Ndugu Wadogo wa Afrika

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Ndugu Wadogo wa Afrika ni wanaume na wanawake Wafransisko wamisionari wa Kanisa Katoliki wenye makao makuu mjini Morogoro (Tanzania).

Cha kwao ni chama cha maisha yaliyowekwa wakfu kwa Mungu kwa njia ya ahadi ya kushika mashauri ya Kiinjili ya useja mtakatifu, ufukara na utiifu kadiri ya utamadunisho safi wa karama ya udugu na udogo waliyorithi kwa mtakatifu Fransisko wa Asizi.

Uundaji na ustawi[hariri | hariri chanzo]

Kilikubaliwa rasmi na askofu Telesphor Mkude tarehe 9 Julai 1997.

Mwaka 2014 wenye ahadi walikuwa 32 (wanaume 8 na wanawake 24) katika jumuia 5, zote katika jimbo Katoliki la Morogoro.

Malengo[hariri | hariri chanzo]

Mtindo wa maisha yao unakusudiwa kumfuata Yesu kwa kutekeleza kijumuia Injili yake na kushikamana na watu wa leo walio fukara zaidi ili uwe habari njema kwao na kwa wale wote wanaotamani dunia ijae haki, amani na upendo.

Wakiamini kwamba hiyo itabaki ndoto ya mchana tu ikiwa wanaume na wanawake watajaribu kuujenga kwa nguvu zao wenyewe, Ndugu Wadogo wa Afrika wanaikimbilia sala usiku na mchana kusudi uhusiano na maongezi na Baba wa wote vizijalie akili furaha ya ukweli, viunganishe mioyo, vitakase na kuimarisha ndani ya kila mmoja nia ya kutumikia kwa ukarimu watu wenye shida kubwa zaidi na viwafanye wote kuwa vyombo vya amani yake.

Roho Mtakatifu, anayeshirikishwa kwa njia ya Yesu mteswa, mzikwa na mfufuka, ndiye anayegeuza hivyo kila mmoja na wote kwa jumla ili kuwafanya kwa pamoja mashahidi wa Kristo hadi mipaka ya mwisho ya dunia.

Tangazo la jina lake, la maisha yake, la msalaba wake mtukufu, la fumbo lake na la mafundisho yake ndiyo huduma kuu wanayoweza kuwapatia ndugu zao katika ubinadamu.

Hilo linaendana na mipango ya kuendeleza watu na vitendo vidogovidogo vya kila siku ambavyo wanawashirikisha waliyojaliwa na mikono ya Mungu kwa njia ya kazi zao au kwa misaada ya watu wengine waliosogezwa jirani na utandawazi.

Ndugu Wadogo wa Afrika, wakijua kwamba wanachoweza kufanya ni kidogo kweli, wanatia maanani ushirika na viungo vyote vya familia ya Mungu, yaani Kanisa linaloongozwa na Papa na Maaskofu wenzake: ndani yake mchango wao mdogo kwa ustawi wa utawala wa Mungu unaweza kuwafaidisha wengi, kwa sababu upendo unazidishwa na uenezi wake.

Upendo huo unatakiwa kupamba kama moto ili kufuta aina yoyote ya ubinafsi na umimi inayowafunga watu ndani yao wenyewe na ya faida zao, ikiwafanya sio tu wasiweze kuzaa lolote bali waharibu maisha yao na ya wenzao, unavyothibitisha ustaarabu wa Magharibi ambao umegeuka utamaduni wa kifo.

Kinyume chake, wao wanataka kudumisha, kustawisha na kueneza tunu bora za makabila ya Afrika ili wachangie utamaduni wa uhai na wa mshikamano usio na mipaka.

Ni kwa Bikira Maria, mama wa Yesu, kwamba wanataka kujifunza unyenyekevu wapokee neema ya moyo safi wenye kuwaka upendo ili kumshangilia Mungu na kumtumikia kila mtoto wake.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]