Thomas Aquinas Mtakatifu
Mtakatifu Thomas Aquinas (Roccasecca, katika eneo la watawala wa Aquino, leo katika wilaya ya Frosinone[1], Italia, 1224 au 1225 - Fossanova, wilaya ya Latina, Italia, 7 Machi 1274) alikuwa mtawa wa Shirika la Wahubiri na padri wa Kanisa Katoliki.
Mwenye akili kubwa ajabu, alishirikisha hekima yake ya pekee kwa mafundisho na kwa maandishi.
Mnyofu, mkimya, aliyekuwa tayari kutumikia, kiutu alipendwa na wote, naye alipendelea watu wa chini, akihubiria mafukara kwa usahili na wema hata zaidi ya mara moja kwa siku.
Kuliko wengine wote, Thoma aliona elimu na masomo kama njia ya kufikia utakatifu; ni kati ya watu bora upande wa nadharia, hasa wa teolojia ya shule, iliyofikia kilele chake katikati ya karne XIII.
Mwanafunzi wa Alberto Mkuu, alitumia hasa mawazo ya mwanafalsafa wa Ugiriki Aristoteli na ya Waarabu waliomtafsiri, lakini pia ya Plato: ili kufafanua imani, alikubali ukweli ulioweza kutolewa na yeyote, kwa sababu kweli zote zinatoka kwa Mungu; kinyume chake alikanusha udanganyifu wowote.
Hivyo aliweza kufanya usanisi mpana ambao mpaka leo Kanisa Katoliki linautambua kama tokeo bora la mafundisho yake lenyewe na kama kielelezo cha namna ya kufikiri na ya kufanya teolojia.
Anajulikana hasa kwa vitabu vyake “Jumla ya Teolojia” (kwa Kilatini Summa theologiae) na “Jumla dhidi ya Wapagani” (kwa Kilatini Summa contra gentiles).
Alitangazwa na Papa Yohane XXII kuwa mtakatifu tarehe 18 Julai 1323, halafu na Papa Pius V kuwa mwalimu wa Kanisa mwaka 1568. Kwa Kilatini anaitwa Doctor Angelicus (Mwalimu wa Kimalaika) au Doctor Communis (Mwalimu wa wote).
Ni msimamizi wa wanateolojia, wanachuo, watoaji na wauzaji wa vitabu, wanafunzi na shule.
Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 28 Januari[2].
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Asili na ujana
[hariri | hariri chanzo]Alizaliwa na Landolfo, sharifu mwenye asili ya Kilombardi, na mke wake, Teodora, katika ngome ya familia yao.
Akiwa mtoto wa miaka 5 tu, alitumwa kuishi na Wabenedikto katika abasia jirani ya Monte Cassino ili apate malezi ya msingi kwa watawa.
Alipofikia umri wa miaka 14 alihamia Napoli, mji mkuu wa Ufalme wa Sicilia, aliposoma katika chuo kikuu maarufu kilichoanzishwa na Kaisari Federiko II. Humo mawazo mbalimbali kama yale ya Aristotle yalifundishwa bila vizuio vilivyokuwepo sehemu nyingine.
Basi, Thoma alianza kutambua thamani ya falsafa ya Mgiriki huyo iliyokuwa imesahaulika kwa muda mrefu lakini wakati huo ilikuja kujulikana upya kupitia wafafanuzi wake wa Kiarabu, Avisena na Averoe.
Ilikuwa na mpango mzima wa mawazo kuhusu ulimwengu, roho na maadili ambao ulikamilika kabla ya Kristo kwa kutumia akili tu, na ambao ulionekana kujitosheleza na kuridhisha kama mtazamo sahihi.
Jambo lingine muhimu la miaka hiyo ni kwamba alikuwa karibu na konventi ya Mt. Dominiko akavutiwa na karama ya shirika lililoanzishwa na mtakatifu huyo. Ingawa alipingwa sana na familia, mwaka 1244 aliamua kujiunga na Wadominiko.
Wakubwa wa shirika, kisha kuhisi ukuu wa akili yake, walimtuma Paris aweze kukamilisha masomo yake, lakini kabla hajafika huko alikamatwa na wanafamilia na kufungwa katika ngome ya baba yake huko Monte San Giovanni Campano alipokaa mwaka mzima, akishinikizwa aoe.
