambo la kwanza lingekuwa niwe mtu wa sala: kutenda lolote la nje ni bure nisipoungana na Mungu”. Inabidi wajikane ili kumlenga Mungu badala ya umimi. Wakikataa kutoa sadaka hiyo, wanabaki nyuma, huenda wakachelewa moja kwa moja. Hapo wanapoteza ari na kuambatana na dhambi fulani nyepesi (yaani kuwa tayari kuitenda kwa makusudi ikipatikana nafasi), hatimaye wanakuwa na nia imara ya kudumu katika hali hiyo.

Elekeo la kucheka watu[hariri | hariri chanzo]

Sababu nyingine tena zinaweza kusababisha uvuguvugu: kutojali dhamiri (k.mf. kwa kusema uongo usiomdhuru jirani); uzembe ambao hatimaye unamfanya mtu aache kupambana na kasoro zake na kilema tawala. Hivyo anafikia kupuuzia ukamilifu asiulenge tena kweli. Anasahau kwamba labda ameahidi kuulenga kwa njia ya mashauri ya Kiinjili; anasahau hasa ukuu wa amri ya upendo.

Kati ya sababu za uvuguvugu tutambue hasa kilema cha kucheka watu kinyume cha haki. Kumfanya mtu achekwe ni kudhihirisha kwamba hatumheshimu; inaweza kuwa dhambi ya mauti ikihusu mambo au watu wanaostahili heshima kubwa (mambo matakatifu, wazazi, wakubwa, watu waadilifu). Dhihaka hizo zinaweza kuwa nzito kwa matokeo yake, kwa kupotosha walio dhaifu wasitende mema. “Mimi ni mtu wa kuchekwa na jirani yake, ni mtu niliyemwita Mungu, naye akanijibu” (Ayu 12:4). Dhihaka za kutisha toka juu zinakuja kuadhibu zile za hapa chini: “Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana anawafanyia dhihaka” (Zab 2:4).

Anayedhihaki ni mchelewaji anayechelewesha wengine na hivyo anakuwa chombo cha shetani bila kujitambua. Msimamo wake ni kinyume cha unyofu wa Kiinjili na cha sala ya kumiminiwa. Asiyetaka kutumia wema anamfanya mwadilifu achekwe, kwa kusisitiza kasoro zake na kuchafua sifa zake njema kwa sababu anajiona hana maadili kama yeye, lakini hataki kuungama alivyo nyuma. Basi, kwa chuki anapunguza thamani halisi ya jirani na haja ya uadilifu wenyewe. Anaweza akadhuru walio dhaifu kwa kuwatia woga, na anapopotea anaweza akachangia upotovu wao.

Matokeo mabaya ya hali hiyo[hariri | hariri chanzo]

Wachelewaji wanaweza wakafikia upofu wa roho na ugumu wa moyo, hivi kwamba ni vigumu kuwafanya wajirekebishe. “Mtaona kwa urahisi zaidi umati wa watu wa ulimwenguni kuacha vilema na kushika maadili, kuliko kuona mtawa mmoja ameacha maisha vuguvugu kwenda maisha ya bidii” (Bernardo wa Clairvaux). Kadiri mchelewaji alivyowahi kufika juu, anguko lake linastahili lawama na uongofu wake unakuwa wa shida; kwa kuwa anafikia hatua ya kudhani hali yake inaridhisha, hana tena hamu ya kupanda juu zaidi. Mtu asipoitambua saa ya kutembelewa na Bwana, pengine hiyo haitarudi kabla hajaomba sana. Wachelewaji wako hatarini: inafaa tuwakabidhi kwa bikira Maria awaombee neema ya kufufua hamu ya ukamilifu. [1]

