Saratani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Kwa kundinyota yenye jina hili angalia Saratani (kundinyota)

Picha ya eksirei inayoonyesha kivuli cha kansa katika mapafu

Saratani (Ar. سرطان sartan) au kansa (Ing. cancer) ni aina za ugonjwa unaoanzishwa na seli za mwili zinazoanza kujigawa yaani kukua bila utaratibu na bila mwisho.

Asili ya jina[hariri | hariri chanzo]

Jina la saratani latokana na neno la Kiarabu sartan linalomaanisha pia "kaa". Sababu yake ni ya kwamba mtaalamu Galenos wa Ugiriki wa Kale aliona uvimbe uliofanana na miguu ya kaa. Jina hili lilitafsiriwa baadaye kwa lugha nyingi. Hata kwa Kiingereza neno "cancer" linaweza kutaja pia jenasi moja ya kaa. Vivyo hivyo jina la kundinyota ya zodiaki ni "Cancer (constellation)" kwa Kilatini - Kiingereza na Saratani (kundinyota) kwa Kiswahili, yote kwa maana ya mnyama si ya ugonjwa.

Matokeo ya ugawaji hovyo wa seli mwilini[hariri | hariri chanzo]

Ukuaji huu unaleta uvimbe mwilini unaozidi kuwa kubwa hadi inabana viungo vya mwili kama neva, mishipa ya damu, ubongo, mapafu, maini, utumbo na kadhalika na kuzuia visifanye kazi. Hivyo inasababisha kifo, mara nyingi baada ya kipindi cha maumivu makali.

Pamoja na hayo kansa / saratani huwa na tabia za kujisambaza mwilini mahali pengi baada ya muda fulani na kusababisha kutokea kwa vimbe nyingi mwilini vinavyoendelea kukua hovyo. Kama uvimbe hauna uwezo wa kusambaa seli zake mwilini na kusababisha vimbe mpya si saratani.

Kansa inaweza kutokea kwa mtu yeyote lakini hutokea zaidi kwa watu wenye umri mkubwa na watu wanaoathiriwa na kemikali mbalimbali. Katika nchi zilizoendelea ambako wanachi hufikia umri mkubwa saratani iko kati ya sababu kuu za kifo.

Uchunguzi na matibabu ya kansa ni utaalamu wa onkolojia ndani ya somo la tiba.