Utawani
[hariri | hariri chanzo]Hatimaye, akiwa amefikia umri wa kujiamulia maisha, alitoroka au alifunguliwa kwa ombi la Papa Inosenti IV.
Baada ya kukaa kidogo Napoli na Roma, alifika Paris (Ufaransa) ili kufundishwa na Alberto Mkuu, mwanasayansi, mwanafalsafa na mwanateolojia wa shirika lake.
Mapema walianza kuheshimiana na kupendana, hivyo mwaka 1248 Thoma alimfuata Alberto Cologne (Ujerumani) alipokuwa ametumwa na viongozi wa shirika aanzishe kituo cha teolojia.
Baadaye, Thoma aliamua kutekeleza mpango wa mwalimu wake wa kulinganisha Ukristo na falsafa ya Aristotle iliyokuwa inazidi kuathiri Ulaya Magharibi na ustaarabu wake uliotegemea imani, ingawa wengine waliipinga falsafa hiyo, hasa kwa sababu wafafanuzi wake wa Kiarabu walikuwa wameipendekeza tofauti, wakisema, k.mf. kwamba ulimwengu ni wa milele kama Mungu.
Hapo Thoma alifanya jambo la maana sana kwa historia yote ya falsafa, teolojia na elimu kwa jumla: kusoma kikamilifu vitabu vya Aristotle na vya wafafanuzi wake, kisha kujipatia tafsiri mpya kutoka Kigiriki ili asitegemee tu walivyoelewa Waarabu hao.
Hapo alifafanua mwenyewe sehemu kubwa ya maandishi ya Aristotle, akitofautisha kweli za kudumu zilizomo, mambo yanayotia shaka na yale yasiyo sahihi kabisa, akionyesha yanavyolingana na Ufunuo wa Kimungu na jinsi yanavyoweza kutumika katika teolojia ya Kikristo.
Kifupi, Thoma alithibitisha hivyo ulinganifu wa imani na hoja za akili, wakati ambapo hizo mbili zilionekana kupingana moja kwa moja, hata kusababisha watu wajione ni lazima waachane na imani na kufuata akili.
Kwa usanisi huo, Thoma aliunda msimamo wa karne zijazo, kwamba kweli haziwezi kupingana kamwe; ikionekana hivyo maana yake ama akili imekosea katika hoja zake, ama kinachodaiwa kuwa ukweli wa imani hakifundishwi nayo.
Kutokana na vipawa vyake kuanzia mwaka 1252 aliitwa kufundisha teolojia kwenye Chuo kikuu cha Paris, akianza kama baccalarius biblis, na baada ya miaka 4 aliweza kufundisha kama profesa.
Wakati huo Thoma alianza kazi ya kutunga vitabu ambayo aliendelea nayo hadi karibu na kifo na ambayo ni ya ajabu hata tukizingatia kwamba alisaidiwa na karani kadhaa, kati yao akiwemo hasa rafiki yake Rejinaldo wa Piperno.
Alipinga falsafa ya wafuasi wa Mwarabu Averroe waliosema imani haiwezi kupatana na akili: "Imani ni kwa watu wanyofu, falsafa ni kwa wasomi".
Thoma alipambana pia na Waagustino ambao walifuata falsafa ya Plato hata kusema ile ya Aristoteli haipatani na imani.
Mwaka 1259 alihiriki mkutano mkuu wa shirika huko Valenciennes, akaingizwa katika jopo la kupanga masomo ya Wadominiko wote.
Baadaye alirudi Italia na kushirikiana na Papa Urbano IV, akiishi kwenye konventi ya Orvieto (1261-1265).
Kwa agizo lake, Thoma alitunga au kupanga matini ya liturujia yote ya sikukuu mpya ya Corpus Domini (Mwili na Damu ya Kristo) iliyoanzishwa tarehe 8 Septemba 1264. Kati ya matini hayo, ambamo zinajitokeza imani na hekima yake, maarufu zaidi kimataifa mpaka leo ni utenzi Pange Lingua, hasa sehemu ya mwisho inayoanzia na maneno Tantum Ergo (Sakramenti Kubwa Hiyo).