Yatokanayo ni kutamani vyeo, kutaka sifa upande wa elimu na kujitafutia starehe: mambo yanayopingana wazi na maendeleo ya Kiroho. Ni muhimu kukesha ili utendaji uongozwe na maadili ya Kimungu. Hayo na matendo yake ni bora kuliko utendaji wowote wa kimaumbile. Kukanusha ukweli huo ni uzushi. Lakini haitoshi kuukiri kinadharia tu, halafu kimatendo kutia maanani k.mf. masomo kuliko maisha ya imani, tumaini na upendo; au kulipua misa ili kuokoa muda kwa ajili ya kazi isiyoweza kuzaa isipohuishwa na roho. Ili kukwepa hatari hiyo tukumbuke mara nyingi kuwa Mungu kwa huruma yake anatujalia mfululizo neema tutekeleze vizuri zaidi amri kuu, yaani tulenge upendo kamili: maisha yetu yatakapotua tutahukumiwa juu ya ukweli wa upendo wetu.[2]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. “Kuna aina nne za watawa: wengine wakamilifu; wengine waovu, wenye kiburi, wanaojiamini, wanaofuata hisi zao, maadui wa taratibu; wengine vuguvugu, waoga, wasiojali, wazembe; hatimaye wengine waadilifu ambao wanalenga ukamilifu, ingawa labda hawataufikia kamwe. Hata mashirika matakatifu zaidi yanaweza yakawa na aina hizo nne za watu, kama yale yaliyolegea; ila katika shirika lililoanguka kutoka juhudi zake za awali, umati unaundwa na watawa vuguvugu, halafu kati ya wanaobaki kuna waovu kadhaa, idadi ndogo ya watu wanaofanyia kazi ukamilifu, na wachache sana waliokamilika. Kumbe katika shirika ambapo taratibu zinashikwa bado, umati ni wa watu wanaolenga ukamilifu, halafu kati ya wanaobaki kuna wakamilifu kadhaa, idadi ndogo ya watawa vuguvugu na wachache sana walio waovu. Hapa tunaweza kuona jambo muhimu: kwamba shirika la kitawa linaelekea kurudi nyuma idadi ya walio vuguvugu inapoanza kuwa sawa na ile ya wenye juhudi, yaani ya wale wanaojitahidi kila siku kupiga hatua mpya katika sala, mkusanyo wa mawazo, ufishaji, usafi wa dhamiri na unyenyekevu. Kwa kuwa wasio na juhudi hizo, hata wakijihadhari na dhambi ya mauti, wanatakiwa kuhesabiwa vuguvugu na wanaambukiza wengine wengi, wakidhuru sana shirika lote. Hao wako hatarini ama mwa kutodumu katika wito ama mwa kutumbukia katika kiburi cha ndani na katika maovu makubwa mno. Wajibu wa viongozi katika nyumba za kitawa ni kufanya kwamba, kwa mifano yao bora na kwa maonyo, maongezi ya ana kwa ana na sala, wale wote walio chini yao wadumu kati ya wenye juhudi wanaolenga ukamilifu, la sivyo wataadhibiwa wenyewe namna ya kutisha. Kuna mambo manne ambayo yanaharibu maisha ya Kiroho na ni misingi ya misimamo mibaya inayopenya jumuia takatifu: 1) kudanganywa na mvuto wa akili na wa sifa za kibinadamu tu; 2) kujitafutia marafiki kwa malengo ya kibinadamu; 3) kutenda kisiasa kwa kufuata busara ya kibinadamu tu, yaani kutumia ujanja ulio kinyume cha unyofu wa Kiinjili; 4) kujitafutia mapumziko mengi mno katika burudani za ziada, au maongezi na masomo yanayoridhisha umbile tu” (Alois Lallemant).
  2. Kadiri ya Y. Tauler, kwa kuwa dhambi yoyote na laana ya milele zinatokana na umimi, inatufaa kuujua kuliko kujua ulimwengu wote. Dalili yake ni kujifanya lengo la yote, badala ya kumlenga Mungu. Ukionyesha upendo, ni bandia tu. Unadhani una wema na kujivunia matendo yake, hasa yenye sura ya uadilifu na utakatifu; unaridhika nayo na kudai ni ya kwake. Ingawa haupendi maadili halisi unajitafutia sifa zinazotokana nayo. Unaona makosa yake si kitu, na unajitahidi kuonekana safi, ingawa sivyo. Pengine unadhani una ari, ndiyo sababu unakaripia vikali makosa ya jirani: “Ungeona dhambi zake, ungesahau zile za wengine, hata zikiwa kubwa sana”. Kila unapolaumiwa hautaki kunyoshwa wala haukomi kujitetea, ukisema, “Hata wengine wana kasoro zao; upande wangu nimetenda daima kwa nia njema, na kama nimekosa ni kwa ujinga au kwa udhaifu tu”. Unajiamini kumlenga Mungu katika yote, kumbe umejifanya lengo la yote na kuishi kwa kujionyesha tu, badala ya kuwa mwema kweli. Hivyo unajifanya lengo la sala pia: katika faraja unajielekezea Mungu na zawadi zake ili kujiridhisha. Ukija kukosa kinachompendeza, mara unakitafuta kingine ili kustarehe na kukielekeza kwake. “Mpaka utakapojifanya lengo, na kutenda kwa ajili yako, na kudai malipo ya matendo yako, na kutovumilia wengine wakutambue ulivyo kweli, basi ujue kwa hakika unajidanganya vibaya sana. Unapomdharau mtu kwa kasoro zake na kutaka kupendelewa kuliko wasioishi kadiri ya mitazamo yako, basi hujajifahamu, kwa kuwa hujajua ubaya uliomo ndani mwako”. Ndicho kinachozuia tusizae matunda ya uzima wa milele. Tunahitaji kujifahamu mpaka ndani ili kumjua Mungu na kumpenda kweli. Kwa ajili hiyo ni lazima tukeshe hisi za nje na za ndani zisitawanyike kwa kufuata viumbe. “Tunapaswa kujijengea chumba moyoni mwetu ili kukikimbilia na kuishi humo kadiri iwezekanavyo, bila kujulikana na ulimwengu, tusije tukaondolewa katika kumtazama Mungu. Tusisahau hata kidogo maisha na mateso ya Mwokozi”. Kumkazia macho kutazaa hamu ya kufanana naye. Tutakapojikuta hatufanani tutamuomba Roho Mtakatifu atuonyeshe zaidi ubaya wa dhambi na matokeo yake. Tutajishusha kwa unyofu na kutumainia huruma ya Mungu ituinue. Kadiri tutakavyowahi kuufisha umimi, sura yake ndani mwetu itakuwa nzuri na hai, tutamlenga katika yote na kumpenda kwa vitendo.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • F. VAN VLIJMEN, W.F., Safari ya Kiroho, Mafundisho kwa Watawa (vitabu 2) – ed. T.M.P. Book Department – Tabora 1978
  • R. GARRIGOU-LAGRANGE, O.P., Hatua Tatu za Maisha ya Kiroho, Utangulizi wa Uzima wa Mbinguni – tafsiri fupi ya Rikardo Maria, U.N.W.A. – ed. Ndugu Wadogo wa AfrikaMorogoro 2006

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hatua ya utakaso kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.