Wikipedia ya Kiswahili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Wikipedia ya Kiswahili
Wikipedia-logo-v2-sw.svg
Ukurasa wa "Mwanzo" mwaka 2004

Wikipedia ya Kiswahili (au Wikipedia kwa Kiswahili) ni toleo la kamusi elezo ya Wikipedia kwa lugha ya Kiswahili.

Wikipedia kwa Kiswahili ilianzishwa mnamo tarehe 8 Machi 2003, na tarehe 16 Agosti, 2018, imefikia makala zipatazo 45,055 na kuifanya iwe Wikipedia ya 90 (kati ya 291 zilizo hai) kwa hesabu ya makala zote.[1]

Kwa hesabu ya makala zenye zaidi ya herufi 200 (yaani bila makala fupi mno) imefikia nafasi ya 71. [2]

Wikipedia ya Kiswahili inafunguliwa na 0,007% ya wanaofungua Wikipedia duniani kote. Walioivinjari mwezi Mei 2017 walikuwa katika nchi zifuatazo: Tanzania 48.5%, Marekani 18.6%, Kenya 14.4%, Ireland 5.1%, Ujerumani 4.9%, kwingineko 8.5%.

Mwezi huohuo, waliofungua Wikipedia nchini Kenya walikuwa 0,10% za wasomaji wote duniani; kati yao waliofungua Wikipedia ya Kiswahili walikuwa 1%. Kumbe nchini Tanzania waliofungua Wikipedia walikuwa 0,04% za wasomaji wote duniani, lakini kati yao 8.6% waliifungua kwa Kiswahili, asilimia inayozidi kukua kadiri makala zinavyoongezeka na kuwa bora zaidi.

Maendeleo

Mnamo Julai 2006 Wikipedia ya Kiswahili ilifikisha makala 1,000.

Mnamo Julai 2007 ilifikisha makala 5,000 na tarehe 26 Septemba 2007, 6,000.

Mnamo tarehe 21 Aprili 2008, Wikipedia ya Kiswahili ilifikisha makala 7,000.

Ilipofika tarehe 19 Desemba 2008 ilifikisha makala 8,000, hasa baada ya kuanzishwa makala nyingi za mbegu za kata za Tanzania.

Makala za mbegu za Tanzania, ziliendelea kuisukuma Wikipedia ya Kiswahili hadi kufikia kiwango cha makala 9,000 tarehe 2 Februari 2009 na makala 10,000 tarehe 21 Februari 2009.

Ilipofika tarehe 9 Aprili 2009, Wikipedia ya Kiswahili ilifikia kiwango cha makala 11,000 na tarehe 25 Aprili 2009 ilifikia makala 12,000.

Mnamo tarehe 20 Juni 2009, Wikipedia ya Kiswahili ilibadilisha ukurasa wake wa mwanzo katika sura mpya.

Mnamo tarehe 17 Agosti 2009 ilifikia makala zipatazo 13,000, na kuendelea kuifanya iwe Wikipedia ya kwanza kwa ukubwa katika Afrika.

Haikushia hapo na ilivyofika tarehe 11 Septemba 2009, Wikipedia hii ilifikia makala 14,000 na tarehe 25 Desemba 2009 makala 15,000.

Wikipedia 20000 articles.png

Tarehe 31 Mei 2010 ilifikia makala 18,000 na tarehe 21 Agosti mwaka huohuo makala 20,000.

Tarehe 28 Oktoba 2011 ilifikia makala 22,000.

Tarehe 15 Februari 2014 ilifikia makala 26,000 na tarehe 28 Oktoba mwaka huohuo makala 27,000.

Tarehe 25 Januari 2015 ilivuka idadi ya makala 28,000.

Tarehe 13 Juni 2015 ilifikia makala 29,000 na kusonga mbele.

Tarehe 22 Septemba mwaka huohuo ilifikia makala 30,000 na kuendelea tena.

Upande wa maharirio, tarehe 10 Oktoba 2015 yamefikia idadi ya milioni 1.

Tarehe 10 Novemba mwaka huohuo ilivuka makala 31,000 na kupiku Wikipedia ya Kiyoruba.

Tarehe 13 Februari 2016 ilivuka idadi ya makala 32,000 na kusonga mbele kiasi cha kufikia 33,000 tarehe 18 Aprili 2016.

Idadi ya 34,000 ilifikiwa tarehe 20 Agosti 2016 kwa makala Kinung.

Makala juu ya James Tate imeifanya itimize idadi ya 35,000 tarehe 12 Januari 2017. Mwaka huohuo, tarehe 20 Mei 2017 idadi ya makala ilifikia 36,000, tarehe 30 Julai ilifikia 37,000 kwa makala juu ya Ziwa Ambussel, tarehe 12 Oktoba 38,000 kwa makala juu ya mto Jubba na tarehe 24 Desemba ilifikia 39,000.

Tarehe 17 Machi 2018 mradi wa milima umeleta makala ya 40,000: Nidze.

Mradi wa mito ya Tanzania umesukuma Wikipedia hii kufikia idadi ya makala 41,000 kwa ukurasa wa Mto Ligunga tarehe 2 Mei 2018 na 42,000 kwa ukurasa wa mto Jigulu tarehe 21 Mei.

Mradi wa mito ya Kenya umefikisha idadi ya makala kuwa 43,000 kwa ukurasa juu ya Mto Kaptarit tarehe 7 Julai 2018, kuwa 44,000 tarehe 30 Julai kwa ukurasa juu ya mto Nyairoko tena kuwa 45,000 tarehe 12 Agosti kwa ukurasa juu ya Mto Ilangi.

Kati ya Wikipedia za Afrika

Kwa lugha zenye asili ya Afrika na visiwa vya jirani, Wikipedia kwa Kiswahili ndiyo ya tatu kwa idadi ya makala zote ikifuatia Wikipedia ya Kimalagasy na Wikipedia ya Kiafrikaans. Kwa kuangalia yaliyomo halisi (bila makala mafupi sana) ndiyo ya pili baada ya Kiafrikaans.

Pia, ndiyo ya kwanza kati ya Wikipedia za lugha za Niger-Kongo kuvuka kiwango cha makala 1,000. Sasa ziko nne.

Wikipedia kwa Kiswahili, ndiyo ya pili katika Afrika kuvuka kiasi cha makala 10,000 baada ya Wikipedia ya Kiafrikaans. [3]

Tazama pia

Marejeo

Viungo vya nje