Waliomfahamu walisisitiza heshima yake kwa fumbo la Ekaristi; pengine alikuwa akiegemeza kichwa chake penye tabenakulo, kama kwa kusikia mapigo ya Moyo wa Yesu na kupata majibu ya maswali magumu aliyojiuliza. Akiadhimisha Misa aliweza akalia machozi ya huruma, furaha na shukrani kwa Bwana aliyejitoa kafara kwa ajili ya binadamu. “Kwa kuwa hii ndiyo sakramenti ya Mateso ya Bwana wetu, ndani yake ina Yesu aliyeteseka kwa ajili yetu. Basi, tokeo lolote la Mateso ya Bwana wetu ni pia tokeo la sakramenti hii.”
Halafu alihamia Roma (1265-1268) ili kuongoza chuo cha Mt. Sabina; ila katikati, mwaka 1267 Papa Clemens IV alimuita kwake Viterbo, alipohubiri mara nyingi katika kanisa la Santa Maria Nuova.
Akiwa Italia ndipo alipoandika vitabu vingi kama vile Summa contra gentiles, De regimine principium, De unitate intellectus contra Averroistas na sehemu kubwa ya kazi yake bora, Summa Theologiae, inayotumika hadi leo katika teolojia kama ilivyoagizwa na Mtaguso II wa Vatikano katika hati mbili, Optatam Totius na Gravissimum Educationis.
Mwaka 1269 alirudishwa Paris; huko wanafunzi wake walikuwa wengi hata kujaza kabisa ukumbi; mmojawao alishuhudia kwamba, “kumsikiliza kulimjaza heri ya dhati”. Hata waliompinga walikiri mafundisho yake ni bora na yanasahihisha yale ya walimu wengine.
Huko akaanza pia kutetea kiteolojia mashirika ya ombaomba na kupinga Uplato mpya wa Waagustino.
Mwaka 1272, akiitwa na mfalme Karolo I wa Angiò, alirudishwa Napoli na kupanga upya masomo ya teolojia kwenye chuo kikuu karibu na konventi yake asili. Huko alijitosa pia kuhubiria watu wa kawaida, nao walimiminika kumsikiliza. Mahubiri ya Kwaresima yake ya mwisho, aliyoyatoa katika kanisa la San Domenico Maggiore, yametunzwa kwa jina la “Opusculi” (yaani “Vijitabu”). Humo tunasoma alivyofafanua kwa usahili Kanuni ya Imani ya Mitume, [[sala++ ya Baba Yetu, Amri Kumi na sala ya Salamu Maria.
Kwa mfano, kuhusu imani, alieleza thamani yake: kwa njia yake roho inaungana na Mungu na kuzaa uzima wa milele; maisha yanapata mwelekeo wa kufaa, nasi tunashinda vishawishi kwa urahisi.
Dhidi ya hoja ya kwamba imani ni upumbavu kwa sababu inamfanya mtu asadiki kitu kisichofikiwa na hisi zake, Thoma alijibu kwamba akili yetu ina mipaka, haiwezi kujua yote. Ingeweza kufahamu kikamilifu mambo yote yanayoonekana na yasiyoonekana, hapo tu ingekuwa upumbavu kukubali ukweli fulani kwa imani. Kumbe hatuwezi kuishi bila kutegemea ushahidi wa wengine kila tunaposhindwa kujua kitu wenyewe. Kama ni hivyo, basi, inafaa tumsadiki Mungu anayejifunua na pia ushahidi wa Mitume wa Yesu. Ni kati ya maajabu ya historia kwamba mapema watu wengi wenye mali na hekima waliwasadiki hao watu wachache, fukara na wanyofu waliovunjwa moyo na kifodini cha mwalimu wao. Lisingetokea kama wasingekutana naye mfufuka.
Thoma alieleza pia kwamba tafakuri juu ya umwilisho wa Mwana wa Mungu inaimarisha imani na tumaini kwa wazo la ujio wake kati yetu kama mmojawetu kwa lengo la kuwashirikisha watu umungu wake; pia inachochea upendo kwa sababu hakuna ishara wazi zaidi ya upendo wa Mungu kuliko kumuona Muumba wa ulimwengu kujifanya kiumbe kama sisi; hatimaye inawasha hamu ya kumfikia Kristo katika utukufu: “Kama ndugu wa mfalme angeishi mbali sana naye, bila shaka angetamani kuishi karibu naye. Basi, Kristo ni ndugu yetu; kwa hiyo tunapaswa kutamani tuwe naye na kuwa moyo mmoja naye”.
Akifafanua Baba Yetu, alionyesha ni sala kamili kutokana na kuwa na sifa tano zinazohitajika: tumaini tulivu, maombi ya kufaa, mpangilio mzuri wa maombi, ari ya upendo na unyofu wa unyenyekevu.
