Nenda kwa yaliyomo

Galenos

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Galen

Galenos wa Pergamon (pia Galen; 129 – mnamo 216) alikuwa tabibu na mwanafalsafa Mgiriki mashuhuri katika Dola la Roma. Anakumbukwa kwa uchunguzi wa mambo ya tiba aliofanya na nadharia zake kuhusu afya na magonjwa. Nadharia zake ziliathiri tiba ya nchi za Ulaya na za Waislamu kwa miaka 1000 hadi mwisho wa enzi ya kati.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Galenou Apanta, 1538

Galenos alizaliwa Pergamon (leo hii: Bergama katika Uturuki), mji wa Ugiriki ya Kale ambao ulikuwa na hekalu muhimu la Asklepios aliyeheshimiwa kama mungu wa tiba.

Baba yake Nikon alikuwa msanifu akamfundisha falsafa, hisabati na sayansi.

Tangu mwaka 146 Galenos alijishughulisha na tiba hasa akaisoma alipohudumia wagonjwa kwenye hekalu la Asklepios. Akaedelea kusafiri hadi Aleksandria wa Misri iliyokuwa kitovu cha elimu ya tiba katika Dola la Roma na mahali pa pekee ambako matabibu waliruhusiwa kufanya utafiti kwenye maiti za watu. Hapa alipata pia nafasi ya kusoma mengi katika maktaba mashuhuri ya Aleksandria.

Mwaka 158 alirudi Pergamon akaajiriwa na kuhani mkuu wa Asia kama tabibu wa wapigaji upanga [1] wake. Galenos alijifunza mengi kutokana na kutibu vidonda na majeruhi; katika maandiko yake aliita kidonda "dirisha la kutazama ndani ya mwili". Alifaulu kwa sababu katika kipindi chake walikufa wajeruhiwa 5 tu, wakati kwenye kipindi cha mtangulizi wake zaidi ya wapiganaji 60 walikufa.

Mwaka 160 alihamia Roma na baada ya kumponya mwanafalsafa mashuhuri Eudemos wa Pergamon alikuwa tabibu wa makabaila wa Roma. Ugonjwa wa tauni ulipoenea mjini alikimbia Roma mwaka 166 akarudi Pegamon. Mwaka 168 aliombwa na Kaisari Marcus Aurelius arudi Italia akawa mshauri na tabibu wa mtoto wa Kaisari na baadaye wa Kaisari Septimius Severus.

Galenos alikufa Roma mnamo mwaka 216. [2]

Mafundisho yake[hariri | hariri chanzo]

Galenos aliacha mafundisho yake katika vitabu 16 vya "Methodi medendi" (mbinu za kutibu). Hapa anafundisha ya kwamba yote yanayotokea au kuonekana yana kusudi lake.

Alikubali mafundisho ya Empedokles kuhusu elementi 4 za moto, ardhi, hewa na maji zinazounda vitu vyote. Hizi elementi zinalingana na viowevu 4 ndani ya mwili (damu, belghamu, nyongo njano na nyongo nyeusi). Hizi tena zinalingana na tiba 4 za joto, baridi, bichi na kavu.

Katika mafundisho ya Galen mwanadamu ni umoja wa mwili na roho. Ndani ya umoja huu uwiano wa viowevu na tabia zote 4 ni muhimu.

Kutokana na mafundisho hayo aliona ya kwamba kila dawa linaongeza au kupunguza tabia na viowevu mwilini. Alitofautisha madawa ya msingi (yenye tabia 1), madawa ya maungano (yenye tabia 2) na madawa ya pekee.

Kwenye madawa alitofautisha tena kutokana na ukali:

  1. . isiyoonekana sana
  2. . inayoonekana
  3. . kali kiasi, inaweza kuleta hasara kiasi
  4. . kali sana, inaleta hasara kwa afya

Galen aliongeza elimu yake kwa kuchunguza miili ya wanyama aliyoikata na kutazama. Kukata miili ya kibinadamu kwa uchunguzi kulipigwa marufuku katika Dola la Roma.

Maandiko ya Galen yalikuwa msingi wa tiba kwa karne nyingi za baadaye. Yalitafsiriwa baadaye pia kwa Kiarabu na kuathiri tiba ya Waislamu.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Katika utamaduni wa Roma ya Kale watu walipenda kuangalia mashindao ambako wapigaji walipigana hadi kifo kwa silaha mbalimbali; wapigaji hao walikuwa wafungwa au watumwa waliowez kupata uhuru baada ya kushinda mara kwadhaa
  2. Kamusi 1 ya karne ya 12 ilitaja umri wake kama miaka 70 hivyo angekufa 199; lakini kufuatana na chanzo cha Kiarabu laikufa katik umri wa miaka 87