Gravissimum Educationis

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Gravissimum Educationis ni jina la Kilatini la hati iliyotolewa na Papa Paulo VI pamoja na washiriki wengine wa Mtaguso wa pili wa Vatikano (kwa kura 2290 dhidi ya 35) tarehe 28 Oktoba 1965. Tafsiri ya jina hilo ni "Uzito wa Malezi".

Hilo ni la kwanza kati ya "matamko" matatu ya mtaguso huo, nalo linazingatia umuhimu wa malezi kwa mtu binafsi, kwa jumuia zake, kwa nchi yake na kwa Kanisa lenyewe.

Watu wa leo wanaelewa zaidi umuhimu huo kwa watoto, vijana na hata watu wazima; ndiyo maana wanafanya mipango mingi wakitumia pia njia mpya zilizoletwa na maendeleo.

Kanisa Katoliki linataka kuchangia juhudi hizo kufuatana na wajibu wake kwa watu wote na kwa mtu mzima (mwili na roho).

Hati hiyo inasisitiza haki ya kila mtu kupata malezi ya kumfaa; halafu waamini wote wana haki ya kupata malezi ya Kikristo, hasa vijana, tumaini la Kanisa.

Wazazi ndio walezi wakuu kwa watoto wao: wasipoutimiza wajibu huo mkubwa, si rahisi kujaza pengo hilo. Familia isaidiwe na jamii na Kanisa kwa njia mbalimbali, hasa shule: walimu waone kazi yao kuwa ni wito. Ni juu ya wazazi kuchagua kwa hiari aina ya shule inayohakikisha watoto wao walelewe wanavyopenda wazazi wenyewe.

Serikali haina haki ya kulazimisha wote kupata malezi ya aina moja, bali inapaswa kusaidia shule huru za wazazi na za kidini.

Kanisa liwashughulikie Wakristo wanaosomea shule zozote, lakini lijitahidi kuwaanzishia shule za kwake likiwahimiza wazazi kuwaandikisha watoto wao katika shule hizo. Katika shule katoliki elimu ya kawaida itolewe katika mazingira ya imani ili kijana alelewe bila ya mgawanyiko wa ndani. Shule katoliki zinaweza kupokea pia wanafunzi wasio wa dini hiyo na kuwa za namna mbalimbali na za ngazi zote, kuanzia za chekechea hadi vyuo vikuu, pamoja na vyuo vya kufundishia dini tu. Kati ya shule hizo zote ushirikiano ni muhimu.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]