Kuhusu Bikira Maria, alimuita “Triclinium totius Trinitatis”, yaani “mahali ambapo Utatu Mtakatifu unastarehe”, kwa maana Nafsi tatu za Mungu hazifurahii kukaa ndani ya mtu yeyote kuliko ndani ya roho yake iliyojaa neema.
Miaka ya mwisho
[hariri | hariri chanzo]Miezi ya mwisho ya maisha yake iliathiriwa na tukio la pekee lililofanya azidi kuzama katika tafakuri. Ni kwamba tarehe 6 Desemba 1273, katika kanisa la Mt. Dominiko, alitoka nje ya nafsi yake na tangu siku hiyo aliacha kuandika, akimueleza kwa unyenyekevu ndugu Reginaldo wa Piperno, msaidizi na muungamishi wake: «Yale yote niliyoyandika naona ni fungu dogo la majani makavu kulingana na yale ambayo nimeyaona na kufunuliwa. Ndio mwisho wa kuandika kwangu na natumaini umekaribia pia mwisho wa maisha yangu».
Ndiyo sababu Summa Theologiae haikukamilika (inaishia kwenye mada ya Kitubio) baada ya kukabili masuala 512 katika hoja 2,669 kwa kuchimba mafundisho ya Biblia na ya mababu wa Kanisa, hasa Augustino wa Hippo).
Utunzi wa Summa Theologiae
[hariri | hariri chanzo]Humo Thoma anazingatia kwanza kwamba Mungu yupo kwa namna tatu: 1) ndani mwake, akiwa asili na lengo la vyote, hivi kwamba viumbe vyote vinatokana naye na kumtegemea; 2) kwa njia ya neema katika uhai na utendaji wa watu anaowatakasa; 3) kwa namna ya pekee kabisa katika nafsi ya Kimungu ya Mwana iliyounganika kweli na ubinadamu wa Yesu na inayotenda katika sakramenti zinazotokana na kazi yake ya ukombozi.
Ndiyo sababu kitabu hicho kikubwa kimegawanyika katika sehemu tatu: “Kwa kuwa lengo kuu la teolojia ni kufundisha ujuzi wa Mungu, si tu jinsi alivyo mwenyewe, bali pia kama asili na lengo kuu la vitu, na hasa la viumbe wenye akili, ilivyo wazi katika yale tuliyoyasema tayari, basi tutafafanua: 1) Mungu; 2) maendeleo ya kiumbe mwenye akili kumuelekea Mungu; 3) Kristo ambaye kama mtu ndiye njia yetu kwa Mungu”.
Ni kama duara inayorudi ilipoanzia: Mungu alivyo anajitokeza kwa nje na kutushika mkono hivi kwamba pamoja na Kristo tumrudie yeye na kuungana naye awe yote katika wote.
Sehemu ya kwanza ya Summa Theologiae inamchunguza Mungu mwenyewe, fumbo la Utatu na kazi yake ya kuumba. Humo tunakuta tafakuri ya dhati juu ya mtu pia, kama kiumbe aliye tunda la upendo wake. Uhai wetu unamtegemea Mungu, lakini ni wa kweli kwa sababu yeye ametaka kututia thamani.
Sehemu ya pili inazidi kumzingatia mtu ambaye, akisukumwa na neema, anatamani kumjua na kumpenda Mungu ili awe na heri sasa na milele. Thoma anafafanua kiteolojia matendo maadilifu, ambayo yanachangiwa na akili, utashi na maono ya mtu, pamoja na uwezo wa neema ya Mungu kupitia maadili na vipaji vya Roho Mtakatifu, mbali ya msaada wa sheria yake. Kwa msingi huo, Thoma anamchora mtu ambaye anaongozwa na Roho Mtakatifu na hivyo kuwa mfano wa Mungu. Hapo anasimama kufafanua maadili matatu ya Kimungu na zaidi ya maadili hamsini ya kiutu, yanayotegemea maadili bawaba manne. Hatimaye anatakari juu ya miito mbalimbali yaliyopo ndani ya Kanisa.
Sehemu ya tatu inachunguza fumbo la Kristo, aliye njia na ukweli, ambalo linatuwezesha kumfikia Mungu Baba. Humo Thoma anaeleza vizuri ajabu umwilisho na Mateso ya Yesu, akiongeza maelezo marefu kuhusu sakramenti ambazo Kristo anatushirikisha faida ya ukombozi. Akitumia vitu alivyochagua, anatugusa mpaka ndani.
Asubuhi moja, Thoma alipokuwa anasali mbele ya msalaba wa kikanisa cha Mt. Nikola mjini Napoli, mtunzasakristia Dominiko wa Caserta alisikiliza maongezi yake na Yesu. Thoma alikuwa anauliza kwa fadhaiko kama aliyoyaandika kuhusu mafumbo ya imani ni sahihi au sivyo. Msulubiwa alimjibu: “Umeandika vema juu yangu, Thoma. Unataka tuzo gani?” Hapo Thoma alisema, “Si kitu kingine, ila wewe mwenyewe”.
Kifo
[hariri | hariri chanzo]Mnamo Januari 1274 Papa Gregori X alimuagiza ashiriki Mtaguso wa pili wa Lyon, na Thoma akafunga safari ingawa hali yake haikuwa nzuri.
Alilazimika kusimama kwenye ngome ya Maenza, lakini alipoona hali inazidi kuwa mbaya asiweze kufikia konventi ya shirika, akitaka kufia monasterini, aliagiza aletwe kwenye abasia ya Wasitoo ya Fossa Nuova (leo Fossanova, karibu na Priverno), ambapo alifariki baada ya wiki chache.
Masalia yake yanatunzwa katika konventi ya Wadominiko des Jacobins huko Tolosa (Ufaransa).
Upekee wake
[hariri | hariri chanzo]Sababu si mafundisho yake tu, bali mbinu alizozitumia katika kusanisi falsafa na teolojia bila kuzichanganya kama ilivyotokea kabla yake. Falsafa kama ile ya Aristotle iliweza kujitegemea katika hoja zake, badala ya kumezwa na teolojia ambayo ilitegemea imani katika Ufunuo wa Mungu na kuja kukamilisha falsafa pale ambapo hiyo haiwezi kufika.
Msingi wa hakika hiyo ya Thoma ni kwamba falsafa na teolojia vilevile zinatokana na chanzo cha kweli zote, ambacho ni Neno wa Mungu, aliyehusika na kazi ya uumbaji na ya ukombozi pia. Ingawa fani hizo zinafuata taratibu tofauti katika kulenga ujuzi sahihi, hazitakiwi kutengana, bali kushirikiana.
Kadiri yake, kwa mfano, akili ya binadamu kwa njia ya hoja inaweza kufikia hakika kuhusu uwepo wa Mungu mmoja, ila imani tu, kwa kupokea Ufunuo kutoka juu, inaweza kuchota katika fumbo la Upendo wa Mungu Utatu.
Wakati imani inakamilisha ujuzi wa akili, hoja pia inasaidia imani kwa namna tatu: “kwa kuthibitisha kweli zinazoandaa kusadiki; kwa kufafanua wazi zaidi kweli za imani kwa njia ya mifano kadhaa; kwa kupinga wale wanaosema dhidi ya imani, ama kwa kuonyesha kauli zao ni za uongo, ama kwa kuonyesha si hakika kuwa za kweli”.
Ulinganifu huo wa msingi kati ya hoja za akili na imani ya Kikristo unajitokeza tena katika wazo lingine muhimu la Thoma: kwamba neema ya Mungu haibatilishi umbile la binadamu, bali inalitumia na kulikamilisha. Hiyo ni kwa sababu, hata baada ya kutenda dhambi, umbile hilo halijaharibika kabisa, ila limejeruhika na kudhoofika. Neema ambayo tunakirimiwa na Mungu na kushirikishwa kwa njia ya Neno aliyefanyika mwili, ni zawadi tu ya hiari yake ambayo umbile letu linaponywa, linatiwa nguvu na kusaidiwa lifikie heri ile linayotamani tu kwa dhati, hata bila kutambua na kuamua. Vipawa vyote vya mtu vinatakaswa, vinageuzwa na kuinuliwa na neema ya Mungu.
Fundisho hilo juu ya uhusiano wa umbile na neema ndani mwetu linatumiwa hasa katika maadilidini ya Thoma. Kiini chake ni sheria mpya ya Injili, ambayo ni Roho Mtakatifu, yaani neema yake wanayopewa wale wanaomuamini Kristo. Mafundisho yote ya Kanisa kuhusu imani na maadili yameunganika na neema hiyo ambayo ni ya msingi katika kuishi kwa uadilifu: kutoka kwake yanapatikana maadili ya Kimungu na ya kiutu. Hivyo Wakristo wote wanaweza kufikia ukamilifu uliopendekezwa na Yesu katika hotuba ya mlimani, ikiwa wanaishi naye katika uhusiano wa imani na wako wazi kupokea kazi ya Roho Mtakatifu.
Pamoja na hayo, “ingawa neema ina nguvu kuliko umbile, hata hivyo umbile linamhusu mtu zaidi, na kwa hiyo ni la kudumu zaidi”. Ndiyo maana kuna nafasi kwa hoja za akili katika kutambua maadili yanayodaiwa na utu kwa jinsi ulivyo. Akili inaweza kuyatambua kwa kutofautisha yanayofaa na yasiyofaa kufikia ile heri inayotamaniwa na mioyo yetu.
Hayo yanahusika pia na majukumu kwa ajili ya wengine, mmojammoja na kwa jumla (ustawi wa jamii). Watungasheria wanapaswa kuzingatia hayo katika kazi yao ya kuratibu maisha ya jamii. Ndio msingi wa kuorodhesha na kutetea haki za binadamu. Si ajabu kwamba fundisho la hadhi ya nafsi ya mtu, inayomfanya kila mmoja awe na haki za msingi kwa sababu tu ni mtu, lilistawi kwanza kati ya waliozingatia urithi wa Thoma katika kuthamini umbile letu: “ndilo lililo kamili kuliko yote yanayopatikana ulimwenguni, yaani mmoja anayeishi akiwa na akili”.
Basi, Thoma alipendekeza mtazamo mpana na lenye tumaini kuhusu akili ya binadamu. Mpana kwa sababu hauishii katika ujuzi wa sayansi zinazotegemea upimaji wa vitu vinavyoonekana, bali unakabili yote yaliyopo, kuanzia Mungu, na hivyo unahimizwa kutafuta maana ya maisha yetu. Lenye tumaini kwa sababu akili, hasa ikiangazwa na imani ya Kikristo, inapigania ustaarabu ambao unathamini hadhi ya kila mtu, unatetea haki zake pamoja na kumhimiza kuwajibika kwa wengine.
Dhati ya mawazo ya Thoma ilitokana daima na maisha yake ya imani na sala yaliyojitokeza katika maneno kama haya: “Ee Bwana, Mungu wangu, unijalie akili ya kukufahamu, moyo wa kukutafuta, hekima ya kukupata, mwenendo wa kukupendeza, udumifu mwaminifu katika kukutarajia, na tumaini la kukukumbatia mwisho”.
Sala yake mojawapo
[hariri | hariri chanzo]Mungu wa wema wote, utujalie tutamani motomoto, tutafute kwa busara, tujue kwa hakika na kutekeleza kikamilifu matakwa yako matakatifu kwa utukufu wa jina lako.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Watakatifu wa Agano la Kale
- Orodha ya Watakatifu Wakristo
- Orodha ya Watakatifu wa Afrika
- Orodha ya Watakatifu Wafransisko
Maandishi yake
[hariri | hariri chanzo]- Ad Bernardum
- Aurora Consurgens
- Compendium theologiae
- Contra errores Graecorum
- Contra impugnantes Dei cultum
- Contra retrahentes
- Contra Saracenos
- De aeternitate mundi
- De alchemia
- De anima
- De articulis Fidei
- De ente et essentia
- De forme absolutionis
- De lapide philosophico
- De malo
- De motu cordis
- De operationibus occultis
- De perfectione
- De potentia
- De principiis naturae
- De rationibus Fidei
- De regimine principum
- De spiritualibus creaturis
- De substantiis separatis
- De unione Verbi Incarnati
- De unitate intellectus contra Averroistas
- De veritate
- De virtutibus
- Summa contra Gentiles
- Summa theologiae
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Wachache wanataja ngome ya familia katika mji wa Belcastro, karibu na Catanzaro, huko Calabria. Fiore, Giovanni (1999). Della Calabria illustrata (kwa Kiitaliano). Rubbettino Editore. ISBN 978-88-498-0196-5. Barrio, Gabriele (1571). De antiquitate et situ Calabriae (kwa Kilatini).
- ↑ Martyrologium Romanum
Marejeo kwa Kiswahili
[hariri | hariri chanzo]- GEROLD SCHMID, Toma na Marieta – ed. Benedictine Publications Ndanda-Peramiho – Peramiho 1978
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]Maisha yake
[hariri | hariri chanzo]- St. Thomas Aquinas (pdf Archived 28 Desemba 2014 at the Wayback Machine.) biography from Fr. Alban Butler's Lives of the Saints
- "St. Thomas Aquinas". Catholic Encyclopedia. 1913.
- St. Thomas Aquinas article by Daniel Kennedy in Catholic Encyclopedia (1912), at NewAdvent.org
- St. Thomas Aquinas Archived 9 Juni 2010 at the Wayback Machine. biography by Jacques Maritain
- St. Thomas Aquinas biography by G. K. Chesterton protected by copyright outside Australia
- Vita D. Thomae Aquinatis Archived 29 Septemba 2011 at the Wayback Machine. a pictorial life of Aquinas from a manuscript by Otto van Veen (1610)
Kuhusu mafundisho yake
[hariri | hariri chanzo]- Actus Essendi Electronic Journal
- Brown, Paterson. "Infinite Causal Regression" Archived 27 Desemba 2010 at the Wayback Machine., Philosophical Review, 1966.
- Brown, Paterson. "St. Thomas' Doctrine of Necessary Being" Archived 27 Desemba 2010 at the Wayback Machine., Philosophical Review, 1964.
Wikisource has the text of the 1911 Encyclopædia Britannica article Aquinas, Thomas. |
- Instituto Teológico São Tomás de Aquino Archived 20 Machi 2011 at the Wayback Machine. (Portuguese)
- On the legend of St. Albert's automaton
- Poetry of St. Thomas Aquinas
- Biography and ideas Archived 25 Novemba 2005 at the Wayback Machine. at SWIF/University of Bari/Italy (Italian)
- Aquinas's Moral, Political and Legal Philosophy
- Thomas Aquinas at Find A Grave
- Thomistic Philosophy Archived 12 Septemba 2017 at the Wayback Machine. Inspired by the enduring thought of Saint Thomas Aquinas
- Article on Thomism by the Jacques Maritain Center of Notre Dame University
- Thomistica.net news and newsletter devoted to the academic study of Aquinas
- Aquinas the Scholar Archived 1 Septemba 2006 at the Wayback Machine. from The Thirteenth, the Greatest of Centuries, ch. XVII. by James Joseph Walsh
- A discussion of Aquinas on BBC Radio 4's In Our Time series 2009
Maandishi yake
[hariri | hariri chanzo]- Shughuli au kuhusu Thomas Aquinas Mtakatifu katika maktaba ya WorldCat catalog
- Complete works of St. Thomas Aquinas in (Kilatini) and (Kiingereza) side by side
- Corpus Thomisticum – his complete works in (Kilatini)
- Documenta Catholica Omnia – his complete works in PDF files, in (Kilatini), (Kiitalia), (Kiingereza), (Kijerumani), (Kihispania), (Kifaransa), (Kireno)
- Summa contra Gentiles
- Summa Theologica
- The Principles of Nature Archived 5 Desemba 2004 at the Wayback Machine.
- On Being and Essence Archived 27 Novemba 2014 at the Wayback Machine. (De Ente et Essentia)
- Catena Aurea (partial)
- Works by Thomas Aquinas katika Project Gutenberg
- Bibliotheca Thomistica IntraText: texts, concordances and frequency lists
- An Aquinas Bibliography
- St Thomas' Multilanguage Opera Omnia
- Thomas Aquinas in English
- De Magistro Archived 12 Mei 2012 at the Wayback Machine. (On the teacher q. 11, a.1 of de Veritate)
- Writings of Thomas Aquinas in Article Form at PhilosophersAnswer.com Archived 24 Agosti 2011 at the Wayback Machine.
- Online Galleries, History of Science Collections, University of Oklahoma Libraries Archived 16 Mei 2012 at the Wayback Machine. High resolution images of works by Thomas Aquinas in .jpg and .tiff format.
- "St. Thomas Aquinas" katika Catholic Encyclopedia
- Opera omnia
- Summa theologiae Archived 4 Februari 2007 at the Wayback Machine.
- Thoma katika Kamusi elezo ya Falsafa kwa Kiingereza
- Thoma katika Stanford Encyclopedia of Philosophy
- Opera omnia katika Kilatini na tafsiri 6